Monthly Archive Juni 2022

Biblia inamaana gani iliposema “Dhambi ilipozidi, Neema ilizidi kuwa nyingi Zaidi”.

Jibu: Tusome..

Warumi 5:20 “Lakini sheria iliingia ili kosa lile liwe kubwa sana; NA DHAMBI ILIPOZIDI, NEEMA ILIKUWA NYINGI ZAIDI”.

Ili tuweze kuelewa vizuri labda tujifunze katika mfano mmoja au miwili ya kimaisha.

Umewahi kujiuliza ni kwanini gharama za usafiri wa Umma zipo chini, kuliko zile za usafiri binafsi?. Leo hii ukisafiri kutoka mkoa mmoja hadi mwingine, kwa kutumia basi la umma, utaona gharama zipo chini, kuliko ukitumia usafiri wako binafsi.

Sasa ni kwasababu gani iko hivyo?..Ni kwasababu mnapokuwa wengi mnachangia zile gharama, na hivyo kusababisha nauli kuwa ndogo kwa kila mmoja, lakini ukiwa peke yako itakubidi ubebe wewe gharama zote za usafiri, Maana yake badala ya kutoka Dar es salaam mpaka Dodoma kwa Tsh. Elfu 20, utajikuta unatumia laki 2 kwa safara hiyo hiyo, endapo utatumia usafiri binafsi.

Kwahiyo kwa ufupi tunaweza kusema “wenye uhitaji wa kusafiri wanapokuwa wengi, basi kunakuwa na neema ya punguzo la bei)”.

Au umewahi kujiuliza ni kwanini baadhi ya dawa au chanjo za magonjwa sugu ambayo yanaathiri watu wengi kwa wakati mmoja, kama Kifua kikuu, Ukimwi, au CORONA yanatolewa bure bila malipo?..si kwasababu madawa hayo ni ya gharama za chini, la! Ni ya gharama kubwa sana, lakini kwasababu yana waathiri watu wengi kwa wakati mmoja, nchi inafanya juhudi dawa hizo zipatikane bila malipo, ili hasara isiwe kubwa kwa taifa!..

Hivyo itaingia gharama ya kuyanunua madawa hayo kwa bei ya juu, na kuyagawa bure kwa wananchi!.

lakini laiti kama magonjwa hayo yangekuwa yanawaathiri watu wachache tu!, basi yangepatikana kwa gharama zile zile za juu tu!

Vivyo hivyo katika Imani, dhambi ya mtu mmoja pekee isingetosha kumleta Kristo ulimwenguni.. Kwasababu gharama ya kumwokoa mwanadamu ni kubwa sana si ndogo!. (Mungu kumtoa mwana wake wa pekee si gharama ndogo!). 1Wakorintho 7:23 “Mlinunuliwa kwa thamani; msiwe watumwa wa wanadamu”. Soma pia 1Petro 1:18.

Hivyo ilibidi wakosaji tuwe wengi, ili Neema nayo iwe nyingi!!…iweze kupatikana bure!! Hiyo ndiyo sababu kwanini Kristo hakuja ulimwenguni siku ile ile Adamu alipoasi.. Bali alikuja miaka mingi baadaye..

Warumi 5:16 “…….kwa maana hukumu ilikuja kwa njia ya mtu mmoja ikaleta adhabu; BALI KARAMA YA NEEMA ILIKUJA KWA AJILI YA MAKOSA MENGI, IKALETA KUHESABIWA HAKI”.

Hiyo ndio sababu pia kwanini kanuni ya kuupokea wokovu imerahisishwa namna hii!.. Ni kitendo tu cha KUMWAMINI Bwana YESU, na KUTUBU!, kwa kudhamiria kuacha dhambi, na KUBATIZWA katika ubatizo sahihi, na KUPOKEA ROHO MTAKATIFU. Basi!.. Ukiifuata hiyo kanuni, utakuwa umeupokea Wokovu kamili, na umeipokea Neema ya Mungu katika Maisha yako.

Itii injili leo, inapokuonya juu ya uvaaji wako mbaya, juu ya vimini unavyovaa na wigi unazovaa, juu ya wanja unaoupaka, juu ya lipstick unazotumia, juu ya suruali unazozivaa, juu ya mitindo yote ya kidunia uliyo nayo.. juu ya ulevi wako, na anasa na utukanaji ulionao!. Tubu leo na kuitii injili, kabla ya ule mwisho kufika..

Ukiyadharau maneno ya Mungu ya Uzima yanayokuonya leo, utafika wakati utatamani wokovu utaukosa.. na wakati huo, upo karibu kufika, wakati mlango wa neema utakuwa umefungwa!.. kitakachokuwa kimesalia ni hukumu ya ziwa la Moto!.

Waebrania 10:28 “Mtu aliyeidharau sheria ya Musa hufa pasipo huruma, kwa neno la mashahidi wawili au watatu.

29 MWAONAJE? HAIKUMPASA ADHABU ILIYO KUBWA ZAIDI MTU YULE ALIYEMKANYAGA MWANA WA MUNGU, NA KUIHESABU DAMU YA AGANO ALIYOTAKASWA KWAYO KUWA NI KITU OVYO, NA KUMFANYIA JEURI ROHO WA NEEMA?.

Kama hujampokea Yesu na kubatizwa na ungehitaji kumpokea leo na kubatizwa, basi tumia namba hizo hapo chini, kuwasiliana nasi ili tukusaidie juu ya hilo, pale mahali ulipo. Au tafuta kwa bidi mahali popote ambapo utaweza kupata msaada huo mapema sana kabla mambo hayajaharibika Zaidi.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

GHARAMA YA UFALME WA MBINGUNI.

BIBLIA INAITAJA NJIA KUU YA MFALME, NJIA HII NI IPI?

KAMA SI YESU, HABARI YETU INGEKUWA IMEISHA ZAMANI SANA.

KWANINI NDOA NYINGI ZINAVUNJIKA? (Sehemu ya 1: Upande wa wanaume)

TUNALINDWA NA NGUVU ZA MUNGU.

Rudi nyumbani

Print this post

UAMINIFU NI KIGEZO KIKUBWA CHA KUTUMIWA NA MUNGU.

Nakusalimu katika jina kuu sana la Bwana wetu Yesu Kristo, utukufu na heshima vina yeye milele na milele.AMEN. Nakukaribisha katika kuyatafakari maneno ya Mungu, na leo tutaona vile uaminifu unavyomshawishi Mungu, kukupa neema Zaidi ya unachokiomba.

Tumekuwa na maombi mengi sana mbele za Mungu, wakati mwingine tunatamani Mungu atutumie kama Fulani katika biblia, Lakini tusipojua kanuni za Ki-Mungu, kamwe hatutakaa tuvipate, haijalishi tutakuwa ni waombaji au wafungaji wazuri namna gani mbele za Mungu.

Mungu kumfanya Musa, kuwa Mchungaji wa taifa la Israeli, haikuwa ni kwasababu ni mwisraeli tu au anaomba sana. Hapana, ni kwasababu ya maamuzi aliyoyafanya zamani, ambayo yalimponza hata kuwa vile kama alivyokuwa kwa miaka 40. Musa aliona kustarehe katika jumba la kifalme, si kitu, moyo wake ukaanza kuugua juu ya ndugu zake waebrania aliokuwa anaona wanateswa, hivyo siku moja alipoona mmojawapo anaonewa na Mmisri, alikuwa radhi kumtetea ndugu yake, mpaka kumuua yule mmisri, kuonyesha kuwa aliwapenda waebrania kwelikweli, Hata siku ya pili yake, alipoona hao hao waebrania wanagombana, hakuwaacha hivi hivi tu, bali alikwenda kutafuta namna ya kuwapatanisha ili wawe na umoja.  Lakini yule aliyemtapeli mwenzake, akamwambia unataka kuniua kama ulivyomuua yule mmisri jana.

Musa angeweza kukana hayo mashtaka hata kwa rushwa kwasababu alikuwa na uwezo huo.. Lakini kinyume chake, akawa tayari, kukubali mashutumu, kwamba yeye ndiye aliyefanya vile, akakimbia akaenda zake jangwani, huku moyo wake ukiugua tu kwa ajili ya ndugu zake. Utaona japokuwa hakujua njia sahihi ya kuwaokoa ndugu zake, lakini alijitahidi kwa kadiri ya uwezo wake, kufanya awezacho.(Matendo 7:22-40)

Huyo ndio mtu ambaye baada ya miaka 40, Mungu anamtokea katika kijiti cha moto, akimwambia, nakutuma uenda Misri ukawaokoe watu wangu kwa mkono mkuu. Ndipo Mungu akamtumia kwa uwezo mkubwa namna ile, kwasababu aliona uaminifu wake, katika kile alichokitamani.

Matendo 7:35 “Musa huyo waliyemkataa, wakisema, Ni nani aliyekuweka kuwa mkuu na mwamuzi? Ndiye aliyetumwa na Mungu kuwa mkuu na mkombozi, kwa mkono wa yule malaika aliyemtokea katika kile kijiti.

36 Huyo ndiye aliyewatoa, akifanya ajabu na ishara katika nchi ya Misri, na katika bahari ya Shamu, na katika jangwa muda wa miaka arobaini”.

Ukitamani kuwa mchungaji, onyesha tabia hizo tangu sasa kabla hujawa mchungaji wa kanisa la Kristo, ili Bwana ashawishwe, kukupa huduma hiyo, je, unalipenda kundi la Mungu, je unalithamini? , je upo tayari kuwalisha watu chakula cha kiroho, na kusimama nao katika shida zao, bila kuruhusu ibilisi awameze?

Hilo ni jambo la muhimu sana, kulifanya sasa ndugu..

Daudi kabla hajafanywa na Mungu kuwa mchungaji wa Israeli, aliwahi kuwa mchungaji wa kondoo na mbuzi, lakini alipoona adui wanataka kuja kulishambulia kundi, hakuliacha na kukimbia, bali aliweza kupambana na simba, Pamoja na dubu na kuwashinda, akiwa na fimbo tu.  Mungu akamuona kuwa huyu anafaa hata kwa watu wangu Israeli kwasababu anathamini, kundi analoliongoza, hata kuwa tayari kuyahatarisha Maisha yake, kwa ajili ya hili..(1Samweli 17:34-36)

Umeona, Bwana Yesu alisema..

Luka 16:10 “Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia”.

Je ni sisi tuitwao wachungaji/Waalimu, wainjilisti,  tunazo tabia hizi?

Wapo watu wengine wanasema, Bwana naomba unipe mali nyingi kama Sulemani, ili nizitumie kuisogeza injili yako mbele. Kumbuka, kabla Mungu hajakupa, atahitaji kwanza, aone ulichonacho unakitoaje? Umebarikiwa laki moja, Je!, ulishawahi kuwa radhi kutoa vyote, au sehemu kubwa ya mali zako kwa Mungu mara nyingi, hata kuwa tayari kulala njaa,  au kukosa mahitaji yako, kwa Mungu?

Ikiwa hivyo hufanyi, unaishia tu kuomba, jua kuwa utajiri huo unaouhitaji, kamwe hutaweza kuupata.

Mtume Paulo, alilijua hilo, ndio maana akawa mwaminifu sana katika kumtumikia Mungu, katika udogo, ndipo Mungu akamfanya kuwa mtume na Mwalimu wa mataifa.

1Timotheo 1:12 “Nami namshukuru Kristo Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu kwa sababu aliniona kuwa mwaminifu, akaniweka katika utumishi wake;”

Hivyo ndugu, chochote, ukitamanicho kwa Mungu, waweza kukupata, lakini, anza sasa, kujitoa kwa hicho, kuwa tayari kuiponza roho yako, hata wakati mwingine kupoteza kila kitu, kwa ajili ya utumishi huo, na hakika yake utakipata kwa Mungu.

Uaminifu wako sasa ni mtaji wa ukitakacho kesho.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

JE UNATAMANI KUMJUA MUNGU, NA HUJUI PA KUANZIA?

THAWABU YA UAMINIFU.

Gongo na Fimbo ni nini?

Unyenyekevu ni nini?

NIFANYE NINI ILI NIPENDWE NA MUNGU?

Je! Shetani anao uwezo wa kuumba, kama Mungu?

Rudi nyumbani

Print this post

Hazina za gizani ni zipi? (Isaya 45:3).

Jibu: Tusome,

Isaya 45:3 “nami nitakupa hazina za gizani, na mali zilizofichwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni BWANA, nikuitaye kwa jina lako, naam, Mungu wa Israeli”.

Hazina za gizani ni baraka zote zilizoshikiliwa na adui shetani ambazo zingepaswa ziwe zetu.

Hazina hizi zinakuwa zinashikiliwa na adui kwa kitambo tu, na pale tunapotia bidii basi tunaweza kuzitwaa na kuzirejesha kwetu.

Mfano wa hazina za gizani ni zile wana wa Israeli walizozipata kutoka katika jeshi la Washami.

Wakati ule ambao Israeli walikuwa wana njaa kali, hata kufikia hatua watu kula mavi ya njiwa, na kichwa cha punda…na wakati huo huo mji wote ulikuwa umezungukwa na jeshi la Washami pande zote.

na Mungu akayasikilizisha majeshi ya washami mishindo ya farasi, na kwa hofu kubwa wakaacha vyakula vyao vyote na kukimbia kutoka katika zile kambi zao walizokuwepo, na wana wa Israeli wakaenda kuzitwaa zile Nyara na vile vyakula.. Hivyo wakawa wamepewa na Bwana hazina zilizikuwepo gizani.

2 Wafalme 7:5 “Basi wakaondoka kabla ya mapambazuko, ili waende mpaka kituo cha Washami; na walipofika mwanzo wa kimo cha Washami, kumbe! Hapana mtu.

6 Kwa maana Bwana alikuwa amewasikizisha Washami kishindo cha miendo ya magari, na kishindo cha farasi, kama kishindo cha jeshi kubwa; wakaambiana, Tazama, mfalme wa Israeli amewaajiri wafalme wa Wahiti, na wafalme wa Wamisri, waje wapigane nasi.

7 Kwa hiyo wakaondoka, wakakimbia kungali giza bado, wakaziacha hema zao, na farasi zao, na punda zao, na kimo chao vile vile kama kilivyokuwa, wakakimbia wapate kujiponya nafsi zao.

8 Basi wale wenye ukoma walipofika mwisho wa kituo, waliingia katika hema moja, wakala, na kunywa, wakachukua fedha, na dhahabu, na mavazi, wakaenda wakavificha; wakarudi, wakaingia katika hema ya pili, vile vile wakachukua vitu, wakaenda, wakavificha.

9 Ndipo wakaambiana, Mambo haya tufanyayo si mema; leo ni siku ya habari njema, na sisi tunanyamaza; mkingoja hata kutakapopambazuka, madhara yatatupata; basi twende tukawaambie watu wa nyumba ya mfalme.

10 Basi wakaenda, wakawaita mabawabu wa mji; wakawaambia, Tulifika kituo cha Washami, na tazama, hapana mtu ye yote huko, wala sauti ya mtu, ila farasi wamefungwa, na punda wamefungwa, na hema zao kama walivyoziacha.

11 Na mabawabu wakaita wakawaambia watu wa nyumba ya mfalme.

12 Mfalme akaondoka usiku, akawaambia watumishi wake, Sasa nitawaonyesha ninyi walivyotutendea Washami. Wanajua ya kuwa tuna njaa; basi wametoka kituoni, ili kujificha kondeni, wakisema Watakapotoka mjini, tutawakamata hai; tena tutapata kuingia mjini.

13 Na mmojawapo wa watumishi wake akajibu, akasema, Kunradhi; baadhi ya watu na watwae farasi watano katika hao waliosalia, waliobaki ndani ya mji (tazama wamekuwa kama mkutano wote wa Israeli waliobaki ndani yake; tazama, wamekuwa kama mkutano wote wa Israeli walioangamia), tukawapeleke tukaone.

14 Basi wakatwaa magari mawili na farasi zake; mfalme akawatuma kuwafuata Washami, akasema, Enendeni, mkaangalie.

15 Wakawafuata mpaka Yordani; na kumbe! Njia yote ilikuwa imejaa mavazi na vyombo, walivyovitupa Washami, wapate kukimbia upesi. Watu wale waliotumwa wakarudi, wakamwambia mfalme.

16 Basi watu wakatoka, wakaziteka nyara hema za Washami. Ikawa kipimo cha unga mzuri kikauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, sawasawa na neno la BWANA”.

Sasa huo ni mfano wa hazina ambazo zilikuwa gizani (yaani zimeshikiliwa na adui), lakini baadaye zikaondolewa kutoka kwa adui na kupewa watu wa Mungu.
Na hata sasa zipo hazina nyingi ambazo zipo gizani, ambazo zinapaswa ziwe za kwetu..Adui kazishikilia, na sisi tusipopiga hatua kwenye kuteka nyara basi adui ataendelelea kuzimiliki na sisi tutaendelea kutateseka.

Na hazina zenyewe zinaweza kuwa ni WATU au VITU. Kuna watu wetu wengi leo ambao wameshikwa na adui vile vile kuna vitu vyetu vingi ambavyo vimeshikwa na adui, ambavyo tukiwa imara katika Imani tunaweza kuvitwaa na kuviteka.
Maandiko yanasema..

2 Wakorintho 10:4 “maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;)

5 tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; NA TUKITEKA NYARA KILA FIKRA IPATE KUMTII KRISTO”.

Maana yake tukivaa silaha hizo za Mungu, basi tutakuwa na uwezo wa kuziteka hazina zote za gizani…kama ni watu wetu wapo gizani, basi tunaweza kuwatoa huko, kama ni vitu vyetu vipo gizani, basi tunaweza kuvirejesha endapo tukivaa silaha hizo na kuingia vitani.

Sasa swali ni je!. Hizo silaha za kwenda kuteka nyara hazina za gizani ni zipi?
Si nyingine zaidi ya zile silaha 7 tunazozisoma katika kitabu cha Waefeso 6:10-18, ambazo ni WOKOVU, KWELI, HAKI, IMANI, UTAYARI,NENO, na MAOMBI.

Ni kupitia silaha hizo tu, ndio tunaweza kuzipata hazina za gizani na mali zilizofichwa sawasawa na hiyo Isaya 45:3.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

Silaha za Mkono wa kuume na za mkono wa kushoto ni zipi

TUZIDI KUWA HODARI KATIKA BWANA.

Je Mkristo kutembea na walinzi (Bodyguards),ni sawa?

Kwanini Mungu aseme, Alaaniwe azuiaye upanga wake usimwage damu (Yeremia 48:10).

Deraya ni nini? Kama tunavyosoma katika Isaya 59:17

Rudi nyumbani

Print this post

Ulafi ni nini kibiblia?

Kikawaida ulafi ni tabia ya kupenda kula kuliko pitiliza, Sio vibaya kula, na pia sio dhambi kula na kushiba..

Lakini tabia hii inapovuka mipaka kiasi kwamba kila kitu kinachokuja mbele ya macho yetu ni kutamani kukila kama vile wanyama..(huo ni ulafi).

Biblia imetaja tabia hii kuwa haitokani na Roho Mtakatifu Kwasaababu matunda ya tabia hiyo ni mabaya.

Wagalatia 5:19 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi,

20 ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,

21 husuda, ulevi, ULAFI, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu”.

Mtu mlafi atatoa chochote ili ale au anywe, hata kama ameshiba, atatafuta kila njia ili aliridhishe tumbo lake kwa chochote atakachokitamani, anaweza hata kuiba, au kudhulumu, au kufanya jambo lolote lisilo la kiMungu ilimradi tu, apate chakula anachokihitaji.

Anaweza kuhudhuria karamu yoyote atakayoalikwa hata kama hiyo karamu ni ya mashetani..lengo lake ni ili ale na kunywa tu!.

Mtu mlafi ni rahisi kuingia katika mtego wowote wa ibilisi, Esau aliuza haki yake ya mzaliwa wa kwanza kwa chakula,

Waebrania 12:16 “Asiwepo mwasherati wala asiyemcha Mungu, kama Esau, aliyeuuza urithi wake wa mzaliwa wa kwanza kwa ajili ya CHAKUKA KIMOJA”.

Hebu tuangalie hekima moja ya Sulemani aliyoiandika kuhusiana na ulafi na madhara yake.

Mithali 23:1 “Utakapoketi kwa chakula pamoja na mtawala, Mwangalie sana yeye aliye mbele yako.

2 Tena ujitie kisu kooni, KAMA UKIWA MLAFI.

3 Usivitamani vyakula vyake vya anasa; Kwa maana ni vyakula vya hila……

6 Usile mkate wa mtu mwenye husuda; Wala usivitamani vyakula vyake vya anasa;

7 Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo. ATAKUAMBIA HAYA, KULA, KUNYWA; LAKINI MOYO WAKE HAUWI PAMOJA NAWE.

8 Tonge lile ulilokula utalitapika, Na maneno yako matamu yatakupotea.”

Umeona?..wanawake wengi na mabinti wanaingia katika mtego wa dhambi ya uasherati kutokana na ulafi (wanatamani kila aina ya chakula wanachokiona), na shetani anakitumia hicho kuwakamata.

Wengine wanaingia katika mitego ya kula rushwa kwasababu ya Ulafi, wengine wanaingia katika mitego ya kuua, au kudhulumu kwasababu ya Ulafi.

Na hata wengine wanaingia katika umaskini kwasababu ya ulafi (biblia inasema hivyo katika Mithali 23:20-21), Kwasababu muda wote mtu huyo anakuwa anafikiria kula tu, na hafikiri vitu vingine.

Na mojawapo ya dalili za siku za mwisho, biblia imetabiri ni watu kuwa WALAFI (watu watakuwa wakila na kunywa).

Luka 17:26 “Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu.

27 Walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakioa na kuolewa, hata siku ile Nuhu aliyoingia katika safina, gharika ikashuka ikawaangamiza wote”.

Hivyo hatuna budi kuwa na kiasi na kujihadhari na ulafi.

Luka 21:34 “Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ULAFI, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo;

35 kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima.

Na pia tabia ya ULAFI, siku zote inaenda kinyume na MFUNGO.

Mtu aliye mlafi, huwa hapendi wala hawezi kufunga na hivyo anakuwa pia anakosa baraka nyingi za kiroho kwasababu maandiko yanasema “mambo mengine hayatoki isipokuwa kwa kufunga na kuomba(Mathayo 17:21)”.

Hivyo kwa hitimisho ni kwamba tunapookoka hatuna budi kuacha na ULAFI pia!, Kwasababu tabia hiyo haitokani na Roho Mtakatifu.

1 Petro 4:3 “Maana wakati wa maisha yetu uliopita watosha kwa kutenda mapenzi ya Mataifa; kuenenda katika ufisadi, na tamaa, na ulevi, na KARAMU ZA ULAFI, na vileo, na ibada ya sanamu isiyo halali.

Bwana atubariki.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

Je! Mbinguni Kutakuwa na kula na kunywa?.

Je tunaruhusiwa kutumia vidonge wakati wa kufunga?

Nini maana ya “chakula hakituhudhurishi mbele za Mungu”?

Katika Mathayo 15:21-28, Yesu alikuwa na maana gani alipomwambia huyu Mama kwamba chakula cha watoto hawapewi mbwa?

CHAKULA CHA ROHONI.

Rudi nyumbani

Print this post

Njia zote za mtu ni safi machoni pake mwenyewe;(Mithali 16:2)

SWALI: Naomba kufahamu nini maana ya huu mstari,

Mithali 16:2 “Njia zote za mtu ni safi machoni pake mwenyewe; Bali Bwana huzipima roho za watu”.


JIBU: Kama vile Biblia inavyosema moyo huwa mdanganyifu kuliko kitu kingine chochote, (Yeremia 17:9), ikiwa na maana ni kawaida ya mwanadamu, kuziona njia zake zote alizozichagua ni sawa mbele zake, ni mara chache sana, kusikia mtu anakiri kuwa uamuzi anaoufanya ni wa kishetani,

Nimekutana na waganga wa kienyeji wanasema kitu tunachokifanya ni sawa, hakina madhara yoyote, ukienda kwa waabudu sanamu, watakuambia vivyo hivyo hizi ni ishara tu, tunaabudu Mungu yuleyule, Ukienda kwa wauza pombe watakuambia nao maneno hayo hayo  n.k… Kwasababu biblia inasema njia “ZOTE” (sio moja) za mtu ni safi machoni pake mwenyewe.

Lakini Bwana huzipima roho za watu. Ikiwa na maana, Mungu anazichunguza nia zetu. Yeye hashawishwi na kile tunachokiona ni sawa, kwa macho yetu, au kwa mitazamo yetu, bali anatazama ndani Zaidi ya mwanadamu, anaweka kwenye mizani, anatazama nia, ya mtu ilikuwa  ni nini, na matokeo yake yatakuwa ni nini mwishoni..

Kwamfano Mafarisayo na Masadukayo, walijihesabia haki, kwa mapokeo yao, wakijiona kuwa ni watakatifu, na bora kuliko wengine, lakini Bwana Yesu aliwaita wanafki. Kwasababu, kazi yao ilikuwa ni kusafisha kikombe kwa nje tu, lakini ndani ni kuchafu, wanafunga ili waonekane na watu, wanaomba ili waonekane ni wazuri katika mambo hayo. Walikuwa wanajifanya kumwita Yesu Rabi, lakini ndani wamejaa wivu. (Mathayo 23:1-39)

Hivyo nasi twapasa tulijue hilo, ili tusidanganyike.

Kitabu cha 1Wakorintho 13, inasema nijaposema kwa lugha za wanadamu na Malaika, nijapoutoa mwili wangu uungue moto, nijapotoa mali zangu zote niwape maskini, nijapokuwa na unabii, na Imani timilifu ya kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo mimi si kitu, ni sawa na bure tu.

Waweza kuwa mhubiri mzuri, mkubwa, unaokoa roho za watu, nawe ukaona njia hiyo ndiyo inayompendeza Mungu zaidi, lakini ndani yako unahubiri kwasababu ya fitina, kama inavyosema Wafilipi 1:15, au upate umaarufu, au upate fedha,.ujue unachokifanya ni bure.

Hivyo, katika lolote tulifanyalo, ili liwe na faida njema nyuma yake, lazima tujue nia yetu ya dhati kufanya hivyo ni nini, Ndicho Bwana anachokitazama sana, kuliko, hichi cha nje tukionyeshacho.

Kulikuwapo na wale watu, waliokataa, kwenda harusini walipoalikwa, na ukitazama kibinadamu sababu za wao kutokwenda zina mashiko kabisa, mwingine anasema ninaoa, hivyo ni sharti niwe na mke wangu kwa kipindi hiki, lakini Bwana Yesu aliona kama ni UDHURU wanatoa wote, kwasababu yeye ndio anayechunguza mioyo, akaona kutoa kwao udhuru ni kwasababu hawakuthamini wito wake tangu mwanzo.

Luka 14:16 “Akamwambia, Mtu mmoja alifanya karamu kubwa akaalika watu wengi,

17 akamtuma mtumwa wake saa ya chakula awaambie wale walioalikwa, Njoni, kwa kuwa vitu vyote vimekwisha kuwekwa tayari.

18 Wakaanza wote kutoa udhuru kwa nia moja. Wa kwanza alimwambia, Nimenunua shamba, sharti niende nikalitazame; tafadhali unisamehe.

19 Mwingine akasema, Nimenunua ng’ombe jozi tano, ninakwenda kuwajaribu; tafadhali unisamehe.

20 Mwingine akasema, Nimeoa mke, na kwa sababu hiyo siwezi kuja.

21 Yule mtumwa akaenda, akampa bwana wake habari ya mambo hayo. Basi, yule mwenye nyumba akakasirika, akamwambia mtumwa wake, Toka upesi, uende katika njia kuu na vichochoro vya mji, ukawalete hapa maskini, na vilema, na vipofu, na viwete.

22 Mtumwa akasema, Bwana, hayo uliyoagiza yamekwisha tendeka, na hata sasa ingaliko nafasi.

23 Bwana akamwambia mtumwa, Toka nje uende barabarani na mipakani, ukawashurutishe kuingia ndani, nyumba yangu ipate kujaa.

24 Maana nawaambia ya kwamba katika wale walioalikwa, hapana hata mmoja atakayeionja karamu yangu”.

Hivyo na sisi tusitoe udhuru katika mambo ya ki-Mungu, unapoitwa uokoke, hata kama unazo sababu elfu za kutokuacha hicho unachokifanya ikiwa Mungu anataka ukiache, tii tu. Kwasababu hatuwezi kumshawishi Mungu kwa mitazamo yetu tu, kwa vile tuonavyo sisi kuwa ni bora, au vafaa Zaidi kwasasa, naye akashawishika, bali anaelewa kila kitu, na matokeo ya vyote mwishoni utakuwaje..

Hatuna budi, kumtii Mungu.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

UTAYAFIKIAJE MANENO SAFI YA MUNGU?

Utii ni nini? na ni nani tunayepaswa kumtii au kutokumtii?

KUWA MWAMINIFU KWA MANENO YAKO MWENYEWE,

AKETIYE MAHALI PA SIRI PAKE ALIYE JUU.

NI VIZURI SISI KUWAPO HAPA.

VIACHENI VYOTE VIKUE HATA WAKATI WA MAVUNO.

MWENGE WAKO WA UHURU UPO WAPI?

Rudi nyumbani

Print this post

LAKINI SISI HATUKUIPOKEA ROHO YA DUNIA.

Biblia inasema..

1 Wakorintho 2:10-12

[10]Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu.

[11]Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu.

[12]LAKINI SISI HATUKUIPOKEA ROHO YA DUNIA, BALI ROHO ATOKAYE KWA MUNGU,makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu.

Zipo Roho mbili tu huku duniani.

Roho wa Mungu, na roho ya dunia. Kama mtu usipoipokea Roho ya Mungu, basi utaipokea roho ya dunia.

Hakuna mwanadamu anayejiongoza yeye mwenyewe  hapa duniani kwa roho yake tu. Hilo halipo.

Sasa kama jinsi hayo maandiko yanavyotuambia Roho wa Mungu huchunguza yote hata mafumbo ya Mungu.. Maana yake ni kuwa  yeye ndiye anayetufunulia siri za ufalme wa mbinguni, pamoja mambo ambayo Mungu anataka sisi tuyafanye tukiwa hapa duniani..ukisoma Yohana 16:13 inasema

[13]Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.

Umeona hiyo ndio kazi ya Roho wa Mungu..ndio maana mtu aliyepokea kweli Roho Mtakatifu hawezi ishi kidunia kwasababu ni roho nyingine kutoka mbinguni kwa baba ipo yake ikimfundisha kuishi kulingana na misingi ya Mungu.

Lakini kinyume chake ni kweli. Watu wote ambao hawana Roho wa Mungu, wanayo roho ya dunia

Na yenyewe inachunguza mambo ya ulimwengu huu na kuwafundisha watu kuishi kiulimwengu. Ndio maana hushangai kuona tabia nyingi mbaya kila siku zikivumbiliwa lengo tu ni kuwafanya kuwa wakidunia.

Ukiona mwanamke unapenda fashion, vimini, kujichubua, unavaa suruali, unaweka mak-eups, kijana unavaa milegezo, unanyoa viduku, unakunywa pombe, unacheza kamari, unasikiliza nyimbo za kidunia,  unakwenda disco, unafanya ushirikina, unazini, unakula rushwa, unaiba, unapenda fedha, unadanganya ni uthibitisho kuwa roho ya dunia imekuvaa ndio maana inakuhimiza na kukufundisha kufanya hayo mambo kwa bidii.

Na mwenye roho hii ni shetani mwenyewe..Na kama ikitokea  Bwana Yesu amerudi leo..basi ujue utabaki hapa duniani. Kwasababu roho yako ni ya hapa hapa na ka  ikitokea umekufa basi utaenda moja kwa moja kuzimu kwasababu huko ndiko hatma ya roho hiyo itakapoishia..

Biblia ipo wazi kabisa inasema..

Warumi 8:9

[9]Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. LAKINI MTU AWAYE YOTE ASIPOKUWA NA ROHO WA KRISTO, HUYO SI WAKE.

Ukikosa Roho wa Mungu, mbinguni huendi. Huu si wakati wa kumvumilia zaidi shetani, au kuwa rafiki wa dunia. Tunapojichanganya na mambo yake ndipo tunapovaliwa na roho hii chafu. Jiponye nafsi yako, ndugu, hizi ni siku za mwisho.

1 Yohana 2:15

[15]Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.

Hivyo ndugu, njia pekee ya kuipokea Roho ya Mungu ambayo itakusaidia na kukufundisha kuishi  maisha yanayompendeza Mungu. Ni kutubu kwa kumaanisha kabisa kugeuka na kuuacha ulimwengu..kisha ukishafanya hivyo unakuwa tayari kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo ikiwa kama haukubatizwa hapo mwanzo.

Baada ya huo wakati ni kuanza kuonyesha bidii ya kujifunza biblia, kuomba, kuzingatia fellowship zitakazokusaidia kukua kiroho. Na Roho wa Mungu akishaona umemaanisha hivyo, atashuka juu yako na kukutia Muhuri, na kukusaidia kuishi maisha ya wokovu.

Huku ukingojea siku yako ifike uende mbinguni, Roho hiyo ilipo.

Ikiwa utahitaji msaada ya kupokea wokovu, àu ubatizo sahihi.Basi wasiliana nasi kwa namba zetu hizi

+255693036618/ +255789001312

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizo

Mada Nyinginezo:

MFALME ANAKUJA

MBINGU MPYA NA NCHI MPYA. (Sehemu ya 1)

BWANA AWEZA KUKUPA ZAIDI SANA KULIKO HIZO.

Kusubu ni nini? Miungu ya kusubu ni ipi?

Je tunaruhusiwa kushirikiana na wasanii wa kidunia katika kumwimbia Mungu?

TUKIO LA MUSA NA ELIYA KUMTOKEA BWANA, LIMEBEBA UJUMBE GANI?

Rudi nyumbani

Print this post