SWALI: Nini maana ya Mithali 21:1
“Moyo wa mfalme huwa katika mkono wa Bwana; Kama mifereji ya maji huugeuza po pote apendapo”.
JIBU: Kuna mithali inayosema “maji hufuata mkondo”. Ikiwa na maana, palipo na mfereji kule kule unapoelekea ndipo maji nayo huelekea. Mfano ukielekeza mrefeji shambani mwako, basi maji yale yataelekea huko si kwingineko, ukielekezea mfereji nyumbani mwako, basi maji yatakuja ndani mwako. Kamwe maji hayajiamulii pa kuririkia.
Vivyo hivyo na Mungu, ndivyo anavyofananisha mamlaka yake juu ya wafalme na wakuu wa dunia hii. Kwamba mashauri yao, hawajiamulii tu peke yao kwa kujitakia. Kwamfano utakumbuka kuna wakati Mungu alimnyanyua Moyo Koreshi mtawala wa Uajemi ili awape ruhusu wayahudi warudi katika nchi yao wakamjengee nyumba.
Ezra 1:1 Ikawa katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, ili kwamba neno la Bwana alilolisema kwa kinywa cha Yeremia lipate kutimizwa, Bwana akamwamsha roho yake Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata akapiga mbiu katika ufalme wake wote, akaiandika pia, akisema, 2 Koreshi, mfalme wa Uajemi asema hivi; 3 Basi kila mtu katika ninyi nyote mlio watu wake, Bwana, Mungu wake, na awe pamoja naye, na akwee mpaka Yerusalemu, ulioko Yuda, akaijenge nyumba ya Bwana, Mungu wa Israeli, (yeye ndiye Mungu), iliyoko Yerusalemu. 4 Na mtu awaye yote aliyesalia mahali po pote akaapo hali ya ugeni, na asaidiwe na watu wa mahali pake, kwa fedha, na dhahabu, na mali, na wanyama, zaidi ya vitu vitolewavyo kwa hiari ya mtu, kwa ajili ya nyumba ya Mungu, iliyoko Yerusalemu
Mungu huyo huyo ndiye aliyemfanya mfalme Nebukadreza kuwa na moyo mkatili ili awachukue watu wake utumwani kwasababu ya makosa yao.(Yeremia 27:6, 43:10)
Mungu anaweza kuwatumia watawala kuadhibu taifa, au kuwabariki watu wake. Hii ni kuonyesha kuwa hakuna tawala yoyote katika hii dunia inamilikiwa na fikra za mwanadamu asilimia 100, bali mengi ya mashauri ya wakuu hutoka juu mbinguni, au yameruhusiwa na Mungu. Wao ni kama maji tu yanayofuata mkondo wa kusudi la Mungu.
Ndio jambo ambalo Mungu alimwambia Mfalme Nebukadreza kwamba “aliye juu ndiye anayetawala”(Danieli 5:21) lakini yeye alidhani ni uongo, mpaka siku alipoondolewa kwenye ufalme wake kwa miaka 7, na kurudishwa baadaye.
Hivyo, jambo hili, sio tu la viongozi wa kidunia, lakini pia hata wa kanisani. Ikiwa kanisa ulilopo linasimamia kweli na utakatifu na Kristo Yesu ndio kiini cha fundisho lao, basi waheshimu sana viongozi wako, kwasababu si kila shauri linalotoka kwenye vinywa vyao, ni wao wamefikiria. Wao ni kama maji tu yaliyomwagwa kwenye mfereji, ili kukuongoza wewe. ukishandana nao, au ukipuuzia kuongozwa nao, wakati mwingine unapingana na maamuzi ya Mungu wako bila kujijua.
Waheshimu viongozi wako wanaokulea kiroho, kama vile unavyowaheshimu watawala ya kidunia.
Bwana akubariki.
Shalom
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618
Mafundisho mengine:
Ni kwa namna gani Kristo analitakasa kanisa kwa Maji katika Neno? (Waefeso 5:26)
MADHARA YA KUKOSA MAJI YA UZIMA BAADA YA KIFO.
About the author