Category Archive Mafundisho

Katika kila kazi mna faida; Bali maneno ya midomo huleta hasara tu.

SWALI: Nini maana ya huu mstari?

Mithali 14:23 “Katika kila kazi mna faida; Bali maneno ya midomo huleta hasara tu”


JIBU: Kitabu cha Mithali na Mhubiri ni vitabu vilivyobeba mafunzo mengi sio tu yale ya kiroho bali pia hata ya maisha ya kawaida. Mstari huo unaelezea uzito wa kitu kinachotendewa kazi zaidi ya kile kinachozungumzwa tu. Kwamfano hapo anaanza kwa kusema “katika KILA KAZI mna faida”.. Maana yake ni kuwa katika kazi yoyote (iliyonjema), inafaida nyuma yake,. Iwe ni ya kudharaulika au yenye heshima, iwe ni ngumu iwe ni rahisi, iwe ni ya kipato kikubwa au kidogo, maadamu kazi fulani inatendeka ni lazima faida tu itaonekana nyuma yake.

Lakini mtu akiwa ni wa mipango mikubwa, mikakati mingi, akili nyingi za kubuni namna ya kutenda kitu Fulani, vikao vingi,  halafu hakitendei kazi, Bwana anasema, badala ya faida kinyume chake ni hasara tu atapata..

Vivyo hivyo na katika roho. Bwana anataka tuwe watendaji wa Neno lake, Sio kusikia tu au kuomba tu peke yake. Unaweza ukaomba usiku kucha lakini kama sio mtendaji wa Neno lake uliombalo, ni unapoteza nguvu tu.

Kwamfano unaomba Bwana akusaidie uushinde uasherati, lakini bado unashikamana na vichocheo vyake vyote, una picha chafu kwenye simu yako, kinywa chako kinazungumza mambo ya kizinzi na vijana wenzako, unachati na watu wa jinsia tofauti muda wote, unatazama tamthilia zenye maudhui hayo, unasikiliza miziki ya kidunia, unaishi na boyfriend/girlfriend. Unategemea vipi tamaa zisikutawale? Utaomba usiku kucha na hutaona matokeo yoyote, kwasababu hukitendei kazi kile unachokiomba.

Bwana alisema kama vile mwili bila roho umekufa, vivyo hivyo imani bila matendo imekufa ndani yake.(Yakobo 2:17). Kukitendea kazi kile kimoja ukiombacho, kina nguvu sana kuliko maneno elfu unayoweza kumwomba Mungu mwaka mzima.

Yakobo 1:22  “Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. 23  Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. 24  Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo”.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Nini maana ya “katika wingi wa hekima mna wingi wa huzuni”.

Nini maana ya huu mstari? “Yeye mwenyewe ataokolewa lakini ni kama kwa moto”

Mithali 14:4 ‘Zizi ni safi ambapo hapana ngombe;

Marijani ni nini katika biblia(Ayubu 28:18,Mithali 8:11)?

Nini maana ya mhubiri 9:11? si wenye mbio washindao katika michezo?

BWANA UNIJULISHE MWISHO WANGU.

Rudi nyumbani

Print this post

HATA WAKATI WENU WA MVI NITAWACHUKUENI. (Isaya 46:3)

Isaya 46:3 “Nisikilizeni, enyi wa nyumba ya Yakobo, ninyi mlio mabaki ya nyumba ya Israeli, mliochukuliwa nami tangu tumboni, mlioinuliwa tangu mimbani; 

4 na hata uzee wenu mimi ndiye, na hata wakati wenu wa mvi nitawachukueni; nimefanya, nami nitachukua; naam, nitachukua na kuokoa”.

Mstari huu wa faraja unatuonyesha fadhili za Mungu jinsi zilivyo nyingi kwa watu wake, Anaonyesha jinsi asivyoweza kuwaacha watu wake, tangu wakiwa tumboni mwa mama zao hadi kufikia uzee wao. Kila hatua ya maisha yupo nao, kila pito liwe rahisi au liwe gumu yupo nao, wakiwa watoto, wakafikia ujana, kisha nguvu zikaisha wakiwa wazee, Mungu yupo nao. Haleluya.

Daudi alilitambua hilo pindi alipoishiwa nguvu zake, akaandika…

Zaburi 37:25 “Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa Wala mzao wake akiomba chakula”.

Hivyo huna haja ya kuhofu kesho yako itakuwaje au uzee wako utaishaje, maadamu upo na Bwana, maadamu unamtumikia, siku hizo zikifika, atakuhifadhi Mungu wako. Mwingine anasema mpaka sasa sina mfuko wa mafao, na nguvu zangu zinakaribia kuisha, ni nani atakayenisaidia, ni nani atakayekuwa karibu na mimi? Jibu ni kuwa  Bwana ndiye atakayekuwa karibu na wewe. Kwasababu tangu zamani ulimtumainia. Lakini hata kama utakuwa na mali, huwezi kuwa na raha moyoni wakati huo endapo Kristo hayupo nafsini mwako sasa.

Hivyo wekeza maisha yako kwa Bwana sasa, ili kesho yako pia iwe na matumaini na raha tele. Ikiwa wewe ni kijana wakati huu uliopo, mtafute muumba wako, upokee WOKOVU kwa kumaanisha kabisa kuuacha ulimwengu, mtumikie Mungu, kimbia kweli kweli tamaa za ujanani, kabla zile nyakati mbaya za hatari hazijafika, Kwasababu maandiko yanasema kuna siku-mbaya mbeleni zitawakumba watu ambao hawakumcha Mungu tangu zamani.

Mhubiri 12:1 “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo”.

Ikiwa upo tayari kutubu dhambi zako leo , na kumkaribisha Bwana Yesu maishani mwako, basi bofya hapa kwa mwongozo wa sala hiyo ya toba >>>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

TUTAMKARIBIA MUNGU KWA IDADI YA MVI ZETU ROHONI.

Je! Wana wenu huwatoa kwa nani? maana yake ni nini?

NINYI AKINA BABA MSIWACHOKOZE WATOTO WENU

UFANYE WEMA WAKO KATIKA MAARIFA.

ANGALIENI MWITO WENU.

Praitorio ni nini? Na Kwanini ilikuwa ni najisi kwa wayahudi kuingia humo? (Yohana 18:28)

Afadhali mtu akutwe na dubu aliyenyang’anywa watoto wake.

Rudi nyumbani

Print this post

Maana ya ‘taabu haitoki mchangani, Wala mashaka hayachipuki katika nchi’ ni nini?

Ayubu 5:6 “Kwani taabu haitoki mchangani, Wala mashaka hayachipuki katika nchi;”

Watu wengi tumekuwa tukilaumu mazingira, tukilaumu wanyama, tukilaumu ardhi, na vitu vingine vya asili kuwa ndio chanzo cha matatizo yetu, chanzo ya shida zetu na mashaka yetu rohoni. Lakini maandiko yanatupa uhalisia kwamba taabu na mashaka havichupuki ardhini, kama vile mchicha umeavyo, bali vinatoka ndani yetu wenyewe.

Makosa  yetu ndio zao la kila aina ya matatizo yetu. Asili ya migogoro katika ndoa, sio ule m-buyu uliokaribu na nyumba zetu. Unaweza kuhama hata nchi ukakaa chini ya mizeituni na mizabibu mizuri, na maua, lakini bado ndoa yako ikaendelea kuwa na matatizo tena makubwa zaidi  hata yale ya mwanzo.

Sababu ya kuteswa na mapepo, sio Yule paka mweusi wa jirani anayekuja kulala batini kwako kila siku usiku. Bali ni kwasababu Kristo hayupo ndani yako.

Sababu ya kutokupiga hatua kiroho, sio hiyo ardhi unayoishi, au unayoimiliki, usihangaike na maombi ya kufungua/ kukomboa ardhi, hangaika na vifungo vilivyomo ndani yako. Ambavyo vinatokana na aidha kutolielewa Neno la Mungu, au kuwa nje ya wokovu.

Biblia inasema..

Yohana 8:36  Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli.

Na tena inasema…

Yohana 8:32  “tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru”.

Rekebisha mwenendo wako, pokea wokovu wa kweli, kisha liishi Neno la Kristo kila siku. Hakika utaona jinsi tatizo lako linavyotalika kirahisi, ndipo utaacha kuyalaumu mazingira ya nje.

Ayubu 5:6 “Kwani taabu haitoki mchangani, Wala mashaka hayachipuki katika nchi;”

Je! Umeokoka?  Kama bado unasubiri nini? Je! Unatambua kuwa hizi ni siku za mwisho, na Kristo yupo mlangoni kurudi, tunaishi katika muda wa nyongeza tu, siku yoyote unyakuo wa kanisa unapita, watakatifu kuchukuliwa mbinguni na wenye dhambi kwenda motoni?. Fanya uamuzi sahihi sasa, ikiwa upo tayari kuokoka leo, basi fungua hapa kwa mwongozo huo >>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

MTU MWENYE KUSITA-SITA KATIKA MAWAZO MAWILI.

LAKINI WAKATI WA TAABU WATASEMA, SIMAMA UKATUOKOE.

Rafiki hupenda sikuzote; Na ndugu amezaliwa kwa siku ya taabu.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 9 (Kitabu cha Ayubu).

Uasherati wa Kiroho maana yake nini?

Rudi nyumbani

Print this post

JE! UPO KATIKA MAJI YA UTULIVU?

Shalom, nakusalimu katika jina la Yesu Kristo mwokozi wetu. Karibu tujifunze maneno ya uzima maadamu siku ile inakaribia.

Katika siku hizi za mwisho ni lazima uwe makini sana na mahali ulipo, kwasababu zama zimebadilika, si kila jambo la kuliamini, vilevile si kila jambo la kutoliamini. Unamuhitaji Roho Mtakatifu sana kukusaidia kuchagua kilicho sahihi.

Bwana anatufananisha sisi na kama kondoo, na yeye kama mchungaji. Na sikuzote, mchungaji mwema, huwa anawapeleka kondoo wake katika maji ya mito-salama. Na si kila mto ilimradi mto tu anawapeleka kondoo zake kunywea maji hapana, bali pale tu palipo na maji ya utulivu ndipo anapowapeleka kondoo zake.

Ndio maana katika Zaburi ya 23 Inasema;

Zaburi 23:1 ‘Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu.  2 Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza’.

Ni kwanini maji ya utulivu, kwasababu maji yenye mvurugano, au yaliyotibuliwa yana hatari nyingi, huwenda ni makao ya viboko na mamba na hivyo kutembea kwao huko ndio kunafanya maji Yale yawe na mvuragano, kwahiyo kondoo akinywa maji pale yupo hatarini kuvutwa na mamba, akafanyika kitoweo.

Au huwenda maji hayo ni mkondo wa mafuriko, hivyo kitu chochote kitakachotelezea kule mtoni, si rahisi kupona kinyume chake ni kitasombwa na kupotelea mbali.

Hivyo maji yasiyotulia, si salama kwa mifugo. Na mchungaji apendaye kondoo huwa hawapeleki mifugo yake hapo.

Ndivyo ilivyo kwa Kristo, anapotuokoa, anatuongoza kwa Roho wake palipo na maji ya utulivu tukae hapo tunywe. Lakini tatizo linakuja ni sisi kuyakataa maji ya utulivu, tunayatafuta maji ya mivurugano.

Ndugu usiangalie ukubwa wa mto, au ukubwa wa Bwawa, haikuhitaji wewe kunywa mto mzima ndio ukate kiu yako. Namaanisha usiangalie wingi wa watu, au ukubwa wa jengo na madhabahu iliyopambwa, au utajiri wa kanisa ndio ufikiri kuwa hapo ni salama kwa roho yako. Bali tazama palipo na utulivu wa kiroho. Hapo ndipo utulize nafsi yako. Kwasababu unaweza kwenda mahali kwa lengo la kuikata kweli kiu yako kwa Bwana lakini kinyume chake ukakutana na mamba wakali wakakumaliza kabisa.

Palipo na maji salama ni wapi?

Kwanza ni pale Palipo na fundisho la Yesu: Yesu ndio maji yenyewe tulivu ya uzima, na sio nabii au mtume au askofu, au kanisa, au pesa, au umaarufu.. Hivyo angalia kiini cha fundisho unalofundishwa mahali ulipo, je yote yanalenga kukukuza kumjua Yesu au linakupeleka katika mambo mengine? Fikiri Tangu umekaa hapo, ni nini umeongeza katika kulijua Neno la Kristo katika kweli yote. Lakini Kama umejazwa maarifa ya ki-mwili tu zaidi yale ya Kristo, yaani  ya ki-ndoa, ki-uchumi, uchawi, biashara, pesa, hiyo ni injili nyingine, ni mafuriko ya adui, hakuna maji tulivu hapo, utazombwa na kuangamia kabisa.

Yohana 4:13  “Yesu akajibu, akamwambia, Kila anywaye maji haya ataona kiu tena; 14  walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele”

Palipo na Upendo: Hicho ni kigezo cha pili.

Yakobo 3:16  “Maana hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya”.

Katika mkusanyiko wowote, fundisho la tendo la upendo wa ki-ndugu linapuuziwa, au halihimizwi, ndani  kuna vita visivyokoma kati ya washirika, pengine huwenda na viongozi kwa viongozi, hiyo ni ishara kuwa utulivu wa Roho haupo hapo, hivyo ni hatari pia kwa maisha yako ya kiroho.

Tujitahidi sana kuwa na vipimo hivi vya kiroho katika kuchagua mahali tukusanyikapo kupata maji ya uzima, vitakusaidia sana, kwasababu hizi ni siku za mwisho, na manabii wengi na makristo wa uongo na madhehebu na dini za uongo  zimezuka kila pembe ili kuwatoa watu kwenye mstari.

Yajali maisha yako ya kiroho. Mpende Kristo na Agizo lake.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

MAFUNDISHO MAALUMU KWA WAONGOFU WAPYA.

JINSI YA KUMSIKIA MUNGU, NA KUPOKEA MAFUNUO AU JUMBE KUTOKA KWAKE.

MWENGE WAKO WA UHURU UPO WAPI?

MADHARA YA KUKOSA MAJI YA UZIMA BAADA YA KIFO.

WALIKUWA WAMECHOKA NA KUTAWANYIKA KAMA KONDOO WASIO NA MCHUNGAJI.

JE! UNAMPENDA BWANA?

Rudi nyumbani

Print this post

WENGINE WANAKESHA KWAAJILI YAKO.

Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia.

Leo nataka tujifunze umuhimu wa kuchunguza mambo, kwani  tusipokuwa watu wa kuchunguza mambo basi tunaweza tusiuelewe uweza wa Mungu.

Asilimia kubwa ya watu wanaobarikiwa hawajui kuwa mafanikio yao ni kutokana na maombi ya watu wengine (ambao wanawaombea wao pasipo kujua), hivyo ni muhimu sana kufikiri wakati wa kufanikiwa.

Hebu tujifunze katika ile habari ya Kana ya Galilaya pale Bwana Yesu alipofanya muujiza wake wa kwanza wa kugeuza maji kuwa divai.

Maandiko yanasema baada ya Bwana Yesu kubadili yale maji kuwa divai, yule Mkuu wa meza, aliyeteuliwa kuandaa  vinywaji vya wageni wa kawaida na mgeni rasmi, hakujua kama ile divai mpya imetoka kwa Bwana, badala yake alidhani mwenye sherehe ndiye aliyeinunua, na ndipo akaenda kumfuata mwenye sherehe (Bwana harusi) na kumpongeza akidhani kuwa yeye ndiye kainunua ile divai mpya na kuwapa watu wote wanywe.

Na yule Bwana harusi naye akashangaa kupewa sifa ambazo si zake, huenda na yeye akadhani kuna mtu tu katikati ya sherehe kajitokeza na kujitolea kununua divai mpya ili kuimeza aibu.. kwamaana divai kuisha katikati ya sherehe na bado kuna watu wa muhimu hawajapata, ilikuwa ni aibu kubwa sana kwa wenye sherehe. Hivyo mpaka mwisho wa sherehe ni wachache sana ndio waliojua siri ya ile divai, kuwa na Bwana Yesu ndiye aliyeitoa.

Tusome,

Yohana 2:1 “Na siku ya tatu palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake Yesu alikuwapo.

2  Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake.

3  Hata divai ilipowatindikia, mamaye Yesu akamwambia, Hawana divai.

4 Yesu akamwambia, Mama, tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia.

5  Mamaye akawaambia watumishi, Lo lote atakalowaambia, fanyeni.

6  Basi kulikuwako huko mabalasi sita ya mawe, nayo yamewekwa huko kwa desturi ya Wayahudi ya kutawadha, kila moja lapata kadiri ya nzio mbili tatu.

7  Yesu akawaambia, Jalizeni mabalasi maji. Nao wakayajaliza hata juu.

8  Akawaambia, Sasa tekeni, mkampelekee mkuu wa meza. Wakapeleka.

9  Naye mkuu wa meza alipoyaonja yale maji yaliyopata kuwa divai, (wala asijue ilikotoka, lakini watumishi walijua, wale walioyateka yale maji), yule mkuu wa meza alimwita bwana arusi,

10  akamwambia, Kila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema; hata watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasa”.

 Sasa nataka tuone nyuma ya Baraka hizo alikuwa nani?, Nyuma ya muujiza huo alikuwa nani, na nyuma ya aliyetoa aibu alikuwa ni nani?.. kisha na sisi tutapata akili wakati wa kufanikiwa.

MWOMBAJI/ WAOMBAJI.

Kulipoonekana tatizo, Marimu alienda kumwomba Bwana na kumsihi sana. Huyu ndiye aliyekuwa mwanzo wa muujiza wa divai. Kama sio Mariamu watu wangeabika kwenye sherehe hata kama sherehe hiyo Kristo alikuwepo ndani.

Vile vile hata leo, ukiona jambo Fulani la heri limetokea mbele yako lililoziba aibu yako, hebu tafakari sana, usijivune wala usikimbilie kusema wewe ni mwenye bahati, huna bahati yoyote, hayo ni matokeo ya wengine kuomba kwaajili yako..haijalishi Kristo yupo na wewe.. Hata katika ile harusi Kristo alikuwepo ndani, alikuwa ni mwalikwa, lakini bado kama pasingekuwepo mwombaji, hakuna kitu kingefanyika.

Ukiona umebarikiwa kwa jambo Fulani au mambo yako fulani fulani yameenda sawa usikimbilie kujisifu, wala kujivuna, kwamba una bahati!!…fahamu kuwa hayo ni matokeo ya wengine kuomba kwaajili yako, na hao huenda unawajua au huwajui.

Mtoto ukifanikiwa jua wakati mwingine ni matokeo ya maombi ya wazazi wako na si kwasababu wewe una akili sana au una ujanja mwingi, kijana ukifanikiwa jua ni matokeo ya maombi ya ndugu zako, au wapendwa wenzako wanaokesha kwaajili yako pasipo wewe kujua.

Unapoona unapiga hatua kimaisha au kiroho, fahamu kuwa ni matokeo ya wanaokuongoza kiroho kukuombea, wala usidhani ni kwa nguvu zako au una bahati..

Waebrania 13:17  “Watiini wenye kuwaongoza, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi”

Ukilifahamu hili siku zote utakuwa mnyenyekevu na kumshukuru Mungu kwa kila jambo na pia kufikiri sana kuwaheshimu wanaokuombea na hata wewe kutenga muda kuwaombea!.. Laiti yule mkuu wa Meza na yule Bwana arusi wangejua kitu Mariamu alichowafanyia, kwenda kuwaombea kwa Bwana wangeshangaa sana, na kunyenyekea sana.

Laiti ungejua mambo watu wanayomwambia Bwana kuhusu wewe, usingebaki kama ulivyo..

Amani ya familia yako, Amani ya jamii yako, Amani ya nchi yako, ni matokeo ya maombi ya watu wengine wa Mungu wanaolia mbele zake usiku na mchana.. wala si kwasababu nyingine?, kama si hao ni kitambo sana mambo ya ulimwengu yangeshaharibika..(2Thesalonike 2:7).

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

SABATO ILIFANYIKA KWAAJILI YA MWANADAMU NA SI MWANADAMU KWAAJILI YA SABATO!

Je! Siku ilihesabiwaje kabla ya jua na mwezi kuumbwa?

Je! Karamu za ‘Idi’ ndio zipo hizo tunazozisoma katika Hosea (12:9)

Ni lini na wapi Ibrahimu aliioona siku ya Bwana akashangilia?.

Je! Mwendo wa Sabato ulikuwaje kibiblia?(Matendo 1:12)

Rudi nyumbani

Print this post

SHUGHULIKA SANA NA DHAMBI YA KUSAHAU.

Nakusalimu katika jina kuu sana na lenye nguvu la Bwana wetu Yesu Kristo. Karibu tujifunze maneno ya uzima ya Mungu wetu.

Sisi kama Wanadamu Kila mmoja wetu haijalishi ameokoka au hajaokoka, ndani yake ameumbiwa kiwango cha “kusahau”. Hii ni karama ya Mungu na ni vizuri kumshukuru Mungu Kwa jambo hili, kwasababu kama tungeikosa wanadamu wote tusingeishi hivi tulivyo Leo.

Lakini kusahau kukisimama Mahali pasipo-papasa, inageuka kuwa hatari kubwa sana, Tena dhambi yenye matokeo mabaya sana rohoni.

Kuna aina ngapi za kusahau?

Sasa kusahau kunaweza kuwa aidha kupoteza kumbukumbu ya lile jambo au tukio, Moja Kwa Moja akilini mwako, uwe kana kwamba hujawahi kulipitia. 

Au kunaweza kuwa kulipoteza tu Kwa muda katika kumbukumbu lakini utakapokumbushwa unalikumbuka Tena.

Kusahau kwenye madhara ni kupi?.

Kabla ya kutazama ‘kusahau’ kwenye hasara tuone kusahau kwenye faida kukoje.

Kusahau kwenye faida kunatimia katika mambo yasiyo na maana, au yenye maudhui hasi kwako. Kwa mfano pale mtu unapotukanwa, au unapopigwa kikumbo barabarani na mtu usiyemjua, unaposikia miziki isiyokufaidia huko nje, unapofiwa, unapodhulumiwa, unaposemwa, unapovunjiwa heshima, unapoaibishwa, unaposingiziwa n.k… Mazingira kama haya ambayo ni hasi…kusahau Kunahitajika sana na ni lazima ujifunze kuruhusu jambo hili liumbike ndani Yako ili uponyeke kwa haraka,.maana ndio sehemu yake hiyo inapopaswa itumike.

Lakini kusahau kusikokujenga ni pale unaposahau Matendo mema, au mambo chanya yakupasayo kutenda. Kwamfano Sheria inasema ” usitupe taka hapa” Halafu inapita wiki Moja umesahau agizo hilo, unarudia tena kutupa taka pale pale ulipokatazwa..Hapo utakuwa hujitafutii jambo lingine zaidi matatizo?

Vivyo hivyo katika Neno la Mungu pale unaposahau sahau Neno la Mungu hapo ndio pabaya sana. Wakristo wengi hatujui kuwa Mungu “anayorudia kutuambia ni mengi kuliko Yale mapya anayotaka kusema nasi”..Ni Kwanini? ni kwasababu tumekuwa wepesi wa kusahau Sheria zake.

Mambo yamekuwa kinyume chake, badala tusahau yaliyo mabaya tukumbuke yaliyo mema, tunasahau mema tunakumbuka mabaya sikuzote.

Ni shambuliko kubwa sana ambalo ibilisi amelipanda mioyoni mwa wanadamu. Ndio sababu uchungu haukomi, masengenyo hayaishi, vita vinazuka Kila siku, fitna, unafki, na uongo havina mwisho ni kwasababu Hali Ile Ile tuliyokuwa nayo nyuma mpaka sasa tunairuhusu ikae kwenye akili zetu.

Wakati nguvu hiyo tungepaswa tuitumie kulihifadhi Neno la Mungu mioyoni mwetu ili Matendo chanya yaendelea kutokea ndani yetu, hatufanyi hivyo.. maandiko yanasema..

Yakobo 1:22-25

[22]Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.

[23]Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo.

[24]Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.

[25]Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake.

Tuweke mfano, tunaweza kusoma kwenye biblia kwamba Upendo hauhesabu mabaya, Wala haujivuni, Wala hauoni uchungu n.k(1Kor 13).. Sasa wakati uliposoma hili  neno, moyoni mwako unasema nitaliishi hili Neno, lakini inapita siku mbili unashangaa umerudia kule kule, unaanza ishi maisha ya namna Ile ya kwanza,. Tatizo lipo hapo kwenye kusahau. Laiti.hilo Neno lingekuwa limeganda viizuri kwenye moyo wako, ingekuwa breki pale tu mambo mabaya yanapojaribu kuvuka mipaka.

Sasa tunawezaje kuishinda Hali hii ya kusahau sahau?

Ni kama vile mwanafunzi darasani, mara nyingi anakuwa ni mtu wa.kurudia rudia kusoma na kufanyia sana mazoezi kile alichofundishwa..lengo la kufanya vile ni kulazimisha akili yake inakili Yale mafundisho kwa muda mrefu ili atakapoingia kwenye mtihani asisahau chochote…Lakini kama akisema Mimi ni ‘genius’ sina muda wa kurudia nilivyofundishwa..ni wazi kuwa mambo mengi yatamruka, na atafeli.

Hivyo na sisi sote ni wanafunzi wa Biblia. Soma biblia Kila siku ifanye kuwa rafiki Yako, usiwe mtu wa kusoma Leo, Tena wiki ijayo au mwezi ujao, ndio unakuja kusoma tena..SoMo tafakari mambo uliyoagizwa mule na Mungu Kila siku..Ndivyo itakavyokuwa rahisi kuliishi Neno la Mungu, kinyume na hapo usijidanganye Utasahau…kwasababu mwisho wa siku yatatoka moyoni mwako, na hivyo dhambi yoyote itakayokatisha mbele Yako, utashindwa kukabiliana nayo mapema. Mungu hapendi tuwe na tabia hii ya kusahau sahau Neno lake.

Kumbukumbu la Torati 6:6-9

[6]Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; [7]nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo. [8]Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako. [9]Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako.

Piga vita kusahau Neno la Mungu.

Bwana akubariki.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Wivu ni nini na kuna aina ngapi za Wivu? Na je ni dhambi kuwa na Wivu?

Utii ni nini? na ni nani tunayepaswa kumtii au kutokumtii?

NINI MAANA YA SISI KUWA WATOTO WA MUNGU?

JE NI KUTII AU KUPATA KWANZA MAARIFA?

YESU ANA KIU NA WEWE.

DHAMBI YA MAUTI

PALE AHADI ZA MUNGU ZINAPOKUJARIBU.

Rudi nyumbani

Print this post

TAA YA MWILI NI JICHO,

Karibu tujifunze biblia,

Mathayo 6:22  “Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru.

23  Lakini jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa na giza. Basi ile nuru iliyomo ndani yako ikiwa giza; si giza hilo”

Umewahi kujiuliza ni kwa namna gani “Jicho” limefananishwa na “Taa ya mwili”?

Siku zote taa ikiwa inaangaza basi nyumba yote inakuwa na Nuru na ndipo vitu vyote vilivyomo ndani vinaweza kuonekana, lakini ikizima nyumba yote inakuwa giza na hakuna kitakachoonekana.

Hali kadhalika na jicho likiwa halioni, au likiwa limefumbwa basi kinachoonekana ni giza, huwezi kuona chochote, huwezi kuona mikono yako, wala miguu yako, wala kiungo kingine chochote, huwezi kuona mbele wala nyuma wala kitu kingine chochote. Kwa ufupi unakuwa ni kipofu!. Hayo ni matokeo ya jicho kuharibika!.

Sasa Bwana Yesu analinganisha Nuru iliyopo ndani yetu na jicho.. Kwamba Nuru iliyopo ndani yetu, kazi yake ni kutuongoza njia, kama vile Jicho linaloona linavyoongoza njia na kuusaidia mwili wote kusonga mbele,  vile vile Nuru iliyopo ndani yetu kazi yake ni kuongoza maisha yetu katika njia sahihi.

Sasa Nuru iliyopo ndani yetu au inayopaswa iwe ndani yetu ni nini?.

Mathayo 5:16 “Vivyo hivyo NURU YENU NA IANGAZE mbele ya watu, wapate kuyaona MATENDO YENU MEMA, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni”.

Umeona hapo?.. kumbe Nuru ni “Matendo yetu mema” .. kwamba matendo yetu yanapokuwa mema, basi ni sawa na macho yanayoona!.. Kumbe matendo yetu yakiwa mabaya sisi ni sawa na vipofu!, wala hatujui tunapokwenda!…kama Bwana Yesu alivyosema katika…

Mathayo 15:14  “Waacheni; hao ni viongozi vipofu wa vipofu. Na kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, watatumbukia shimoni wote wawili”.

Je unataka kuona mambo yaliyopo mbele yako? na njia unayoielekea? kama ni salama?.. je! Unataka kuona hatari inayokuja na kuepukana nayo?.. Basi fanya matendo mema!!…usiende kwa waganga wala wasoma nyota wala manabii, wewe yasafishe matendo yako tu!, na utaona mambo yajayo!..

Hiyo ndio siri nyingine iliyopo nyuma ya “Matendo yetu mazuri”.. sio tu yanaupendeza moyo wa Mungu na kutupa baraka.. bali pia yanatuongoza na kutufanya tuone mambo yajayo (yaliyopo mbele yetu).

Na unayasafishaje matendo yako?.. Si kwa nguvu zako bali kwa Neema iliyopo ndani ya damu ya Yesu, ambayo hiyo inakuja kwa njia ya kutubu dhambi na kumaanisha kuziacha pamoja na kupata ubatizo sahihi..

Hapo Roho Mtakatifu ataingia ndani yako na kukupa uwezo wa wewe kufanya matendo yampendezayo Mungu, na hivyo macho yako ya kiroho yatakuwa angavu… Utakuwa na uwezo wa kuona hatari zilizopo mbele yako na kuepukana nazo, utakuwa na uwezo mkubwa wa kuona hasara zilizopo mbele yako na kuzikwepa, utakuwa unauwezo wa kuona mema yaliyopo mbele yako na kuyafuata na vile vile utakuwa na uwezo wa kuona hatari inayokufuata nyuma yako n.k

Lakini kanuni ni hiyo moja tu!..Ifanye Nuru yako (matendo yako) yaangaze!

Bwana akubariki.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

TWAENENDA KWA IMANI NA SI KWA KUONA.

Kama ulimwengu ujao utakuwa na watakatifu tu, sasa hao watakaotawaliwa watatoka wapi?

RUHUSU TOHARA IPITE JUU YA KARAMA YAKO.

ITII SAUTI ILIYOPO NYUMA YA KILA ISHARA YA MUNGU!

LAKINI MAKINDA WAWEZA KUYATWAA UWE NAYO.

Rudi nyumbani

Print this post

Kwanini samaki wasio na mapezi na magamba hawakuruhusiwa kuliwa?

Mambo ya Walawi 11:9-12

[9]Katika hao wote walio ndani ya maji mtakula hawa; kila aliye na mapezi na magamba, ndani ya hayo maji, na ndani ya bahari, na ndani ya mito, mtakula hao.

[10]Na hao wote wasio na mapezi na magamba, ndani ya bahari, na ndani ya mito, katika hao waendao majini, na katika wote wenye uhai, waliomo majini, hao ni machukizo kwenu,

[11]watakuwa machukizo kwenu; msiile nyama yao, na mizoga yao itakuwa machukizo kwenu.

[12]Kila asiye na mapezi wala magamba aliye ndani ya maji ni machukizo kwenu.

Mapezi ya samaki, ni vile vitu kama mbawa ngumu zenye mfano wa miiba  zinazokaa Kwa juu, au pembeni au nyuma mwa mwili wa samaki.Ukitazama samaki kama perege, sato au sangara utaona mapezi Yao.Na faida za mapezi hayo ni kuwa yanasaidia kuogelea, kuelea vema kwenye maji, kukunja Kona, kuongeza kasi na kusimama au kugeuka Kwa haraka.

Halikadhalika samaki waliokuwa na magamba ndio tu walioruhusiwa kuliwa. Na magamba yaliwasaidia kujilinda na maadui au wadudu wavamiaji kwenye mwili. Kwani ngozi ya samaki ni laini hivyo isipofunikwa na magamba magumu kama yale, meno makali ya maadui yanapopita ni rahisi kujeruhiwa, Yanakaa kama dirii kifuani mwa askari.

Lakini si samaki wote walikuwa na haya mapezi na magamba, Bali wengine hawakuwa nayo mfano wa Hawa ni kama kambale, papa, pomboo, pwezi.

Sasa Kwanini viumbe hivyo vikatazwe kuliwa na ufunuo wake ni upi Rohoni?

Kama tunavyofahamu agano la kale ni kivuli Cha agano jipya, sio kwamba viumbe hivyo vikiliwa vitamkosesha mtu mbingu, au vitamnajisi roho , hapana. Bali vilifanywa vile kwa makusudi ili kutupitishia sisi ujumbe wa Rohoni katika agano letu jipya. Kwamba na sisi kama tutafanana na mojawapo wa viumbe hivyo Rohoni basi tunakuwa najisi mbele za Mungu.

Samaki mwenye magamba ni mwenye ulinzi wa kutosha dhidi ya mashambulizi ya maadui. Na sisi tunapokosa ulinzi wa Rohoni mfano wa yule askari anayezungumziwa katika Waefeso 6, mwenye dirii ya haki kifuani, ngao ya Imani mkononi na chepeo ya wokovu kichwani. Tunakuwa ni wadhaifu, kiasi Cha kutoweza simama mbele ya adui yetu shetani. Hivyo ni kuhakikisha kuwa umesimama imara katika wokovu wako, lakini pia utambue haki uliyopewa katika  msalaba wa Yesu Kristo na Imani Yako timilifu ndani ya wokovu wako. Hapo utakuwa umejidhatiti vya kutosha mfano wa samaki mwenye gamba gumu, au mamba aliyefunikiwa na ngozi yenye gamba.

Ayubu 41:13 “Ni nani awezaye kumbambua magamba yake? Ni nani atakayepenya dirii yake maradufu?  14 Ni nani awezaye kuifungua milango ya uso wake? Meno yake yatisha kandokando yake.  15 Magamba yake yenye nguvu ndiyo fahari yake, Yamefungamana pamoja kama kwa kufungwa kwa muhuri.  16 Jinsi yalivyoshikamana Hata upepo hauwezi kupita kati.  17 Yamefungamana pamoja; Yameshikamana, hata hayawezekani kutengwa”

Vilevile samaki aliyekuwa na mapezi alikuwa ni mwepesi kukatiza katika maji. Ni sawa na mabawa Kwa ndege, au miguu na kwa mtu. Hivyo na sisi katika ulimwengu huu wa dhambi ili tusionekane kuwa najisi tuvae mapezi yetu ambayo maandiko yanasema .Ndio ule utayari wa kuihubiri injili.

Waefeso 6:15

[15]na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;

Tusienende Kama watu wasio na kusudi maalumu la kufanya duniani, tuvae utayari, ndio mapezi yetu tutembee ulimwengu kote kiuhubiri/ kushuhudia habari njema.Kwasababu tukikosa haya, siku ile ya mwisho, tutatengwa samaki wema na waovu..Kisha wale waovu watatupwa nje.

Mathayo 13:47  ‘Tena ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya samaki wa kila namna;

48  hata lilipojaa, walilivuta pwani; wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa. 49  Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki’

Tusiwe samaki najisi.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Injili iliyopo kwa Samaki aina ya Eeli.

Pomboo ni nini katika biblia?(Kutoka 25:5, Ezekieli 16:10)

Mjombakaka ni nani kwenye maandiko? (Walawi 11:29)

Lumbwi ni nini katika biblia?

Je! Ni kweli kuna samaki mtu (Nguva) Baharini.

Je! Ni dhambi kumpiga au kumuua mnyama bila sababu yoyote?

Manyoyota ni nini (Ayubu 37:6)

Rudi nyumbani

Print this post

ALIPOKUWA ANGALI MBALI, BABA YAKE ALIMWONA.

Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo Bwana wetu. Karibu katika kujifunza maneno ya uzima ya mwokozi wetu.

Leo tutaona jinsi “moyo wa toba ya kweli” unavyopokelewa kitofauti sana na Mungu. Kama tunavyoifahamu ile habari ya mwana mpotevu, jinsi alivyoingiwa na tamaa, ya kwenda kuanzisha maisha yake ya anasa mbali na baba yake. Na siku zilipozidi kwenda, mali zilipoisha, njaa kali ikamkuta Akaanza kula vyakula vya majalalani ambavyo viliwastahili tu nguruwe.  Lakini Biblia inasema, hakung’ang’ania tu  kuendelea kutaabika katika hali ile ile milele mpaka kufa kwake. Bali alijinyenyekeza akazingatia kurudi kwa baba yake akiwa na moyo wa toba, ili baba yake amfanye tu mtumwa. Na alipofanya vile, akiwa njiani anarudi, biblia inatumbia kuna tukio lilitokea.

Na tukio lenyewe ni “kuonekana kwake tokea mbali” . Tusome;

Luka 15:17  “Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. 18  Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; 19  sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako. 20  Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana. 21  Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena. 22  Lakini baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni; 23  mleteni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi; 24  kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia”

Embu tafakari, iweje, Baba yake ndio awe wa kwanza kumwona tokea mbali na sio watumwa ambao sikuzote wao ndio wanaosimama mlangoni mwa nyumba au kuzunguka zunguka huku na huko, au kwanini isiwe hata ndugu zake wengine, badala yake baba yake ndio anayekuwa wa kwanza kumwona?

Sio kana kwamba hao wengine walikuwa hawali mboga za majani, hawaoni mbali kwa macho yao kuwa hafifu, hapana, bali Baba yake alikuwa na jicho lingine la rohoni kama DARUBINI. Hilo lilikuwa linaona mahangaiko, na manyanyaso ya mwanaye tokea mbali, kiasi kwamba alipofanya geuko moyoni mwake, tayari baba yake alishahisi, na akiwa njiani anakuja tayari baba yake alishajua kuwa mwanawe yupo njiani. Hivyo kabla hata mtoto hajamwona Baba, kabla hata hajaifikia nyumba yao akiwa kilomita kadhaa mbali, tayari baba alikwenda kukutana naye na kumkumbatia na kumbusu sana.

Ndivyo ilivyo kwa Mungu wetu. Pale mtu anapokuwa na moyo wa toba ya kweli rohoni, haihitaji wewe kwenda kusema maneno mengi sana mbele za Mungu, kana kwamba ndio utasikiwa. Yeye anayo darubini yake, Lakini kule kuzingatia tu kurudi kwa Baba yako wa mbinguni, ukaanza kuchukua hatua. Hiyo ni toba kubwa sana ambayo itamfanya Mungu, kabla ya wewe kumfikia tayari ameshakufikia, haraka sana na kukupa tiba ya moyo wako, na raha nafsini mwako.

Hii ni kuonyesha kuwa toba ya kweli, ni ule moyo uliogeuka. Sio tu kuongozwa sala maalumu. Ndio tunajua sala ikiambatana na geuko ni vema sana, lakini ikiwa utasalishwa sala hizo elfu 10 halafu ndani yako, ni vilevile tu, hapo unapoteza muda wako ndugu.

Alikuwepo Yule mwanamke mwenye dhambi nyingi sana, alipokwenda kwa Bwana Yesu saa ile ile akaanza kulia akitubia dhambi zake, akidondosha machozi yake miguu pa Yesu, huku akiyapangusa kwa nywele zake. Lakini Yesu alipomwona akasema ‘Umesamehewa dhambi zako nyingi’, mwanamke Yule hakusalishwa sala yoyote.(Luka 7:36-50).

Ili Mungu afike kwako upesi, kuwa na toba ya kweli, ili upate kibali cha haraka kwa Mungu, sio wingi wa maombi yako, bali geuko la dhati. Na Bwana mwenyewe atakufikia kabla hujamfikia yeye.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

WALA HAKUACHA MTU ACHUKUE CHOMBO KATI YA HEKALU.

Kwanini Nuhu alimlaani Kaanani badala ya mtoto wake Hamu,

UMUHIMU WA KUISHI MAISHA YAMPENDEZAYO MUNGU SASA.

MUME / MKE BORA KUTOKA KWA BWANA UTAMWONA UKIWA KATIKA MAZINGIRA GANI?

JE! UKRISTO UNAMPA MTU DHAMANA YA KUWA TAJIRI?

Forodhani ni mahali gani?

Rudi nyumbani

Print this post

TAFUTA HEKIMA, MAARIFA, UFAHAMU NA BUSARA.

Jina la Mwokozi Mkuu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia.

Mithali 2:10 “Maana hekima itaingia moyoni mwako, Na maarifa yatakupendeza nafsi yako;

 11 Busara itakulinda; Ufahamu utakuhifadhi. 

Haya ni mambo manne ambayo ni muhimu sana kuwa ndani yetu.

  1. Hekima – Ni uwezo wa kupanga na kupambanua mambo
  2. Maarifa- Ni elimu au taarifa kuhusiana na jambo fulani
  3. Ufahamu- Ni hali  ya kuweza kufahamu jambo Fulani kwa kina
  4. Busara- Ni hali ya kuona mbele (yaani mambo yajayo) na kuamua lililo sahihi. Mithali 27:12

Mambo haya manne ni Bwana pekee anayeweza kuyatoa.. Mithali 2:6 “Kwa kuwa Bwana huwapa watu hekima; Kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu” .

Zifuatazo ni faida kuu tatu (3) za kupata Hekima, Maarifa, ufahamu na busara.

  1. KUOKOKA NA NJIA YA UOVU.

Hii ni faida ya kwanza ya kupata Hekima, Ufahamu, busara na Maarifa; “Kumwokoa mtu na njia ya uovu”

Mithali 2:10 “Maana hekima itaingia moyoni mwako, Na maarifa yatakupendeza nafsi yako;

11 Busara itakulinda; Ufahamu utakuhifadhi. 

12 ILI KUKUOKOA NA NJIA YA UOVU, Na watu wanenao yaliyopotoka; 

13 Watu waziachao njia za unyofu, Ili kuziendea njia za giza; 

14 Wafurahio kutenda mabaya; Wapendezwao na upotoe wa waovu; 

15 Waliopotoka katika njia zao; Walio wakaidi katika mapito yao”

Njia ya Uovu ni njia yoyote ile ambayo itampelekea mtu kufanya maovu, mfano wa hayo ni yale yanayotajwa katika Wagalatia 5:19-21 “uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo”.

2. KUKUOKOA NA MALAYA:

Mithali 2:16 “…Ili kuokoka na malaya, Naam, malaya mwenye kubembeleza kwa maneno yake..”

Mtu aliye Malaya ni yule anayefanya uasherati aidha kwa lengo la kutafuta pesa au kujifurahisha, na hili ni neno linalotumika kuwakilisha jinsia zote mbili za watu wenye tabia hizo. Na Malaya anaweza kuwa ni mtu aliye ndani ya ndoa au nje ya ndoa.

Mtu mwenye busara (Maana yake anayeona mbele), hawezi kunaswa na mtego wa Malaya.. Mfano wa mtu aliyekuwa na busara katika biblia ambaye aliokoka na mtego wa Malaya ni Yusufu, ambaye alitegewa mtego na mke wa Potifa, lakini aliushinda mtego ule wa ibilisi.

Lakini kama Yusufu hangekuwa na Busara akilini mwake, basi angenaswa katika mtego ule wa  uasherati alipobembelezwa na mke wa Potifa, na hivyo angekuwa amejiingiza katika matatizo makubwa sana, ambayo yangehatarisha hata maisha yake ya kimwili na kiroho.. kama biblia inavyosema hapa..

Mithali 2:16 “Ili kuokoka na malaya, Naam, malaya mwenye kubembeleza kwa maneno yake;

17 Amwachaye rafiki wa ujana wake, Na kulisahau agano la Mungu wake. 

18 Maana nyumba yake inaelekea mauti, Na mapito yake yanakwenda kwenye wafu. 

19 Katika hao wamwendeao harudi hata mmoja, Wala hawazifikilii njia za uzima”

Soma tena maandiko mengine yanayohusu tabia za Malaya, jinsi anavyobembeleza katika Mithali 7:7-23, Mithali 22:14 na Mithali 23:27.

Ukiona mtu kanaswa na mtego basi ni matokeo ya kupungukiwa Hekima, busara, maarifa na ufahamu.. kama biblia inavyosema katika Mithali 6:32 “Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake” .Kwasababu mtu aliyejaa mambo hayo hawezi kunaswa na mitego hiyo.

3. KUKUPELEKA KATIKA NJIA YA WATU WEMA

Faida ya kwanza tuliona ni “kumwokoa mtu katika njia ya uovu” lakini Hii ya tatu na ya mwisho, ambayo ni “Kukupeleka mtu katika njia ya watu wema”.. Hekima, busara, Maarifa na ufahamu haviishii tu kumwokoa mtu na njia mbaya na kumwacha hapo katikati bali pia kumpeleka/kumwongoza katika njia nzuri.

Mithali 2:20 “Ili upate kwenda katika njia ya watu wema, Na kuyashika mapito ya wenye haki.

21 Maana wanyofu watakaa katika nchi, Na wakamilifu watadumu ndani yake. 

22 Bali waovu watatengwa na nchi, Nao wafanyao hila watang’olewa”.

Watu wema wana Njia yao, wapo katika mkondo wao, si kila mahali wanapita, na hao ndio wanaodumu katika nchi, … Sasa ili kuiona hiyo njia waliyopo basi Hekima, Busara, Maarifa na ufahamu vinahitajika. Na vyote hivyo vinatoka kwa Mungu.

Sasa swali? Mtu anapataje Hekima, Ufahamu, Busara na Maarifa ili kuepukana na hayo yote, na kupata faida hizo.

Tukitaka Hekima, Maarifa, Ufahamu na Busara biblia imetupa kanuni rahisi katika kitabu cha Ayubu.

Ayubu 28:20 “Basi hekima yatoka wapi? Na mahali pa ufahamu ni wapi? 

21 Kwa kuwa imefichwa mbali na macho ya wote walio hai, Na kusitirika na ndege wa angani. 

22 Uharibifu na Mauti husema, Tumesikia habari zake kwa masikio yetu. 

23 Mungu ndiye aijuaye njia yake, Naye anajua mahali pake. 

24 Maana anatazama hata miisho ya nchi, Na kuona chini ya mbingu nzima. 

25 Apate kuufanyia upepo uzito wake; Naam, anayapima maji kwa kipimo. 

26 Hapo alipoiwekea mvua amri, Na njia kwa umeme wa radi. 

27 Ndipo alipoiona na kuitangaza; Aliithibitisha, naam, na kuichunguza. 

28 Kisha akamwambia mwanadamu, Tazama, KUMCHA BWANA NDIYO HEKIMA, NA KUJITENGA NA UOVU NDIO UFAHAMU”.

Kumcha Bwana na kuepukana na Uovu ndio chanzo cha Hekima, maarifa, busara na ufahamu.

Maana yake Jishughulishe sana na masuala ya kiMungu sana, Jifunze Neno la Mungu, kusanyika na wengine katika maombi, ibada na kufanya uinjilisti na mambo mengine yote yanayofanana na hayo, kwa kufanya hivyo ndivyo Hekima, na hayo mambo mengine yatakapoingia ndani yako na kujaa.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

HEKIMA NI NINI? NA UFAHAMU UNAPATIKANA WAPI?

Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana.

Mjombakaka ni nani kwenye maandiko? (Walawi 11:29)

Nini maana ya “Mwenye hekima huvuta roho za watu”

Mwandishi wa kitabu cha Zaburi ni nani?

Rudi nyumbani

Print this post