Ni muhimu kujua kanuni za kuomba, ili tusije tukajikuta tunapiga mbio bure, kwa kuomba maombi yasiyokuwa na majibu. Kwanza ni muhimu kumjua unayemwomba ni Mungu wa namna gani.. Usipozijua tabia za unayemwomba, na ukienda kumwomba..unaweza ukamchukiza badala ya kumpendeza.
Sasa zipo hoja nyingi, ambazo ni harufu mbaya mbele za MUNGU wetu, lakini leo tutajifunza hoja moja ambayo ni hoja inayoonekana kama Nzito, machoni petu, lakini mbele za Mungu wetu ni harufu mbaya..
Na hoja yenyewe ni ya KUWASHITAKI WALE TUNAOWAONA KUWA MAADUI ZETU, MBELE ZA MUNGU.
Hebu tusome kisa kifuatacho, kisha tujifunze tabia ya Bwana Yesu ambayo shetani katupiga upofu tusiijue…
Luka 12:13 “Mtu mmoja katika mkutano akamwambia, Mwalimu, MWAMBIE NDUGU YANGU ANIGAWIE URITHI WETU.
14 Akamwambia, MTU WEWE, NI NANI ALIYENIWEKA MIMI KUWA MWAMUZI AU MGAWANYI JUU YENU?”
Kikawaida hata mimi nilitegemea Bwana Yesu, angesuluhisha hii KESI!, Kwa kuwaweka mezani na kuzungumza na pande zote mbili, ili yule anayestahili HAKI apewe, na yule asiyestahili AONYWE!!.. Lakini ilikuwa kinyume chake!… Bwana Yesu anaanza kushughulika kwanza na huyu aliyeleta Mashitaka!… na kumwuliza..NI NANI ALIYEMWEKA YEYE AWE MWAMUZI JUU YAO, AU MGAWANYI!!!.. Ni kama vile Bwana anazikataa hizo mada!, ni kama vile havutiwi nazo, ni kama vile zinampotezea muda!!!. Ndio maana hata mashitaka ya Martha juu ya ndugu yake Miriamu hayakuwa kama alivyotegemea. (Luka 10:40-42).
Sasa maandiko yanasema Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele, hajabadilika, na hatabadilika (Waebrania 13:8)… kama aliyakataa mashitaka ya huyu mtu hadharani, dhidi ya adui yake, basi atakayataa hata na mashitaka yetu katika SALA!!!.. Kwasababu ni yeye yule, habadiliki.
Ni kweli umedhulumiwa kiwanja chako!, ni kweli umeonewa, ni kweli umestahili haki…Ila unapokwenda kwenye maombi, kamwe usimshitaki huyo unayemwona kama adui yako, kwasababu hutaambulia chochote!…maombi yako ni kama kichefuchefu tu kwa Bwana!..
Ni vizuri kumjua unayemwomba ana tabia gani kabla ya kumwomba!.. hii ndio shida kubwa inayosababisha watu wengi kutojibiwa maombi yao, na hawajui ni kwanini. Tatizo ni kwamba hawamjui wanayemwomba ana tabia gani.. Ndugu, Bwana Yesu hana tabia kama uliyonayo wewe, au niliyo nayo mimi na wala hutuwezi kumfundisha tabia zetu..na kamwe hawezi kufuata tabia zetu..na wala hana cha kujifunza kutoka kwetu.. sisi ndio tuna cha kujifunza kutoka kwake, na tunapaswa tuige tabia yake ili tufanikiwe.
Sasa tabia yake ni hii..
Mathayo 5:38 “Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho, na jino kwa jino;
39 Lakini mimi nawaambia, MSISHINDANE NA MTU MWOVU; LAKINI MTU AKUPIGAYE SHAVU LA KUUME, MGEUZIE NA LA PILI.
40 Na mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia.
41 Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili”.
Maana yake ni kwamba kama mtu Kakupiga shavu moja bila kosa lolote, badala ya kwenda KUPIGA MAGOTI KUMSHITAKI KWA BWANA!.. wewe Mpe shavu la pili, alipige na hilo halafu nenda kapige magoti! Mshukuru Mungu kwakuwa umefanikiwa kumpa na shavu la pili alipige…Utakuwa umeyatenda mapenzi ya Mungu…na umeomba maombi yenye hoja… HALAFU SASA SUBIRIA MAJIBU YAKE!!!.
Mtu kakudhulumu kipande kidogo cha ardhi, mwongeze na mita kadhaa..halafu mshukuru Mungu..Hapo utakuwa umeukosha moyo wa Bwana Yesu kuliko unavyodhani!!!… Na utaona matokeo yake.. Ndani ya kipindi kifupi, utaona jinsi Bwana atakavyomtengeneza yule mtu, kwasababu atamgusa moyo na atajiona ni mkosaji, na utashangaa anakurudishia ile sehemu ya ardhi aliyokudhulumu, ndivyo maandiko yanavyosema.. kuwa Njia za mtu zikimpendeza Bwana, humpatanisha na maadui zake..
Mithali 16:7 “Njia za mtu zikimpendeza Bwana, Hata adui zake huwapatanisha naye”.
Kwasababu Bwana anataka Nuru yetu iangaze…kwamba watu wanapoyatazama matendo yetu mema, jinsi gani tulivyo wema..ndipo wapokee neema ya wokovu..lakini tukiwa watu wakaidi, wakushindana wa kutupiana maneno, wakushitakiana mchana kutwa na usiku kucha..bila shaka sisi hatutakuwa na utofauti wowote na shetani… maana tafsiri ya jina shetani ni MSHITAKI, AU MCHONGEZI. Usiku na mchana anatushitaki mbele za Mungu (Soma 1Petro 5:8 na Ufunuo 12:10). Sasa na sisi tusiwe mashetani wengine!!..kwa kupeleka mashitaka mbele za Mungu.
Ndugu, ukitaka baraka basi mwabudu na msikilize Bwana Yesu Kristo wa kwenye biblia, ambaye yupo hai sasahivi..na Bwana Yesu wa kwenye biblia ni huyu mwenye maneno yafuatayo..
Mathayo 5:43 “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako;
44 lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,
45 ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki”.
Na watumishi wake pia watakuwa na maneno hayo hayo…lakini pia yupo yesu mwingine asiyekuwa wa kwenye biblia, huyo anakuambia Mpige adui yako mchukie adui yako, ukimfuata huyo au ukiwafuata watumishi wake basi jua unaenda kuzimu.
2Wakorintho 11:4 “Maana yeye ajaye akihubiri YESU MWINGINE ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea roho nyingine msiyoipokea, au injili nyingine msiyoikubali, mnatenda vema kuvumiliana naye!”
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
NDIPO HUENDA AKACHUKUA PEPO WENGINE SABA.
YAFUATAYO NI MAWAZO YA ADUI HIVYO USIYASIKILIZE.
Mathayo 8:11 “Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni;
12 bali WANA WA UFALME WATATUPWA KATIKA GIZA LA NJE, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno”.
Je umewahi kujiuliza ni kwanini Bwana Yesu aseme maneno hayo??, kuwa Wana wa Ufalme watatupwa nje?. Watakuwaje wana wa Ufalme halafu tena watupwe nje?…hao si ndo wangepaswa waingie ndani??.. Je Bwana Yesu alikosea?
Jibu ni la!, hakukosea..bali ni kweli Wana wa Ufalme watatupwa nje!!.
Sasa ili tuwajue hawa wana wa Ufalme ni akina nani?. Hebu tuutafakari mfano mwingine wa Bwana alioutoa mahali pengine.
Mathayo 22:1 “Yesu akajibu, akawaambia tena kwa mithali, akisema,
2 Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyemfanyia mwanawe arusi.
3 Akawatuma watumwa wake WAWAITE WALIOALIKWA KUJA ARUSINI; nao wakakataa kuja.
4 Akatuma tena watu kwa wengine, akisema, WAAMBIENI WALE WALIOALIKWA, Tazameni, nimeandaa karamu yangu; ng’ombe zangu na vinono vimekwisha kuchinjwa, na vyote vimekuwa tayari, njoni arusini.
5 Lakini hawakujali, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwenye biashara yake;
6 nao waliosalia wakawakamata watumwa wake, wakawatenda jeuri, na kuwaua.
7 Basi yule mfalme akaghadhibika; akapeleka majeshi yake, akawaangamiza wauaji wale, akauteketeza mji wao.
8 Kisha akawaambia watumwa wake, Arusi i tayari, LAKINI WALE WALIOALIKWA HAWAKUSTAHILI.
9 Basi enendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni arusini.
10 Watumwa wale wakatoka wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; arusi IKAJAA WAGENI”.
Katika mfano huo utaona kuna makundi mawili, kundi la kwanza ni WAALIKWA, (ambao tunaweza kuwaita kama “wana wa Harusi”, au waliostahili kuingia harusini, ambao walipewa kadi zao maalumu za mwaliko na waliandaliwa viti kabisa, na wanafahamiana na Bwana harusi).. Lakini wapo ambao hawakupewa kadi kabisa…wala walikuwa hawajaalikwa, kwaufupi hawakuwa kwenye bajeti yoyote, wala walikuwa hawafahamiani na Bwana harusi.
Lakini mwishoni tunaona wale WANA WA HARUSI, ambao walikuwa na nafasi harusini, ambao walifahamiana sana na Bwana harusi, ambao ni ndugu zake, na jamaa zake na Bwana harusi, waliokuwa wamekusudiwa hiyo sherehe, yaani kwaufupi karamu ilikuwa ni kwaajili yao na furaha yao…mwisho wa siku hakuna hata mmoja, aliyeingia katika hiyo karamu..badala yake walitokea wengine wakaingia katika karamu..ambao hawakustahili, wasiojuana hata na Bwana harusi, waliotoka kutoka njia panda za barabarani, kutoka mitaani, kutoka masokoni na kutoka sehemu mbali mbali…wakaingia karamuni..harusi ikajaa WAGENI.. (Zingatia hilo neno wageni!)
Kupitia mfano huu tayari tutakuwa tumeshajua ni kwanini Bwana Yesu aseme haya…
Mathayo 8:11 “Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni;
12 bali WANA WA UFALME WATATUPWA KATIKA GIZA LA NJE, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno”
Leo hii wana wa Ufalme duniani ni wengi sana… Kwa ufupi wote ambao wameisikia Injili, na injili inajirudia rudia masikioni mwao, lakini wanaitolea udhuru kila mara, hawapo tayari kujikana nafsi na kumfuata Yesu, hao tayari ni WANA WA UFALME, ambao Bwana anawaalika lakini hawaalikiki!!!.
Pamoja na kwamba wamehubiriwa uzuri wote wa mbinguni, na faida za kiroho watakazozipata endapo wakiamua kubadilisha Maisha yao, na kuishi kulingana na Neno la Mungu na mapenzi ya Mungu, Pamoja na kuwa wamejihakikishia kuwa ni kweli wanaishi nyakati za kurudi Bwana wao… lakini bado watatoa udhuru..
Utasikia wanasema.. “Ni kweli natamani kusimama kiimani lakini kazi zangu zinanibana, nakosa muda wa kusoma biblia” .. “Ni kweli natamani kuwa mwombaji na kuhudhuria ibadani lakini kazi ni nyingi, nakuwa bize mpaka jumapili”… “Ni kweli natamani kuacha pombe, na kuacha kuvaa kikahaba na kihuni ila naamini sikumoja tu nitaacha”.. “Ni kweli Neno linanufundisha kubatizwa, lakini siwezi kwasasa, kwasababu mchungaji wangu na familia yako hawaamini hilo” n.k n.K.
Sasa hili ndio kundi la WANA WA UFALME, ambao siku ile, biblia imetabiri WATATUPWA NJE, Kutakakowako KILIO NA KUSAGA MENO!!.
Ndugu usifurahie tu kulisikia Neno, au kulisoma Neno na kulielewa, bali furahia na kushangilia UNAPOLITENDA NENO. Biblia sio kitabu cha taarifa, au simulizi..bali ni kitabu cha MAELEKEZO ya Nini cha kufanya!..Maana yake tunapaswa tukitendee kazi kile tunachoelekezwa kwenye biblia, sio tukisome tu!!..au tuhubiriwe tu!..
Leo tunaishi katika kizazi cha watu wanaopenda sana kusikiliza mahubiri, wanapenda sana kuhubiriwa, wanaopenda sana kufundishwa biblia, lakini si wanaopenda KUTENDA KILE WANACHOKISIKIA AU WANACHOKISOMA AU WANACHOFUNDISHWA!!!!.
Yakobo 1:22 “Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, HALI MKIJIDANGANYA NAFSI ZENU.
23 Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo.
24 Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.
25 Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, HUYO ATAKUWA HERI KATIKA KUTENDA KWAKE.
Vile vile usifurahie kuwa Mtu wa UDHURU!.. Ukidhani Udhuru ni wako ndio utakaomfanya Bwana akuhurumie siku ile, la!.. Yeye siku zote analiangalia Neno lake alitimize na si udhuru zetu..
Luka 9:61 “Mtu mwingine pia akamwambia, Bwana, nitakufuata; lakini, nipe ruhusa kwanza nikawaage watu wa nyumbani mwangu.
62 Yesu akamwambia, Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu“.
Mathayo 10:37 “Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili.
38 Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili.
39 Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona”.
Jikane nafsi mtu wa Mungu… Unyakuo wa kanisa upo Karibu!
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
NENO LA MUNGU KATIKA UTIMILIFU WOTE.
GHARAMA YA UFALME WA MBINGUNI.
Tofauti kati ya ufalme wa mbinguni na ufalme wa Mungu ni ipi?
Hapo ndipo, atakapompa Mungu Baba ufalme wake.
Bwana Yesu asifiwe,
Ufukufu na Heshimu ni vyake milele na milele. Amina.
Napenda tutafakari, Pamoja kwa makini maneno haya ambayo Bwana Yesu alimfunulia mtume wake Petro, ni maneno ambayo yatakufaa sasa wewe kijana ambaye bado una nguvu za kufanya utakalo hivi sasa..
Embu Tusome;
Yohana 21:18 “Akasema, Amin, amin, nakuambia, Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na MWINGINE atakufunga na kukuchukua usikotaka”.
Hii kauli ni ya kuitafakari sana, sio ya kuichukulia juu juu, Hapa Bwana anamweleza Petro jinsi ujana wake unavyoweza kumpa uhuru wa ‘nani wa kujifunga chini yake’, na kumtumikia, mfano akiamua, ajifunge na kuwa mtumwa wa mali, uamuzi ni wake, akitaka ajifungue kisha ajifunge kwa mwingine tena, bado uwezo huo anao, leo anaweza akajifunga kwa Mungu, kesho kwa shetani, ni jinsi apendavyo kwasababu nguvu hizo anazo rohoni.
Hapo ndipo lile neno linalosema, “nimewaandikia ninyi vijana kwasababu mna nguvu ya kumshinda yule mwovu”(1Yohana 2:14), linapotimia, maana yake, uwezo wa kujifungua au kujifunga kwa shetani, unao, angali bado una nguvu..
Lakini tunaona Bwana Yesu anampa angalizo lingine na kumwambia, utakapokuwa mzee, “MWINGINE”..Atakufunga na kukuchukua usikotaka..
Sasa ulishawahi kutafakari huyo ‘mwingine’ ni nani?
Huyo mwingine ni Aidha “Mungu” au “Shetani”.. Maana yake ni kuwa utafika wakati, ambapo kama hutajiweka chini ya Mungu tangu sasa, shetani atakuweka chini yake kipindi hicho, penda usipende,..yaani utamilikiwa na shetani asilimia mia ya Maisha yako, na kukufanyia chochote apendacho juu yako..
Ukishafikia hii hatua, kamwe huwezi tena kumgeukia Mungu, wala hata kuzielewa Habari za Mungu, kwasababu tayari wewe ni mfungwa wa shetani.
Hali kadhalika kinyume chake ni kweli, unapofanyika chombo cha Mungu sasa angali una nguvu..utafika wakati huna nguvu, Mungu atakuchukua moja kwa moja na kukupeleka atakapo yeye.. Huko ndipo wakati ambapo uzee wako unaishia vema..hata kama ni kwa kifo kwasababu ya ushuhuda, lakini kamwe hutakaa upotee tena milele..kwasababu umeshafungwa tayari na Mungu, hivyo hakuna namna yoyote utakaa upotee au uanguke mikononi mwa shetani.
Ndio maana biblia inasema..
Mhubiri 12:1 “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo”.
Maana yake ni kwamba usipomkumbuka muumba wako leo, wakati una nguvu (wakati wa ujana wako) utafikia wakati, utapoteza furaha yako yote ya maisha.. Hicho ndicho kipindi cha kufungwa na ibilisi, na kupelekwa usipotaka..Angalia vema utaona wazee wengi ambao wamekuwa wakipuuzia injili tangu ujanani, mwisho wao huwa hauwi mzuri, kunakuwa na ugumu mkubwa sana kuwashawishi kwa Habari ya wokovu. Huwa wanapitia wakati mgumu sana kiroho kwasababu tayari “mwingine” ameshawafunga na kuwachukua wasipotaka..
Hivyo Bwana Yesu alikuwa anamtahadharisha Mtume Petro, sio tu kwa Habari ya kifo chake, lakini pia kwa maamuzi anayoyachukua sasa..lazima yawe ya busara.. Utumwa anaouchagua sasa, ndio utakaomuhifadhi baadaye..
Kama ni Kristo, basi Kristo atamwokoa, lakini kama ni shetani basi shetani atampeleka alipo yeye..
Ndugu, siku hizi ambazo waweza kusikia injili, na ukashawishika moyoni, ndizo siku zako za ujana, embu sasa anza kujiweka chini ya Kristo, akuongoze, achana na ulimwengu na mambo yake, wanadamu hawawezi kukufaidia chochote kwa siku zijazo.
Anza kuisafisha njia yako sasa, kama vile biblia inavyotushauri katika..
Zaburi 119:9 “Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako”.
Kumbuka, ni kipindi kifupi sana tumebakiwa nacho hadi kurudi kwa Bwana Yesu mara ya pili, Kama unadhani, Unyakuo bado sana, fikiria mara mbili, dalili zote zimeshatimia, injili inayoendelea sasa sio ya kubembelezewa wokovu, bali ni ya kujiingiza katika ufalme kwa nguvu. Huna sababu ya kuendelea kufichwa uhalisia, dakika hizi ni za majeruhi, siku yoyote, parapanda inalia, PARAPANDA INALIA!!
Bwana atusaidie.
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
PETRO AKAMWAMBIA YESU “BWANA NA HUYU JE”?
NI YESU YUPI UMEMPOKEA?, NI ROHO IPI UMEIPOKEA? NA INJILI IPI UMEIPOKEA?
Je! Ni kanisa lipi sahihi kumuabudia Mungu?
Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita.
Ni sahihi kusema sikuitiwa kuhubiri ubatizo kama Paulo alivyosema (1Wakorintho 1:17)?.
Katika 1Wakorintho 1:17, Paulo anasema hakuitiwa kubatiza, Je na mimi kama sijaitiwa kubatiza, bali nimeitiwa kuhubiri watu waokoke tu!, nitakuwa na hatia, nisipohubiri suala la ubatizo wala kuligusia kabisa?
Jibu: Ni muhimu kufahamu kuwa kila mtumishi wa kweli wa Mungu, haijalishi awe nani, ameitiwa KULIHUBIRI NENO LA MUNGU KATIKA UKAMILIFU WOTE, pasipo kubagua kipengele chochote katika maandiko. Huo ndio wito tuliopewa..
Tutatofautiana tu namna ya kuhubiri, kwasababu tunazo karama mbali mbali lakini INJILI NI MOJA KWETU WOTE!, Na wote tutahubiri kitu kimoja.. Hakuna mahali tumepewa maagizo ya kuhubiri tofauti tofauti au kulipunguza Neno la Mungu.
Sasa tukirudi kwenye swali, ni kwanini Paulo aseme sikuitiwa kubatiza?
Hebu tusome, mstari huo kwa utarati kisha tuendelee..
1Wakorintho 1:17 “Maana Kristo HAKUNITUMA ILI NIBATIZE, bali niihubiri Habari Njema; wala si kwa hekima ya maneno, msalaba wa Kristo usije ukabatilika”.
Hapa hakusema “MAANA KRISTO, HAKUNITUMA NIHUBIRI UBATIZO,” lakini badala yake anasema “KRISTO HAKUNITUMA NIBATIZE”. Maana yake kuhubiri Ubatizo Paulo alikuwa anauhubiri kama kawaida,(Soma Matendo 19:1-5 utalithibitisha hilo), lakini kitendo cha kufanya Ubatizo hakuwa anakifanya sana, bali mara moja moja sana… Ndio maana tukirudi juu kidogo katika mistari hiyo tunaona yeye mwenyewe anajishuhudia kubatiza watu baadhi..
1Wakorintho 1:14 “Nashukuru, kwa sababu sikumbatiza mtu kwenu, ILA KRISPO NA GAYO;
15 mtu asije akasema kwamba mlibatizwa kwa jina langu.
16 TENA NALIWABATIZA WATU WA NYUMBANI MWA STEFANA; zaidi ya hao, sijui kama nalimbatiza mtu ye yote mwingine”.
Umeona hapo anasema aliwabatiza Krispo, na Gayo Pamoja na watu wa nyumbani mwa Stefana.. Kuashiria kuwa alikuwa anabatiza, lakini hakuwa anaifanya hiyo huduma mara kwa mara, kulinganisha na huduma ya kwenda kuzunguka huku na huko kuhubiri Neno kwa watu aliyokuwa anaifanya.. Na wote walioamini injili yake aliwaongoza katika makanisa wabatizwe au watu maalumu wakabatizwe!..ili yeye apate nafasi ya kuendelea kuhubiri injili sehemu nyingine…Na ilipotokea hakuna mtu wa kuwabatiza kwa mahali hapo, basi alichukua yeye hilo jukumu la kuwabatiza!. kama hapo kwenye Matendo 19:2-6.
Ni sawa na jinsi Mitume walivyogawanya jukumu la kuwahudumia wajane, kwa wale Mashemasi 7 ili wao wadumu katika kulihubiri Neno.
Matendo 6:2 “Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, HAIPENDEZI SISI KULIACHA NENO LA MUNGU NA KUHUDUMU MEZANI.
3 Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili;
4 na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno.
5 Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia;
6 ambao wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu yao”.
Kwahiyo kwa hitimisho ni kwamba, Hakuna mtu yeyote ambaye ameitiwa kufundisha Neno moja la kwenye biblia na kuliacha lingine…Wote tunapaswa tuhubiri injili yote, iliyo kamili, yaani injili ya toba, ubatizo, Imani, Roho Mtakatifu, na mambo mengine yote ya kiimani, pasipo kupunguza chochote wala kuongeza. sawasawa na (Ufunuo 22:18-19).
Sababu kuu inayowafanya asilimia kubwa ya wahubiri wabague baadhi ya maneno kwenye biblia na kufundisha baadhi tu, ni kwasababu wanaogopa kuumiza hisia za watu au kupoteza waumini!, na wala si kitu kingine!!.. Jambo ambalo ni la hatari sana!.. kuacha kuhubiri Neno la Mungu kwasababu ya kohofia hisia za mtu, atajisikiaje, au atakuonaje.
Ni heri kuonekana hufai, lakini umelizungumza Neno la Mungu katika ukamilifu wote, Ni heri mtu ahuzunike moyoni kwasababu ya kweli ya Neno uliyomweleza, kwasababu itamuumiza moyo sasa, lakini baadaye itakuwa ni tiba kwake na atakuja kumshukuru Mungu sana kwaajili yako..
2Wakorintho 7:10 “Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti”.
Lakini unajua kabisa ubatizo aliobatizwa sio sahihi, mavazi anayovaa sio ya kiimani, kazi anayoifanya sio halali, na kwasababu unaogopa usiumie utakapomwambia ukweli, unaishia kumfariji kuwa wewe hujaitiwa kuhubiri ubatizo au Mavazi au kazi mtu anayoifanya, wewe umeitiwa kumhubiria amwamini Yesu tu!.. Fahamu kuwa ndio unazidi kumpoteza huyo mtu!.
Maran atha!
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Karama ya pili inayozungumziwa katika 2Wakorintho 1:15 ndio ipi?
JE! UMEBATIZWA UBATIZO SAHIHI?
Je! Ni kanisa lipi sahihi kumuabudia Mungu?
MFANO WA MAMBO HAYO NI UBATIZO.
Ulishawahi kukutana na kundi la watu ambao linakutafuta tu wakati wa shida, kama ndio, kuna hali Fulani unajisikia ambayo sio nzuri, ni kweli wapo ambao mazingira yanawabana washindwe kukutafuta nyakati nyingine, lakini wapo ambao wewe kwao ni mtu wa kuwatatulia tu matatizo, Habari nyingine na wewe hawana..
Kuna mtu mmoja alikuwa ananifuata nimtatulie tu matatizo yake, lakini baada ya hapo ukimpigia hata simu umsalimie, hapokei, na anabadilisha line ya simu moja kwa moja ili usimpate, baadaye anakuja kukutafuta tena, na jambo linalofuata hapo ni kuomba msaaada..
Unajua hata kama utamsaidia, lakini utasema kwanini iwe hivi, kwanini tusiwe na mahusiano hata na nyakati nyingine zote..
Sasa hiyo hali ndiyo ambayo Mungu anapitia sasahivi kwa wanadamu wengi duniani, biblia inasema..
Yeremia 2:27 “waliambiao gogo la mti, Wewe u baba yangu; na kuliambia jiwe, Ndiwe uliyenizaa; kwa maana wamenipa mimi visogo, wala hawakunielekezea nyuso zao; LAKINI WAKATI WA TAABU WATASEMA, SIMAMA UKATUOKOE”.
Umeona, wanadamu wengi sasa kinachowapeleka kwa Mungu, si kingine Zaidi ya kuomba, wafunguliwe, kuomba waponywe, kuomba wafanikishwe kiuchumi, kuomba kazi, n.k.
Lakini ukiangalia mahusiano waliyonayo na Mungu ni hafifu sana au hakuna kabisa.. Hana muda wa kusoma biblia kuyajua mapenzi ya Mungu ni nini katika Maisha yake, kumaliza hata dakika 20 kila siku katika kutafakari Neno la Mungu hawezi, kuomba kunamshinda, kwenda ibadani ni mara moja kwa mwezi, ikizidi sana mara mbili, na hata akienda ni ili Mungu amjibu lile ombi lake alilomuomba lakini sio kumwabudu katika Roho na Kweli.
Anachokiona kirahisi kwake, ni kwenda kununua maji ya upako na mafuta, ili amwage kwenye biashara zake, ili mambo yake yaende sawa.. Au pale anapopitia hali mbaya sana ya magonjwa ndipo anapomfuata Mungu ili amsaidie,. Hapo ndipo atafunga na kuomba, na kusoma Neno kila siku kwa bidii..Lakini siku nyingine zote anaishi maisha ya dhambi.
Ndugu, tujue kabisa Mungu hapendezwe na huo mfumo wetu wa Maisha, Mungu ametuzira watu wengi sana na sisi hatujui, ndio maana inakuwa ngumu sana kusaidiwa na Mungu kwasababu, Maisha yetu ni ya kinafki mbele zake.
Lakini ukiendelea kusoma pale Bwana anasema..
Yeremia 2:27 “waliambiao gogo la mti, Wewe u baba yangu; na kuliambia jiwe, Ndiwe uliyenizaa; kwa maana wamenipa mimi visogo, wala hawakunielekezea nyuso zao; lakini wakati wa taabu watasema, Simama ukatuokoe.
28 LAKINI WAKO WAPI MIUNGU YAKO ULIOIFANYA? Na wasimame hao, kama wakiweza kukuokoa wakati wa taabu yako; kwa maana hesabu ya miungu yako ni sawasawa na hesabu ya miji yako, Ee Yuda.
29 MBONA MNATAKA KUTETA NAMI? Ninyi nyote mmeniasi, asema Bwana”.
Umeona tusimgeuze Mungu kama ni sehemu ya kutatulia matatizo yetu tu, ili hali Maisha yetu hayaendani na wokovu. Tusitete na Mungu, Mambo hayo kayafanye kwa waganga wa kienyeji lakini usifanye kwa Mungu, kwasababu utajikuta unaangukia tu laana badala ya baraka.
Hivyo tuanze sasa, kumtafuta Mungu nyakati zote, tuhakikishe tunayatenda mapenzi yake, tuonyeshe bidii zetu kwake, kwamba tunampenda sio kiunafiki, bali kwa mioyo yetu kweli. Tunamtafuta sio atufanye kuwa mabilionea, bali atufanye kuwa wana wake kama Yesu Kristo. Na ndio sasa hata hayo mengine atasaidia bila hata kutumia nguvu wala kumwomba..
Kumbuka katika nyakati hizi za mwisho, watakaokwenda kwenye UNYAKUO, sio kila mtu asemaye ninamwamini Mungu tu, halafu basi,..Bali ni watu wayatendao mapenzi ya Mungu kikamilifu sawasawa na Neno la Kristo.
Mathayo 7:21 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.
22 Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?
23 Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”
Bwana atupe jicho la kuona, na kuyatendea kazi.
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
USIJARIBU KUMGEUZA MUNGU MGANGA WA KIENYEJI,UTAKUFA.
MLANGO MWINGINE WA ADUI KUTULETEA MAJARIBU.
NI KWA NAMNA GANI SHETANI ANAIZUIA INJILI?
Talanta ni nini katika biblia (Mathayo 25:14-30)
WAKATI ULIOKUBALIKA NALIKUSIKIA
Biblia inatuambia kuwa ilikuwa ni desturi ya Bwana Yesu kuingia hekaluni siku za sabato..Je! hiyo haimaanishi kuwa ni lazima na sisi tuishike sabato? (Luka 4:16)?.
Jibu: Tusome
Luka 4:16 “Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; NA SIKU YA SABATO AKAINGIA KATIKA SINAGOGI KAMA ILIVYOKUWA DESTURI YAKE, AKASIMAMA ILI ASOME”.
Bwana Yesu kuingia siku ya sabato katika masinagogi haimaanishi kuwa na yeye alikuwa anaiadhimisha au kuiabudu siku hiyo, kama walivyokuwa wanafanya wayahudi..La!.. yeye ndiye aliyekuwa Bwana wa Sabato (Luka 6:5).. hivyo kamwe hakuwahi kuitumikia au kuiadhimisha sabato kama walivyokuwa wanafanya wayahudi.
Sasa kama ni hivyo, ni kwanini biblia iseme ilikuwa ni DESTURI YAKE kwenda hekaluni kila sabato?
Ni kwasababu siku ya sabato ndio siku ambayo wayahudi wengi walikuwa wanakusanyika hekaluni kusikiliza maneno ya Mungu, siku nyingine walikuwa wanafanya kazi…hivyo ili Bwana awapate ilikuwa hana budi awafuate hekaluni katika siku hiyo hiyo ambayo wao wanaiheshimu, lakini endapo wangekuwa wana siku nyingine ya kukusanyika hekaluni tofauti na hiyo sabato, basi ingekuwa ni desturi ya Bwana kuwafuata katika hiyo siku.
Ni sawa na mtu atenge siku moja ya jumamosi au jumapili, na kuifanya kuwa desturi yake kwenda kufanya UINJILISTI WA NYUMBA KWA NYUMBA!!.. Sasa kwa kuitenga hiyo siku haimaanishi kuwa anaiadhimisha hiyo siku.. bali anaitumia hiyo siku kufanya uinjilisti wa nyumba kwa nyumba kwasababu katika siku hizo watu wengi wanakuwa manyumbani, hivyo ni siku nzuri za kufanya uinjilisti, tofauti na siku nyingine za katikati ya wiki ambazo watu wengi wanakuwa katika shughuli zao, na si manyumbani.
Na Bwana Yesu, na mitume wengine wote walizitumia siku za Sabato kuingia katika masinagogi kuhubiri, si kwasababu wanaziadhimisha siku hizo, bali kwasababu katika siku hizo ndizo watu wengi wanakuwa wanapatikana katika majengo ya ibada.
Sasa swali lingine hili; Sabato halisi ni ipi? na ni siku gani tupasayo kuabudu? Ili kufahamu kwa urefu fungua hapa >> Sabato halisi ni lini, Je! ni Jumapili au Jumamosi?, Ni siku gani itupasayo kuabudu?
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
IMESALIA RAHA YA SABATO KWA WATU WA MUNGU.
Nini maana ya ombeni kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi wala siku ya sabato?.
Sabato halisi ni lini, Je! ni Jumapili au Jumamosi?, Ni siku gani itupasayo kuabudu?
SABATO ILIFANYIKA KWAAJILI YA MWANADAMU NA SI MWANADAMU KWAAJILI YA SABATO!
Swali: Katika Mathayo 5:14 biblia inasema kuwa “Nuru yetu na iangaze mbele za Watu”, halafu tukienda kwenye Mathayo 6:1 maandiko yanasema “tusifanye wema wetu machoni pa watu”, hapa nahitaji ufafanuzi.
Jibu: Tusome
Mathayo 5:14 “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima.
15 Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani.
16 VIVYO HIVYO NURU YENU NA IANGAZE MBELE YA WATU, WAPATE KUYAONA MATENDO YENU MEMA, WAMTUKUZE BABA YENU ALIYE MBINGUNI”.
Tusome pia Mathayo 6:1-2..
Mathayo 6:1 “Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, KUSUDI MTAZAMWE NA WAO; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni.
2 Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ILI WATUKUZWE NA WATU”
Mistari hiyo miwili haijichanganyi, isipokuwa fahamu zetu ndizo zinazojichanganya.
Bwana Yesu aliposema Nuru yetu na iangaze mbele za watu.. ni ili Mungu atukuzwe kupitia matendo yetu mema tunayoyafanya!… Lakini tukifanya jambo lolote ambalo halitamrudishia Mungu utukufu bali litatupa sisi utukufu, huo sio wema Bwana Yesu alioumaanisha kuwa tuungaze..Ndio maana hapo kwenye Mathayo 5:16 anamalizia kwa kusema.. “wapate kuyaona matendo yenu mema, WAMTUKUZE BABA YENU ALIYE MBINGUNI.”..Na sio watutukuze sisi!!!.
Lakini tunapofanya Wema huku lengo letu ni watu watupe sisi utukufu, au watusifu, au watuone ni mashuhuri, huo sio wema bali ni Ubaya uliovaa vazi la wema ndani yake.. ndio maana katika huo mstari wa 2, Bwana anaweka msisitizo kwa kusema…
Mathayo 6:2 “Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ILI WATUKUZWE NA WATU”.
Umeona hapo lengo la wao kufanya mema yote hayo ni ili watukuzwe na watu, na si Mungu atukuzwe kupitia wao!..Hivyo hiyo ni dhambi!..
Jambo lolote tulifanyalo lisilomrudishia Mungu utukufu hata kama liwe jema kiasi gani, mbele za Mungu ni dhambi!.
Wakati Fulani Mfalme Herode aliwafanyia Wema watu wa Tiro kwa kuwasamehe na kuwapatia riziki, na akaandaa hotuba ambayo iliwafurahisha sana watu wa Tiro, hata kufikia hatua watu hao kumtukuza kwa kusema “Sauti yake ni sauti ya Mungu na si mwanadamu!”..
Na utaona baada ya pale, Mungu alimpiga Herode kwa Chango, kwasababu hakumpa Mungu utukufu, bali alijitukuza yeye!..(Habari hiyo unaweza kuisoma katika kitabu cha Matendo 12:20-24).
Kwahiyo na sisi hatuna budi kuzipima dhamira zetu katika wema wote tunaoufanya.. Je! Lengo letu ni kumpa Mungu utukufu, au kujitukuza sisi. Kama wema tunaoufanya ni kwa lengo la Mungu kutukuzwa basi huo tuufanye kwa bidii sana kwasababu mwisho wake ni Mungu kutukuzwa, lakini kama lengo ni sisi kutukuzwa, basi tujihadhari na huo.
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
NGAZI 7 AMBAZO MKRISTO NI LAZIMA AZIPANDE KUUFIKIA UKAMILIFU.
LAKINI NINYI, NDUGU, MSIKATE TAMAA KATIKA KUTENDA MEMA.
NI SAA KUMI NA MBILI (12) TU, ZA KRISTO KWAKO.
Ibada ni nini,Na je ili ikamilike inapaswa iwe na nini na nini?
Jibu: Tusome,
Luka 12:49 “Nimekuja kutupa moto duniani; na ukiwa umekwisha washwa, ni nini nitakalo zaidi?
50 LAKINI NINA UBATIZO UNIPASAO KUBATIZIWA, nami nina dhiki kama nini hata utimizwe!”
Ubatizo Bwana Yesu aliokuwa anaumaanisha hapo, ni kile kitendo cha KUZIKWA na KUFUFUKA kwake. Kwasababu maana yenyewe ya Neno ubatizo ni KUZIKWA.
Hivyo kwa kupitia mauti ya Bwana Yesu, Deni la dhambi zetu limefutwa/LIMEZIKWA. Na kama vile alivyofufuka katika upya na utukufu, pasipo mzigo wa dhambi zetu, vile vile na sisi tunapomwamini yeye na kubatizwa kwa njia ya maji, kama ishara ya kuakisi ubatizo wake yeye (wa kuzikwa na kufufuka kwake) tunakuwa tunakufa kwa habari ya dhambi na tunafufuka katika upya.
Wakolosai 2:12 “MKAZIKWA PAMOJA NAYE KATIKA UBATIZO; NA KATIKA HUO MKAFUFULIWA PAMOJA NAYE, KWA KUZIAMINI NGUVU ZA MUNGU ALIYEMFUFUA KATIKA WAFU.
13 Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote”.
Kwahiyo ubatizo wa Maji ni kivuli cha Ubatizo wa Bwana Yesu, (wa kuzikwa kwake na kufufuka kwake). Kama vile Bwana alivyozikwa katika makosa yetu na kufufuka pasipo makosa yetu, na sisi tunapozama katika maji na kuibuka juu… katika ulimwengu wa roho, tunakuwa tumekufa katika utu wa kale na tumefufuka katika utu upya. (Dhambi zetu zinakuwa zimeondolewa, Matendo 2:38).
Tunakuwa tunatembea katika utukufu ule ule ambao Bwana Yesu alitembea nao baada ya kufufuka kwake.. Na katika ulimwengu wa roho tunakuwa tumeketi naye..
Waefeso 2:5 “hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, tumeokolewa kwa neema.
6 AKATUFUFUA PAMOJA NAYE, AKATUKETISHA PAMOJA NAYE KATIKA ULIMWENGU WA ROHO, katika Kristo Yesu”
Kwahiyo kwa hitimisho ni kwamba Ubatizo Bwana alioumaanisha katika Luka 12:50 ni KUZIKWA na KUFUFUKA KWAKE. Na kabla ya huo kutimizwa ilipasa Bwana apitie mateso mengi (dhiki), kwa kukataliawa na kuteswa Kalvari, ndio maana anamalizia kwa kusema “nami nina dhiki kama nini hata utimizwe!”
Luka 9:22 “akisema, Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa NA SIKU YA TATU KUFUFUKA”.
Kufuatia maandiko hayo utaona ni jinsi gani ubatizo wa maji ulivyokuwa wa muhimu, na wala si wa kuupuuzia hata kidogo, Na maandiko yanasema mtu asipozaliwa kwa Maji na kwa Roho, (Yohana 3:5) hawezi kuurithi uzima wa milele. (na Kuzaliwa kwa maji ni ubatizo wa Maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo).
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
JE! UMEBATIZWA UBATIZO SAHIHI?
JE KANISA LITAPITIA DHIKI KUU?
Katika (Mathayo 25:8 na Marko 16:8) Wale wanawake walitangaza kufufuka kwa Bwana au walikaa kimya?
MFANO WA MAMBO HAYO NI UBATIZO.
Jina la Bwana Yesu libarikiwe, karibu tujifunze tena maneno ya Uzima ya Bwana wetu, Yesu Kristo. Neno la Mungu ni taa inayoongoza miguu yetu, na Mwanga wa njia zetu! (Zab. 119:105).
Ipo hali Fulani ambayo, Watoto wa kiume wengi wanakuwa na mapenzi mengi kwa mama zao, na kinyume chake asilimia kubwa ya Watoto wa kike wanakuwa na mapenzi Zaidi kwa baba zao kuliko mama zao. Ingawa si wakati wote au kwa Watoto wote inakuwa hivi, lakini asilimia kubwa inatokea kuwa hivyo.
Na biblia pia utaona imetaja au kuonyesha kuwepo kwa aina hii ya mahusiano kati ya wazazi na Watoto wa jinsia tofauti.
Hebu tusome visa kadhaa vya baadhi ya wafalme wa kwenye biblia, kisha kisha tuendelee mbele.
Yeremia 52:1 “SEDEKIA alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja hapo alipoanza kumiliki; naye akamiliki miaka kumi na mmoja huko Yerusalemu; NA JINA LA MAMA YAKE ALIITWA HAMUTALI, BINTI YEREMIA WA LIBNA.
2 NAYE ALITENDA YALIYO MABAYA MACHONI PA BWANA, sawasawa na yote aliyoyatenda Yehoyakimu.
3 Maana, kwa sababu ya hasira ya Bwana, mambo haya yalitokea katika Yerusalemu na katika Yuda, hata akawaondosha wasiwe mbele za uso wake, naye Sedekia akamwasi mfalme wa Babeli.
Hapa tunaona Mama wa Sedekia anatajwa kama sababu ya Ubaya wa Mfalme Sedekia… Sasa sio huyo tu!
1Wafalme 14:21 “Rehoboamu akaanza kutawala alipokuwa mwenye miaka arobaini na mmoja, akatawala miaka kumi na saba huko Yerusalemu, mji aliouchagua Bwana miongoni mwa kabila zote za Israeli, ili aliweke jina lake huko. NA JINA LA MAMAYE ALIITWA NAAMA, MWAMONI.
22 BASI YUDA WAKAFANYA MAOVU MACHONI PA BWANA; WAKAMTIA WIVU, KWA MAKOSA YAO WALIYOYAKOSA, KULIKO YOTE WALIYOYAFANYA BABA ZAO.
Ijapokuwa Rehoboamu alikuwa ni mwana wa Sulemani, na mjukuu wa Daudi, lakini mama yake anatajwa kumfanya awe mbaya…(sasa sio huyo peke yake..)
1Wafalme 15:1 “Mwaka wa kumi na nane wa mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati, Abiya alianza kutawala juu ya Yuda.
2 Miaka mitatu akatawala huko Yerusalemu; NA JINA LA MAMAYE ALIITWA MAAKA, BINTI ABSALOMU.
3 AKAZIENDEA DHAMBI ZOTE ZA BABAYE, ALIZOZIFANYA KABLA YAKE; wala moyo wake haukuwa mkamilifu na Bwana, Mungu wake, kama moyo wa Daudi babaye”.
Si huyu peke yake…
1Wafalme 8:26 “Ahazia alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala; akatawala mwaka mmoja huko Yerusalemu. NA JINA LA MAMAYE ALIITWA ATHALIA BINTI OMRI MFALME WA ISRAELI.
27 Akaiendea njia ya nyumba ya Ahabu, AKAFANYA YALIYO MABAYA MACHONI PA BWANA, kama walivyofanya nyumba ya Ahabu, kwa kuwa alikuwa mkwe wa jamaa ya Ahabu”.
Sio hawa tu…Unaweza kusoma pia habari za Mfalme Yothamu (2Wafalme 15:33), na Mfalme Manase (2Wafalme 21:1-2) na wengine wengi katika biblia, ambao utaona Uovu wao umesababishwa na mama zao.
Vile vile walikuwepo watu wa kawaida ambao hawakuwa wafalme, ambao pia tabia zao ziliathiriwa na mama zao, mfano wa hao ni yule kijana wa mwanamke wa kiisraeli, ambaye Habari zake tunazisoma katika Walawi 24:10-14, kijana huyu alimtukana Mungu, na akapigwa mawe mpaka kufa, na wengine wengi.
Lakini pia walikuwepo wafalme ambao walifanya mazuri, na Uzuri wao huo, Pamoja na sifa zao mbele za Bwana zilisababishwa na Mama zao..
1Wafalme 22:42 “Yehoshafati alikuwa mwenye miaka thelathini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka ishirini na mitano huko Yerusalemu. NA JINA LA MAMAYE ALIITWA AZUBA BINTI SHILHI.
43 AKAIENDEA NJIA YOTE YA ASA BABAYE; WALA HAKUGEUKA, AKIFANYA YALIYO MEMA MACHONI PA BWANA…..”.
1Wafalme 14:2 “Naye alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka ishirini na kenda katika Yerusalemu; NA JINA LA MAMAYE ALIITWA YEHOADANI WA YERUSALEMU.
3 AKAFANYA YALIYO MEMA MACHONI PA BWANA, ila si kama babaye Daudi; akafanya kama yote aliyoyafanya baba yake Yoashi”.
1Wafalme 15:2 “Alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala; akatawala miaka hamsini na miwili huko Yerusalemu. NA JINA LA MAMAYE ALIITWA YEKOLIA WA YERUSALEMU.
3 AKAFANYA YALIYO MEMA MACHONI PA BWANA, kama yote aliyoyafanya babaye Amazia”.
Sasa katika maandiko hayo yote, unaweza kujiuliza ni kwanini ni waMama, wanahusishwa na si waBaba?.. Ni kwasababu kuna muunganiko wa kipekee kati ya Mama na mtoto wake wa kiume, ambapo Mama asipoutumia vizuri huo muunganiko, anaweza kujikuta anaharibu hatima ya mtoto wake wa kiume moja kwa moja. (Ni vizuri kulijua hili mapema, ili mambo yatakapoharibika huko mbeleni, usije ukasema ulikuwa hujui!!)
Mama unapokuwa mtu wa kidunia, unakuwa mtu wa kumkataa Mungu, fahamu kuwa na mtoto wako wa kiume ni rahisi sana, kuamini hiyo njia yako kuwa ni njia sahihi, kuliko hata mtoto wako wa kike.
Lakini mtoto wako wa kiume anapokuona wewe ni mtu unayemcha Mungu, ni mtu unayeutafuta sana uso wa Mungu, na kuukataa ubaya, ni rahisi sana, mwanao wa kiume, na yeye kuwa kama wewe, hiyo ni (Siku zote weka hilo akilini).
Wafalme wote waliofanya machukizo kwa Bwana, waliharibiwa na Mama zao. Vile vile wafalme wote waliofanya Mema mbele za Bwana, na hata kusifiwa ni kutokana na Mama zao. Hakuna mahali popote wababa wametajwa, katika kutenengeneza hatima za Watoto wao wa kiume.
Hivyo kama Mama, Jifunze kuwapeleka Watoto wako Kanisani, ukiwapeleka wewe Zaidi ya baba hawawezi kuiacha hiyo njia, hata kama watakuja kuyumba kidogo, lakini watairudia tu njia hiyo siku moja!..
Vile vile wafundishe kusoma Neno, na kushika vifungu vya biblia, na kuomba.. Ukifanya hayo kwa Watoto wako wewe kama Mama, ni rahisi mambo hayo kuwaingia Zaidi kuliko kama angefanya Baba.
Halikadhalika msifie mwanao katika mambo ya ki-Mungu na mema, zaidi ya mambo ya ulimwengu huu tu…sauti yako ina thamani kubwa zaidi kwake kuliko baba yake, angefanya hivyo.
Na vile vile wewe Mtoto wa kiume, jifunze kumsikiliza Mama yako, anayekufundisha njia za Mungu, na kukuelekeza njia sahihi.. Kwasababu usipomsikiliza huyo, hakuna mwingine utakayekuja kumsikiliza tena katika Maisha yako.
Ipo methali ya watu wa ulimwengu isemayo “ASIYEFUNZWA NA MAMAYE, HUFUNZWA NA ULIMWENGU”. Ni watu wa kidunia wameitunga methali hii kufuatia uhalisia waliouona, kuwa kwa Mama kunayo mafunzo makuu, Zaidi ya kwa baba.
Hivyo Wewe kama Mama mtengeneze mwanao katika njia ya haki Mithali 22:6 “Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee”., ..na wewe kama mtoto wa kiume, msikilize Mama yako.
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
MWANAMKE, BINTI, MAMA.( Sehemu ya 1)
MWANAMKE, BINTI, MAMA. (Sehemu ya 2)
Je suruali ni vazi la kiume tu?
Ni kweli Paulo alipuuzia maonyo aliyopewa ya kwenda Yerusalemu?
SWALI: Biblia inamaana gani kusema “ maana vitu vyote ni watumishi wako”?. Je wanaotumia vifaa vya upako kama vile chumvi, maji, udongo, kuombea watu, wanatimiza kusudi lile lile la Mungu kwasababu na vyenyewe vinafanya kazi ya Mungu kwa nafasi hiyo? Je kwa mujibu wa andiko hilo ni sawa?
Zaburi 119:90 “Uaminifu wako upo kizazi baada ya kizazi, Umeiweka nchi, nayo inakaa.
91 Kwa hukumu zako vimesimama imara hata leo, MAANA VITU VYOTE NI WATUMISHI WAKO”.
JIBU: Ni kweli kama andiko hilo linavyosema, vitu vyote tunavyoviona katika mbingu na katika nchi ni watumishi wa Mungu, yaani, jua, mwezi, nyota, mawingu, milima, moto, maji, upepo, mafuta, udongo, mende, mbu, nzi, konokono, kipepeo vyote vinamtumikia Mungu.
Lakini swali ambalo tunapaswa tujiulize je vinamtumkia Mungu katika utumishi gani?
Ulishawahi kwenda kumuomba mjusi akusaidie kuomba rehema mbele za Mungu? Ulishawahi kuliomba jua likupe rizki, ulishawahi kuamka asubuhi na kuuambia mwezi ukuponye magonjwa yako, na ukuepushe na ajali?
Kwanini usifanye hivyo, ilihali vyote vinamtumikia Mungu?.. Lazima ufahamu utumishi wao ni upi mbele za Mungu, kwamfano, biblia inasema..
Zaburi 19:1 “Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, Na anga laitangaza kazi ya mikono yake”.
Ikiwa na maana kuwa tutazamapo mbingu na anga, basi tunahubiriwa utukufu wa Mungu kwa kupitia hivyo, hapo tayari vimeshamtumikia Mungu, lakini hatuwezi kwenda kutumia mawingu ili Bwana atujibu maombi yetu.
Mungu kaweka njia kwa kila jambo, Na njia pekee ambayo alituchagulia sisi ili tumfikie Mungu, na kupokea wokovu wetu, na baraka zetu ni kwa kupitia YESU KRISTO tu na JINA LAKE Hapo ndipo tunapoweza kusaidiwa mahitaji yetu, na dua zetu. Kwasababu hatuna jina lingine au kitu kingine chochote kiwezacho kutuokoa sisi isipokuwa Jina lake tu. . (Matendo 4:12)
Sasa wapo watu wanasema, mbona, Yesu alitumia udongo, mbona manabii walitumia chumvi,..Wanashindwa kuelewa yapo MAINGILIO YA MUNGU. Ambapo Mungu mwenyewe upo wakati anashuka mahali Fulani kwa muda , kulitimiza kusudi lake Fulani, ndipo anapotumia chochote apendacho, kisha baada ya hapo hakuna kitu kingine cha ziada katika hicho kitu.
Ndio maana utaona wakati ule alipomtumia punda kuzungumza na Balaamu, hatuona tena, punda wakitumika kuzungumza na watu, kana kwamba ndio kanuni, halikadhalika, Elisha alipoambiwa alale juu ya yule kijana kisha atakuwa mzima, hatuona tena, tendo hilo likifanyika hadi leo hii, tukilala juu ya wagonjwa ili wapate afya.
Ipo hatari kubwa sana ya kutumia vitu vya Mungu na kuvigeuza kuwa ndio kanuni za uponyaji, kosa mojawapo lililowafanya wana wa Israeli Mungu achukizwe nao, hadi kupelekwa tena utumwani Babeli, lilikuwa ni kuitumia ile sanamu ya shaba, Musa aliyoagizwa na Mungu aitengeneze kule nyikani, watu waiangaliapo wapone.
Hivyo watu wasiomjua Mungu, na MAINGILIO YAKE YA MUDA, wakaigeuza kuwa ndio sehemu ya ibada, walipofika nchi ya ahadi wakaiundia madhabahu kisha wakaanza kumwomba Mungu kupitia ile, mwisho wa siku wakawa wanaabudu mapepo pasipo wao kujijua na matokeo yake wakapelekwa Babeli utumwani.
Hivyo nawe pia ukiona mahali popote uendapo, vitu kama hivyo vimefanywa kama kanuni, kila wiki ni maji ya upako, mafuta, chumvi, au kingine chochote, ujue kuwa huna tofauti na wale waabudu sanamu, na jua na mwezi, na unayemwabudu hapo sio Mungu bali ni shetani mwenyewe. Na Unamkasirisha Bwana sana.
Jina ambalo tumepewa sisi, tulitegemee kwa kila kitu, na kila saa ni jina la YESU KRISTO TU.. Hilo ndio uligeuze kuwa sanamu yako, na si kitu kingine chochote. Kama ulikuwa unafanya hivyo basi acha mara moja.
Wakolosai 3:17 “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye”.
Hivyo, kwa hitimisho ni kuwa, mstari huo haumaanishi maji, au chumvi, au udongo, au kitu kingine chochote kinaweza kufanya shughuli ya upatanisho wa mwanadamu. Hapana ni uongo. Vinamtumikia Mungu, lakini sio katika mambo ya wokovu wetu.
Bwana atuepushe na sanamu.
Shalom
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
USIJARIBU KUMGEUZA MUNGU MGANGA WA KIENYEJI,UTAKUFA.
KWA KUWA WASEMA MIMI NI TAJIRI.
Bwana alimaanisha nini kusema“maana mtenda kazi astahili posho lake”
Nimekuwa kama mwari nyuni wa jangwani,