Category Archive Mafundisho

TUYASHIKE SANA MAUNGAMO YETU.

Waebrania 4:14  “Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu

Kuungama maana yake ni kukiri kwa wazi jambo fulani mbele ya wote… Katika ukristo tunaungama kwa “kukiri kwa vinywa vyetu kuwa Yesu ni Bwana na mwokozi wa maisha yetu, na kukiri kwa vinywa vyetu kuwa sisi ni wenye dhambi, na kutubu!”.. sawasawa na Warumi 10:10.

Warumi 10:9 “Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.

10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu”.

Biblia inazidi kutufundisha kuwa ni lazima TUYASHIKE MAUNGAMO YETU, maana yake tusikiri tu kwa vinywa na kusahau, bali yale tuliyoyakiri mbele za Mbingu na Nchi, hayo TUYAISHI siku zote za maisha yetu.

Sasa swali tunayashikaje/tunayaishije Maungamo yetu?.

Tusome 1Timotheo 6:12.

1Timotheo 6:12 “PIGA VITA VILE VIZURI VYA IMANI; SHIKA UZIMA ULE WA MILELE ULIOITIWA, ukaungama maungamo mazuri mbele ya mashahidi wengi

 13  Nakuagiza mbele za Mungu anayevihifadhi hai vitu vyote, na mbele za Kristo Yesu, aliyeyaungama maungamo mazuri yale mbele ya Pontio Pilato”.

Kumbe tunayashika Maungamo yetu kwa kuvipiga vita vya Imani, na kushika ule uzima wa milele tulioitiwa!. Hebu tutazame moja baada ya lingine.

1.PIGA VITA VYA IMANI.

Vita vipo vingi, lakini kama wakristo tumeagizwa kupigana vita vya aina moja tu!, NAVYO NI VILE VYA IMANI!. Na vita hivyo hatupambani na wanadamu wenzetu, bali na roho za mapepo na falme zao katika ulimwengu wa roho…

Waefeso 6:11  “Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.

12  Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho”.

Kwa maelezo marefu kidogo kuhusiana na vita hivi vya Imani na jinsi ya kupambana fungua hapa >>> TUZIDI KUWA HODARI KATIKA BWANA.

 2) SHIKA UZIMA WA MILELE.

Yohana 17:2 “kama vile ulivyompa mamlaka juu ya wote wenye mwili, ili kwamba wote uliompa awape uzima wa milele.

3 Na uzima wa milele ndio huu, WAKUJUE WEWE, MUNGU WA PEKEE WA KWELI, NA YESU KRISTO ULIYEMTUMA”.

Uzima wa milele maana yake ni “kumjua sana Mungu na Yesu Kristo aliyemtuma”… Hivyo tunavyodumu katika kutafuta kumjua Mungu na siri iliyopo ndani ya mwanae Yesu Kristo ndivyo uzima wa milele unavyozidi kudumu ndani yetu. Lakini tutakapopunguza kumtafuta Mungu, ndivyo ule uzima wa milele unavyozidi kufifia ndani yetu.

Je unayashika Maungamo yako?.

Bwana atusaidie.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

JINSI YA KUPIGANA MAOMBI YA VITA.

VITA DHIDI YA MAADUI

USIMPE NGUVU SHETANI.

TAFUTA UZIMA WA MILELE NA SI UZIMA TU!.

Kuungama ni nini?

Rudi nyumbani

Print this post

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 14 (Yoeli, na Obadia).

Jina Kuu la ukombozi wa roho zetu, (Jina la YESU KRISTO) lihimidiwe daima!

Karibu katika mwendelezo wa uchambuzi wa vitabu vya biblia, tumekwisha kuvitazama vitabu kadhaa vya nyuma na leo tutavitazama vitabu vitatu vya mbele, ambavyo ni kitabu cha Yoeli, Amosi na Obadia. Hivyo ni vizuri kwanza kusoma vitabu hivi mwenyewe katika biblia, ndipo ukapitia uchambuzi huu, na kumbuka uchambuzi huu ni ufupisho tu!, na si wa kutegemea kama darasa kamili au ufunuo kamili wa vitabu hivi, hivyo ni muhimu sana kusoma biblia na kumruhusu Roho Mtakatifu afunue, ndipo masomo mengine yafuate juu yake.

Ikiwa bado hujavipitia vitabu vya awali, ni vizuri ukavipitia kwanza kabla ya vitabu hivi ili tuweze kwenda pamoja.

KITABU CHA YOELI:

Kitabu cha Yoeli, ni kitabu cha 29 katika orodha ya vitabu vya agano la kale, na kimeandikwa na Nabii Yoeli mwenyewe, mapema katika karne ya 8 kabla ya Kristo, kipindi cha Mfalme Uzia wa Yuda, na maana ya jina “Yoeli” ni “Yahwe ni Mungu”.  

Kitabu cha Yoeli kina Milango (Sura) tatu tu!, na kila sura/mlango una ujumbe tofauti.

Yoeli: Mlango wa kwanza.

Katika mlango wa kwanza Nabii Yoeli, anaelezea madhara yaliyoletwa na Nzige, na parare, na madumadu waliotokea Israeli. Historia inaonyesha kipindi cha miaka kadhaa kabla ya Yoeli kuandika kitabu hiki, kulitokea Janga ambalo lililetwa na Mungu kutokana na maasi.

Na janga hilo lilikuwa la Kuzuka kwa Nzige, parare na madumadu ambao walikula mazao yote, na kutokusaza chochote, Uharibifu wa Nzige hao uliwashangaza wote, kwani walikula mazao yote.

Na baada ya pigo hilo, ndipo Mungu anampa Nabii Yoeli ujumbe wa kuwaambia watu wake, kwamba watafakari hayo yaliyotokea, na wapate akili, na kutubu,.. watafakari jinsi wadudu hao walivyoharibu mazao kiasi kwamba makundi yote ya watu waliathirika, mpaka makuhani pia waliadhirika kwani hakikupatikana hata cha kutoa katika nyumba ya Mungu, maana yake zile sadaka za unga zilizokuwa zinatolewa ndani ya hekalu hazikutolewa tena..(Yoeli1:9).

Yoeli 1:1 “Neno la Bwana lililomjia Yoeli, mwana wa Pethueli. 

2 Sikieni haya, enyi wazee; Sikilizeni, enyi wenyeji wote wa nchi. Je! Mambo haya yamekuwako katika siku zenu, Au katika siku za baba zenu? 

3 Waarifuni watoto wenu habari yake, Watoto wenu wakawaambie watoto wao, Na watoto wao wakakiambie kizazi kingine.

4 Yaliyosazwa na tunutu yameliwa na nzige; na yaliyosazwa na nzige yameliwa na parare; na yaliyosazwa na parare yameliwa na madumadu. 

5 Levukeni, enyi walevi, mkalie; Pigeni yowe, ninyi nyote mnywao divai; Kwa sababu ya divai mpya; Maana umekatiliwa mbali na vinywa vyenu. 

6 Maana taifa limepanda juu ya nchi yangu, Lenye nguvu, tena halina hesabu; Meno yake ni kama meno ya simba, Naye ana magego ya simba mkubwa. 

7 Ameuharibu mzabibu wangu; ameuvunja mtini wangu; ameyaambua magamba yake kabisa; ameuangusha chini; matawi yake yamefanywa kuwa meupe”.

Kutokana na pigo hilo la Nzige, Mungu anawaita watu wake wote watubu!, ikiwemo makuhani, wafunge kwa kulia na kuomboleza, na tena wafunge katika saumu ya kweli (Yoeli 1:13-14).

Yoeli: Mlango wa 2.

Katika mlango wa Pili, Mungu analifananisha jeshi hilo la Nzige na jeshi atakalolinyanyua la watu ambao watavamia Israeli na kuharibu watu na vitu, kwa jinsi hiyo hiyo ya Nzige walivyoharibu mazao! Kwasababu ya maasi ya Israeli. Hivyo anazidi kuwaasa watubu!, kwa kupiga mbiu kwa watu wote, kwani jeshi hilo la watu ambao Bwana analifananisha na nzige litakapopita litapageuza Israeli jangwa (Yoeli 2:3), na Mungu atalipa uwezo wa kuharibu kwa uharibifu mkuu (Soma Yoeli 2:4-10).

Lakini katika Mstari wa 12, Bwana anarudia kutoa shauri la kutubu! Ili aiponye nchi kutokana na pigo la nzige, waliokula mazao, vile vile kwa pigo ambalo atakwenda kulipiga Taifa hilo kwa jeshi la watu wabaya atakaowatuma kuwadhuru.

Yoeli 2:12 “Lakini hata sasa, asema Bwana, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea;

 13 rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie Bwana, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya. 

14 N’nani ajuaye kwamba hatarudi na kugeuka, na kutuachia baraka nyuma yake, naam, sadaka ya unga, na sadaka ya kinywaji, kwa Bwana, Mungu wenu?

15 Pigeni tarumbeta katika Sayuni, Takaseni saumu, kusanyeni kusanyiko kuu; 

16 Kusanyeni watu, litakaseni kusanyiko, Kusanyeni wazee, kusanyeni watoto, Na hao wanyonyao maziwa; Bwana arusi na atoke chumbani mwake, Na bibi arusi katika hema yake.

17 Hao makuhani, wahudumu wa Bwana, na walie Kati ya patakatifu na madhabahu, Na waseme, Uwaachilie watu wako, Ee Bwana, Wala usiutoe urithi wako upate aibu, Hata mataifa watawale juu yao; Kwani waseme kati ya watu, Yuko wapi Mungu wao?

Mstari wa 17-32: (Ahadi ya kuponywa miaka ya njaa)

Bwana anatoa ahadi ya marejesho ya chakula katika miaka iliyoliwa na parare na nzige (katika pigo la Nzige). endapo watatubu!

Yoeli 2:25 “Nami nitawarudishia hiyo miaka iliyoliwa na nzige, na parare, na madumadu, na tunutu, jeshi langu kubwa nililotuma kati yenu. 

26 Nanyi mtakula chakula tele na kushiba, na kulihimidi jina la Bwana, Mungu wenu, aliyewatendea mambo ya ajabu; na watu wangu hawatatahayari kamwe.

27 Nanyi mtajua ya kuwa mimi ni katikati ya Israeli, na ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu, wala hakuna mwingine; na watu wangu hawatatahayari kamwe”.

Lakini haiishii tu kutoa ahadi ya kuponya miaka iliyoliwa na Nzige, bali pia Bwana anatoa ahadi nyingine ya kipekee ya kuwabariki watu katika roho, (yaani kuwamwagia Roho wake Mtakatifu).

Yoeli 2:28 “Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono;

29 tena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina roho yangu”.

Mlango wa 3 wote unahusu ahadi ya Bwana ya kuwapigania Israeli dhidi ya majeshi yaliyowaonea, baada ya wao kutubu, na kumrudia yeye.

Sasa tukirudi katika biblia, tunasoma baada ya Nabii Yoeli kuondoka, Israeli hawakutubu kikamilifu, ijapokuwa walipigwa na janga hilo la Nzige, na parare na madumadu na tunutu..lakini waliendelea kuwa vile vile, mpaka Bwana alipotimiza neno lake hilo la kuleta jeshi la watu ambao wataharibu nchi mfano wa hao nzige waliotangulia, na jeshi halikuwa lingine Zaidi ya lile la Wakaldayo, ambalo Bwana Mungu aliliruhusu lifike Yuda na kuharibu hekalu na kuwaua wayahudi wengi na baadhi yao kuwachukua utumwani Babeli.

Na kule utumwani walikaa miaka 70, na baada ya ile miaka 70, Danieli alisimama kutubu kwa niaba yao baada ya kuujua unabii wa Yeremia kuhusu muda wao wa kukaa utumwani, na waliporejea Bwana aliwapa majuma 69 (ambayo ni miaka 483) ya kuujenga Yerusalemu kabla ya kutimiza ahadi yake ya kumwanga Roho Mtakatifu.

Na miaka hiyo ilipotimia Bwana aliachilia Roho wake mtakatifu sawasawa na ahadi yake aliyoiahidi, katika Yoeli 2:28, ambapo ilitimia ile siku ya Pentekoste (Matendo 2:17).

Matendo 2:14  “Lakini Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia, Enyi watu wa Uyahudi, na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, lijueni jambo hili, mkasikilize maneno yangu.

15  Sivyo mnavyodhani; watu hawa hawakulewa, kwa maana ni saa tatu ya mchana;

16  lakini jambo hili ni lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli,

17  Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto.

18  Naam, na siku zile nitawamwagia watumishi wangu wanaume na wanawake Roho yangu, nao watatabiri”.

Na mpaka leo hii Roho Mtatifu yupo, na ndiye Muhuri wa Mungu juu ya mtu (Warumi 8:9, Waefeso 4:30, 2Wakorintho 1:22).

Kwa undani Zaidi kuhusiana na wadudu hawa (parare, nzige, madumadu na tunutu) na ujumbe gani wa ziada wamebeba kiroho, fungua hapa >>>Nzige, Parare, madumadu na tunutu ni wadudu gani? (Yoeli 2:25)?

KITABU CHA OBADIA:

Kitabu cha Obadia ni kitabu kilichoandikwa na Nabii Obadia mwenyewe, na kina Mlango mmoja tu!, hivyo kukifanya kuwa kitabu kifupi kuliko vitabu vyote vya agano la kale. Maana ya jina ‘Obadia’ ni “Mtumishi wa Bwana”.

Kitabu cha Obadia kinahusu Hukumu Mungu alioitangaza juu ya Taifa la Edomu (Nchi ya Edomu sasahivi ni maeneo ya kusini-magharibi mwa nchi ya Yordani).

Kwaasili Edomu ulikuwa ni urithi wa Esau aliyekuwa ndugu yake Yakobo! (Mwanzo 25:30 na Mwanzo 36:8)... Na tangu Esau na Yakobo wakiwa tumboni mwa mama yao, walikuwa wakipambana!.

Mwanzo 25:22 “Watoto wakashindana tumboni mwake. Naye akasema, Ikiwa ni hivi, kuishi kwanifaa nini? Akaenda kumwuliza Bwana.

23 Bwana akamwambia,Mataifa mawili yamo tumboni mwako,Na kabila mbili za watu watafarakana tangu tumboni mwako.Kabila moja litakuwa hodari kuliko la pili,Na mkubwa atamtumikia mdogo. 

24 Siku zake za kuzaa zilipotimia, tazama! Mapacha walikuwamo tumboni mwake”

Kutokana na unabii huo wa Esau kupambana na Israeli, ulifika wakati kiburi cha wana wa Esau (Edomu) kilinyanyuka kwa kiwango kikubwa..kwani walijinyanyua mbele za Mungu na kufanya dhambi na vile vile kuwafanyia mabaya makubwa wana wa ndugu yao Yakobo (yani wana wa Israeli). Na hivyo Mungu kutamka hukumu juu yao kwa kinywa cha Nabii wake Obadia.

Obadia 1:1 “Maono yake Obadia. Ndivyo asemavyo Bwana MUNGU juu ya Edomu; Tumepata habari kwa Bwana, Na mjumbe ametumwa kati ya mataifa, Akisema,Haya,inukeni ninyi;Na tuinuke tupigane naye. 

2 Tazama, nimekufanya mdogo kati ya mataifa; Umedharauliwa sana. 

3 Kiburi cha moyo wako kimekudanganya, Wewe ukaaye katika pango za majabali, Mwenye makao yako juu sana; Asemaye moyoni, Ni nani atakayenishusha mimi? 

4 Ujapopanda juu kama tai, Ijapokuwa kioto chako kimewekwa kati ya nyota, Nitakushusha kutoka huko; asema Bwana”.

Lakini mbali na hilo, historia inaonyesha kuwa kipindi Wakaldayo wameuhusuru Yerusalemu na baadaye kuivamia na kuharibu mali, wana wa Edomu walishirikiana na wakaldayo kushirikiana nao, na hata kuchukua mali nyingi za wana wa Israeli, sawasawa na unabii huo alioutoa Obadia miaka mingi kabla ya wana wa Israeli kuchukuliwa utumwani..

Obadia 1:11 “Siku ile uliposimama upande, siku ile wageni walipochukua mali zake, na watu wa kabila nyingine walipoingia katika malango yake, na kumpa kura juu ya Yerusalemu, wewe nawe ulikuwa kama mmoja wao”. 

Hivyo kwa kosa hilo na mengine ambayo hayajatajwa katika biblia, Bwana Mungu alitangulia kuwaonya lakini hawakutubu, hivyo ulipofika wakati Edomu iliadhibiwa sawasawa na hukumu hiyo, lakini pia iliyopo sasa itakuja kuadhibiwa katika vita vya mwisho vya Ezekieli 38.

Maelezo kwa kina kuhusu Edomu fungua hapa >>>Edomu ni nchi gani kwasasa?

Na baada ya Bwana kuiadhibu Edomu, kutokana na mabaya waliyoifanyia Israeli, Bwana anatoa ahadi ya kuijenga Yerusalemu, baada ya ubaya wao kupita.

Obadia 1:18 “Na nyumba ya Yakobo itakuwa moto, na nyumba ya Yusufu itakuwa mwali wa moto, na nyumba ya Esau itakuwa mabua makavu, nao watawaka kati yao, na kuwateketeza; wala hatasalia mtu awaye yote katika nyumba ya Esau; kwa kuwa Bwana amesema hayo”.

Ni nini tunajifunza katika kitabu hiki cha Obadia?..

Tunachoweza kujifunza kikubwa ni kwamba Mungu anatoa unabii unaokuja kama onyo!, ili yamkini mtu au Taifa lisije kuangukia katika hukumu ya Mungu, Watu wa Edomu walipewa unabii huu kama ushauri kwamba wakati wa msiba wa Israeli wasishirikiane na watu wakaldayo, na onyo hilo walipewa miaka mingi kabla ya Israeli kuja kuvamiwa na wakaldayo, lakini hawakutii unabii huo, na wakafanya waliyoyafanya na leo hii hawapo!.. Wanaoishi Edomu sasa si wana wa Esau bali wana wa Ishmaeli, ambao kulingana na unabii wa kibiblia watafutwa katika vile vita vya Ezekieli 38, na 39, kama walivyofutwa hawa wana wa Edomu.

Na sisi vile vile hatupaswi kutweza unabii (yaani kudharau unabii wa kibiblia). Unabii wa biblia unasema kuwa siku za mwisho watatokea watu wa dhihaka, watu wasiotii wazazi wao, wakaidi, wasiotaka kufanya suluhu, watukanani n.k (soma 2Timotheo 3:4), na kwamba watu wa namna hii hawataurithi ufalme wa Mungu.

Sasa unabii huu ni kweli utatimia, hivyo si wa kuutweza/kuupuzia..kwasababu ni kweli siku za mwisho, ambazo ndizo hizi hawa watu wametokea, hivyo hatupaswi kuwa miongoni mwa watakaotimiza unabii huo wa watakaodhihaki na kupotea, badala yake tutimize unabii wa watakaokolewa kwa kumfuata Mungu na kuitii Injili.

1Wathesalonike 5:20 “ msitweze unabii;”

Bwana atusaidie.

Usikose mwendelezo..

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 13 (Kitabu cha Hosea).

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 12 (Kitabu cha Isaya)

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 11 (Mithali, Wimbo ulio bora, Mhubiri)

Vitabu vya Deuterokanoni ni vya kiMungu?

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 5

Rudi nyumbani

Print this post

Ielewe Wafilipi 4:8, Ina maana gani kwa mwaminio

Wafilipi 4:8  Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.

Katika vifungu hivyo utaona neno “yoyote” limetumika sana. Ikiwa na maana yapo mengi, ya aina mbalimbali, ambayo hayajaandikwa hapo.  Na hapo biblia inaegemea katika “yale yaliyo mema”.

Tukumbuke kuwa biblia haijaandika matendo yote mema mwanadamu anayopaswa kuyafanya. Kama ingekuwa hivyo basi kingekuwa ni kitabu kikubwa sana, ambacho hakuna mwanadamu yoyote angeweza kukimaliza kwa kukisoma. Lakini imetoa kama muhtasari tu, au mwongozo wa kufuata.

Kwamfano huwezi, kuona katika maandiko tunaagizwa ‘tuimbe kwaya kanisani’, lakini hayo ni moja na yenye kupendeza, au kuona tunaambiwa tuhubiri injili kwa njia ya maigizo. Lakini, tumebuni wenyewe na mwenye dhambi anapotizama filamu hizo, huwa inachangia katika kuwasogeza karibu kwa Kristo. Maadamu havitoki nje ya maudhui mema.

Au tunapotumia vipaza sauti, au tunaposambaza vipeperushi vya injili barabarani, huwezi ona agizo hilo, popote kwenye maandiko. Lakini ni moja ya yale yaliyo ya kweli.

Hivyo kwa hitimisho ni kuwa yapo mambo mengi ambayo tunaweza kuyafanya, na Bwana hatuzuii kuyatafakari, ndio maana akamalizia kwa kusema ‘yatafakari hayo’. Maana yake tutafiti na tutumie njia zote, ambazo tunaona hatma yake itakuwa ni kuujenga ufalme wa Mungu, au kuufanya upendeze zaidi.

Angalia katika ujuzi wako, angalia katika elimu yako, ni kwa namna gani utafanya jambo la ki-Mungu lenye kukuletea sifa njema kwake. Utumishi wa Mungu sio pale madhabahuni tu kuhubiri, utumishi wa Mungu ni mpana. Hivyo Hapo hapo ulipo tafakari  ni kwa namna gani utaujenga ufalme wa Mungu wako, na Bwana atakupa akili njema.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618 Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mafundisho mengine:

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA KITABU CHA TITO.

Nini maana ya kikombe cha maji ya baridi(Mathayo 10:42)?

Mambo yale yaliyo mbali, na yale yaendayo chini sana,

NAFASI YAKO NI IPI KATIKA MWILI WA KRISTO?

Matulizo ya mapenzi ni nini? (Wafilipi 2:1).

Birika ni nini?, na yale Matao matano katika birika la Bethzatha ni nini?

REKEBISHA YAFUATAYO ILI MAMBO YAENDE SAWA.

Rudi nyumbani

Print this post

Je agano la kale litatoweka kabisa kulingana na Waebrania 8:13?

Jibu: Tusome,

Waebrania 8:13 “Kwa kule kusema, Agano jipya, amelifanya lile la kwanza kuwa kuukuu. Lakini kitu kianzacho kuwa kikuukuu na kuchakaa ki karibu na kutoweka”.

Neno “kuukuu” maana yake ni “kitu kilichochakaa/ kilichoisha muda wake”.. Hivyo hapo biblia inaposema kuwa Agano la kwanza amelifanya kuwa kuukuu tafsiri yake rahisi ni kwamba “Agano la kwanza yaani lile la kale amelifanya kuwa chakavu (lililoisha muda wake)/ lisilofaa tena”.

Lakini swali ni je!.. kupitia mstari huo inamaanisha kuwa Agano la kale litapotea kabisa na halitatumika?…kiasi kwamba halifai tena wala halitatumika?

Jibu ni la! Bwana Yesu alisema mwenyewe kuwa “hakuna yodi moja wala nukta moja ya torati itakayoondoka (soma Mathayo 5:18)”… Na Zaidi sana alisema hakuja kuitangua torati bali kuitimiliza.

Mathayo 5:17 “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza.

18  Kwa maana, amin, nawaambia ,Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka,yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka ,hata yote yatimie”.

Sasa swali linarudi pale pale kama hivyo ndivyo kwamba Bwana YESU hakuja kuitangua torati bali kuitimiliza, na kwamba agano la kale bado litaendelea kuwepo, ni kwanini hapo katika Waebrania 8:13 biblia iseme kuwa litatoweka kabisa?. Je! Biblia inajichanganya??

Jibu ni La! biblia haijichanganyi bali tafakari zetu ndizo zinazojichanganya!.

Ili tuelewe vizuri tutafakari mfano ufuatao.

Kampuni moja limetoa aina Fulani la gari, na aina hiyo ya gari ikatumika kwa miaka kadhaa, lakini baada ya miaka 10 ikatoa toleo lingine jipya la aina ile ile ya gari, na hivyo kampuni hilo likaacha kuzalisha lile toleo la kwanza lililo dhaifu na kujikita katika uzalishaji wa toleo jipya.

Sasa ni wazi kuwa kwa jinsi miaka inavyozidi kwenda lile toleo la kwanza litaenda kupotea kabisa na kubaki hili la pili… kwa lugha nyepesi tunaweza kusema kuwa… “Kampuni lile limelifanya toleo la kwanza kuwa kuu, na hivyo lipo karibuni kutoweka kabisa”.

Lakini kwa kutoa toleo jipya haimaanishi kuwa limelipinga lile la kwanza, kwamba badala ya kuzalisha magari sasa linazalisha treni. Hapana! Bali kinyume chake limeliimarisha lile la kwanza, ikiwa na maana kuwa kama tairi za toleo la kwanza zilikuwa dhaifu, basi toleo la pili limeziongezea uimara, lakini gari ni lile lile, vile vile  kama mwonekano wa toleo la kwanza ulikuwa si mzuri basi toleo la pili limeongeza uzuri wa kimwonekano lakini gari ni lile lile.

Na ndivyo katika habari ya agano jipya na lile la kale, Hakuna kilichoondolewa, na kuletwa kingine kipya, bali ni kile kile kilichokuwepo kimeimarishwa Zaidi, kuwa bora Zaidi, kuwa imara Zaidi, kuwa chenye uwezo Zaidi n.k

Kwamfano biblia inasema katika mojawapo ya amri katika agano la kale kuwa “usizini” ikaishia hapo… Sasa hii amri ilikuwa ni dhaifu, kwasababu inasema usizini tu!, mtu anaweza asizini kweli lakini moyoni mwake akalipuka tamaa..

Lakini sasa Bwana YESU aliye mjumbe wa agano jipya anakuja kuitimiliza amri hiyo kuwa “mtu amtazamaye mwanamke kwa kumtamani amekwisha kuzini naye nafsini mwake”. Hata kabla ya kwenda kufanya kile kitendo.

Mathayo 5:27  “Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini;

28  lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake”

Na vile vile katika amri ya “kuua” ni hivyo hivyo…(soma Mathayo 5:21-22).

Kwahiyo kwa lugha nyepesi ni kwamba Agano la pili ni toleo jipya la Agano la kwanza. Lakini mambo ni yale yale.

Sasa swali lingine.. Ni wakati gani ambapo agano la kale lilianza kuwa kuu kuu?

Jibu: Ni wakati wa kuja kwa Bwana Yesu kwa mara ya kwanza.

Kipindi Bwana Yesu alipokuja, yeye ndiye mwanzilishi wa agano jipya, na kuanzia huo wakati ndio agano la kale katika maarifa yake machanga lilipoanza kuisha muda wake, na mpaka leo hatulitumii tena, limetoweka! Na nguvu katika damu ya Yesu ndani ya agano jipya inatawala.

Ndio maana maarifa machanga ya agano la kale, mfano matumizi ya damu za wanyama kama sadaka za kafara zimebaki kutumiwa na watumishi wa shetani, na katika ukristo Damu ya Yesu ndio utimilifu wa Torati za kafara. Na yeyote anayetumia kafara za wanyama leo hii, awe anajiita mtumishi wa Mungu au mtu yeyote yule anafanya ibada za miungu.

Kwahiyo leo hii katika ukristo hatuna matambiko, wala kafara za wanyama, wala utakaso kupitia damu za wanyama, wala hatuishi kwa kujizuia kuua lakini mioyoni tuna hasira, au tamaa.. bali tunaishi kwa Roho mtakatifu na tunamuabudu Mungu katika roho na kweli.

Bwana atubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

MJUMBE WA AGANO.

Je! waliokufa kabla ya Bwana Yesu wataokolewaje?

LISHIKILIE SANA LILE AGIZO LA KWANZA.

Tofauti kati ya ufalme wa mbinguni na ufalme wa Mungu ni ipi?

Kiti cha Rehema kilikuwaje? (Kutoka 40:20)

Rudi nyumbani

Print this post

Fahamu maana ya Mhubiri 10:9 Mwenye kuchonga mawe ataumizwa kwayo;

SWALI: Nini maana ya Mhubiri 10:9 Mwenye kuchonga mawe ataumizwa kwayo; Naye apasuaye miti huona hatari katika hiyo.


JIBU: Mstari huu unatuonyesha hatari ya kazi yoyote inayotendwa na mtu. Hapo ametumia mfano wa wanaochonga mawe. Wajenzi wa zamani walikwenda kuchonga mawe miambani kwa ajili ya ujenzi wa majengo yao, lakini wakiwa kule walikutana na hatari nyingi, aidha kuangukiwa na mawe hayo, na kuwaponda viungo vyao, vifaa vyao  vya uchongaji kuwajeruhi.

Vilevile anatumia tena mfano wa wanaopasua miti, kwa ajili ya mbao za ujenzi, bado na wao pia wanakutana na hatari, aidha kuangukiwa na miti yenyewe, au shoka kuteleza na kumjeruhi mtu au yeye.

Kumbukumbu 19:5 kama aingiapo mtu na mwenziwe mwituni kwenda kukata kuni, akapeleka mkono wake na shoka ili kukata mti, likatoka shoka katika mpini, likampiga yule mwenziwe hata akafa; basi na akimbilie katika miji hii mmojawapo awe hai.

Ni sawa na mjenzi ambaye amezoea kupiga sana nyundo au kuwepo maeneo ya ujenzi muda wake mwingi, utaona upo wakati nyundo itateleza na kumponda kidole chake, au atakanyaga msumari n.k. Tofauti na kama angekuwa hajishughulishi na kazi hiyo yupo nyumbani tu.

Hii ni kufunua nini rohoni?

Kama wana wa Mungu tufahamu kuwa kazi yake ya kwenda kung’oa mapando ya mwovu, katika shamba la Bwana  tutarajie kukutana na madhara yake, si wakati wote utakuwa ni mwepesi tu (yaani kuvuna), zipo nyakati tutakutana na kupigwa, au kudhalilishwa, au kufungwa na wakati mwingine hata kuuawa. (Mathayo 10:17-19)

Mtume Paulo alipokuwa katika ziara zake za kupanda ukristo Asia na Ulaya, alikutana na hatari nyingi, ikiwemo kupigwa mawe na watu wabaya, kufungwa, na kurushiwa vitisho mbalimbali. Wamishionari kama dr David Livingstone walioleta injili Afrika zamani walikutana na hatari za magonjwa kama malaria, na wanyama wakali.

Lakini katika yote, Bwana ameahidi, mafanikio makubwa,  kuliko hatari zake. Hivyo hatupaswi kuogopa na kudhani kuwa kazi ya Mungu ni kazi ya kwenda kujichinja wakati wote. Hapana, zipo nyakati nyingi za raha, na mafanikio makubwa ya rohoni yasiyokuwa na ghasia yoyote, lakini Bwana hajatuficha pia hatari zake wakati mwingine. Ili tutakapokutana nazo tusihuzunike moyo na kukata tamaa, bali tuendelee na kazi.

Bwana akubariki.

Je! Umeokoka? Je! Umesamehewa dhambi zako? Kama ni la, ni nini kinachokusubirisha? Ukifa leo utakwenda wapi, kumbuka lipo ziwa la moto, kumbuka ipo hukumu kwa waovu. Tubu leo mgeukie Kristo akusafishe dhambi zako,  Ukabatizwe katika jina la Yersu Kristo upokee ondoleo la dhambi. Hizi ni siku za mwisho, Kristo anakaribia kurudi.

Ikiwa upo tayari leo kufanya hivyo basi fungua hapa kwa mwongozo huo>>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618. Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mafundisho mengine:

Yeye abomoaye boma, nyoka atamwuma.

Je! fedha ni jawabu la mambo yote? (Mhubiri 10:19).

TUUTAFUTE UMOJA WA ROHO.

Fahamu maana ya Mithali 28:20 Mtu mwaminifu atakuwa na baraka tele;

NI KWA NAMNA GANI SHETANI ANAIZUIA INJILI?

FANYA MAAMUZI KABLA HAZIJAKARIBIA SIKU ZA HATARI.

Rudi nyumbani

Print this post

Je! fedha ni jawabu la mambo yote? (Mhubiri 10:19).

Jibu: Tusome,

Mhubiri 10:19 “Karamu hufanywa kwa ajili ya kicheko, Na divai huyafurahisha maisha; NA FEDHA HULETA JAWABU LA MAMBO YOTE”.

Kulingana na huu mstari je ni kweli fedha ni jawabu la kila kitu?.

Jibu ni La! Fedha haitoi jawabu la mambo yote, kama ndio basi fedha ingeweza kununua uzima wa milele, hivyo kusingekuwa na haja ya Bwana Yesu kutoa uhai wake kwaajili ya uzima wa roho zetu.

Lakini biblia inatufundisha kuwa tumekombolewa kwa damu ya Yesu na si kwa fedha.

1 Petro 1:18 “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu

19 bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo”.

Vile vile fedha haiwezi kutibu kifo, wala kununua amani, kwasababu wapo watu wenye pesa nyingi lakini hawana amani n.k.

Lakini kama hivyo ndivyo kwamba fedha si jawabu la mambo yote, kwanini biblia iseme ni jawabu la mambo yote?.

Ili kupata jibu la swali hili ni vizuri tukausoma mstari huo kwa kutafakari kwa kina sehemu za kwanza za mstari huo na zile za mwisho.

Mstari huo unaanza kwa kusema.. “Karamu hufanywa kwa ajili ya kicheko” na unaendelea kwa kusema… “Na divai huyafurahisha maisha”…na unamalizika kwa kusema “NA FEDHA HULETA JAWABU LA MAMBO YOTE”.

Sasa swali ni mambo gani hayo ambayo fedha inaleta majibu yake?.

Jibu: Ni mambo hayo yanayotajwa hapo juu, maana yake yahusuyo karamu hizo ziletazo kicheko zenye ulevi…. na si mambo mengine tofauti na hayo.

Na kweli mambo ya kidunia karibia yote jawabu lake ni fedha, maana yake ukiwa na fedha utaweza kuyafanya au kuyapata, na ukizikosa fedha pia unaweza kuyakosa.

Anasa zote za kidunia zinahitaji pesa, na wanaotaka anasa wanazitafuta pesa kwasababu hilo ndio jibu lake.

Lakini wana wa Mungu, hawaishi kwa fedha wala fedha si jawabu la mambo yao yote…bali Damu ya Yesu ndio jawabu la mambo yao yote.

Wana wa Mungu hata pasipo pesa wanaweza kuishi vizuri kabisa, na pia hawana tabia ya kupenda fedha, bali fedha yao ni Damu ya Yesu katika Roho Mtakatifu.

Je upo ndani ya agano la damu ya Yesu au Mungu wako ni fedha?.

Waebrania 13:5 “Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa”

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

Aibusu midomo atoaye jawabu la haki (Mithali 24:26)

KUOTA UNAPEWA PESA, KUNA MAANISHA NINI?

Pesa za bindoni ni nini?(Marko 6:8)

MFANO WA MAMBO HAYO NI UBATIZO.

KANUNI YA KUOMBA NA KUPOKEA.

Rudi nyumbani

Print this post

Je ni sawa kuomba novena ya Mtakatifu Rita wa Kashia?

Mtakatifu Rita, ambaye kwa kanisa katoliki anajulikana pia kama ‘mwombezi wa mambo yasiyowezekana’, na ‘mfanya miujiza’.

Ni mama aliyezaliwa mwaka 1381, katika mji unaitwa Kashia, taifa la Italy. Aliolewa akiwa na umri mdogo lakini baada ya mume wake na watoto wake wawili  kufa aliamua kujiunga na utawa, ijapokuwa alipitia changamoto, kujiunga na jamii hiyo kwasababu tayari alikuwa ameshaolewa(sio bikira), lakini mwishoni alifanikiwa.

kulingana na kanisa katoliki maombi ya Rita yaliwaletea wengi majibu, lakini pia alitambulika kwa jeraha dogo kwenye kipaji cha uso wake, wakiamini kuwa ni alama ya ukristo, kufuatana na mateso ya Yesu msalabani, mahali alipowekewa taji ya miiba. Alikufa kati ya umri wa miaka  75-76.

Na ilipofika tarehe 24 May 1900, papa Leo XIII, Alimtangaza kuwa mtakatifu. Yaani ukitangazwa kuwa mtakatifu, unakidhi vigezo vya kuwa mwombezi wa walio hai.

Tangu huo wakati wakatoliki wengi duniani wamekuwa wakimfanyia novena, na litania. Na wengi wakishuhudia kuwa matatizo yao sugu, yakitatuliwa, hivyo imemfanya kuwa maarufu sana.

Lakini Je! Jambo hili ni kweli? Ni vema kufahamu kuwa katika maandiko matakatifu (BIBLIA), Hakuna mahali popote, tunafundishwa kuwa watakatifu waliokufa zamani au sasa wanaweza kutuombea. Zaidi sana wanakuwa hawaelewi neno lolote linaloendelea duniani, biblia inasema hivyo katika;

Mhubiri 9:5 kwa sababu walio hai wanajua ya kwamba watakufa; lakini wafu hawajui neno lo lote, wala hawana ijara tena; maana kumbukumbu lao limesahauliwa.

Umeona? Kwahiyo desturi hii, ya kupeleka maombi yetu kwa watakatifu watuombee, ni ya kipagani, Ni ibada za sanamu,  ambayo asili yake ilianzia kwenye dini zinazoamini mizimu inaweza kuwasiliana nasi. Kusema hivi haimaanishi tunawapinga wakatoliki, au tunatangaza chuki hapana, bali tunasemezana ukweli ili tupone, kwasababu safari yetu ni moja sote tuurithi uzima wa milele, sisi tunasema ni wakristo.

https://www.high-endrolex.com/11

Haijalishi utakuwa ulifanya novena ya Rita ikakuletea majibu kiasi gani, bado ni ibada ya sanamu, kumbuka pia shetani analeta majibu, si ajabu mambo hayo kutendeka, ili watu wapumbazike katika hayo.

2Wakorintho 11:14  Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru.

Mwombezi wetu ni mmoja tu naye ndiye YESU KRISTO (1Yohana 2:1). Lakini sio pamoja na Petro, au Paulo, au Eliya, au Mariamu, au Yusufu. Hao wote ni watakatifu ambao walihitaji ukombozi tu kama sisi, na wenyewe walituelekeza kumtazama Yesu Kristo, na sio wao.

Mtume Paulo alisema maneno haya;

1Wakorintho 1:13  Je! Kristo amegawanyika? Je! Paulo alisulibiwa kwa ajili yenu? Au je! Mlibatizwa kwa jina la Paulo?

Hivyo hakuna haja ya kupeleka maombi yako kwa mtakatifu yoyote, na vilevile wale walio kule hawawezi kutuombea sisi pia. Halikadhalika wewe huwezi kumwombea mwenye dhambi aliyekufa, kwamba Bwana amtoe matesoni. Imani hiyo haipo pia katika biblia. Soma (Waebrania 9:27). Mafundisho ya watu kupitia toharani hayapo katika biblia.

Tujifunze kusoma biblia tutafunguka kwa mengi, mapokeo ya kidini sio Neno la Mungu. Hao wanaoabudu miti na mawe twaweza kuwacheka, lakini tukawa kama wale tu isipokuwa katika mfumo mwingine, tusipopenda kusoma biblia. Tukikataa kuwa wafuasi tu wa kidini tukapenda Neno la Mungu, Roho Mtakatifu atatusaidia kufunguka kwa mengi.

Hivyo ikiwa wewe ulikuwa ni mmojawapo wa wanaopeleka maombi kwa Rita wa kashia, au  kwa mtakatifu mwingine yoyote acha sasa kufanya hivyo. Tubu dhambi ukabatizwe, upokee Roho Mtatakatifu ambaye atakuongoza na kukutia katika kweli yake yote(Yohana 16:13).

Ikiwa upo tayari leo kuokoka, basi waweza fungua hapa kwa ajili ya mwongozo wa sala ya Toba >>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618 Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mada Nyinginezo:

Novena ni nini? Na je ipo kibiblia?

Roho Mtakatifu ni nani?.

LITANIA YA BIKIRA MARIA JE! NI SALA YA KIMAANDIKO?

KUNA AINA NGAPI  ZA MAOMBI?

Kuomba katika roho ni kupi? na je nifanye nini ili niweze kuomba hivyo?

SISI TU MANUKATO YA KRISTO.

MLANGO MWINGINE WA ADUI KUTULETEA MAJARIBU.

Rudi nyumbani

Print this post

USIKWEPE CHUO CHA UTAKATIFU.

Zawadi kubwa Mungu aliyompa mwaminio ni UTAKATIFU. 

Utakatifu ni ile hali ya kuwa mkamilifu kama Mungu, kutokuwa na dosari au kasoro yoyote, msafi asilimia mia moja, bila kosa lolote ndani yako. 

Sasa heshima hii tumetunukiwa na Mungu, jambo ambalo hapo zamani halikwepo, ilihitaji matendo ya haki ya Mtu kuufikia, lakini hapakuwahi kutokea mwanadamu yoyote aliyeweza kufikia cheo hicho cha juu sana cha Mungu, yaani kutokuwa na dhambi kabisa.

Lakini pale tunapomwamini Bwana Yesu, siku hiyo hiyo, Mungu anatufanya Watakatifu kama yeye, haijalishi bado tutakuwa na asili ya dhambi nyingi kiasi gani. Hiyo ndio maana ya neema. Tunaitwa watakatifu bila ya kujisumbua kwa lolote.

Lakini sasa lengo la Mungu sio tuwe “watakatifu katika dhambi” Bali “tuwe watakatifu katika utakatifu”. Hivyo kuanzia huo wakati anaanza kumfundisha mtu kuusomea hadi kuuhitimu Utakatifu wake, aliopewa ili aendane na cheo alichotunukiwa tangu mwanzo.

Na hapo mtu akishindwa kupiga hatua, basi anaondolewa heshima hiyo kwake, na hivyo hawezi tena kuwa kama Mungu, na matokeo yake wokovu unampotea.

Mwaka Fulani hapa nchini kwetu kulikuwa na askari mmoja aliyeonyesha kitendo cha kishujaa kukataa rushwa ya milioni 10, ambapo alishawishiwa aipokee ili aifute kesi ya watuhumiwa wawili waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka,. Lakini yeye hakukubali, na ilipokuja kubainika, mkuu wa jeshi la polisi (IGP) akafurahishwa naye, Akampandisha cheo (kwani alikuwa ni askari wa chini). Lakini cha kushangaza baada ya kama miaka miwili tukaja kusikia Yule askari aliyepandishwa cheo ameshushwa cheo kile. Kufuatilia ni kwanini imekuwa hivyo? Jeshi la polisi likatoa taarifa kuwa alionyesha utovu wa nidhani, wa kukataa kwenda kwenye mafunzo ya cheo chake kipya.  Akidhani kwasababu IGP amempandisha basi inatosha hakuna haja ya mafunzo tena. Akasahau kuwa ufahamu wake wa kielimu ni lazima uendane na cheo chake, kwamba akiwa bado na cheo kikubwa, wakati huo huo anapaswa aendelee kusoma,na kujifunza kimatendo, ili aweze kutumika ipasavyo. Lakini akashushwa cheo na kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa kukataa kutii amri ya jeshi.

Ndivyo ilivyo katika UTAKATIFU tunaopewa na Mungu bure, ni lazima tuutendee kazi kwa kila siku kupiga hatua mpya ya mabadiliko. Huwezi kusema umeokoka (wewe ni mtakatifu), halafu maisha yako ya mwaka jana na mwaka huu ni yaleyale wewe sio mtakatifu.  Kila siku lazima uwe na mabadiliko, ulikuwa unabeti, unaacha kubeti, ulikuwa unavaa mavazi ya uchi uchi, unayachoma moto, ulikuwa unajichubua, unaacha, ulikuwa unasengenya unakaa mbali na wasengenyaji, ulikuwa unakesha kwenye muvi usiku kucha unaacha hayo, unatumia muda wako mwingi kwenye kujisomea biblia, ulikuwa ni mtu wa rushwa unaanza kuondoa vitendo hivyo kwenye biashara yako. Ulikuwa huwezi kufunga na kuomba unaanza kujizoeza kuwa mtu wa rohoni, unafunga, unaomba, na kukesha, Huko ndiko Mungu anakokutaka. Anaona umekiheshimu cheo alichokupa.

Ukiwa ni mtu wa kupiga hatua kila siku, basi Mungu atazidi kukuona wewe ni MTAKATIFU na hivyo utakuwa karibu na yeye. Lakini ukiishi hoe hae, hutambuliki kama umeokoka, au vipi, tabia zilezile za zamani unaendelea nazo, wala hujihangaishi kuziondoa. Usijidanganye wewe umeokoka.

Bwana atusaidie..

Je! Upo ndani ya Kristo? Je unataarifa kuwa hizi ni siku za mwisho? Yesu amekaribia kurudi? Ni nini utamweleza Mungu siku ile endapo leo utaukataa wokovu unaoletwa kwako bure..  Tubu dhambi zako, mgeukie Bwana, akupe Roho Mtakatifu, akupe heshimu hiyo ya utakatifu. Hivyo Ikiwa upo tayari kufanya hivyo basi fungua hapa kwa ajili ya mwongozo wa sala ya toba >>>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618 Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mada Nyinginezo:

FUNDISHO KUU LA NEEMA YA MUNGU KWETU.

MATUNDA 9 YA ROHO MTAKATIFU

UTAKASO NI SEHEMU YA MAISHA YA MKRISTO YA KILA SIKU.

USITAZAME NYUMA!

Kwanini hatuirithi neema kama tunavyoirithi dhambi?

HATARI YA KUHUBIRI INJILI TOFAUTI NA ILIYOANDIKWA KWENYE BIBLIA.

Wakili ni nani kibiblia? Uwakili ni nini?

Rudi nyumbani

Print this post

JUA HALITAKUPIGA MCHANA, WALA MWEZI WAKATI WA USIKU.

Nakusalimu katika jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo. Nakukaribisha katika kuyatafakari maneno ya uzima.

Ulishawahi kuutafakari vema huu mstari?

Zaburi 121:5 Bwana ndiye mlinzi wako; Bwana ni uvuli mkono wako wa kuume.  6 Jua halitakupiga mchana, Wala mwezi wakati wa usiku.  7 Bwana atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako.  8 Bwana atakulinda utokapo na uingiapo, Tangu sasa na hata milele.

Ni rahisi kumwelewa mtu anayekuambia, “leo jua limenipiga”, lakini si rahisi kumwelewa mtu anayesema “leo mwezi umenipiga” Ni wazi kuwa utamwona anakuchezea akili.  Si ni kweli?..Lakini hapa katika vifungu hivi ambavyo Mungu anaeleza ulinzi wake kwa watu wake jinsi ulivyo, anatumia mifano hiyo miwili  ya jua na mwezi. Na anaonyesha kuwa kama vile jua linavyompiga mtu, ndivyo na mwezi nao unavyompiga mtu.

Akiwa na maana gani?  

Tunajua kuwa mwezi hauna nguvu yoyote ya kumuunguza mtu au kumchosha, tofauti na jua. Lakini Mungu anaona hata mwangaza tu  huo wa mwezi ni pigo kwa mtu. Akiwa na maana  si katika mateso magumu, au dhiki kubwa zinazoonekana kwa macho ndio anazoshughulika nazo Mungu, lakini pia hata katika zile ndogo sana, ambazo unaweza kuona zikiendelea kuwepo hazina madhara yoyote kwako, Bwana anakulinda nazo.

Kwamfano wewe huwezi kuona umepata hasara pale nywele yako moja imepungua kichwani mwako, tena si rahisi kugundua,  lakini yeye anaithamini na ndio maana amezihesabu zote. Ikidondoka moja tu, anaona mapungufu, umekutana na mateso..

Mathayo 10:30  lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote.,

Vivyo hivyo rohoni, unaweza kumwomba Mungu, niepushe na majaribu, kichwani kwako ukafikiri hili na hili labda magonjwa, umaskini, vita, vifungo,ajali,  kuteswa kwasababu ya imani, N.K. ndio Bwana anashughulika navyo hivyo kukulinda, au kukupa nguvu ya kuvishinda. Lakini anahakikisha hata zile honi za magari unazopishana nazo barabarani, haziyaharibu masikio yako, jani ulilokanyaga jana, halijaharibu mguu wako, bacteria walio katika mikono yako, hawaui seli za ngozi, idadi ya minyoo walio tumboni mwako, hawaendi kula maini na figo zako, kiwembe kinachopita kichwani mwako kila siku haking’oi mizizi ya nywele, n.k…Haya mambo unaweza kuona ni ya kawaida tu, lakini Bwana akitoa mkono wake umeisha.

Kwa ufupi ni kuwa zipo Nyanja nyingi sana za hatari, ambazo Bwana anatuepusha nazo, Ndio maana tunapaswa tuwe waombaji sikuzote, unapojiona upo salama, omba, unapojiona upo kwenye matatizo omba, muda wote dumu uweponi mwa Bwana. Hata kama utaona kama majaribu yamekulemea, Bwana ameahidi ushindi mwishoni, Ayubu alilemewa na mateso lakini mwishoni alirejeshewa mara dufu.

Ulinzi wa Mungu ni uhakika kwa watu wake, dumu katika katika maombi ili Bwana apate nafasi ya kutulinda vema, nyakati za jua na nyakati za mwezi. (Mathayo 26:41)

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618 Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mada Nyinginezo:

MAJARIBU MATANO (5) YA MKRISTO.

Je! Siku ilihesabiwaje kabla ya jua na mwezi kuumbwa?

MIEZI 13 YA KIYAHUDI.

UWEZA WA MUNGU UNAONEKANA WAPI?

Mwandamo wa mwezi/Mwezi mpya Ni nini kibiblia?

Kumaka ni nini katika biblia? (Mathayo 8:27)

Rudi nyumbani

Print this post

Kumaka ni nini katika biblia? (Mathayo 8:27)

Jibu: Neno “kumaka” limeonekana mara mbili katika biblia na maana yake ni “kushangaa/ mshangao”. Mtu anapokutana na jambo au anapoona kitu au tukio la ajabu ambalo hajawahi kuliona au kukutana nalo hapo kabla huwa anapatwa na mshangao! Sasa huo mshangao ndio unaoitwa “kumaka”.

Mathayo 8:27  “Wale watu WAKAMAKA wakisema, Huyu ni mtu wa namna gani hata pepo na bahari zamtii?”

Hapa wanafunzi walipomwona Bwana Yesu anazikemea pepo za bahari na kumtii, waliingiwa na mshangao wa ajabu kujiuliza yule ni mtu wa namna gani?

Utalisoma tena tukio hilo katika Luka 8:27, Lakini pia utaona Bwana Yesu alifanya mambo mengi makubwa ambayo yaliwashangaza watu wengi, (soma Marko 5:42, na Luka 4:36).

Hiyo ni kuonesha uweza wa Bwana Yesu Kristo wa kutenda miujiza ulivyokuwa Mkuu. Lakini uweza Mkuu na Muujiza Mkuu Bwana Yesu alioufanya na anaondelea kufanya leo, ambao hakuna mwingine yeyote awezaye kuufanya ni Muujiza wa KUFUTA DHAMBI!.

Miujiza mingine yote Bwana Yesu alisema nasi pia tunaweza kuifanya, lakini ule wa kusamehe dhambi ni yeye tu ndiye anayeweza kuufanya.

Marko 2:9 “Vyepesi ni vipi, kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende?

10  Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (hapo amwambia yule mwenye kupooza)”

Kwahiyo na sisi tunapaswa kuutafuta na kuupokea huu muujiza mkuu anaotoa Bwana Yesu wa kusamehewa dhambi, kwasababu kama hatutasamehewa dhambi na tukaponywa magonjwa peke yake bado haitatufaidia chochote, lakini tukipata msamaha wa dhambi hata kama tusipopokea uponyaji wowote katika mwili bado ni faida kubwa kwetu, kwasababu tutaurithi uzima wa milele.

Je! Umepokea msamaha wa dhambi zako?.. na je unaijua kanuni ya kupokea msamaha mkamilifu kutoka kwa Bwana?

Kanuni ya kupokea msamaha wa dhambi ni rahisi, nayo ni Kutubu kwa kumaanisha kuacha dhambi, kubatizwa na kupokea Roho Mtakatifu. Hatua hizo tatu ukizifuata, utapokea muujiza ambao hujawahi kuupokea katika maisha yako yote.

Matendo 2:36  “Basi nyumba yote ya Israeli na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyemsulibisha kuwa Bwana na Kristo.

37  Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?

38  Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

39  Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie”

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618 Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mada Nyinginezo:

NI NINI BWANA ANATAKA KUTOKA KATIKA MUUJIZA ALIOKUFANYIA?

BABA UWASAMEHE

NINI MAANA YA KUTUBU

UMEONDOLEWA DHAMBI?

TAFUTA MSAMAHA HALISI, NA SI MSAMAHA TU!

Rudi nyumbani

Print this post