KIASI NI NINI KATIKA UKRISTO?

KIASI NI NINI KATIKA UKRISTO?

Kiasi kama tafsiri yake  ilivyo ni  kuwa na uwezo wa kudhibiti jambo/tendo lisipitilize mipaka yake, yaani litendeke kwa sehemu tu.

Katika Ukristo, kiasi ni moja ya matunda tisa (9), ya Roho Mtakatifu.

Wagalatia 5:22 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, 23 upole, KIASI; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria”.

Ikiwa na maana ukipungukiwa nacho (kiasi), ni uthibitisho mojawapo kuwa Roho wa Mungu hayupo ndani yako.

Kwasababu huu  ulimwengu una mambo mengi, ambayo, pengine sio mabaya, lakini yakipitiliza matumizi yake, yanabadilika na kuwa mabaya na sumu kubwa sana, kuliko hata matendo yenyewe mabaya.

Sasa swali ni Je, tunapaswa tuwe na kiasi katika mambo gani?

Zifuatazo ni sehemu muhimu, ambazo, Roho Mtakatifu anataka sisi tuwe nazo na kiasi.

  1. Katika ndoa.

1Wakorintho 7:4 “Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe.

5 Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu”.

Kukosa kiasi katika tendo la ndoa, hupelekea watu wengi sana kumtenda Mungu dhambi, wengine wanatenda mambo hayo hata kinyume na maumbile, wengine kutafuta njia za visaidizi n.k. wengine muda wao wote wanachowaza ni tendo lile tu, akili zao zote zinafikiria humo, mpaka inawapelekea kukosa muda kusali. Hivyo kiroho chao kinapungua sana kwasababu ya kuendekeza tamaa za mwili.

Biblia inasema..

1Wakorintho 7:29 “Lakini, ndugu, nasema hivi, muda ubakio si mwingi; basi tokea sasa wale walio na wake na wawe kama hawana;

Ikiwa na maana, tuishi kama vile, hakuna jambo jipya tumeongeza, pale tulipooa au kuolewa, hiyo itatusaidia sana, kuishi Maisha ya utakatifu na kumcha Mungu, katika hichi kipindi kifupi tulichobakiwa nacho duniani.

2. Kiasi katika shughuli za ulimwengu;

Bwana ametuweka duniani tufanye kazi, pia tujitafutie rizki, lakini anatutahadharisha, tusipitilize, mpaka kufikia hatua ya mioyo yetu kuzama huko moja kwa moja tukamsahau yeye, hata muda wa ibada, au kuomba au kuwaeleza wengine Habari njema tukakosa..Hiyo ni hatari kubwa sana.

1Wakorintho 7:31 “Na wale wautumiao ulimwengu huu, kama hawautumii sana; kwa maana mambo ya ulimwengu huu yanapita”.

Yaani fanyakazi huku ukijua mahusiano yako, au ratiba yako na Mungu haivurugwi hata kidogo.. Kwasababu ukiupeleka moja kwa moja moyo wako huko, ni lazima tu ulale kiroho, na matokeo yake, utakufa na bado hujayatengeneza mambo yako vizuri na Mungu.

1Wathesalonike 5:6 “Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, NA KUWA NA KIASI.

7 Maana walalao usingizi hulala usiku, pia na walewao hulewa usiku.

8 Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu”.

Usihangaishwe sana na shughuli za dunia hii.. Kuwa na kiasi katika hayo, ili mbegu yako imee vizuri. Zingatia sana hilo. Kama unatingwa na mihangaiko ya duniani, na moyoni mwako unaona ni sawa, basi ujue moyoni mwako Roho Mtakatifu hayupo.

3. Kiasi katika huduma

Mungu anataka watumishi wake pia wawe na kiasi.. Hamaanishi kiasi katika kumtumikia hapana, anataka sana tuzidi kumtimika kwa bidii,  bali anamaanisha kiasi katika karama.

Anasema..

Warumi 12:3 “Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunia; BALI AWE NA NIA YA KIASI, kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani.

4 Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja;

5 Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake.

Hii ni kutuonyesha kuwa hakuna hata mmoja wetu mwenye karama zote, Ni YESU tu peke yake. Hivyo ridhika, na ulichokirimiwa, ukiwa ni mchungaji, usitake wewe wewe ndio uwe ni nabii, na mwalimu, na mwimbaji, na mwinjilisti, na mtume n.k. Huwezi kuwa Yesu.

Jifunze kuwapa wengine nafasi, na kunyanyua karama zao, pia fahamu kuwa wapo watakaokuwa na karama bora kukuzidi wewe. Ukilijua hilo utajifunza kuwa mnyenyekevu, na ndivyo Mungu atakavyokutumia Zaidi.

     4. Kiasi katika haki:

Mhubiri 7:16 “Usiwe na haki kupita kiasi; Wala usijiongezee hekima mno; Kwani kujiangamiza mwenyewe?

Hapa pia Mungu hamaanishi kwamba tusiwe na haki nyingi kupitiliza hapana, anapenda sana tuwe hivyo. Lakini anachomaanisha hapo ni kuwa tusiwe watu wa kujihesabia haki kupitiliza,(yaani kujisifia) kwani matokeo yake ni kujiangamiza wenyewe.

Bwana Yesu alitoa mfano wa yule Farisayo na mtoza ushuru waliokwenda kusali kule hekaluni, lakini yule Farisayo akaanza kumwambia Mungu mimi ni mkamilifu kuliko huyu mtoza ushuru, mimi ninafunga mara mbili kwa juma, mimi natoa zaka, mimi nahudhuria mikesha kila wiki, mimi nahubiri sana n.k. Lakini yule mtoza ushuru akasema Bwana nirehemu mimi ni mwenye dhambi..Matokeo yake yakawa yule mtoza ushuru akahesabiwa haki kuliko yule Farisayo..

Ndipo Yesu akasema..

Luka 18: 14 “…kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa”.

Uendapo mbele za Mungu, au mbele za wanadamu kuwa na kiasi.. Mwache Mungu akuhesabie haki mwenyewe. Usijifisie kwa lolote.

5. Kiasi katika kunena.

Biblia inasema..

Mithali 10:19 “Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu; Bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili”.

Kwanini haisemi, katika Uchache wa maneno, hapakosi kuwa na maovu?..Ni kuonyesha kuwa, unapokuwa mzungumzaji kupitiliza, ni rahisi sana kujikwaa ulimi, lakini ukiwa si mwepesi wa kuzungumza zungumza,  yaani kila Habari au kila jambo unachangia, basi utajiepusha na maovu mengi.

Mhubiri 5:2 “Usiseme maneno ya ujinga kwa kinywa chako, wala moyo wako usiwe na haraka kunena mbele za Mungu; kwa maana, Mungu yuko mbinguni, na wewe upo chini, Kwa hiyo maneno yako na yawe machache”.

6. Kiasi katika vyakula, na vinywaji.

Vinywaji kama divai, vilikuwa ni vya kitamaduni Israeli, wakati ule, kwasababu pia ndani yake waliamini kuna tiba, (1Timotheo 5:23) hivyo vilikuwa vinanyweka kwa kiasi sana, kwasababu vilikuwa na kiwango cha  kileo ndani yake.

Paulo akamwagiza Timotheo kuhusiana na Mashemasi na wazee wa kike katika makanisa, akamwambia.

1Timotheo 3:8 “Vivyo hivyo mashemasi na wawe wastahivu; si wenye kauli mbili, si watu wa kutumia mvinyo sana,si watu wanaotamani fedha ya aibu.

Lakini sasa kwa watu kukosa kiasi, leo hii, wanakwenda kunywa pombe ambayo haiwasaidii chochote, wala haina umuhimu wowote katika mwili, Wakati wa sasa tunazo dawa, kwanini ukanywe divai.

Na biblia imeweka wazi kabisa, walevi wote sehemu yao itakuwa katika lile ziwa la moto (1Wakorintho 6:10).

Sio kila kitu ule, au unywe. Zuia koo lako, zuia tumbo lako. Wakati mwingine funga, Litunze hekalu la Mungu. Utaona faida yake

 7.Kiasi katika mwenendo.

Hapa anatoa angalizo, katika mienendo yetu na mionekano.  Hususani kwa vijana.

Tito 2:6 “Vivyo hivyo na vijana waume uwaonye kuwa na kiasi”;

Jiulize kwanini hasemi, wazee au Watoto? Anasema vijana kwasababu Anajua kabisa vijana wengi wakike na wakiume  waliokoka wanakosa, kiasi katika ujana wao.

Hakuna sababu ya kukesha katika muvi au magemu, au mipira kutwa kuchwa. Ukiwa umeokoka, ili hali unajua kabisa kusoma biblia, kuomba na kuhubiri kunakusubiria.

Hakuna sababu ya  binti wa Mungu avae/ aonekane kama mabinti wa ulimwengu huu. Unaweka mawigi, unavaa suruali, uweka kucha za bandia, n.k. Kuwa “natural”..

1Timotheo 2:9 “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, NA MOYO WA KIASI; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani”;

Soma pia (1Timotheo 3:11)

Kijana, huna sababu ya kunyoa kiduku, uonekane kama msanii fulani, kwenye tv. Kumbuka Mwonekano wako unakupunguzia utukufu wako.

Kwahiyo, kwa kuhitimisha ni kuwa KIASI katika mambo yote ni muhimu sana. Hivyo tujitahidi kwa upande wetu kila mmoja aangalie ni wapi amekosa kiasi, basi arekebishe mapema, na Roho Mtakatifu atajaa tena ndani yetu kutusaidia kuushinda ulimwengu.

Kumbuka hizi ni nyakati za mwisho, Biblia inasema..

1Petro 5:8 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze”.

Umeona! Ibilisi anawatufuta watu wanaokosa kiasi ili awemeze, Usiwe mmojawapo!

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

MATUNDA 9 YA ROHO MTAKATIFU

Unyenyekevu ni nini?

Je ushabiki wa mpira ni dhambi?

Wibari ni nani?(Mithali 30:26)

Biblia inaposema “Wote tumetenda dhambi” si inamaanisha hakuna mtakatifu duniani?

Nini maana ya mstari huu: (Mtu ambarikiye mwenzake kwa sauti kuu asubuhi na mapema; Itahesabiwa kuwa ni laana kwake.Mithali 27:14 )?

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 11 (Mithali, Wimbo ulio bora, Mhubiri)

Je! Mtu ambaye hajaoa anaruhusiwa kulichunga kundi?

“Vya Kaisari mpeni kaisari”  ni vipi hivyo tunavyopaswa tumpe?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
1 year ago

Somo zuri sana la kiasi, Asante Kwa ujumbe maridhawa kabis