SWALI: Biblia inamaana gani kusema “ maana vitu vyote ni watumishi wako”?. Je wanaotumia vifaa vya upako kama vile chumvi, maji, udongo, kuombea watu, wanatimiza kusudi lile lile la Mungu kwasababu na vyenyewe vinafanya kazi ya Mungu kwa nafasi hiyo? Je kwa mujibu wa andiko hilo ni sawa?
Zaburi 119:90 “Uaminifu wako upo kizazi baada ya kizazi, Umeiweka nchi, nayo inakaa.91 Kwa hukumu zako vimesimama imara hata leo, MAANA VITU VYOTE NI WATUMISHI WAKO”.
Zaburi 119:90 “Uaminifu wako upo kizazi baada ya kizazi, Umeiweka nchi, nayo inakaa.
91 Kwa hukumu zako vimesimama imara hata leo, MAANA VITU VYOTE NI WATUMISHI WAKO”.
JIBU: Ni kweli kama andiko hilo linavyosema, vitu vyote tunavyoviona katika mbingu na katika nchi ni watumishi wa Mungu, yaani, jua, mwezi, nyota, mawingu, milima, moto, maji, upepo, mafuta, udongo, mende, mbu, nzi, konokono, kipepeo vyote vinamtumikia Mungu.
Lakini swali ambalo tunapaswa tujiulize je vinamtumkia Mungu katika utumishi gani?
Ulishawahi kwenda kumuomba mjusi akusaidie kuomba rehema mbele za Mungu? Ulishawahi kuliomba jua likupe rizki, ulishawahi kuamka asubuhi na kuuambia mwezi ukuponye magonjwa yako, na ukuepushe na ajali?
Kwanini usifanye hivyo, ilihali vyote vinamtumikia Mungu?.. Lazima ufahamu utumishi wao ni upi mbele za Mungu, kwamfano, biblia inasema..
Zaburi 19:1 “Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu, Na anga laitangaza kazi ya mikono yake”.
Ikiwa na maana kuwa tutazamapo mbingu na anga, basi tunahubiriwa utukufu wa Mungu kwa kupitia hivyo, hapo tayari vimeshamtumikia Mungu, lakini hatuwezi kwenda kutumia mawingu ili Bwana atujibu maombi yetu.
Mungu kaweka njia kwa kila jambo, Na njia pekee ambayo alituchagulia sisi ili tumfikie Mungu, na kupokea wokovu wetu, na baraka zetu ni kwa kupitia YESU KRISTO tu na JINA LAKE Hapo ndipo tunapoweza kusaidiwa mahitaji yetu, na dua zetu. Kwasababu hatuna jina lingine au kitu kingine chochote kiwezacho kutuokoa sisi isipokuwa Jina lake tu. . (Matendo 4:12)
Sasa wapo watu wanasema, mbona, Yesu alitumia udongo, mbona manabii walitumia chumvi,..Wanashindwa kuelewa yapo MAINGILIO YA MUNGU. Ambapo Mungu mwenyewe upo wakati anashuka mahali Fulani kwa muda , kulitimiza kusudi lake Fulani, ndipo anapotumia chochote apendacho, kisha baada ya hapo hakuna kitu kingine cha ziada katika hicho kitu.
Ndio maana utaona wakati ule alipomtumia punda kuzungumza na Balaamu, hatuona tena, punda wakitumika kuzungumza na watu, kana kwamba ndio kanuni, halikadhalika, Elisha alipoambiwa alale juu ya yule kijana kisha atakuwa mzima, hatuona tena, tendo hilo likifanyika hadi leo hii, tukilala juu ya wagonjwa ili wapate afya.
Ipo hatari kubwa sana ya kutumia vitu vya Mungu na kuvigeuza kuwa ndio kanuni za uponyaji, kosa mojawapo lililowafanya wana wa Israeli Mungu achukizwe nao, hadi kupelekwa tena utumwani Babeli, lilikuwa ni kuitumia ile sanamu ya shaba, Musa aliyoagizwa na Mungu aitengeneze kule nyikani, watu waiangaliapo wapone.
Hivyo watu wasiomjua Mungu, na MAINGILIO YAKE YA MUDA, wakaigeuza kuwa ndio sehemu ya ibada, walipofika nchi ya ahadi wakaiundia madhabahu kisha wakaanza kumwomba Mungu kupitia ile, mwisho wa siku wakawa wanaabudu mapepo pasipo wao kujijua na matokeo yake wakapelekwa Babeli utumwani.
Hivyo nawe pia ukiona mahali popote uendapo, vitu kama hivyo vimefanywa kama kanuni, kila wiki ni maji ya upako, mafuta, chumvi, au kingine chochote, ujue kuwa huna tofauti na wale waabudu sanamu, na jua na mwezi, na unayemwabudu hapo sio Mungu bali ni shetani mwenyewe. Na Unamkasirisha Bwana sana.
Jina ambalo tumepewa sisi, tulitegemee kwa kila kitu, na kila saa ni jina la YESU KRISTO TU.. Hilo ndio uligeuze kuwa sanamu yako, na si kitu kingine chochote. Kama ulikuwa unafanya hivyo basi acha mara moja.
Wakolosai 3:17 “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye”.
Hivyo, kwa hitimisho ni kuwa, mstari huo haumaanishi maji, au chumvi, au udongo, au kitu kingine chochote kinaweza kufanya shughuli ya upatanisho wa mwanadamu. Hapana ni uongo. Vinamtumikia Mungu, lakini sio katika mambo ya wokovu wetu.
Bwana atuepushe na sanamu.
Shalom
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp: Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
NEHUSHTANI (NYOKA WA SHABA).
USIJARIBU KUMGEUZA MUNGU MGANGA WA KIENYEJI,UTAKUFA.
KWA KUWA WASEMA MIMI NI TAJIRI.
Bwana alimaanisha nini kusema“maana mtenda kazi astahili posho lake”
Nimekuwa kama mwari nyuni wa jangwani,
Nini maana ya “chakula hakituhudhurishi mbele za Mungu”?
Unyenyekevu ni nini?
Rudi nyumbani
Print this post
MUNGU awabariki
MUNGU awabariki kwa fundisho zuri