Category Archive Wanandoa

Je! ndoa ni lazima ifungwe kanisani? kama ndio, imeandikwa wapi?

SWALI: Je! tunalisoma wapi kwenye maandiko panasema ndoa inapaswa ifungwe kanisani. Utaratibu huo upoje?


JIBU: Ili kujibu swali hili tuanzie mbali kidogo.

kufahamu ndoa ni nini? aina za ndoa, kisha mahali sahihi pa kufungia ndoa ni wapi?.

Ndoa ni nini?

Ndoa ni muunganiko kati ya watu wawili(mwanaume na mwanamke ) unaotambulika na kuheshika kijamii, au kisheria.

Pale mwanaume anapomwona mwanamke na kupatana naye waishi pamoja kama mume na mke, kwa kufuata taratibu husika za kijamii, labda kukutanishwa kwanza wazazi, au walezi, wazee wa ukoo, kupokea mahari, kisha kuidhinisha jambo hilo, au serikali kuidhinisha, hiyo tayari inaitwa ndoa.

Aina mbili za ndoa.

  1. Ndoa za wapagani
  2. Ndoa za kikristo.

Ndoa za wapagani. Hizi ni ndoa lakini hazijadhibitiwa na kanuni timilifu za Mungu. Mfano wa hizi, ndio hizo kama za kijamii, na kiserikali, au za dini nyingine zote mfano wa ki-hindu, kiislamu, ki-budha n.k. zote hizi ni ndoa za wapagani.

Zingatia: (Hapa hatumaanishi zile za mashetani, kama za jinsia moja, au za wanadamu na wanyama hapana kwasababu hizo sio ndoa, bali tunazungumzia hizi za kawaida kabisa za asili).

Kiuhalisia mtu anaweza akawa katika mojawapo ya ndoa hizi, na asihesabike kuwa ni mkosaji kwasababu ndoa hasa ni jambo la kiutamaduni, ambalo huusisha wanadamu wote, bila kuchagua dini, rangi, au kabila.

Hivyo si sawa kudhani kuwa kwasababu watu fulani hawajafungishwa ndoa kikristo(kanisani) basi, zote hizo sio ndoa kwamba ni sawa tu hata kwenda kuoa tena hapo, au kuivuruga, wasiishi pamoja. Ukifanya hivyo Mungu atakuwajibisha kwa kuzivuruga ndoa za watu wengine. 

Aina ya pili ya ndoa ni ndoa ya kikristo.

Hii ni ndoa inayofungwa katika kanuni timilifu za Mungu alizozikusudia tangu mwanzo.

Kanuni zenyewe ni hizi

    i) Wote wawe waamini.

(1Wakorintho 7:39, 1Wakorintho 9:5, 2Wakorintho 6:14 – 16)

Kuamini si lazima muwe katika viwango sawa kiroho, lakini wote muwe upande mmoja wa Kristo, (Kwasababu hayo mengine yanaweza rekebika). Lakini mmoja ni mganga wa kienyeji, mwingine mkristo,.au mmoja ni muislamu mwingine mkristo. Hilo si sawa ni sharti wote wawe wakristo. Kwasababu hakuna ushirika wowote kati ya nuru na giza.

Kwasababu Ndoa ya kikristo ni lazima iwe katika jina la Bwana, vinginevyo, itaangukia katika lile kundi lingine.

      ii) Mume mmoja, mke mmoja.

Tofauti na ndoa za wapagani. Ambazo kwao unaweza kuwa na mke zaidi ya mmoja, lakini mtu anayetaka ndoa yake itimilike mbele za Kristo, basi mume/mke atambue kuwa hana ruhusa ya kuongoza mwenza mwingine. 

Mathayo 19:4-5

[4]Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke, 

[5]akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? a

      iii) Malazi yawe safi:

Waebrania 13:4

[4]Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu. 

Malazi kuwa safi maana yake ni nidhamu ya kiasi, katika kukutana kimwili. Mkristo hapaswi kuwa mtu wa hulka ambaye wakati wote anawaza zinaa, mpaka anakosa muda wa kujishughulisha na mambo ya rohoni.

1 Wakorintho 7:5

[5]Msinyimane isipokuwa mmepatana kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu. 

Vilevile viitendo kama kuingiliana kinyume na maumbile haviruhusiwi ndani ya ndoa (1Wakorintho 6:9).

      iv) Hakuna talaka. 

Tofauti na ndoa za wapagani, mtu anaweza kuacha/kuachwa kwa sababu yoyote, labda mfano wamechokana, au wameudhiana, lakini katika ukristo hilo jambo halipo mtaendelea kuishi pamoja mpaka kifo kitakapowatenganisha. 

Bwana alitoa ruhusa hiyo katika eneo la uasherati tu lakini ukumbuke, alisema pia ‘samehe mara saba sabini’. Hivyo kwa kauli hiyo hakuna popote tunaona wigo wa wanandoa kuachana kwa sababu yoyote ile.(1Wakorintho 7:39-40)

      V) Mume ni sharti ampende mkewe. 

Mume kumpenda mkewe ni amri ya kindoa, anawajibu wa kumtunza na kumuhudumia na kujitoa kwa ajili yake, kama Kristo alivyolipenda kanisa.(Waefeso 5:25-31)

     Vi) Mke ni sharti amtii mumewe.

Ni amri mke amtii mumewe kwa agizo atakaloambiwa/ elekezwa. Tofauti na ndoa za wapagani ambazo hili linaweza lisiwe la muhimu. Kwenye ukristo, ni lazima utii wa mwanamke uonekane kwa mumewe.

Waefeso 5:22

[22]Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. 

Sasa vigezo hivi wakivikidhi hawa wakristo ambao wameokoka na wanatarajia kuishi kama mke na mume. Basi hiyo huitwa  ndoa ya Kikristo iliyokidhi vigezo vitimilifu vya Mungu,.haijalishi imefungwa kanisani au kwenye familia, .

Swali ni je? kwanini watu wafungie kanisani? Na  Je ni takwa? 

Mkristo ambaye anathamini ukamilifu wote wa ki-Mungu, katika maeneo yake yote ya kiroho na kimwili, kufungia ndoa yake kanisani itakuwa ndio chaguo lake bora. Kwanini iwe hivyo?

Hizi ndio faida za ndoa kufungiwa kanisani

  1.  Kanisa ni mahakama ya wakristo

Biblia inatueleza mashtaka yetu, hayapaswi kutatuliwa na watu wa ulimwengu, bali ndani ya kanisa. Kwasababu kanisa ni zaidi ya mahakama yoyote, ambayo Mungu ameiheshimu mpaka akaamua malaika zake wahukumiwe katika hiyo.

Hivyo endapo kuna migogoro, au kutoelewana, au kupatiwa misaada, au mashauri, au maonyo, au maongozi,  basi kanisa, limewekwa na Mungu kwa ajili yako kukusaidia katika hayo yote. 

Lakini ikiwa hukuifungia ndoa yako kanisani. Fahamu kuna mambo kama hayo yatakupita, au yatakuwa magumu kwetu kutatulika.

1 Wakorintho 6:1-3

[1]Je! Mtu wa kwenu akiwa ana daawa juu ya mwenzake athubutu kushitaki mbele ya wasio haki, wala si mbele ya watakatifu? 

[2]Au hamjui ya kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Na ikiwa ulimwengu utahukumiwa na ninyi, je! Hamstahili kukata hukumu zilizo ndogo? 

[3]Hamjui ya kuwa mtawahukumu malaika, basi si zaidi sana mambo ya maisha haya? 

    2) Ushuhuda mwema.

Mungu anapenda mambo mema atufanyiayo tumtukuze mbele ya kusanyiko la watakatifu. Tunajua Ndoa ni kitu chema, hivyo tunapoweka wazi mbele za Bwana,  na mbele ya kanisa lake, yeye hutukuzwa lakini pia tunapokea baraka za kanisa, Ikiwa tunapoumwa na kuponywa hatuoni sawa kukaa na shuhuda zetu ndani, tunakwenda kushuhudia mbele ya kanisa, si zaidi ndoa zetu?, ni ushuhuda mkubwa, ambao utawafariji wengine, lakini pia utaihubiri injili ya Kristo.

Zaburi 35:18

[18]Nitakushukuru katika kusanyiko kubwa; 

Nitakusifu kati ya watu wengi. 

Hivyo, kwa maelezo hayo tunaweza kusema hakuna sababu ya Mkristo yoyote kuifungia ndoa yake, mbali na kanisa. 

Lakini hiyo haimaanishi kuwa usipofungia kanisani, ndoa yake haitambuliwi na Mungu. Maadamu umekidhi vigezo “mama”, tulivyoviorodhesha juu. Hiyo ni ndoa.

Bwana akubariki

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >>

https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

MAFUNDISHO YA NDOA.

MISTARI YA BIBLIA KUHUSU NDOA.

Je! Ni sahihi kuoa/kuolewa na mtu uliyemzidi umri?

Rudi Nyumbani

Print this post

Kupenda fedha kutaibomoa ndoa yako.

Mafundisho maalumu kwa wanandoa – Wanawake.

Ikiwa utapenda kupata mafundisho mengine ya namna hii, basi fungua link hii uweze kuyasoma. >>.

https://wingulamashahidi.org/category/mafundisho-ya-wanandoa/

Habari ya Samsoni na Delila inafundisho kubwa nyuma yake kwa wanandoa. Wengi wanafikiri Delila alikuwa mwanamke kahaba ambaye Samsoni alimuokota tu na kukutana naye. Lakini uhalisia ni kwamba Delila alikuwa ni mke wa Samsoni.

Lakini mwanamke huyu, aliweza kubadilishwa akili kwa tamaa tu ya fedha. Ni mwanamke ambaye alipendwa sana na Samsoni, chochote ambacho angetaka kwa Samsoni angepatiwa. Lakini Wafilisti walipoona mwenendo wa Samsoni jinsi alivyompenda sana mwanamke huyu. Wakatumia fursa ile, kumshawishi Delila, kwa kumuahidia donge kubwa la fedha. Ili tu atoe siri ya asili ya nguvu zake.

Delila, akakubali, akaanza kumshawishi Samsoni, kwa kipindi kirefu, na hatimaye akafunuliwa siri ya nguvu zake. Akaenda akaziuza kwa wafilisti, kwa vipande vya fedha.

Waamuzi 16:4 Ikawa baada ya hayo akampenda mwanamke mmoja katika bonde la Soreki, jina lake akiitwa Delila.

5 Nao wakuu wa Wafilisti wakamwendea, wakamwambia, Mbembeleze, upate kujua asili ya nguvu zake nyingi, na jinsi tutakavyoweza kumshinda, tupate kumfunga na kumtesa; nasi tutakupa kila mtu fedha elfu na mia moja.

6 Delila akamwambia Samsoni, Tafadhali uniambie asili ya nguvu zako nyingi, na jinsi uwezavyo kufungwa, ili uteswe.

Kama mke, upendo wako unapohamia kwenye fedha, ni dalili madhubuti kuwa unaua  nguvu ya ndoa yako (ambayo ipo kwa mume). Usitangulize mali mbele ya ndoa yako, wala usishawishiwe na fedha kwa chochote ukadharau thamani ya mumeo. Samsoni hakuwa mfanya biashara au mwajiriwa wa kampuni Fulani, hakuwa hata na akaunti benki. Lakini alikuwa mwamuzi wa Taifa teule la Mungu. Mtetezi wa wanyonge, na mkombozi wa walioonewa, hakujitajirisha yeye, alilitajirisha taifa,. Jambo ambalo Delila hakulithamini. Akawa tayari kuoelewa na fedha(wafilisti) na sio nguvu zake(Samsoni).

Leo wapo wamama, ambao wanachotafuta kwa waume zao ni fedha tu,fedha tu, fedha tu.. wakikosa hiyo wapo tayari kufanya chochote. Wengine hata kuanzisha mahusiano na watu wengine wenye uwezo wa juu,  hawajua kuwa mwanaume anaweza asiwe tajiri kifedha, lakini ana nguvu za kuiendesha na kuilinda familia yako, jamii yako, ndugu zako, kipawa alichonacho kikaweza kukufanya wewe ukae vizuri au kuistaajabisha jamii au taifa, Lakini endapo tu utakiona hicho na kukithamini ndani yake.

Hivyo, kama mwanamke, toa moyo wako hapo kabisa.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

https://wingulamashahidi.org/category/mafundisho-ya-wanandoa/

Mtande ni nini? Ni funzo gani lipo nyuma yake?

KITENDAWILI CHA SAMSONI

Je! mtu anapofunga kwa muda wa SAA 24,anapaswa kunywa maji au kitu chochote?

Rudi Nyumbani

Print this post

NDOA TAKATIFU NI MKE MMOJA/MUME MMOJA.

Ndoa za wake wengi ni za ibilisi!..ndoa za wake wengi ni za ibilisi!!… ndoa za wake wengi ni za ibilisi!!!. Hali kadhalika ndoa za waume wengi ni za ibilisi, kama tu zilivyo za jinsi moja (zote ni zao la ibilisi).

Zipo hoja kuwa kwasababu Daudi, Sulemani na manabii wengine wakale walioa wake wengi, basi hata leo ni halali kuoa wake wengi.. tena zipo hoja zifananishazo wanyama wa porini na wa kufungwa na uhalali wa kuoa wake wengi.

Hoja zote hizi ni za ibilisi… Ndugu, usiongeze wake, wala wala usiongezee waume.

Bwana YESU alipokutana na yule mwanamke Msamaria kisimani hakumwambia akawalete WAUME ZAKE!.. Ingawa alikuwa ana wanaume wengi (na Bwana alilijua hilo), lakini alimwambia nenda “kamlete mumeo”… ikimaanisha kuwa ndoa halali na takatifu ni ya mume mmoja na mke mmoja.

Sasa Kristo alikuwa anamjua Sulemani, na Daudi..

Yohana 4:15 “Yule mwanamke akamwambia, Bwana, unipe maji hayo, nisione kiu, wala nisije hapa kuteka.

16  Yesu akamwambia, NENDA KAMWITE MUMEO, uje naye hapa.

17  Yule mwanamke akajibu, akasema, Sina mume. Yesu akamwambia, Umesema vema, Sina mume;

18  kwa maana umekuwa na waume watano, naye uliye naye sasa siye mume wako; hapo umesema kweli”.

Bwana YESU kabla ya kukutana na huyu mama, alikuwa anamjua Daudi pamoja na Sulemani na idadi ya wake wake waliooa!.. Lakini tunaona hakumwambia huyu mwanamke Msamaria, kwamba akawalete waume zake!!.. Bali alimwambia kamlete mumeo! (maana yake mmoja tu).. bado huoni tu, kuwa ndoa za mitara ni batili na za ibilisi!.

Na tena biblia inasema hapo Mwanzo Mungu alimwumba mwanaume na mwanamke, na si mwanaume na wanawake, au mwanamke na wanaume (soma Mwanzo 1:27 na Mathayo 19:4).

Huoni kuwa ndoa hizo za wake wengi zitakukosesha maji ya uzima!.. Na pia fahamu kuwa ndoa za wake wengi sio zile tu zinazohusisha mtu kuwa na wake wengi katika boma moja kwa wakati mmoja…la! Hata zile za kuacha na kuoa mwingine ilihali yule wa kwanza bado yupo hai.. hiyo ni mitara! Ndicho kilichokuwa kwa huyu mwanamke Msamaria.

Huyu mwanamke msamaria alikuwa na wanaume watano kulingana na darubini ya kimbingu! Ingawa haishi nao, lakini alikuwa nao watano, na anayeishi naye ni wa 6, vile vile kuna watu leo hii wamecha wake zao na kuoa wengine, na kuacha tena na kuoa wengine, (hawa hawana tofauti na wale waliooa wake wawili na kuishi nao wote kwa pamoja).

Na madhara ya ndoa za mitara ni “KUKOSA MAJI YA UZIMA”..

Yapo maji ya Uzima tuyanywayo hapa Duniani, na yapo yale tutakayoyanywa katika mbingu mpya na nchi mpya.

Maji ya Uzima duniani ni YESU KRISTO, tumpatapo yeye tunapata uzima wa milele (Yohana 4:14), lakini ukijiunganisha na hizi ndoa za mitara hawezi kuingia ndani yako!.. vile vile maji ya uzima baada ya maisha haya tutayanywa kutoka katika ule mto wa maji ya Uzima katika mbingu mpya na nchi mpya.

Ufunuo 22:1 “Kisha akanionyesha mto wa maji ya uzima, wenye kung’aa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwana-Kondoo,

2  katikati ya njia kuu yake. Na upande huu na upande huu wa ule mto, ulikuwapo mti wa uzima, uzaao matunda, aina kumi na mbili, wenye kutoa matunda yake kila mwezi; na majani ya mti huo ni ya kuwaponya mataifa.

3  Wala hapatakuwa na laana yo yote tena. Na kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo ndani yake. Na watumwa wake watamtumikia;

4  nao watamwona uso wake, na jina lake litakuwa katika vipaji vya nyuso zao.

5  Wala hapatakuwa na usiku tena; wala hawana haja ya taa wala ya nuru ya jua; kwa kuwa Bwana Mungu huwatia nuru, nao watatawala hata milele na milele”.

Neema ya Bwana YESU itufunike.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

MAFUNDISHO YA NDOA.

MISTARI YA BIBLIA KUHUSU NDOA.

VIGEZO VYA KUWA KARIBU NA YESU KRISTO KATIKA ULIMWENGU UJAO.

NDOA NI NINI?

KUWA NA  MAFUTA YOTE YA ROHO MTAKATIFU NDANI YAKO.

Rudi Nyumbani

Print this post

Je! Ni dhambi kutumia njia za kisasa za uzazi wa mpango.

Kwanza ni vema kufahamu uzazi wa mpango ni nini na kama ni dhambi au la!.

Uzazi wa mpango ni kuzaa kwa mpangilio ulioutaka wewe, kwamfano ukijiwekea malengo ya kuzaa watoto 30, huo ni uzazi wa mpango maadamu yalikuwa ni malengo yako, au ukijiwekea malengo ya  kuzaa mmoja maisha yako yote huo pia ni uzazi wa mpango. Kinyume chake uzao usio wa mpango, ni ule wa  kutojali idadi ya watoto utakaouzaa, wala kutojali muda wa uzaaji wako.

Lakini je! Jambo hili linaruhusiwa na Mungu?

Ukweli ni kwamba uzazi wa mpango si dhambi. Kwasababu gani?

Licha ya kwamba Mungu ameweka maagizo yake kupitia biblia takatifu, lakini pia, ameweka hekima yake kupitia mambo ya asili (1Wakorintho 11:14, Warumi 1:20), Hivyo mambo ya asili yanatufundisha pia agizo la Mungu .

Si kila wakati mama atashika ujauzito, bali upo wakati wa hatari na wakati usio wa hatari. Sasa kwa hekima huo tayari ni utaratibu Mungu kamwekea mtu, atambue majira yake, achukue tahadhari. Umeona? Kwa namna nyingine Mungu anasema, kuna majira utapata mtoto, na kuna majira hutapata mtoto. Hivyo uamuzi ni wako, ukitaka kuzingatia mazunguko huo, ni wewe, usipojali pia ni wewe.

Sasa mtu ambaye anayechagua kuzingatia mzunguko huo wa asili wa Mungu, huyo tayari yupo katika uzazi wa mpango. Na pia ni agizo la Mungu tuwe na uwezo wa kuwatunza wale wa nyumbani kwetu (1Timotheo 5:8)

Lakini je! Vipi ambao wanatumia njia za kisasa za uzazi wa mpango je na wao wapo sawa?

Tukisema njia za kisasa, ni kama zile za kutumia vidonge, kutumia sindano, kutumia vizuizi kama mipira (kwa wanaume na wanawake), kuweka kitanzi, na kuweka vipandiki/vijiti.  Zote hizi ni njia za kisasa.

Hapa ni lazima tufahamu pia lengo ni nini?. Bila shaka lengo ni lile lile moja la uzazi wa mpango kwa wanandoa, na si vinginevyo. Lakini mwanadamu ameamua kutumia njia zake za kisasa, ili kufanikisha hilo?

Je! Ni kosa?

Ili kujibu swali hilo, tufikirie pia mambo mengine ya kisasa, leo hii tuna vitu vingi vya kisasa vimebuniwa na wanadamu, kwamfano kuna kuku wa kienyeji lakini pia wapo wa kisasa, kuna mchicha wa kienyeji lakini pia ipo ya kisasa, kuna matunda ya kienyeji lakini pia yapo ya kisasa. Je! Ni dhambi kutumia vitu hivyo, kwasababu vimebuniwa na mwanadamu?

Jibu ni hapana.

Lakini vinaweza kuwa na madhara yake, kwasababu mwanadamu hawezi kuumba kitu kiukamilifu. Ndio maana asilimia kubwa ya vitu hivi vya kisasa, huwa si vizuri kiafya. Vivyo hivyo katika matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango. Yaweza isiwe dhambi kwako kutumia. Lakini madhara ya kiafya, pia waweza kukumbana nayo. Wengine hupata shida ya vizazi, wengine ugumba kabisa kulingana na njia iliyotumika, lakini wengine hawapatwi na madhara. Hivyo amani ya Kristo iamue ndani yako.

Lakini ile y asili ni bora zaidi. Ukitumia njia ya kalenda, ni salama lakini pia Mungu ametubunia hiyo, ukijizoesha kuifuatilia utaweza tu kupangilia uzazi wako.

Lakini fahamu pia uzazi wa mpango, maadamu amani ya Kristo imeamua moyoni mwako, si dhambi mbele za Mungu.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Je ni halali kwa mkristo kufanya biashara ya Forex?

JE! KUBET NI DHAMBI?

Je Kutoa Mimba ni dhambi?

Rudi Nyumbani

Print this post

Ielewe vema Kumbukumbu 25:11,inamaana gani.

SWALI: Nini maana ya Kumbukumbu 25:11

Kumbukumbu 25:11 “Washindanapo waume wao kwa wao, akakaribia mke wa mmojawapo, ili kumwokoa mumewe katika mkono wa ampigaye, yule mke akatoa mkono wake, na kumkamata tupu yake;  12 umkate ule mkono wake, lisiwe na huruma jicho lako”

JIBU: Bwana asifiwe, Haya ni mafundisho maalumu wayahusuyo wana-ndoa. Lakini pia kanisa la Kristo.

Kama ukiutafakari mstari huu, utaona picha ya mwanamke mwenye huruma, ambaye, ameona mume wake, anapigana na adui yake, na pengine alikuwa anakaribia kushindwa. Hivyo kwasababu ya upendo wake kwa mumewe, akaamua kwenda kumwokoa. Lakini tunaona njia aliyoitumia badala imletee alilolitarajia, ikamletea matatizo yeye mwenyewe.

Kwasababu gani? Kwasababu alikwenda kugusa sehemu zake za siri, Na hiyo ikawa kosa kwake, lililostahili adhabu ya kukatwa mkono. Laiti kama angemkamata mahali pengine labda tuseme mguuni, au penginepo, ni wazi kuwa kusingekuwa  na adhabu  yoyote au adhabu iliyo kali namna ile.

Ni kufunua nini?

Ni mipaka ya mwanamke awapo ndani ya ndoa yake. Fikiria hata kwa adui ya mume wake huyu mwanamke, hukupaswa kuvuka mipaka ya kindoa, si zaidi kama angefanya hivyo kwa rafiki wa karibu wa mume wake ndio ingekuwa kosa kubwa kabisaa?. Leo hii kumekuwa na migogoro mingi ndani ya ndoa, na ukitazama utagundua tabia ya wanawake kutojiwekea mipaka yao, wakutanapo na wanaume wengine wa nje.

Kwamfano mwanamke yupo kazini. Halafu Boss wake/ mfanyakazi mwenzake anazungumza mazungumzo ya mizaha, ya kizinzi, utaona na yeye analiridhia hilo, au kulifurahia au anaona ni kawaida tu. Anashindwa kujiwekea mipaka, Anaipoteza nidhamu yake, anaruhusu mazoea yaliyopitiliza ambayo hayampasi mtu kama yeye kuwa nayo. Sasa hiyo ni hatari kubwa.

Wewe kama mwanamke unapaswa ujiwekee mipaka ya hali ya juu. Ukiona migororo inaendelea baina ya wanaume, jiwekee mipaka ya kitabia na kimwenendo. Uwe salama, ili mkono wako usifike kusikostahili. Uvaaji wako, usemi wako, uwe kama mtu aliye kwenye “KIFUNGO” cha ndoa. Watu wakuheshimu, wenye mizaha wakuonapo wakae kimya. Usiruhusu kabisa mazungumzo yako na mtu mwingine yafike kwenye maeneo ya sirini, iwe kwenye simu, ofisini, njiani, shuleni, mtaani, nyumbani, au popote pale. Weka MLANGO mkubwa wenye makomeo ya chuma . Mazungumzo hayo yawe na mume wako tu, na sio mwingine yoyote.

Halikadhalika inatupa na picha ya rohoni pia. Sisi kama kanisa ni lazima tufahamu kuwa wote ni “WAKE” wa Bwana wetu Yesu Kristo. Na hivyo anataka tuwe na tahadhari tuendapo kumuhubiri yeye kwa watu wa nje, tujichunge tusijaribiwe wenyewe, kwa vitendo vyao. Kwasababu itatugharimu kinyume chake.

Tukutanapo na wazinzi kuwahubiria, tusivutwe kwenye uzinzi wako, tukutanapo wa watukanaji, tusirudishe matusi, tukutanapo na wenye fedha, tusigeuzwe injili yetu. Bali tubaki kwenye mipaka yetu ile ile.

Wagalatia 6:1  Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

Nini maana ya Mithali 16:30 Afumbaye macho, kusudi lake ni kuwaza yaliyopotoka; 

Maana ya Mithali 29:21 “Amtunduiaye mtumwa wake tangu utoto, Mwisho wake atakuwa ni mwanawe”

Kula uzao wa tumbo lako maana yake nini? (Kumbukumbu 28:53)

MISTARI YA BIBLIA KUHUSU NDOA.

USIONDOE ALAMA YA MPAKA ILIYOWEKWA NA MABABA.

Kwanini kuwe na kitabu Cha kumbukumbu la Torati na kwanini kiitwe vile?

Rudi nyumbani

Print this post

MAMBO YA KUJIFUNZA KWA KLOPA NA MKE WAKE!

(Masomo maalumu kwa wanandoa).

Je unamjua Klopa au Kleopa kwenye biblia?.. na tena unamjua Mke wake?

Tuanze kwa mke wa Klopa, kabla hatujaenda kwa Klopa mwenyewe…

 Jibu: Tusome,

Yohana 19:25  “Na penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, MARIAMU WA KLOPA, na Mariamu Magdalene”.

Mariamu wa Klopa alikuwa ni mke wa mtu aliyeitwa Klopa. Na kwanini aliitwa vile kwa sifa ya jina la Mume wake?.. ni kwasababu ya mwenendo wa mume wake. Laiti kama mume wake angekuwa na sifa mbaya, basi biblia isingemtaja huyu Mariamu kwa sifa ya jina la mumewe, lakini mpaka imemtaja mumewe ni kuonyesha kuwa alikuwa na kitu cha kipekee.

Sasa huyu Klopa/Kleopa ni nani?

Huyu Klopa au Kleopa ndio yule aliyetokewa na Bwana Yesu akiwa na mwenzake walipokuwa wanaelekea kijiji kimoja kilichoitwa Emau, baada ya Kristo kufufuka,.. wakiwa katika mazungumzo yao, maandiko yanasema Yesu mwenyewe aliungana nao pasipo wao kumtambua, na baadaye walifumbuliwa macho na kumtambua na kutoweka.

Tusome,

Luka  24:13  “Na tazama, siku ile ile watu wawili miongoni mwao walikuwa wakienda kijiji kimoja, jina lake Emau, kilichokuwa mbali na Yerusalemu kama mwendo wa saa mbili.

14  Nao walikuwa wakizungumza wao kwa wao habari za mambo hayo yote yaliyotukia.

15  Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao.

16  Macho yao yakafumbwa wasimtambue.

17  Akawaambia, Ni maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea? Wakasimama wamekunja nyuso zao.

18  AKAJIBU MMOJA WAO, JINA LAKE KLEOPA, akamwambia, Je! Wewe peke yako u mgeni katika Yerusalemu, hata huyajui yaliyotukia humo siku hizi?

19  Akawauliza, Mambo gani? Wakamwambia, Mambo ya Yesu wa Nazareti, aliyekuwa mtu nabii, mwenye uwezo katika kutenda na kunena mbele za Mungu na watu wote;

20  tena jinsi wakuu wa makuhani na wakubwa wetu walivyomtia katika hukumu ya kufa, wakamsulibisha.

21  Nasi tulikuwa tukitumaini ya kuwa yeye ndiye atakayewakomboa Israeli. Zaidi ya hayo yote, leo ni siku ya tatu tangu yalipotendeka mambo hayo;

22  tena, wanawake kadha wa kadha wa kwetu walitushitusha, waliokwenda kaburini asubuhi na mapema,

23  wasiuone mwili wake; wakaja wakasema ya kwamba wametokewa na malaika waliosema kwamba yu hai.

24  Na wengine waliokuwa pamoja nasi walikwenda kaburini wakaona vivyo hivyo kama wale wanawake walivyosema, ila yeye hawakumwona…”

Umeona? Kumbe Kleopa alikuwa ni miongoni mwa wafuasi wa Bwana Yesu, lakini cha kipekee ni kwamba na mke wake pia alikuwa ni mwanafunzi wa Bwana na ndiye aliyekuwa pale msalabani pamoja na Mariamu Magdalena na Mariamu mamaye Yesu.

Kwa kifupi walikuwa ni watu waliompenda sana Bwana Yesu, ni watu waliokuwa wanafuatilia sana habari za Bwana Yesu, wakati mke wa Kleopa akiwa kule kaburini pamoja na akina Mariamu Magdalena, Bwana aliwatokea wao wa kwanza, kabla hata ya akina Petro, na Yohana, na Andrea na mitume wengine wote. Na kabla Bwana hajawatokea mitume wake (akina Petro na wengineo), aliwatokea Kleopa na mwenzake ( hawa wawili ndio wanaume wa kwanza kumwona Bwana aliyefufuka).

Akina Petro baada ya kupewa taarifa walienda kaburini lakini hawakumwona, lakini akina Kleopa hawakufika kaburini lakini walimwona wa kwanza, tena Zaidi sana walikuwa wanaondoka Yerusalemu lakini Bwana aliwafuata huko na kuwatokea wao kwanza, na tena Bwana ndiye aliyekula nao wa kwanza, na zaidi sana aliwatumia hao kwenda kuwashuhudia mitume 12 kuwa Bwana kafufuka kweli kweli, na walipokwenda Yerusalemu kuwashuhudia ndipo Kristo alipojidhihirisha kwa mitume wake.

Luka 24:31 “Yakafumbuliwa macho yao, wakamtambua; kisha akatoweka mbele yao.

32  Wakaambiana, Je! Mioyo yetu haikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na kutufunulia maandiko?

33  Wakaondoka saa ile ile, wakarejea Yerusalemu, wakawakuta wale kumi na mmoja wamekutanika, wao na wale waliokuwa pamoja nao,

34  wakisema, Bwana amefufuka kweli kweli, naye amemtokea Simoni.

35  Nao waliwapa habari ya mambo yale ya njiani, na jinsi alivyotambulikana nao katika kuumega mkate. 36  Na walipokuwa katika kusema habari hiyo, yeye mwenyewe alisimama katikati yao, akawaambia, Amani iwe kwenu.

37  Wakashituka, wakaogopa sana, wakidhani ya kwamba wanaona roho.

38  Akawaambia, Mbona mnafadhaika? Na kwa nini mnaona shaka mioyoni mwenu?

39  Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikenishikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo”.

Ni nini tunajifunza kwa Kleopa na Mkewe?

Kikubwa tunachoweza kujifunza kutoka kwao ni roho na moyo wa kumpenda na kumfuatilia Bwana sana, Kleopa na Mke wake walikuwa ni watu waliomsogelea sana Bwana ndio maana hata taarifa za kufufuka kwa Bwana wao ndio wa kwanza kuzipata. Wote wawili walikuwa ni watu waliompenda Bwana, hakuna hata mmoja aliyemzuia mwenzake katika kumtafuta Bwana.

Na wewe kama Baba kuwa kama Kleopa, usimzuie mke wako kumtafuta Mungu, au kuwa karibu na Mungu muda mwingi, vile vile na wewe mama, kuwa kama mke wa Kleopa, usimzuie mume wako kwenda katika kutafuta uso wa Mungu, wote mfanyeni Kristo kuwa wa Kwanza, na Kristo atawachagua nyie kumwona yeye wa kwanza kabla ya wengine.

Mtamwona Yesu katika familia yenu wa kwanza kabla ya wengine.

Mtaona wema wa Kristo kwenye ndoa yenu kabla ya wengine wote.

Nyie ndio mtakuwa wa kwanza kutoa ushuhuda wa maajabu ya Yesu kwenye maisha yenu kabla ya wengine.

Hiyo yote ni kama mtamfanya Kristo wa kwanza, na kama hamtazuiana katika kumtafuta Yesu.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

NEEMA YA MUNGU KWA MARIAMU.

Nini maana ya huu mstari; Mithali 10:22 “Baraka ya Bwana hutajirisha, Wala hachanganyi huzuni nayo”

MAMA, TAZAMA, MWANAO.

FAHAMU MAISHA YA YESU KABLA YA HUDUMA.

Je unaruhusiwa kufanya tendo la ndoa ukiwa katika mfungo?

Rudi nyumbani

Print this post

MSIWE NA UCHUNGU NAO!

Usiwe na Uchungu na Mke wako!.

(Masomo maalumu kwa Wanandoa)-UPANDE WA WANAUME/ MAJUKUMU YA WANAUME.

Neno la Mungu linasema..

Wakolosai 3:19  “Ninyi waume, wapendeni wake zenu MSIWE NA UCHUNGU NAO”

Hapo biblia imetoa maagizo mawili; 1)Kupenda na 2)Kutokuwa na uchungu.

1.Kupenda:

Kila mwanaume analo jukumu la kumpenda Mke wake kuanzia siku ile alipofunga naye ndoa mpaka siku ile kifo kitakapowatenganisha!. (Na hiyo ni Amri sio ombi). Tena anapaswa ampende kwa viwango vile vile vya kama Kristo alivyolipenda kanisa..

Waefeso 5:25  “Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake”

Kwahiyo kila Mwanaume ana wajibu wa kumpenda Mke wake siku zote za maisha yake… Ukiona upendo kwa mke wako unapungua, basi tafuta kuurejesha huo upendo kwa gharama zote!.(Jambo hilo linawezekana kabisa endapo ukimwomba Mungu, na wewe ukitia bidii katika kuurejesha upendo)

2. Kutokuwa na uchungu nao:

Amri ya pili waliyopewa wanaume juu ya wake zao, ni “KUTOKUWA NA UCHUNGU NAO” . Na mpaka biblia inasema “wanaume wasiwe na uchungu na wake zao” maana yake ni kwamba “wanawake wana mambo mengi ambayo wakati mwingine yanaleta machungu mengi”.

Kwamfano Matumizi mabaya ya Pesa… Hili ni moja ya jambo ambalo linaweza kumletea Mwanaume uchungu, hususani kama sehemu kubwa ya fedha anazitoa yeye, na pia tabia ya kuzungusha maneno ya siri ya familia kwa marafiki au kwa watu wasio na uhusiano wowote na familia,  jambo hili pia linaweza kuleta uchungu kwa mwanaume. Na pia tabia ya kurudia makosa yale yale, na tabia ya kutokusikia au kukosa umakini wa baadhi ya mambo na hivyo kusababisha hasara Fulani,  au kuwa wazito kufanya baadhi ya mambo, hizi zinaweza kuleta uchungu kwa mwanaume.

Lakini kwa sababu hizo au nyingine zozote, ni amri wanaume wote kutokubali uchungu ndani yao kwasababu ya kasoro hizo za wanawake.

Sasa Kwanini ipo hivyo?

Biblia imeweka wazi kuwa ni kwasababu “wanawake ni vyombo visivyo na nguvu”..

1Petr3:7 “Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, KAMA CHOMBO KISICHO NA NGUVU; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe”

Kwahiyo kama mwanamke ni chombo dhaifu, ni lazima tu kitakuwa hivyo siku zote!.. hivyo ni lazima kuchukuliana nacho katika hali hiyo.. Lakini usipokichukulia kama ni vyombo dhaifu, na kukifanya kuwa ni chombo chenye nguvu, basi utakuwa ni mtu wa kuumia moyo kila wakati, na kujikuta unakuwa mtu uliyejaa uchungu na hasira na hata kufikia kuwa mtu wa ugomvi na makelele ndani ya nyumba. Jambo ambalo ni dhambi!!

Waefeso 4:31 “UCHUNGU WOTE NA GHADHABU NA HASIRA NA KELELE na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya”

Hivyo ni wajibu wa kila mwanaume aliyeoa kutokuwa na uchungu na Mke wake.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Mada Nyinginezo:

Neno “Uchungu wa mauti” lina maana gani kibiblia?

Mshahara wa Mbwa ni upi? Kama tunavyousoma katika Kumbukumbu 23:18

SHINA LA UCHUNGU, LISICHIPUKE NDANI YETU.

Nini maana ya msiwe waalimu wengi (Yakobo 1:3)?

MAJARIBU 10 WANA WA ISRAELI WALIYOMJARIBU MUNGU.

Rudi nyumbani

Print this post

MASWALI NA MAJIBU: YAHUSUYO NDOA- Sehemu ya 2.

Shalom

Hii ni sehemu ya pili ya maswali na majibu yahusuyo ndoa.. Sehemu ya Kwanza unaweza kuisoma kupitia  link hii >> MASWALI-NDOA

SWALI 01: Je Mkristo anaruhusiwa kuoa mtu wa Imani nyingine? Yaani akafunga naye ndoa tu, na kila mmoja akaendelea na imani yake.

Jibu: Ndoa ya kikristo ni ndio inayohusisha Imani moja, Bwana mmoja, Roho mmoja, tumaini moja, Ubatizo mmoja na Mungu mmoja..

Waefeso 4:3  “na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani.

4  Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.

5  Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja.

6  Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote”

Kwahiyo kabla ya Ndoa ni lazima wawili hao wafikie kuwa na imani moja, na ubatizo mmoja na Roho Mmoja na Mungu mmoja, wasipofikia huo umoja basi hiyo sio ndoa ya kikristo.

Sasa nini cha kufanya endapo ikitokea mmoja si wa imani ya  kikristo?, Jibu: Huyo ambaye tayari kashaokoka anapaswa amhubirie mwenzake habari za Wokovu kwanza, na aamini na kubatizwa na kupokea Roho Mtakatifu (kwaufupi awe mkristo aliyesimama kweli kweli) na baada ya hapo ndipo wafunge ndoa, lakini kumbuka, si abadilike kwasababu tu anataka kuoa au kuolewa!, hapana bali anapaswa apate badiliko la kweli kiasi kwamba hata kama asipoolewa na huyo basi bado Kristo atabaki kuwa Mwokozi wake siku zote za maisha yake.

SWALI 02: Je kuna umuhimu wowote wa kupima afya kabla ya kufunga Ndoa?

Jibu: Ndio upo umuhimu wa kufanya hivyo kama kuna huo ulazima. Kuhakikisha afya zenu zipo sawa kabla ya kufanya lolote, maandiko hayajakataza kufanya hivyo. Na endapo ikitokea mmoja kakutwa na maradhi ambayo yatawafanya wawili hao wasiweze kukutana kimwili!.. Basi hapo ni uchaguzi wa Yule aliye salama, kama upendo wake ni mwingi kama ule wa Kristo, anaweza kuishi na huyo anayemchagua, lakini kamba si hawezi basi yupo huru kutafuta mwingine aliye chaguo lake hafanyi dhambi.

Lakini kama tayari wameshafunga ndoa na mmoja akapata maambukizi ya maradhi hayo basi Yule aliye salama hapaswi kumwacha huyo aliye na maradhi, wataendelea kubaki pamoja siku zote. Vile vile kama mmojawapo kapata ulemavu ambao utamfanya asiweze kabisa kukutana na mwenzake basi Yule aliye mzima pia hapaswi kumwacha mwenzake aliye na udhaifu, siku zote za maisha yake.

SWALI 03: Je wakristo wanaruhusiwa kutoa Ujauzito (Mimba)?

Jibu: Mkristo haruhusiwi kutoa ujauzito (mimba), kwasababu yoyote ile isipokuwa ya kiafya kwa maelezo ya madaktari:

Kwamfano  Ikitokea mtoto kafia tumboni hapo ni lazima ile mimba changa iondolewe ili kuokoa maisha ya mama, vile vile ikitokea itilafu katika tumbo la mama, ambayo ili mama awe salama (asipoteze maisha) na kama mama huyo hana imani ya kutosha ya kuamini kuwa anaweza kuishi bila kuitoa na akawa salama, na hivyo akakubali itolewe kufuatia maelezo hayo ya daktari, mama huyo hafanyi dhambi!, kwasababu ya usalama wake mwenyewe.

Lakini sababu nyingine yoyote ya kutoa mimba tofauti na hiyo ya kiafya, ni dhambi!..Kwamfano mwanamke kapata ujauzito bahati mbaya na alikuwa hana mpango wa kuipata hiyo, hapo hapaswi kuutoa huo ujauzito, au kapata ujauzito kwa njia ya ukahaba, hapo hapaswi kuitoa hiyo mimba, atabaki nao mpaka hatua ya kujifungua.

SWALI 04: Ni nani mtu sahihi wa kumpelekea matatizo ya ndoa? Endapo kukitokea kutokuelewana?

Jibu: Endapo kukitokea kutoelewana, ni vizuri kuomba kwa Bwana suluhisho na kurejea biblia kujua ni nini biblia inasema kuhusu hali hiyo, lakini kama bado mwanandoa anahisi anahitaji msaada zaidi basi anapaswa ayafuate makundi yafuatayo.

1: MCHUNGAJI WA KWELI WA BWANA:

Si wachungaji wote ni waaminifu, lakini pia wapo walio wa kweli na waaminifu, watu hao ni kituo bora cha kupata ushauri wa kiMungu na maombezi.

2. MZAZI:

Kama unaye mzazi aliyeokoka basi hicho pia ni kituo bora sana cha kupokea mashauri bora..na yenye msingi mkubwa.

Kamwe usitafute ushauri kwa marafiki, majirani, ndugu wa mbali, au watu usiowajua kuhusiana na mambo ya kindoa.

SWALI 05: Endapo nikagundua baada ya kufunga ndoa Mwenzangu ana matatizo katika uzazi wake (hana uwezo wa kuzaa au kuzalisha)..Je naweza kwenda kupata mtoto nje na kuendelea kuwa naye?

Jibu: Kama mwanandoa mmoja anamatatizo ya uzazi yanayomfanya asiweze kuwa na mtoto, hapo mwanandoa mwingine asiyekuwa na matatizo hayo hapaswi kumwacha Yule mwenye matatizo, wala kuondoka na kwenda kupata mtoto wa kando, atabaki naye huyo huyo siku zote za maisha yake, huku wakimwomba Bwana awafungue!.

Na kama ni mapenzi ya Bwana wao kuwa na watoto, basi Bwana atawapa mtoto haijalishi ni miaka mingapi itapita (Ibrahimu na Sara walipata watoto katika uzee), na Mungu ni Yule Yule hajabadilika.

Lakini pia kama wanaona ahadi za Mungu bado zipo mbali wanaweza ku-adopt  mtoto/watoto na kuwalea kama watoto wao.. Vipo vichanga vingi visivyo na wazazi, na mtu akiwalea hao mbele za Mungu ni zaidi hata ya Yule mwenye watoto 100 waliotoka katika uzazi wake.

SWALI 06: Je mkristo anaruhusiwa kupanga uzazi?

Jibu: Ndio wakristo wanaweza kupanga idadi ya watoto wanaotaka kuwa nao!. Biblia haijatoa amri ya kuzaa idadi ya watoto 10 au 50, ni kila mtu atakavyotaka yeye. Lakini imetoa tu angalizo kuwa tuwe watu wenye uwezo wa kuwatunza wakwetu (1Timotheo 5:8  Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini.)

Kwahiyo ni lazima Mkristo awe na uwezo wa kuwatunza watoto wake, hivyo ni lazima awe na uzazi wa mpango.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

MASWALI NA MAJIBU: YAHUSUYO NDOA-1

MAFUNDISHO YA NDOA.

MFANO WA MAMBO HAYO NI UBATIZO.

TOFAUTI YA MITUME, MANABII, WAINJILISTI, WACHUNGAJI NA WAALIMU NI IPI?

Je ni viatu gani Musa aliambiwa avivue?  Vya mwilini au vya rohoni? (Kutoka 3:5).

Rudi nyumbani

Print this post

MASWALI NA MAJIBU: YAHUSUYO NDOA

SWALI 01: Je wakristo tunaruhusiwa kuoa mke zaidi ya mmoja?

Jibu: Kwa mujibu wa biblia, Ndoa ya kikristo ni ya mke mmoja na mume mmoja.

Marko 10:6 “Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke.

7 Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe;

8 na hao wawili watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja”.

SWALI 02: Je kama mtu alifunga ndoa ya kiserikali, au kimila ndoa hiyo inatambulika mbinguni?..Yaani Mungu anawatambua kama ni mume na mke kihalali?.

Jibu: Ndio! Mbinguni watu hao wanatambulika kama ni mke na mume, ingawa ndoa yao haitakuwa ndoa takatifu ya kikristo..maana yake kuna mambo hawataweza kuyafanya wakiwa katika hiyo hali, mfano wa mambo hayo ni Uchungaji wa kundi, au Uaskofu au Ushemasi. Kwasababu nafasi hizo ni za kuhubiria wengine njia sahihi, hivyo haiwezekani mtu awahubirie wengine wafunge ndoa takatifu ya kikristo wakati yeye mwenyewe hayupo katika ndoa kama hiyo. (Atakuwa mnafiki).(Tito 1:6-7).

Hivyo ni sharti aibariki ndoa yake hiyo na kuwa ndoa takatifu ya kikristo ili asifungwe na baadhi ya mambo.

Mfano wa ndio hizi ambazo ni za kipagani lakini Mungu alikuwa anazitazama ni kama ile ya Herode ambayo Yohana mbatizaji aliikemea.

Marko 6:17 “Kwa maana Herode mwenyewe alikuwa ametuma watu, akamkamata Yohana, akamfunga gerezani, kwa ajili ya Herodia, mkewe Filipo ndugu yake, kwa kuwa amemwoa;

18 kwa sababu Yohana alimwambia Herode, Si halali kwako kuwa na mke wa nduguyo”.

Herode hakuwa mkristo lakini alipomwacha tu mke wake na kwenda kumchukua wa ndugu yake ikawa ni chukizo mbele za Bwana, na vivyo hivyo ndio zote zilizofungwa ambazo zimehusisha mahari pamoja na makubaliano pande zote, basi ndio hizo Mungu anazitazama na zinapaswa pia ziheshimiwe.

SWALI 03: Je Wakristo tunaruhusiwa kutoa talaka?

Jibu: Wakristo hawaruhusiwi kuachana baada ya kuoana. Kwahiyo talaka hairuhusiwi katika ndoa ya kikristo wala mwanaume haruhusiwi kumwacha mke wake katika hali yoyote ile ya udhaifu wa kimwili.

Luka 16:18 “Kila amwachaye mkewe na kumwoa mke mwingine azini; naye amwoaye yeye aliyeachwa na mumewe azini”

SWALI 04: Je! Kama Mwanamke alikuwa ameolewa na mwanaume ambaye tayari alikuwa na Mke, je anapookoka anapaswa amwache huyo mume wake au aendelee naye?.

Jibu: Kulingana na maandiko anapaswa amwache kwasababu tayari huyo alikuwa ni mume wa mtu, hivyo ili maisha yake yawe na ushuhuda na aishi kulingana na Neno ni lazima amwache huyo na akaolewe na mwanaume mwingine ambaye hajaoa (lakini katika Bwana tu), au akae kama alivyo.

SWALI 05: Kama mwanaume alikuwa ameoa wanawake wawili na kashaishi nao muda mrefu na kuzaa nao watoto, lakini ukafika wakati akaokoka je anapaswa amwache mmoja na kuendelea na mwingine au?

Jibu: Kama mwanaume alikuwa amemwoa mwanamke wa kwanza katika ndoa ya kikristo (yaani iliyofungishwa kanisani), na baada ya ndoa hiyo akaongeza mwingine wa pili…Na baadaye akatubu na kuokoka upya!. Hapo hana budi kumwacha huyo wa pili kwasababu alikuwa anafanya uzinzi kulingana na biblia, haijalishi ameishi na huyo mwanamke kwa miaka mingapi, na amepata naye watoto wangapi..anapaswa amwache na kubaki na mke wake wa kwanza.

Lakini kama alimwoa mke wa kwanza kipagani na kulingana na sheria za kipagani akaongeza wa pili, na  akaishi nao muda mrefu na wanawake hao wote wawili bado wanahitaji kukaa naye, hapaswi kuwaacha labda mmoja wapo wa wanawake hao aridhie mwenyewe kumwacha kwa hiari yake..

Lakini kama ataendelea kubaki nao mtu huyo ndoa yake hiyo ya wake wawili haitawezi kubarikiwa kanisani, na pia yeye mwenyewe hataweza kuwa Mchungaji, askofu au Mwinjilisti au shemasi bali atakuwa muumini wa kawaida tu, kwasababu biblia inasema ni lazima Askofu awe mume wa mke mmoja..

Tito 1:6 “ikiwa mtu hakushitakiwa neno, naye ni mume wa mke mmoja, ana watoto waaminio, wasioshitakiwa kuwa ni wafisadi wala wasiotii.

7 Maana imempasa askofu awe mtu asiyeshitakiwa neno, kwa kuwa ni wakili wa Mungu; asiwe mtu wa kujipendeza nafsi yake, asiwe mwepesi wa hasira, asiwe mlevi wala mgomvi, asiwe mpenda mapato ya aibu”.

SWALI 06: Je?.Kujifungua kwa operation au kuzalishwa na wakunga wakiume ni halali kwa mwanandoa wa kikristo?.

Jibu: Operesheni ni njia mbadala ya kukiondoa kiumbe tumboni ili kusalimisha maisha ya mama na mtoto..Hivyo kibibla sio dhambi, kwasababu lengo lake ni kuokoa maisha na si lengo lingine.

Vile vile kuzalishwa na mkunga wa jinsia ya kiume si dhambi, kwasababu lengo ni lile lile kusaidia kuokoa maisha,..Katika eneo la uokozi ni eneo ambalo haliangalii jinsia..

Kwasababu pia zipo operesheni kubwa zaidi hata za kuzalisha ambazo zinahusisha kuondoa au kurekebusha viungo vya ndani kabisa vya uzazi wa mwanamke au mwanaume, ambazo operesheni hizo madaktari wake bingwa wanakuwa ni wa jinsia tofauti na wanaofanyiwa, hivyo hapo kama mtu anataka kupona kwa njia hiyo ya matibabu basi hana uchaguzi, wa atakayemfanyia hiyo operesheni.

Kwahiyo katika mazingira kama hayo, jinsia yoyote itakayotumika kumfanyia matibabu huyo mgonjwa wa kikristo, itakuwa si dhambi kwa mkristo huyo anauefanyiwa hiyo operesheni wala kwa yule anayemfanyia.

Shalom.

Usikose sehemu ya pili…

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

MISTARI YA BIBLIA KUHUSU NDOA.

MAFUNDISHO YA NDOA.

KWANINI NDOA NYINGI ZINAVUNJIKA? (Sehemu ya 2: Upande wa wanawake)

KWANINI NDOA NYINGI ZINAVUNJIKA? (Sehemu ya 1: Upande wa wanaume)

Pale mwanandoa mmoja anaposhindwa kutimiza wajibu wake ufanyaje?

Rudi nyumbani

Print this post

EPUSHA WIVU KATIKA NDOA:

MAFUNDISHO MAALUMU KWA WANANDOA: Epusha Wivu katika ndoa:

Sehemu ya kwanza: Upande wa Mwanamke.

Huu ni mfululizo wa mafundisho maalumu yawahusuyo wanandoa: Ikiwa hukupata sehemu za nyuma, basi waweza kututumia ujumbe kwa namba zetu zilizo chini ya somo hili, tukutumie;

Leo tutaona  jinsi wivu unavyoweza kuathiri kwa sehemu kubwa mahusiano ya wanandoa.

Kibiblia wivu upo wa aina mbili:

1)  Wivu wa kipepo: Ni ule wa kumuonea mtu kijicho, yaani kutotaka, mwenzako kufanikiwa kwasababu wewe hukufanikiwa kama yeye alivyofanikiwa, kutaka kile ambacho mwenzako anacho uwe nacho wewe huku hutaki yeye awe nacho. Biblia imetuonya sana dhidi ya wivu huu, kwasababu ni zao la shetani. Ndio walikuwa nao masadukayo na makuhani kwa Bwana wetu Yesu na mitume wake, pale walipoona neema ya Mungu ipo juu yao kubwa lakini kwao haipo, (Matendo 5:17, Warumi 13:13)

2)  Wivu wa kimahusiano: Wanandoa, Huu ni wivu ambao ni wa asili, Mungu kauweka ndani ya mtu, huu upo katika mahusiano ya kindoa,au maagano Na ndio Wivu ambao Mungu amekiri pia mwenyewe anao.(Kutoka 20:5)..Huu ni wa kuulinda sana, hususani pale unapoingia kwenye ndoa, kwasababu madhara yake ni makubwa zaidi hata ya hasira, au ghadhabu. Biblia inasema hivyo katika..

Mithali 27:4 “Ghadhabu ni kali, na hasira ni gharika; Lakini ni nani awezaye kusimama mbele ya wivu”.

Huu ndio umesababisha watu, kugombana, kuchukiana, kusalitiana  na hata wakati mwingine kuuana, na kuwasababishia matatizo na wengine ambao hata hawahusiki.

Leo  tutatazama, ni kwa namna gani, kinywa cha mwanamke, kinaweza kuwasha wivu mbaya sana, kwa upande wa pili. Na somo linalofuata tutaona tabia ambazo mwanaume anapaswa ajiepushe nazo, kuepukana na madhara ya wivu kwenye ndoa yake.

 hii itakusaida, kuishi kwa amani na utulivu na kuinusuru ndoa yako, .

Sasa embu tusome kisa hichi tunachokiona katika 1Samweli 18:7. Si kisa cha kindoa lakini ni kisa kimuhusucho Daudi na Sauli, Wengi wetu tunajua sababu iliyomfanya Sauli amchukie Daudi, ambaye hapo mwanzo alimpenda ilikuwa ni Wivu. Lakini wachache sana, wanafahamu CHANZO cha wivu huo, kilikuwa ni nini?

Biblia inatupa majibu, kilikuwa ni wanawake, waliotoka na kutoa sifa zao, mahali pasipostahili kwa wakati ule. Embu Tusome.

1Samweli 18:5 “Basi Daudi akatoka kwenda kila mahali alikotumwa na Sauli, akatenda kwa akili; SAULI AKAMWEKA JUU YA WATU WA VITA; jambo hili likawa jema machoni pa watu wote, na machoni pa watumishi wa Sauli pia.

6 Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda.

7 NAO WALE WANAWAKE WAKAITIKIANA WAKICHEZA, WAKASEMA, SAULI AMEWAUA ELFU ZAKE, NA DAUDI MAKUMI ELFU YAKE.

8 Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme?

9 Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile”.

Hicho ndicho kilichokuwa chanzo, cha vita vya Daudi na anguko la Sauli,. Wanawake wale walikuwa wanasema kweli, kwa waliyoyaona, lakini hawakutumia busara kuimba mbele ya mfalme, kwa wakati ule.. Huwenda hata Daudi, alitamani wakae kimya, wasimsifie yeye zaidi ya mfalme wake, mbele ya umati.. Lakini wale wanawake hilo halikuwa akilini mwao. Hawakujua kuwa kumbe nyimbo zao, sifa zao, maneno yao, ni panga ndani ya mioyo ya wakuu wao.

Ndio ikawa sababu ya Sauli kughahiri, hata vyeo vyote alivyompa Daudi, akampokonya na kumfukuza na kutaka kumuua kabisa, kwa kosa tu la wale wanawake.  Lakini kama wale wanawake wangetumia busara, kumwimbia mfalme zaidi, basi Daudi angeendelea kustarehe na kudumishwa katika ufalme ule.

Maana yake ni nini?

Maneno yoyote ya sifa yanayotoka kinywani mwako wewe kama mwanamke, yana matokeo makubwa sana kwa upande wa pili. Sasa tukirudi katika upande wa ndoa, Wivu unatokea pale ambapo unathamini, au unasifia wanaume wengine zaidi ya mume wako. Ukiwa umeolewa tambua kuwa mume wako ndio,bora kuliko wanaume wote ulimwenguni, ndio mwenye sifa zote kuliko wanaume wote ulimwenguni.Hata kama wale wengine wamemzidi yeye kwa kiwango kikubwa kiasi gani, acha kuwazungumza zungumza mbele ya mume wako.

Hii ni kwa faida yako, na kwa wengine. Wanaume wengi wanagombana na marafiki zao vipenzi, kisa tu wake zao,wanapowasifia, wanakuwa mpaka maadui kwa sababu ndogo ndogo tu kama hizi,..Labda utasikia mmoja anasema, “mume wangu,rafiki yako huwa anapendezaga uvaaji wake, yaani navitiwa nao”..Kauli kama hizi ziepuke kinywani mwako, ili kunusuru, urafiki au ujirani wenu.

Kwa ufupi kauli zozote za sifa, zichungumze mara mbili mbili; Unaweza usione shida yoyote, au ukadhani ni jambo dogo tu, lakini upokee huu ushauri utakufaa kwa siku za mbeleni, , hilo jambo linamuathiri sana mwanaume. Usimzungumze zungumze mwanaume mwingine mbele ya mumeo, isipokuwa kwa kiasi, hata wale unaowaona kwenye tv, au unaowasiliana nao kwenye simu. Kumbuka wivu unawashwa na mambo madogo sana.

Bwana akubariki.

Je! Umeokoka? Je! Unauhakika wa maisha yako ya milele baada ya kifo? Kumbuka Kristo yupo mlangoni kurudi, dalili zote zimeshatimia, Huu si wakati wa kumbelezewa tena wokovu, ni wakati wa kujitahidi kuingia ndani ya Safina(Yesu Kristo) kwa nguvu zote, maana muda umekwisha.. Tubu dhambi zako, ukabatizwe mgeukie Bwana akupe uzima wa milele.

Maran Atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Pale mwanandoa mmoja anaposhindwa kutimiza wajibu wake ufanyaje?

KWANINI NDOA NYINGI ZINAVUNJIKA? (Sehemu ya 1: Upande wa wanaume)

KWANINI NDOA NYINGI ZINAVUNJIKA? (Sehemu ya 2: Upande wa wanawake)

WANA-NDOA: Baba Mkwe, Na mama Mkwe.

MISTARI YA BIBLIA KUHUSU NDOA.

Ndoa ya serikali ni halali?

Rudi nyumbani

Print this post