Category Archive Home

MZEITUNI HALISI UTAKAPOPACHIKWA.

Kuna watu wanasema sasa tunaishi katika agano jipya hivyo Mungu hatazami tena Taifa, wala mtu wala jinsia bali wote ni sawa kulingana na Wagalatia 3:28. Na hivyo wanadai kuwa hakuna kitu kama hicho taifa la Israeli kurudiwa na Mungu tena na Mungu kutembea nao kama ilivyokuwa katika agano la kale, sisi wote ni sawa na Kristo hivyo hakuna haja ya kutazama kinachoendelea Israeli, lile ni kwasasa ni taifa tu kama mataifa mengine. Ni kweli kabisa mbele za Kristo hakuna hivyo viambazi, wote ni sawa hakuna myahudi wala myunani, wala mke au mume, lakini katika kanuni ya utendaji kazi wake, ameweka mipango, mipaka, na kanuni na taratibu, na muda..

Kwamfano ilimpasa Mungu awapige upofu kwanza wayahudi(yaani Waisraeli) ili sisi, yaani mimi na wewe tuipokee neema, Mungu aliwafanya wawe vile kwa makusudi kabisa kwa ajili yetu na laiti asingefanya vile, leo hii sisi tusingemjua Kristo. Wokovu huu ungebakia kuwa ni wa wayahudi tu biblia inasema hivyo…Vile vile kama pia ukitazama kwa ukaribu utaona Neema ilipokuja kwa mataifa, haikuja na kukaa kila mahali kwa wakati mmoja japo kweli ilisikika ulimwenguni kote,lakini neema haikukaa kila mahali, ilikuwa inazunguka ukisoma maandiko na historia utoana ilianza bara la Asia, baadaye ikaja kuenea bara la Ulaya, baadaye ikafika Marekani, na mwisho wa siku sasa ipo kwetu huku Afrika..Na ndio maana utaona kuna mwitikio mkubwa wa watu kumtafuta Kristo huku kuliko mabara mengine yote duniani, lakini mfano kama ungekuja kipindi cha karne ya 19 huku Afrika, ungekutana na uchawi na ushirikina tu, wakati ulaya ndio ulikuwepo uamsho mkuu wa Roho.

Hivyo neema hii inatabia ya kutembea, na sasa inakaribia kuondoka na kurejea Israeli ilipoanzia, Na Bwana aliahidi kabla haijarudi atarudisha watu wake Israeli katika Taifa lao nao watakaa salama, kisha baadaye atawaletea uamsho. Jambo hilo tumeliona likitimia mwaka 1948, baada ya kukaa zaidi ya miaka 2500, ugenini kwenye mataifa mengine.Tofauti na wale wanaosema kuwa Israeli hawatarudiwa tena..Biblia ilitabiri kuwa watarudi nchini kwao.

Yeremia 34:23 “Kisha neno la Bwana likamjia Yeremia, kusema,

24 Je! Hufikiri neno hili walilolisema watu hawa, wakinena, Jamaa zile mbili alizozichagua Bwana amezitupilia mbali? Hivyo ndivyo wanavyowadharau watu wangu, ili wasiwe taifa tena mbele yao.

25 Bwana asema hivi, Ikiwa agano langu la mchana na usiku halikai imara, ikiwa mimi sikuziamuru kawaida za mbingu na dunia;

26 ndipo nitawatupilia mbali wazao wa Yakobo, na Daudi, mtumishi wangu, hata nisitwae wazao wake watawale juu ya wazao wa Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo; kwa maana nitawarudisha wafungwa wao, nami nitawarehemu.”

Unaona hapo Bwana anasema kama vile agano lake la mchana na usiku likivunjika, yaani siku moja ipite kusiwe mchana, au kusiwe usiku basi na atawatupilia mbali watu wake wayahudi, lakini kama halijawahi kutanguka, basi kwame hatakaa awasahau wayahudi.

Nataka nikuambie ndugu Uamsho wao utakuwa wa kipekee sana, ni ule Mtume Paulo alisemea juu ya mzeituni halisi uliokatwa na kurudishwa kwenye shina lake halisi, unategemea vipi matunda yasitoke halisi zaidi, ikiwa sisi tuliokuwa mizeituni mwitu tukapachikwa kwenye mzeituni halisi na tukatoa matunda halisi, je si zaidi hao waliokuwa halisi wenyewe, watatoa kilicho bora zaidi..

Warumi 11:15 “Maana ikiwa kutupwa kwao kumeleta upatanisho kwa ulimwengu, je! Kukubaliwa kwao kutakuwa nini kama si uhai baada ya kufa?

16 Tena malimbuko yakiwa matakatifu, kadhalika na donge lote; na shina likiwa takatifu, matawi nayo kadhalika.

17 Lakini iwapo matawi mengine yamekatwa, na wewe mzeituni mwitu ulipandikizwa kati yao, ukawa mshirika wa shina la mzeituni na unono wake,

18 usijisifu juu ya matawi yale; au ikiwa wajisifu, si wewe ulichukuaye shina, bali ni shina likuchukualo wewe.

19 Basi utasema, Matawi yale yalikatwa kusudi ili nipandikizwe mimi.

20 Vema. Yalikatwa kwa kutokuamini kwao, na wewe wasimama kwa imani yako. Usijivune, bali uogope.

21 Kwa maana ikiwa Mungu hakuyaachia matawi ya asili, wala hatakuachia wewe.

22 Tazama, basi, wema na ukali wa Mungu; kwa wale walioanguka, ukali, bali kwako wewe wema wa Mungu, ukikaa katika wema huo; kama sivyo, wewe nawe utakatiliwa mbali.

23 Na hao pia, wasipokaa katika kutokuamini kwao, watapandikizwa; kwa kuwa Mungu aweza kuwapandikiza tena.

24 Kwa maana ikiwa wewe ulikatwa ukatolewa katika mzeituni, ulio mzeituni mwitu kwa asili yake, kisha ukapandikizwa, kinyume cha asili, katika mzeituni ulio mwema, si zaidi sana wale walio wa asili kuweza kupandikizwa katika mzeituni wao wenyewe?

25 Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili.

26 Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa, Mwokozi atakuja kutoka Sayuni; Atamtenga Yakobo na maasia yake.

27 Na hili ndilo agano langu nao, Nitakapowaondolea dhambi zao.”

Ndugu yangu kuna wakati unafika hii neema inayochezewa na watu itarudi makao yake makuu (Israeli), na hawa wayahudi ambao unawaona sasa hawana habari na Yesu, wapo vuguvugu, hawaeleweki, biblia inasema ndani ya siku moja Mungu atawamwagia Roho ya neema, nao watatubu kwa kumaanisha kabisa, yaani mji mzima wa Yerusalemu utakuwa unaomboleza siku hiyo , wakimwombolezea Bwana Yesu ambaye walikuwa wakimpinga tangu zamani.

Zekaria 12:10 “Nami nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, roho ya neema na kuomba; nao watamtazama yeye ambaye walimchoma; nao watamwombolezea, kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao wataona uchungu kwa ajili yake, kama vile mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya mzaliwa wake wa kwanza.

11 Siku hiyo kutakuwa na maombolezo makuu huko Yerusalemu, kama maombolezo ya Hadadrimoni katika bonde la Megido.

12 Nayo nchi itaomboleza, kila jamaa peke yake; jamaa ya nyumba ya Daudi peke yao, na wake zao peke yao; jamaa ya nyumba ya Nathani peke yao, na wake zao peke yao;

13 jamaa ya nyumba ya Lawi peke yao, na wake zao peke yao; jamaa ya nyumba ya Shimei peke yao, na wake zao peke yao.

14 Jamaa zote zilizosalia, kila jamaa peke yake, na wake zao peke yao”.

Wakati huo, neema itakuwa imeshaondoka kwenye mataifa yote dunia, hapo ndipo Mungu ataitumia Israeli kuwa fimbo kwa mataifa yote, usitamani wakati huo ukukute..Leo hii tumeshaanza kuona dalili ndogo ndogo, jiulize kwanini taifa la Israeli ni dogo kuliko hata mkoa wa Songwe, halina kitu chochote cha kuvutia wala haina teknolojia ya kutisha sana kama mataifa ya mashariki na Magharibi lakini kila mtu anaizungumzia, isitoshe bado wanaigopa, na hapo hata Mungu hajatia mguu wake kutembea nao, jiulize wakati huo ukifika itakuwaje?.

Ndugu ni mambo mengi ya kutisha yapo mbele yetu ambayo hata sisi wenyewe hatuyajui vizuri, ni heri tukabakia katika upande salama, Vita ya Harmagedoni ambayo itakuja kupigwana kipindi kifupi baada ya unyakuo itapiganiwa pale pale Israeli…( ukihitaji maelezo marefu juu ya vita hii, nitumie ujumbe inbox nitakutumia somo lake..)

Huu ni wakati wa kuweka mambo yetu sawa, ikiwa bado hujatubu, mgeukie muumba wako sasa, na ikiwa bado upo nusu nusu, vuguvugu, uimarishe wito wako sasa, kabla nyakati za hatari hazijafika.

Bwana akubariki sana. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Zinazoendana:

MAMBO YATAKAYOTOKEA ISRAELI SIKU ZA HIVI KARIBUNI

UFUNUO: Mlango wa 7 & 11

AMIN! NAWAAMBIA KIZAZI HIKI HAKITAPITA!


Rudi Nyumbani

Print this post

MUNGU MWENYE HAKI.


Shalom mtu wa Mungu karibu tujifunze juu ya Haki ya Mungu.

Ni wazi na inajulikana na wote kuwa Mwenyezi Mungu aliyetuumba sisi viumbe vyake vyote ni Mungu mwenye haki, hilo halina kipingamizi, lakini ni vizuri kuijua kwa mapana haki hiyo ya Mungu inatendaje kazi katikati ya viumbe vyake. 

Kazi anazofanya shetani na malaika wake walioasi ndio hizo hizo wanazozifanya Malaika wa Mbinguni ambao hawajaasi, shetani na Malaika zake wanajishungulisha sana na mambo ya wanadamu namna ya kuwavuta wanadamu wengi upande wao, kadhalika na Malaika watakatifu wanajishughulisha sana na mambo ya wanadamu namna ya kuwavuta wanadamu upande wa Mungu.

Sasa anayepambana na shetani si Mungu, Mungu hashindani na kiumbe chochote kile, yeye ni Mkuu kupita upeo wa fahamu zetu wote, hivyo hawezi kushindana na kiumbe chochote alichokitengeneza yeye…Kwahiyo anayeshindana na shetani ni Mikaeli pamoja na malaika wenzake watakatifu na si Mungu. Mikaeli ni Malaika mkuu wa vita aliyeko mbinguni aliye kiongozi wa vita kama vile shetani alivyo kiongozi wa malaika wengine walioasi….wapo malaika wa aina tofauti tofauti.

Ufunuo 12:7 “Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake;

8 nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni

9 Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye”.

Sasa kama Mungu hashindani na shetani, swali linakuja yeye atakuwa anafanya kazi gani?

Jibu: Mungu anasimama kama wakili au hakimu, kuwapatia haki wale wanaostahili haki…

Hivyo kazi ya malaika watakatifu ni kusisimama kututetea sisi wanadamu kila siku mbele za uso wa Mungu, na kazi ya shetani na malaika zake ni kutushitaki…maana tafsiri yenyewe ya jina ‘shetani’ ni ‘mshitaki’…kazi yake ni kutafuta kasoro ndogo ndogo na kubwa katika Maisha yetu na kuzipeleka kwa Hakimu Mkuu (Mungu) kutafuta haki ya kututesa au kutuangamiza.

Sasa anapokuja kwako na kukuta kuwa wewe ni mwasherati, au mchawi, na unafanya hayo huku ukijua kabisa ni dhambi…..moja kwa moja anakimbiza hizo hoja mbele za Mungu, na kutaka ruksa ya kukutawala Maisha yako, atamwambia Mungu huyu kwa mapenzi yake mwenyewe anafanya hayo, na wala hajalazimishwa, ananitumikia mimi, amesikia injili yako na anajua kabisa kwa matendo yake atakwenda kuzimu, lakini bado anayafanya hayo..hivyo huyu ni wangu.. nipe ni wangu huyo.

Na wale malaika wa Mungu wanapokosa kitu cha kukutetea mbele za Mungu, kutokana na mambo unayoyafanya ya umakusudi na ukiwa na akili timamu, shetani anashinda hoja mbele za Mungu na kupewa haki yake..Mungu hana upendeleo hata kidogo ndio asili yake hiyo, anamlipa kila mtu kulingana na anachostahili, shetani anampa haki yake na Malaika vile vile anawapa haki zao… Ndio hapo mtu anajikuta ghafla ulinzi wa kiMungu umeondoka juu yake, anaanza kupitia hili na lile..na wakati mwingine hata kufa.

Lakini anapokuja na kukuta umemwamini Bwana Yesu Kristo, na umeoshwa kwa damu yake, na unaishi Maisha matakatifu, hata kama kuna viudhaifu vidogo vidogo, hivyo havitoshi kumpa shetani ushindi juu ya Maisha yako, kwasababu wale malaika ambao kazi yao ni kutembea na sisi wanautazama uso wa Baba yetu mbinguni kila siku kupeleka taarifa njema juu yetu,(Mathayo 18:10) hivyo hoja zao za kutumilikisha sisi kwa Mungu zinashinda kila siku na kujikuta tunaishi Maisha ya ulinzi na amani. Hiyo yote ni kwasababu umefunga milango yote shetani kupata vijisababu vya kukushtaki…(Kwa maelezo marefu juu ya huduma za hawa malaika watakatifu unaweza ukatutumia ujumbe inbox, tutakutumia maelezo yake kwa urefu)…

Lakini unaposikia injili na huku moyoni mwako unajua kabisa ni maneno ya Mungu ya uzima, na unaidharau kwa namna moja au nyingine, basi hiyo tayari ni point kubwa sana kwa shetani kuipeleka mbele za Mungu kupata kibali cha kuyatawala Maisha yako. Wale malaika wanaokulinda wanashindwa kukutetea na kuondoka..

Hivyo ni jambo la muhimu sana na kuzingatia kuyahakiki maisha yetu kila siku, kwasababu biblia inasema shetani adui yetu ni kama simba angurumaye anazunguka huko na huko kumtafuta mtu wa ammeze..

1 Petro 5:8 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzungukazunguka, akitafuta mtu ammeze”.

Shetani hawezi kuyatawala Maisha yako ukiwa ni mtu wa unayeishi Maisha ya kumpendeza Mungu, ukiwa chini ya Damu ya mwanakondoo..Usalama wetu ni kuwa chini ya Damu ya Yesu tu , na huko sio kusema tu ‘najiweka chini ya Damu ya Yesu’..unaposema hivyo ni sawa na kusema ‘najiweka chini ya sheria za nchi’..je ukisema hivyo itakuwa na madhara yoyote?..unaona ukitaka kujiweka chini ya sheria za nchi ni kuziishi zile sheria,kuzileta kwenye Maisha yako, sio kuzitamka tu!…kadhalika kujiweka njini ya damu ya Yesu ni kuileta ile damu kwenye Maisha yako sio kuitamka tu!..kutamka kunakuja baada ya kuileta kwenye matendo hiyo damu.

Kadhalika shetani hatumnyanganyi mamlaka juu ya Maisha yetu kwa kutamka tu! (na kusema Shetani huna mamlaka juu ya Maisha yangu), hapo bado hatujamwondoa…Ili kumwondoa ni lazima tuvidhibiti vifursa vyake vyote anavyovitumia kutushitaki sisi mbele za Mungu…Na baada ya kuvifunga hivyo ndipo tunamalazia na kutamka kuwa shetani huna mamlaka yoyote juu ya Maisha yetu.

Hakuna pepo lolote linaloweza kumwingia mtu kabla halijapata kibali mbele za Mungu…Ukiona kuna roho ipo ndani yako basi jua kuna mahali mlango umeufungua maishani mwako, na hivyo shetani kapata kijisababu cha kukushitaki mbele za Mungu na kushinda.

Baadhi ya milango inayosababisha roho za mapepo kuingia ndani ya watu ni uasherati, ibada za sanamu, ushirikina, matumizi ya vipodozi na uvaaji mbaya ikiwemo mawigi, uvaaji suruali kwa wanawake, vimini, na nguo zinazobana, na upakaji wa lipstick,wanja, uvaaji hereni na uchoraji wa tattoo, utazamaji pornography, usikilizaji miziki ya kidunia ..na mambo mengine yanayofanana na hayo…

Mambo hayo ndiyo yanayoongoza kumpa shetani nafasi ya juu ya kutawala Maisha ya watu, ikiwemo kuleta magonjwa, ugomvi, shida, taabu, kukosa amani, kukosa furaha na raha pamoja na kifo.

Hivyo ukitaka kukaa mbali na shetani, suluhisho ni kutofungua mlango wowote wa kumpa shetani upenyo wa kukushtaki kwa kukaa mbali na hivyo vitu tulivyovitaja hapo juu na vingine vyote vinavyofanana na hivyo..

Kumbuka pia kukamilisha hatua zako za wokovu kama hujakamilisha, hatua hizo zipo tatu, 1)KUAMINI, 2)KUBATIZWA, na 3)KUPOKEA ROHO MTAKATIFU. Hatua hizo ni za muhimu, na pia kumbuka ubatizo sahihi ni wa kuzama mwili wote kwenye maji mengi kama neno lenyewe ubatizo linavyomaanisha, na pia ni kwa JINA LA BWANA YESU kulingana na Matendo 2:38, Na Roho Mtakatifu ni Mungu mwenyewe anakupa kwasababu ni ahadi yake aliyowaahidi wale wote wamwombao. Na hapo sasa shetani atakapojaribu kwenda kukushitaki mbele za Mungu atashindwa, kwasababu umekamilishwa ipasavyo katika wokovu.

hivyo ukiwa hujakamilisha hatua hizo bado unayo nafasi sasa, zikamilishe kabla mwisho haujafika, kwasababu tunaishi katika siku za Mwisho, muda wowote parapanda inalia na wafu watafufuliwa na sisi tulio hai tutanyakuliwa na Bwana kwenda mawinguni, Je utakuwa mmoja wao wa watakaoenda na Bwana?

Bwana akubariki sana. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

KUNDI LA MALAIKA WALETAO MABAYA.

HUDUMA YA MALAIKA WATAKATIFU.

BIBLIA INASEMA “HAMJUI YA KUWA MTAWAHUKUMU MALAIKA? (1WAKORINTHO 6:2-3)”JE! SISI TUTAWAHUKUMUJE MALAIKA?.


Rudi Nyumbani

Print this post

MWISHO WA HAO WAMSAHAUO MUNGU.

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe daima, karibu tujifunze maneno ya uzima, Kama tunavyofahamu tunaishi ukingoni kabisa mwa wakati, siku zile ambazo Bwana Yesu alisema upendo wa wengi utapoa duniani kwasababu ya kuongezeka kwa maasi (Mathayo 24:12) Ndizo tunazoishi sasa.

Sasa Upendo unaozungumziwa hapo sio tu upendo wa ndugu, bali pia upendo wa kumpenda Bwana utapoa ndani ya watu wengi.

Unakuta mtu alianza vizuri na Bwana, mwanzoni, alikuwa amesimama vizuri, anamtafuta Mungu kwa bidii, anasali, anajilinda na ulimwengu, anavaa mavazi ya heshima, na Zaidi ya yote anawahubiria wengine habari njema.. lakini kwasababu ulimwengu wasasa umebadilika, na yeye anabadilika nao, hapo mwanzo alikuwa haendi disco lakini sasa ameanza kuwa muhudhuriaji mzuri, hapo mwanzo alikuwa havai suruali na vimini lakini sasa ni mvaaji hodari, hapo mwanzo alikuwa ni mwombaji mzuri lakini sasa kasongwa na kampani za watu wa kidunia, mizunguko ya huku na kule kila kukicha haiishi, na kwasababu smartphone zimekuja sasa, utamkuta ule muda ambao angepaswa awe analiafakari Neno la Mungu nyumbani kwake na familia yake, utamkuta ana chat kwenye mitandao na katika magroup ya whatsapp hata 50 yasiyokuwa na maana, na kutazama mambo yasiyostahili mitandaoni, na pornograph.

Na hali hiyo inaendelea hivyo hivyo mpaka baadaye anajikuta kamsahau Mungu kabisa ambaye alishamwokoa zamani, anaona sasa wokovu hauna maana tena, hauna faida yoyote, ni kujinyima tu bure kusikokuwa na sababu za msingi, na hivyo anaamua kuishi maisha ya kidunia huku akidhani kuwa ndio kayapenda maisha yake kumbe ndio ameyaangamiza…Biblia inasema:

Ayubu 8:8 “Basi, uwaulize, tafadhali, vizazi vya zamani, Ujitie kuyaangalia yale baba zao waliyoyatafuta;

9 (Kwani sisi tu wa jana tu, wala hatujui neno, Kwa kuwa siku zetu duniani ni kivuli tu;)

10 Je! Hawatakufunza wao, na kukueleza, Na kutamka maneno yatokayo mioyoni mwao?

11 Je! Hayo MAFUNJO yamea pasipo matope Na MAKANGAGA kumea pasipo maji?

12 Yakiwa yakali mabichi bado, wala hayakukatwa, Hunyauka mbele ya majani mengine.

13 NDIVYO ULIVYO MWISHO WA HAO WAMSAHAUO MUNGU; Na matumaini yake huyo mbaya huangamia;

14 Uthabiti wake utavunjika, Na matumaini yake huwa ni nyuzi za buibui.

15 Ataitegemea nyumba yake, isisimame; Atashikamana nayo, isidumu.

16 Yeye huwa mti mbichi mbele ya jua, Nayo machipukizi yake huenea katika bustani yake.

17 Mizizi yake huzonga-zonga chuguu, Huangalia mahali penye mawe.

18 Lakini, aking’olewa mahali pake, Ndipo patamkana, na kusema, Mimi sikukuona.

19 Tazama, furaha ya njia yake ni hii, Na wengine watachipuka kutoka katika nchi.”

Unaona hapo mwandishi anasema, Sisi ni wa juzi tu, tuwaulize watu walitutangulia zamani, tuwaulize wakina Sulemani, n.k. je! MAFUNJO yamea pasipo matope Na MAKANGAGA kumea pasipo maji?. Mafunjo na makangaga ni aina ya mime mirefu ambayo hiyo huwa inaota sehemu za mabwawa au maziwa, sehemu zenye maji mengi, mahali pengine popote palipo na upungufu wa maji haziwezi kuota, ni sawa tu na yale magugu maji,…Na ndio hapo anauliza je! Mimea hiyo inaweza kuota katika nchi kame kama vile katani iotavyo jangwani,?…Jibu ni La!, anasema ndivyo ilivyo kwa watu wale wamsahauo Muumba wao.

Mpaka mtu amsahau Mungu, ni wazi kuwa hapo nyuma alikuwa ameshafahamiana naye, huwezi kumsahau mtu ambaye humfahamu, vivyo hivyo wanaozungumziwa hapo ni wakristo wale ambao hapo nyuma walikuwa sawa na Mungu lakini sasa wamepoa, hapo kabla walikuwa moto kwa Mungu lakini sasa wamevutwa na ulimwengu. Wala hawazungumziwi watu wasiomjua Mungu kabisa..

Mwandishi anaendelea kusema.. “Yeye huwa mti mbichi mbele ya jua,”. Ikiwa na maana kuwa mpaka huo mti umekuwa mbichi ni wazi kuwa ulishawahi kuwepo pembezoni mwa mito ya maji, lakini ghafla haupo tena katika mito bali upo mbele ya jua.. Unatazamia vipi mti huo utakuwa na maisha marefu?. Vivyo hivyo na sisi tunapomsahau Mungu katika dunia hii mbovu inayopita, siku za mwanzoni tunaweza tusione matokeo yoyote, hiyo ni kwasababu ule ubichi bado upo ndani yetu, lakini siku chache mbeleni, tutakapo kauka ghafla ndipo tutakapojua kuwa kumbe tulikosea na tutakapotaka kugeuka tumrudie yeye hatutaweza tena kwasababu tayari tulishakatwa siku nyingi.. Hata leo hii ukikuta mti mkubwa, huwezi kuona matokeo ya kukauka majani yake siku hiyo hiyo, lakini nenda rudi baada ya siku mbili, tatu ndipo uakapoona tofauti.

Zaburi 50:22 “Yafahamuni hayo, Ninyi mnaomsahau Mungu, Nisije nikawararueni, Asipatikane mwenye kuwaponya.”

Katika nyakati hizi za hatari njia pekee ya kuishi maisha ya kutokumsahau Mungu ni kuhakikisha, kwanza kila siku unalitafakari Neno la Mungu, sio kusoma tu, hapana bali kutenga muda wa kutosha kulitafakari Neno, wengi wanaishia katika kusoma tu kama vile kitabu halafu basi, hiyo haikuongezei chochote, ni sawa na umetengewa sahani ya ugali, lakini ule ugali wote hauwezi kwenda tumboni moja kwa moja kama usipopitia kinywani, utafunwe, uvunjwe vunjwe na meno kisha uingie kidogo kidogo mpaka wote uishe, vivyo hivyo, ukiwa na pupa ya kulisoma Neno la Mungu kama kitabu tu ama gazeti, kama kutimiza wajibu Fulani ulioambiwa na mhubiri Fulani…

kisha kwenda kulala, litakuboa tu, na hutapata jambo jipya ndani yake, utaona kuna mambo magumu, hayaeleweki, lakini kwanza ukichukua muda kusali na kumwomba Roho Mtakatifu akusaidie, kisha ukatafakari lile unalolisoma hata kama ni mstari mmoja kwa muda mrefu ukililinganisha na maisha yako kisha, ukaweka mipango ya kulitendea kazi, basi lile Neno la Mungu litakuwa na manufaa makubwa sana kwako. Hatuhesabiwi haki kwa kumaliza kuisoma biblia yote, bali kwa kuielewa..

Kumbukumbu 8:11 “Jihadhari, usije ukamsahau Bwana, Mungu wako, kwa kutozishika amri zake, na hukumu zake, na sheria zake, ninazokuamuru leo”.

Pili, jenga desturi ya kuhudhuria ibadani, ukutane na waaminio wenzako, kaa na ndugu ambao ni wakristo wenzako wenyewe nia ya kwenda mbinguni pamoja na wewe, tafuta marafiki wenye faida za kimbinguni..Chuma hunoa chuma, lakini kama muda wako wote utakaa na marafiki wa kidunia ambao hao wakati wote hata habari na Mungu hawana, na wewe uliyempokea Kristo unaendelea kukaa nao, ipo dalili kubwa sana ya kumsahau Mungu.

Na mwisho kuwa mtu wa maombi. Ukizingatia vigezo hivyo ni ngumu kujikuta umerudi nyuma kwa sababu yoyote ile. Kumbuka nyakati hizi ndio zile nyakati za hatari sana ambazo zilitabiriwa kuwa watu watakuwa wa kupenda sana anasa kuliko kumpenda Mungu..Hivyo tunaaswa kuwa makini sana katika safari yetu ya wokovu.

Waefeso 5:15 “Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima;

16 mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu.

17 Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana.

18 Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho;

19 mkisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu;

20 na kumshukuru Mungu Baba sikuzote kwa mambo yote, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo;

21 hali mnanyenyekeana katika kicho cha Kristo.”

Bwana akubariki sana. Tafadhali “Share” Ujumbe huu kwa wengine. Na Bwana atakubariki. Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group


Mada Zinazoendana:

NINI MAANA YA KUISHI KWA KUUKOMBOA WAKATI?

MKUMBUKE MKE WA LUTU.

ZIKUMBUKE FADHILI ZA MUNGU


Rudi Nyumbani

Print this post

ALIFANYIKA SADAKA KWA AJILI YETU!


Unapomwona maskini na kumhurumia na kuamua kumsaidia kwa kile alichopungukiwa, na kuifanya huzuni yake iondoke, hapo ni sawa na umeichukua huzuni yake, unapokutana na mtu ambaye hana chakula kabisa na ukaamuhurumia na kuamua kumpa kile chakula kidogo ulichokuwa nacho wewe ambacho ungepaswa ukile wewe, hapo ni sawa umeichukua njaa yake na kujitwika juu yako,Unapomwona mtu anakwenda kufa na wewe ukajitoa kufa kwa niaba yake, hapo ni sawa na umeichukua mauti yake.

Na kwetu sisi wanadamu ndio hivyo hivyo, kwa dhambi zetu tulistahili kufa, tulistahili kupotea kabisa lakini alitokea mmoja aliyetuhurumia ambaye hakustahili kufa, hakustahili kupotea, hakustahili kuadhibiwa akachukua hayo matatizo yetu yote na kujitwika juu yetu ili sisi tuwe huru..

Ndio hapo ili kwamba sisi tusife hana budi yeye kufa kwa niaba yetu, ili kwamba sisi tusiadhibiwe hana budi yeye kuadhibiwa kwa niaba yetu na hiyo yote ni kutokana tu na huruma yake kwetu sisi..


2 Wakorintho 8:9 “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake”.

Ili kwamba upande mmoja uwe na vingi na lazima upande mwingine upungukiwe, ili kwamba sisi tupone ni lazima mmoja aangamie, hiyo ndiyo sababu Bwana Yesu Kristo alikufa kwa ajili yetu ili kwamba sisi tupate uzima wa milele…kulikuwa hakuna njia nyingine ya mkato ya sisi kuokolewa bila ya njia hiyo ya mmoja kuchukua matatizo ya mwingine…hata mahakamani pasipopatikana mdhamini hakuna kuachiwa huru..Ndio maana Biblia inasema..

Yohana 1:29 “Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu!”.


Na kama alichukua matatizo yetu na kujitwika juu yake ni dhahiri kuwa kwa hali ya kawaida asingepaswa kufufuka tena, kwasababu makosa yetu sisi yalistahili adhabu ya milele…Lakini SIRI iliyopo kubwa hapo ni kwamba, Kristo alifufuka tena, kwa ukamilifu wake alisimama na kushinda hoja! Hivyo mauti ikashindwa juu yake, kuzimu ikashindwa juu yake, na hivyo akavishinda vyote na kufufuka bila dhambi yoyote..Hatia yote aliishinda.

Waebrania 9:28 “Kadhalika Kristo naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu”.

Ni sawa na wewe ukutwe na makosa fulani yanayostahili kufungwa kifungo cha maisha, halafu atokee mtu na kuichukua kesi yako wewe na ashtakiwe kwa kupandishwa kizimbani kabisa na ahukumiwe na kufungwa, na kisha baada ya siku chache unamwona mtaani yupo huru, anakwambia kesi imekwisha! Wote tupo huru wala usiwe na wasiwasi… Lazima utajiuliza ni nini kimetokea?..aidha katoroka gerezani au labda kesi yake imerudiwa kusikilizwa tena na ikatokea kashinda hoja? Yatakuwepo maswali mengi yasiyo na majibu!..Na zaidi ya yote huyo kukuondolea wasiwasi anakwambia nimekabidhiwa UJAJI MKUU wa Taifa lote, hukumu zote zipo chini yake na wafungwa wote wapo chini yake.

Na ndicho kilichotokea kwa Bwana Wetu Yesu Kristo, alijitwika kesi yetu na kuhukumiwa kufa, ambapo sisi ndio tungestahili kufa lakini baada ya siku chache, alifufuka na kutoka kaburini na kuwaambia wanafunzi wake…Mathayo 28:18 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani”.

Bwana Yesu kwasasa ndiye aliye mhukumu wa watu wote walio hai na waliokufa..

Matendo 10:40 “Huyo Mungu alimfufua siku ya tatu, akamjalia kudhihirika,

41 si kwa watu wote, bali kwa mashahidi waliokuwa wamekwisha kuchaguliwa na Mungu, ndio sisi, tuliokula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu.

42 Akatuagiza tuwahubiri watu na kushuhudia ya kuwa huyu ndiye aliyeamriwa na Mungu awe Mhukumu wa walio hai na wafu”.

Lakini Neema hiyo Kristo aliyoibeba sio kwa watu wote!..Ni kwanini sio kwa watu wote? Ni kwasababu sio watu wote watapenda au watataka wokovu, wengine hawatataka kuokolewa, hivyo haiwezekani kuwalazimisha..Kila mtu Mungu kampa uhuru wa kuchagua apendalo, UZIMA au MAUTI.

Kumbukumbu 30: 15 “Angalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya;”

Yesu ndio Nuru ya ulimwengu, chagua Nuru leo ambao ndio UZIMA, na si giza..Kwasababu wengi katika siku hizi za mwisho watachagua giza na wala si Nuru kwa hiari yao wenyewe..kama maandiko yanavyosema.

Yohana 3: 18 “Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. 

19 Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. 

20 Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa”.

Kama hujasalimisha maisha yako kwake ni vyema ukafanya hivyo leo kwa kutubu dhambi zako zote kwa kudhamiria kutokurudia kuzifanya tena, na kutafuta ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Bwana Yesu Kristo, kwaajili ya ondoleo la dhambi zako(sawasawa na Matendo 2:38 inavyosema).na Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake mtakatifu atakayekusaidia kushinda dhambi.

Kwa kufanya hivyo utakuwa umeutua mzigo wako wa dhambi na Bwana Yesu atakuwa amekuingiza miongoni mwa wale waliochukuliwa dhambi zao na hivyo utakuwa umenusurika na hukumu ya Mungu itakayoijilia ulimwengu wote kipindi sio kirefu kijacho..

Bwana akubariki sana.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

SADAKA ILIYOKUBALIKA.

MWILI NA DAMU YA YESU KRISTO.

TOFAUTI KATIKA YA ZAKA NA SADAKA NI IPI?


Rudi Nyumbani

 

 

Print this post

MAVAZI YA NDANI NA YA NJE.

Madhabahu zote wana wa Israeli walizomjengea Mungu ilikuwa ni lazima wazijenge katika mahali pa juu, hivyo ndivyo walivyoagizwa na Mungu, mahali ambapo pameinuka, au waiinue madhabahu yenyewe juu,..kwasababu maana ya neno lenyewe madhabahu ni ‘”palipo inuka”, hakukuwa na nama yoyote madhabahu ikajengwa bondeni, au shimoni na Mungu alifanya hivyo makusudi kufunua mambo makubwa kiroho, jambo hilo hilo hata wapagani baadaye walikuja kuliiga, nao pia madhabahu zao wakawa wanazijenga sehemu za juu, au wanazinyanyua juu, na ndio maana utasoma kwenye biblia sehemu nyingi wakati wa enzi za wafalme, Bwana anawakemea wayahudi kwa makosa yao ya kutokuziondoa sehemu za juu,..akiwa na maana ya madhabahu zao za sanamu walizozijijengea kwa uchawi wao, Shetani siku zote ni mwigaji, hakuna jambo jipya alilowahi kulibuni yeye mwenyewe, alipomuona Mungu anawaagiza wana wa Israeli watoe kafara za wanyama kwa ajili ya upatanisho wa dhambi zao, yeye naye akaiga mambo hayo hayo, na ndivyo ilivyokuwa hata katika madhabahu zake.

Sasa wakati madhabahu ilipojengwa na kunyanyuliwa juu, mtu yeyote atakayeiendea ambaye ni kuhani alipewa masharti ya kuiendea na mavazi rasmi ya kuvaa. Kuhani mkuu au kuhani yoyote ilikuwa ni lazima avae mavazi ya kumsitiri mwili wake wote, hivyo ziliandaliwa kanzu nzuri za kitani, ndefu, ambazo mtu akivaa hizo zilimsitiri mwili wake wote, lakini hiyo peke yake haikutosha kumsitiri mtu maeneo yote, kwani wakati wa kuiendea madhabahu ambayo imenyanyuliwa ni lazima utapandisha ngazi ili kuifikia juu, na hivyo kanzu kwa upande wa chini huwa haisitiri, kunakuwa wazi, na ilikuwa mfano uchi wao ukionekana tu madhabahuni pa Mungu ilikuwa ni mauti, Mungu mwenyewe anakuua.

Kutoka 20:26 “Tena hutapanda kwenda madhabahuni kwangu kwa daraja, uchi wako usidhihirike juu yake.”

Hivyo kutatua tatizo hilo, Bwana akawapa makuhani wake wote amri kuwa watengenezewe suruali ambazo watazivaa kwa ndani ili kusudi kwamba watakapopanda kwenda madhabahuni, uchi wao usionekane kwa chini, wawe salama.


Kutoka 28:39 “Na hiyo kanzu utaifuma ya kitani nzuri ya kazi ya urembo, ufanye na kilemba cha nguo ya kitani nzuri, nawe utafanya mshipi wa kazi ya mwenye kutia taraza. 

40 Kisha utafanya kanzu kwa ajili ya wana wa Haruni, nawe wafanyie mishipi, wafanyie na kofia kwa utukufu na uzuri. 

41 Nawe mvike huyo nduguyo Haruni na wanawe nao mavazi hayo; nawe watie mafuta, na kuwaweka kwa kazi takatifu, na kuwatakasa, ili wapate kunitumikia mimi katika kazi ya ukuhani. 

42 Nawe wafanyie suruali za nguo ya kitani, ili kufunika tupu ya miili yao; suruali hizo zitafika tangu kiunoni hata mapajani;43 na Haruni na wanawe watazivaa, hapo watakapoingia katika hema ya kukutania, au hapo watakapoikaribia madhabahu ili watumike katika mahali patakatifu; wasije wakachukua uovu, wakafa; hii itakuwa ni amri ya milele kwake yeye, na kwa wazao wake.”

Lakini tunapaswa tujiulize mambo haya yanafunua nini katika agano jipya?. Jambo la kwanza ni kwamba Madhabahu ya Mungu tunayomwabudia katika Roho imenyanyuka sana tena imenyanyuka juu kuliko hata ya akina Haruni nayo ipo mbinguni na sadaka yake juu yake, ambayo ni Bwana wetu Yesu Kristo, Vyote hivi vipo mbinguni.

Hivyo tunapokwenda mbele ya madhabahu hii, kupeleka mahitaji yetu, au kumfanyia Mungu ibada, tunapaswa tuwe makini sana, kwanza tunapaswa tuwe tumesitiriwa sio tu kwa mavazi ya nje, bali pia na kwa yale ya ndani vinginevyo tunaweza tukajiona tupo sawa lakini kumbe tunajitafutia kifo, badala ya uzima.

Mavazi ya nje ni yapi?. Ni mwonekano wako wote wa nje kwa ujumla,.Ikiwa leo hii unaweza kutembea barabarani na vimini wewe kama mwanamke na suruali na nguo zinazochora maungo yako..na kibaya Zaidi huoni hata aibu kuingia nazo katika nyumba ya ibada, madhabahuni pa Mungu na mavazi hayo ni dalili kubwa ya kujichumilia mauti. Vile vile unakuwa mlevi, na bado unakwenda mbele za Mungu, huko ni kujitafutia kifo ndugu, kama umeamua kuwa baridi ni heri ukawa baridi kwelikweli, kuliko kuwa vuguvugu.

Mtume Petro wakati anavua akiwa nusu uchi, Bwana alipotokea alijitupa kwenye maji kuficha uchi wake, kwasababu ya kumheshimu Bwana, na yeye alikuwa ni mwanamume…

itakuwaje kwako wewe mwanamke! Mbele ya Bwana? Unafikiri unapaswa ujisitiri kiasi gani?

Vilevile mavazi ya ndani, ni mambo yaliyo moyoni mwako, mambo ambayo kwa nje hayawezi kuonekana lakini kwa ndani hayaelezeki kwa jinsi yalivyo mabaya, mfano wa wale mafarisayo na waandishi Bwana Yesu aliowazungumzia..

Mathayo 23:28 “Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi”.

Ndani unayo chuki na watu, unao wivu, ndani umewawekea wengine vinyongo na vikwazo, ndani umeweka kisasi halafu bado unapanda madhabahuni pa Mungu kwenda kumwomba, au kumfanyia ibada, hapo ni sawa na kuhani aliyevaa kitani nzuri ndefu ambayo kwa nje unaonekana kweli wewe ni mwema lakini mbele za Mungu upo uchi..

Hiyo ni mbaya sana, unatazama pornography kwa siri, unazini kwa siri kwasababu wanakwaya wenzako hawajakuona unadhani pia Mungu hakuoni, unakwenda disco kisirisiri, lakini huku nyuma unakwenda kumwimbia Mungu na kumwabudu..Nataka nikuambie ni heri usifanye kabisa au utubu uamue kumwishia Mungu.

Fahamu kuwa kanisa hili tunaloishi ndilo kanisa la saba lijulikanalo kama kanisa la Laodikia, na ndio la mwisho, na kama huufahamu ujumbe wa kanisa hilo unaweza kusoma katika Ufunuo 3:14-21 uone kama tabia zinazozungumziwa pale haziendani na ukristo uliopo sasa?. Hili ni kanisa vuguvugu, ambalo linajiona kuwa Tajiri lakini ni uchi, maskini na dhaifu..

Ufunuo 3:14 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu. 

15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.

 16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.

17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi. 

18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.

 19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.

 20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami. 

21 Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi. 

22 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa”

Unaona hapo? Bwana anatupa shauri tununue kwake mavazi meupe aibu ya uchi wetu isipate kuonekana, “kumbuka huo ni ushauri sio lazima”..na mavazi hayo anayoyazungumzia ni yale ya nje na ya ndani. Ndugu usipumbazwe na mambo mengi maovu unayoyaona sasahivi ulimwenguni. Yalitabiriwa yatakuwa hivyo na kuzidi kuongozeka katika siku za mwisho,. Lakini pia Bwana alituahidia sisi wa kanisa la Mwisho la Laodikia thawabu kubwa kuliko makanisa mengine yote yaliyotutangulia ikiwa tutashinda.

Tafakari aliposema tutaketi pamoja naye Mfalme wa wafalme, Bwana wa Mabwana Yesu Kristo katika Enzi yake, hilo sio jambo dogo. Hivyo kwa mtu yoyote mwenye akili timamu atayahesabia Maisha haya ya kitambo tu kuwa si kitu cha kulinganisha na thawabu hizo zinazokuja.

Hivyo ndugu, ikiwa bado upo nje ya Kristo, Usiipuzie hii neema iliyopo sasa. Tubu kwa kumaanisha kabisa kuacha dhambi, kisha uende ukabatizwe kulingana na maandiko kwa kuzamishwa katika maji mengi kwa jina la BWANA YESU ukapate ondoleo la dhambi zako, na Bwana atakupa kipawa cha Roho mtakatifu (Matendo 2:38).

Bwana yupo mlangoni kurudi, naye mwenyewe anasema anakuja upesi! Na wala hatakawia.

Ubarikiwe sana. 

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

MAVAZI YAPASAY KUVALIWA NA WANAWAKE NI YAPI?

JE! NI DHAMBI KWA KIJANA ALIYEOKOKA KUVAA SURUALI ZA KUBANA (MODEL), KUNYOA MITINDO?


Rudi Nyumbani


Print this post

UNALITUMIA KWA HALALI NENO LA KWELI?.

Unaweza ukawa ni mchungaji mzuri,au mwalimu mzuri wa Neno la Mungu, unaweza ukawa una mafunuo mengi na kufahamu mambo mengi, lakini je! Katika huduma yako au utumishi wako unalitumia kwa halali Neno la kweli?. Mtume Paulo alimwambia Timotheo Hata mtu akishindana katika machezo hapewi taji, asiposhindana kwa halali.(2Timotheo 2:5). Unaona? tuchukulie mfano wanariadha, ikiwa mtu atatumia dawa za kusisimua misuli ili awe na pumzi zaidi ya wengine pale atakapokimbia, ni kweli anaweza akawa mshindi lakini hatapewa taji pale atakapobainika kafanya hila katika huo mchezo, kwasababu hajashiriki kwa halali katika michezo, au ikiwa mtu ataanza kukikimbia kabla ya kipenga kupigwa, huyo naye atatolewa katika mashindano kwasababu hajashiriki kihalali katika michezo, vilevile ikiwa waliagizwa wazunguke uwanja mara 10, lakini akatokea mmojawapo kakaidi amri na kukatisha katikati ya uwanja..Tunajua ni kitu gani kitakachofuata, bila shaka atapigwa Penalti na atatolewa katika mashindano hata kama ilikuwa imebaki mzunguko mmoja amalizie na ushindi, hiyo yote ni kwasababu hajashiriki kihalali.…

Vivyo hivyo katika mienendo yetu tunapolipeleka Neno la Mungu tusipojifunza Kulitumia kihalali, tunaweza tukajikuta katika hasara na tabu yetu mwisho wa siku inakuwa ni bure. 

Na ndio maana mbeleni kidogo Paulo aliendelea kumsisitiza Timotheo maneno haya:

2Timotheo 2:15 “Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, UKITUMIA KWA HALALI NENO LA KWELI”

Unaona, anamsihi ajionyeshe kuwa amekubaliwa na Mungu, ajionyeshe kuwa amekomaa katika mashindano ya wokovu, sio mtu atakayeleta aibu mbeleni kwa kushindwa kumaliza ungwe yake vizuri, na ndio tafsiri ya hilo Neno “mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari,” …kutahayari maana yake ni ‘kuabisha’

DALILI IPI ZITAKUTAMBULISHA KUWA HAUTUMII KWA HALALI NENO LA KWELI?

Sababu kuu Paulo ambayo aliitoa pale ni “Mashindano ya Maneno”.

2 Timotheo 2:14 “Uwakumbushe mambo hayo, ukiwaonya machoni pa Mungu, wasiwe na mashindano ya maneno, ambayo hayana faida, bali huwaharibu wasikiao.

15 Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, UKITUMIA KWA HALALI NENO LA KWELI.

16 Jiepushe na maneno yasiyo na maana, ambayo si ya dini; kwa kuwa wataendelea zaidi katika maovu,

17 na neno lao litaenea kama donda-ndugu. Miongoni mwa hao wamo Himenayo na Fileto,

18 walioikosa ile kweli, wakisema ya kwamba kiyama imekwisha kuwapo, hata kuipindua imani ya watu kadha wa kadha”.

Unaona?, sio hapo tu, sehemu nyingi sana Mtume Paulo alikuwa anamwonya Timotheo ajiepusha na mashindano ya maneno, ambayo madhara yake ni kama donda-ndugu. Donda-ndugu ni kidonda sugu kisichopona, kinakwenda miezi na miezi, miaka na miaka, hata kitibiweje hakitibiki, njia pekee ya kukiondoa ni kukata kile kiungo au lile Eneo. Sasa hiyo imefananishwa na mashindano ya maneno kwa watu wa Mungu, kwa jinsi mtu anavyojizoesha katika hali hiyo ndivyo anavyojiharibu nafsi yake kidogo kidogo, mpaka mwisho wa siku anajikuta anagota katika itikadi Fulani ya kidini ambayo hawezi tena kubadilika hata kama ni ya uongo, anabakia kuwa ni mtu wa mijibizano tu na mashindano ya itikadi zake siku zote, na ndio watu kama hao mwisho wa siku wanazama katika mafundisho potofu ambapo kuwatoa huko haiwezekani tena….

Mungu hakai katika mashindano, ikiwa mtu kakusudiwa kuamini ataamini, kama haamini, hawezi kuamini, pengine sio wakati wake huo. Ndugu ikiwa umepewa neema ya kuwa mhubiri wa injili basi usitumie karama yako kuwa mtu wa mashindano, hayo hayawezi kumjenga mtu zaidi yanamuharibu tu Yule asikiaye, ‘tutumie kwa halali Neno la kweli’,..Tudumu katika mfundisho ya Neno la Mungu..

Leo utaona kuna mijadala baina ya wa-kristo na waislamu, tazama kwa makini uone kama kuna mtu yeyote anajegwa au anavutwa kwa Kristo kwa malumbano yale..kinyume chake unazaliwa ugomvi, matusi na mizaha, hata wale ambao walikuwa wanaonyesha dalili za kuja kwa Kristo, wakiona machafuko yale ndio wana-kwenda mbali zaidi, hiyo yote ni kwasababu hatulitumii kwa halali Neno la Kweli, na hivyo mbele za Mungu tunatapanya badala ya kukusanya. 

Na ndio maana Mtume Paulo bado alikuwa anaendelea kumsihi Timotheo, tusome:

2Timotheo 2:23 “Walakini uyakatae maswali ya upumbavu yasiyo na elimu, ukijua ya kuwa huzaa magomvi.

24 Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu;

25 akiwaonya kwa upole wao washindanao naye, ili kama ikiwezekana, Mungu awape kutubu na kuijua kweli;

26 wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa naye, hata kuyafanya mapenzi yake.”

Hivyo Sisi ndio Timotheo wa sasa tukubali maonyo haya ya mitume, tukapokee taji bora lililowekwa mbele yetu.

Bwana akubariki sana.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

TUZO UTAPEWA KULINGANA NA NAFASI YAKO

TUNAPOSEMA TUISHI KWA NENO, INAMAANISHA TUISHI MAISHA YA NAMNA GANI?

MANENO YA MUNGU YANAPINDULIWAJE?


Rudi Nyumbani

Print this post

HATA ILIPOTIMIA SIKU YA PENTEKOSTE.

Matendo 2:1 “Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja.

2 Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi.

3 Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.

4 Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.

5 Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu.

6 Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe.

7 Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya?

8 Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo?

9 Warparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia”,

10 Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu,

11 Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.

12 Wakashangaa wote wakaingiwa na shaka, wakiambiana, Maana yake nini mambo haya?

13 Wengine walidhihaki, wakisema, wamelewa kwa mvinyo mpya”.

Hata ilipotimia siku ya Pentekoste!!…Sentensi hiyo inaonyesha ni kama vile siku hiyo tayari ilikuwa imepangwa…na hivyo ni kama vile ilikuwa inangojewa ifike…ni sawa na mtu aseme… “hata ilipotimia siku ya kufikishwa kizimbani” au “hata ilipotimia siku ya kufanya kufanya mtihani”…sentensi hizo zinaonesha kuwa kuna tarehe Fulani zilizokuwa zimepangwa kwa tukio Fulani…Biblia inazidi kusema kuwa “walikuwako wote mahali pamoja”..kuashiria kuwa walishaambiwa wasisambaratike bali wakae pamoja mpaka hiyo siku ifike.

Mstari wa pili unasema 2 Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi”.

Uvumi uliotokea hapo sio uvumi wa upepo huu wa asili tunaoujua, ambapo ukitokea miti inapepesuka, mapazi yanapeperuka n.k bali ni uvumi wa upepo wa roho, ambao ili kuulezea vizuri biblia imefananisha na kama uvumi wa upepo wa kawaida wa asili…ndio maana hapo biblia inasema UVUMI KAMA, Zingatia hilo neno ‘kama’ ikiwa na maana sio upepo wa kawaida bali ni mwingine wa Roho

Sasa huu ni upepo wa Roho ambao hauwezi kuonekana kwa macho, kazi yake ni kumpeleka mtu mahali ambapo hajataka kwenda kwa nguvu zake mwenyewe, au hajataka kufanya kwa nguvu zake mwenyewe au kutamka kwa akili zake mwenyewe…Huu ndio Bwana Yesu aliosema mahali Fulani kuwa mtu aliyezaliwa mara ya pili anakuwa nao..

Yohana 3:8 “Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho”. 

Unaona kila mtu aliyezaliwa kwa Roho Mtakatifu kuna upepo Fulani wa Roho unaompeleka mahali asipopachagua yeye…Kwa urefu juu ya somo hili la upepo wa Roho, unaweza kulisoma mwisho kabisa mwa somo hili.

Sasa uvumi huu wa Upepo wa Roho ulipowashukia hawa watu siku ile ya Pentekoste ni nini kiliwatokea?..Tusome

Mstari unaofuata unasema….. “3 Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.

4 Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka”.

Ni wazi kuwa upepo ule ungewasukuma kuzungumza kitu ambacho hawajataka kuzungumza kwa akili zao, kingewafanya waende mahali ambapo hawajataka kwenda kwa akili zao, kama tu vile upepo wa kawaida unapovuma mahali unaweza hata kuezua mabati na kuwahamisha watu kuwatupa mahali ambapo hawajataka kwenda..

Na ndicho kilichotokea hapa, wote wakajikuta wanaanza kuzungumza lugha ambazo kwa akili zao hawajataka kuzizingumza bali wamesukumwa kuzizungumza.

Na biblia inasema kukawatokea “ndimi”…ndimi ni wingi wa neno “ULIMI”..Na ulimi tafsiri yake iliyotumika hapo sio ulimi tunaotumia kula, bali “LUGHA”…Kwahiyo hapo ziliwashukia ‘lugha’…Sasa swali ni je! Ni lugha moja? Au ngapi?…Jibu lipo hapo hapo..’ ‘zikawatokea ndimi zilizogawanyikana’….yaani ziliwatokea lugha zilizogawanyikana…sio lugha moja…bali nyingi, na kila mtu iliyomshukia ilikuwa na tofauti na ya mwenzake…Ni kama tu kilichotokea pale Babeli, kila mtu alijikuta anaongea lugha yake…

Na biblia inasema wote wakaanza kuzungumza kwa lugha mpya, kila mmoja ya kwake tofauti na mwingine, kwa jinsi Roho alivyowajalia..ikiwa na maana kuwa si kwa jinsi ya akili zao bali kwa jinsi Roho alivyowajalia.

Na pia kumbuka Ndimi zilizowatokea zilikuwa ni ndimi za Moto, yaani lugha za moto!..Lugha za moto ni tofauti na lugha za kawaida.

Lugha za moto au ndimi za moto ni lugha ambazo mtu aliyejawa na Roho Mtakatifu anazizungumza ambazo zimejaa Neno la Mungu linalochoma nafsi ya Mtu anayesikia na kumfanya atubu au aache uovu anaoufanya…Na lugha hizi za moto/ndimi za moto hazipo tu kwa wahubiri wanaozungumza kwa njia ya maneno, bali hata kwa waimbaji wanaoimba nyimbo zinazowabadilisha watu wanaosikia na zinazomtukuza Mungu, hizo ndio lugha za moto au ndimi za Moto ambazo pia ziliwatokea hawa watu siku ya Pentekoste.

Kama walikuwa watu 120, pale walipokusanyika, upepo wa Roho uliposhuka, lugha 120 zilitokea pale pale, labda ingekuwa ni nyakati hizi, zingesikika lugha 120 tofauti tofauti watu wale wakizizungumza, kama ni kiingereza, kichina, kimasai, Kiswahili, kimakonde, kifaransa n.k

Na maneno waliyokuwa wanazungumza yalikuwa ni maneno ya kumtukuza Mungu katika hizo lugha walizokuwa wanazungumza, labda mmoja alikuwa anasema…’ ‘wewe Bwana unaweza kwa lugha ya kichina’…mwingine ‘tubuni ufalme wa Mungu umekaribia kwa lugha ya kifaransa’…labda mwingine tena akasikika akisema ‘utukufu una wewe ee Mungu wa miungu kwa lugha ya kiswahili’ n.k

Sasa Yerusalemu kipindi hicho kulikuwa na watu kutoka duniani kote waliokuwa wanakuja kuabudu, kila mmoja akasikia watu wanazungumza kwa lugha ya walikotokea, wakashangaa sana…Ni sawa leo uende kijiji cha china huko katikati kabisa halafu usikie mtu mchina anamsifu Mungu kwa lugha ya kwenu ya kihaya? Lazima utashangaa huyo mtu kajuaje hiyo lugha na hali yeye ni mchina na hajawahi kufika Tanzania na wala hawajui watanzania…Ndicho kilichotokea pale siku ya Pentekoste…watu kutoka kila kona walisikia lugha zao zikizungumzwa Yerusalemu na watu waliojazwa Roho….Na watu kuona hiyo ishara ikawaogopesha sana! Wakawaendea na kuwauliza maana ya mambo hayo ni nini? Ndipo wale waliojazwa na Roho na kusukumwa na upepo wa Roho na kuanza kusema kwa ndimi za moto wakawaambia…

Matendo 2:37 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?

38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.

40 Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi’’.

Unaona maana ya kunena kwa lugha mpya?..sio haya machafuko ambayo tunayaona sasahivi, watu wanazungumza maneno yasiyojulikana na hakuna mtu wa kutafsiri, Roho Mtakatifu hayupo hivyo! Mmoja anaponena lazima wawepo wafasiri anayesikia kile kilichonenwa,kama hapa siku ya pentekoste watu waliokuwa nje walisikia lugha zao za asili hao tayari walikuwa ni wafasiri…sasa endapo wangesikia watu wanazungumza lugha zisizoeleweka na kisha hakuna mtu wa kuwafasiria wangevutwaje kwa Kristo?

Ndugu, ndimi hizi za moto..bado zinapita sasa..Unaposikia injili na unaona unakuchoma ndani ya moyo wako na kukuvuta utubu! Fahamu kuwa ni Roho Mtakatifu anakuvuta kwake…anataka ugeuke uache dhambi na anasa, na mabaya yako yote, akuoshe kwa damu yake.

Biblia inasema hao watu baada ya kuchomwa mioyo yao? Wakawauliza mitume wafanyaje?!…Pengine na wewe una swali hilo hilo leo?…Nifanyaje?..Jibu lipo hapo hapo kwenye biblia mstari unaofuata..

“Tubu ukabatizwe kwa jina lake Yesu Kristo, upate ondoleo la dhambi”..

Hivyo hapo ulipo tenga dakika chache peke yako, tubia dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha kabisa…unakusudia kuacha uasherati kama ulikuwa unaufanya, rushwa, utukanaji, ukahaba, wizi, ulevi, anasa, ushoga, ulawiti, uuaji, usagaji, utazamaji pornograph, ufanyaji masturbation, n.k na kisha katafute ubatizo sahihi, wa kimaandiko kama ulivyoyasoma hapo juu, ubatizo sahihi ni wa kuzama mwili wote kwenye maji na kwa jina la BWANA YESU huo utakufanya umpe Roho Mtakatifu kibali cha kufanya kazi ndani yako..kwa kufanya hivyo utakuwa umetimiza matakwa yote ya Mungu anayotaka juu ya maisha yako..na kujiweka katika mstari mzuri wa kwenda mbinguni.

Bwana akubariki sana.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

UPEPO WA ROHO.

JE! KUNENA KWA LUGHA MPYA KUKOJE?

JE! NI LAZIMA WATU WOTE WANENE KWA LUGHA?

MBINGUNI NI WAPI?

KUWA MAKINI NA MITANDAO, NI SHIMO REFU.


Rudi Nyumbani

Print this post

NJAA ILIYOPO SASA.

Kama vile wema na fadhili zake hazikomi kutufuata siku zote za maisha yetu basi na Jina la Bwana wetu Yesu Kristo lizidi kubarikiwa daima, Milele na milele.Amina. Karibu tujifunze maneno ya uzima.

Kama wanavyosema ni heri mtu ufe kwa kupigwa rasasi kichwani ambapo ndani ya sekunde chache tu unajua utakuwa umeshaondoka kuliko kufa kwa njaa, kufa kwa kukosa maji au chakula, kwani kifo cha namna hiyo huwa ni cha taratibu na cha mateso ya muda mrefu,.

Biblia yenyewe inakubaliana na hayo maneno tukisoma katika

Maombolezo 4:9 “Heri wale waliouawa kwa upanga Kuliko wao waliouawa kwa njaa; Maana hao husinyaa, wakichomwa Kwa kukosa matunda ya mashamba.’’

Unaona na hiyo sio katika mwili tu, bali pia ipo katika Roho ni heri  wale watu ambao Mungu alishawauwa kiroho siku nyingi, kuliko wale watu ambao bado wapo hai, wana hangaika huku na huko kutafuta chakula cha rohoni lakini hawakipati, watu wa namna hiyo kifo chao cha kiroho kinakuwa ni kibaya sana na cha mateso mengi..

Mwanzoni mwa mwaka wa 2007 nikiwa mimi pamoja na ndugu wengine 5,Mungu alituambia waziwazi kwa unabii kuwa kuna kipindi cha ukame kinapita duniani kote, Kwa wakati huo sikujua ni kwa namna gani njaa itakuja nilidhani Neno la Mungu litakuwa halihubiriwi kabisa, Kumbe sivyo.

Sikuzote ili kujipima kama upo katika njaa au haupo, ni uwezo wa kutambua ubora wa chakula unachokula, jaribu kufanya uchunguzi kaa siku moja bila kula kuanzia asubuhi mpaka jioni halafu uletewe maharage ya juzi uambiwe ule, nakuambia utauona ni mtamu kweli, lakini subiri njaa ile iwe imeshapoa halafu uletewe maharage yale yale ule, moja kwa moja utaanza kuona kasoro nyingi zilizopo katika yale maharage ambazo hapo mwanzo hukuziona, pengine utasema maharage gani haya hayana ladha, hajaungwa vizuri kwanza yamechacha, na yamezidi chumvi hayafai kuliwa yataniletea kiungulia..

Husemi hivyo kwasababu ya dharau ya shibe hapana lakini unazungumza ukweli wake kuwa sio bora, Sasa hapo ni kwasababu ile Njaa mwanzoni ilikudanganya hata kwa vitu visivyokuwa na manufaa kwa mwili wako kuviona vinafaa. Biblia inasema:

Mithali 27:7 “Nafsi iliyoshiba hukinai sega la asali; Bali nafsi yenye njaa huona kila kitu kichungu kuwa kitamu.”

Ndivyo ilivyo katika hizi siku ambazo kila mtu anajua kuwa ni za mwisho, Mungu alisema ataleta njaa duniani kote, si njaa ya kukosa chakula cha kimwili, bali njaa ya watu kukosa kuyasikia maneno yake..

Amosi 8:11 “Angalia, siku zinakuja, asema Bwana MUNGU, ambazo nitaleta njaa katika nchi; si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya Bwana.

12 Nao watatanga-tanga toka bahari hata bahari; na toka upande wa kaskazi hata upande wa mashariki; watapiga mbio, wakienda huko na huko, kulitafuta neno la Bwana, wasilione.

13 Siku hiyo wanawali wazuri na wavulana watazimia kwa kiu.

14 Na hao waapao kwa dhambi ya Samaria, na kusema, Kama aishivyo Mungu wako, Ee Dani, na, Kama iishivyo njia ya Beer-sheba, hao nao wataanguka, wasiinuke tena.”

Sababu hiyo basi njaa hiyo inawatafuna watu leo hii kiasi cha kufikia hatua ya kuoana hata yale mafundisho manyonge kuwa ni yenye nguvu..yale mafundisho ya uongo kuwa ni ya kweli.

Kila ufunuo, kila unabii unaokuja hata kama haumjengi mtu, basi utapokelewa tu kwa moyo wote,na watu wanashukuru Mungu kwa huo, hiyo yote ni kwasababu ya njaa. Hata mtu akisema mimi ni YESU au Mungu, huku akitoa maandiko yake machache yanayothibitisha anachokisimamia bado watu wataona ni Neno la Mungu lililo hai …Kusingekuwa na njaa, manabii wa uongo na waalimu wa uongo wasingepata sehemu ya kupelekea mafundisho yao manyonge, lakini kwasababu uhitaji upo mkubwa hata vile feki navyo vinapata soko..kama tu vile simu za kichina.

Ndugu, janga hili la rohoni, linanihusu mimi na wewe, tusipotaka kumwendea na kukaa chini ya Yusufu wetu wa sasa ambaye ni YESU KRISTO, atupaye chakula sahihi cha roho kwa wakati husika..Hakika tutakufa kwa kiu na kwa njaa. Tutazunguka huko na huko, tutakwenda Nigeria, china mpaka ulaya, tukidhani kule ndipo chakula kipo, lakini mwisho wake baada ya mahangaiko hayo na mateso hayo yote tunakufa kwa njaa na kwenda kuzimu. Embu jiulize taabu zako zote, unaishia kwenda kukutana na mlevi kuzimu ambaye hajawahi hata kuwa na shughuli na Mungu.

Ashukuriwe Mungu, Ni Bwana Yesu pekee aliyeahidi atatupa msaidizi ambaye atatufundisha na kuturejesha katika kweli yote..Na msaidizi huyu ni Roho Mtakatifu, mtu yoyote atakayempokea huyu hakika hata potea, wala hatakufa kwa njaa kwani kama alivyoahidi atahakikisha anakaa mahali ambapo chakula halisi cha kweli kipo kwa maana palipo mzoga ndipo watakapokusanyika TAI (Mathayo 24:28)

Unachopaswa kufanya ni kumtii Kristo kwa kumkaribisha aje ndani ya maisha yako akubadilishe uwe kiumbe kipya. Na hiyo inakuja kwa kutubu kwa kudhamiria kabisa kuacha dhambi, na kwenda kubatizwa katika ubatizo wa maji mengi kwa jina lake, kama ishara ya ondoleo la dhambi zako. Kisha ukishafanya hivyo yeye mwenyewe atakuwa na jukumu la kukupa Roho wake Mtakatifu akuongoze na kukutia katika kweli yote(Yohana 16:13). Huyo ndiye atakayekupa wewe nguvu ya kuendelea mbele, wakati wa kipindi hichi kikali cha njaa..

Usijaribu kujitafutia mwenyewe chakula kwa kanuni zako, utakufa kwa njaa..Ndio utafananishwa na hao biblia inayosema “watatanga-tanga toka bahari hata bahari; na toka upande wa kaskazi hata upande wa mashariki; watapiga mbio, wakienda huko na huko, kulitafuta neno la Bwana, wasilione (Amosi 8:12)”…Ni kwasababu gani? Ni kwasababu hawakutaka kufuata uongozi wa Roho Mtakatifu,

Ndugu Roho Mtakatifu ndio salama yetu katika haya majira ya siku za mwisho za njaa tunazoishi. Bila Roho Mtakatifu, Hakuna mbingu wala hakuna kumjua Mungu, bali ni kukisubiria kifo..Mtafute yeye angali yupo, kwa maana ahadi hiyo ni ya kila mtu amwombaye Baba..

“…je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?”(Luka 11:13)

Ubarikiwe sana.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

NJAA IPO! USIACHE KULA ASALI

NITAKUNYWAJE MAJI YA UZIMA?

MADHARA YA KUKOSA MAJI YA UZIMA BAADA YA KIFO


Rudi Nyumbani

Print this post

MTEGEMEE MUNGU, NA SI MWANADAMU.


Yeremia 17:5 “ Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana. 

6 Maana atakuwa kama fukara nyikani, Hataona yatakapotokea mema; Bali atakaa jangwani palipo ukame, Katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu.”

Jina la Bwana libarikiwe, Biblia inasema amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake, na moyoni mwake amemwacha Bwana.

Matokeo ya kumwacha Mungu moyoni ni kumtegemea mwanadamu, unapoamini kuwa mtu fulani ndio kashikilia hatma ya Maisha yako, huko ni kumtegemea mwanadamu…

Unapoziamini methali za wanadamu na kuliacha Neno la Mungu huko ni kumtegemea mwanadamu, Unapoamka asubuhi na jambo la kwanza ni kumfikiria boss wako na hata humshukuru Mungu kwa kukuamsha salama, huko ni kumtegemea mwanadamu,

Unapotii maagizo ya watu fulani waliokuzunguka na kuyadharau maagizo ya Mungu, kwa kisingizio usipotii utakosa kazi, utakosa fursa, utakosa heshima, utakosa hadhi. Huko ni kumtegemea mwanadamu na hivyo ni kujikuta unaishi katika laana.

Biblia inasema pia amelaaniwa mtu yule amfanyaye mwanadamu kuwa KINGA YAKE. Unapomtegemea mtu fulani asilimia mia kama mlinzi wako, au kama tumaini lako, ni kuishi chini ya laana…Unapomtegemea mlinzi wako wa getini na kujitumainisha na walinzi wanaokuzunguka ni kujiweka chini ya laana, ndio! Utakuwa na walinzi sio dhambi…lakini kuweka tumaini lako la kwanza juu yao..na kusema wao, wasipokuwepo wewe umekwisha..Ni kuishi chini ya laana, Biblia inasema..

Zaburi 127 :1 “Bwana asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji Yeye aulindaye akesha bure. 2 Kazi yenu ni bure, mnaoamka mapema, Na kukawia kwenda kulala, Na kula chakula cha taabu; Yeye humpa mpenzi wake usingizi”.

Unapowaamini madaktari asilimia mia kwamba uzima wako upo juu ya elimu yao, na utaalamu wao, na huku moyoni mwako Imani na Mungu imepotea kabisa, huko ni kumtegemea mwanadamu hivyo ni kujiweka chini ya laana…Elimu ya udaktari yote haiwezi kutibu kifo, lakini yupo mmoja awezaye kuwafufua waliokufa, huyo ndio wa kumtegemea hivyo kujitumainisha kwa madawa, au kwa mahospitali na huku moyoni mwako Mungu hana nafasi..ni kuishi chini ya laana, mwisho wa siku daktari akitoa ripoti hii kuwa una siku kadhaa za kuishi, au wiki kadhaa, unapaniki sana, hiyo ni hatari sana…… madaktari wanapaswa wawe tu ni vyombo ambavyo Mungu anavitumia kutuhudumia, lakini sio waponyaji wako, wala watu wanaostahili kuchukua heshima ya Mungu, kwasababu Mungu anaweza kutumia njia nyingine kukuponya bila kutumia hao..hivyo tumaini letu lote ni kutoka kwa Bwana.

Lakini pia Biblia inasema..

Yeremia 17:7 “Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake.

8 Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda.”

Ukimfanya Bwana ndio jawabu lako la mwisho, na kumwamini yeye kuwa ndio kila kitu…Neno linasema utakuwa kama mti uliopandwa kando kando ya maji..hautaona hofu wakati wa hari (jua/kiangazi)..wala hautahangaika wakati wa uchache wa mvua, wala hautaacha kuzaa matunda…

Dalili ya kwanza ya kujipima kama unamtegemea mwanadamu au la ni hofu ya Maisha!! Ukishaanza kuona una hofu fulani ya Maisha kuogopa unaweza kupatwa na jambo fulani baya kutoka kwa watu, usipofanya kitu fulani…labda usipotoa rushwa, au usipokubali kushirikiana nao kwenye jambo fulani na watu fulani, au usipojaribu kufuata njia zao au kuishi kama wao, au kuishi kama wanavyotaka,au kuvaa kama wao, unaanza kuwa na hofu ya kufa, au hofu ya Kesho itakuaje, nitavaaje, nitakulaje, nitaishije!…hizo ni moja ya dalili za kumtegemea mwanadamu…lakini wote wanaomtegemea Bwana biblia inasema hawatakuwa na hofu, hawatakuwa na wasiwasi kuwa Kesho,au Kesho kutwa watakosa riziki, wanajua kabisa katika shughuli zao Mungu atakuwa pamoja nao tu hata kama leo wanajiona hawana kitu, wanajua Kesho Mungu atafungua njia itapatikana tu! Hivyo hawapepeswi na maneno wala upepo wa hofu za Maisha haya…

Wakitishiwa kuwa watafukuzwa kazi wasipofanya jambo fulani, hilo haliwababishi, wakitishiwa kuwa watahatarisha kazi zao wasipomtii boss wao kwenda kumkusanyia rushwa hawaweweseki, kama Danieli alivyozingirwa na maadui waliompangia mabaya kwa mwenendo wake wa kukataa kula rushwa..

Biblia inasema pia mtu yule amtegemeaye mwanadamu hataacha kuzaa matunda, kwanini? kwasababu anakuwa kama amepandwa kando kando ya mto…Na kuzaa matunda kuko kwa namna Mbili..kuzaa matunda ya mwili kama kufanikiwa katika mambo yote ya mwilini…shughuli na kazi zinakuwa zinafanikiwa, na pia uzao wa tumbo unabarikiwa, na namna ya pili ni kuzaa matunda ya roho, ambayo ni upendo, upole, kiasi, uvumilivu, Fadhili, furaha, amani, n.k (Wagalatia 5:22) pamoja na kuwaleta watu kwa Kristo, ambayo thawabu yake ni juu mbinguni.

Bwana akubariki sana.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

KITABU CHA UKUMBUSHO

NI JAMBO LINALOMTAMANISHA SANA BWANA TUMWOMBE BILA KUKATA TAMAA?

TWEKA MPAKA VILINDINI.


Rudi Nyumbani

Print this post

MUNGU KUSEMA NA WEWE PEKEE, HAITOSHI KUKUPA USHINDI.


Tukisoma kitabu cha Waamuzi ile sura ya 19, tunaona habari ya mtu mmoja Mlawi ambaye alikuwa na suria wake mzinifu, Hiyo pekee haikutosha yule suria aliondoka na kurudi nyumbani kwa baba yake, Lakini kwa jinsi Yule mtu alivyokuwa anampenda Suria wake miezi minne ilipoisha alifunga safari kutoka mjini kwake na kwenda kumfuata nyumbani kwa baba yake ili kumsihi arudi nyumbani.

Lakini alipokuwa njiani kurudi nyumbani na giza limeshaingia alikutana na mzee mmoja aliyetoka shamba ambaye alimwona amesimama barabarani hana pa kulala, hivyo alimkaribisha nyumbani kwake alale usiku ule ili kesho yake aendelee na safari yake, lakini kumbe huku nyuma wenyeji wa ule mji walikuwa wanawafuatilia, na usiku ule ule wakamfuata Yule mzee nyumbani wakigonga mlango wake kwake wakisema tutolee huyo mtu tulale naye, mambo yale yale yaliyotendekea sodoma yanajirudia tena Israeli, lakini Yule mzee alikuwa mkarimu sana, akawasihi awape binti yake ambaye ni bikira wamfanyie ouvu wao, wamuache Yule mgeni aliyeingia nyumbani kwake akae katika hali ya usalama, lakini walikataa, nusu wamuue Yule mzee, ndipo Yule mtu akaamua kutoka akawapa suria wake wamfanye wanachotaka kumfanya..

Kwa ukatili mkubwa sana wale watu walimbaka Yule mwanamke usiku kucha, tengeneza picha pengine wanaume zaidi ya 100 walikuwa pale nje, mpaka kunapambazuka bado wanaendelea kumfanyia uovu ule, hadi walipoona mwanga unakaribia kutoka ndipo wakamwacha wakaondoka, Yule mwanamke kufika tu mlangoni mwa ile nyumba hali ikawa mbaya zaidi akafa pale pale, Asubuhi mume wake anafungua mlango amwambie amka tuondoke zetu, anakutana na maiti mlangoni..

Kama tunavyosoma habari akamchukua Yule mwanamke akaenda kujifungia nyumbani mwake mwenyewe, akamkata kiungo baada ya kiungo akavigawa mafungu 12. Kisha akavichukua na kwenda kuviweka katika mipaka yote ya Israeli kwa idadi ya makabila yao, ndipo watu kuona kitendo kile walishtuka sana. Wakijiuliza jambo hili maana yake ni nini?. Kwani halijawahi kutokea katika Israeli tangu walipotoka Misri, Ndipo Yule mtu akaanza kuwaelezea jinsi tukio lilivyokuwa.

Watu wote wakasema haiwezekani ni lazima hao watu ambao wamefanya hivi huko Benyamini watolewe wauawe ili kuondoa ouvu Israeli. Lakini Benyamini walipoambiwa wawatoe watu hao waligoma..Kwao halikuwa kama jambo la kushtusha sana, kuonesha ni jinsi gani walivyokuwa wameoza kwa uovu kama wa Sodoma na Gomora..Ndipo makabila yote 11 ya Israeli yaliyosalia yakaapa hawatakaa wawape binti zao, na zaidi ya yote wakakusanyika kwenda kuisambaratisha Benyamini juu ya uso wa Israeli.

Siku ile ile watu mashujaa wakahesabiwa. Ndipo wakamuuliza Mungu juu ya kabila lipi lianze kwenda kupigana nao, ndipo Mungu akawajibu na kuwaambia lianze kwenda kabila la Yuda. Lakini walipokwenda mambo yalikuwa tofauti na walivyotazamia, badala ya kuwaangamiza Benyamini wale waovu wao ndio walioangamizwa, walipigwa kwa mapigo makuu, watu 22,000 wa Israeli waliuliwa siku ile.

Lakini Israeli hawakukata tamaa tena, walijipanga upya kwa mara ya pili, tunasoma.

Waamuzi 20:22 “Lakini watu hao, watu wa Israeli, walijitia nguvu, wakaviandaa vile vita mara ya pili mahali pale walipojiandaa siku ya kwanza.

23 Wana wa Israeli WAKAKWEA JUU NA KULIA MBELE ZA BWANA HATA JIONI; wakamwuliza Bwana, wakisema, Je! Niende nikaribie tena kupiga vita juu ya wana wa Benyamini ndugu yangu? Bwana akasema, Haya, kweeni, mwende kupigana naye.

24 Basi wana wa Israeli wakakaribia juu ya wana wa Benyamini siku ya pili.

25 Benyamini alitoka kupigana nao kutoka Gibea siku ya pili, wakaangamiza hata nchi watu kumi na nane elfu tena katika watu wa Israeli; hao wote walikuwa wenye kutumia upanga.

Tunaona hapo japo Mungu aliwaambia wakwee kupigana nao lakini bado hawakufua dafu, watu wengine 18,000 wa Israeli waliuliwa vibaya na jeshi dogo la Wabenyamini.

Ni rahisi kusema, mbona Mungu si mwaminifu kwetu, mbona tumelia mbele zake siku nzima na ametupa majibu kabisa tukwee lakini matokeo yanakuja tofauti?. Mbona tuna lengo zuri la kumwondolea uovu Israeli, lakini waovu ndio wanazidi kufanikiwa na kututukana.

Lakini tunasoma, mara ya Tatu walipokwenda mbele za Bwana, hawakwenda na vilio na kufunga tu peke yake, lakini pia wanamtolea Bwana Sadaka za Amani na za kuteketezwa.Tusome..

Waamuzi 20:26 “Ndipo wana Israeli wote, na hao watu wote, wakakwea, wakaenda Betheli, na kulia, wakaketi hapo mbele za Bwana, wakafunga siku hiyo hata jioni; NAO WAKASONGEZA SADAKA ZA KUTEKETEZWA NA SADAKA ZA AMANI MBELE ZA BWANA.

27 Kisha wana wa Israeli wakauliza kwa Bwana (kwa sababu sanduku la agano la Mungu lilikuwako huko siku hizo,

28 na Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni, alikuwa anasimama mbele ya hilo sanduku siku hizo), wakasema, Je! Nitoke tena niende kupigana na wana wa Benyamini ndugu yangu, au niache? Bwana akawaambia, Haya, kweeni; kwa kuwa kesho nitamtoa na kumtia mkononi mwako.

29 Basi Israeli akaweka watu wavizie kinyume cha Gibea kuuzunguka pande zote.”

Tunasoma safari hii Mungu hakuwaambia wakwee tu, bali aliongezea na kuwaambia “Kesho nitawatoa na kuwatia mikononi mwenu”. Na baada ya hapo ukiendelea kusoma utaona jinsi Benyamini ilivyoshambuliwa na kuangamizwa vibaya mno, kwa nafasi yako pekee soma habari yote ilivyoishia utaona jinsi maangamizi yale yalivyokuwa makubwa…Ilikuwa bado kidogo tu lile kabila lingefutika lote, watu wa Benyamini walibakia wachache kama faru tulionao mbugani. Na kama sio Israeli kughairi mashambulizi yao na kuwaruhusu wale waliosalia wakaibe wake huko leo hii tungekuwa tunayafahamu na kuyaosoma makabila 11 tu ya Israeli.

Lakini kiini cha somo tunachojifunza hapo ni nini?.

Haijalishi unachokwenda kuomba mbele za Mungu ni chema kiasi gani, haijalishi unalia mbele za Mungu kiasi gani, haijalishi unafunga wiki, miezi au miaka kiasi gana, kuna mambo mengine hayawezi kutoka hivi hivi bila ya kuhusisha SADAKA. Kama vile hao walivyotoa sadaka za aina mbili za kuteketezwa na za amani, vivyo hivyo na sisi katika agano jipya tunazo sadaka za aina mbili, Ya kwanza ni ya kuteketezwa ambayo ni Yesu Kristo, aliyeteketezwa kwa ajili yetu,alichinjwa kwa ajili yetu.

Hivyo Kama upo nje ya Yesu Kristo ndugu halafu unamwendea Mungu na kumwomba akupiganie katika vita vyako, nataka nikuambie utaishia pabaya na kuvunjika moyo, na kuona kama Mungu hayupo. Vile vile na wewe uliye ndani ya Kristo, unamwomba Bwana akupiganie katika majaribu yako, halafu unakwenda mbele zake mikono mitupu, kuna uwezekano mkubwa wa tatizo lako kutokuondoka…

Kwasababu wapo wakristo ambao ni Hodari wa kuomba kweli kweli na kulia na kufunga mfano wa hawa wana wa Israeli. Lakini kwenye suala la kumtolea Mungu, wanadharau, wanaona kama Mungu hatazami hilo, wanasema yeye sikuzote huwa anatazama moyo. Nataka nikuambie, Mungu anapendezwa na moyo wa shukrani, pale unapomtolea Mungu mfuko wako anaona huyu mtu ananithamini, sio kwamba anayo haja ya fedha yako, lakini ni utaratibu wake, anapendezwa zaidi ya wenye moyo wa utoaji. unapomwendea Mungu na kumwomba akufanikishe katika jambo lako zito au jepesi jifunze kuambatanisha na sadaka ipeleke madhabahuni pake ndugu.

Unaweza kusema ooh! Mungu ameniambia yupo pamoja na mimi, Mungu kanionyesha maono, Mungu kanipa unabii, lakini utashangaa kwanini bado unashindwa pamoja na maono yako yote, Ni kwasababu unakuwa kama hawa Waisraeli.

Mungu kila wakati alikuwa anawaambia Kweeni, ni yeye kabisa alikuwa anawasapoti katika walichokuwa wanakifanya lakini tunaona japo walikuwa na jeshi la watu LAKI NNE, walipigwa na jeshi dogo la watu ELFU 26 tu la Wabenyamini. Na wewe vilevile usishangae kushindwa na mambo madogo, ukilinganisha na nguvu iliyoiwekeza katika hilo mbele za Mungu, Tatizo linaweza kuwepo hapo.

Anza kujifunza kumtolewa Bwana, naye atazifanya njia zako kuwa nyepesi.

Bwana akabariki. Tafadhali “Share ” Ujumbe huu kwa wengine. Na Bwana atakubariki. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

TOFAUTI KATIKA YA ZAKA NA SADAKA NI IPI?

SADAKA ILIYOKUBALIKA.

Rudi Nyumbani

 

Print this post