Category Archive Wazazi na Watoto

Je! Siku ya unyakuo watoto wachanga watanyakuliwa?

SWALI: Je! Siku ya unyakuo watoto wachanga watanyakuliwa? Na vipi kuhusu walio bado tumboni, na wenyewe watanyakuliwa au wataachwa?


JIBU: Hili ni moja ya swali gumu  kwasababu biblia haijaeleza moja kwa moja ni nini kitawatokea watoto siku ile ya Unyakuo, Hivyo tutajaribu kueleza kwa kadiri ya tunavyoona katika baadhi ya vifungu kwenye maandiko.

Ukitazama katika biblia, utaona, wapo watoto walipata neema kutokana na haki za wazazi wao, mfano wa hawa ni watoto wa Nuhu, na Lutu,  vilevile wapo watoto walioadhibiwa kutokana na makosa ya wazazi wao. Utaliona hilo pia katika vile vizazi vyote vya Sodoma na Gomora, pamoja na gharika  vyote viliteketezwa, hadi watoto walipata adhabu kwa dhambi za wengine. Lakini hiyo haimaanishi kuwa wataadhibiwa tena baada ya kifo.

Pia tukumbuke kuwa hata katikati ya kipindi cha dhiki kuu, bado watu wataendelea kutungishwa mimba na kuzaliwa, hivyo litakuwepo kundi la vichanga ambavyo vitazaliwa katikati ya dhiki kuu na vitakufa katika maangamizi yao..Hilo tunalithibitisha katika andiko hili;

Mathayo 24:19 “Ole wao wenye mimba na wanyonyeshao siku hizo!

20 Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato.

21 Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe.

22 Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo”.

Unaona? Kwahiyo siku ile ikifika, kuna uwezekano wa watoto wengine kunyakuliwa (hata wale walio tumboni), na vilevile wengine kubaki, japo hatuwezi kusema hivyo ndivyo ilivyo, Yote tunamwachia Mungu. Ikiwa ni wote watanyakuliwa, au ni baadhi, Tunachopaswa kufahamu ni kuwa Mungu ni wa haki, atayaleta yote katika mizani, na yote yatakuwa sawa tu mwisho wa siku, na tutaona kabisa hukumu zake ni za haki. Kama vile Malaika mbinguni wanavyokiri hivyo..

Ufunuo 16:7 “Nikaisikia hiyo madhabahu ikisema, Naam, Bwana Mungu Mwenyezi, ni za kweli, na za haki, hukumu zako”.

Cha muhimu tunachopaswa kujua ni kuwa sisi ambao tayari tumeshafikia kimo cha kuyajua mema na mabaya, Kama hatutayatengeneza mambo yetu sasa, kwa kumpokea Bwana Yesu Kristo kwa kumaanisha kabisa, na kujitwika misalaba yetu na kumfuata, tujue kuwa unyakuo ukipita tutaachwa. Na matokeo yake, yatakuwa ni kuingia katika mateso makali ya dhiki kuu pamoja na Jehanamu ya moto.

Je! Umeokoka? Je! Umebatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako? Kumbuka Unyakuo ni wakati wowote, tubu umruidie muumba wako. Parapanda ni siku yoyote inalia, hakuna dalili iliyosalia..

Bwana Yesu akubariki.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

Print this post

MZAZI, JALI MAISHA YA KIROHO YA MTOTO WAKO.

Kuna pepo moja lililowasumbua sana mitume wa Yesu, hilo halikuwa sawa na pepo mengine waliyokutana nayo, walihangaika nalo mchana kutwa lakini hawakufua dafu mpaka alipokuja Bwana Yesu mwenyewe kulikemea na kulitoa.

Lakini leo hatutazungumzia juu ya pepo hilo kwasababu habari yenyewe tunaijua, ila katika habari hiyo lipo jambo ambalo ni vizuri sisi tukajifunza, husasani kwa wazazi au walezi, wanaoishi na watoto wadogo. embu tusome tena alichokifanya Yesu kisha, tuende kwenye ujumbe wenyewe..

Marko 9:20 “Wakamleta kwake; hata alipomwona, mara yule pepo alimtia kifafa; naye akaanguka chini, akagaa-gaa, akitokwa na povu.

21 Akamwuliza babaye, AMEPATWA NA HAYA TANGU LINI? Akasema, TANGU UTOTO.

22 Na mara nyingi amemtupa katika moto, na katika maji, amwangamize; lakini ukiweza neno lo lote, utuhurumie, na kutusaidia”.

Sasa katika habari hiyo, usidhani Yesu alikuwa hajui matatizo ya huyo mtoto ndio maana akamwuliza vile, Kumbuka Yesu alikuwa anajua kila kitu wala alikuwa hana haja ya mtu kumuadhithia chochote, biblia inatuambia hivyo katika  Yohana 16:30, Lakini  aliuliza vile kwa lengo la kutaka watu wote wajue matatizo ya Yule mtoto yalianzia wapi, na ndio maana akamuuliza vile yule mzazi “Amepatwa na haya tangu lini?”.

Ndipo yule mzee akamjibu na kusema,  “amepatwa na haya tangu utotoni”. Ulishawahi  kuutafakari vizuri huu mstari, tangu utotoni? ..Hiyo ni kutuonyesha kuwa kuna mapepo ambayo, agenda yao kuu, ni watoto. Kwasababu yanajua yakianzia katika msingi, baadaye yatakuwa ni magumu kutoka.

Inashangaza leo hii kuona wazazi hawajali maisha ya kiroho ya watoto wao, wanaona kama wao ni watoto tu, shetani hawezi kuwashambulia, hawajui kuwa wanapaswa kulindwa kwasababu shetani huwa hatambui cha mtoto au cha mzee, lengo lake ni kuharibu. Kama alimuingia Nyoka ambaye ni mnyama tu, ataachaje kumwingine mtoto ambaye ni mwanadamu? ndio target yake kubwa?

Mzazi, anamruhusu mtoto wako mdogo atezame tv masaa 24 wakati wote hata zile programu ambazo haziendani na umri wake anamwacha azitazame, anamwacha asikilize miziki ya kidunia, tena Zaidi ya yote unafurahi anapocheza,  lakini nyimbo za tenzi hata moja haujui, Mzazi mwingine hata hampeleki mtoto wake Sunday school ili afundishwe njia ya kikristo angali akiwa mdogo, yeye anachojua ni kumnunulia mtoto wake nguo nzuri tu, kumtafutia nursery nzuri ya kusoma, anajali vya mwilini vya mwanawe anapuuzia na vile vya rohoni. Hata kumwombea mtoto wake anashindwa.

Nachotaka nikuambie ni kuwa tusipowawekea msingi mzuri watoto wetu, shetani atatusaidia kuwawekea wake, kama alivyofanya kwa mtoto wa huyu mzee tunayesoma habari zake.  Lile pepo lina haki ya kuwa gumu kutoka kwasababu tayari lilikuwa na msingi tangu utotoni. Na ukiangalia lengo la hilo pepo si lingine zaidi ya kumwangamiza tu, mara litake kumtupa kwenye maji, kwa bahati nzuri pengine watu wanamuona wanamuokoa, mara litake kumtupa kwenye moto, lakini Mungu anafungua rehema zake anaepukika.

Leo hii utaona kumenyanyuka kundi kubwa la watoto ambao wanaonyesha tabia ambazo hazieleweki chanzo chake ni nini, na wewe unaweza ukadhani ni yeye anafanya kumbe ni pepo ambalo tayari lilishamvaa tangu utotoni ndio linaonyesha tabia hizo ndani yake.

Wazazi ndio wanapaswa waanze kubadilika, ndio watoto wabadilike.  Wewe kama mzazi, kama hutaonyesha kujali maisha ya kiroho ya mtoto wako, usidhani mtoto atabadilika mwenyewe au atakuwa na tabia njema huko mbeleni.

Mithali 22:6 “Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee”

SASA UTAYAZUIAJE MAPEPO YA UHARIBIFU KAMA HAYO YASIMWINGIE MWANAO?

Kwanza ni kwa kutumia kiboko: Biblia inasema hivyo, …Pale unapoona kuna tabia Fulani ambayo sio nzuri, mfano kiburi, anatukana, hana nidhamu, hapo hapo hupaswi kuiacha hiyo tabia imee, mpaka hilo pepo liumbike ndani yake.. Utalitoa hilo kwa kiboko.

Mithali 23:13 “Usimnyime mtoto wako mapigo; Maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa.

14 Utampiga kwa fimbo, Na kumwokoa nafsi yake na Kuzimu”.

Pili Ni  kwa kumfundisha kanuni za imani: Unamfundisha biblia, unamfundisha nyimbo za kikristo, unamfundisha kusali, unamfundisha hata kukariri  vifungu vya biblia, hata kama hataelewa sasahivi lakini vitabaki moyoni mwake kama hazina itakayokuja kumsaidia baadaye. Na  hakikisha pia unampelekea kwenye mafundisho ya watoto kanisani.

Tatu  Unamwombea; Mara kwa mara unahakikisha unamfunika mwanao, kwa damu ya Yesu Kristo, unatenga muda mrefu wa kumuombea.

Na Nne unamzuia kufanya/kutazama mambo ambayo hayapasi: Si lazima kila unachokitazama wewe, mtoto naye akitazame, magemu anayoyacheza mtoto si yote yanamaudhui mazuri, vilevile nguo unazomvisha mtoto si zote ni njema. Hivyo jifunze kumchagulia mtoto vinavyomfaa.

Ukizingatia hayo, basi mapepo kama hayo ambayo ni hatari na sugu, hayatamkuta mwanao. Kumbuka biblia inasema shetani ni kama simba angurumaye, akitafuta mtu ammeze, hivyo usipuuzie haya maagizo, mjenge mwanao, mjenge mdogo wako, mjenge mtoto yoyote auishiye naye.

Na Bwana atakubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

AGENDA KUBWA YA SHETANI KWA KANISA HILI LA LAODIKIA.

KILEMBA CHA NEEMA, JE! UMEMVIKA MWANAO?

RUDI KUMPA MUNGU UTUKUFU.

Rudi Nyumbani:

Print this post

MALEZI YA MTOTO MCHANGA.

Yafahamu malezi ya mtoto mchanga kibiblia.


Ukitaka mtoto wako mchanga awe na afya na ukuaji bora, na baadaye aishi Maisha aliyokusudiwa na Mungu ya mafanikio rohoni..Basi ni vema ukatafuta ushauri wa kiblia, ili ujue ni jinsi gani unapaswa umlee mwanao tangu akiwa katika hatua za awali za uchanga wake.

TUKIANZANA NA MALEZI  YA KIMWILI:

Embu tukiangazie kisa kimoja katika biblia, naomba usome chote, na mwisho wa Habari hiyo utajifunza jambo kubwa sana ambalo pengine hata hukuwahi kulitafakari hapo kabla..Ni tukio linalomuhusu Sulemani na wanawake wale wawili makahaba.

Tusome..

1Wafalme 3:16 Ndipo wanawake wawili, makahaba, walimwendea mfalme, wakasimama mbele yake.  17 Na mwanamke mmoja akasema, Ee bwana wangu, mimi na mwanamke huyu tunakaa katika nyumba moja; nami nalizaa nilipokuwa pamoja naye nyumbani.  18 Kisha, siku ya tatu baada ya kuzaa kwangu, ikawa mwanamke huyu naye akazaa; na sisi tulikuwa pamoja; hapakuwa na mtu mwingine pamoja nasi nyumbani, isipokuwa sisi wawili tu.  19 Na mtoto wa mwanamke huyu akafa usiku, maana alimlalia. 20 Akaondoka kati ya usiku, akamwondoa mtoto wangu ubavuni pangu, mimi mjakazi wako nilipokuwa usingizini, akamweka kifuani pake, na mtoto wake mwenyewe, aliyekuwa amekufa, akamweka kifuani pangu.  21 Nilipoondoka asubuhi nimnyonyeshe mtoto wangu, kumbe? Amekufa. Hata asubuhi nilipomtazama sana, kumbe! Siye mtoto wangu niliyemzaa.  22 Ndipo yule mwanamke wa pili akasema, Sivyo hivyo; bali mtoto wangu ndiye aliye hai, na mtoto wako ndiye aliyekufa. Na mwenzake akasema, Sivyo hivyo; bali mtoto wako ndiye aliyekufa, na mtoto wangu ndiye aliye hai. Ndivyo walivyosema mbele ya mfalme.  23 Ndipo mfalme akasema, Huyu anasema, Mtoto wangu yu hai, na mtoto wako amekufa. Na huyu anasema, Sivyo hivyo; bali mtoto aliyekufa ni wako, na mtoto aliye hai ni wangu.  24 Mfalme akasema, Nileteeni upanga. Wakaleta upanga mbele ya mfalme.  25 Mfalme akasema, Mkate mtoto aliye hai vipande viwili, kampe huyu nusu, na huyu nusu.  26 Ndipo mwanamke yule, ambaye mtoto aliye hai ni wake, akamwambia mfalme kwa maana moyoni mwake alimwonea mtoto wake huruma, akasema, Ee bwana wangu, mpe huyu mtoto aliye hai, wala usimwue kamwe. Lakini yule mwingine akasema, Asiwe wangu wala wako; na akatwe.  27 Ndipo mfalme akajibu, akasema, Mpe huyu wa kwanza mtoto aliye hai, maana yeye ndiye mama yake.  28 Na Israeli wote wakapata habari za hukumu ile aliyoihukumu mfalme wakamwogopa mfalme; maana waliona ya kuwa hekima ya Mungu ilikuwa ndani yake, ili afanye hukumu.

Katika Habari hiyo nataka utazame  mambo makuu matatu..

  1. Jambo la kwanza: Jinsi ya uwekaji mtoto.
  2. Jambo la Pili: Utazamaji wa mtoto.
  3. Jambo la Tatu: Unyonyeshaji.

Tukianzana na hilo la kwanza: Utaona mwanamke yule mwerevu, alikuwa kila alipolala alikiweka kichanga chake Ubavuni. Ikiwa na maana alijitahidi kwa kadiri awezavyo kulala chali, ili mtoto apate nafasi ya kumwegemea yeye aidha ubavuni pake au kifuani pake, na sio yeye amwegemee mtoto,..Lakini yule mwingine hakulijali hilo, alimgeuza mtoto kuwa godoro, akamlalia..Na matokeo yake yakawa ni kifo.

  • Zingatia: Unapozaa mtoto, hakikisha mwanao muda wote yupo ubavuni pako.. Hakikisha Unamjali wakati wote, hata ule wakati ambao hujalala, mweke mgongoni mwako, usimwache kizembe zembe bila kumwangalia hiyo  itakuwa ni kwa usalama wa mwanao.

Pili: Kama yule mwanamke angekuwa “hamchunguzi/hamdadisi” sana mtoto wake: Basi angeibiwa mwanawe bila habari. Lakini yeye tangu siku ya kwanza alikuwa anamkagua hadi kufikia siku ya tatu tayari alikuwa ameshamjua mwanawe ndani nje..,!, alijua umbile la mwanawe, na alama zake,..Hata pale alipojaribu tu kuchanganyiwa mtoto alilimtambua hilo mara moja.

  • Zingatia: Je! Wewe umeshamjua mtoto wako wote ndani ya siku tatu za kwanza? Kiasi kwamba wakiwekwa katikati ya  vichanga 1000 utaweza kumtaumbua mwanao? . Fanya hivyo kwasababu Hiyo itakusaidia pia kugundua tatizo ikiwa litampata mwanao kwa haraka.Lakini ikiwa wewe upo buzy tu, na mambo yako, humwangalii mtoto wako.Unamwachia msaidizi wako akufanyie kila kitu Ujue lipo jambo litamwiba mwanao, na wewe usijue chochote. Akiumizwa wewe hutajua, akiugua wewe hutajua chochote n.k.

Malalamiko mengi, ya wazazi, kuhusu Watoto wao kudhalilishwa kijinsia yanatokana na wazazi kutokuwa na tabia ya kuwachunguza Watoto wao, wanakuja kugundua  hali imeshakuwa mbaya sana hairekebishiki. Anza kujijengea tabia hiyo ni kwa heri yako na kwa usalama wa kichanga chako.

Tatu: wanawake wale walikuwa ni wanyonyeshaji wa maziwa yao wenyewe ya asili kwa vichanga vyao na sio ya ng’ombe.

  • Zingatia: Ukiishia kumpa mtoto wako mchanga maziwa ya makopo, kwa kuogopa kuharibika maumbile yako basi ujue upendo wake utahamia kule kwa Wanyama. Fanya hivyo ikiwa tu hakuna jinsi, labda mtoto kagoma kunyonya, au mama maziwa hayatoki, au pana matatizo mengine  ya kiafya lakini vinginevyo mnyonyeshe mwanao maziwa yako mwenyewe kwa afya bora wa mwili wake, na kinga zake, hata madaktari wanashauri hivyo.

KWA UPANDE WA MALEZI YA KIROHO.

Sasa ili mtoto wako mchanga awe na ulinzi wa ki-Mungu maishani mwake..Mchukue ukamweke wakfu mbele za Mungu. Hakikisha pia huendi mikono mitupu, ambatanisha na sadaka yako ya shukurani kwa Mungu kwa kile alichokupa/alichowapa.

Ipo mifano mingi ya kimaandiko ya wanawake wenye akili walipeleka Watoto wao wapeleka mbele za Bwana wabarikiwe, na mpaka leo tunaona Watoto hao jinsi walivyokuwa nguzo muhimu katika Imani, Ukimsoma Samweli, yeye hakuwa vile hivi hivi tu, bali ni baada ya mama yake kumpeleka mbele za Bwana (Soma Samweli 1&2).

Ukimsoma Yohana Mbatizaji naye vivyo hivyo,. Ukimsoma pia Bwana wetu Yesu Kristo naye vivyo hivyo, wote walipelekwa mbele za Bwana. Vivyo hivyo mchukue mwanao, mpeleke nyumbani kwa Bwana awekwe wakfu kwa Bwana kwa kuwekewa mikono na wachungaji au wazee wa kanisa..Hiyo itakuwa ni salama ya Maisha ya baadaye ya mwanao.(Luka 2:22-24).

Huhitaji kusubiri mpaka awe mkubwa, siku za mwanzoni mwanzoni, au wiki za mwanzoni haraka bila kukawia mpeleke kwa Bwana..Kumbuka mtoto mchanga habatizwi kulingana na maandiko, Hivyo usifanye hivyo kwasababu haitasaidia chochote. Mpeleke akawekewe mikono tu awe wakfu kwa Bwana.

Na hili ndio jambo kuu kuliko yote ya kuzingatia. Unaweza ukaijali afya yake, lakini kama Mungu hamtambui ni kazi bure.Kwasababu shetani ndiye atakayemtambua.

Vilevile ni jukumu lako kumwombea mwanao kila wakati, Tenga muda maalimu wa kumwombea, walau lisaa 1 kila kipindi. Mwombee afya yake, mwombee ukuaji wake, mwombee kila pembe ambayo Mungu atakuongoza. Vilevile unapomwimbia Mungu imba Pamoja naye,  Na hiyo ndio dalili nzuri upendo Mungu anaotaka mazazi aonyeshe kwa vichanga vyao.

Hivyo kwa kuhitimisha zingatia hayo mambo makuu 5.

  1. Muweke ubavuni mwako  daima.
  2. Mjue mtoto wako.
  3. Mnyonyeshe maziwa yako mwenyewe.
  4. Kamweke wakfu kwa Mungu.
  5. Mwombee.

Lakini kumbuka pia yote hayo ili yawe na maana ni lazima na wewe kama mzazi/wazazi, muwe mmemkabidhi Kristo Maisha yenu (yaani muwe mmeokoka). Hizi ni nyakati za mwisho na za hatari sana kama ulikuwa hujui, Pale Bwana Yesu aliposema..

Mathayo 24:19  “Ole wao wenye mimba na wanyonyeshao siku hizo! 20  Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato. 21  Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe”.

Jiulize ni kwanini alisema, ole kwa wanyonyeshao kama wewe?..Alisema hivyo kwasababu alijua mwisho ukiwakuta watu wa namna kama ya kwako, wakati huo utakuwa ni mgumu sana kwao..Embu jiweke  katika mazingira kama hayo halafu usikie YESU karudi kulinyakua kanisa..Umebaki hapa duniani , halafu mpinga-Kristo anaanza kuchinja watu utakuwa katika hali gani na mwanao.

Angalia magonjwa yanayotokea duniani ya ajabu (covid-19), angalia, majanga, angalia matetemeko makubwa, mauaji ya ajabu na ya kinyama, angalia tetesi za vita vya ki-atomiki na kuibuka kwa manabii wa uongo..Hapo hatuwezi kusema tuna vizazi vingine mbele vya kuishi, pengine mimi na wewe tutashuhudia tukio zima la Unyakuo..Sasa utakuwa wapi ikiwa leo hii hujaokoka ndugu yangu..

Lakini ukitubu sasa, Kristo yupo tayari kukusamehe, unachopaswa kufanya ni kumaanisha tu, kutoka katika moyo wako, na kusema kuanzia leo mimi ninaacha dhambi ninamgeukia..Na wakati huu huu Kristo ataanza kufanya kazi ndani ya Maisha yako, Hivyo kama upo tayari kufanya hivyo leo.

Basi uamuzi unaoufanya ni wa busara sana ambao hautakaa uujutie maisha yako yote kama ilivyokuwa hata kwetu sisi. Unachopaswa kufanya, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU  MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako. Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.

Ubarikiwe sana

Mada Nyinginezo:

KILEMBA CHA NEEMA, JE! UMEMVIKA MWANAO?

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia..!!

SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

KILEMBA CHA NEEMA, JE! UMEMVIKA MWANAO?

kilemba cha neema, Je! Umemvika mwanao ?


Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe..Karibu tujikumbushe mambo muhimu katika maisha yetu..Na hayo si mengine zaidi ya maonyo ya Neno la Mungu…Leo kwa Neema za Bwana tutajikumbusha majukumu machache ya wazazi juu ya watoto wetu..

Biblia inasema katika…

Kutoka 20: 12 “Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako”.

Neno hili ni Neno la Mungu kwa watoto wote ambao wanao wazazi…Na hata kama hawana wazazi labda wamefariki au hawaishi nao kwa namna moja au nyingine…Basi nafasi hiyo ya Baba na Mama itachukuliwa na walezi wao…Hao wanasimama kama Baba zao na Mama zao kihalali kabisa mbele za Mungu..hata kama wapo katika vituo vya malezi vya mayatima…hao walezi wao wanachukua nafasi hiyo ya Baba na Mama…wana amri kutoka kwa Mungu kuheshimiwa kama wazazi halisi…Kwasababu kuna Baraka kubwa sana katika kuwaheshimu wazazi na kuwasikiliza..

Kadhalika haijalishi mzazi ni mwovu kiasi gani lakini ni lazima kumheshimu, na kumtii haijalishi yeye hajiheshimu kiasi gani ni wajibu wa kila mtoto kumheshimu mzazi wake..Kwasababu ndio amri ya kwanza yenye ahadi…

Waefeso 6:1 “Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki.

2 Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi,

3 Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia”

Kupata heri na kuishi siku nyingi ni vitu viwili tofauti…Unaweza kuishi siku nyingi lakini maisha yasiwe ya heri..Hivyo, vyote viwili vinapaswa viende pamoja…

Jukumu la mzazi kwa mtoto.

Sasa Kitu cha Muhimu cha kufahamu kwa mzazi ni kwamba…Hatima ya mtoto, mzazi anaweza kuchangia kwa asilimia kubwa kuitengeneza au kuiharibu…Mzazi anaweza kukazana kweli kumpenda mwanawe, kumlipia karo, kumtafutia shule bora..kumpatia lishe bora, kumlinda..kumhakikishia bima ya afya n.k Lakini kama hatamtengenezea mwanawe mazingira ya kumheshimu au kumtii.. huyo mtoto hawezi kupata heri yoyote huko anakokwenda, wala hawezi kuishi maisha marefu…haijalishi atapatiwa elimu nzuri kiasi gani sasa…au atakuwa na afya nzuri kiasi gani sasa au maarufu kiasi gani…Maisha yake yatakatika katikati na yatakuwa ya tabu.

Hivyo mzazi ukilijua hilo utahakikisha mwanao anakuheshimu na kukutii…

Hayo ndio mambo ya kwanza ya kuzingatia kabla hata ya kwenda kuangalia ufaulu wake wa darasani…usifurahie anapofaulu sana na huku adabu yake inazidi kwenda chini..furahia pale heshima yake na utii wake unapozidi kupanda kwasababu unajua..hata kama atapepesuka kiafya sasa..hatakufa!..ataishi muda mrefu kwasababu Neno la Mungu linasema hivyo..hata kama hana heri sasa, lakini atakuja kuwa na heri baadaye katika kipindi cha maisha yake yote..

Hivyo kazana kumfundisha awe na tabia ya kukusikiliza…chochote utakachomwambia akutii na afanye kwa kupenda na si kwa kulazimishwa lazimishwa..mfunze tabia nzuri na heshima na utiii kwako na kwa watu wengine, mvishe mavazi ya adabu na mfundishe kuwa mtii….Mjaribu mara kwa mara kuangalia utii wake umefikia wapi ukiona umepungua tafuta namna ya kuurudisha…..mtume dukani mrudishe hata mara mbili au tatu, mpime..ujue kiwango cha utii alichonacho na heshima.

Mpime mwanao;

Mpime anapokuwa na wageni na watu wengine anakuwa na tabia gani zisizofaa na zile zinazofaa mpongeze…ukiona kasoro tumia fimbo kidogo, maana biblia inasema ukimpiga hatakufa…Wengi hawatumii fimbo wakidhani wanamharibia ujasiri mtoto, fimbo isiyokuwa na mafunzo sahihi ndiyo inayomharibia ujasiri..lakini fimbo yenye ujumbe wa kujenga ndiyo inayomjenga zaidi mtoto…

Na Mungu alivyowaumba watoto hawana kinyongo ili kwamba waweze kutengenezeka..ukimwadhibu sasahivi baada ya nusu saa mnacheka na kufurahi, ule upumbavu utakuwa umendoka lakini upendo wake kwako bado upo…..ukimwacha sasa bila kumfunza atakapokuwa mtu mzima hali za kuwa na vinyongo na uchungu zitakapomjia itakuwa ni ngumu kumtengeneza….kila utakalomwambia atakuwa anakwambia unamnyanyasa,..mara unaingilia uhuru wake..mara hujali hisia zake, mara wewe ni mkoloni, mara unamwaibisha n.k

Mfundishe biblia;

Pia katika utoto aliopo, mfundishe biblia..mpe mistari kadhaa ya kuikariri na kuishika kwasababu watoto wengi bado hawajaweza kuipambanua mistari..wape tu waikariri itawasaidia ukubwani..kuliko kukariri nyimbo za kidunia..pia wafundishe nyimbo za kuabudu, na kumsifu Mungu na wafundishe sala za kuomba muda wote na habari za Yesu ambazo ndizo za muhimu kuliko zote..Na wapime je hivyo unavyowafundisha au wanavyofundishwa na wengine wanavizingatia.??

Ukimpima mtoto vizuri na kujua kuwa anakutii na kukuheshimu na anaheshima kubwa ambayo mpaka watu wa nje wanaishuhudia na kusema Yule mtoto anaheshima na adabu…Basi, kuna Baraka ambazo Mungu anaziachia ambazo ulimwengu hauwezi ukaziona..hapo ndipo nyota njema ya mtoto inapoanzia..

Biblia inasema hayo mafunzo hatayaacha hata atakapokuwa mzee…

Mithali 22: 6 “Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee”…

Wengi wanaogopa kuwafundisha wanao adabu na heshima kwasababu wanahisi wakishafikisha umri Fulani labda wa kuvunja ungo au kubalehe watakengeuka..Huo ni uongo wa shetani!!…Watoto wengi wanakengeuka ukubwani kwasababu wazazi wao ambao hapo kwanza walikuwa wanawalea vizuri leo wamekengeuka!..sasa kama mzazi kakengeuka mtoto atasalimikaje?..Mzazi alikuwa anakwenda kanisani na mwombaji sasa hafanyi hivyo tena..mtoto ataendeleaje kwenda kanisani?…Mtoto alikuwa amezoea nyumbani ni mahali pa ibada sasa nyumbani kunapigwa kila siku kwenye TV, nyimbo za kidunia, mtoto ataendeleaje kuwa mtakatifu?….Lakini kama mzazi akibaki vile vile Yule mtoto kamwe hawezi kukengeuka hata atakapokuwa mzee..biblia sio kitabu cha Uongo!… Haiwezi kusema mtoto hataiacha ile njia halafu aje kuiacha!..sasa Mungu atakuwa ni mwongo.

Sasa faida nyingine ya mwisho na kuu ambayo mtoto anaweza kuipata kutoka kwako mzazi kwa kumfanya akutii na hata akusikilize na kukuheshimu katika viwango vya juu ni KUVIKWA KILEMBA CHA NEEMA KICHWANI PAKE?.

Faida hiyo ya kuvikwa KILEMBA CHA NEEMA KICHWANI PAKE.Biblia inaisema katika..

Mithali 1: 8 “Mwanangu, yasikilize mafundisho ya baba yako, Wala usiiache sheria ya mama yako,

9 Kwa maana hayo yatakuwa KILEMBA CHA NEEMA KICHWANI PAKO, Na mikufu shingoni mwako”.

Hii ni Baraka kubwa sana ambayo wazazi wengi hawaijui…Hapa duniani tunaishi kwa Neema,…Hivyo Neema ya Kristo inapokuwa nyingi juu yetu..ndipo tunapokuwa na nafasi zaidi ya kumkaribia Mungu, ndipo tunapokuwa na nafasi kubwa zaidi ya kuwa watumishi wa Mungu…Na utumishi wa Mungu sio tu ule wa kuhubiri madhabahuni hapana! bali hata ule wa Danieli ni utumishi wa Mungu..Pale Mungu anapokuweka katika ngazi Fulani ya juu na huko anakutumia kuwatunza watu wake..Hivyo Neema kama hiyo ni njema kwa mtu yeyote…Mtu anayemtumikia Mungu,.. Mungu atamheshimu biblia inasema hivyo (katika Yohana 12:26).

Mfundishe kwa bidii kukutii;

Sasa ni nani asiyetaka kuheshimiwa na Mungu?..Je! unataka mwanao aheshimiwe na Mungu?…Kwa kuvikwa neema ya kuwa mtumishi wake?…Ni kwa kumfanya akutii na kukuheshimu..huku na wewe ukionyesha kielelezo cha kumcha Mungu maisha yako yote ili usimwangushe..

Kuwa na mtoto ni Baraka!..Hususani kama umemvisha kilemba hicho cha neema….Neno la Mungu linasema wapeni watu vitu nanyi mtapewa kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika ndivyo watu watakavyowapa kifuani mwenu…..Na wewe umempa mwanao hicho kipimo cha Neema ya Mungu juu ya kichwa chake kubwa namna hiyo…Bwana atamtumia huyo huyo kukulipa..kukurudishia kipimo cha kujaa na kushindiliwa nakusukwasukwa hata kumwagika katika siku za mbeleni..Na kwasababu mwanao au wanao watakuwa wanatembea na hiyo NEEMA kubwa sana kichwani mwao basi kila watakalomwomba Mungu, Mungu na kila watakalolifanya litafanikiwa katika maisha yao.

Bwana akubariki.

Kama wewe mzazi hujaokoka!..Tambua kuwa huwezi kuwavika wanao KILEMBA HICHO CHA NEEMA vichwani mwao..Wataharibikiwa na kuwa na maisha mabaya..kwasababu maisha yako wewe ni mabaya!..Hivyo ni vizuri leo hii ukamgeukia Kristo akuoshe dhambi zako kweli kweli kwa damu yake..Ili uwe mzazi/mlezi bora…Unachopaswa kufanya ni kutubu kuanzia leo na kumwambia Bwana akusamehe..akusamehe, uasherati wako kama ulikuwa unaufanya..akusamehe kwa kutowajali wanao,..akusamehe kwa kila uchafu uliokuwa unaufanya..na hivyo unamwahidi kwamba utafanya tena..

Baada ya kutubu kabatizwe katika ubatizo sahihi kwaajili ya ondoleo la dhambi (Matendo 2:38)..Kumbuka ubatizo sahihi ni ule wa kuzamishwa mwili wote kwenye maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo. Baada ya kufanya hivyo Roho Ambaye atakuwa ndani yako atakuongoza kufanya mengine yote yaliyosalia na kukupa uelewa wa ajabu wa kuyaelewa maandiko na kukusaidia kushinda dhambi ambazo kwa nguvu zako ulikuwa huwezi.

Kumbuka pia Yesu Kristo atarudi..Biblia inasema “Itatufaidia nini tuupate ulimwengu mzima na kisha tupate hasara za nafsi zetu’’..Hivyo uwe unalitafakari hilo kila siku.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Maran atha!..Shalom.

Mada Nyinginezo:

LENGO LA SHETANI KWA WATOTO WA KIZAZI HIKI.

MOTO HUFA KWA KUKOSA KUNI.HATA UASHERATI NAO

KIMBIA! KIMBIA! KIMBIA!

UNATAKA KUBARIKIWA? BASI USIKWEPE GHARAMA ZAKE.

BONDE LA KUKATA MANENO.

Rudi Nyumbani:

Print this post