SIRI KUU NNE (4), UNAZOPASWA UZIFAHAMU NDANI YA KRISTO.

SIRI KUU NNE (4), UNAZOPASWA UZIFAHAMU NDANI YA KRISTO.

Nakusalimu katika jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo. Uweza na nguvu ni vyake milele na milele. Amen.

Kuna mambo ambayo Mungu aliyaweka wazi, lakini pia kuna mambo ambayo Mungu aliyaficha ndani ya Kristo mpaka utimilifu wa wakati wake mwenyewe utakapofika. Hivyo ni vema ukafahamu siri hizo  alizozificha tangu mwanzo, na ngapi zimeshatimia, na ngapi zipo mbioni kutimia.

Siri hizo hazipo kwa mwingine zaidi ya Yesu Kristo.

Wakolosai 2:2 “..wapate kujua kabisa siri ya Mungu, yaani, Kristo;”

Na hivyo ndani ya Kristo ziliandikwa siri kuu Nne, ambazo leo tutaziona.

SIRI YA KWANZA

Yesu ndio yeye mwenyewe:

1Timotheo 3:16  Na bila shaka siri ya utauwa ni kuu. Mungu alidhihirishwa katika mwili, Akajulika kuwa na haki katika roho, Akaonekana na malaika, Akahubiriwa katika mataifa, Akaaminiwa katika ulimwengu, Akachukuliwa juu katika utukufu.

Mungu alijificha sana, kiasi kwamba hakuna aliyemtambua kuwa ndiye yeye Yehova katika umbo la kibinadamu, na ndio maana maandiko yanasema, kama watu wa ulimwengu huu wangemtambua kuwa yeye ndiye tangu mwanzo, wasingelimsulibisha.

1Wakorintho 2:7  bali twanena hekima ya Mungu katika siri, ile hekima iliyofichwa, ambayo Mungu aliiazimu tangu milele, kwa utukufu wetu; 8  ambayo wenye kuitawala dunia hii hawaijui hata mmoja; maana kama wangaliijua, wasingalimsulibisha Bwana wa utukufu;

Lakini bado tunaona ni jambo ambalo limejificha katika macho ya wengi hata sasa, lakini ashukuriwe Mungu tayari limeshafunuliwa hivyo hilo sio siri tena. Ni vizuri kuifahamu siri hii kwasababu wakati mwingine kushindwa kumtambua Kristo kama ndiye MUNGU mwenyewe. Hupunguza viwango vyako vya kutembea na yeye, na kumwelewa. Fahamu kuwa Yesu ni Mungu halisi Yehova mwenyewe kwenye umbile la kibinadamu ( Tito 2:13, Yohana 1:1, Wakolosai  2:9).

SIRI YA PILI

Mataifa nao ni warithi.

Waefeso 3:4  Kwa hayo, myasomapo, mtaweza kuutambua ufahamu wangu katika siri yake Kristo. 5  Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho; 6  ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili;

Wale wapagani, walioitwa makafiri na wayahudi, wafilisti, waashuru, wamisri, wakaanani, n.k. hao Mungu anakuja kuwafanya kuwa warithi wa uzima wa milele. Jambo ambalo halikujulikana na wanadamu au wayahudi kwa kipindi kirefu, wakidhani Mungu ni wakwao tu. Lakini leo hii anaabudiwa katika dunia nzima. Ilikuwa ni SIRI, lakini sasa imedhihirishwa. Soma (Wakolosai 1:27)

Siri hii ukiifahamu  itakufanya usibague mtu wa kumuhubiria injili, kitu mwanadamu chini ya jua anastahili kumjua Mungu katika Kristo Yesu. Hivyo usibague kama wewe ambavyo hukubaguliwa. Hubiri kwa watu wa dini zote, kabila zote na lugha zote.

SIRI YA TATU:

Wayahudi watarudiwa tena.

Warumi 11:25  Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili. 26  Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa, Mwokozi atakuja kutoka Sayuni; Atamtenga Yakobo na maasia yake. 27  Na hili ndilo agano langu nao, Nitakapowaondolea dhambi zao. 28  Basi kwa habari ya Injili wamekuwa adui kwa ajili yenu; bali kwa habari ya kule kuchaguliwa wamekuwa wapenzi kwa ajili ya baba zetu.

Tuwaonapo sasa wayahudi wapo mbali na injili ya Kristo, haitakuwa hivyo kwao milele. Mungu anasema “utimilifu wetu utakapowasili”. Yaani mpango wa Mungu wa wokovu kwetu utakapotimia. Basi na wao pia watarudiwa. Na Mungu atasimama nao, na kuwatetea. Na kuwaokoa (Zekaria 12:10-14). Na Mungu anasema kurudiwa kwao kutakuwa na utukufu mwingi zaidi.

Hivyo kuifahamu siri hii, itakuwasadia wewe ambaye umepata neema hii bure kutoichezea, bali kuithamini sana, kwasababu ikiwa wale waliipoteza, vivyo hivyo na sisi tunaweza ipoteza kwa kutokuamini kwetu. Na ndivyo itakavyokuja kuwa baadaye. Israeli watakaporudiwa kwa kipindi kifupi, sisi tutakuwa tumekwenda kwenye unyakuo, watakaobaki watalia na kuomboleza. Hivyo ni muhimu kuutimiza wokovu wako kwa kugopa na kutetemeka, kama maandiko yanavyotuambia (Wafilipi 2:12). Ithamini neema ya Kristo.

SIRI YA NNE

Kurudi kwa Bwana.

Kipindi kile Bwana alipokuwa duniani, wanafunzi walimuuliza kuhusiana na siku ya kurudi kwake, ndipo akawaeleza wazi kuwa hakuna mtu  aijuaye, isipokuwa Baba tu (Mathayo 24:36). Lakini Kristo alipopaa juu alipokea ufalme na enzi na nguvu, maana yake pia alitambua mpango wote alipowekewa na Baba yake, tunalithibitisha hilo katika kuvunjwa kwa ile mihuri saba (Ufunuo 6).

Na baadaye tunaona biblia inasema..

Ufunuo 10:7  isipokuwa katika siku za sauti ya malaika wa saba atakapokuwa tayari kupiga baragumu; hapo ndipo SIRI YA MUNGU ITAKAPOTIMIZWA, kama alivyowahubiri watumishi wake hao manabii.

Hii siri ya Mungu itakayotimizwa ndio hiyo inayohusiana na kutambua wakati husika wa Bwana kurudi. Na ndio maana ukisoma katika vifungu vya juu kidogo utaona yapo mambo ambayo Yohana aliyasikia lakini akakatazwa kuyaandika. Kuonyesha kuwa ipo sehemu ya Neno la Mungu, ambayo haijafunuliwa kwetu sisi, Mungu atakuja kufanya hivyo baadaye.

Ufunuo 10:3  Naye akalia kwa sauti kuu, kama simba angurumavyo. Na alipolia, zile ngurumo saba zikatoa sauti zao. 4  Hata ngurumo saba zilipotoa sauti zao, nalikuwa tayari kuandika. Nami nalisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Yatie muhuri maneno hayo yaliyonenwa na hizo ngurumo saba, usiyaandike.

Hivyo hii ndio siri moja tu, ambayo ipo ndani ya Kristo hatujafunuliwa bado.  Lakini wakati u karibu.

Je! Unatambua kuwa hizi ni siku za mwisho, umejiandaaje na karamu ya mwana-kondoo mbinguni kwa tukio la unyakuo.  Tubu dhambi  zao, umegukie Kristo akupe ondoleo la dhambi zako bure. Ikiwa upo tayari leo kumpokea Yesu maishani mwako, basi fungua hapa kwa mwongozo wa sala ya Toba >>>

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

Makerubi wenye sura nne, ni kweli wapo? na je! wanyama wataenda mbinguni?

KUWA MAKINI, HATUA ZA UNYAKUO ZINAENDELEA.

UTAWALA WA MIAKA 1000.

MBINGU MPYA NA NCHI MPYA. (Sehemu ya 1)

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments