Kwanini Mungu anasema tusiwe na ‘tabia’ ya kupenda fedha? Tuwe radhi na vitu tulivyo navyo?. Ujasiri gani unaotaka kutuaminisha kwa kauli hiyo katika zama hizi ambazo tunajua bila fedha huwezi kutatua changamoto nyingi za kimaisha?
Waebrania 13:5 Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa. 6 Hata twathubutu kusema, Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini?
JIBU: Ametuagiza hivyo kwasababu ya hakikisho alilotuahidia katika kauli yake aliyosema “sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa”. Ukiitafakari kauli hiyo haimaanishi kuwa hatutakaa kamwe kupitia vipindi vya kupungukiwa, hapana, lakini anasema sitakupungukia ‘kabisa’, yaani ikafikia hatua ya kukosa kabisa hitaji Fulani, mpaka kufa na kuwa omba-omba barabarani, hapo hatutapafikia.
Daudi anasema..
Zaburi 37:25 Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa Wala mzao wake akiomba chakula
Umeona ameahidi kuwa nasi nyakati zote,
Ni kweli upo wakati ambapo ukiitazama baadaye yako au kesho yako unaona giza, lakini bado Bwana anasema usiwe na hofu, kwasababu hiyo kesho yenyewe itajisumbukia, yeye mwenyewe atatengeneza njia ya namna ya kukusaidia katika siku hiyo uliyopo.
Lakini ubaya ni pale ambapo tutataka Mungu atupe sawasawa na wingi tunaoutarajia. Kibiblia hilo sio hakikisho la Bwana, anaweza kukupa cha wakati huo tu, au akakupa zaidi ya hivyo ulivyomwomba. Ni jinsi yeye apendavyo, na anafanya hivyo kwa sababu zake mwenyewe ambazo ni njema kwako, lakini mwisho wa siku yote yatakuwa sawa tu, usiwe na hofu.
Pia ni vema kufahamu kuwa kauli hiyo haitufanyi sisi kuwa wavivu tusubirie tu kitu kutoka kwake. Hapana, anataka tujishughulishe katika sehemu mbili.
Sehemu ya kwanza ni kuutafuta ufalme wake, na haki yake.
Mathayo 6:33 Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. 34 Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.
Yaani uwe katika utumishi wa Bwana, unamtafuta na unaifanya kazi yake, kama vile mwajiriwa, alivyo katika utumishi wake. Ukifanya hivyo kwa uaminifu Bwana hawezi kukupungukia kabisa atakupa tu rizki yako, kwa njia zake mwenyewe.
Na sehemu ya pili ni aidha tuwe katika kufanya kazi za mikono. Tunapojishughulisha, na kitu Fulani cha kutupatia kipato, Bwana atatusaidia huko huko, tutajazwa mema yake.
Na kwasababu Bwana hataki mioyo yetu izame kule moja kwa moja, anataka tupate na nafasi ya kumfanyia ibada, na ndio maana ameahidi hatatuacha kabisa, Hivyo usione shida kufunga biashara yako, na kwenda kwenye maombi muda wa maombi ufikapo, jumapili kuahirisha kazi zako zote na kwenda nyumbani kwa Bwana, ondoa hofu kuwa utapoteza wateja. Kumbuka tu ile kauli ya sitakuacha kabisa, wala kukupungukia kabisa.
Hata kama utapoteza hiyo, Bwana atakufungulia rehema zake na kukupatia iliyo bora zaidi ya ile.
Hivyo kwa hitimisho ni kuwa wewe kama mwana wa Mungu, hupaswi kuweka moyo wako kwenye mali au fedha, yaani kufikiria kwamba bila kuwekeza sana maisha yako huko utapata shida mbeleni. Hapana, bali upatapo kingi au kidogo, basi ridhika maadamu Kristo yupo ndani yako, ameahidi kukusaidia nyakati zote.
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp: Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618
Mafundisho mengine:
Nijapokuwa sipo kwa mwili, lakini nipo pamoja nanyi kwa roho,
Kupiga ramli ni nini katika biblia?
Je kauli ya Bwana Yesu inajichanganya? Katika Yohana 8:14 na Yohana 5:31?
Kwanini Mungu aliwaagiza wana wa Israeli wasikisaze chakula?
Jiepushe na tamaa ya Mali/kupenda fedha.
JUA HALITAKUPIGA MCHANA, WALA MWEZI WAKATI WA USIKU.
Rudi nyumbani
Print this post