Title August 2021

TULITAFUTE KWA BIDII TUNDA LA ROHO.

Wagalatia 5:22 “Lakini TUNDA LA ROHO ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,

23 upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria”.

Hapo biblia inasema inasema  “Tunda la Roho” na si “Tunda la roho”.. Roho hapo imeanza kwa herufi kubwa, vile vile inasema “Tunda” na si  “Matunda”.. maana yake lipo moja tu!.. Hivi ni vitu viwili vya msingi kuvijua, katika andiko hili kabla ya kuzidi kuendelea kusoma..

Leo kwa neema za Bwana tutajifunza kwa ufupi, tofauti ya vitu hivi viwili, ili itusaidie kujua ni nini tunachopaswa kuwa nacho sasa!.

  1. Tunda la Roho.

Ikumbukwe kuwa popote pale neno “Roho” linapoandikwa likianza kwa herufi kubwa “R” linamaanisha Roho Mtakatifu, lakini mahali linapoanza kuandikwa kwa herufi ndogo “r” linamaanisha aidha roho ya mwanadamu au roho ya mwovu. Hivyo katika mstari huo Roho imeanza kwa herufi kubwa ikimaanisha ni Roho Mtakatifu na si la roho ya mwanadamu.

Mahali pengine ambapo unaweza kusoma kuhusu hilo ni (Yohana 16:13,Yohana 15:26, Matendo 2:18, Matendo 6:10).

Kwahiyo Roho Mtakatifu anapoingia ndani yetu ndipo Tunda hili linapozaliwa, hatuwezi kuwa na Tunda lolote ndani yetu linalompendeza Mungu bila kupokea Roho Mtakatifu… Sasa hebu tusogee mbele kidogo kujifunza ni kwanini sio Matunda bali ni Tunda.

  1. Tunda la Roho

Labda katika mstari huo, tungeweza kuusahihisha na kusema.. “Lakini MATUNDA ya Roho ni Upendo, furaha, uvumilivu, fadhili n.k”.. lakini biblia haijasema hivyo!, bali imesema “TUNDA la Roho ni upendo, furaha, uvumilivu n.k”.. Ikimaanisha kuwa tunda ni moja tu na si mengi!.

Jambo ambalo ni sahihi kabisa, hata katika uhalisia wa maisha, hakuna mti ambao unaweza kuzaa matunda aina mbili.. mti mmoja unazaa tunda la aina moja tu!, haiwezekani katika Mchungwa, ukakuta maembe katika shina moja, na katika shina lingine ukakuta, papai au pera, hapana!, bali utakuta kama ni mchungwa, unazaa machungwa tu!, kama ni mpera utakuta ni mapera tu mti mzima!..

Luka 6:44 “kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana, katika miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu”.

Sasa na katika maandiko tunda la Roho Mtakatifu ni moja tu!, kama tulivyojifunza..Sasa kama ni hivyo basi hayo yaliyotajwa mbele yake ni nini?

Jibu ni kwamba, hayo yaliyotajwa ni LADHA ZA HILO TUNDA!. Maana yake ni kwamba Tunda ni moja lakini ndani yake lina ladha hizo nyingi..(ambazo ndio Upendo, furaha, amani, fadhili, kiasi, utu wema n.k).

Ni sawa niseme leo, Tunda la muembe ni tamu, zuri, laini, chachu kidogo, lenye harufu nzuri n.k. Hapo nimetaja tabia za tunda moja tu na si mengi!.

Sasa na Tunda la Roho ni hivyo hivyo, Mtu mwenye Roho Mtakatifu anazaa tunda lenye mchanganyiko wa ladha hizo: yaani upendo,  amani, furaha, fadhili, utu wema, kiasi, KWA UFUPI UTAKATIFU!. Hivyo tabia zote hizo zipo ndani ya tunda moja.

Haiwezekani mtu awe na upendo halafu akose fadhili, kama hana fadhili maana yake hana upendo, haijalishi atauigiza upendo kiasi gani, vile vile haiwezekani mtu awe na amani akose utu wema au kiasi..Mambo hayo yote yanakwenda pamoja kwasababu yote yanapatikana katika tunda moja la Roho Mtakatifu.

Hivyo siku zote kumbuka mtu wa Mungu, kwamba kama huna Roho Mtakatifu ndani yako huwezi kuwa na amani, upendo, uvumilivu, ambayo yote hayo kwa ujumla ni utakatifu. Na vile vile unapopokea Roho Mtakatifu ni lazima tabia zote hizo zionekane, haitakiwi kupunguka hata mojawapo!!.

Wagalatia 5:22 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,

23 upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria”

Umeona umuhimu wa Roho Mtakatifu???…Je umepokea Roho Mtakatifu?.. kwa kutubu na kumwamini Yesu, na kubatizwa??.. kama bado kumbuka huwezi kamwe kuzaa tunda lolote katika Roho, vile vile biblia inasema wote wasio na Roho Mtakatifu hao sio wake (soma Warumi 8:9). Je na wewe ni miongoni mwa ambao sio wake?.. Habari njema ni kwamba, Mungu anatupenda wote, na ahadi hiyo ya Roho Mtakatifu sio ya watu Fulani baadhi tu!, hapana! Bali ni ya watu wote watakaomkimbilia yeye, haijalishi ni warefu, wafupi, wanene, wembamba, wazima, wagonjwa, maskini, matajiri, waliosoma au ambao hawajasoma.. Hiyo ni ahadi ya Baba kwa kila mtu anayepumua!..

Matendo 2:38  “Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

39  KWA KUWA AHADI HII NI KWA AJILI YENU, NA KWA WATOTO WENU, NA KWA WATU WOTE WALIO MBALI, NA KWA WOTE WATAKAOITWA NA BWANA MUNGU WETU WAMJIE”.

Lakini huna budi kwanza kumkubali Yesu moyoni mwako, na kwenda kubatizwa ubatizo sahihi ili ahadi hii ya Roho Mtakatifu ije juu yako. Na kumbuka ubatizo sahihi ni ule wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo kulingana na mstari huo hapo juu!.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?

NITAUPATAJE UPENDO WA KI-MUNGU NDANI YANGU?

AHADI YA ROHO ILIYOSALIA SASA KWA KIPINDI CHETU.

JE! UMEBATIZWA UBATIZO SAHIHI?

Rudi nyumbani

Print this post

YANAYOENDELEA SASA KATIKA MADHABAHU YA MUNGU ROHONI.

Madhabahuni ni mahali ambapo Mungu amepachagua kukutana na mwanadamu. Hivyo palipo na madhabahu ya Mungu mtu anaweza kuwasilisha dua zake, ibada yake, na shukrani zake, na Mungu akazipokea. Mahali pasipo na madhabahu haiwezekani kukutana na Mungu, na kama ikitokea hivyo basi ujue ni kwa neema zake tu, kakujibu pengine kwasababu hukuujua ukweli. Lakini hakuna njia mtu anaweza kuwasiliana na Mungu pasipo madhabahu.

Sasa tunapozungumzia madhabahu hatumaanishi lile eneo la mbele kanisani linalopambwa, hapana, hicho ni kivuli tu cha madhabahu, madhabahu halisi kwasasa ipo rohoni kule mbinguni, kiti cha enzi cha Mungu kilipo. Na Yesu mwenyewe ndio nyenzo ya kutufikisha hapo, Ikiwa na maana ili uweze kumfikia Mungu ni sharti DAMU ya Yesu ikutangulie kwanza kuzifunika dhambi zako. Hapo ndipo utajua ni kwanini alisema yeye ndio njia kweli na uzima, mtu hafiki kwa Baba isipokuwa kwa njia yake yeye.(Yohana 14:6) .Watu wengi wanadhani wanaweza kumkaribia Mungu kwa matendo yao wenyewe au dini zao. Hilo halipo kabisaa.

Sasa turudi kwenye kiini cha somo. Ni nini kinaendelea sasahivi  katika madhabahu ya Mungu rohoni. Kama tulivyotangulia kusema madhabahuni ni mahali ambapo watakatifu wanafikisha Maombi yao au  haja zao kwa Bwana.

Na ni vizuri kufahamu watakatifu wamegawanyika katika makundi mawili. Kundi la kwanza ni watakatifu walio hai duniani, na kundi la pili ni watakatifu waliokufa. Na wote hawa wanawasilisha mahitaji yao mbele ya madhabahu ya Mungu mbinguni. Na leo kwa ufupi tutajifunza ni mahitaji gani wanayasalisha mbele za Mungu.

Utakumbuka Bwana Yesu alitufundisha kuomba, na katika kuomba kule alisema tutamke maneno hili..

Mathayo 6:9 “Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, UFALME WAKO UJE,…

Hii ikiwa na maana kuwa kila mtakatifu aliyepo duniani, kumwomba Mungu ufalme wake uje, ni sehemu ya maisha yake ya kila siku. Hivyo mbele ya madhabahu ya Mungu iliyopo mbinguni, maombi haya yanafikishwa na malaika na kuwekwa mbele ya madhabahu ya Mungu,..Na hivyo Mungu anachofanya ni kuiharakisha ile siku ya kurudi kwake, ifike upesi.

Ufunuo 8:3 “Na malaika mwingine akaja akasimama mbele ya madhabahu, mwenye chetezo cha dhahabu, akapewa uvumba mwingi, ili autie pamoja na maombi ya watakatifu wote juu ya madhabahu ya dhahabu, iliyo mbele ya kiti cha enzi”.

Unaona? Lakini si hilo tu, bado upande wa pili wa watakatifu nao waliokufa katika dhiki, wanayo maombi yao wanayoyapeleka..embu tusome..

Ufunuo 6:9 “Na alipoifungua muhuri ya tano, NIKAONA CHINI YA MADHABAHU ROHO ZAO WALIOCHINJWA KWA AJILI YA NENO LA MUNGU, na kwa ajili ya ushuhuda waliokuwa nao.

10 Wakalia kwa sauti kuu, wakisema, Ee Mola, Mtakatifu, Mwenye kweli, hata lini kutokuhukumu, wala kuipatia haki damu yetu kwa hao wakaao juu ya nchi?

11 Nao wakapewa kila mmoja nguo ndefu, nyeupe, wakaambiwa wastarehe bado muda mchache, hata itakapotimia hesabu ya wajoli wao na ndugu zao, watakaouawa vile vile kama wao”.

Unaona, hawa nao wanaonekana wapo chini ya madhabahu, wakiomba.. Hivyo wakati watakatifu wa duniani wanaomba ufalme wake uje..Watakatifu walio ardhini wanaomba mwisho wa waovu ufike.

Walio mbele ya madhabu wanalia Unyakuo ufikie upesi, utawala wa amani wa miaka 1000 uje haraka, karamu ya mwanakondoo ianze upesi.. wakati huo huo waliochini ya madhabahu wanaomba, waovu walipizwe kisasi, wauaji, wafikishwe katika kiama chao, mbingu zikunjwe kunjwe kama ukurusa, mapigo ya vitasa saba yamiminwe juu ya nchi, ili isafishwe, waje wastarehe na Bwana ulimwenguni milele.

Haya ni maombi mazito sana, na yanausumbua moyo wa Mungu, usiku na mchana, vilio vyao na vyetu vinamfikia kila dakika kila sekunde, kutoka huku duniani na kule peponi walipo watakatifu waliokufa.

Na tunasoma majibu Bwana aliyowapa wale waliolala yalikuwa ni haya..”WASTAREHE KIPINDI KIFUPI SANA”.. Kumbe kimebaki kipindi kifupi, majibu ya maombi yote yajibiwe, ndugu yangu, siku isiyokuwa na jina Yesu atarudi, Kama tunavyoona dalili zote, jinsi zinavyotimia kwa kasi sasa, mfano wa gonjwa hili la Corona (Luka 21:11). Hii ni kuonyesha kuwa siku yoyote tutashuhudia tukio la UNYAKUO.

Siku hiyo pengine ni leo usiku, tutashangaa ghafla kundi fulani dogo sana la watu halipo. Ukiona hivyo basi ujue umebaki, na utakachokuwa unasubiria ni kisasi cha Mungu mwenyewe duniani.  Ambacho kitatanguliwa kwanza na ile dhiki kuu ya mpinga-kristo (666), ile ambayo Bwana Yesu alisema haijawahi kutokea wala haitakaa itokee . Na baada ya hapo ndipo mapigo ya vitasa saba yafuate (Ufunuo 16), Kisha, ulimwengu wote kumalizwa. Watu watatamani mauti lakini itawakimbia, ni kilio na kusaga meno.

Usifikiri tuna muda mrefu tena kama zamani, injili ya sasa sio ya kubembelezewa wokovu. Ni wewe mwenyewe ushtuke utoke usingizini, utengeneze mambo yako na Mungu wako. Ukipumbazwa na injili za manabii wa uongo, wanaokufundisha, ustarehe hapa duniani, kana kwamba hii dunia ni urithi wako utaishi hapa milele. Jihadhari sana, kwasababu Yesu alishatuonya juu yao kwamba watawadaganya hata yamkini walio wateule(Marko 13:22).

Hivyo tubu dhambi zako kwa kumaanisha kabisa kugeuka, kisha ukabatizwe katika ubatizo sahihi, wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo. Na Bwana atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu. Hapo ndipo utakuwa umezaliwa mara pili. Na ukiendelea kudumu katika wokovu na utakatifu basi hata Kristo akirudi usiku wa leo, unakwenda naye mbinguni.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Kwanini madhabahu zilitengenezwa kwa mawe yasiyochongwa?

Mahali pa juu palikuwa ni wapi kama tunavyosoma katika biblia?

TUFANANE NA WATAKATIFU WA MAKEDONIA.

Je! Mwandishi wa kitabu cha Warumi alikuwa ni Paulo au Tertio?

Ni nani aliyesema “Nitume mimi”? katika (Isaya 6:8)

Rudi nyumbani

Print this post

KU WAPI, EWE MAUTI, KUSHINDA KWAKO?

Ipo siku moja mauti itashindwa kabisa kabisa…

Siku moja tutavikwa miili mipya ya utukufu!, katika siku hiyo, parapanda ya Mungu italia, na wote tuliomwamini Yesu, tulio hai..kama hatutakufa mpaka siku ile ya kurudi kwake, basi tutamwona Bwana akitokea mawinguni, na kisha wafu waliopo makaburini nao pia wataisikia sauti ya parapanda, na wao pia watafufuka.

Katika siku hiyo, kama mtu alikufa katika udhaifu fulani labda alikufa akiwa kiwete, au kiziwi au kipofu, au alikufa na ugonjwa wa kansa, lakini alikuwa ndani ya Imani, basi atafufuliwa na kurudi katika mwili wake, akiwa mzima kabisa, akiwa si kipofu tena, wala si kiziwi tena, wala si kiwete tena, wala si mgonjwa tena, kama mtu alikufa na Kisukari, basi atafufuliwa bila huo ugonjwa..

Siku hiyo kama vile Bwana alivyomfufua Lazaro ambaye alikufa pengine katika ugonjwa Fulani uliomsababishia mauti, lakini alipofufuliwa alifufuka katika uzima! Hakuwa na huo ugonjwa tena, vinginevyo angerudia kufa tena wakati ule ule!, kadhalika kabla ya kufufuliwa alikuwa kaburini ananuka, lakini baada ya kufufuka ile harufu ilipotea!, vinginevyo asingeweza kuishi na watu tena..

Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile.. Wote waliokufa katika dhiki zao watafufuliwa katika uzima, wote waliokufa katika huzuni watafufuliwa katika ushindi na amani.. na baada ya kuvikwa miili mipya ya utukufu wataimba maneno haya… KU WAPI! EWE MAUTI KUSHINDA KWAKO?, KU WAPI EWE MAUTI KUSHINDA KWAKO??… MAUTI IMEMEZWA KWA KUSHINDA.

Ni kweli walikufa katika udhaifu wao, lakini tumaini la ufufuo walikuwa nalo!. Kwamba siku moja wataishinda mauti, watarudi tena kuwa hai na hawatakufa tena!

1Wakorintho 15:51 “ Angalieni, nawaambia ninyi siri; hatutalala sote, lakini sote tutabadilika,

52  kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika.

53  Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa.

54  Basi huu uharibikao utakapovaa kutokuharibika, na huu wa kufa utakapovaa kutokufa, hapo ndipo litakapokuwa lile neno lililoandikwa, MAUTI IMEMEZWA KWA KUSHINDA.

55  Ku wapi, Ewe mauti, kushinda kwako? U wapi, Ewe mauti, uchungu wako? ”

Swali la kujiuliza kwa wewe uliye nje ya wokovu, au uliye vuguvugu, siku hiyo utakuwa wapi wakati watakatifu wanafufuliwa na kuvikwa kutokuharibika??. Kwasababu watakaoshinda mauti si wote!, bali ni wale waliokufa katika Kristo tu!, walioyatakasa maisha yao walivyokuwa duniani.

Je umempokea Yesu? Je unauhakika siku ile, utaishinda mauti? kwa kufufuliwa na kuingia katika uzima??..au Kama ukikutwa ukiwa hai, utanyakuliwa na kwenda na Bwana mawinguni?.. Kuna huna uhakika sana, basi tayari huo ni uthibitisho kuwa hutaishinda mauti?, hutafufuliwa siku ile Bwana atakapokuja, na hata kama akija na kukukuta hai katika hali uliyopo hutanyakuliwa, badala yake utabaki na kukutana na dhiki kuu ya mpinga kristo na kufa katika ile siku ya Bwana.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

NGUVU YA UPENDO WA KRISTO.

Bwana Yesu alikufa akiwa na umri gani?

INJILI YA MANENO LAINI ITAKUGHARIMU.

Ahera ni wapi? Kama tunavyosoma katika biblia.

Nini maana ya “Ulipo mzoga, ndipo watakapokutanika tai?

Rudi nyumbani

Print this post

Je ni sahihi kusikiliza miziki ya kidunia?.

Jibu: Mpaka imeitwa miziki ya kidunia maana yake imebeba maudhui ya kidunia: Na biblia inasema yeye aliye rafiki wa dunia ni adui wa Mungu.

1Yohana 2:15  “Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.

16  Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia.

17  Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele”

Miziki yote ya kidunia inahubiri au kutangaza mojawapo ya vitu vifuatavyo: uasherati, vurugu, kiburi, kutukuza vitu vya ulimwengu huu kama mali na fahari zake, na kilicho kikuu Miziki hii inachokihubiri ni UVUGUVUGU.

Sasa kwanini uvuguvugu?

Utakuta wimbo una beti moja au mbili zinazotangaza kupendana, au zinazotaja uweza wa Mungu, na kumsifia Mungu, lakini ina beti sita za matusi, au beti 4 zinazotangaza uasherati na anasa za ulimwengu huu, Hivyo zinatangaza uvuguvugu asilimia mia moja!..na Mtu anapoisikiliza, na yeye ile roho ya uvuguvugu, ni lazima imwingie…na  Bwana Yesu aliukataa na kuulani uvuguvugu!.

Ufunuo 3:15 “Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.

16  Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu”

Mungu anauchukia uvuguvugu kuliko hata kuwa baridi!..yaani kwa Mungu ni heri mtu awe baridi kabisa lakini si vuguvugu.

Hivyo si sahihi kabisa kwa Mkristo kusikiliza miziki ya kidunia. Kwasababu inatangaza mambo ya kidunia.

Na mtu anayeokoka ni lazima aifute miziki hiyo na kuacha kuisikiliza kabisa.. na kuanza kuujaza moyo wake mambo ya kiMungu.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

TAZAMA, NASIMAMA MLANGONI.

Je watu ambao hawajasikia kabisa injili watahukumiwa?

WAOMBEENI WANAOWAUDHI.

KUWA MAKINI NA MITANDAO, NI SHIMO REFU.

Ukweli dhidi ya uongo.

 Je kualikwa kwenye sherehe za watu ambao si wakristo ni dhambi?

Rudi nyumbani

Print this post