Ulimwengu wa Roho ni nini? Na mtu anawezaje kuwa wa rohoni?

Ulimwengu wa Roho ni nini? Na mtu anawezaje kuwa wa rohoni?

Kwa tafsiri za kiulimwengu, ulimwengu wa roho Ni ulimwengu usioonekana kwa macho ambao unasadikika viumbe kama malaika, mapepo, au roho za wafu huishi na kutenda kazi. Na kwamba vyenyewe ndio vinavyoyaathiri maisha ya ulimwengu huu unaoonekana.

Na kwamba ili mtu aweze kutembea vizuri hapa duniani hana budi kufahamu au kuwasiliana navyo, ili viwape taarifa, au kushindana navyo pale vinapokinzana nao, kwa kuzingatia misingi Fulani maalumu ya kiroho. Na wengine wanaamini kuwa ni mahali ambapo pana mifumo kama hii ya kidunia, mfano  majumba, magari, falme na mamlaka, isipokuwa tu hapaonekani kwa macho n.k. ipo mitazamo mingi.

Lakini kibiblia Mungu anataka tufahamu kwa picha ipi juu ya huu ulimwengu wa Roho?

Awali ya yote biblia inatuambia ulimwengu wa roho upo. Na hauonekani kwa macho.

Waebrania 11:3  Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri.

Umeona, kumbe vitu vyote tunavyoviona kwa macho vilitokea mahali ambapo hapaonekani. Na huko si pengine zaidi ya rohoni.

Lakini jinsi unavyotazamwa kiulimwengu ni tofauti na jinsi Mungu anavyotaka sisi tuutazame.

Mungu anataka tutambue kuwa ulimwengu wa Roho, ni mahali ambapo sisi tunakutana na yeye kuwasiliana, pia kumwabudu, na kumiliki, na kutawala, na kubarikiwa, kuumba, kujenga, kufunga na kufungua, na kupokea mahitaji yetu yote kutoka kwake. Kwasababu yeye ni Roho,  zaidi ya kufikiri ni mahali ambapo tunakwenda kupambana na wachawi na mapepo au kuona vibwengo na mizimu.

Alisema..

Yohana 4:23  Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. 24  Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.

Hivyo, pale tu mtu anapoonyesha Nia ya kutaka kumjua Mungu (asiyeonekana), muumba wa mbingu na nchi. Tayari hapo anaanza hatua ya kuingia katika ulimwengu wa roho ambao Mungu aliuumba kwa ajili yake, na si kitu kingine.

Ndipo hapo sasa anapofahamu kuwa anauhitaji wokovu ili aweze kumkaribia Mungu.  Anaanza kumwamini Yesu, anapokea msamaha wa dhambi, kisha Roho Mtakatifu, na baada ya hapo anaishi kwa kulifuata Neno la Mungu aliloliamini. Sasa huyu mtu ambaye Ameokoka, anaitwa mtu wa rohoni, lakini Yule ambaye anaishi katika Neno la Mungu kwa kulitii, huyu sasa ndiye anayetembea rohoni.

Hivyo haijalishi kama alishawahi kuona malaika, au pepo, au kusikia sauti, au kuona maono. Maadamu analiamini Neno la Mungu, na nguvu zake, na kuliishi. Huyo yupo katika ulimwengu wa Roho tena katika viwango vya juu sana. Kwasababu maandiko yanasema kwa kupitia hilo (NENO), vitu vyote viliumbwa.

Kuishi katika Neno ndio kuishi rohoni. Maana yake ni kuwa  unaishi kwenye ulimwengu wa Neno.

Sasa utauliza, na haya mashetani sehemu yao ni ipi katika ulimwengu wa roho?

Haya nayo yanaingia rohoni, kwa lengo moja tu kuwapinga wale watu ambao wanatembea katika ulimwengu wa roho (yaani ulimwengu wa Neno). Hivyo yanajiundia mikakati, falme, ngome, na milki, ili tu yakuangushe wewe, uache kumwamini Mungu na Neno lake, na mpango wake wa wokovu kupitia Yesu Kristo. Uendelee kuwa mtu wa mwilini.

Ndio hapo sasa Bwana anatutahadharisha kuwa yatupasa tuwapo rohoni tusiwe hivi hivi tu. Bali tuhakikishe kweli silaha zote tumezivaa, kwasababu, mashetani haya pamoja na wajumbe wake wapo kwa lengo la kutuondoa kwenye Neno la Mungu.

Waefeso 6:10  Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.

11  Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.

12  Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya KATIKA ULIMWENGU WA ROHO.

13  Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.

14  Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,

15  na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;

16  zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.

17  Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;

18  kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote

Hivyo kwa hitimisho ni kuwa unapookoka, wewe tayari ni mtu wa rohoni. Ni mlango wa wewe kuonana na Mungu. Umeshaingia ulimwengu wa roho. Hivyo ili uweze kuona matunda yote ya Mungu, ni sharti uliishi kwa kuliamini Neno lake na ahadi zake, maisha yako yote yawe hivyo. Uwe mtu wa Neno. Lakini mtazamo wa kwamba siku unaona maono na malaika, au kusikia sauti ya Mungu kwenye masikio yako, au wachawi na mapepo ndio mara ya kwanza umeingia rohoni,. Si kweli. Bali Uanzapo kuliamini na kulitendea kazi Neno la Mungu.

Bwana akubariki.

Hivyo ni vifungu baadhi ambavyo utakutana na hilo neno, kwenye maandiko, vitakavyokusaidia kuelewa vema.

Waefeso 1:3  Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ULIMWENGU WA ROHO, ndani yake Kristo;

Waefeso 1:17  “Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye;18  macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; 19  na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; 20  aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ULIMWENGU WA ROHO”

Soma pia Waefeso 2:6,  3:10

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

NITAONGEZAJE NGUVU ZANGU ZA ROHONI?

CHAKULA CHA ROHONI.

ITAMBUE KARAMA YA MUNGU.

YANAYOENDELEA SASA KATIKA MADHABAHU YA MUNGU ROHONI.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments