RUDI KUMPA MUNGU UTUKUFU.

RUDI KUMPA MUNGU UTUKUFU.

Kuna tofauti ya kumpa Mungu utukufu na kumshukuru Mungu. Mungu anapokufanyia jambo zuri, lakukupa faraja na furaha, na moyoni ukafurahi, ni kawaida ya kila mwanadamu mwenye moyo wa shukrani, huwa anakwenda kupiga magoti na kumshukuru Mungu wake kwa alilomtendea aualiyomtendea, na zaidi sana huwa anaambatanisha hata na sadaka yake ya shukrani.

Sasa hilo ni jambo moja ambalo linampendeza sana Mungu wetu, pale tunapomshukuru, lakini lipo lingine linalompendeza pia ambalo litatufungulia milango ya baraka mara mbili. Na jambo hilo si lingine zaidi ya KURUDI KUMPA MUNGU UTUKUFU.

Kurudi kumpa Mungu utukufu, ni kitendo cha kurudi na kutangaza kwa wazi, yale yote Mungu aliyokufanyia.. Hivyo Mungu wako anakuwa anatukuzwa katikati ya watu.

Ni jambo linalodharaulika na wengi lakini ni la umuhimu sana. Kurudi kumpa Mungu utukufu…Je umeshawahi kurudi kumpa Mungu utukufu kwa jambo lolote jema alilokufanyia?

Hebu tusome hichi kisa maarufu kwenye biblia..

Luka 17:11 “Ikawa walipokuwa njiani kwenda Yerusalemu, alikuwa akipita katikati ya Samaria naGalilaya.

12 Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali,

13 wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu!

14 Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakiendawalitakasika.

15 Na mmoja wao alipoona kwamba amepona, alirudi, HUKU AKİMTUKUZA MUNGU KWA SAUTİ KUU;

16 akaanguka kifudifudi miguuni pake, akamshukuru; naye alikuwa Msamaria.

17 Yesu akajibu, akanena, Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi?

18 JE! HAWAKUONEKANA WALİORUDİ KUMPA MUNGU UTUKUFU İLA MGENİ HUYU?

19 Akamwambia, Inuka, enenda zako, imani yako imekuokoa”

Waliponywa wote kumi lakini ni huyu mmoja tu ndiye Aliyepaza sauti yake, kwa sauti kuu, akitangaza jinsi alivyoponywa njia nzima, mpaka alipofika kwa Bwana Yesu..Pengine wale 9 walikwenda kutoa sadaka zao za shukrani tu!..Lakini hawakumtukuza Mungu, walakutangaza waliyofanyiwa kwa wazi, kwasababu zao wenyewe, labda waliona aibu, au waliogopa kutengwa, au kuonekana wa kikale…Lakini huyu hakujali hayo, alitangaza kwa watu lililomtokea kuanzia mwanzo hadi mwisho..

Na hivyo likawa ni jambo jema mbele za Mungu..

Je na wewe ulishawahi kurudi kumpa Mungu utukufu?… Bwana alipokuponya ugonjwa ambao ilikuwa ni ngumu kupona, je! Ulishawahi kusimama na kutangazia watu wawili au watatu mambo makuu Mungu aliyokufanyia?..au uliishia kuwatukuza madaktari tu! Kwamba walikupambania lakini hukuwahi kumtaja Mungu maneno yasiyozidi mawili?..Kama ndivyo basi badilika leo.

Je ulishawahi kumpa Mungu utukufu kwa huyo mtoto uliyempata ambaye ulihangaika miaka mingi bila kupata mtoto?..Ni kweli pengine ulitoa sadaka ya shukrani, hiyo ni vizuri…lakini bado haitoshi…Mungu wako anapaswa atukuzwe mbele za watu kwa hicho alichokufanyia.. Inapaswa watu wamwonapo mwanao aliyekupa Mungu, wamfikirie Mungu wako na si daktari wako wala jitihada zako.

Nyumba Mungu aliyokupa, mali alizokupa, afya aliyokupa, uzima anaokupa, cheo alichokupa, elimu aliyokujalia, nguvu alizokupa n.k…Je Mungu wako anatukuzwa katika huo? Au jitihada zako?..Watu wanapaswa wakitazama cheo chako wanakumbuka ushuhuda uliowasimulia wa jinsi Mungu alivyokuweka pale kimiujiza, na sio wanakumbuka jinsi ulivyopambana…Watu wanapokuona leo umesimama ni mzima, wanapaswa wakumbuke ushuhuda uliowaambia jinsi ulivyokuwa hatiani kupona na ukamwomba Mungu na Mungu akakufungulia mlango wa uponyaji… ili Mungu wako atukuzwe kwao.

Watu wanapokuona una hiki au kile..wanapaswa wautafakari uzuri wa Mungu wako, na utukufu wake, kwa utukufu uliomrudishia wakati unavipata hivyo…kila kitu wajue ni Mungu kakusaidia na si nguvu zako.

Na hatumpi Mungu wetu utukufu kwa yale aliyotutendea kwa kuwawekea watesi wetu CD za  mipasho!.. Kwasababu siku hizi zipo nyimbo za dini ambazo hazina tofauti na nyimbo za kidunia (Taarabu)..zimejaa maneno ya kiburi na ushindani. Kwamba Mungu kanitendea hichi ili maadui

zangu waone waumie moyo…Hapana! mpango wa Mungu sio maadui zetu waumie moyo na waone Mungu alichotufanyia halafu basi!. Mungu hatupiganii ili awachome watu mioyo, bali ili awageuze nia zao wamgeukie yeye.

Hivyo ukimpa Mungu utukufu mbele za watu, jinsi inavyopaswa, kwa kutangaza kwa kina ulipotoka na ulipo sasa, na jinsi gani Mungu alivyokuokoa, kwa neema…Wale wanaokusikiliza akili zao zitahama kutoka kushindana na wewe, na kuhamia kumtafakari Mungu wako, na hivyo nao pia wamtamtamani Mungu wako aliyekutendea mambo makuu namna hiyo. Na watakuuliza “nami nifanyaje Mungu anitendee kama alivyokutendea wewe”

Lakini ukianza kuwawekea mipasho, watakuchukia na hawatavutiwa na unachokiamini, hivyo utakuwa nawe pia unaifanya kazi ya ibilisi ya kuwapeleka watu mbali na Mungu, na moyoni ukidhani umemtukuza Mungu kwa nyimbo zako hizo za kiburi na majivuno kumbe ndio unaenda kinyume na mapenzi ya Mungu.

Hivyo Usiache kamwe kurudi kumpa Mungu utukufu kwa jambo lolote lile analokutendea, hata liwe dogo kiasi gani…Nenda kalitangaze kanisani, kalitangaze kwa rafiki zako, kalisimulie kwa ndugu, kalisimulie kwa yoyote yule ambaye utapata nafasi ya kumsimulia..hakikisha tu lengo lako ni Mungu atukuzwe na si wewe utukuzwe, au kujisifu.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

JE KUNA UISLAMU KATIKA BIBLIA?

Mavu ni nini katika biblia?(Kutoka 23:28, Kumb 7:20)

UTAWALA WA MIAKA 1000.

CHAPA YA MNYAMA

WINGU KUBWA LA MASHAHIDI.

BABA YANGU ANATENDA KAZI HATA SASA!.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments