VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 14 (Yoeli, na Obadia).

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 14 (Yoeli, na Obadia).

Jina Kuu la ukombozi wa roho zetu, (Jina la YESU KRISTO) lihimidiwe daima!

Karibu katika mwendelezo wa uchambuzi wa vitabu vya biblia, tumekwisha kuvitazama vitabu kadhaa vya nyuma na leo tutavitazama vitabu vitatu vya mbele, ambavyo ni kitabu cha Yoeli, Amosi na Obadia. Hivyo ni vizuri kwanza kusoma vitabu hivi mwenyewe katika biblia, ndipo ukapitia uchambuzi huu, na kumbuka uchambuzi huu ni ufupisho tu!, na si wa kutegemea kama darasa kamili au ufunuo kamili wa vitabu hivi, hivyo ni muhimu sana kusoma biblia na kumruhusu Roho Mtakatifu afunue, ndipo masomo mengine yafuate juu yake.

Ikiwa bado hujavipitia vitabu vya awali, ni vizuri ukavipitia kwanza kabla ya vitabu hivi ili tuweze kwenda pamoja.

KITABU CHA YOELI:

Kitabu cha Yoeli, ni kitabu cha 29 katika orodha ya vitabu vya agano la kale, na kimeandikwa na Nabii Yoeli mwenyewe, mapema katika karne ya 8 kabla ya Kristo, kipindi cha Mfalme Uzia wa Yuda, na maana ya jina “Yoeli” ni “Yahwe ni Mungu”.  

Kitabu cha Yoeli kina Milango (Sura) tatu tu!, na kila sura/mlango una ujumbe tofauti.

Yoeli: Mlango wa kwanza.

Katika mlango wa kwanza Nabii Yoeli, anaelezea madhara yaliyoletwa na Nzige, na parare, na madumadu waliotokea Israeli. Historia inaonyesha kipindi cha miaka kadhaa kabla ya Yoeli kuandika kitabu hiki, kulitokea Janga ambalo lililetwa na Mungu kutokana na maasi.

Na janga hilo lilikuwa la Kuzuka kwa Nzige, parare na madumadu ambao walikula mazao yote, na kutokusaza chochote, Uharibifu wa Nzige hao uliwashangaza wote, kwani walikula mazao yote.

Na baada ya pigo hilo, ndipo Mungu anampa Nabii Yoeli ujumbe wa kuwaambia watu wake, kwamba watafakari hayo yaliyotokea, na wapate akili, na kutubu,.. watafakari jinsi wadudu hao walivyoharibu mazao kiasi kwamba makundi yote ya watu waliathirika, mpaka makuhani pia waliadhirika kwani hakikupatikana hata cha kutoa katika nyumba ya Mungu, maana yake zile sadaka za unga zilizokuwa zinatolewa ndani ya hekalu hazikutolewa tena..(Yoeli1:9).

Yoeli 1:1 “Neno la Bwana lililomjia Yoeli, mwana wa Pethueli. 

2 Sikieni haya, enyi wazee; Sikilizeni, enyi wenyeji wote wa nchi. Je! Mambo haya yamekuwako katika siku zenu, Au katika siku za baba zenu? 

3 Waarifuni watoto wenu habari yake, Watoto wenu wakawaambie watoto wao, Na watoto wao wakakiambie kizazi kingine.

4 Yaliyosazwa na tunutu yameliwa na nzige; na yaliyosazwa na nzige yameliwa na parare; na yaliyosazwa na parare yameliwa na madumadu. 

5 Levukeni, enyi walevi, mkalie; Pigeni yowe, ninyi nyote mnywao divai; Kwa sababu ya divai mpya; Maana umekatiliwa mbali na vinywa vyenu. 

6 Maana taifa limepanda juu ya nchi yangu, Lenye nguvu, tena halina hesabu; Meno yake ni kama meno ya simba, Naye ana magego ya simba mkubwa. 

7 Ameuharibu mzabibu wangu; ameuvunja mtini wangu; ameyaambua magamba yake kabisa; ameuangusha chini; matawi yake yamefanywa kuwa meupe”.

Kutokana na pigo hilo la Nzige, Mungu anawaita watu wake wote watubu!, ikiwemo makuhani, wafunge kwa kulia na kuomboleza, na tena wafunge katika saumu ya kweli (Yoeli 1:13-14).

Yoeli: Mlango wa 2.

Katika mlango wa Pili, Mungu analifananisha jeshi hilo la Nzige na jeshi atakalolinyanyua la watu ambao watavamia Israeli na kuharibu watu na vitu, kwa jinsi hiyo hiyo ya Nzige walivyoharibu mazao! Kwasababu ya maasi ya Israeli. Hivyo anazidi kuwaasa watubu!, kwa kupiga mbiu kwa watu wote, kwani jeshi hilo la watu ambao Bwana analifananisha na nzige litakapopita litapageuza Israeli jangwa (Yoeli 2:3), na Mungu atalipa uwezo wa kuharibu kwa uharibifu mkuu (Soma Yoeli 2:4-10).

Lakini katika Mstari wa 12, Bwana anarudia kutoa shauri la kutubu! Ili aiponye nchi kutokana na pigo la nzige, waliokula mazao, vile vile kwa pigo ambalo atakwenda kulipiga Taifa hilo kwa jeshi la watu wabaya atakaowatuma kuwadhuru.

Yoeli 2:12 “Lakini hata sasa, asema Bwana, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea;

 13 rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie Bwana, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya. 

14 N’nani ajuaye kwamba hatarudi na kugeuka, na kutuachia baraka nyuma yake, naam, sadaka ya unga, na sadaka ya kinywaji, kwa Bwana, Mungu wenu?

15 Pigeni tarumbeta katika Sayuni, Takaseni saumu, kusanyeni kusanyiko kuu; 

16 Kusanyeni watu, litakaseni kusanyiko, Kusanyeni wazee, kusanyeni watoto, Na hao wanyonyao maziwa; Bwana arusi na atoke chumbani mwake, Na bibi arusi katika hema yake.

17 Hao makuhani, wahudumu wa Bwana, na walie Kati ya patakatifu na madhabahu, Na waseme, Uwaachilie watu wako, Ee Bwana, Wala usiutoe urithi wako upate aibu, Hata mataifa watawale juu yao; Kwani waseme kati ya watu, Yuko wapi Mungu wao?

Mstari wa 17-32: (Ahadi ya kuponywa miaka ya njaa)

Bwana anatoa ahadi ya marejesho ya chakula katika miaka iliyoliwa na parare na nzige (katika pigo la Nzige). endapo watatubu!

Yoeli 2:25 “Nami nitawarudishia hiyo miaka iliyoliwa na nzige, na parare, na madumadu, na tunutu, jeshi langu kubwa nililotuma kati yenu. 

26 Nanyi mtakula chakula tele na kushiba, na kulihimidi jina la Bwana, Mungu wenu, aliyewatendea mambo ya ajabu; na watu wangu hawatatahayari kamwe.

27 Nanyi mtajua ya kuwa mimi ni katikati ya Israeli, na ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu, wala hakuna mwingine; na watu wangu hawatatahayari kamwe”.

Lakini haiishii tu kutoa ahadi ya kuponya miaka iliyoliwa na Nzige, bali pia Bwana anatoa ahadi nyingine ya kipekee ya kuwabariki watu katika roho, (yaani kuwamwagia Roho wake Mtakatifu).

Yoeli 2:28 “Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono;

29 tena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina roho yangu”.

Mlango wa 3 wote unahusu ahadi ya Bwana ya kuwapigania Israeli dhidi ya majeshi yaliyowaonea, baada ya wao kutubu, na kumrudia yeye.

Sasa tukirudi katika biblia, tunasoma baada ya Nabii Yoeli kuondoka, Israeli hawakutubu kikamilifu, ijapokuwa walipigwa na janga hilo la Nzige, na parare na madumadu na tunutu..lakini waliendelea kuwa vile vile, mpaka Bwana alipotimiza neno lake hilo la kuleta jeshi la watu ambao wataharibu nchi mfano wa hao nzige waliotangulia, na jeshi halikuwa lingine Zaidi ya lile la Wakaldayo, ambalo Bwana Mungu aliliruhusu lifike Yuda na kuharibu hekalu na kuwaua wayahudi wengi na baadhi yao kuwachukua utumwani Babeli.

Na kule utumwani walikaa miaka 70, na baada ya ile miaka 70, Danieli alisimama kutubu kwa niaba yao baada ya kuujua unabii wa Yeremia kuhusu muda wao wa kukaa utumwani, na waliporejea Bwana aliwapa majuma 69 (ambayo ni miaka 483) ya kuujenga Yerusalemu kabla ya kutimiza ahadi yake ya kumwanga Roho Mtakatifu.

Na miaka hiyo ilipotimia Bwana aliachilia Roho wake mtakatifu sawasawa na ahadi yake aliyoiahidi, katika Yoeli 2:28, ambapo ilitimia ile siku ya Pentekoste (Matendo 2:17).

Matendo 2:14  “Lakini Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia, Enyi watu wa Uyahudi, na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, lijueni jambo hili, mkasikilize maneno yangu.

15  Sivyo mnavyodhani; watu hawa hawakulewa, kwa maana ni saa tatu ya mchana;

16  lakini jambo hili ni lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli,

17  Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto.

18  Naam, na siku zile nitawamwagia watumishi wangu wanaume na wanawake Roho yangu, nao watatabiri”.

Na mpaka leo hii Roho Mtatifu yupo, na ndiye Muhuri wa Mungu juu ya mtu (Warumi 8:9, Waefeso 4:30, 2Wakorintho 1:22).

Kwa undani Zaidi kuhusiana na wadudu hawa (parare, nzige, madumadu na tunutu) na ujumbe gani wa ziada wamebeba kiroho, fungua hapa >>>Nzige, Parare, madumadu na tunutu ni wadudu gani? (Yoeli 2:25)?

KITABU CHA OBADIA:

Kitabu cha Obadia ni kitabu kilichoandikwa na Nabii Obadia mwenyewe, na kina Mlango mmoja tu!, hivyo kukifanya kuwa kitabu kifupi kuliko vitabu vyote vya agano la kale. Maana ya jina ‘Obadia’ ni “Mtumishi wa Bwana”.

Kitabu cha Obadia kinahusu Hukumu Mungu alioitangaza juu ya Taifa la Edomu (Nchi ya Edomu sasahivi ni maeneo ya kusini-magharibi mwa nchi ya Yordani).

Kwaasili Edomu ulikuwa ni urithi wa Esau aliyekuwa ndugu yake Yakobo! (Mwanzo 25:30 na Mwanzo 36:8)... Na tangu Esau na Yakobo wakiwa tumboni mwa mama yao, walikuwa wakipambana!.

Mwanzo 25:22 “Watoto wakashindana tumboni mwake. Naye akasema, Ikiwa ni hivi, kuishi kwanifaa nini? Akaenda kumwuliza Bwana.

23 Bwana akamwambia,Mataifa mawili yamo tumboni mwako,Na kabila mbili za watu watafarakana tangu tumboni mwako.Kabila moja litakuwa hodari kuliko la pili,Na mkubwa atamtumikia mdogo. 

24 Siku zake za kuzaa zilipotimia, tazama! Mapacha walikuwamo tumboni mwake”

Kutokana na unabii huo wa Esau kupambana na Israeli, ulifika wakati kiburi cha wana wa Esau (Edomu) kilinyanyuka kwa kiwango kikubwa..kwani walijinyanyua mbele za Mungu na kufanya dhambi na vile vile kuwafanyia mabaya makubwa wana wa ndugu yao Yakobo (yani wana wa Israeli). Na hivyo Mungu kutamka hukumu juu yao kwa kinywa cha Nabii wake Obadia.

Obadia 1:1 “Maono yake Obadia. Ndivyo asemavyo Bwana MUNGU juu ya Edomu; Tumepata habari kwa Bwana, Na mjumbe ametumwa kati ya mataifa, Akisema,Haya,inukeni ninyi;Na tuinuke tupigane naye. 

2 Tazama, nimekufanya mdogo kati ya mataifa; Umedharauliwa sana. 

3 Kiburi cha moyo wako kimekudanganya, Wewe ukaaye katika pango za majabali, Mwenye makao yako juu sana; Asemaye moyoni, Ni nani atakayenishusha mimi? 

4 Ujapopanda juu kama tai, Ijapokuwa kioto chako kimewekwa kati ya nyota, Nitakushusha kutoka huko; asema Bwana”.

Lakini mbali na hilo, historia inaonyesha kuwa kipindi Wakaldayo wameuhusuru Yerusalemu na baadaye kuivamia na kuharibu mali, wana wa Edomu walishirikiana na wakaldayo kushirikiana nao, na hata kuchukua mali nyingi za wana wa Israeli, sawasawa na unabii huo alioutoa Obadia miaka mingi kabla ya wana wa Israeli kuchukuliwa utumwani..

Obadia 1:11 “Siku ile uliposimama upande, siku ile wageni walipochukua mali zake, na watu wa kabila nyingine walipoingia katika malango yake, na kumpa kura juu ya Yerusalemu, wewe nawe ulikuwa kama mmoja wao”. 

Hivyo kwa kosa hilo na mengine ambayo hayajatajwa katika biblia, Bwana Mungu alitangulia kuwaonya lakini hawakutubu, hivyo ulipofika wakati Edomu iliadhibiwa sawasawa na hukumu hiyo, lakini pia iliyopo sasa itakuja kuadhibiwa katika vita vya mwisho vya Ezekieli 38.

Maelezo kwa kina kuhusu Edomu fungua hapa >>>Edomu ni nchi gani kwasasa?

Na baada ya Bwana kuiadhibu Edomu, kutokana na mabaya waliyoifanyia Israeli, Bwana anatoa ahadi ya kuijenga Yerusalemu, baada ya ubaya wao kupita.

Obadia 1:18 “Na nyumba ya Yakobo itakuwa moto, na nyumba ya Yusufu itakuwa mwali wa moto, na nyumba ya Esau itakuwa mabua makavu, nao watawaka kati yao, na kuwateketeza; wala hatasalia mtu awaye yote katika nyumba ya Esau; kwa kuwa Bwana amesema hayo”.

Ni nini tunajifunza katika kitabu hiki cha Obadia?..

Tunachoweza kujifunza kikubwa ni kwamba Mungu anatoa unabii unaokuja kama onyo!, ili yamkini mtu au Taifa lisije kuangukia katika hukumu ya Mungu, Watu wa Edomu walipewa unabii huu kama ushauri kwamba wakati wa msiba wa Israeli wasishirikiane na watu wakaldayo, na onyo hilo walipewa miaka mingi kabla ya Israeli kuja kuvamiwa na wakaldayo, lakini hawakutii unabii huo, na wakafanya waliyoyafanya na leo hii hawapo!.. Wanaoishi Edomu sasa si wana wa Esau bali wana wa Ishmaeli, ambao kulingana na unabii wa kibiblia watafutwa katika vile vita vya Ezekieli 38, na 39, kama walivyofutwa hawa wana wa Edomu.

Na sisi vile vile hatupaswi kutweza unabii (yaani kudharau unabii wa kibiblia). Unabii wa biblia unasema kuwa siku za mwisho watatokea watu wa dhihaka, watu wasiotii wazazi wao, wakaidi, wasiotaka kufanya suluhu, watukanani n.k (soma 2Timotheo 3:4), na kwamba watu wa namna hii hawataurithi ufalme wa Mungu.

Sasa unabii huu ni kweli utatimia, hivyo si wa kuutweza/kuupuzia..kwasababu ni kweli siku za mwisho, ambazo ndizo hizi hawa watu wametokea, hivyo hatupaswi kuwa miongoni mwa watakaotimiza unabii huo wa watakaodhihaki na kupotea, badala yake tutimize unabii wa watakaokolewa kwa kumfuata Mungu na kuitii Injili.

1Wathesalonike 5:20 “ msitweze unabii;”

Bwana atusaidie.

Usikose mwendelezo..

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 13 (Kitabu cha Hosea).

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 12 (Kitabu cha Isaya)

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 11 (Mithali, Wimbo ulio bora, Mhubiri)

Vitabu vya Deuterokanoni ni vya kiMungu?

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 5

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments