Dhamiri ni nini kibiblia?

Dhamiri ni nini kibiblia?

Dhamiri au Dhamira ni nini kibiblia?


“Dhamiri” au kwa lugha nyingine “Dhamira” ni hisia ya ndani ya mtu (ya asili) inayompa kupambanua lililo jema na lililo baya, lililo zuri na lisilo zuri, linalofaa na lisilofaa. Hisia hii kila mtu anayo na haitokani na mafundisho au maelekezo, bali mtu anakuwa anazaliwa nayo.

Dhamiri ni kama mtu mwingine wa pili, aliyeko ndani yako ambaye anasahihisha hisia zako au maamuzi yako, kabla hujayafanya au baada ya kuyafanya. Kama jambo halipo sawa basi dhamiri inakushuhudia aidha kwa kukosa Amani au raha au ujasiri..

Vile vile kama jambo lipo sawa basi dhamiri yako ya ndani inakushuhudia kwamba kile ufanyacho ni chema, aidha kwa kupata furaha Fulani au Amani au ujasiri.

Kwamfano mtu anapofikiri “kuua/ kumwaga damu” au “kuiba”.. kabla ya kufanya kile kitu “dhamiri” ya ndani itamshuhudia kuwa kile kitu si sawa! Pasipo hata kuambiwa na mtu au kuhubiriwa, kuna kitu tu ndani yake kinamwambia hicho si sawa!.. Na kama ni mtu wa kujali basi haraka sana atahairisha maamuzi yake hayo.

Katika biblia neno Dhamiri limeonekana mara kadhaa.

Sehemu ya kwanza maarufu ni ule wakati ambao baadhi ya Waandishi na Mafarisayo walimletea Bwana YESU mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, kwa lengo la kutaka kumwua lakini pia kumjaribu Bwana. Lakini maandiko yanasema walipopewa ruhusa ya kumtupia mawe, wote walichomwa dhamiri zao na hakuna aliyemhukumu.

Yohana 8:3  “Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati.

4  Wakamwambia, Mwalimu, mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini.

5  Basi katika torati, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii; nawe wasemaje?

6  Nao wakasema neno hilo wakimjaribu, ili wapate sababu ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama, akaandika kwa kidole chake katika nchi.

7  Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe.

8  Akainama tena, akaandika kwa kidole chake katika nchi.

9  Nao waliposikia, WAKASHITAKIWA NA DHAMIRI ZAO, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati.

10  Yesu akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia, Mwanamke, wako wapi wale washitaki wako? Je! Hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia?

11  Akamwambia, Hakuna, Bwana. Yesu akamwambia, Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena.]”

Vile vile biblia inatabiri kuwa katika siku za mwisho, watatokea watu ambao watasema uongo ijapokuwa dhamiri zao zinawashuhudia, lakini hawatazisikiliza, na watu hawa watawafundisha watu mafundisho ya mashetani.

1Timotheo 4:1  “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani;

2  kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe;

3  wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli”

Mistari mingine ihusuyo dhamiri ni pamoja na Matendo 23:1, Warumi 2:15, Warumi 9:1, Warumi 13:5, na 1Timotheo 1:9.

Ikiwa ndani yako unahisi “Dhamiri yako imekufa” au “imepungua nguvu”… maana yake husikii chochote kikikuzuia au kukuhukumu unapofanya jambo lisilo sawa, basi fahamu kuwa adui kaharibu utu wako wa ndani, na hivyo unamhitaji Bwana YESU akuhuishe utu wako wa ndani kwa damu yake.

Unapompokea BWANA YESU, na kubatizwa na kujazwa na Roho wake mtakatifu, ule utu wako wa ndani uliokufa au uliofifia yeye (Bwana YESU) anauhuisha upya…na hivyo Dhamiri yako inafufuka na inakuwa safi. Hivyo fanya maamuzi leo ya kumsogelea yeye karibu na imarisha mahusiano yako naye.

Waebrania 9:14  “basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?”

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

MFANO WA MAMBO HAYO NI UBATIZO.

Nimempa Shetani watu hao, ili wafundishwe wasimtukane Mungu.

IKO NJIA IONEKANAYO KUWA SAWA MACHONI PA MTU.

NAFASI YA MWANAMKE KATIKA KANISA

Manabii walisema “Neno la Mungu likanijia” ..Maana ya hili neno ni nini?.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments