Title January 2019

UPENDO

Upendo ni kiini cha ukristo na pia ni KILELE CHA UKRISTO. Mungu hajaufunua Upendo kama moja ya tabia zake, kwa mfano hajasema mahali popote kuwa yeye ni mwenye upendo kama anavyosema juu ya tabia zake nyingine alizonazo, mfano Mungu muweza yote, au Mungu mwenye nguvu, Mungu wa rehema, au Mungu mwenye mamlaka n.k. hapana bali anapofikia kwenye suala la Upendo anasema “MIMI NI UPENDO”, yaani yeye kama alivyo ni UPENDO na si kama moja ya tabia zake..Hivyo hulifanya hili Neno upendo katika mtazamo wa rohoni kuwa na tafsiri pana zaidi kuliko sisi tunavyoweza kulichukulia.

1Yohana 4:16 “Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. MUNGU NI UPENDO, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake”.

Upendo ule unaozungumziwa kwenye biblia sio upendo wa kusema nakupenda kimdomo na wala si upendo wa kihisia bali ni upendo UNAOTENGENEZWA ndani ya moyo wa mtu, kwasababu chanzo chake si mwanadamu bali ni Mungu. Hivyo sio wa kutokea tu ndani ya siku moja, pale mtu anapozaliwa mara ya pili. Na ndio maana ukisoma katika kitabu cha 2Petro 1:1-10, utaona kuwa Upendo unachukua hatua ya mwisho kabisa baada ya mtu kupita hatua zote sita za kuelekea ukamilifu, upendo ndio unatokea mwishoni,

2 Petro 1: 5 “Naam, na kwa sababu iyo hiyo mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yenu tieni na WEMA, na katika wema wenu MAARIFA,

6 na katika maarifa yenu KIASI, na katika kiasi chenu SABURI, na katika saburi yenu UTAUWA,

7 na katika utauwa wenu UPENDANO WA NDUGU, na katika upendano wa ndugu, UPENDO.

8 Maana mambo hayo yakiwa kwenu na kujaa tele, yawafanya ninyi kuwa si wavivu wala si watu wasio na matunda, kwa kumjua Bwana wetu Yesu Kristo”.

huwezi kurukia hatua ya mwisho ukasema kuwa unao upendo wakati hatua zile 6 bado hujazikamilisha ndani yako.Maana ile hatua ya mwisho ni Mungu mwenyewe. Hivyo ili kufikia hatua hiyo ya juu kabisa kileleni Mungu alipo, mahali ambapo utakuwa karibu sana na Mungu katika roho kuliko pengine popote ni hapo utakapoufikia Upendo wa Mungu ndani yako. Na hivyo ili kufika hapo inahitaji BIDII na si vinginevyo. Hiyo haiji kwa kuombewa wala kwa kuwekewa mikono. Biblia inasema ni kwa jitihada na bidii. Kama inavyosema:

1Petro 1: 1.22 “Mkiisha kujitakasa roho zenu kwa kuitii kweli, hata kuufikilia upendano wa ndugu usio na unafiki, basi JITAHIDINI kupendana kwa moyo.  Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la Mungu lenye uzima, lidumulo hata milele”.

“Zaidi ya yote iweni na JUHUDI NYINGI katika kupendana; kwa sababu upendano husitiri wingi wa dhambi.” (1Petro 4:8).

Unaona biblia inasema pia katika:

1Yohana 4:20. “Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona. NA AMRI HII TUMEPEWA NA YEYE, ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake”.

Pamoja na hayo biblia inatuambia hata tukiwa na uwezo wa kuzungumza lugha za malaika hata tukiwa na imani timilifu ya kuweza kuhamisha milima, hata tukitoa mali zetu kuwapa maskini, hata tukitoa miili yetu iungue kwa moto lakini kama hatutakuwa na huo Upendo unaozungumziwa kwenye Neno la Mungu..hatuwezi kuwa kitu mbele za Mungu.

Ukiangalia hayo kwa ukaribu utaona upendo ni kitu cha utofauti na kile tunachokidhania Upendo wa Mungu ni jambo linalojengeka ndani ya mtu katika kipindi cha muda, hivyo inahitaji bidii ya kulipalilia ili liumbike, vinginevyo itakuwa ni ngumu kulifikia..Embu turudi pale kwenye 1Wakoritho 13 tuone biblia inasema nini juu ya Upendo mkamilifu..

“4 Upendo HUVUMILIA, HUFADHILI; UPENDO HAUHUSUDU; upendo HAUTAKABARI; HAUJIVUNI;

5 HAUKOSI KUWA NA ADABU; HAUTAFUTI MAMBO YAKE; HAUONI UCHUNGU; HAUHESABU MABAYA;

6 HAUFURAHII UDHALIMU, BALI HUFURAHI PAMOJA NA KWELI;

7 HUVUMILIA YOTE; HUAMINI YOTE; HUTUMAINI YOTE; HUSTAHIMILI YOTE.

8 Upendo HAUPUNGUI NENO WAKATI WO WOTE; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika”.

Unaona unaweza kutoa mali zako zote kuwapa maskini, lakini je! uvumilivu upo ndani yako?, Tumaini lipo ndani yako? kustahimili mabaya kwa ajili ya Kristo kupo ndani yako? Adabu njema ipo ndani yako? majivuno yameondoka ndani yako?. Kuamini yote unayoambiwa na Mungu kupo ndani yako,? Unaweza ukasaidia maskini sana lakini je! Uchungu upo ndani yako? Unaweza ukawa na karama ya kunena kwa lugha na kuona maono, na kutabiri, lakini je! Unahesabu mabaya kwa ndugu yako n.k??.

Sasa hivi vyote vikiungana na kuonekana ndani ya mtu ndio Neno Upendo wa Mungu linaumbika. Lakini huwezi kusema wewe hauhusudu kama hutaonyesha bidii ya kutokufanya hivyo..kama wewe ni wa kukaa kuwazungumzia vibaya wengine, na bado ni mkristo, hata kama utakuwa una karama kubwa kiasi gani basi mbele za Mungu wewe si kitu ndivyo biblia inavyosema. Kama hutaonyesha bidii katika uvumilivu kwenye mambo yote kwanza kwa ajili ya imani yako na kwa ajili ya kudhulumiwa au kuonewa huwezi kusema upendo wa Mungu upo ndani yako.

Hivyo ni wajibu wetu sisi sote (mimi na wewe), kuonyesha bidii kuutafuta upendo kwasababu ndio kifungo cha ukamilifu, ndio kilele cha ukristo wetu. Na hii inakuja Kwa kuvitunza kwa bidii hivyo vigezo vilivyotelewa hapo juu, mpaka kufikia hatua ya vyenyewe kujengeka ndani yetu na kuwa ni TABIA yetu. Sasa tukishafikia hatua hiyo biblia inasema hapo sisi ni watu wakamilifu sana.

Wakolosai 3:14 “Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu”.

Tunapaswa tuyatawale maisha yetu kwa kanuni za Neno la Mungu, kwa bidii, kuonyesha zile tabia zinazoambatana na Upendo wake. Kila siku tukiyarekebisha maisha yetu, na kutengeneza upya pale tulipojikwaa jana, ikiwa tulishindwa kuwavumilia ndugu zetu au marafiki zetu kwa mabaya waliyotutenda na kukataa kuwasamehe, ni wakati wa kujirekebisha, kufanya bidii kusamehe, ikiwa tulikuwa tunatafuta mambo yetu wenyewe, tunapaswa tufanye bidii kubadilika, ikiwa tulikuwa hatufadhili tunapaswa pia tufanye bidii kufadhili, na kuwa na adabu ili tuonekane kuwa ni watoto wa Mungu. Na kufikia hatua ya kupendana sisi kwa sisi pasipo unafki,

1Yohana 4: 12 “Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote.

Tukipendana, Mungu hukaa ndani yetu, NA PENDO LAKE LIMEKAMILIKA NDANI YETU”.

Hivyo sisi sote tuzidi kuonyesha bidii katika kupendana mpaka tumfikie Bwana mwenyewe ambaye ni UPENDO.Kama Bwana wetu Yesu alivyofikia.

Ubarikiwe sana.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

LENGO LA SHETANI KWA WATOTO WA KIZAZI HIKI.

UKOMA NA UJANE ULIO NDANI YAKO, UMEUPATIA TIBA?

MKUMBUKE MKE WA LUTU.

USIACHE KUJIFUNZA NENO LA MUNGU

KAMA UNAPENDA MAISHA, NA KUTAKA SIKU YAKO IWE NJEMA.


Rudi Nyumbani

Print this post

NJIA YA MSALABA

Yohana 19: 16 “Basi ndipo alipomtia mikononi mwao ili asulibiwe; nao wakampokea Yesu.

17 Akatoka, hali akijichukulia msalaba wake, mpaka mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, au kwa Kiebrania, Golgotha.

18 Wakamsulibisha huko, na wengine wawili pamoja naye, mmoja huku na mmoja huku, na Yesu katikati.

19 Naye Pilato akaandika anwani, akaiweka juu ya msalaba, imeandikwa, YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI”

Bwana Yesu alisema mimi ndimi NJIA, na KWELI na UZIMA..mtu haji kwa Baba ila kwa njia ya mimi (Yohana 14:6). Litafakari hilo neno “ILA KWA NJIA YA MIMI” Kumbuka aliposema ILA KWA NJIA YA MIMI hakumaanisha kuwa wafuasi wake au washabiki wake.Hapana alimaanisha kitu kingine kabisa tofauti na hicho.

Tuchukue mfano leo hii, mwanariadha maarufu duniani, ambaye amepokea tuzo bora kuliko wote duniani…atoe sentensi aseme “mtu hawezi kuifikia tuzo niliyo nayo mimi isipokuwa kwa njia yangu mimi” je! Kwa sentensi hiyo unadhani atakuwa anamaanisha  kuwa ili mtu awe kama yeye anapaswa awe mshabiki wake au mfuasi wake??…Ni wazi hamaanishi hivyo, utagundua kuwa anamaanisha kwamba mtu akitaka kuwa kama yeye, ni lazima kwanza awe mwanariadha kama yeye, na pili awe na bidii kama za kwake, ajue mbinu anazozitumia za yeye kufanikiwa..

Unaona kwahiyo NJIA ya mwanariadha sio kuwa mshabiki wake wala mfuasi wake bali ni kuwa na bidii kama ya kwake, kufanya mazoezi magumu kama aliyoyafanya yeye, kujitoa kama alivyojitoa yeye, kutokata tama kama yeye asivyokata, kukubali kupitia changamoto zote kama alizozipitia yeye pasipo kukata tamaa n.k…Kwahiyo utagundua kuwa kumbe Kupata tuzo kama aliyoipata yeye sio jambo jepesi ni zaidi na kuwa mshabiki wake au kuwa mfuasi wake.

Kadhalika na Bwana Yesu aliposema mtu haji kwa Baba ila kwa njia yake yeye…hakumaanisha tuwe wafuasi wake, au washabiki wake, kwamba tumshabikie kila mahali tueleze sifa zake na umahiri wake tu, halafu inatosha, hapana alimaanisha kuwa ili mtu afike kwa Baba kama yeye atakavyofika, hana budi kupitia njia kama alizopitia yeye, na si njia nyingine yeyote.. Ilikuwa ili aipate tuzo iliyo bora ilimpasa, kudharaulika, kutukanwa, kutemewa mate kwa ajili ya Imani, kutengwa, kuchukiwa pasipo sababu na zaidi ya yote ilimpasa siku moja ABEBE MSALABA WAKE aelekee Golgotha.

“17 AKATOKA, HALI AKIJICHUKULIA MSALABA WAKE, mpaka mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, au kwa Kiebrania, Golgotha.”

Na yeye akasema mtu yeyote akitaka kumfuata na apitie njia hiyo hiyo, akubali kuchukiwa, akubali kutemewa mate, akubali kudharaulika kwa ajili ya Imani, akubali kukataliwa, akubali kuyaacha mambo ya ulimwengu hata ikiwezekana ndugu, wazazi na jamii na Mwisho wa yote na yeye pia akubali KUBEBA MSALABA WAKE kuelekea Golgotha yake kama yeye alivyofanya. Kwasababu hawezi kuwaambia watu wabebe misalaba yao na wakati yeye mwenyewe habebi.

 Ni njia ngumu lakini ndio Mungu aliyoichagua, tukitaka kufika kwa Baba mbinguni hatuna budi tupitie hiyo…hakuna njia nyingine ya Mkato, ni lazima tubebe Misalaba yetu. Ndio maana Bwana Yesu alisema mara nyingi kila mahali..

Mathayo 16: 24 “Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, MTU YE YOTE AKITAKA KUNIFUATA, NA AJIKANE MWENYEWE, AJITWIKE MSALABA WAKE, ANIFUATE. Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona”.

Na kama Mungu, alivyompa Bwana wetu Yesu Kristo nguvu ya kushinda majaribu mazito kama yale, nguvu hiyo hiyo atatupa sisi endapo tutakubali kumfuata yeye kwa mioyo yetu yote na kwa roho zetu zote. Endapo tutaikubali hii njia ya msalaba iliyodharaulika..

Bwana baada ya kudharaulika kwa ajili ya Imani, mwisho wa siku aling’aa kama jua, Biblia inasema aliidharau aibu,na hivyo Mungu akamuadhimisha mno, akamkirimi jina lile lipitalo kila jina.

Wafilipi 2: 8 tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.

9 Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina;

10 ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi;

11 na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba”.

Bwana atusaidie tusiwe WASHABIKI WAKE au WAFUASI WAKE, bali tuwe watu tunayoiendea njia yake, tukiwa ni walevi na bado tunajiita wakristo sisi bado ni washabiki, tukiwa tunaenda kanisani na bado tunasengenya sisi bado tu ni washabiki, gharama za mbio hatuzijui, ikiwa bado tunavaa nusu uchi na mavazi yasiyostahili mbele za Mungu, bado sisi ni washabiki hatutaweza kufika kwa Baba wanaofika kwa Baba ni wale wanaoiendea NJIA YA BWANA YESU KRISTO, yeye hakuwa mlevi, hakuwa mtukanaji, hakuwa mwizi, hakuwa mwabudu sanamu, hakuwa mwasherati, hakuwa mfuasi wa mambo ya ulimwengu huu. Hiyo ndiyo njia tunayowekewa tuifuate, kama Mwana wa Mungu kapitishwa kwa hiyo, unadhani sisi wengine tutatengenezewa njia nyingine mbadala ya mkato?? Hapana njia ni moja tu, na imeshawekwa na kuthibitishwa na Mungu nayo ni njia ya YESU KRISTO.

Hivyo kama hujampa Bwana Yesu Maisha yako, usikawie kufanya hivyo, nyakati hizi tunazoishi ni za hatari, muda unakaribia kusimamishwa, na umilele kuanza, Bwana asirudi leo na kukukuta upo hivyo ulivyo, asikukuta katika hali hiyo ya uvuguvugu uliyo nayo, Mkabidhi leo maisha yako kikamilifu, kwa kudhamiria kabisa kutoka moyoni mwako, Kuanza maisha mapya na UKAIFUATE NJIA YA MSALABA, na yeye mwenyewe atakuwezesha kuiendea, Na kuumaliza mwendo salama. Ili siku ile uwe na ujasiri wa kusimama mbele zake.

Wafilipi 1: 6 “..yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu;

Bwana akuangazie Neema yake.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Print this post

NJIA YA BWANA INATENGENEZWA WAPI?

Kabla Bwana YESU kuanza huduma yake ya wokovu hapa duniani, Ilimpendeza Mungu amtangulizie kwanza mtu atakayemwandalia mazingira mazuri ya yeye kufanyia huduma yake, mtu atakayemtengenezea njia ya kupendeza iliyonyooka ili apate kupita juu yake. Mungu hakuona vema mwanawe mpendwa afanye kazi katika mazingira ambayo hayajaandaliwa kwa namna yoyote, hivyo kwa hekima zake nyingi akaona ni vema amtangulize kwanza mtu atakayeanza kuzungumzia habari za kuja kwake kabla ya yeye kufika, kusudi kwamba atakapofika watu wawe tayari kumpokea kwa furaha, kadhalika awe mtu atakayeigusia habari ya injili ambayo yeye atayaokuja kuihubiri mbeleni na ndio hapo tunakuja kumuona Yohana mbatizaji akihubiri habari za ubatizo na toba pamoja na ufalme wa mbinguni mambo ambayo hayakujulikana na wayahudi hapo mwanzo.

Na injili hiyo hiyo ya ufalme wa mbinguni ndiyo YESU aliyoanzana nayo katika huduma yake. Jambo lililomfanya Yohana kuonekana mtu MKUU sana katika ufalme wa mbinguni kuliko hata wote waliomtangulia katika agano la kale. Kwasababu yeye pekee ndiye aliyefanikiwa kumtengenezea Mungu NJIA ya kutembelea hapa duniani hakukuwa na mwingine yeyote aliyefanikiwa kufanya vile au kufikia viwango vile kabla yake.

Marko 1: 1 “Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.

2 Kama ilivyoandikwa katika nabii Isaya, Tazama, namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, ATAKAYEITENGENEZA NJIA YAKO.

3 Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake.

4 Yohana alitokea, akibatiza nyikani, na kuuhubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi.

5 Wakamwendea nchi yote ya Uyahudi, nao wa Yerusalemu wote, wakabatizwa katika mto wa Yordani, wakiziungama dhambi zao.

6 Na Yohana alikuwa amevaa singa za ngamia na mshipi wa ngozi kiunoni mwake, akala nzige na asali ya mwitu”.

Lakini swali la kujiuliza hapo ni kwanini Yohana alionekana kuwa ni mtu azungumzaye kutoka NYIKANI. Tunapaswa tujue maana ya maisha yake ya nyikani na jangwani, ili kwamba tufahamu ni kitu gani kilichompelekea awe mtu wa namna ile, kumbuka Mungu huwatumia manabii wake kuwa ISHARA kwa ajili ya Neno lake ili kufunua mambo ya rohoni. Sasa kama tukisoma Isaya 40:3 inasema..

Isaya 40:3 “Sikiliza, ni sauti ya mtu aliaye, ITENGENEZENI NYIKANI njia ya Bwana; NYOSHENI JANGWANI njia kuu kwa Mungu wetu.

4 Kila bonde litainuliwa, Na kila mlima na kilima kitashushwa; Palipopotoka patakuwa pamenyoka, Na palipoparuza patasawazishwa;

5 NA UTUKUFU WA BWANA UTAFUNULIWA, Na wote wenye mwili watauona pamoja; Kwa kuwa kinywa cha Bwana kimenena haya.”

Unaona hapo?. Isaya anasema NJIA YA BWANA haitengenezwi mahali pengine popote isipokuwa nyikani, kadhalika NJIA KUU YAKE hainyooshwi mahali pengine popote isipokuwa jangwani..Hivyo JANGWANI na NYIKANI ni mahali ambapo njia ya Bwana inapotengenezewa..

Na ndio maana tunaomwona mtu kama Yohana Mungu alimtumia kama ishara ya wazi kuwa mtu wa majangwani na nyikani kuonyesha kuwa huko ndiko Njia ya Mungu inapotengenezewa..Yeye aliufahamu ujumbe huo ambao nabii Isaya aliuhubiri kwa miaka zaidi ya 700 iliyopita, akajua hilo Neno si la mtu Fulani pekee tu, bali ni kwa yeyote atakayeliishi, na hilo Neno linaishi kwa kila kizazi na ndio maana utamwona japo Yohana alikuwa ndiye mtu aliyemtengenezea Bwana njia lakini bado aliwahubiria watu na makutano kuwa wao nao WAMTENGENEZEE BWANA NJIA YA KUSHUKIA..

Ukiendelea kusoma hapo katika Isaya utaona inasema:

“4 Kila bonde litainuliwa, Na kila mlima na kilima kitashushwa; Palipopotoka patakuwa pamenyoka, Na palipoparuza patasawazishwa;

5 NA UTUKUFU WA BWANA UTAFUNULIWA, Na wote wenye mwili watauona pamoja; Kwa kuwa kinywa cha Bwana kimenena haya.”

Sasa mabonde yanayozungumziwa hapo ni mabonde yote yanayoweza kukwamisha kusudi la Mungu lisifunuliwe kwa watu wake kupitia wewe, hayo yote yataondolewa si pengine zaidi ya jangwani na nyikani, milima yote, na makando kando yote yanayoweza kukwamisha utukufu wa Mungu usifunuliwe juu ya watu wote yataondolewa pale tu mtu atakapokubali kuipitia njia ya nyikani na jangwani.

Kumbuka wana wa Israeli wasingeweza kumjua Mungu wa Yakobo ni nani na anataka nini katika maisha yako kama ingekuwa ni kutoka tu Misri na moja kwa moja kufika Kaanani, japo waliuona kweli mkono wa Mungu ukiwapigania na kuwashindania dhidi ya maadui zao, kwa ishara nyingi na miujiza mingi lakini bado wangefika nchi ya ahadi pasipo kumjua Mungu wanayemtumikia. Iliwapasa kwanza wapitie njia ya JANGWA NA NYIKA muda mrefu ili Mungu awape amri zake na sheria zake. Iliwapasa wapitie kule ili Mungu aondoe vinyago vilivyokuwa ndani ya mioyo yao. Walikaa nyikani mbali na mataifa mengine kwa muda mrefu wakilishwa tu mana siku zote walizokuwa kule jangwani. Mungu hakuwaruhusu wafanye biashara yoyote na mataifa ya pembeni, wala shughuli zozote za kimaisha, yeye pekee ndiye aliyekuwa anawalisha mana. Aliwatenga mbali sana na tamaa za ulimwengu na macho mahali ambapo ukiangalia mkono wa kulia huoni miji wala majengo mazuri isipokuwa milima na mabonde tu kwa muda wa miaka mingi, mahali pakame sana, walisahau anasa na vitu vitamaniwavyo vya ulimwengu huu, Mungu aliwaua kwa habari ya dunia, aliwanyenyekeza kiasi kwamba vile viburi walivyotoka navyo Misri hawakuingia navyo Kaanani.

Na huko ndiko walipotoka na sheria na kanuni za kutembea na Mungu katika hiyo nchi waliyokuwa wanaiendea. Huko ndipo walipomtengenezea Mungu NJIA KUU ya kutembelea kwa utukufu wake.

Milima yote ya kiburi ilishushwa kule jangwani, mabonde yote ya ouvu yalisafishwa walipokuwa kule jangwani. Walipokuwa wanasua sua kwa kutokumwamini Mungu walitengenezwa upya Hivyo walipokuwa wakiingia katika nchi ya ahadi walikuwa tayari kwa kumtumikia Mungu na kwa kupitia wao MUNGU KUONYESHA UTUKUFU WAKE KWA MATAIFA YOTE YA DUNIA NZIMA.

Mwangalie Musa, mwanzoni alidhani kuwa anaweza kuwaokoa wana wa Israeli,kwa siasa na elimu yake na cheo chake alichokuwa nacho Misri, lakini haikuwa hivyo badala yake ndio alijitafutia matatizo, mpaka pale alipokimbilia jangwani huko nchi isiyokuwa na raha zile alizokuwa anazipata katika jumba la kifalme Misri, na kukaa huko muda mrefu kumtafakari na kuulizia juu Mungu wa baba yake Ibrahimu. Mungu alimtweza huko kwa muda wa miaka 40, akiiua ile asili ya kidunia iliyokuwa ndani yake, akiishusha milima yote ya majivuno iliyokuwa imejificha ndani yake, akitoa elimu yake ya kipagani iliyokuwa imeujaza moyo wake kwa muda wa miaka 40 alikuwa anamwandalia tu Mungu njia ya kupitia, mpaka pale alipokamilishwa biblia inasema alikuwa ni mjuzi wa usemi na kunena [mwanasiasa mzuri] (Matendo 7:22) lakini alipokutana na Bwana hata ule ujuzi wake wa kuongea hakuwa nao tena ndani yake ulishakufa, Bwana pia anamshuhudia Musa na kusema kuwa yeye ndio alikuwa mtu MPOLE kuliko wote duniani(Hesabu 12:3), jaribu kufikiria jambo hilo, utagundua kuwa kutembea na Mungu au kuwa karibu na Mungu sio kiwango cha upako ulichonacho, hapana bali ni jinsi gani moyo wako umeandaliwa katika kanuni azitakazo yeye. Sasa baada ya Musa kufikia viwango hivyo ndipo UTUKUFU WA MUNGU ULIPOFUNULIWA JUU YAKE. NA WATU WOTE WAKAUONA.

Mambo yanatupa mwongozo gani katika Roho?.

Kumbuka Wana wa Israeli katika mwili ndio sisi(Wakristo) katika roho. Kwasababu hata Bwana wetu aliandikiwa hivyo..katika Mathayo 2:15 ikisema…Kutoka Misri nalimwita mwanangu..Unaona maneno hayo yalikuwa ni ya wana wa Israeli, baadaye yakaja kuwa ya Bwana wetu Yesu Kristo kadhalika pia ni ya kwetu sisi leo hii kama tukitii KUTOKA MISRI MUNGU ALITUITA..Na kama tuliitwa kweli kutoka Misri hatuna budi kupitia njia ya nyikani na jangwani ili kuifikia nchi ambayo Mungu ataachilia UTUKUFU WAKE kuwaokoa wengine.

SASA NYIKANI NA JANGWANI NI WAPI KWA SASA?.

Unapopompa Bwana maisha yako kwa mara ya kwanza, hauna budi kuwa radhi kusalimisha kila kitu chako kwake ili aweze kukufanya kuwa mwanafunzi wake, ili Mungu baadaye aweze kukutumia wewe kuachilia utukufu wake uwaangazie wengine ni sharti ukubali kutii kupitia madarasa ya Mungu na ndio maana Bwana Yesu aliwaambia maneno haya wale wote ambao walitaka kuwa wanafunzi wake.

Luka 14.25 “Makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia,

26 Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

27 MTU YE YOTE ASIYEUCHUKUA MSALABA WAKE NA KUJA NYUMA YANGU, HAWEZI KUWA MWANAFUNZI WANGU.

28 Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia?

29 Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki,

30 wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza.

31 Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini?

32 Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali.

33 BASI, KADHALIKA KILA MMOJA WENU ASIYEACHA VYOTE ALIVYO NAVYO, HAWEZI KUWA MWANAFUNZI WANGU.”

Unaona hapo?. Zipo gharama za kuwa mwanafunzi, kumbuka sio watu wote wanaweza wakawa wanafunzi wa Kristo,. Kama Usipokuwa tayari kupoteza kila kitu ulichonacho kwa ajili ya Kristo, kama vile mwanafunzi shuleni, anasahau kabisa dunia ikoje anakaa bweni miaka kadhaa akisoma tu,asijishughulishe na kitu kingine na kusahau tamaa za nje alizokuwa anaziona, na ndivyo ilivyo kwa wale wanaopenda kuwa wanafunzi wa Kristo, usipokubali kupita katika njia ya jangwa na kuishi maisha ya kumwangalia yeye tu, hutaweza kuwa mwanafunzi wake, usipokuwa tayari kuichukia hata nafsi yako kwa ajili ya Kristo, usipokuwa tayari kuacha anasa zako, usipokuwa tayari kuacha hizo biashara haramu kwa ajili ya Kristo, na usipokuwa tayari kuchukiwa na ndugu, hata wakati mwingine wazazi kwa ajili ya Kristo, huwezi kuwa mwanafunzi wake, usipokuwa tayari kuishi kwa kumtegemea Mungu tu, akufundishe, kama wana wa Israeli jangwani, kama Yohana jangwani, kama Musa jangwani, kama Eliya jangwani, kama Elisha nyikani, huwataweza kumwandalia Mungu njia ya kushukia. Usipokuwa tayari kupoteza vitu uvipendavyo kwa ajili ya madarasa ya Kristo hutaweza kumtengenezea njia ya yeye kushukia.

Isaya 40:3 “Sikiliza, ni sauti ya mtu aliaye, ITENGENEZENI NYIKANI njia ya Bwana; NYOSHENI JANGWANI njia kuu kwa Mungu wetu.

Hivyo yeye atakayeshinda kulivuka hilo jangwa na hiyo nyika ambayo Mungu atampeleka huko makusudi kwa ajili ya kumfundisha hapo ndipo atatiwa mafuta na Mungu mwenyewe ili kuwahudumia watoto wake.

Bwana Yesu anasema mtu wa namna hiyo ni mkuu zaidi ya nabii yoyote yule. Mtu yoyote Yule ambaye atamtengenezea Bwana njia iliyonyooka, huyo ni mkuu kushinda nabii yoyote Yule alishawahi kutokea duniani Bwana YESU anasema hivyo.

Mathayo 11:9…..Naam, nawaambia, na aliye mkuu zaidi ya nabii.

10 Huyo [mtu huyo] ndiye aliyeandikiwa haya, Tazama, mimi namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako mbele yako.

Hivyo kama na sisi tunataka tuwe wajumbe watakaomtangulia mbele yake, inatupasa tumwandalie njia kwanza kabla ya kufika, na njia haiandaliwi mahali popote tu isipokuwa NYIKANI NA JANGWANI.

Tusijidanganye tunasema sisi ni watumishi wa Mungu, sisi tuna nena kwa lugha, sisi tuna upako, sisi tunatoa pepo, sisi tunaponya magonjwa, na huku madarasa ya Mungu tumeyakwepa, na huku ndani ya mioyo yetu tuna viburi, ndani ya mioyo yetu tuna sanamu, ndani ya mioyo yetu hatujaumbiwa saburi na unyenyekevu, ndani ya mioyo yetu ni wanung’unikaji, tusijidanganye ikiwa tumelikwepa hilo jangwa ambalo kwa hilo tungefundishwa sheria na kanuni za Mungu,

Na maombi yangu, tusikwepe madarasa ya Mungu yanapoletwa mbele yetu, pale tunapoteremshwa jangwani tusipindishe njia na kutaka kurukia moja kwa moja Kaanani siku hiyo hiyo, Mungu huwa anatembea katika kanuni zake, ikiwa wewe ni mtoto kweli wa Mungu siku inakuja Mungu atakapeleka nyikani tu, hilo ni darasa lisilokwepeka. vinginevyo mbele za Mungu tutaonekana watoto wachanga tusiomjua yeye. Hawakuwa na bahati mbaya mitume wa Kristo kupoteza vyote walivyonavyo kwa ajili ya Kristo, kadhalika haitakuwa bahati mbaya kwetu nasi tukipoteza vyote tulivyonavyo kwa ajili ya Kristo, kwasababu hiyo ndiyo njia pekee ya kuwa WAKUU MBELE ZA MUNGU na kuwa wanafunzi wake.

Ubarikiwe sana.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

MBINGUNI YUPO NANI SASA?

MELKIZEDEKI NI NANI?.

MWEZI NI ISHARA GANI KWETU?.

SEHEMU YA MAANDIKO ILIYOFICHWA.

MAVAZI YAPASAYO


Rudi Nyumbani

Print this post

UMEFUNGWA KATIKA GIZA NA UVULI WA MAUTI?

Ni rahisi kudhani kuwa watu wote walio waovu, au wauaji au wanaofanya vitendo vya giza kama vile uchawi ni mambo ambayo walizaliwa kuyapenda, na hiyo wakati mwingine inapelekea hata maombi yetu kwa Mungu tunayoyaelekeza kwao ni ya kifo tu, na si kingine. Lakini hatujui kuwa wengi wao wanaofanya mambo kama hayo mwanzoni hawakuwa na nia ya kuwa wachawi, au wauaji, bali ilitokea kuna wakati waliingiwa na tamaa ya kitu Fulani labda tuseme mali, na ndani ya mawazo yao wanafikiria mali tu na si kingine, huo ndio mtengo mkubwa shetani anaowanasia watu kwasababu biblia ilishasema katika..

1Timotheo 6.10 “Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni KUPENDA FEDHA; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.”

Unaona sasa katika kuhangaika kwao ndio wanajikuta kidogo kidogo wanaanza kwenda kwa waganga, na kule kwa mganga anapewa labda masharti Fulani ambayo yanamgharimu kuwa mshirikina, na kwa jinsi siku zinavyozidi kuendelea, kwa kuwa lengo la shetani ni kumvuta kwake ili awe mtumishi wake wa UHARIBIFU hivyo anampa vitu anavyovihitaji kwa muda na baadaye analazimishwa kuwa mchawi na huko ndiko anapopewa majukumu makubwa hata ya kutoa roho za watu ili tu aendelee kuishi na kwamba asipofanya hivyo yupo katika hatari ya kuuliwa yeye naye, sasa hatua hiyo aliyofikia hata akijaribu kutoka hawezi, haoni pa kukimbilia, hivyo anajikuta anamalizia kuendelea tu hivyo hivyo huku dhamira yake ikiugua kila siku akifahamu kuwa anayofanya sio sahihi, lakini hawezi kutoka kwasababu ameshaingia katika mtego asioweza kujinasua tena..

Na sisi kwa kuwa hatuna jicho lingine la mbali katika ulimwengu wa roho tunawaombea kifo,.Hatujui kuwa chanzo cha mambo yote ni ibilisi. Kadhalika unakuta na mtu mwingine alijiingiza katika kazi za ujambazi, lengo lake halikuwa kuuwa watu, hapana bali ni kupata mali, sasa hajui kuwa kumbe ni lengo la shetani kumfanya awe muuaji, pasipo kufahamu yeye anaingia huko, na mwisho wa siku katika harakati zake za wizi, siku moja pale anapoona kuwa anakaribia kukamwata analazimika kutoa bunduki na kumpiga mtu na kumuua pasipo yeye mwenyewe kupenda kwa lengo la kujilinda. Lakini sisi huku tunasema Yule jambazi ni katili sana, hana hata huruma.

Kadhalika wapo watu wengine ambao sio wachawi na wala sio wafanyaji wa vitendo viovu, lakini shetani naye anafanikiwa kuwanasa katika mitego yake ya uharibifu.

Kwamfano ngoja nikupe kisa kimoja ambacho kimetokea hapa mtaani kwetu wiki hii.

Kuna kijana mmoja mdogo tu kama miaka 18, ni kijana ambaye ni mtulivu, hakuwa mlevi wala mtumiaji wa sigara, wala hakuwa katika vikundi vya vijana waporaji wa mitaani, lakini ghafla siku ya jumapili tulipata habari kuwa amejinyonga kwa kamba ndani kwao. Na kule kwenye msiba kulikuwa na mtu mwingine aliyehudhuria msibani naye anasema ndugu yake wiki hii hii kajinyonga. Sasa Kama ukichunguza watu wa namna hii vyanzo vinavyowapelekea wao mpaka kufikia hatua hiyo ngumu namna hiyo za kujitoa uhai hazijulikani..

Kwamfano huyu kijana wa kwanza alishawahi kujaribu kujiua mara mbili, haukufanikiwa moja alijaribu kumvamia dereva wa dalala ili aachie usukani gari lipinduke watu wafe pamoja naye kwenye gari, lakini alishikiliwa na watu, na baadaye kupigwa sana nusu kuuawa, na mara ya pili tena alikunywa sumu lakini walimuwahi akapona.

Sasa kwa namna ya kawaida kwa nje, ni rahisi kusema hawa watu ni WAJINGA, WAUAJI, au WANA DHAMBI NYINGI, WAKATILI, MASHETANI n.k. pasipo kujua kuwa wamenaswa katika mitego ambayo hawawezi kutoka kiuwepesi kama wewe unavyodhani na ndio maana wamelazimika kufanya hivyo, sio kwa hiari yao bali ni sababu ya vifungo vya giza kutoka kwa yule adui zimewafanya kuwa hivyo au kufanya vitendo kama hivyo.

Nguvu hiyo hiyo ilimnasa hata mmoja wa mtume wa BWANA wetu YESU KRISTO, naye ni Yuda, ambaye yeye ndio kabisa alikuwa anakula na kutembea na Bwana kila mahali je! Si zaidi kutunasa na sisi watu wa kawaida tusipokuwa makini?. kumbuka lengo la Yuda halikuwa kumsaliti Bwana ili auawe, hapana bali lilikuwa ni fedha tu basi, lakini kwasababu shetani alikuwa anaona mbali akijua kabisa Yuda atajutia kwa tendo lile na kisha baadaye amshawishi ajinyonge hivyo akatumia udanganyifu wa mali kumvuta kwake, na aliponaswa, akiona kuwa maji tayari yameshamwagika hayawezi tena kuzoleka. sasa ile nguvu ya adui ndipo ilipoanza kufanya kazi ndani yake kumpa sababu ya yeye kujiondoa uhai wake..Usidhani ni rahisi kujinasua unapofika katika hatua kama hiyo..Ni ngumu sana hapo inahitaji mkono wa Mungu ulio hodari..Lakini Yuda alizidiwa mpaka kufikia hatua ya KUJINYONGA.

Watu wa namna hii wapo wengi, wamenaswa katika mitego ya adui ya namna mbali mbali na hawawezi kutoka, inawezekana wewe unayesoma habari hii ni mmojawapo. Imefika hatua umezama kwenye uchawi na ushirikina wa viwango vya juu na unaona ni ngumu kutoka tena huko, umezama katika uuaji, umetoa mimba nyingi, umeua watu na shetani anakuambia kuwa wewe dhambi yako haiwezi kusameheka tena, na hivyo unahitaji njia ya kuutoa uhai wako, pengine umekata tamaa ya kuishi baada ya kugundua kuwa umeambukizwa ukimwi au unaugonjwa wa kufisha kama saratani, hivyo kila siku unatamani roho yako itoke usiendelee kuishi tena unatamani hata upate ajali ufe. Ndugu usifanye hivyo yupo tabibu anayeweza kuuganga moyo wako na kukufanya kuwa upya tena kana kwamba hukuwahi kutenda dhambi yoyote, kana kwamba hukuwahi kuumwa, au kumkosea Mungu.

Kama yeye mwenyewe anasema WENYE AFYA HAWAHITAJI TABIBU, BALI WALIO HAWAWEZI.(Mathayo 9:12).Huhitaji kudhani kuwa tatizo lako halina mtetezi..Kumbuka moja ya makusudi maalumu Bwana YESU yaliyomleta duniani ni pamoja na hiyo ya kuwaganga waliovunjika mioyo, na waliofungwa kufunguliwa kwao. Na hakuna yoyote mwingine zaidi yake anayeweza kuwa na hiyo Taaluma.

Isaya 61: 1 “Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao”.

Yeye pekee ndiye anayeweza kukupa wewe tumaini la uzima, haijalishi umeasi kiasi gani, haijalishi umefungwa katika vifungo vikubwa kiasi gani haijalishi umeshajiunga katika vikundi vya kichawi (occultic groups) vingi kiasi gani, haijalishi umeloga au umehudhuria kwa waganga wengi kiasi gani, haijalishi umeuwa na umetoa mimba nyingi kiasi gani, haijalishi una ugonjwa wa mauti kiasi gani ambao uliupata kwa kutokana na uzembe wako wa kuzini ovyo, hiyo haijalishi embu soma hapa:

Zaburi 107: 10 “Waliokaa katika giza na uvuli wa mauti, Wamefungwa katika taabu na chuma,

11 KWA SABABU WALIYAASI MANENO YA MUNGU, WAKALIDHARAU SHAURI LAKE ALIYE JUU.

12 Hata akawadhili moyo kwa taabu, Wakajikwaa wala hakuna msaidizi.

13 WAKAMLILIA BWANA KATIKA DHIKI ZAO, AKAWAPONYA NA SHIDA ZAO.

14 ALIWATOA KATIKA GIZA NA UVULI WA MAUTI, AKAYAVUNJA MAFUNGO YAO.

15 Na wamshukuru Bwana kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu.

16 Maana ameivunja milango ya shaba, Ameyakata mapingo ya chuma.”

17 WAPUMBAVU, KWA SABABU YA UKOSAJI WAO, Na kwa sababu ya maovu yao, hujitesa.

18 Nafsi zao zachukia kila namna ya chakula, Wameyakaribia malango ya mauti.

19 Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao.

20 HULITUMA NENO LAKE, HUWAPONYA, HUWATOA KATIKA MAANGAMIZO YAO”.

Bwana leo atalituma Neno lake na kukuponya kama utakuwa tayari kumruhusu yeye ayabadilishe maisha yako. Uwe tu tayari kutubu dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha kabisa, uwe tayari kusema kuanzia leo mimi na ulimwengu basi, mimi na shetani basi, mimi na dhambi basi namgeukia Bwana Yesu, tumaini langu, kisha ukishatubu hatua inayofuata ni kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO ili upate ondoleo la dhambi zako, popote pale upendapo. Na kuanzia hapo na kuendelea Bwana atakupa uwezo wa kipekee wa kumshinda adui, hayo mapepo yaliyokufunga na yaliyokuwa yanakutishia kukuua yataondolewa na YESU mwenyewe,bila hata kutumia nguvu. huo ugonjwa wa mauti wanaosema hauponyeki YESU KRISTO atakuponya, hiyo hofu ya kutokusamehewa iliyo ndani yako na inayokutaka ujiue,jua tu ni ibilisi ndio kaiweka na Yesu pekee ndio ataiondoa.. Hivyo chukua uamuzi sasa maadamu damu ya Yesu ipo kukuganga, usisubiri baadaye au kesho, saa ya wokovu ni sasa.

Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; NANYI MTAPATA RAHA NAFSINI MWENU;

30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”

RAHA YA NAFSI YAKO UTAIPATA KWA YESU TU PEKEE.

Ubarikiwe sana.Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Print this post

MAFUNDISHO YA MASHETANI

1 Timotheo 4 : 1 “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani;”

Biblia inasema, nyakati za mwisho wengine, watajitenga na IMANI, Imani inayozungumziwa hapo si imani nyingine zaidi ya Imani katika Yesu Kristo.

Mungu alimuumba mwanadamu na sehemu mbili, Sehemu ya Roho na Sehemu ya mwili.

Sehemu ya mwili ndio hii tunayoiona kwa macho, milima, mabonde, miti, nyumba, bahari, wanadamu, wanyama n.k. Na sehemu ya Roho hatuioni kwa macho, imefungwa kwetu wanadamu.

Sehemu hii ya Roho ndio mahali Mungu, anapoonekana, na ndio mahali malaika wanapoonekana na ndio mahali shetani na malaika zake wanapoonekana, ndio mahali vita vinapopiganwa na ndio mahali vyanzo vya mambo yote vinapotokea.

Sasa baada ya Adamu kuanguka, Bwana hajaruhusu tuingie katika ulimwengu wa Roho, hakuruhusu macho yetu ya Roho yafumbuliwe tuone kila kitu kinachoendelea katika ulimwengu wa Roho.Na endapo tungefumbuliwa macho tuone mambo gani yanaendelea katika ulimwengu wa Roho duniani kusingekuwa mahali pa kukalika, kwasababu tungekuwa tunaona mambo mengi mno ya ajabu, na kila siku tungekuwa tunaona mambo mapya. Tungekuwa tunaona mambo mengine ambayo yangekuwa hata hayatusaidii..Ingekuwa ni dunia iliyojaa vurugu mno. Kwasababu ulimwengu wa Roho umejaa mambo mengi.

Tuchukue mfano, wakati ule Nabii Elisha alipomwomba Mungu amfungue macho Yule mtumwa wake, na alipofunguliwa macho aliona kilima chote kimejaa jeshi la malaika wenye upanga..Sasa kumbuka malaika hata siku moja hawapigani na wanadamu, bali wanashindana na majeshi ya mapepo wabaya.. kwahiyo kama kulikuwa na majeshi ya malaika wa mbinguni, ni wazi kuwa yalikuwepo pia majeshi ya mapepo yaliyokuwa tayari kushindana na lile jeshi la malaika, kwahiyo kama Bwana angeruhusu Yule mtu aendelee kuona yale mambo ya rohoni ni wazi kuwa angeona vita viwili vinaendelea, vya kwanza vya malaika na vya pili vya wanadamu.

2 Wafalme 6: 15 “Hata asubuhi na mapema mtumishi wake yule mtu wa Mungu alipoondoka, na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi la watu, na farasi na magari, wameuzingira mji ule. Mtumishi wake akamwambia, Ole wetu! Bwana wangu, tufanyeje?

16 Akamjibu, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.

17 Elisha akaomba, akasema, Ee Bwana, nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona. Bwana akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote”.

mafundisho ya mashetani

Kwahiyo unaweza ukaona kuwa ulimwengu wa Roho, wa malaika upo, na una mambo mengi mno, yasiyoelezeka na mengine ni magumu kuyatambua, yamekaa kimafumbo jaribu kufikiri Yohana aliyeandika kitabu cha ufunuo anaona malaika wana Uso wa TAI, mwingine ana kichwa cha NDAMA, mwingine ana kichwa kama cha SIMBA na bado wana mabawa, na wana kwato!! Umewahi kujiuliza hivyo viumbe endapo tukiwa tunaviona kila siku duniani kutakuwaje?? Nabii Ezekieli naye alionyeshwa mambo hayo hayo,Nabii Isaya naye alionyeshwa mambo hayo hayo, lakini hawakuyaelewa kwa undani mambo hayo kwasababu ni mambo ya Rohoni.

Kwahiyo ni wazi kuwa Sio mpango wa Mungu, tuwe na uwezo kila dakika kuyaona mambo ya rohoni, vinginevyo maisha yatakuwa hayana maana.

Lakini maandiko yanasema Yohana 4.23 Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. 24 MUNGU NI ROHO, NAO WAMWABUDUO YEYE IMEWAPASA KUMWABUDU KATIKA ROHO NA KWELI.”

Sasa hapa ndipo pa kuzingatia sana, maana pasipoeleweka vizuri, ni rahisi shetani kumzamisha mtu katika MAFUNDISHO YA MASHETANI.

Biblia inasema “saa yaja ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli”

Biblia iliposema “katika roho na kweli” haikumaanisha kuwa itafika wakati tutakuwa tunazama katika ulimwengu wa roho na kufikia kumwona Mungu na malaika, na hatimaye kumwabudu tukiwa tunamwona wazi kama tunavyowaona mwanadamu wenzetu.. Hapana haikumaanisha hivyo…

Na Shetani ndipo alipoanzia hapa kupandikiza mafundisho yake ya mashetani.

Nini maana ya kumwabudu Mungu katika ROHO NA KWELI?

Kabla ya kujua maana ya kumwabudu Mungu katika roho na kweli, hebu turudi nyuma kidogo…Kumbuka kama tulivyosema ulimwengu wa Roho ni ulimwengu wa Malaika, ikiwa na maana kuwa vita vyote na mambo yote yanayoendelea katika ulimwengu wa Roho Mungu huwa anawatumia malaika zake kuyafanikisha, mambo hayo namna ya kuyafanya na jinsi ya kuyafanya hayamuhusu mwanadamu hata kidogo sio sehemu ya mwanadamu..Ni kazi ya malaika Kwamfano Mungu alipomtuma Malaika Gabrieli kwa Mariamu kumpa taarifa za kuzaliwa kwa Mwokozi Bwana Yesu Kristo namna ya kuitengeneza ile mimba tumboni mwa Mariamu pasipo Mwanaume kuhusika haikuwa kazi ya Mariamu, au mwanadamu yoyote yule bali ilikuwa ni kazi ya Malaika wa Mungu katika uwezo wa Roho.

Mungu alipoyaleta yale mapigo yote kwa farao, na kuwaongoza katika lile jangwa kimiujiza haikuwa kazi ya mwanadamu kuyatengeneza yale mapigo..mwanadamu alikuwa na kazi yake tutakuja kuiona mbele kidogo.

Kadhalika kazi ya kuleta tauni katikati ya watu wakati wa Mfalme Daudi haikuwa kazi ya wanadamu bali ilikuwa ni kazi ya Malaika wakifanya kazi katika ulimwengu wa roho..Hao ndio Bwana aliowatia mafuta kuweza kufanya mambo makubwa yasiyowezekana kwa namna ya kawaida.

Sasa mwanadamu ambaye anamcha Mungu hajapewa maarifa hayo, mwanadamu anayemcha Mungu hajapewa uwezo wa kuingia kwenye ulimwengu wa roho na kutengeneza mambo au kuingia na kupambana na roho za malaika walioasi.

Sasa uwezo mwanadamu anayemcha Mungu aliopewa na Mungu ni mwongozo wa namna ya kuwafanya hawa malaika waweze kumhudumia yeye. Mwongozo wa namna ya kutembea na kundi hili la malaika watakatifu.

Ni sawasawa na mwanadamu na Farasi, mwanadamu hajapewa uwezo wa kukimbia kwa kasi kama farasi, hajapewa mapafu kama ya farasi, lakini amepewa uwezo wa kumwongoza Yule farasi amtii yeye ampeleke katika mwendo anaotaka..

Na huo mwongozo mwanadamu aliopewa utakaomsaidia yeye kutembea na malaika walio na nguvu na uwezo katika ulimwengu wa Roho ni BIBLIA TAKATIFU (yaani NENO LA MUNGU). Ni kama tu Mtu asiyekuwa na MANUAL ya kuendesha gari, hataweza kuliendesha gari hilo hata iweje, kadhalika mtu ambaye hajafundishwa namna ya kumpanda farasi na kumwendesha hataweza kumwendesha, badala yake anaweza akajikuta hata akajeruhiwa na Yule farasi farasi.

Naamini kidogo kidogo utakuwa umeshaanza kuelewa nini maana ya kuingia katika ROHO…Kwahiyo maana ya kuingia katika roho sio kugeuka na kuanza kujifananisha na malaika, au mapepo hapana bali ni kuelewa uwezo uliopewa wa kutembea na malaika ambao hao ndio wanaojua namna ya kutengeneza mambo katika ulimwengu wa roho.

Kwasababu hiyo basi Mwanadamu anayemcha Mungu hawezi akajua njama za adui zote na elimu yake kwa mapana na marefu, hawezi akajua idadi ya mapepo yaliyopo, hawezi akajua yanafanyaje fanyaje kazi..malaika watakatifu ndio wanaojua (wamepewa uwezo huo na Mungu mwenyewe) ..Sisi tunachojua tu tukitaka tulindwe na Yule adui Kwanza tumwamini Bwana Yesu Kristo, kisha tukabatizwe kisha tuishi maisha matakatifu na ya uangalifu, tukidumu katika kusali na ushirika. Hiyo inatosha kabisa kuwafanya wale malaika watakatifu watupiganie dhidi ya mapepo wabaya.

Tukitaka tusife tuishi maisha marefu, wale malaika Bwana aliowapaka mafuta katika ulimwengu wa Roho wanajua namna ya kumzuia shetani na mapepo wake wasituguse mpaka tutakapotimiza umri wa kuondoka duniani, hivyo kama maandiko yanavyosema “waheshimu baba yako na mama yako upate siku nyingi na za heri” hivyo wale malaika watakatifu wanatembea na mtu anayelishika neno hilo, na mtu Yule anajikuta anakingiwa na ajali na dhiki za Yule mwovu na kutimiza umri wa maisha yake..Sasa huyu mtu tayari kashaingia katika roho. Anakuwa anamwabudu Mungu katika roho na kweli. Kwasababu maneno ya Yesu Kristo ndio Roho. (Yohana 6:63)

Au mtu wa Mungu anapoumwa wale malaika wanaohusika na uponyaji, waliohusika na kuitengeza mimba ya Mariamu pasipo mwanamume kwa uwezo wa roho ndio hao hao pia wana uwezo wa kuondoa ugonjwa pasipo daktari lakini wanafanya kazi na mtu anayeliaimi neno hili “kwa kupigwa kwake sisi tumepona”.

Kwahiyo hizo ndizo silaha zetu sisi katika ulimwengu wa Roho, kulishika NENO la Mungu pamoja Na kuwa na IMANI katika Neno lake.

Na ndio maana Mtume Paulo alisema katika..

Waefeso 4: 11 “Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.

12 Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.

13 Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.

14 Basi simameni, hali mmejifunga KWELI VIUNONI, na kuvaa dirii ya haki kifuani,

15 na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;

16 zaidi ya yote mkiitwaa NGAO YA IMANI, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.

17 Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni NENO LA MUNGU;”

Unaona hapo? Ukilijua Neno la Mungu kwa undani,wewe tayari ni Mtu wa rohoni, ambaye unashindana vita visivyoonekana kwa macho na unashinda, hauna haja ya kuona mapepo, hauna haja ya kuona wachawi, hauna haja ya kuona majini, vibwengo, hauna haja ya kumwona hata shetani mwenyewe,..na zaidi ya yote hauna haja ya kuwaona hata malaika..Wao wanafanya kazi zao katika ulimwengu wa roho ambao wewe ndio unaoupalilia kwa kulishika na kuliamini Neno la Mungu..

Sasa mafundisho ya mashetani leo ni yapi?

Mafundisho ya mashetani ni yale yanayokufundisha kwamba unaweza ukaingia katika ulimwengu wa roho na wewe ukashindana na mapepo kama wanavyofanya malaika…Ndio hapo shetani anatumia nguvu kubwa kuwavuta watu wasilijue Neno la Mungu, na kuwafanya wakeshe kutafuta kujua elimu za mapepo, utakuta anawafundisha watu aina za mepepo na majini, na utendaji wao kazi. Wengine wanawafundisha watu wasile vyakula Fulani au wasipande miti Fulani majumbani mwao, kwasababu vina uhusiano wa moja kwa moja na mapepo n.k.

Wengine wanafundisha watu kwamba usiende kuogelewa baharini au mtoni saa 7 au kabla ya kuogelea baharini, kemea kwanza pepo la maji, kwamba kabla ya kupita karibu na makaburi kemea kwanza pepo la mauti lisije likakuingia, unapokaribishwa kwa mtu usiyemjua usile kwanza chakula Fulani, kwamba ukiona mtu kakuamkia na kukuonyesha ishara Fulani, kemea hilo ni pepo la mauti, unapougua kichomi basi umetumiwa jini Fulani n.k..

Unapofika mahali Fulani usipende kutenda wema, nyota yako itachukuliwa n.k nataka nikwambie ndugu hizo zote ni ELIMU ZA MASHETANI.!!

Sisi tuliompa Bwana Yesu Kristo maisha yetu tunafahamu Neno moja tu!! Nalo ni hili “Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo, Wala hapana uganga juu ya Israeli. Hesabu 23:23”. Hiyo ndio silaha tuliyo nayo sisi..Ni namna gani inatenda kazi?? Hatujui Malaika ndio wanaojua…wao ndio wanaojua kuna aina ngapi za vibwengo, na wachawi, na mapepo na namna ya kuwashughulikia sisi sio kazi yetu kujua aina za mapepo na utandaji kazi wao…

Tunapotenda wema na kuambiwa nyota zetu zitachukuliwa…hilo hatulijui sisi tunachojua ni kwamba.. “hakuna hata unywele mmoja wa vichwa vyetu utakaopotea, na nywele zetu zote zimehesabiwa Luka 21:18” Ni kwa namna gani hilo linatenda kazi? Hiyo sio kazi yetu kujua, Malaika watakatifu ndio waliobobea katika mambo ya rohoni hao ndio wanazo hizo teknolojia ya kuzihifadhi nyota zetu kama zipo, sisi hatuna huo uwezo. Sisi kazi zetu ni kulishika Neno lake tu!

Biblia inatuonya hizi elimu/mafundisho siku za mwisho yatakuwa mengi, yakiwatoa watu katika Imani lengo ni kuwafanya watu wajitenge na Imani, . Na badala ya kumfungua mtu, utakuta ndio zinamfunga na kumfanya awe mwoga wa wokovu wake, Hata siku moja Mungu hamletei mtu hofu, bali ujasiri, utakuta watu wamehama nyumba zao kwa kuogopa zimezindikwa na wanahubiriwa hivyo na wanaojiiita watumishi. Wengine kila kukicha ni kufundishwa utendaji kazi wa mapepo tu!! Kila kitu kitakachokuja mbele yako ni kukemea, ukiingia hospitali kemea, kabla ya kulala mwaga damu ya Yesu chooni, mapepo yasikuvae, saa kumi jioni majini aina Fulani yanafunguliwa hivyo usipende kula kitu Fulani huo wakati. Na mambo mengine mengi yanayofanana na hayo, kila kitu ni mapepo mapepo tu!!

Dada/Kaka unayesoma haya, tafuta kulijua Neno la Mungu na kuliamini, hayo mengine sio kazi yetu kujua, Mtafute Bwana alisema katika Neno lake Maneno yake ndiyo Roho na Uzima(Yohana 6:64)…na maneno yake sio mengine zaidi ya Biblia takatifu, kwahiyo kwa lugha nyingine unaweza kusema biblia takatifu ndio Roho na uzima..Hivyo kuwa mtu wa rohoni ni kuyaishi na kuyaamini maneno ya Yesu Kristo 100% na si kingine.

Kama unataka leo hii uwe mtu wa rohoni, mtii leo maneno yake anayokuambia, kwa kukusudia kutubu dhambi zako kabisa kwa kumaanisha kuacha uasherati wako, kwa kukusudia kuacha pombe zako, uvaaji wako mbaya {vimini, surali,wigi,wanja,lipstick, herein n.k}, kwa kumaanisha kuacha wizi wako, utukanaji wake, rushwa zako, usengenyaji wako n.k Ili uwe na uhakika wa kuurithi ufalme wa mbinguni na kuruhusu Malaika wa Bwana watembee na wewe siku zote za maisha yako, na kuepukana na mafundisho ya mashetani

Mungu akubariki

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Kama umempa Bwana maisha yako, tafadhali tangaza habari zake kwa kadri uwezavyo kwa watu wengine wasiomjua yeye.


Mada zinazoendana


SHETANI NI NANI?

 DHAMBI ILIYOMKOSESHA SHETANI NI IPI?

HUDUMA KUMI (10) ZA SHETANI DUNIANI NI ZIPI?


Rudi Nyumbani

Print this post

JE! UMEFUNDISHWA?

Wafilipi 4.10 “Nalifurahi sana katika Bwana, kwa kuwa sasa mwisho mmehuisha tena fikira zenu kwa ajili yangu, kama vile mlivyokuwa mkinifikiri hali yangu lakini hamkupata nafasi.

11 Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina mahitaji; maana nimejifunza kuwa radhi na hali yo yote niliyo nayo.

12 Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, NIMEFUNDISHWA kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa.

13 Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu”.

Katika maandiko haya Mtume Paulo, anasema AMEFUNDISHWA kushiba na kuona njaa…Hebu litafakari hilo neno kwa undani “NIMEFUNDISHWA”. Kufundishwa maana yake ni kupewa maarifa ambayo ulikuwa huyajui, hivyo ni wazi kuwa Mtume Paulo kuna wakati alikuwa hajafundishwa baadhi ya mambo mpaka ulipofika wakati Fulani wa kupokea mafundisho za dizaini hiyo..

Na moja ya mambo hapa ambayo Mtume Paulo anasema amefundishwa ni hili la “KUSHIBA NA KUONA NJAA”. Ikiwa na maana kuwa kuna wakati Mungu alimpitisha katika kipindi cha uhitaji mkubwa (kipindi kikali cha kuona njaa) ili amfundishe huko.. Na kuna wakati pia Mungu alimpitisha katika kipindi cha kushiba ili pia ajifunze.

Kwahiyo tunaona kuwa mojawapo ya tabia ya Mungu ni kumpitisha Mtu katika VIPINDI VIWILI, vya KUSHIBA na KUONA njaa. Vipindi vya KUPUNGUKIWA na KUWA NA VINGI, Vipindi vya kupandishwa juu na vipindi vya kushushwa.(Mhubiri 3). NIA NA MADHUMUNI YA MUNGU..NI ILI TUFIKIE MAHALI TUWE RADHI NA VITU TULIVYONAVYO. Tufikie mahali tusipepesuka na hali yoyote tutakayokutana nayo katika siku za usoni.

Unajua kuna tabia moja Fulani ambayo baadhi ya majeshi mengi duniani wanayo,  pindi wanapomsajili mwanachama mpya katika jeshi huwa wanamchukua Yule mtu kwasababu ndio kajiunga kwa mara ya kwanza,hajui kanuni cha jeshi, wanamchukua na kuanza kumwonea au kumfanyia mambo ya kumuudhi…utaona kafika tu kesho yake, anaanza kupigwapigwa pasipo sababu, pengine ametulia tu hajafanya kosa lolote anajikuta  mtu anatokea na kuanza kumtukana pasipo sababu na kumshurutisha kufanya jambo Fulani, utakuta kalala na mtu anakuja kumwamsha na kumpiga bila sababu, na mambo mengi mabaya ya kuudhi hapo hakuna wa kumsaidia. Sasa huo ndio umekuwa utaratifu wa majeshi mengi duniani kufanya hivyo, nia na makusudi yao sio kumtesa Yule mgeni, au kumwonea hapana bali kumtolea ndani yake “ile hasira ya asili (kupanic) ambayo kila mtu anakuwa amezaliwa nayo ” Ili kumpa uwezo wa kustahimili mambo magumu atayoweza kukutana nayo katika vita.

Kwahiyo utaona mara za kwanza anapigwa, na kuanza kunung’unika saa hiyo hiyo, na wakati mwingine kurudisha mapigo au matusi au kununa kwa muda mrefu, na kutengeneza kinyongo lakini siku zinavyozidi kwenda anakuwa anazoea zile hali hivyo hata akifanyiwa hayo mambo mara nyingi vipi  anajikuta  hapaniki tena kama zamani, anakuwa kawaida, haumii moyo tena kama alivyokuwa anaumia..Hiyo inamsaidia Yule mwanajeshi akiwa vitani atumie AKILI ZAIDI KULIKO HISIA. Kwahiyo hayo ni moja ya mafundisho tu ya majeshi ya watu wa Ulimwengu huu. Hicho ndicho kinachomtofautisha mwanajeshi na raia wa kawaida. Utashangaa ni kwanini anaweza akaona ndugu yake  mpendwa vitani labda kaka yake kapigwa risasi na kuuliwa, badala ya kuvunjika moyo na kulia pale, yeye ndio atambeba na kumuhifadhi kisha kuendelea na vita kana kwamba hajafiwa..Lakini ukirudi kwa watu wa kawaida mfano msiba umetokea kidogo tu utaona watu wanaanza kupiga mayowe  na wengine hata kukufuru..Ni kwasababu gani? Ni kwasababu hawajafundishwa. Hilo tu.

Lakini Kristo naye ana mafunzo yake, kabla ya kumpeleka mtu, katika vita vya kiroho..Na mojawapo ya mafundisho ndio hayo “KUFUNDISHWA KUONA NJAA na KUSHIBA”.

Wana wa Israeli kabla ya kufika nchi ya Ahadi, Bwana aliwapitisha jangwani na wakati mwingine alikuwa anawaacha waone njaa na kiu kwa muda mrefu ili awafundishe. Ili Watakapoingia nchi ya Kaanani wasilalamike watakapopitia mitikisiko kidogo tu. Walikuwa wanatembe jangwa masiku hawaoni maji.

Kumbukumbu 8: 1 “Amri hii ninayokuamuru leo mtaishika kuitenda, mpate kuishi na kuongezeka, na kuingia katika nchi ile ambayo Bwana aliwaapia baba zenu; nanyi mtaimiliki.

2 Nawe utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu wako ALIYOKUONGOZA MIAKA HII AROBAINI KATIKA JANGWA, ili akutweze, kukujaribu kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake, au sivyo.

3 Akakutweza, AKAKUACHA UONE NJAA, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa MWANADAMU HAISHI KWA MKATE TU, BALI HUISHI KWA KILA LITOKALO KATIKA KINYWA CHA BWANA”.

Unaona! Wana wa Israeli kuna kipindi Mungu aliwaacha makusudi waone njaa lakini walikuwa hawafi wala hawaumwi, Ili wajue tu kuwa Mtu anaweza kuishi bila kula vyakula vya kimwilini na asife bali akaishi kwa Neno la Mungu tu.

Na ndio maana Bwana Yesu naye vivyo hivyo alipokwenda mlimani alifunga siku 40 usiku na mchana bila kula, na mwovu alipomjia na kumjaribu ageuze  jiwe kuwa mkate..alimpa jibu lile lile kuwa “MTU HATAISHI KWA MKATE TU BALI KWA KILA NENO LINALOTOKA KATIKA KINYWA CHA BWANA”..Kwasababu gani alimjibu vile ni kwasababu “HUKO NYUMA ALISHAFUNDISHWA KUSHIBA NA KUONA NJAA” kwahiyo kwake yeye AWE NACHO au ASIWE nacho vyote ni sawasawa. Awe na chakula asiwe na chakula kwake yeye ni sawa sawa..Anayaweza mambo yote kwa yeye AMTIAYE Nguvu. Anachojua ni kwamba Mungu hatamtupa kabisa.

Na ndio Mtume Paulo naye, hakuwahi kutamani fungu kutoka kwenye makanisa aliyoyazaa yeye kiroho, ingawa angestahili kupata fungu kutoka huko, lakini badala yake ndio anawaambia watu wa kanisa la Filipi ambalo walitamani sana kumuhudumia kwa mali zao..

Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina mahitaji; MAANA NIMEJIFUNZA KUWA RADHI NA HALI YO YOTE NILIYO NAYO. 

12 Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, NIMEFUNDISHWA kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa.

13 Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu”.

Hiyo ina maana kuwa HAHUBIRI INJILI YA KRISTO kwasababu anataka FEDHA, au kwasababu ANA FEDHA, hapana Bali anahubiri injili ya Kristo kwasababu ana NIA YA KRISTO NDANI YAKE, AWAVUTE WENGI KWAKE…AWE NACHO ASIWE NACHO KWAKE YEYE NI SAWASAWA Injili ya KRISTO ataendele kuihubiri.

Na sisi je! Tumefundishwa KUWA RADHI NA VITU TULIVYO NAVYO? Kwamba ifikie mahali hatumfuati Bwana Yesu kwasababu tunatafuta utajiri, au mali kutoka kwake, au hatumfuati kwasababu Tuna mali., Yaani ifikie hatua tunasema TUMEFUNDISHWA KUWA RADHI NA VITU TULIVYO NAVYO. Tumefundishwa kuridhika na vitu tulivyo navyo..viwe vingi au vichache tutamtumikia Bwana, tuwe tuna  Elimu tusiwe na Elimu kwetu iwe ni mamoja, tuwe matajiri tuwe maskini Thamani ya Kristo Kwangu ni ile ile. Niwe na chochote nisiwe na chochote tutaihubiri injili ya Kristo.

Kama hatujafunzwa hivyo Basi tumwombe Bwana atufundishe masomo hayo ili tuweze kutembea naye pasipo manung’uniko wala malalamiko Kama alivyotembea na Mtume Paulo..Hiyo itatusaidia sisi tunapopitia vipindi vya kupungukiwa tusijione wanyonge, na kuanza kutanga huku na huko, bali tujue ni vya muda tu, sisi tusonge mbele na Imani mpaka kuja kwake YESU KRISTO ambapo yeye mwenyewe atatufariji kwa taabu zetu hapa duniani.

Tafadhali wahubirie wengine habari njema ya Msalaba kwa kadri uwezavyo.

Ubarikiwe.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

KARAMA ILIYO KUU NI IPI?

MOYO ULIOELEKEA KWA MUNGU.

ROHO MBAYA KUTOKA KWA BWANA.

NI KWASABABU YA YESU KRISTO.

JE! SISI KAMA WAKRISTO NI DHAMBI KUSHEHEREKEA KRISMASI?


Rudi Nyumbani

Print this post

UPEPO WA ROHO.

YOHANA 3:3 “Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.

4 Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa?

5 Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu.

6 Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.

7 Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili.

8 Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho.”

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo lisifiwe daima, Ni siku nyingine tena Bwana aliyotupa kwa neema zake na leo tutaangalia vifungu hivyo ni kwanini Yesu aliifananisha hali ya mtu aliyezaliwa kwa Roho na kama UPEPO UVUMAO.

Yapo mambo matatu hapo Bwana aliyoyasema  kuhusu Upepo,

1)   La kwanza ni Upepo Huvuma upendako

2)   La pili ni: Sauti yake waisikia (lakini hauuoni)

3)   Na la tatu ni Hujui utokako wala unakokwenda.

Na mwisho akamalizia kusema “NDIVYO ILIVYO HALI YAKE MTU ALIYEZALIWA NA ROHO”. Hii ina maana gani? Ni wazi kuwa inamaanisha  pale Roho wa Mungu anapoingia ndani ya mtu kwa mara ya kwanza basi hali yake inabadilika na kufanana na tabia inayoweza kulinganishwa na tabia ya upepo.

Tabia hizi ni mara tu baada ya mtu kuzaliwa kwa Roho, kwahiyo tunaweza kusema Upepo huo ni Roho mtakatifu ndani ya mtu. Kwasababu ndiye aliyemfanya kuwa hivyo. Kama tunavyofahamu tabia ya upepo, kwanza ni kitu kisichoweza kuonekana  kwa macho lakini utaisikia sauti yake pale unapovuma, au utauhisi katika mwili wako pale unapopita karibu na wewe, lakini usijue chanzo  chake ni wapi na hatma ya safari yake itaishia wapi!!.

Kadhalika  Roho Mtakatifu anapoingia ndani ya mwamini tabia hizi za upepo wa Roho huingia ndani yake. Pale mtu alipoamua na kudhamiria kweli kumpa Kristo maisha yake. Basi kuanzia huo wakati na kuendelea ndani yake kunakuwa na nguvu isiyojulikana chanzo chake ni nini kwa nje! Watu wa nje wanaweza kushangaa mbona huyu mtu tabia yake imebadilika kwa ghafla hivi,wasijue ni nani aliyembadilisha, wakijaribu kachunguza labda ni dini hawaoni, labda ni dhehebu hawaoni, labda ni mwanadamu hawaoni, na ndio hapo utaona maisha ya yule mtu yanabadilika, pengine mambo aliyokuwa anapenda kuyafanya hapo mwanzo yanageuzwa ghafla, maisha aliyokuwa anaishi nyuma yanageuka ghafla, mara nyingine atajikuta anachukia hata kufanya baadhi ya vitu alivyokuwa anavifanya nyuma, anajikuta kiini cha maisha yake ni kumwangalia Bwana YESU tu mahali popote alipo…Baadhi ya mambo yasiyokuwa na maana yataanza kumkera, anaanza kutokujiona kuwa huru akiwa katika vikao vya usengenyaji, tofauti na alivyokuwa hapo mwanzo..

Hii yote inatokea ni kwasababu yule Roho aliye ndani yake humsukuma kufanya vitu ambavyo hata pengine yeye mwenyewe hajui ni kwanini anavifanya, saa nyingine anaweza akadhani ni kwa akili zake anafanya hivyo.Au ni kwasababu ametokea tu kupenda mwenyewe Lakini ukweli ni kwamba sio yeye anafanya hivyo bali ni Roho wa Mungu ndani yake atembeaye kama upepo usioonekana anamwelekeza asikojua yeye.

Atajikuta anaanza kuchukia kupenda pombe, ambapo hapo mwanzo alikuwa anazitamani, anajikuta kuvaa vimini na suruali anajiona kama yupo uchi au anajiaibisha mbele za watu hivyo anajikuta anaanza kupenda kuvaa sketi ndefu ambazo hapo mwanzo alikuwa akivaa anajiona kama mshamba. Anajikuta anatamani kusoma biblia, au kusikiliza Neno la Mungu sana, ambapo hapo kwanza alikuwa hana mpango navyo. Anajikuta kampani za marafiki wa kidunia ni mzigo mkubwa kwake tofauti na jinsi alivyokuwa nyuma. Anajikuta hata akipitia dhiki kubwa kiasi gani kwa ajili ya imani hapepesuki mpaka watu wa nje! Wanashangaa huyu mtu ni wa dizaini gani. N.k.

Na hata baada ya muda mrefu kupita ukimuuliza ilikuwaje kuwaje ukaweza kuacha dhambi na mambo ya kidunia pamoja na majaribu mazito kiasi kile atakwambia kwa kweli sifahamu nguvu hiyo ilitoka wapi,nilijikuta tu ninamsimamo na maamuzi yangu..nilijikuta tu kuna nguvu fulani ndani yangu ikinisukuma kunipeleka sehemu Fulani,sasa huo ulikuwa ni ule upepo wa Roho ambao ulikuwa unampeleka asikotazamia yeye kwenda,.ataishia kukwambia ni neema za Mungu tu.

Na ndio maana katika siku ile ya Pentekoste Roho aliposhuka kwa watu kwa mara ya kwanza Ishara ya kwanza aliyoshuka nayo ni ishara ya  UVUMI WA UPEPO uendao kwa kasi, sio kwasababu  Mungu alikuwa anataka kuwaonyesha watu uweza wake wa kuamuru tufani, hapana, bali Upepo ule ulifunua jambo kubwa sana katika roho  kwa waumini wa kweli waliokuwa Yerusalemu..na ndio maana ukichunguza kwa makini baada ya pale maisha na mienendo ya mitume ilibadilika  ghafla tangu ule wakati, walipokea ujasiri usio wa kawaida kuhubiri injili, walijawa na Imani kwa Mungu, hawakuwaogopa maadui zao tena, na kwenda kujificha kama ilivyokuwa pale mwanzo.. Mara nyingi roho alikuwa akiwatwaa na kuwapeleka wasikojua, na huko wanapofika wanalihubiri Neno la Mungu kwa ushujaa mwingi..Tunamwona mtu kama Filipo alitwaliwa na Roho na kupelekwa kule Roho alipopenda kumpeleka.

Matendo 2:1 “Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja.

2 KUKAJA GHAFULA TOKA MBINGUNI UVUMI KAMA UVUMI WA UPEPO WA NGUVU UKIENDA KASI, UKAIJAZA NYUMBA YOTE WALIYOKUWA WAMEKETI.

3 Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.

4 Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka”.

Unaona kulikuwa na Upepo wasiojua ulipotoka ,Ule ulifunua UPEPO WA ROHO, ambao ndio ulioathiri maisha yao kuanzia ule wakati na kuendelea.

Unaona umuhimu kwa kuzaliwa kwa Roho? Leo hii ni kwasababu gani huwezi kushinda tamaa, na dhambi, ni kwasababu moja tu, nayo ni hii HAUJAZALIWA MARA YA PILI hivyo ule upepo wa Roho hauwezi ukawa na nguvu juu ya maisha yako. Haujamkaribisha Roho ndani ya maisha yako. Kama ungekuwa umezaliwa kwa Roho ile nguvu ingekusukuma mahali usipojua kama vile UPEPO uvumapo na usingeona kuwa dhambi ni jambo gumu kuliacha kwasababu ni Roho mwenyewe angekuwa anatenda kazi ndani yako.. Nguvu ile Ingekusukuma kule usikoweza kufika, ingekusukuma kutenda mapenzi ya Mungu na kumtazama Kristo kila wakati.

Kumbuka Nikodemo  alikuwa ni Farisayo wa mtu dini sana, anayejua maandiko sana lakini hakuwa amezaliwa mara ya pili, unaona? kumbe unaweza ukawa wa kidini na usiwe na Roho Mtakatifu ndani yako. Ndugu Usiridhike na dhehebu lako, au kanisa lako ukajiona kuwa tayari umekamilika na huku unaona kabisa maisha yako ya kikristo yanadorora siku baada ya siku..Na ndio maana maandiko yanasema, MTU ASIPOZALIWA KWA MAJI NA KWA ROHO HAWEZI KUUINGIA UFALME WA MBINGUNI hapo hata kama uwe unayafahamu maandiko kiasi gani, huwezi kuuingia ufalme wa mbinguni, Bwana Yesu anasema hivyo.

Lakini Mtu anazaliwaje kwa Roho na kwa Maji?

Ni kwa kukudhamiria kabisa kutubu na kuacha dhambi na maisha ya kale.Wengi hawafanyi hivyo, toba haitoki moyoni bali midomoni na ndio maana inakuwa ngumu Roho wa Mungu kukaa ndani yao. Na maana ya toba sio kuomba msamaha tu, bali ni KUGEUKA AU KUACHA. Hivyo unapogeuka na kukusudia kuacha dhambi hata usiposema kwa mdomo hiyo tayari ni TOBA, Hivyo ukizingatia hayo na Mungu akishaona nia yako yeye mwenyewe atakuosha “roho yako”,  kwa maji (ambayo ni DAMU yake na Neno lake) na kukugawia Roho wake ndani yako atakayekuweza kukusaidia kuishinda dhambi siku zote za maisha uliyopo hapa duniani..

Kama maandiko yanavyosema:

 Ezekieli 36: 24 “Maana nitawatwaa kati ya mataifa, nami nitawakusanya na kuwatoa katika nchi zote, na kuwarudisha katika nchi yenu wenyewe.

25 Nami NITAWANYUNYIZIA MAJI SAFI, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote.

26 Nami nitawapa ninyi moyo mpya, NAMI NITATIA ROHO MPYA NDANI YENU, NAMI NITATOA MOYO WA JIWE ULIOMO NDANI YA MWILI WENU, NAMI NITAWAPA MOYO WA NYAMA.

27 NAMI NITATIA ROHO YANGU NDANI YENU, NA KUWAENDESHA KATIKA SHERIA ZANGU, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda.

28 Nanyi mtakaa katika nchi ile niliyowapa baba zenu, nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.”

Hivyo mambo hayo hayatimiliki pasipo kuambatana na ishara ya wazi ya nje kuonyesha kuwa hicho kilichotendeka nje ndicho kilichofanyika rohoni mwako. Kwahiyo ni lazima mtu akazamishwe kwenye MAJI mengi akabatizwe kwa maji tele,kama Bwana alivyoagiza na ni katika JINA LA YESU, kuonyesha kuwa ameoshwa dhambi zake kwa maji ya Roho, kisha ndipo awe na uhakika kuwa amepokea ubatizo wa Roho Mtakatifu ndani yako.

Hivyo ikiwa haujachukua uamuzi huo fanya hivyo haraka, ili neema hii ipate kuwa juu yako. Na ule UPEPO wa ROHO MTAKATIFU utakuvumisha na kukupeleka usikojua wewe, Na mwisho wake utashangaa umetulia mahali Mungu ambapo alikusudia..na utakuwa na uhakika siku ile kunyakuliwa juu kwenda mbinguni kumlaki Bwana, katika upepo huo wa kisulisuli kama Nabii Eliya.

Chukua muda wako kuwahubiria habari njema za wokovu, ndugu zako, marafiki zako na jamaa zako popote pale ulipo, ili na wao wapone, shetani asipate mazao.

Mungu akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

IMANI YENYE MATENDO;

MWAMBA WETU.

JIFANYIE RAFIKI KWA MALI YA UDHALIMU.

HISIA YA MUNGU ILIYO MBAYA KULIKO ZOTE


Rudi Nyumbani

Print this post

NUHU WA SASA.

Mwanzo baada ya Adama na Hawa kuasi, Bwana aliwafukuza kutoka uweponi mwake, ndani ya ile bustani ya Mungu (Edeni)..Lakini tunaona baada tu ya kufukuzwa haikuishia hapo, bali tunaona pia ARDHI ililalaaniwa kwa ajili yao. Ikiwa na maana kuwa kila kinachopatikana kutoka ardhini, kitapatikana kwa tabu kuanzia huo wakati na kuendelea..Ilikuwa ni pigo kubwa kwasababu karibia kila kitu kinatoka ardhini, kwasababu hata mwanadamu mwenyewe anatoka ardhini, na ndio maana hata yeye anapatikana kwa uchungu, na kwasababu hiyo Bwana Mungu alimwambia mwanamke atazaa kwa uchungu..Na sio mwanadamu tu, bali hata wanyama na viumbe vyote hiyo laana iliwapata kwasababu nao pia wanatoka ardhini…Hivyo ile laana ya ardhi kulaaniwa NI PANA KIDOGO zaidi ya tunavyoielewa.

Lakini kama tukijifunza kitabu cha Mwanzo kwa undani zaidi, tutazidi kuona kuwa hiyo laana ya ardhi kulaaniwa haikuishia tu pale Adamu aliasi, bali utaona kuwa kwa jinsi muda ulivyokuwa unaenda na maasi yalivyokuwa yanazidi kuongezeka ile laana nayo ilikuwa inajiongeza.. Ndio maana utaona Kaini baada ya kumwua ndugu yake Habili, ile laana ya ardhi kulaaniwa iliongezwa kwake…

Mwanzo 4: 9 “Bwana akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?

10 Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako INANILILIA KUTOKA KATIKA ARDHI. 11 Basi sasa, UMELAANIWA WEWE KATIKA ARDHI, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako;

12 UTAKAPOILIMA ARDHI haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani.

13 Kaini akamwambia Bwana, Adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki.

14 Tazama, UMENIFUKUZA LEO KATIKA USO WA ARDHI, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua.”

Unaona hapo? Baada ya laana ya kwanza Bwana Mungu aliyomlaani Adamu na uzao wake juu ya ardhi, tunaona Kaini anazidishiwa tena mara mbili baada ya kumwua ndugu yake..hivyo ni laana juu ya laana..

Kwahiyo hali hiyo ya laana kujiongeza juu ya laana iliendelea kwa miaka na miaka kutokana na maasi ya wanadamu…Mpaka ilipofika wakati karibia na gharika Bwana alipomchagua mtu ambaye kwa kupitia yeye ataisimamisha ile laana ya ARDHI KULAANIWA kila kukicha..Na ndio tunasoma Bwana alimnyanyua Nuhu kwa kizazi chake, Mtu mkamilifu na wa Haki, ambaye alipata sana Neema mbele ya Macho ya Mungu..kama tunavyosoma mtoto huyo alipozaliwa tu Baba yake kwa Imani akatoa unabii juu yake na kusema…

Mwanzo 5: 28 “Lameki akaishi miaka mia na themanini na miwili, akazaa mwana.

29 Akamwita jina lake Nuhu, akinena, HUYU NDIYE ATAKAYETUFARIJI KWA KAZI YETU NA KWA TAABU YA MIKONO YETU KATIKA NCHI ALIYOILAANI BWANA.

30 Lameki akaishi baada ya kumzaa Nuhu miaka mia na tisini na mitano, akazaa wana, waume na wake”.

Unaona, tangu Adamu mpaka Kuzaliwa kwa Nuhu, ni takribani zaidi ya miaka 1500 ilipita..kwahiyo kwa kipindi chote hicho matatizo yalikuwa makubwa sana duniani kwasababu ya Ardhi iliyolaaniwa na inayoendelea kulaaniwa kutokana na dhambi zilivyokuwa zinazidi kuongezeka..Kwahiyo Baba yake Nuhu, kabla hajafa alijua atazaliwa mwana ambaye kwa kupitia yeye hiyo laana itasimama na itakuwa faraja kwa vizazi vijavyo..

Na Nuhu alipokuwa mtu mzima, baada ya Baba yake kufa alianza kumtafuta Mungu na kwenda katika njia zake, na kutojichangamana na maasi ya ulimwengu..Na hivyo Bwana akapendezwa naye kuliko watu wote waliokuwa wanaishi duniani kwa wakati huo, kumbuka dunia ya wakati ule ilikuwa na watu wengi kama dunia ya sasa, lakini yeye akakubalika sana machoni pa Bwana.

SASA NI WAKATI GANI? NUHU ALIPOISIMAMISHA HIYO LAANA?.

Kwasababu tunaona Baba yake alishatabiri kuwa yeye ndiye atakayefariji uzao wao katika nchi aliyoilaani Bwana, hivyo ni lazima uje wakati ambapo Bwana ataisimamisha hiyo laana kupitia Nuhu. Na wakati huo sio mwingine zaidi ya WAKATI BAADA YA GHARIKA KUPITA..pale ambapo Nuhu alimtolea Bwana sadaka nzuri iliyompendeza na Bwana akaridhika na sadaka ile na KUAPA KUTOILAANI TENA NCHI kwa namna yoyote ile..Tunasoma hayo katika..

Mwanzo 8: 18 “Basi Nuhu akatoka, yeye, na wanawe, na mkewe, na wake za wanawe pamoja naye;

19 kila mnyama, na kila kitambaacho, na kila ndege, kila kinachokwenda juu ya nchi kwa kabila zao, wakatoka katika safina.

20 Nuhu akamjengea Bwana madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu.

21 Bwana akasikia harufu ya kumridhisha; Bwana akasema moyoni, SITAILAANI NCHI TENA BAADA YA HAYO KWA SABABU YA WANADAMU, MAANA MAWAZO YA MOYO WA MWANADAMU NI MABAYA TANGU UJANA WAKE; wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya. 22 Muda nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma”.

Unaona hapo? Bwana anasema “sitailaani tena nchi” na sio “sitamlaani tena mwanadamu” nchi na ardhi ni kitu kimoja. Kwahiyo baada ya Nuhu kumtolea Bwana sadaka iliyokubalika mbele zake, Bwana akaisimamisha na ile laana iliyokuwa inaendelea kujiongeza siku baada ya siku.

Mwanzo 9: 8 “Mungu akamwambia Nuhu, na wanawe pamoja naye, akisema, 9 Mimi, tazama, nalithibitisha agano langu nanyi; tena na uzao wenu baada yenu;

10 tena na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi, ndege, na mnyama wa kufugwa, na kila mnyama wa mwitu katika nchi pamoja nanyi; wote wanaotoka katika safina, hata kila kilicho hai katika nchi.

11 Na agano langu nitalithibitisha nanyi; WALA KILA CHENYE MWILI HAKITAFUTWA TENA KWA MAJI YA GHARIKA; WALA HAKUTAKUWA TENA GHARIKA, BAADA YA HAYO, KUIHARIBU NCHI.

12 Mungu akasema, Hii ndiyo ishara ya agano nifanyalo kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi, kwa vizazi vyote hata milele;

13 Mimi nauweka upinde wangu winguni, nao utakuwa ni ishara ya agano kati yangu na nchi.

14 Hata itakuwa nikitanda mawingu juu ya nchi, upinde utaonekana winguni,

15 nami nitalikumbuka agano langu, lililoko kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili, wala maji hayatakuwa gharika tena kuwaharibu wote wenye mwili.

16 Basi huo upinde utakuwa winguni; nami nitauangalia nipate kulikumbuka agano la milele lililoko kati ya Mungu na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili kilichoko katika nchi.

17 Mungu akamwambia Nuhu, Hii ndiyo ishara ya agano nililoliweka kati yangu na wote wenye mwili walioko katika nchi.”

Lakini tunaona kuwa japokuwa Bwana aliisimamisha ile laana bado kulikuwa na matatizo madogo madogo yaliyoendelea kutokea.. kulikuwepo bado na vipindi vya njaa duniani ingawa mvua badao zilikuwa zinanyesha kwa misimu, bado vilikuwepo, vipindi vya matetemeko, vipindi vya taabu, nyakati za kula kwa jasho n.k Hivyo kwa lugha nyingine ni kwamba Nuhu alisimamisha laana isiendelee lakini hakuiondoa laana kabisa.

Agano Mungu aliloingia na Nuhu, halikutosha kuondoa LAANA YOTE MUNGU aliyoilaani ARDHI, lilikuwa ni agano la kuleta UNAFUU tu wa maisha juu ya wanadamu.

Hivyo ni lazima aje mwingine mfano wa Nuhu ambaye sio tu kuisimamisha laana bali KUIONDOA KABISA LAANA ISIWEPO, dunia irudi katika hali yake ya kwanza, kusiwepo na tabu tena, kusiwepo na kula kwa jasho tena, zisiwepo shida tena n.k Na huyu si mwingine zaidi ya YESU KRISTO.

Na kama tunavyoona ili kwamba Bwana aibariki tena ardhi kama alivyofanya kwa Nuhu, ni lazima gharika ipite Kwanza kuiharibu dunia yote, kisha ndio ije ile baraka na kabla hajaiharibu dunia kwa gharika, alimuhifadhi kwanza Nuhu na wanawe ndani ya safina.

Vivyo hivyo katika siku hizi za mwisho wakati BWANA MUNGU anataka kwenda kuifuta kabisa laana ya DUNIA, ARDHI ILIYOLAANIWA. Bwana Mungu alimnyanyua YESU KRISTO kwa mfano wa Nuhu, ili kwa kupitia yeye Bwana ayarejeshe mambo yote yaliyoharibika, arejeshe dunia iwe kama Edeni, aiondoe laana yote ambayo haikumalizika kuondolewa na Nuhu.

Na ni lazima gharika kwanza ije ili kuondoa waovu wote, ulimwenguni ndipo mambo yote yafanywe kuwa mapya..Hivyo kabla ya Yesu Kristo kuja duniani kurejesha mambo yote, siku zake zitafananishwa kama siku za Nuhu, ataijenga safina ambayo ni NENO LAKE, na kuwaingiza watu wake humo, na kisha kuihukumu dunia kwa moto kama Nuhu alivyoihukumu kwa gharika.

Waebrania 11: 7 “Kwa imani Nuhu akiisha kuonywa na Mungu katika habari za mambo yasiyoonekana bado, kwa jinsi alivyomcha Mungu, aliunda safina, apate kuokoa nyumba yake. Na hivyo AKAUHUKUMU MAKOSA ULIMWENGU, akawa mrithi wa haki ipatikanayo kwa imani.”

Kwahiyo Yesu Kristo ndiye mhukumu wa ulimwengu na mrithi, ATAKAYETUFARIJI SISI KATIKA ARDHI HII ILIYOLAANIWA NA BWANA, na faraja hiyo haitakuja sasa, bali baada ya ulimwengu huu kuteketezwa, ndipo hapo dunia itarejeshwa na kuwa kama paradiso ya kwanza. Katika utawala wa miaka 1000 na katika umilele.

Ndugu yangu unayesoma haya. Hii dunia haiwezi kufanywa upya kabla maangamizi hayajaja, hii dunia haina muda mrefu kama wengi wanavyodhani, Kristo mfano wa Nuhu anawaingiza wanawe sasa kwenye safina yake aliyoitengeneza yeye mwenyewe (NENO LAKE) na akisha maliza kuwaingiza wote mlango wa neema unafungwa, na kisha ghadhabu ya Mungu kumwagwa ulimwenguni kote. Na anasema kama ilivyokuwa katika siku za Nuhu ndivyo itakavyokuwa katika siku za kuja kwake mwana wa Adamu, siku za Nuhu watu walikuwa wanakula na kunywa,(anasa), walikuwa wanaoa na kuoana (ndoa za jinsia moja),walikuwa waasherati kama leo, wanaojipenda wenyewe, watu wa fashion, wanawake na wanaume wasiovaa mavazi ya kujisitiri, walikuwepo watu wa dhihaka, wauaji, wasengenyaji, wasiosamehe, wala rushwa, wacheza dansi n.k Ndio hao hao wapo sasa..Tusiangukie katika hilo kundi ndugu yangu. Bwana alimfunulia Mtume Petro mambo hayo yatakayotokea siku hizi za mwisho na kusema..

2 Petro 3: 2-12

“1 Wapenzi, waraka huu ndio wa pili niwaandikiao ninyi; katika zote mbili naziamsha nia zenu safi kwa kuwakumbusha,

2 mpate kuyakumbuka yale maneno yaliyonenwa zamani na manabii watakatifu, na ile amri ya Bwana na Mwokozi iliyoletwa na mitume wenu.

3 Mkijua kwanza neno hili ya kwamba katika siku za mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki, wafuatao tamaa zao wenyewe,

4 NA KUSEMA, IKO WAPI AHADI ILE YA KUJA KWAKE? KWA MAANA, TANGU HAPO BABU ZETU WALIPOLALA, VITU VYOTE VINAKAA HALI IYO HIYO, TANGU MWANZO WA KUUMBWA.

5 Maana hufumba macho yao wasione neno hili ya kuwa zilikuwako mbingu tangu zamani, na nchi pia, imefanyizwa kutoka katika maji, na ndani ya maji, kwa neno la Mungu;

6 kwa hayo dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia.

7 Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu.

8 Lakini, wapenzi, msilisahau neno hili, kwamba KWA BWANA SIKU MOJA NI KAMA MIAKA ELFU, NA MIAKA ELFU NI KAMA SIKU MOJA.

9 BWANA HAKAWII KUITIMIZA AHADI YAKE, KAMA WENGINE WANAVYOKUDHANI KUKAWIA, BALI HUVUMILIA KWENU, MAANA HAPENDI MTU YE YOTE APOTEE, BALI WOTE WAFIKILIE TOBA.

10 Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea.

11 Basi, kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa,

12 mkitazamia hata ije siku ile ya Mungu, na kuihimiza; ambayo katika hiyo mbingu zitafumuliwa zikiungua, na viumbe vya asili vitateketea na kuyeyuka? “

Unaona hapo juu anavyosema? “BWANA HAKAWII KUITIMIZA AHADI YAKE, KAMA WENGINE WANAVYOKUDHANI KUKAWIA, BALI HUVUMILIA KWENU, MAANA HAPENDI MTU YE YOTE APOTEE, BALI WOTE WAFIKILIE TOBA.”

Anakuvumilia leo ili utubu, ili utubie uasherati wako, ili utubie usengenyaji wako, ili utubie uvaaji wako mbaya, ili utubie dansi zako unazoenda kucheza kila siku, ili utubie kutokusamehe kwako, ili utubie kula kwako rushwa, ili utubie hasira zako zinazowaka pasipo sababu, anataka kukuingiza kwenye safina yake katika dakika hizi za mwisho za majeruhi. Na kutubu sio tu kuomba msamaha, hapana bali maana yake ni KUGEUKA NA KUACHA UNAYOYAFANYA. Na baada tu ya kuamua kwa dhati kugeuka, hatua inayofuata ni ubatizo wa maji mengi, na kwa jina lake YESU (Matendo 2:38).

Hivyo Mgeukie leo YESU. Kwasababu yeye ndiye Mungu aliyemchagua na kumtia mafuta kwa UKOMBOZI, hakuna mwingine zaidi yake, kila kitu kimewekwa chini yake, na yeye ndiye atakayeihukumu hii dunia mfano wa Huhu. Ili ayafanye mambo yote kuwa mapya baada yake, ili siku ile ATUFARIJI tukafurahi naye katika mbingu mpya na chini mpya ambayo itashuka hapa duniani, mahali ambapo tutakuwa na raha milele, mahali ambapo kutakuwa hakuna magonjwa wala njaa, wala shida, wala mauti,wala dhiki, wala maadui..Mahali ambapo tutafutwa machozi yetu na tutakula mema yote ya nchi Bwana aliyotuandalia zaidi hata ya ilivyokuwa pale Edeni.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine mambo haya, na Bwana atakubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

MAMBO (2) YATAKAYOKUTENGA NA IMANI SIKU HIZI ZA MWISHO.

SWALI LA KUJIULIZA!

CHAKULA CHA ROHONI.

TABIA ZA ROHONI.

UBATILI


Rudi Nyumbani

Print this post

FAHAMU KINACHOMGHARIMU MUNGU, KUTOA URITHI WAKE.

Kamusi inatoa tafsiri ya neno “KURITHI” kwamba ni kitendo cha kupokea mali baada ya kifo cha mmiliki wa mali hiyo. Hii ikiwa na maana kuwa mali inapopaswa kurithishwa haiwezi kutoka mikononi mwa mrithishaji mpaka siku atakapokufa mwenyewe. Hivyo yule atakayerithishwa siku zote hapaswi kujimilikisha mali zile hata kama atakuwa anazihudimia kwa kiasi gani, mpaka siku atakapokufa mmiliki mwenyewe ndipo ziwe zake moja kwa moja kihalali.

Na ni lazima pia mrithishaji na mrithishwaji wawe na mahusiano ya kibinafsi na ya kipekee na kama hiyo haitoshi, ni lazima pia waingie katika makubaliano ya kimaagano au ya ki-waraka ili kutambulisha kuwa walidhiana katika mapatano hayo. Haiwezekani mtu kutokea siku ya kifo na kudai urithi kama mmojawapo wa warithishwaji angali hakuwa na mahusiano yoyote na mwenye mali au makubaliano.

Biblia nayo inakubaliana na tafsiri hiyo,Tukisoma:

Waebrania 9:16 “Maana agano la urithi lilipo, lazima IWEPO MAUTI YAKE ALIYELIFANYA.

17 Kwa maana agano la urithi lina nguvu palipotukia kufa kwa mtu; kwa kuwa halina nguvu kabisa, akiwa yu hai yeye aliyelifanya”.

Unaona hapo?. Ni kwanini KIFO kitokee? Ni kwasababu moja tu ili kwamba ile mali iwe ni milki halali ya yule mrithishwaji MILELE. Kwasababu kifo kisipokuwepo inaweza kutokea siku moja pengine yule aliye hai akadai tena mali zake, na kugeuka kuwa sio urithi tena..

Kwasababu sheria moja ya urithi ni lazima uwe ni wa milele.. Na kifo tu pekee ndio kinaweza kuleta hilo jambo. Hivyo tunaweza kusema nguvu ya urithi ni KIFO.

Hayo mambo yanafunua nini rohoni? Kumbuka Mungu alitoa ahadi kuu za urithi kwa watoto wake juu ya nchi aliyowaandalia itakayokuja huko mbeleni. Na tunafahamu kuwa mbingu hizi na dunia hii ni mali ya Mungu sasa?, milima, sayari, nyota, mito , habari mabara n.k vyote hivi ni mali yake.

(Kutoka 19:5).Na mwanadamu aliwekwa ndani yake pale Edeni lakini kwa kutokutii kwake akamruhusu shetani ainyakue mikononi kwake, mpaka kupelekea kuingia katika matatizo tuliyonayo sasa hivyo ikamgharimu Mungu amtume mwanawe mpendwa Yesu Kristo ili aje kuukomboa tena ulimwengu uliokuwa umepotea. Na tunafahamu kuwa ushindi huo ulipatikana pale Kalvari miaka 2000 iliyopita hapo ndipo umiliki wa mbingu hizi na nchi hizi ziliporudi tena kwa Mungu baba kwa kupitia YESU mwokozi wetu.

Hivyo, vitu vyote vilivyopo ulimwenguni sasa vinamilikiwa na YESU KRISTO mwenyewe, isipokuwa huu mfumo wa utawala mbovu wa shetani unaoiharibu dunia sasa kwa kitambo ndio upo mikononi mwa shetani. Lakini kwa kuwa YESU ni mshindi alishapanga siku ya maangamizi ya vitu vyote ili kuitengeneza upya dunia na kuifanya kuwa bustani ya Mungu yenye makao mazuri yasiyoneneka. Matengenezo hayo yataanza katika ule utawala wa miaka 1000, ambapo kila kitu kiovu kitasafishwa na YESU KRISTO atakapokuja kutawala na watakatifu wake hapa duniani.

Sasa hapo ndipo Mungu atakapoutoa ule urithi alioutunza kwa ajili ya watoto wake ambao tangu zamani aliundaa kwa ajili yao, urithi ambao Ibrahimu aliuona tokea mbali ukamfanya mpaka aishi kama mpitaji hapa duniani.

Waebrania 11:8 “Kwa imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa urithi; akatoka asijue aendako.

9 Kwa imani alikaa ugenini katika ile nchi ya ahadi, kama katika nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile.

10 MAANA ALIKUWA AKIUTAZAMIA MJI WENYE MISINGI, AMBAO MWENYE KUUBUNI NA KUUJENGA NI MUNGU.”

Unaona hapo Yatafakari maneno hayo vizuri “10 MAANA ALIKUWA AKIUTAZAMIA MJI WENYE MISINGI, AMBAO MWENYE KUUBUNI NA KUUJENGA NI MUNGU.

kama biblia inavyosema katika Mathayo 5: 5 “Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi”.

Ndugu Ipo nchi tutakayokuja kuirithi sisi watoto wa Mungu baada ya utawala huu mbovu wa shetani kuharibiwa kabisa hapo dunia itakapofanywa kuwa upya tena wakati huo ndipo urithi wetu utaachiliwa. Hapo ndio kila mtoto wa Mungu ambaye alijiona kuwa yeye si kitu alipokuwa duniani, aliyejinyima nafsi yake na mambo ya ulimwengu mpaka kuonekana kama ni takataka ya dunia sasa kwa mambo ambayo atakutana nayo huko katika siku hizo, hata kumbuka tena taabu yake aliyoipitia, biblia inasema kama vile mwanamke aliyetoka kujifungua anavyosahau uchungu aliopitia baada ya kuona kiumbe kipya kuja duniani.Ndivyo itakavyokuwa kwa watoto wa Mungu siku ile.

1Petro 1:3 “Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu;

4 TUPATE NA URITHI USIOHARIBIKA, USIO NA UCHAFU, USIONYAUKA, ULIOTUNZWA MBINGUNI KWA AJILI YENU.”

Sasa swali linakuja je! ili Mungu atupe huo urithi wa mbingu mpya na nchi mpya, ambao ametuahidia inampasa na yeye afe ili tuwe na umiliki halali wa urithi huo milele?

Jibu ni hapana, kama tunavyojua kuwa Mungu anaishi milele, hafi, sasa kitakachofanyika ni kuwa MUNGU ATAKUFA KWA HABARI YA UMILIKI WA NCHI HIYO INAYOKUJA, ikiwa na maana kuwa dunia ijayo itakuwa ni MILKI HALILI YA MWANADAMU MILELE.. Yaani mwanadamu atakuwa na maamuzi ya kufanya jambo lolote katika nchi hiyo aliyoandaliwa na Mungu.. Unajua kwasasa huwezi kufanya lolote kwasababu dunia hii ni mali ya Mungu, embu jaribu kufikiria mfano ingekuwa ni mali yako, ungeamua kufanya nini?. Unaona ni kama jambo ambalo haliwezekani lakini itakuwa hivyo.

Mungu wakaandalia watakatifu wake urithi wa milele, siku hiyo Mungu hatawauliza chochote juu ya urithi huo, kana kwamba sio yeye aliyeiumba dunia bali wao..

Jambo pekee litakalofanyika ni kwamba tutamjua yeye katika viwango vingine, Tutamwabudu Mungu katika viwango vingine , mbali ni hivi tunavyovijua mbali na masuala ya mbingu na nchi, mambo ambayo kwasasa hatuwezi kuyastahimili mpaka tutakapofika kule kwanza…siku hizo hatutamwabudu yeye kama tunavyomwabudu sasa, Huko tutakapomjua Mungu kwa mapana na marefu, huko ndiko tutakapomjua Mungu kuwa ni zaidi ya mbingu na nchi, na vitu tunavyoviona Haleluya!.

Ni vizuri tukiyafahamu hayo, ili kusudi kwamba mambo ya ulimwengu huu mabovu ya kitambo tuyaonapo tuone kuwa ni takataka tukifananisha na urithi usioharibika Mungu aliotuandalia huko mbeleni na ndio maana biblia ilikazia sana kusema maneno haya:

Waefeso 1.18 “macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; NA UTAJIRI WA UTUKUFU WA URITHI WAKE KATIKA WATAKATIFU JINSI ULIVYO”

Pia Kumbuka biblia inaposema mbingu mpya na nchi mpya, inamaanisha jambo zaidi ya hii sayari yetu inayojulikana kama dunia..Inamaanisha kuwa ni pamoja na sayari zote, na nyota zote na magimba yote yaliyopo angani. Yote yatakuwa ni makao na urithi Mungu aliwaandalia wanadamu watakatifu.

Sayari hii yetu ni kama makao makuu tu, wanasayansi wanafanya utafiti wa kupata uwezekano wa makazi mapya ya wanadamu katika sayari nyingine, na kweli wameziona lakini hawawezi kuzifikia, kwasababu ni mbali na upeo wa kibinadamu kufika huko. Wanachunguza chunguza uwezekano wa kuishi katika sayari zilizo kando kando ya dunia lakini bado hawataweza kwasababu huo sio urithi wao. Huo ni urithi wa wana wa Mungu Bwana aliowaandalia wale wazishikao amri zake.

Ayubu 9: 7 “Aliamuruye jua, nalo halichomozi; Nazo nyota huzipiga muhuri”.Na pia inasema..

Zaburi 147: 4 “Huihesabu idadi ya nyota, Huzipa zote majina”.

Kitu kikishapewa jina na Mungu mwenyewe inamaanisha kuwa kitu hichi kina uhai, na pia kinakaliwa. Sasa kama nyota zote kazipa majina na kazipiga muhuri itafika wakati kama ilivyokuwa pale mwanzo Nchi ilikuwa ukiwa lakini Roho wa Mungu alipotujua juu ya dunia hii , pakawa mahali pa kukaliwa na watu. Ndivyo itakavyokuwa kwa sayari nyingine na magimba mengine yaliyopo angani.

Ili kusudi kwamba Mungu awe wa milele na asiyeisha, ni lazima awe na urithi ambao kuisha kwake unahitaji umilele. dunia pekee hii haitaweza kustahimili umilele, kwani kuna wakati itafika tutajua kila kitu kilichopo duniani.

Na ndio maana pale anasema macho ya mioyo yetu yatiwe nuru ili tujue utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo;…Zingatia hilo neno UTAJIRI WA UTUKUFU WA URITHI WAKE.. yaani utukufu wa urithi wake una TAJIRI usiopunguka..

Hayo ni machache tu yapo mambo mengi yahusuyo urithi Mungu aliowaandalia watoto wake. Leo hii watu wanajiona kuwa hii dunia ni ya kwao japo si ya kwao, wanajiona kuwa wanaweza kufanya kila kitu, wanajiona kuwa wapo huru kana kwamba hakuna anayewamiliki.. Sasa kama wao kwasasa wanajiona hivyo na hawajijui kuwa wanamilikiwa pasipo wao kujijua kwasababu hii nchi hawajarithishwa wao. Itakuwaje siku hiyo pale Mungu atakapomaliza kuitengeneza upya hii dunia na kuwapa watoto wake..

WATAKUWA HURU KIASI GANI?..NI ZAIDI YA UHURU unaweza kuudhani. Kwa Mungu hakuna utumwa.

Lakini leo hii tusipoyaona hayo na kuupenda huu ulimwengu uliojaa utumwa wa kila namna, ulimwengu wa kitambo, ambao mwisho wake upo karibu, hatutaki kutazama mambo ya milele yanayodumu, tunapuuzia wokovu, tunadhani kuwa Mungu ni mtu wa kando wa sisi kujiamulia mambo tu, kana kwamba tusipompokea yeye kuna kitu anapungukiwa…Hapana ndugu siku ile tutajuta pale tutakapoona tumekosa urithi huo ulio bora, na wenzetu wanaingia katika raha ya milele na sisi tunaenda katika ziwa la moto.

Siku ile ya hukumu Bwana atakapotenga mbuzi na kondoo, kondoo wake wakiwa upande wake wa kiume na mbuzi (waovu) wakiwa upande wa kushoto atawaambia maneno haya:

Mathayo 25:34 “Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, URITHINI UFALME MLIOWEKEWA TAYARI TANGU KUUMBWA ULIMWENGU;”

Unaona? Wataurithi ufalme Mungu aliwaandalia tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu.Lakini waliosalia wote sehemu yao itakuwa katika lile ziwa la moto. Kama biblia inavyoeleza katika..

1Wakorintho 6:9 “Au hamjui ya kuwa wadhalimu HAWATAURITHI UFALME WA MUNGU? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti,

10 wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang’anyi.”

Hivyo tuyachunguze maisha yetu leo kama je! kweli tunastahili kupewa urithi huo? Je! tumeshaingia katika agano hilo la kufanyika kuwa warithi wa Baba yetu wa mbinguni?. Kumbuka Agano hilo halifanyiki nje ya Damu ya YESU Kristo. Ikiwa bado haujaokolewa fanya hivyo sasa maadamu neema ipo, uoshwe dhambi zako kwa kutubu na kubatizwa katika ubatizo uliosahihi wa maji mengi katika jina la YESU ili upate ondoleo la dhambi zako. Na ikiwa bado unasua sua njia panda upo vuguvugu ni wakati sasa wa kufanya imara wito wako na uteule wako. Ili urithi huo usikupite.

Bwana akubariki.

Tafadhali Washirikishe wengine habari njema za Yesu Kristo, popote pale ulipo.


Mada Nyinginezo:

NGUVU YA HEKIMA NA AKILI

MADHARA YA KUTAFUTA ISHARA.

TULICHUNGUZE UMBO LA YESU NA MWENENDO WAKE.

NOTI YA UFALME WA MBINGUNI


Rudi Nyumbani

Print this post

UTIMILIFU WA TORATI.

Tukisoma Agano la Kale, biblia inaelezea maisha ya watumishi wake, jinsi walivyokuwa na jinsi walivyoishi. Tunajua kabisa wengi maisha yao hayakukamilika, kwasababu torati waliyopewa isingeweza kuwakamilisha na kuwa wakamilifu, Kwasababu torati yenyewe haikutimilika..

Ndio maana utamwona Mtu kama Daudi aliyependwa sana na Mungu, alioa wake wengi, na mwanawe Sulemani alikuwa na wake wengi vile vile. Utamwona Daudi mtu aliyeupendeza Moyo wa Mungu alikuwa anaua, na aliua watu wengi na bado BWANA hakumuhesabia makosa.

Utamwona Daudi hakubatizwa lakini bado alikuwa ni mtu anayeupendeza moyo wa Mungu. Alikuwa anashindana na kuwatakia shari maadui zake, na kuwachukia lakini bado alikuwa ni mteule wa Bwana.

Sasa kwa jicho la haraka haraka unaweza ukasema, kama Daudi alikuwa ana wake wengi, alikuwa anawashambulia na kushindana na maadui zake, alikuwa anaua na bado ni mtumishi wa Mungu, na mimi sio vibaya nikifanya hayo hayo na bado kwani Mungu atakuwa na mimi. Ni rahisi kusema hivyo.

Lakini ningependa ufahamu kitu kimoja, agano la kale(au agano la kwanza) lilikuwa sio utimilifu wa mambo yote…lilikuwa ni muhtasari tu wa Agano halisi la Mungu. Na ndio maana Bwana Yesu alisema katika..

Mathayo 5:17 “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza.”

Unaona hapo? Bwana alikuja KUITIMILIZA, yaani kuifanya ieleweke vizuri…yaani ikiwa na maana kuwa, Torati iliposema USIUE, Haikumaanisha tu kumkamata mtu na kuutoa uhai wake bali iliimanisha kwanza USIMCHUKIE KABISA NDUGU YAKO, Vivyo hivyo Torati iliposema USIZINI, Haikumaanisha tu kwenda kufanya zinaa ya nje, hapana bali ilimaanisha pia MTU HATAKIWI KUTAMANI KABISA NDANI YA MOYO WAKO. Kwahiyo unaweza ukaona hapo kutoka “kuzini” mpaka “kutokutamani” huko ni kukitimiliza kile kipengele kilichosalia..kwasababu Torati asili yake ni Rohoni.

Hivyo Daudi na watakatifu wa agano la kale walipokuwa wanaua hawakuwa wanafanya jambo lililosahihi, ingawa kwa wakati ule Bwana aliruhusu wafanye vile kwasababu wakati wa Utimilifu wa Torati, ulikuwa bado haujafika.

Kadhalika Daudi, na Sulemani mwanae, na watakatifu wote wa Agano la kale walipooa wake wengi, walikuwa hawafanyi jambo lililo sahihi machoni pa Bwana, ilikuwa sio mpango kamili wa Mungu wawe na wake na wengi, Lakini Bwana aliliruhusu waendelee kuoa wake wengi na kutoa talaka,hivyo hivyo mpaka UTIMILIFU utakapofika.

Watakatifu wa agano la kale, walikuwa wanaapa, lakini hayakuwa ni mapenzi ya Mungu mwanadamu yeyote aape, lakini Bwana aliwaruhusu waendelee kufanya hivyo mpaka wakati wa Utimilifu utakapofika. Na mara nyingine aliruhusu ifanyike hivyo kwasababu tu ya ugumu wa mioyo yao.

Ndipo wakati wa UTIMILIFU ulipofika, Mungu alimtuma mwanawe mpendwa Yesu Kristo ili kuhubiri UTIMILIFU wote WA TORATI.

Na ndio hapo Bwana Yesu alisema..

Mathayo 5:21 “Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue, na mtu akiua, itampasa hukumu.

22 Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto”.

Mathayo 5:27“Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini; 28 lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake”.

Mathayo 5.33 “Tena mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiape uongo, ila mtimizie Bwana nyapo zako;

34 lakini mimi nawaambia, Usiape kabisa; hata kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu;

35 wala kwa nchi, kwa maana ndiyo pa kuwekea miguu yake; wala kwa Yerusalemu, kwa maana ndio mji wa Mfalme mkuu.

36 Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi.

37 Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu”

Mathayo 5:38“Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho, na jino kwa jino;

39 Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili.”

Kaka/dada unayesoma haya, UMESIKIA kwamba imenenwa unaweza ukaokolewa tu, maadamu unatenda mema, na kuzishika amri 10 za Mungu, lakini Kristo anasema.. Mtu hawezi kuuona ufalme wa mbingu, asipozaliwa mara ya pili.

Na tena umesikia mahali wanasema ubatizo sio wa lazima, mbona hata Daudi hakubatizwa lakini Mungu alimkubali, Ndugu usiamini huo uongo leo KRISTO ANAKUAMBIA… “AAMINIYE NA KUBATIZWA ATAOKOKA ASIYEAMINI ATAHUKUMIWA” (Marko 16:15-16).

Umeona hapo? Anasema asiyeamini atahukumiwa, Ndugu yangu usipoamini na kubatizwa utahukumiwa, hayo ni maneno ya Mkuu wa Uzima mwenyewe YESU KRISTO, Na yeye hawezi kusema uongo.

Inawezekana mahali Fulani umesikia mtu Fulani akikuambia kwamba unatakiwa umfuate Yesu tu, kwa wepesi usijiweke rehani saana..Lakini yeye anakwambia leo

Luka 9:23-25 “..Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha. Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe?.”

tena umesikia mahali pengine wakisema kuwa ni ruksa kuwa na wake wengi au waume wengi..lakini kristo mtimilifu wa torati anakuagiza leo maneno haya

Luka 19: 9 “nami nawaambia ninyi, kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini…..

7 wakamwambia, jinsi gani basi musa aliamuru kumpa hati ya talaka, na kumwacha?

8 akawaambia, musa, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu, aliwapa ruhusa kuwaacha wake zenu; lakini tangu mwanzo haikuwa hivi”.

Tena umesikia dhehebu Fulani likisema, mtu akifa leo hupitia kwanza TOHARANI kutakaswa dhambi zake kisha atakwenda mbinguni, na wengine wanasema mtu akifa amekufa wala hakuna kiyama ya wafu. Lakini Bwana Yesu anasema “27 Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu;(Waebrania 9:27)”. Unaona? Usidanganyike ndugu kufanya ibada za wafu, au kuwaombea wafu, wala usidanganyike kuwa ukifa leo ni unapotea tu kama wale masadukayo walivyokuwa wanaamini. Fahamu kuwa ukishakufa wewe utakuwa ni wakusubiria hukumu aidha peponi au jehanum, Hivyo usikubali kusikiliza hadithi za kutungwa, zitakazokufanya ustarehe katika dhambi zako ukidhani kuwa kuna nafasi ya pili uko uendako, au kuna kupotea tu hakuna hukumu.

Ndugu, mtii YESU KRISTO leo, usiseme kwasababu Daudi alikuwa na wake wengi, basi na wewe ndio uwe na wake wengi, usiseme kwasababu Daudi hakubatizwa na wewe usiutafute ubatizo leo, usiseme kwasababu Daudi alikuwa anashindana na maadui zake na kuwaua na wewe leo ukatafute kuwaangamiza wale wanaokuchukia.. usifanye hivyo mtimilifu wetu yesu kristo ndiye anayetuagiza tusifanye hivyo. tusishindane na watu waovu, wala tusijilipize kisasi. sio kila njia ya watakatifu wa agano la kale ilikuwa ni kamilifu, mtazame YESU Kristo yeye ndiye njia na kweli na uzima. na ndiye aliyepakwa mafuta kutufundisha maneno ya uzima. huyu yesu kristo ndiye aliyefanyika bora kuliko wanadamu wote na malaika wote..na ndio maana ile sauti ilitoka mbinguni na kusema… “huyu ndiye mwanangu mpendwa wangu msikieni yeye”.

Waebrania 2: 1 “Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi,

2 mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika mwana [yesu kristo], aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu.

3 yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa ukuu huko juu;

4 amefanyika bora kupita malaika, kwa kadiri jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao.”

Mwamini YESU uokolewe hizi ni saa za majeruhi.

ubarikiwe

tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine na mungu atakubariki.


Mada Nyinginezo:

UBATIZO SAHIHI

MVUTO WA TATU!

ROHO YA MPINGA KRISTO IKITENDA KAZI SIKU HIZI ZA MWISHO

NYAKATI SABA ZA KANISA NA WAJUMBE WAKE.


Rudi Nyumbani

Print this post