Katika Waebrania 6:1-3 Mtume Paulo alikuwa ana maana gani kusema “1 Kwa sababu hiyo, tukiacha kuyanena mafundisho ya kwanza ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu;?

Katika Waebrania 6:1-3 Mtume Paulo alikuwa ana maana gani kusema “1 Kwa sababu hiyo, tukiacha kuyanena mafundisho ya kwanza ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu;?

JIBU: Waebrania 6:1-3 Inasema..

“1 Kwa sababu hiyo, tukiacha kuyanena mafundisho ya kwanza ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu; tusiweke msingi tena wa kuzitubia kazi zisizo na uhai, na wa kuwa na imani kwa Mungu, 2 na wa mafundisho ya mabatizo, na kuwekea mikono, na kufufuliwa wafu, na hukumu ya milele. 3 Na hayo tutafanya Mungu akitujalia.”  

Ndio Bwana anatuonyesha kwamba ukristo ni safari isiyoishia tu pale mtu anapotubu na kubatizwa na kumwamini Mungu, bali ni jambo endelevu siku baada ya siku tunakua, na ndio maana mtume Paulo anasema hapo TUKAZE MWENDO ili tuufikilie huo utimilifu. Hatupaswi kila siku tu tukae kwenye mafundisho yanayohusu ubatizo sahihi, au kutubu au kumwamini Mungu, au ziwa la moto, hayo ni mafundisho ya chini sana, kwamba pindi tu pale mtu alipompa Bwana maisha yake alipaswa ayatambue.

Na hivyo anakuwa na wajibu wa kusonga mbele kujifunza mambo mengine ya muhimu zaidi.   Lakini inasikitisha kwamba utakuta mtu anadai yeye ni mkristo wa muda mrefu lakini bado suala la ubatizo sahihi linampiga chenga, mwingine haamini kabisa mambo hayo, mwingine hata ubatizo anaona hauna umuhimu kwake, anaamua kuendelea kubaki hivyo hivyo tu kwa muda mrefu, angali akijua kabisa biblia inafundisha kuwa pale tu mtu anapoamini , bila kupoteza muda anapaswa akabatizwe, kuukamilisha wokovu wake, lakini bado kwake anaona ni jambo linaloweza kusubiri tu, halina umuhimu sana .(Matendo 8:35-38) .  

Sasa kama mambo hayo machanga yanakuwa bado ni mitihani kwa watu unategemea vipi Mungu aachilie neema kwa watumishi wake kufundisha mambo mengine ya ndani zaidi yatakayomfanya mtu akomae kiroho?. Ikiwa mtu haweza kuhesabu moja mpaka kumi, ya nini kufundishwa milinganyo?. Hivyo yatubadilishe mienendo yetu kwanza, ili Bwana aachilie neema ya kutufundisha mambo mengine ya ndani yahusuyo ufalme na na siri zimuhusuzo Bwana wetu YESU KRISTO.  

Vinginevyo tukiendelea kumzimisha Roho ndani yetu kwa kutokutaka kutii maagizo madogo, tutatii vipi yale makubwa, tutaendelea tu kubaki katika hali ile ile ya uchanga kwa muda mrefu bila mabadiliko yoyote, hatutastahili kupata chakula kigumu cha kutufanya tukue. Kama Mtume Paulo alivyosema kwa Waebrania..  

Waebrania 5: 11 “..Ambaye tuna maneno mengi ya kunena katika habari zake; na ni shida kuyaeleza kwa kuwa mmekuwa wavivu wa kusikia.12 Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu.13 Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga.14 Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya”

Ubarikiwe sana.

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments