JIBU: Ndivyo inavyodhaniwa na wengi, hususani linaposomwa lile andiko lisemalo
1Timotheo 2:13 “Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye.”
Maneno hayo yanathibitisha kuwa Adamu ndiye aliyepewa kipaumbele cha kwanza kuliko mwanamke.. Lakini ifahamike kuwa Mungu ni Mungu wa utaratibu. Tunapotaka wote tufanane, wote tuje kwa wakati mmoja, na wote tuwe na mamlaka yanayofanana, basi maisha yangekuwa hayana maana. Hivyo Ili Mungu kutimiza kusudi lake, na kuweka mambo yote katika utaratibu ilimpasa aweke ngazi lakini hilo halimaanishi kuwa mmoja ni bora zaidi ya mwingine..Kwasababu kama tukichukulia kigezo cha kuumbwa kwa mwanaume kwanza zaidi ya mwanamke ndio tiketi..
Kumbuka pia wanyama na mimea yote iliumbwa kwanza kabla hata ya Adamu kuumbwa..Sasa hapo tuseme wanyama wamepewa upendeleo mkubwa zaidi ya sisi?. Jibu ni hapana, lakini tatizo kubwa linakuja pale wanaume wanapotaka kuwa kama wanawake na wanawake wanapotaka kuwa kama wanaume, katika utendaji kazi wao Mungu aliowawekea, hususani pale katika suala la UONGOZI katika kanisa, na nyumbani. Biblia inasema je! MAUMBILE NAYO HAYATUFUNDISHI?(1Wakorintho 11:14).
Tujifunze katika maumbile ya kila mmoja, jinsi alivyoumbwa, ili tupate kulijua kusudi la Mungu katikati yetu, jaribu kufikiria suala la uleleaji wa mtoto, baba hata aweze kufanya shughuli zote za ndani namna gani, hata aonyeshe upendo kwa mtoto mkuu dizaini gani bado hataweza kumtolea mtoto chakula mwilini mwake. Hiyo shughuli nzito na jukumu la kipekee namna hiyo ameumbiwa mwanamke tu (mama). Shughuli nzito ya kumlea akiwa kijusi tumboni, mpaka kiumbe kipya duniani na changamoto zake zote, wakati mwingine hata wengine kupoteza maisha yao kwa changamoto hizo, ni mama peke yake ndiyo aliyeumbiwa, mwanaume hata awe shujaa kiasi gani,..akijaribu kufanya hivyo atakuwa anapoteza muda wake…..hawezi kufanya hivyo hata atamanije!!….Kadhalika kazi ya ulinzi, uangalizi wa nyumba, kazi za kutumia nguvu nyingi, mwanamke hata akijitahidi vipi kwenda kubeba viroba vya michanga atakuwa anajiumiza tu mwenyewe.
Shughuli hizo na taabu hizo Mungu kamuumbia mwanaume. Japo zipo zinazofanywa na wote hilo lipo wazi, lakini tatizo linakuja ni pale kila jambo, ambalo mwanaume ametawazwa na Mungu kulifanya mwanamke naye anataka kulifanya..asilimia 50 kwa 50..Na hilo ndio limekuwa tatizo kubwa.Ambao ni mpango mkamilifu wa shetani, mwanaume anavaa suruali mwanamke naye anataka kuvaa suruali, mwanaume anavaa kaptura mwanamke naye anataka kuvaa kaptura, mwanaume ananyoa nyewe zake, mwanamke naye ananyoa kipara afanane na mwanaume. Kwa mfano tukirudi kwenye kanisa:
Biblia inasema
1Wakorintho 14.34 “Wanawake na wanyamaze katika kanisa, maana hawana ruhusa kunena bali watii, kama vile inenavyo torati nayo..”Na pia inasema 1Timetheo 2: 12 “Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe katika utulivu”.
Utakuta Baadhi yao wanaona kama Mungu kawaweka nyuma katika kazi yake, na hivyo wanaamua kuyahalifu kwa makusudi maagizo ya Mungu na kwenda kufundisha makanisani, na kuwatawala waume zao. Wakidhani kuwa ndio wanajenga, kumbe hawajui kuwa wanabomoa. Hekima ya Mungu ni kubwa zaidi ya mwanadamu, akisema hivi anamaanisha hivyo, yeye anajua ni jinsi gani mwanaume atatenda vizuri katika eneo hilo zaidi ya mwanamke na ndio maana akasema hivyo..
Lakini kwa anayemwona Mungu hapo kakosea kuweka ngazi, na mamlaka katika kazi yake mwenyewe aliyoibuni duniani biblia ipo wazi yanasema hivi:
1Wakorintho 14: 37 “Mtu akijiona kuwa ni nabii au mtu wa rohoni, na ayatambue hayo ninayowaandikia, ya kwamba ni maagizo ya Bwana. 38 LAKINI MTU AKIWA MJINGA, NA AWE MJINGA”.
Baki katika nafasi uliyoitiwa, Biblia haina mfumo dume hapana bali ina utaratifu. Na utaratibu huo ni Mungu mwenyewe ndio kauweka kulingana na jinsia.
Ubarikiwe.
Mada Nyinginezo:
NAFASI YA MWANAMKE KATIKA KANISA
UZAO WAKO UTAMILIKI MALANGO YA KUZIMU;
NJIA KUU YA KUINGIA KATIKA ULE MJI.
JIBU: Tunapaswa tufahamu vizuri utumishi wa Mungu jinsi ulivyogawanyika ili tusikose maarifa tukidhani ya kuwa Mungu anatenda kazi sehemu moja tu kanisa, mahali pengine hayupo, wala hajihusishi na mambo hayo. Tukisoma biblia tunaona Mungu anao watumishi wa aina mbili: 1) Watumishi wa ufalme wa mbinguni: 2) Watumishi wa kidunia:
Watumishi wa ufalme wa mbinguni: Ni wale wote wanaofanya kazi zihusuzo ufalme wa mbinguni tu, kuhakikisha habari njema zinawafikia watu wengi kwa njia ya injili, kulichunga kundi la Mungu wakati wote, kulihudumia kwa kila namna kupitia karama za Roho ambazo Mungu aliziachia katika kanisa..Na mfano wa watumishi hawa tunawajua ni wachungaji, waalimu, mitume, manabii, na wainjilisti, mashemasi, karama za maombezi, lugha, uponyaji, Neno la Hekima, Maarifa n.k..
Lakini Mfano wa watumishi wa kidunia, ni wale ambao wameamuriwa na Mungu kutimiza kusudi lake maalumu hapa duniani. Na mfano wa hao ni Serikali na taasisi zake zote zilizo chini yake..
Na Wengine mfano, ni mashirika mengine yote yasiyo ya Umma, yanayohusika na kutoa huduma za kijamii kwa watu. Hawa wote wanatimiza kusudi maalumu la Mungu lakini sio kusudi kamilifu lile ambalo alilitaka kila mmoja alifikie. Hivyo Mungu huwa anatumia vyombo hivi vyote viwili kwa aidha kubariki, au kijilipizia kisasi, kwa walio waovu na walio wema. Sasa kama imetokea Mfano mtu anayo kiu ya kuijua haki, anapenda kutafuta kujua masuala ya Mungu kwa bidii hata kama yeye sio mkristo..Jambo Mungu analofanya ni kumsaidia kwa kumpelekea huyu mtu mtumishi wake wa ufalme wa mbinguni ili amfikishie huduma hiyo aliyokuwa anaihitaji mahali pale alipo.
Mfano tunamwona Kornelio katika biblia, yeye hakuwahi hata siku moja kumfahamu YESU, lakini kwa jinsi alivyokuwa anabidii katika kumtafuta Mungu na kutenda haki na kutoa sadaka nyingi, basi Petro alitumwa kwake kwenda kumshuhudia habari njema za YESU KRISTO (Matendo 10), Mfano wa mwingine kama huo tunaona kwa yule Mkushi aliyetoka Afrika kwenda kuhiji Yerusalemu, lakini alipokuwa njiana anarudi nchini kwake huku anasoma torati mahali palipoandikwa habari za YESU lakini katika fumbo. Mungu aliona kiu yake hivyo kutokana na bidii yake kwa Mungu ya kutaka kujua, basi Mungu akamtumia Mtumishi wake Filipo aende kumwelezea habari zile kwa ufasaha zaidi.
Vivyo hivyo mtoto wa Mungu anapomwomba Mungu ampe riziki za dunia, hawezi kwenda kumtafutia kazi kanisani kwasababu makanisa sio taasisi za kutengeneza fedha, au sio sehemu za biashara, Bwana Mungu atakachokifanya ni kuhakikisha anamtafutia nafasi nzuri katika taasisi Fulani husika, labda wizara Fulani ambapo pengine atamweka chini ya ma-manager Fulani wa serikali..ambao watamwajiri na kumpatia mshahara mzuri..sasa hao ma-manager ni watumishi wa Mungu kwa Yule mtoto wa Mungu anayetafuta riziki za kidunia.
Vivyo hivyo mtoto wa Mungu anapohitaji, maji safi au umeme mzuri, Bwana Mungu hawezi kumpelekea mchungaji au nabii kumpatia huduma hiyo, atampelekea watumishi wake wengine wanaohusika na mambo hayo kama tanesco na Idara ya Maji, watahakikisha wanamfikishia maji na umeme mpaka chumbani kwake anapolala.
Hali Kadhalika pale mtu anapokuwa mwovu, anapotenda mabaya, anapomfanyia Mungu makosa kwa makusudi wapo vile vile watumishi Mungu aliowaandaa kwa ajili ya shughuli kama hizo ili kujilipizia kisasi kwake, na mojawapo wa hao watumishi wa Mungu ndio hivyo vyombo vya dola, mtu anapoua, unapoiba, unapobaka, unapokula rushwa,. Asidhani kuwa Mungu atasema naye kwa upole kama asemavyo naye kanisani, Na ndio hapo anakamatwa na kutiwa gerezani na wakati mwingine kuhukumiwa kunyongwa kama atakuwa anastahili adhabu hiyo,. Sasa Kwa namna ya kawaida unaweza kusema ni hawa watu wamemtendea hivyo, lakini kiuhalisia sio wao bali ni Mungu ndiye aliyemlipiza kisasa kwa makosa yake mwenyewe. Na ndio maana biblia inasema:
Warumi 13:1 “Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu.
2 Hivyo amwasiye MWENYE MAMLAKA HUSHINDANA NA AGIZO LA MUNGU; NAO WASHINDANAO WATAJIPATIA HUKUMU.
3 Kwa maana watawalao hawatishi watu kwa sababu ya matendo mema, bali kwa sababu ya matendo mabaya. Basi, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Fanya mema, nawe utapata sifa kwake;
4 kwa kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu kwako kwa ajili ya mema. LAKINI UFANYAPO MABAYA, OGOPA; kwa maana hauchukui upanga bure; kwa kuwa ni mtumishi wa Mungu, amlipizaye kisasi mtenda mabaya kwa ajili ya ghadhabu.
5 Kwa hiyo ni lazima kutii, si kwa sababu ya ile ghadhabu tu, ila na kwa sababu ya dhamiri.
6 Kwa sababu hiyo tena mwalipa kodi; kwa kuwa wao ni wahudumu wa Mungu, wakidumu katika kazi iyo hiyo”.
Unaona hapo? Sasa tukirudi kwenye swali lililoulizwa linalosema: Mimi ni askari magereza, na nimeamuriwa kumnyonga mfungwa aliyekuwa mwalifu kwa kosa la uuaji. Je! kufanya hivyo ninatenda dhambi?. Jibu ni kuwa “hutendi dhambi” .
Kwani wewe umeamuriwa kutimiza wajibu wako, kwa kosa ambalo lilishaonekana limefanywa na mtu mwenyewe, mpaka kufikia hapo ni Mungu mwenyewe ameruhusu. kwasababu maagizo hayo hayajatoka kwako bali yametoka juu, lakini hutahesabiwa thawabu katika hilo mfano wa wale wanaomtumikia Mungu kwa habari ya kuokoa roho za watu na sio kuangamiza,..Na ndio maana ni vema pia kujua pale unapokuwa mkristo, ufahamu kazi unayotaka kuifanya ujue na majukumu yake yatakavyokuwa, Sio kila kazi itampa mkristo amani kuifanya, japo hata afanyapo hatahesabiwa makosa.
Uamuzi ni wako binafsi. Hivyo kabla hujaamua kujiingiza kwenye utumishi wowote piga kwanza faida zake na hasara zake. Je! Utumishi uufanyao ni ule utimizao mapenzi makamilifu ya Mungu au ni ule wa kisasi cha Mungu, kabla hujawa mwanajeshi jitafakari mara mbili mbili, kabla hujawa polisi jitafakari mara mbili mbili na daktari vivyo hivyo na kazi nyingine zote.
Ubarikiwe.
Mada Nyinginezo:
MAWE YALIYOKWISHA KUCHONGWA MACHIMBONI.
KUCHEZA KARATA NI SAHIHI KWA MTU ALIYE MKRITO?
WALIO NA HEKIMA NDIO WATAKAOELEWA.
Punyeto ni dhambi?..Na je! Kuoa ni suluhisho la kuzuia tamaa kama biblia inavyosema katika 1 Wakorintho 7:9?.
JIBU: Bwana Yesu alisema amtazamaye mwanamke kwa kumtamani amekwisha kuzini naye nafsini mwake. Sentensi hiyo inaonyesha kuwa dhambi haianzii nje ya mwili bali inaanzia moyoni, hivyo zinaa pia inaanzia moyoni, ikishafanyika moyoni ndipo inatoka nje, kwahiyo chochote kinachofanyika mwilini ni matokeo ya kitu kilichofanyika tayari rohoni, hivyo uasherati, masturbation (punyeto), utazamaji wa pornography hayo yote ni matokeo ya uasherati ambao tayari yalishafanyika ndani ya moyo wa mtu.
Ndio masturbation ni dhambi. Na suluhisho pekee la kuikwepa hiyo dhambi ni kumkabidhisha Bwana Yesu maisha yako ki-kweli kweli, na kudhamiria kuanza maisha mapya katika Kristo, na kuamua KUACHA!! Wengi wanatafuta kuombewa waache kutazama pornography au kufanya masturbation lakini hawajadhamiria kuamua kuacha hivyo vitu,..wanasubiria miujiza ishuke wajikute wameacha na huku bado mioyo yao inaelekea kwenye zinaa…Nataka nikuambie ndugu yangu unayemtafuta Mungu,Hakuna maombi yoyote ya kuondoa hicho kitu ndani ya mtu, ili hivyo vitu viondoke ni kuamua kwanza kuchukua uamuzi wa kuacha hayo mambo ndipo Bwana anakuongezea UWEZO wa kushinda hayo mambo,. Kumbuka na Biblia inasema waasherati wote sehemu yao ni katika ziwa la moto. Na pia kuhusu kuoa biblia imeweka wazi katika kitabu cha
1 Wakorintho7 :1 “Basi kwa habari ya mambo yale mliyoandika, ni heri mwanamume asimguse mwanamke.2 Lakini kwa sababu ya ZINAA kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe”.
Ukisoma kwa makini huo mstari wa 2 anasema kwasababu ya ZINAA kila mtu mwanamume awe na mke wake mwenyewe…sio kwasababu ya KUEPUKA TAMAA…bali kwasababu ya ZINAA…na zinaa maana yake ni kufanya mapenzi nje ya ndoa au kabla ya ndoa, Hii ikiwa na maana kuwa, kuwa na mke hakumzuii mtu kulipuka tamaa…kama tabia ya mtu ni kutamani! Hiyo tabia hataiacha hata akioa au akiolewa..pengine ataepuka zinaa tu baada ya kuoa/kuolewa kwasababu atakuwa na mke/mume wake ndani!…. Lakini tama ya kutazama wanawake wengine itakuwa palepale kama atakuwa hajabadilishwa.
Kwahiyo suluhisho pekee la kuzuia tamaa kwa aliyeoa au asiyeoa, ni kumkabidhi Kristo maisha kwanza, na kukusudia kuacha dhambi, (kumbuka Mungu hawezi kumsaidia mtu ambaye hajakusudia kwa dhati kuacha kile kitu kibaya anachokifanya)..mtu akishakusudia kuacha kwa vitendo tabia ya kutamani, kujitenga na vichochezi vyote vya uasherati, muvi zenye vimelea vya ngono ndani yake, pornography, matusi, maneno ya mizaha yasiyokuwa na maana, ndipo Roho Mtakatifu anakuja juu yake na kumsaidia na hivyo anajikuta vile vitu havimsumbui tena maishani mwake. Tofauti na yule anayetamani tu kuacha lakini haonyeshi jitihada yoyote ya kutaka hivyo vitu viondoke ndani yake.
Ubarikiwe!
Mada Nyinginezo:
JE! KUSHIRIKI AU KUJIHUSISHA KWENYE MICHEZO NI DHAMBI?
NIFANYE NINI ILI NIIKWEPE HUKUMU.
MADHARA YA DHAMBI YA UASHERATI.
NITASHINDAJE HALI YA KUUMIZWA NA MANENO YA WATU!
JIBU: Ubarikiwe ndugu…Mlozi ni mti fulani, unaositawi sana sana huko mashariki ya kati (Lebanoni, Israeli, Palestina n.k.).Jina lake kwa kiyahudi unaitwa “SHAKEI” na tafsiri yake ni KUTAZAMA/KUANGALIA...Kwahiyo Yeremia kuonyeshwa pale Mti wa Mlozi ni lugha tu ya picha anayoonyesha kwamba Bwana ANATAZAMA, na je! anatazama nini?..Anatazama NENO lake ili alitimize alilolinena juu ya Israeli..na ndio maana ukisoma hapo anasema..
Yeremia 1: 11 Tena neno la Bwana likanijia, kusema, Yeremia, waona nini? Nikasema, Naona ufito wa mlozi. 12 Ndipo Bwana akaniambia, Umeona vema, kwa maana ninaliangalia neno langu, ili nilitimize…
Kumbuka pia Mungu huwa anatazama Neno lake ili alitimize kwa namna zote, Hivyo kama ni jema, ni lazima alitimize, na kama ni baya juu ya watu wake ni lazima alitimize pia!.Kote kote. Lakini tunaona Israeli walikuwa waasi kwa Mungu tangu zamani, ukisoma katika habari za wafalme utaona jambo hilo, jinsi walivyokuwa wanamuasi Mungu mpaka akawaapia kuwa wataenda utumwani tena Babeli, kwa vinywa vya manabii wake waliotangulia kabla ya Yeremia mfano Isaya n.k. Na ndio maana hapo Yeremia anaonyeshwa kama UFITO(FIMBO) tu, ya mlozi, Ikimaanisha kuwa Mungu analitazama NENO lake, na kulitimiza juu yao kama ADHABU na sio BARAKA...
kwasababu FIMBO ni kwaajili ya kuadhibu siku zote tunajua hilo. Hivyo Ukizidi kuendelea mistari inayofuata ndio utaona mabaya yote Mungu aliyoyanena juu ya yao yalikuja kutimia ikiwemo kuchukuliwa utamwani Babeli.
ubarikiwe
Mada Nyinginezo:
SANDUKU LA AGANO LILIKUWA LINAWAKILISHA NINI KATIKA AGANO JIPYA?
NI RAHISI KWA NGAMIA KUPENYA KATIKA TUNDU LA SINDANO, JE! NI SINDANO IPI HIYO INAYOZUNGUMZIWA?
AMIN! NAWAAMBIA KIZAZI HIKI HAKITAPITA
JIBU: Mafarisayo na Msadukayo chimbuko lao ni moja dini zao zimeegemea katika Torati ya Musa, wote hawaamini maagizo mengine nje ya torati isipokuwa tofauti inakuja katika kuamini kiama cha wafu.. Mafarisayo wanaamini kuwa kuna kiama cha wafu (yaani maisha baada ya kufa, wanaamini yote yaliyoandikwa katika torati hata tumaini ya kuja kwa Masihi duniani) lakini masadukayo hawaamini kama kuna kufufuliwa kwa wafu, wanaamini kuwa mtu akishakufa, amekufa hakuna chochote baada ya hapo, wala hakuna malaika wala ulimwengu wa roho wala mbingu.
Ukisoma Mathayo 22:24-34 utaona Bwana Yesu akiwajibu hao mafarisayo kuhusu mitazamao wao hafifu ya maandiko Na kuwaambia kuwa Mungu asingesema yeye ni Mungu wa Ibrahimu, na Isaya na Yakobo kama watu hao ni wafu sasa. Kwasababu siku zote Mungu si Mungu wa wao bali wa wanaoishi..Hivyo Neno hilo linathibitisha kuwa kiama kipo. Ukisoma tena Matendo 23 Utaona Mtume Paulo akiyagonganisha madhehebu hayo mawili.
Matendo 23: 6 “Paulo alipotambua ya kuwa sehemu moja ni Masadukayo, na sehemu ya pili ni Mafarisayo, akapaza sauti yake katika ile baraza, Ndugu zangu, mimi ni Farisayo mwana wa Farisayo; mimi ninahukumiwa kwa ajili ya tumaini la ufufuo wa wafu.
7 Alipokwisha kunena hayo palikuwa na mashindano baina ya Mafarisayo na Masadukayo, mkutano ukafarakana.
8 Kwa maana Masadukayo husema ya kwamba hakuna kiyama wala malaika wala roho; bali Mafarisayo hukiri yote.
9 Pakawa na makelele mengi. Waandishi wengine wa upande wa Mafarisayo wakasimama, wakateta, wakisema, Hatuoni uovu wo wote katika mtu huyu; bali ikiwa roho au malaika amesemanaye, ni nini?
10 Ugomvi mkubwa ulipotokea, yule jemadari akachelea Paulo asije akararuliwa nao, akaamuruaskari washuke na kumwondoa kwa nguvu mikononi mwao, na kumleta ndani ya ngome.”
Hivyo kwa maandiko hayo utapata kuelewa tofauti ya watu hawa ipo wapi.. MYUNANI: Sio dini au imani, bali ni watu wa taifa la uyunani, kwasasa ni Ugiriki.Hivyo katika agano jipya mahali popote anapotajwa myunani, linalenga watu wa aina mbili, aina ya kwanza ni aidha wayahudi wanaotokea katika nchi za wayunani, na hivyo wanajulikana kama wayunani lakini kiasili ni wayahudi, kwa mfano wale watu waliotaka kumwona Bwana zamani zile ni wayahudi lakini sio wa kuzaliwa Israeli. tunasoma:.
Yohana 12:20 “Palikuwa na WAYUNANI kadha wa kadha miongoni mwa watu waliokwea kwenda kuabudu kwenye sikukuu.
21 Basi hao walimwendea Filipo, mtu wa Bethsaida ya Galilaya,wakamwomba, wakisema, Bwana, sisi tunataka kumwona Yesu “
Unaona? Kadhalika pia wale watu waliokuwa Yerusalemu siku ile ya Pentekoste, (Matendo 2) wakishangaa matendo makuu ya Mungu, biblia inasema walikuwa Warparthi na Wamedi na Waelami,n.k. wote hawa hawakuwa watu wa mataifa mengine (yaani watu wasio wayahudi) hapana bali walikuwa ni Wayahudi waliotoka katika hayo mataifa yaliyotajwa hapo,Na aina ya pili: ni Wayunani ambao asili yao ni Uyunani kabisa, watu wa mataifa. Mfano tunaweza kumwona mwanamke huyu aliyezungumziwa hapa ni myunani lakini hana uyahudi wowote ndani yake:
Marko 7:24 “Akaondoka huko, akaenda zake hata mipaka ya Tiro na Sidoni. Akaingia katika nyumba,akataka isijulikane na mtu; lakini hakuweza kusitirika.
25 Ila mara mwanamke, ambaye binti yake yuna pepo mchafu, alisikia habari zake,akajaakamwangukia miguuni pake.
26 Na yule mwanamke ni Myunani, kabila yake ni Msirofoinike. Akamwomba amtoe pepo katikabinti yake.
27 Akamwambia, Waache watoto washibe kwanza; maana si vizuri kukitwaa chakula cha watoto,na kuwatupia mbwa
28 Naye akajibu, akamwambia, Naam, Bwana, lakini hata mbwa walio chini ya meza hulamakombo ya watoto.
29 Akamwambia, Kwa sababu ya neno hilo, enenda zako, pepo amemtoka binti yako.
30 Akaenda zake nyumbani kwake, akamkuta yule kijana amelazwa kitandani, na yule pepo amekwisha kumtoka.”
Kadhalika tunaona watenda kazi wa Mungu wengine kama Tito, mwanafunzi wa Paulo (Wagalatia 2:3).
Na Timotheo (Matendo 16:1) hawa wote biblia inawataja kama ni Wayunani, na sio wayahudi.
Ubarikiwe sana.
Mada Nyinginezo:
NIFANYAJE ILI NIJUE KUWA UAMUZI NINAOKWENDA KUCHAGUA KUFANYA NI MAPENZI YA MUNGU?
USIWE SABABU YA WATU KUMKUFURU MUNGU.
JIBU:Shalom!. Ni vizuri tuifahamu sifa ya Mungu, ili tusiishie tu kumchukulia yeye yupo mbinguni kaketi kwenye kiti cha Enzi, mahali pengine popote palipo pachafu hawezi kuingia wala kukanyaga, wala kujua kinachoendelea huko.
Zaburi 139:7 “Niende wapi nijiepushe na roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako? 8 Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko. 9 Ningezitwaa mbawa za asubuhi, Na kukaa pande za mwisho za bahari; 10 Huko nako mkono wako utaniongoza, Na mkono wako wa kuume utanishika. 11 Kama nikisema, Hakika giza litanifunika, Na nuru inizungukayo ingekuwa usiku; 12 Giza nalo halikufichi kitu, Bali usiku huangaza kama mchana; Giza na mwanga kwako ni sawasawa.”
Na ndio maana ukisoma ule mstari ule mstari wa 6 juu yake kidogo unasema hivi.. “Maarifa hayo ni ya ajabu, yanishinda mimi, Hayadirikiki, siwezi kuyafikia.” Hii Ikiwa na maana kuwa uweza wa Mungu hautambulikani, na njia zake hazitafutikani hata tukijaribu kumtafakari Mungu vipi, hatuwezi kumpima kwa akili zetu hizi za kibinadamu kwa jinsi alivyoenea kila mahali. Hiyo Inatuthibitishia kuwa Mungu pekee ndiye anayeweza kuwepo kila mahali, na ndio pekee mwenye funguo za makao ya viumbe vyote ulimwenguni,..hakuna mwingine yeyote mwenye uwezo huo.Kama tunavyofahamu..
Zipo falme Kuu tatu zinazotembea katika duara lote la uumbaji wa Mungu, Ufalme wa kwanza ni ufalme wa Mungu mwenyewe ambao huo upo katika ulimwengu wa roho, na ufalme wa pili ni ufalme wa giza nao pia upo katika ulimwengu wa roho, na ufalme ya tatu ni ufalme ya wanadamu ambao ndio huu tunaouona katika mwili na ndio huu tunaoishi mimi mimi na wewe. Na falme hizi zote kila mmoja inayo utendaji kazi wake wenyewe, na nguvu zake, na mamlaka yake yenyewe, na kama zilivyojipanga ile Falme ya kwanza ndiyo yenye nguvu zaidi mbali na nyingine zote ndiyo ya Mungu wetu, kisha hapo chini unafuata ufalme wa giza ambao ndio shetani anaumiliki, na wa mwisho ndio huu wa kwetu sisi wanadamu. Sasa Yule mwenye nguvu zaidi ndiye mwenye uwezo wa kuingia na kutoka kwenye ufalme wa chini yake.
Kwa mfano ufalme wa mbinguni ambao ndio wa Mungu wetu, unaouwezo wa kuamua lolote juu hizi falme mbili za chini, unaouwezo wa kuzitumia au kuziamurisha lolote la kufanya, zinaweza kutumiwa pia kutimiza kusudi Fulani la Mungu kwa muda kwa kipindi fulani. Vivyo hivyo na ufalme wa pili ambao ni wa giza unao nguvu wa kuumurisha ufalme wa chini yake (yaani sisi tunaouishi), kamwe mwanadamu hata afanyaje hawezi kuushinda ufalme wa ibilisi kama hana Mungu, atatawaliwa tu na falme hizo mbili, na ndio maana shetani naye alikuwa na ujasiri wa kujigamba mbele ya Yesu na kumwambia hivi vyote ni vyangu nami humpa yeyote nimtakaye na huku sisi tunajua kuwa dunia na vyote viijazavyo ni mali ya Mungu. Unadhani shetani alikuwa anajisifia bure?, hapana kwasababu ufalme wake ni kweli una nguvu zaidi ya ufalme wa wanadamu..
Hivyo alikuwa na haki ya kusema vile. Hali kadhalika ule ufalme ulio dhaifu hauwezi kuelewa mambo yanayoendelea katika ufalme ulio juu yake wenye nguvu hata uwe na bidii kiasi gani. Hivyo ufalme wa ibilisi hauwezi kujua lolote linaloendelea katika ufalme wa Mungu, hata atafute kiasi gani hawezi kujua chochote. Sasa Tukirudi kwenye swali lililoulizwa Je!Mungu anaweza kuleta majibu kupitia nguvu za giza maana nashindwa Kuelewa ninaposoma habari za mfalme Sauli .kupata majibu kwa mwanamke .mwenye pepo.nisaidie hapo. Jibu ni Ndio Mungu anaoweza kuleta majibu sio tu kupitia ufalme wa giza, bali pia kupitia ufalme wa kibinadamu, Kwasababu yeye yupo mahali popote,.kama hapo juu anavyosema
Zaburi 139:8 “Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko.9 Ningezitwaa mbawa za asubuhi, Na kukaa pande za mwisho za bahari; 10 Huko nako mkono wako utaniongoza, Na mkono wako wa kuume utanishika. ”
Lakini yeye kuwa uwezo huo wa kupitisha ujumbe wake kupitia falme hizo zote mbili haimaanishi kuwa unampendeza au umemfikia Mungu kinyume chake ni hukumu inafuata…Pia hiyo haimaanishi kuwa mtu anapokwenda kwa mganga kumtafuta Mungu atamwona, kumbuka wote wanaokwenda kwa waganga hawana lengo la kumtafuta Mungu, hakuna hata mmoja, huwa wanakwenda kutafuta njia za kutatuliwa matatizo yao na wala sio kumtafuta Mungu,kama wangekuwa na lengo la kumtafuta Mungu wasingedhubutu kutumia njia hizo ambazo wanajua kabisa Mungu amezikataa. Hata Sauli mwenyewe hakwenda kumtafuta Mungu kule kwa mganga,bali samweli amsaidie kutatua ufumbuzi wa shida iliyo mbele yake..
Na ndio huko huko Mungu wakati mwingine anatokea kuzungumza na watu, na ikishafika hatua kama hiyo basi ujue kuwa kinachofuata ni hukumu tu kwa kwenda kinyume na mapenzi ya Mungu. Hata wachawi wenyewe huwa wanakutana na sauti ya Mungu huko huko katika shughuli zao zikiwaonya matendo yao, lakini hawawezi kusema siri hizo wanazo wao wenyewe, wale ambao wanakuja kuokolewa ukiwauliza watakuthibitishia hilo kwamba kuna wakati Fulani ambao Mungu alishawahi kuwaonya.
Sio tu Sauli alikwenda kwa waganga..Yupo ambaye alikuwa ni mchawi kabisa biblia inamtaja naye ni Balaamu, nabii wa uongo, huyu naye Mungu alikuwa anazungumza naye akimwonya asiwalaani Israeli, lakini yeye hakusikia sauti ile ya Mungu akatia ukwazo kwa wana wa Israeli, Mungu baadaye akaja kumuua. Hivyo huo uwezo Mungu anao,lakini sio njia Mungu anayoitumia kuleta majibu ya maombi wa watu. Njia yoyote nje ya Yesu Kristo, yaani njia ya sanamu, njia ya uganga, njia ya sayansi, hakuna hata moja yenyewe uwezo wa kufikisha maombi kwa Mungu, wala usijaribu kufanya hivyo utaangukia hukumu, isiyoponyeka. japo Mungu anaweza kuzitumia hizo kuleta majibu kwa watu tena majibu yaambatanayo na hukumu wala sio jambo jema.
Ubarikiwe.
Mada Nyinginezo:
JINSI WATU WANAVYOZAMA KATIKA USHIRIKINA NA UCHAWI.
JE! NI KWELI KUNA VIUMBE VINAVYOISHI SAYARI NYINGINE (ALIENS)?
BWANA YESU ALIMAANISHA NINI ALIPOSEMA; MAFARISAYO HUPANUA HIRIZI ZAO, NA KUONGEZA MATAMVUA YAO?
HATARI YA KUTOKUITAFAKARI BIBLIA VIZURI?
JIBU: Kwanza ni muhimu kufahamu nini maana ya watoto wa kwenye chupa…ikitokea mama anakuwa ana mayai lakini anapata shida kushika mimba huwa kuna uwezekano wa kuyatoa mayai yake kutoka kwenye uzazi na kuyaweka kwenye kifaa maalum kinachoitwa test tube au kwa kiswahili chupa, sasa wakishaliweka hilo yai la mwanamke mule huwa wanachukua mbegu za mwanamume na kuziweka kule kitaalamu ili kurahisisha lile yai kurutubishwa kirahisi…na baada ya lile yai kurutubishwa ndani ya ile chupa wanalichukua lile yai na kulirudisha kwenye tumbo la yule mama na kuendelea na hatua nyingine za ukuaji wa yule mtoto kwenye tumbo la mama yake…hiyo ndio maana ya mtoto wa kwenye chupa, sio kwamba yule mtoto anawekwa kwenye chupa maisha yake yote hapana….ni yai tu ndio linalorutubishiwa kule na kurudishwa mahali husika…
kwahiyo hakuna mazingira yoyote nje na tumbo la mama mtoto anaweza kukua..wanadamu hawajafikia huo uwezo. Tumbo la mama ndio sehemu pekee mtoto anaweza kukua mpaka kufikia hatua ya kuzaliwa.Sasa tukirudi kwenye swali je! ni dhambi yai kurutubishiwa kwenye chombo hicho maalumu nje na tumbo la mama??J
ibu ni kwamba Mungu anaangalia nia ya mtu kufanya vile ni ipi, wengi wanaofanya hivyo unakuta wana matatizo ya kutokushika mimba, kwahiyo njia rahisi wanayoshauriwa na madaktari ni kutumia hiyo njia, hivyo sio dhambi kwasababu nia yao ni kutafuta mtoto sio kuua mtoto. Na hatua hiyo ya kurutubisha yai kwenye chupa ni hatua ya awali kabisa hata mtoto hajaanza kutengenezwa. Ingekuwa kufanya hivyo ni dhambi basi pia kuzaa kwa operation ingekuwa ni dhambi kwasababu sio njia ya asili Mungu aliyoiumba kwa kuzalia watoto. Kwahiyo inategemea na sababu ya mtu kufanya hivyo ni nini?, kama mtu anafanya kwa nia nyingine tofauti na hiyo basi ni dhambi, Lakini ingekuwa ni vizuri zaidi kumtegemea Mungu kuliko madaktari yaani kumwamini Mungu kuliko kutafuta njia mbadala, lakini pia hatuna imani zinazofanana…wako wenye imani kuwa Mungu atawapa watoto pasipo njia hizo na wapo wasio na imani hiyo…Lakini mtu akitumia hiyo njia hafanyi dhambi endapo tu atakuwa na nia njema.
Warumi 14:5…”Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe.
Ukiwa na swali, lolote unaweza ukatutumia, kwa neema za Bwana tutakujibu na kukutumia kwa njia ile iliyo rahisi kwako (inbox, e-mail, au whatsapp)Weka jina lako, na swali lako”.
Ubarikiwe!
Mada Nyinginezo:
JE! NI HALALI KWA MTU WA MUNGU KUTUMIA NJIA ZA UZAZI WA MPANGO,IKIWAMO MIPIRA?
JE! MUNGU ANAUPENDELEO KWA WANAUME ZAIDI YA WANAWAKE?
VIGEZO VYA KUWA KARIBU NA YESU KRISTO KATIKA ULIMWENGU UJAO.
MAJARIBU MATATU YA YESU KRISTO
JIBU: Waebrania 6:1-3 Inasema..
“1 Kwa sababu hiyo, tukiacha kuyanena mafundisho ya kwanza ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu; tusiweke msingi tena wa kuzitubia kazi zisizo na uhai, na wa kuwa na imani kwa Mungu, 2 na wa mafundisho ya mabatizo, na kuwekea mikono, na kufufuliwa wafu, na hukumu ya milele. 3 Na hayo tutafanya Mungu akitujalia.”
Ndio Bwana anatuonyesha kwamba ukristo ni safari isiyoishia tu pale mtu anapotubu na kubatizwa na kumwamini Mungu, bali ni jambo endelevu siku baada ya siku tunakua, na ndio maana mtume Paulo anasema hapo TUKAZE MWENDO ili tuufikilie huo utimilifu. Hatupaswi kila siku tu tukae kwenye mafundisho yanayohusu ubatizo sahihi, au kutubu au kumwamini Mungu, au ziwa la moto, hayo ni mafundisho ya chini sana, kwamba pindi tu pale mtu alipompa Bwana maisha yake alipaswa ayatambue.
Na hivyo anakuwa na wajibu wa kusonga mbele kujifunza mambo mengine ya muhimu zaidi. Lakini inasikitisha kwamba utakuta mtu anadai yeye ni mkristo wa muda mrefu lakini bado suala la ubatizo sahihi linampiga chenga, mwingine haamini kabisa mambo hayo, mwingine hata ubatizo anaona hauna umuhimu kwake, anaamua kuendelea kubaki hivyo hivyo tu kwa muda mrefu, angali akijua kabisa biblia inafundisha kuwa pale tu mtu anapoamini , bila kupoteza muda anapaswa akabatizwe, kuukamilisha wokovu wake, lakini bado kwake anaona ni jambo linaloweza kusubiri tu, halina umuhimu sana .(Matendo 8:35-38) .
Sasa kama mambo hayo machanga yanakuwa bado ni mitihani kwa watu unategemea vipi Mungu aachilie neema kwa watumishi wake kufundisha mambo mengine ya ndani zaidi yatakayomfanya mtu akomae kiroho?. Ikiwa mtu haweza kuhesabu moja mpaka kumi, ya nini kufundishwa milinganyo?. Hivyo yatubadilishe mienendo yetu kwanza, ili Bwana aachilie neema ya kutufundisha mambo mengine ya ndani yahusuyo ufalme na na siri zimuhusuzo Bwana wetu YESU KRISTO.
Vinginevyo tukiendelea kumzimisha Roho ndani yetu kwa kutokutaka kutii maagizo madogo, tutatii vipi yale makubwa, tutaendelea tu kubaki katika hali ile ile ya uchanga kwa muda mrefu bila mabadiliko yoyote, hatutastahili kupata chakula kigumu cha kutufanya tukue. Kama Mtume Paulo alivyosema kwa Waebrania..
Waebrania 5: 11 “..Ambaye tuna maneno mengi ya kunena katika habari zake; na ni shida kuyaeleza kwa kuwa mmekuwa wavivu wa kusikia.12 Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu.13 Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga.14 Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya”
Ubarikiwe sana.
JIBU: Biblia haikatazi mtumishi yeyote wa Mungu kutambuliwa kwa karama aliyo nayo. Kwamfano kuitwa mchungaji, au mwinjilisti au mtume, au mwalimu au nabii au askofu n,k. Hakuna mahali ilipokataza, Lakini kuongeza Neno hapo juu yake mfano “mkuu” au “kiongozi ” “mighty” “chief” “lead” “great” n.k. hiyo ni roho ya kujiinua na ni roho ya mpinga-kristo yenyewe. Kwani vyeo hivyo vinamuhusu Bwana wetu YESU KRISTO mwenyewe.. Yeye ndiye mchungaji mkuu biblia inasema hivyo..yeye ndiye mtume mkuu, yeye ndiye nabii mkuu, Yeye ndiye Bwana wa mabwana, na yeye ndiye Mfalme wa wafalme.Na ndio maana utaona hakuna Mtume yeyote wa Kristo alijiita kuwa yeye ni mtume mkuu, bali cheo hicho walikitambua kuwa ni cha Kristo mwenyewe.
Waebrania 3:1 “Kwa hiyo, ndugu watakatifu, wenye kuushiriki mwito wa mbinguni, mtafakarini sana MTUME NA KUHANI MKUU wa maungamo yetu, Yesu, aliyekuwa mwaminifu kwake yeye aliyemweka, kama Musa naye alivyokuwa, katika nyumba yote ya Mungu.”
Waebrania 3:20 “Basi, Mungu wa amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu MCHUNGAJI MKUU wa kondoo, kwa damu ya agano la milele, yeye Bwana wetu Yesu,”
Unaona? Hivyo hao watu wote wanaojivika hivyo vyeo vya juu zaidi ya walivyopewa, utatambua kuwa dhima yao ni kuvuta watu kwao, wawafuate wao na si Kristo, na ndio maana utaona hawaoni hata haya kujivuka vyeo vya juu kama hivyo. Lakini biblia inasema ajikwazaye atashushwa..Watu wa namna hiyo Bwana mwenyewe atawashusha, kwasababu yeye kasema Utukufu wake hatagawana na mwingine yeyote.
Ubarikiwe.
Mada Nyinginezo:
MANABII WALISEMA “NENO LA MUNGU LIKANIJIA” ..MAANA YA HILI NENO NI NINI?
Jina la Bwana YESU litukuzwe daima. Karibu tujifunze Neno la Mungu, leo kwa neema za Bwana tutajifunza juu ya njia sahihi ya kufunga.
Zipo aina nyingi za kufunga lakini kwa vyovyote vile, hatufungi ili Mungu atusikie au atujibu maombi yetu, Mungu hasubiri kwanza tuteseke ndio atusikie hapana kwani alishaweka wazi katika Neno lake, kuwa yeye anajua tunachohitaji kabla hata hatujamwomba (Mathayo 6:8)…Lakini pamoja na hayo Kufunga kunasaidia kuongeza uwezekano wa wewe kupata majibu ya maombi yako au kupata unachokitafuta kwa haraka tofauti na yule asiyefunga. Ni sawa tu na mwanafunzi anayesomea maktaba na Yule anayesomea nyumbani, anayesomea maktaba anaongeza uwezekano mkubwa wa kufaulu mitihani kuliko Yule anayesomea nyumbani, kwasababu kule maktaba kunakuwa na utulivu mkubwa na mazingira mazuri ya kujisomea kuliko nyumbani..Lakini hiyo haimfanyi afaulu mtihani moja kwa moja Yule wa nyumbani anaweza kufanya vizuri kushinda hata yeye..Lakini itampasa awe mtu wa kujitambua sana.
Vivyo hivyo na katika kufunga, Mtu mwenye desturi ya kuomba kwa kufunga anajijengea daraja zuri la yeye kuwasiliana na Mungu kuliko Yule apelekaye dua zake kwa Mungu bila kufunga, Kwasababu Kufunga kunampa utulivu Fulani wa Roho tofauti na mtu asiyefunga.
Na hiyo yote ni Kutokana na kutokuwa na Mungu katika mwili, au kutokumwona Mungu katika mwili ndio maana inatupelekea tumtafute Mungu kwa umakini zaidi kuliko kama tungekuwa tunamwona kwa macho…Mitume walipokuwa na Bwana duniani hakukuwa na sababu ya kufunga, ufunge ya nini wakati unayemtafuta upo naye hapo? Mpaka watu wengine wakashangaa inakuwaje hawa ni mitume wa Bwana lakini hawafungi, Ndipo Bwana akawaambia wanachokifanya hawajakosea kwasababu mimi nipo, Siku zitakuja nitakapoondoka ndipo watakapofunga kama wengine…
Marko 2:18 “Nao wanafunzi wake Yohana na Mafarisayo walikuwa wakifunga; basi walikuja, wakamwambia, Kwani wanafunzi wa Yohana na wanafunzi wa Mafarisayo hufunga, bali wanafunzi wako hawafungi?
19 Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kufunga maadamu bwana-arusi yupo pamoja nao? Muda wote walipo na bwana-arusi pamoja nao hawawezi kufunga.
20 Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana-arusi, ndipo watakapofunga siku ile.”
Hivyo kitendo cha kufunga hakikwepeki sasa kwa mkristo yeyote. Na zipo aina nyingi za kufunga, lakini aina iliyozoeleka ni ile ya kuacha kula chakula. Lakini mfungo huu unafanywa kimakosa na wengi kwasababu ya kutokufahamu ni kwanini mtu anaacha kula..Na ndio hapo mtu mmoja atafunga vizuri kweli hata wiki tatu au mwezi au siku arobaini, lakini anafanya kama desturi za dini nyingine wanavyofanya, ukiangalia huku nyuma utamwona anaendelea na maisha yake ya kidunia anadhani kusikia kule njaa ndo Mungu anampa thawabu,. Hajui kuwa Mungu hamjibu mtu kwa mateso,(Maombolezo 3:31-35) sasa hapo mtu wa namna hiyo kaamua tu kujitesa bure..Hakuna chochote atakachokipata kutoka kwa Mungu.
Au unakuta mwingine anafunga kwa lengo la kumuomba Mungu mambo ambayo sio sawa na mapenzi yake, mwingine atamwomba Mungu ampe mali, lakini ndani ya moyo wake anawaza aitumie kwa anasa, mwingine atamwomba Mungu ampe hiki au kile, lakini nia yake moyoni ni kutumia kwa mambo maovu.. mtu wa namna hiyo pia asitazamie kupata kitu.
Isaya 58:3 “Husema, Mbona tumefunga, lakini huoni? Mbona tumejitaabisha nafsi zetu, lakini huangalii? Fahamuni, siku ya kufunga kwenu mnatafuta anasa zenu wenyewe, na kuwalemea wote watendao kazi kwenu.
4 Tazama, ninyi mwafunga mpate kushindana na kugombana, na kupiga kwa ngumi ya uovu. Hamfungi siku hii ya leo hata kuisikizisha sauti yenu juu.
5 Je! Kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je! Ni siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? Je! Utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na Bwana?
6 Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira?
7 Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe?
8 Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde.
9 Ndipo utaita, na Bwana ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa. Kama ukiiondoa nira; isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu;
10 na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri.”
Unaona? Dhumuni la msingi kabisa la kujizuia kutokula mtu anapaswa afahamu ni kuyaleta mapenzi ya mwili chini na kuruhusu mapenzi ya Mungu yaje juu, ile njaa inakukumbusha kwenda mbele za Mungu kwa unyenyekevu mwingi , sikuzote mtu mwenye njaa anakuwa katika uhitaji sana kuliko mtu aliye shiba, hivyo mtu wa namna hiyo anapokwenda mbele za Mungu kumaanisha kwake kunakuwa kwa kiwango cha juu zaidi kuliko mtu aliyeridhika, hata maombi yake yanakuwa marefu sana, jaribu hata kwako utaligundua hilo..Na hiyo ndio faida kubwa ya kutokula wakati wa maombi. Hivyo inapelekea maombi yako kuwa na nguvu zaidi mbele za Mungu kuliko wengine.
Vile vile kuna kufunga ambako sio kwa kula, bali kwa kujizuia na mambo mengine yanayoweza kukusonga usiisikie sauti ya Mungu. Kufunga kwa namna hii kumekuwa kwa kawaida kwa watumishi wengi wa Mungu, Nabii Elisha ilimpasa atumie muda mwingi kujitenga na mazingira ya watu ili kudumisha joto la uhusiano wake na Mungu. Sio kwamba kuna shida kujihusisha na mambo ya kawaida ya kila siku, hapana lakini ni utaratibu wa Mungu kuzungumza katika sauti ya utulivu, na kama ni sauti ya utulivu hivyo naye huwa anahitaji mazingira tulivu ya kumwelewa.
Ufunuo wowote Mungu anaompa mwanadamu, hampi akiwa katika mazingira ya usumbufu wa akili, Usijidanganye kuwa Mungu atakupa ufunuo wowote katika hali ya masumbufu, kama utaisoma biblia na huku unasikiliza miziki ya kidunia, au huku una chat, au huku unafanya mambo mengine, Ni heri uifunge uje usome baadaye usiku peke yako…. inahitaji utulivu wa fikra na mawazo..Na hapo ndipo inakupasa ufunge baadhi ya vitu unavyovifanya, au ulivyozoea kuvifanya..Na kwa jinsi unavyovifunga kwa muda mrefu zaidi ndivyo unavyoongezeka uwezekano wa Mungu kusema na wewe kwa haraka na kwa mara nyingi zaidi.
Kufunga kuna faida kwasababu yeye mwenyewe anasema wote wafanyao hivyo huwapa thawabu kama hawatafanya kinafki na kwa nia mbaya..(Mathayo 6:16)
Ni ahadi yake kukulipa, Funga tu kwa kumaanisha kumsogelea Mungu zaidi, utapata zaidi ya kile ulichomwomba. Kuna mtu aliuliza swali je! Maandiko yanasema tunapaswa tufunge kuanzia saa ngapi hadi saa ngapi na ni kwa siku ngapi?..Jibu ni kuwa Biblia haijatoa masharti yoyote juu ya muda wa kufunga au siku za kufunga..Imezoeleka siku 3, siku 21 na siku 40 kwasababu ndio siku ambazo zimeonekana zikifungwa na wengi..Lakini hiyo haimaanishi kuwa nawe ufunge muda huo, ni vile Roho atakavyokuongoza na kulingana na aina ya dua uipelekayo kwa Mungu, unaweza ukafunga, siku moja, au wiki, au mwezi, au mwaka, na Mungu akaridhia, vile vile unaweza ukafunga saa 6 kwa siku, saa 12, au siku tatu bila kula, au siku 40 bila kula , ni vile tu Mungu atakavyokupa neema..Lakini vyovyote vile kufunga ni muhimu kwa kila mkristo. Na kuna manufaa na thawabu nyingi.
Ubarikiwe sana.
Maran atha!
Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp