SWALI: Ule mfano wa wanawali 10 (Mathayo 25), wale watano hawakuwa na mafuta ya ziada katika chupa zao je yale mafuta ya ziada yanawakilisha nini?
Mathayo 25 : 1-11
“Ndipo ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali kumi, waliotwaa taa zao, wakatoka kwenda kumlaki bwana arusi. 2 Watano wao walikuwa wapumbavu, na watano wenye busara. 3 Wale waliokuwa wapumbavu walizitwaa taa zao, wasitwae na mafuta pamoja nao; 4 bali wale wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao. 5 Hata bwana arusi alipokawia, wote wakasinzia wakalala usingizi. 6 Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki. 7 Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao. 8 Wale wapumbavu wakawaambia wenye busara, Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika. 9 Lakini wale wenye busara wakawajibu, wakisema, Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie. 10 Na hao walipokuwa wakienda kununua, bwana arusi akaja, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye arusini; mlango ukafungwa. 11 Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, Bwana, Bwana, utufungulie. 12 Akajibu akasema, Amin, nawaambia, siwajui ninyi.
JIBU: Kama hiyo mistari ya Mathayo 25 inavyoelezea, kwamba wote walikuwa ni wanawali ikiwa na maana kuwa wote ni wakristo wanaomngojea Bwana. Na yale mafuta waliokuwa nayo wote ni “Roho Mtakatifu”. Lakini wengine walionekana kuwa na mafuta ya ziada, na wengine hawana.Hii inafunua aina mbili za wakristo watakaokuwepo siku za mwisho,
AINA YA KWANZA: Hawa ni wale wakristo werevu waliopokea Roho Mtakatifu na kuruhusu Roho wa Mungu kufanya kazi ndani yao kwa kutaka kujifunza na kuendelea kupokea mafunuo zaidi ya Roho wa Mungu mpaka kufikia cheo cha utimilifu Kristo (Waefeso 4:13), mtu wa dizaini hii kila siku anakuwa tayari kujifunza jambo jipya, hivyo anahama kutoka utukufu hadi utukufu kila siku kiu na bidii ya kuendelea kumjua Mungu inaongezeka,ndani yake, anakuwa hafungwi na mifumo fulani ya dini au dhehebu, bali Neno la Mungu ndio taa yake, mtu kama huyu anakuwa haridhiki kukaa katika hali moja ya kiroho kwa muda mrefu.
Hivyo basi Mungu anamfungulia mlango wa kufahamu mafunuo ya ziada (hiyo ndiyo ile mana iliyofichwa, ambayo si kila mtu ataipata ufunuo 2:17) kutokana na jitihada yake ya kumtafuta Mungu hivyo basi inamfanya yeye kuwa watofauti na wakristo wengine. Kwahiyo hata Bwana atakapokuja atakuwa na NURU ya kwenda kumlaki hatakuwa gizani. Na siku hiyo haitamjilia kama mwivi kwasababu taa yake inawaka siku zote.
AINA YA PILI: Hawa ni wale wakristo wapumbavu ambao walishapokea Roho Mtakatifu (ambayo ndio yale mafuta kwenye taa zao) lakini sasa baada ya kupokea Roho wa Mungu WANAMZIMISHA ndani kwa kutomruhusu tena aendelee kuwafundisha mambo mapya, na kuwatoa hatua moja ya kiroho hadi nyingine. Kwasababu kumbuka kazi ya Roho Mtakatifu ni kutuongoza katika kuijua kweli yote, soma Yohana 16:13″ Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake”.
Kwahiyo aina hii ya wakristo wanakuwa wameridhika na hali walionayo na mafundisho ya dini zao au madhehebu yao tu, hawataki kujifunza jambo jipya na wakiambiwa hata kama linatoka kwa Mungu hawatataka kusikia,kwasababu dini yao haiwaambii hivyo, kiu na bidii ya kuendelea kumjua Mungu hawana ndani yao, mwanzoni walianza na moto, lakini ikafika wakati fulani ule moto ukazimika, huko ndio kumzimisha ROHO.
Hivyo basi wakati Bwana atakapokuja hawatakuwa na NURU ya kumtambua na kwenda kumlaki, Kwao siku ile itakuwa kama mwivi ajavyo usiku. wataingia katika ile dhiki kuu ya mpinga-Kristo. Kwahiyo kama wewe ni mkristo fahamu jambo moja Mungu mpaka leo anatenda kazi anaongea, anatoa mafunuo mapya, anaonya, anawapasha watu habari ya mambo yajayo, na anawapa wale tu wanaompenda na kumtafuta kwa bidii na kutaka kuufahamu ukweli hao ndio atakaowafunulia, Ndugu fahamu tu UNYAKUO hautakuwa SIRI kwa watu wote, wale wapumbavu ndio hawatajua siku ya kuondoka, lakini wenye mafuta ya ziada watajua.
Kwahiyo ukiwa kama mkristo kwa ulimwengu tunaoishi leo mtafute Bwana kwa moyo wako wote mwombe Bwana aendelee kujifunua kwako ili siku ile isikujie kama mwivi. hivyo usiwatazame hao wakristo wapumbavu wewe kuwa mwerevu kwa kumruhusu Roho Mtakatifu kuendelea kufanya kazi ndani yako siku baada ya siku.
Ubarikiwe sana.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada zinazoendana:
KARAMU YA MWANA-KONDOO.
UTALIPWA KATIKA UFUFUO WA WENYE HAKI.
UNYAKUO.
SIKU YA HASIRA YA BWANA.
KIFAA BORA CHA MATUMIZI.
JE! NI KWELI KUNA VIUMBE VINAVYOISHI SAYARI NYINGINE (ALIENS)?
Rudi Nyumbani:
Print this post
Amina nimebrikiwa
Amen ubarikiwe nawe pia..