Monthly Archive Juni 2022

HIZO NDIZO ROHO ZA MASHETANI.

Jina la mwokozi wetu Yesu Kristo lihimidiwe milele. Karibu tuyatafakari maandiko. Na leo tutaona ofisi kuu tatu za shetani, ambazo, zinafanya kazi humu duniani.

Biblia inasema..

Ufunuo 16:13 “Nikaona roho tatu za uchafu zilizofanana na vyura, zikitoka katika kinywa cha yule joka, na katika kinywa cha yule mnyama, na katika kinywa cha yule nabii wa uongo.

14 Hizo ndizo roho za mashetani, zifanyazo ishara, zitokazo na kuwaendea wafalme wa ulimwengu wote kuwakusanya kwa vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi”.

Hapa, tunaona watatu wanatajwa, ambao ni;

  1. Joka
  2. Mnyama
  3. Nabii wa uongo

Haya ni mapepo makuu matatu ya juu sana na yanayofanya kazi kwa kushirikiana, na kichwa chao akiwa ni ibilisi mwenyewe. Muunganiko huu ndio unaoukamilisha utawala mchafu wa mashetani unaofanya kazi duniani.

Sasa Ofisi ambayo, inafanya kazi sasa kwa nguvu ni hiyo ya JOKA, lakini hizo nyingine mbili zilizosalia yaani ya Mnyama na Nabii wa Uongo, kwasasa zinafanya kazi katika siri, lakini zitakuja kufanya kazi vema, katika kipindi cha dhiki, baada ya unyakuo kupita. Kipindi hicho ndio zitawepa mamlaka kamili ya kujidhihirisha duniani.

Sasa tuone kazi za hizi roho tatu ni zipi;

  1. Tukianzana na huyo wa kwanza yaani Joka.

Kama tunavyofahamu kazi kuu ya JOKA ni kumeza: Biblia inapomtaja joka (shetani), inalenga moja kwa moja katika kummeza Kristo mahali popote anapozaliwa,

soma Ufunuo 12:3-5

“3 Ikaonekana ishara nyingine mbinguni; na tazama, joka kubwa jekundu, alikuwa na vichwa saba na pembe kumi, na juu ya vichwa vyake vilemba saba.

4 Na mkia wake wakokota theluthi ya nyota za mbinguni, na kuziangusha katika nchi. Na yule joka akasimama mbele ya yule mwanamke aliye tayari kuzaa, ili azaapo, amle mtoto wake.

5 Naye akazaa mtoto mwanamume, yeye atakayewachunga mataifa yote kwa fimbo ya chuma. Na mtoto wake akanyakuliwa hata kwa Mungu, na kwa kiti chake cha enzi”.

Na ndio maana utaona pindi Kristo anazaliwa duniani, Joka hili lilisimama ndani ya Herode, kutaka kumuua, lakini lilishindwa..Hivyo mahali popote Kristo anapozaliwa, ni lazima joka ajitokeze kuleta vita, hata sasa mtu anapotaka kuokoka kwa kumaanisha kweli kumfuata Kristo, ajue kuwa ni lazima atakutana na vita vya hili joka, kwasababu sikuzote halitaki kumwona Kristo katika mioyo ya watu.

Na ndio mwishoni biblia inasema, likaenda kusimama katika mchanga wa bahari, yaani mahali ambapo, nchi kavu na Habari vinakutana, fukwe (beach), Yaani ikifunua kuwa lipo mpakani, kuwazuia watu wanataoka kutoka katika giza kuja katika nuru, hapo ndipo vita ilipo.. Kwa maelezo marefu juu ya hili fungua link hii usome >>>> NAYE AKASIMAMA JUU YA MCHANGA WA BAHARI.

Ufunuo 12:17 “Joka akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu; naye akasimama juu ya mchanga wa bahari”.

Hivyo, fahamu kuwa ukitaka kuwa mtakatifu, basi ujue pia joka litasimama kukupinga vikali. Lakini halitaweza kukushinda, ikiwa umedhamiria kweli kumfuata Kristo. Lakini ukiwa nusu nusu, yaani unataka hutaki, litameza Kristo wako, na hutazalisha chochote katika wokovu wako.

          2.  Mnyama.

Biblia inapotaja mnyama, inazungumzia utawala ya ibilisi kupitia falme kubwa za dunia. Alishatumia falme za dunia kadha wa kadha huko nyuma, kama vile Babeli, Umedi, Uyunani na Rumi, kuangusha watakatifu wa Mungu. Na utaunyanyua tena ufalme mwingine ambao utakuwa na nguvu sana, ufalme huu kichwa chake kitakuwa ni RUMI,  na utafanya kazi kwa kipindi kifupi sana yaani miaka pungufu ya saba (7), lakini utaleta, mabadiliko makubwa sana duniani, kiasi kwamba kila mtu atalazimishwa aufuate huo utawala.

Usipoufuata, hutaweza kuuza wala kununua, wala kuajiriwa. Biblia inasema utawala huo wa kishetani ambao utakuwa na chapa ya 666 nyuma yake, utafurahiwa na watu wote watatakaokuwa wamesalia, ambao majina yao hayakuandikwa katika kitabu cha uzima cha mwana-kondoo kabla ya kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu. Lakini wale wote watakaoonyesha dalili ya kuukataa au kuupinga, mwisho wao utakuwa ni kifo cha mateso makali sana ya dhiki.

Ufunuo 13:8 “Na watu wote wakaao juu ya nchi watamsujudu, kila ambaye jina lake halikuandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo, aliyechinjwa tangu kuwekwa misingi ya dunia”.

Jambo ambalo wengi wetu hatulijui ni kuwa, utawala huu tayari ulishafanya kazi huko nyuma,ambao ni ni Rumi, na ulishawaua watakatifu wengi sana Zaidi ya milioni 80, Lakini sasa Mungu ameuzuia kwa muda, lakini ndio utakaokuja kuzuka tena na kuyaongoza mataifa yote, katika utawala mpya, moyo wa utawala huo ni Vatican, Rumi, utakuwa na nguvu nyingi Zaidi ya ule wa kwanza, kwasababu utakuwa na sapoti ya mataifa yote makubwa unayoyajua leo hii duniani.

Ufunuo 17:8 “Yule mnyama uliyemwona alikuwako, naye hayuko, naye yu tayari kupanda kutoka kuzimu na kwenda kwenye uharibifu. Na hao wakaao juu ya nchi, wasioandikwa majina yao katika kitabu cha uzima tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu, watastaajabu wamwonapo yule mnyama, ya kwamba alikuwako, naye hayuko, naye atakuwako”.

   3.   Nabii wa Uongo.

Kama jina lake lilivyo, ni nabii, kazi yake ni kuwapotosha watu, kwa kuwapa maagizo ya uongo, wadhani kuwa wanapokea maagizo kutoka kwa Mungu kumbe ni kwa ibilisi. Biblia inasema hata sasa wapo manabii wa uongo, ambao wanaiga kazi ya mkuu wao, atakayekuja. Nabii huyu ndiye mpinga-kristo mwenyewe.

1Yohana 2:18 “Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho”.

Mpinga-Kristo huyu ambaye atakuja rasmi mara baada ya unyakuo wa kanisa kupita, atapewa uwezo wa kufanya ishara za uongo na shetani mwenyewe,atapewa uwezo wa kutenda miujiza feki kama ile ya Yane na Yambre kipindi cha Musa.

2Wathesalonike 2:6 “Na sasa lizuialo mwalijua, yule apate kufunuliwa wakati wake.

7 Maana ile siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi; lakini yuko azuiaye sasa, hata atakapoondolewa.

8 Hapo ndipo atakapofunuliwa yule asi, ambaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake, na kumwangamiza kwa ufunuo wa kuwapo kwake;

9 yule ambaye kuja kwake ni kwa mfano wa kutenda kwake Shetani, kwa uwezo wote, na ishara na ajabu za uongo”;

Na kazi yake kubwa itakuwa ni kuwashurutisha watu, waipokee ile chapa ya mnyama, na wengi watamuamini sana na kuipokea kwasababu ya zile ishara atakazokuwa anazifanya duniani.

Ufunuo 13:12 “Naye atumia uwezo wote wa mnyama yule wa kwanza mbele yake. Naye aifanya dunia na wote wakaao ndani yake wamsujudie mnyama wa kwanza, ambaye jeraha lake la mauti lilipona.

13 Naye afanya ishara kubwa, hata kufanya moto kushuka kutoka mbinguni uje juu ya nchi mbele ya wanadamu.

14 Naye awakosesha wale wakaao juu ya nchi, kwa ishara zile alizopewa kuzifanya mbele ya huyo mnyama, akiwaambia wakaao juu ya nchi kumfanyia sanamu yule mnyama, aliyekuwa na jeraha la upanga naye akaishi.

15 Akapewa kutia pumzi katika ile sanamu ya mnyama, hata ile sanamu ya mnyama inene, na kuwafanya hao wote wasioisujudu sanamu ya mnyama wauawe.

16 Naye awafanya wote, wadogo kwa wakubwa, na matajiri kwa maskini, na walio huru kwa watumwa, watiwe chapa katika mkono wao wa kuume, au katika vipaji vya nyuso zao;

17 tena kwamba mtu awaye yote asiweze kununua wala kuuza, isipokuwa ana chapa ile, yaani, jina la mnyama yule, au hesabu ya jina lake.

18 Hapa ndipo penye hekima. Yeye aliye na akili, na aihesabu hesabu ya mnyama huyo; maana ni hesabu ya kibinadamu. Na hesabu yake ni mia sita, sitini na sita.

Na mwisho kabisa, roho hizi zote tatu, yaani ya joka, mnyama na nabii wa uongo, zitaungana, na kuwaendelea wafalme wote wa duniani, ikiwemo wa hilo taifa lako unaloishi,  ili wapatane kwa kitu kimoja, kupigana na Mungu mwenyezi, pale Israeli, katika vita ile ya Harmagedoni, kipindi hicho ndicho Kristo atahitimisha vyote kwa kuwaua wanadamu wengi sana, na kuanzisha utawala wake mpya wa amani wa miaka elfu moja hapa duniani, naye atatawala kama MFALME WA WAFALME, NA BWANA WA MABWANA. Haleluya.

Hivyo ndugu, fahamu kuwa hizi ni nyakati za mwisho, kipindi kifupi sana tumebakiwa nacho,  Unyakuo ni siku yoyote, dalili zote zimeshatimia, mfumo wa yule mnyama upo tayari, unatendakazi tu kwa siri kwa dini ya uongo ya rumi, ni wakati wowote kunyanyuka, Tubu dhambi zako mgeukie Bwana Yesu kwa kumaanisha. Kubali kujitwika msalaba wako umfuate, kwasababu parapanda italia siku yoyote.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

UNYAKUO.

UFUNUO: Mlango wa 12

UFUNUO: Mlango wa 13

UFUNUO: Mlango wa 17

USIPOTEZWE NA MANENO YA MANABII WA UONGO.

DANIELI: Mlango wa 1

NA JINA LAKE AITWA, NENO LA MUNGU.

Rudi nyumbani

Print this post

Bwana alimaanisha nini kusema“maana mtenda kazi astahili posho lake”

Moja ya maagizo ambayo Bwana Yesu aliwapa wanafunzi wake alipowatuma kwenda kuhubiri injili mbali, lilikuwa ni kutokulipisha fedha katika huduma yoyote watakayoitoa, halikadhalika   kutokubeba chochote katika safari yao. Yaani wasiwe na maandalizi yoyote ya njiani, Lakini mwishoni kabisa mwa maagizo yake aliyasema maneno haya “maana mtenda kazi astahili posho lake”.. Sasa swali linakuja Je hili posho ni lipi alilostahili huyu mtandakazi ili hali ameitwa atoe bure?

Mathayo 10:8 “Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.

9 Msichukue dhahabu, wala fedha, wala mapesa mishipini mwenu;

10 wala mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala viatu, wala fimbo; maana mtenda kazi astahili posho lake”.

JIBU: Posho alilostahili ni lile ambalo Bwana Yesu mwenyewe atampa katika kazi ya injili anayoipeleka, kwa kupitia watu wakarimu ambao Bwana Yesu mwenyewe atawagusa moyo huko waendako aidha kwa kuwapa maji, au chakula, au nguo, na wakati mwingine hata fedha.

Hiyo yote ni kuonyesha kuwa Bwana Yesu anaweza kumtunza mtumwa wake, katika mazingira yoyote atakayomtuma. Na ndio maana mwishoni kabisa akawaambia maneno haya;

Luka 22:35 “Akawauliza, Je! Hapo nilipowatuma hamna mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu? Wakasema, La!

Ni ni kufunua kuwa hatupaswi kuwa na wasiwasi wa maandilizi yoyote ya huduma ya Kristo, pale ambapo hatuna chochote,  Bwana anataka tuwe wepesi (SIMPLE), tusijali sana tutakula nini, tutavaa nini huko tuendako, kesho tutatolea wapi nauli ya kurudi, hilo jambo Bwana hataki sisi kama watumwa wake tulifikirie, kwasababu ameahidi kabisa ikiwa tunatenda kazi yake kiuaminifu, basi tumestahili posho lake, hivyo anza kutumika.

Lakini haimaanishi kuwa, wakati wote, hata kama unacho, ndio ujifanye hauna, hapana, bali, upo wakati wewe kama mtumishi wa Mungu utabarikiwa na utakuwa na vya kuendea huko katika ziara, hivyo vitumie hivyo, Na ndio maana wakati mwingine Bwana aliwaambia wajibebe fimbo ya njiani, na kujifungia viatu, wakati sehemu nyingine kama tuliyosoma hapo juu aliwakataza.(Marko 6:8-9)

Kwahiyo, kwa vyovyote vile, Bwana atatunza, ilimradi tunamtumkia yeye kwa uaminifu. Tusiwe na wasiwasi na huduma yake, Haleluya..

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

ANGALIENI MWITO WENU.

WITO WA MUNGU HAUVUKI NENO LAKE.

MAAGIZO AMBAYO HAYAJAAGIZWA!

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA KITABU CHA TITO.

BWANA AWEZA KUKUPA ZAIDI SANA KULIKO HIZO.

HERI WAPATANISHI, MAANA HAO WATAITWA WANA WA MUNGU

Rudi nyumbani

Print this post

UJUE UCHAWI WA MANABII WA UONGO?.

Kuna makundi mawili ya WACHAWI!.

 1. Wachawi wa kawaida wanaojulikana; wanaopaa na Nyungo, na kuloga na kuwanga!. Hawa wanamharibia mtu Maisha yake ya kimwili tu, kufanya mtu awe na kasoro fulani fulani za kimwili, au kimaisha.

2. Manabii wa Uongo: Hili ni kundi la Pili la wachawi!, ambalo ni hatari sana kuliko hilo la kwanza!.. kundi hili haliwalogi watu kimwili bali kiroho.. yaani kazi yake ni kumsababisha mtu aukose uzima wa milele kwa kuiacha Imani au kwa kutoijua imani.

Hili kundi la Pili, ndio lile Mtume Paulo alilolizungumzia katika kitabu cha Wagalatia na lile Bwana alilotuambia tujihadhari nalo.

Wagalatia 3:1 “Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulibiwa?

2 Nataka kujifunza neno hili moja kwenu. Je! Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani?

3 Je! Mmekuwa wajinga namna hii? BAADA YA KUANZA KATIKA ROHO, MNATAKA KUKAMILISHWA SASA KATIKA MWILI?

Na Bwana Yesu alituonya tujihadhari na kundi hilo la Pili, Zaidi ya lile la kwanza.

Mathayo 7:15 “Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali”.

Manabii wa uongo ni wachawi wanaologa roho, ambao wamevaa mavazi ya karama za Mungu, wanajiita wachungaji, waalimu, wainjilisti, waimbaji, wahubiri n.k lakini katika utu wao wa ndani ni waharibifu wa roho za watu!.

Hawa hawatakuonea wivu wewe kuwa Maisha mazuri hapa duniani, tena watakuhubiria hayo!, watakupaka na mafuta, na kukulisha chumvi, na udongo ilimradi tu, upate mafanikio, wala hawataona wivu wewe kuzaa Watoto, wala hawatakuonea wivu wewe kufurahi duniani, kama lile kundi la kwanza, ambalo halitaki ufanikiwe hapa duniani.

Manabii wa uongo!, wenyewe hawana shida na wewe kufanikiwa.. wenyewe wanashida moja tu kwako!.. kwamba USIURITHI UZIMA WA MILELE!!!!. Hilo tu!!

Hebu tujifunze kwa nabii mmoja wa uongo katika biblia, (aliyekuwa mchawi wa roho za watu), na kisha tutapata kujifunza zaidi…

Matendo 13:6 “Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, MCHAWI, NABII WA UONGO, Myahudi jina lake BAR-YESU;

7 mtu huyu alikuwa pamoja na liwali Sergio Paulo, MTU MWENYE AKILI. Yeye liwali akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno la Mungu.

8 Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), AKASHINDANA NAO, AKITAKA KUMTIA YULE LIWALI MOYO WA KUIACHA ILE IMANI”.

Umeona hapo kazi ya huyo mchawi (aliye nabii wa uongo) ni ipi?.. Haikuwa kumwangia na kumloga Sergio asiwe Tajiri, au asiwe na akili, au asiwe na Watoto, bali ilikuwa ni KUMTIA MOYO WA KUIACHA IMANI YA BWANA YESU!!!.

Ndugu, Manabii wa uongo hata leo wanafanya kazi hiyo hiyo!.. wanashikilia biblia, wanahubiri, na wana majina ya kikristo (kama huyu Bar-Yesu) na mbaya zaidi wanatoa mpaka pepo, lakini ndani yao ni wauaji wa roho!!..

Kaka/Dada usifurahie kufarijiwa na mhubiri anayekuambia kuwa mambo yote ni sawa na huku hayaoni maisha yako yaliyojaa uzinzi, usifarijiwe na mchungaji yeyote, au nabii, au mwalimu, au padri, anayekuambia kuwa wewe ni mtoto wa Mungu, unayependwa na ilihali wewe ni mwizi, ni mlevi, ni muabudu sanamu, ni mgomvi, ni mtu wa hasira, ni mtu wa kutosamehe, ni mtu wa vinyongo na mtazamaji pornography, ni mtu wa kujichua ni mtu wa kuvaa na kutembea nusu uchi.. Tambua kuwa wewe bado hujawa mtoto wa Mungu katika hiyo hali ya dhambi uliyopo.

Jua huyo mchungaji au mwalimu anayekufundisha hivyo, hakupeleki kwenye Imani, bali anakutoa kwenye Imani..

Hiyo ndio kazi kubwa ya manabii wa Uongo!. KUKUFANYA UKAE MBALI NA ILE KWELI, AU USIIELEWE KABISA!!. Na ubaya ni kwamba hawa manabii wa uongo, WENGI WAO wanaujua ukweli! Lakini kwasababu wapo kwaajili ya kazi waliotumwa na baba yao (ibilisi), basi ndio wanaendelea kuwapotosha watu makusudi..

Neno la Mungu linasema..

Wagalatia 5:19 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi,

20 ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,

21 husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, KATIKA HAYO NAWAAMBIA MAPEMA, KAMA NILIVYOKWISHA KUWAAMBIA, YA KWAMBA WATU WATENDAO MAMBO YA JINSI HIYO HAWATAURITHI UFALME WA MUNGU”.

Itafute kweli yote ya Neno la Mungu..na JIHADHARI NA MANABII WA UONGO!..

Bwana Yesu anarudi na hizi ni siku za Mwisho.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

Usimwache mwanamke mchawi kuishi! Biblia ilimaanisha nini?

Nini maana ya “Torati na manabii”?

JIHADHARI NA UONGO WA SHETANI UNAOKARIBIANA NA UKWELI.

Tofauti ya kazi ya Damu ya Yesu na Jina la Yesu ni ipi?

ROHO YA MPINGA KRISTO IKITENDA KAZI SIKU HIZI ZA MWISHO

Rudi nyumbani

Print this post

Je kuchonga Nywele na Ndevu ni dhambi?

Jibu: Kabla ya kupata jibu la swali hili, hebu tujiulize kwanza swali lifuatalo: Je! Kuchonga nyusi (kuzitinda) ni dhambi??

Kama kuchonga nyusi ni dhambi, au ni kosa au ni jambo lenye taswira mbaya, na lisilopendeza basi pia kuchonga nywele za kichwani au kidevuni pia ni dhambi.. kwasababu zote ni nywele na zipo katika eneo la kichwa. Kama tutamhukumu anayechonga nyusi na tukamwacha anayechonga ndevu au nywele za kichwani, basi tutakuwa wanafiki!!.

Ni jambo gumu kidogo kulipokea lakini ukweli ndio ukweli, kuwa Wote wanaochonga ndevu, au vichwa vyao, au Nyusi zao, wanaenda kinyume na Neno la Mungu.  Na mimi nilikuwa hivyo zamani, lakini nimebadilika!..na nitazidi kubadilika kama nitagundua kuna mambo mengine ambayo nayafanya yanayokinzana na Neno au kanuni zake.

Tumepewa ruhusa ya kuzipunguza nywele zetu, lakini si kuzichonga!..tunapozichonga tunajitoa katika uhalisia na kwenda katika udunia, na kufanana na watu wa kidunia.

Sasa kwa kusema hivi sio kwamba tusiwe watanashati! La!.. tunapaswa tujiweke watanashati, lakini bila kuharibu uhalisia wetu.

Maandiko yanasema..

Walawi 19:27 “MSINYOE DENGE pembe za vichwani, wala msiharibu pembe za ndevu zenu”.

Sasa Neno “kunyoa denge” tafsiri yake ni “kuchonga”.. Hivyo maana ya huo mstari ni huu “Walawi 19:27 “Msichonge pembe za vichwani, wala msiharibu pembe za ndevu zenu”.

Maandiko yanasema miili yetu ni Hekalu la Roho mtakatifu, na kupitia miili yetu, tunahubiri injili kwa watu walio nje! Hivyo kimwonekano na kimwenendo hatupaswi kufanana kabisa na watu ambao wapo nje ya wokovu..

Kwasababu wakituona tunafanana nao watajiona wao wapo sawa katika njia zao mbaya, na mwisho wa siku ndio tunahubiri uvuguvugu ambao Kristo aliukataa na kuulaani katika kitabu cha Ufunuo 3:16.

1Wakorintho 3:16 “Hamjui ya kuwa NINYI MMEKUWA HEKALU LA MUNGU, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?

17 Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi”.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

Je kwa mkristo aliyeokoka, ni dhambi kunyoa ndevu zake?

NGUVU YA MNADHIRI WA BWANA.

Kwanini ndugu wanaokaa pamoja wawe kama mafuta ya Haruni?

Panda/ Sauti ya panda ni nini kibiblia?(Danieli 3:5)

KUJIPAMBA NI DHAMBI?

Rudi nyumbani

Print this post

Kupoza maana yake nini katika biblia? (Mathayo 10:8).

 Kupoza ni nini?

Jibu: “Kupoza” ni Kiswahili kingine cha neno “kuponya”. Hivyo badala ya kutumia neno kuponya, linaweza kutumika neno “kupoza” likawa na maana ile ile. (kama vile neno mtu na mwanadamu inavyoweza kuwa na maana moja).

Bwana Yesu aliwapa Mitume wake uwezo wa kupoza wagonjwa kupitia jina lake.

Marko 6:12 “Wakatoka, wakahubiri kwamba watu watubu.

13 Wakatoa pepo wengi, wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, WAKAWAPOZA”.

Na uwezo huo haukuishia tu kwa wale mitume 12, bali aliendelea hata watumishi wengine wengi waliomwamini Bwana Yesu kama akina Stefano na akina Barnaba, na Paulo.

Matendo 28:8 “Ikawa babaake Publio alikuwa hawezi homa na kuhara damu. Paulo akaingia kwake, akaomba, akaweka mikono yake juu yake, na KUMPOZA.

9 Yalipokwisha kutendeka hayo wengine waliokuwa na magonjwa katika kisiwa wakaja WAKAPOZWA”.

Na uwezo huo haukuishia tu kwa wakristo wa kanisa la Kwanza, bali hata leo uwezo huo Bwana katupa, wote tumwaminio pale tunapokwenda kuhubiri injili..

Mathayo 10:7 “Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia.

8 POZENI WAGONJWA, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure”.

Na si katika kuhubiri tu!.. bali hata popote pale tutakapokuwepo, uwezo huo utakuwa nasi..

Marko 16:17 “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya;

18 watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya”.

Yesu, anafanya miujiza hata leo!.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

LIPO LA KUJIFUNZA KWA WALE MASHUJAA 37 WA DAUDI.

SI MAPEPO YOTE NI YA KULIPUKA.

Nini maana ya msiwe waalimu wengi (Yakobo 1:3)?

NDIPO HUENDA AKACHUKUA PEPO WENGINE SABA.

Nini tofauti ya Uwezo na Uweza kibiblia?

Rudi nyumbani

Print this post

Kupiga ramli ni nini katika biblia?

Ramli ni elimu ya ufalme wa giza, wanayotumia waganga na wenye mapepo ya utambuzi katika kutabiri mambo yajayo, hivyo mtu yeyote anayetumia elimu hiyo kutabiri mambo yajayo, mtu huyo anapiga ramli.

Na watu walipiga ramli aidha kwa njia ya kutumia viganja vya mikono, au kwa kutumia viungo vya Wanyama.

Katika agano la kale, Bwana Mungu aliwakataza wana wa Israeli wasipige ramli ya aina yoyote ile, baadhi walitii na wengi hawakutii, bali waliendelea kupiga ramli na kufanya mambo mengine mabaya…jambo lililowafanya watolewe kutoka katika nchi yao na kupelekwa Babeli na Ashuru utumwani.

2Wafalme 17:16 “Wakaziacha amri zote za Bwana, Mungu wao, wakajifanyizia sanamu za kusubu, yaani, ndama mbili, wakafanya na Ashera, wakaliabudu jeshi lote la mbinguni, wakamtumikia Baali.

17 Wakawapitisha watoto wao, waume na wake, motoni, WAKAPIGA RAMLI, wakafanya uchawi, wakajiuza nafsi zao wapate kufanya yaliyo maovu machoni pa Bwana, hata kumkasirisha.

18 Kwa hiyo Bwana akawaghadhibikia Israeli sana, akawahamisha mbali na uso wake; wala hapana aliyesalia ila kabila ya Yuda peke yake

19 Hata na watu wa Yuda hawakuyashika maagizo ya Bwana, Mungu wao, lakini walikwenda katika amri za Israeli walizokuwa wamezifanya wenyewe.

20 BASI BWANA AKAKIKATAA KIZAZI CHOTE CHA ISRAELI, AKAWATESA, NA KUWATIA KATIKA MIKONO YA WATU WENYE KUWATEKA NYARA, HATA ALIPOKWISHA KUWATUPA, WATOKE MACHONI PAKE”.

Lakini swali la kujiuliza, je ni kweli Ramli ina matokeo yoyote??..Kwamba mtu akienda kwa mganga na kupiga ramli ili ajue kesho yake itakuwaje, ni kweli atatabiriwa sahihi mambo yajayo?.

Jibu ni la!.. Shetani kamwe hajui kesho kutatokea nini, kama vile mwanadamu asivyojua kesho ni nini kitatokea. Mwenye uwezo wa kujua kesho ni Mungu peke yake!, kwasababu yeye ndio MWANZO na MWISHO, fahamu zake hazina mipaka.

Lakini shetani anachoweza kufanya ni kupanga jambo leo ambalo anatumaini kuwa kesho litatokea. Kwahiyo mtu anayekwenda kwa mganga, akitaka kujua kesho yake itakuwaje..shetani atakachokifanya ni kumpangia huyo mtu kesho yake, jinsi itakavyokuwa.

Kwamfano mtu anakwenda kwa mganga kutaka kujua kama kesho atatembelewa na wageni au la!.. na yule mganga akamtabiria na kumwambia kwamba kesho atatembelewa na wageni, na tena akawataja na majina, na muda watakaokuja.. Na kweli kufikia hiyo kesho, hao wageni wakaja kama alivyotabiriwa jana.

Sasa hapo sio kwamba huyo mganga, kimiujiza kapelekwa kesho na kuona matukio yake. Bali anachokifanya ni kutuma mapepo, ambayo yatakwenda kuwaingia hao watu aliowataja na kuwashawishi wamtembelee huyo mtu katika huo muda aliopanga yeye siku ya kesho.

Kwahiyo hao wageni na wenyewe kama hali zao za kiroho zipo chini, basi wataingiliwa na hayo mapepo na kesho kwa kujua au kutokujua wanajikuta wanakwenda safari ambayo hawajaitegemea, ili kutimiza ubashiri wa huyo mganga!.

Kwahiyo wote wanaopiga ramli, ndio kitu wanachofanyiwa na shetani (wanatengenezewa matukio) pasipo wao kujua, wakidhani wanaambia mambo yajayo. Hiyo ndio sababu Bwana aliwakataza na anatukataza Watoto wake hata leo, tujiepushe na Ramli na aina yoyote ile pamoja na ushirikina, kwasababu zinaasisiwa na shetani, baba wa Uongo. (Yohana 8:44).

Shetani angekuwa anajua mambo yajayo (future), basi angejua hata siku ya unyakuo ni lini, lakini hajui chochote!. Anachojua kiufasaha ni mambo yaliyopita tu!, kwasababu tayari ni matukio ambayo yameshatokea, jambo ambalo pia lipo ndani ya uwezo wetu sisi wanadamu kujua mambo yaliyopita, lakini si kujua mambo yajayo.

Kwahiyo unapokwenda kwa mganga kupiga ramli kutaka kujua kesho yako, fahamu kuwa ni umeenda kwa shetani kutengenezewa kesho yako na si kuambiwa kesho yako, Utatengenezewa vifo na shetani, utatengenezewa mikosi, na shida, na vile vile utatengenezewa baraka bandia ambazo mwisho wake ni laana.

Ukitaka kuijua kesho yako itakuwaje soma Neno la Mungu..Hilo ndio litakupa unabii kamili na wa uhakika wa kesho yako jinsi itakavyokuwa.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

Kwanini Mungu aliwaagiza wana wa Israeli wasikisaze chakula?

Je shetani ana uwezo wa kujua mawazo ya mtu?

Nini maana ya kupiga Kite! Katika biblia.

Je ni halali kupiga kura kanisani kuchagua viongozi?

Rudi nyumbani

Print this post

“Si watu wa kutumia mvinyo sana”, je tunaruhusiwa kutumia mvingo kidogo?(1Timotheo 3:8).

Jibu: Tusome..

1 Timotheo 3:8 “Vivyo hivyo mashemasi na wawe wastahivu; si wenye kauli mbili, SI WATU WA KUTUMIA MVINYO SANA, si watu wanaotamani fedha ya aibu”.

Kufuatia mstari huu  wengi wamejikuta wamezama katika ulevi. Pasipo kujua msingi wa andiko hili kwa undani.

Tukisoma maandiko pasipo msaada wa Roho Mtakatifu tutajikuta tunaangamia badala ya kuponyeka..

2 Wakorintho 3:6 “Naye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; KWA MAANA ANDIKO HUUA, BALI ROHO HUHUISHA”.

Umeona?..andiko linaweza KUUA!!, shetani alijaribu kulitumia Andiko kumwangamiza Bwana Yesu kule jangwani wakati anajaribiwa.. “Alimwambia, jitupe chini kwakuwa imeandikwa (Mathayo 4:6-7)”..Lakini kwasababu Bwana alikuwa amejaa Roho Mtakatifu aliweza kutambua hila za shetani, na kumshinda.

Kwahiyo tukirudi katika hilo andiko linalosema kuwa Mashemasi wasiwe watu wa kutumia mvinyo sana, ni vizuri kujua muktadha wa andiko hilo, ili tusije tukafanya makosa katika kupambanua maandiko.

Sasa ili tuelewe vizuri andiko hilo maana yake ni nini, hebu twende mbele kidogo mpaka mlango wa 5, wa kitabu hicho hicho cha 1Timotheo. (Tafadhali zingatia maneno yaliyoainishwa kwa herufi kubwa).

1 Timotheo 5:23 “Tokea sasa usinywe maji tu lakini tumia mvinyo KIDOGO, kwa ajili ya TUMBO lako, na MAGONJWA yakupatayo mara kwa mara”.

Hapa tunaona Mtume Paulo kwa kuongozwa na Roho anamwambia Timotheo asitumie maji tu, bali na Mvinyo, (Na mvinyo wenyewe si mwingi bali KIDOGO).

Na ni kwasababu gani atumie mvinyo?..je! ni kwasababu ya burudani, au kujisisimua?? au kujiliwaza??, au kupunguza mawazo???…jibu ni la!..Bali ni kwasababu ya TUMBO na MAGONJWA, yampatayo mara mwa mara.

Maana yake mvinyo huo ulitumika kwa ajili la Matibabu ya magonjwa..na si kwaajili ya ulevi au kujisisimua..ndio maana hapo Paulo anamalizia kwa kusema KIDOGO..kiasi ambacho hakiwesi kumlewesha mtu, kwasababu ukitumika mwingi, utavuka lengo la matibabu, na kumfanya mtu alewe.

Na mvinyo uliokuwa unatumika, kwa matumizi ya matibabu, haukuwa kila aina ya mvinyo tu!..bali uliokuwa unatumika ni DIVAI tu!. Zamani Divai ilitumika kwa matumizi mengi, ikiwemo matibabu ya tumbo na sio tumbo tu bali hata majeraha.. Tunaweza kulithibitisha hilo katika ile Habari ya msamaria mwema.

Luka 10:33 “Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia,

34 akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia MAFUTA NA DIVAI; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza”.

Sasa Paulo kama alivyomuasa hapo Timotheo (ambaye ni askofu wa makanisa )kwamba ATUMIE MVINYO KIDOGO (Zingatia hili neno KIDOGO!!) kwa ajili ya tumbo na magonjwa ya mara kwa mara, na si burudani, ndio hivyo hivyo anawaasa mashemasi na maaskofu wengine kwamba na wao wasiwe watu wa kutumia mvinyo nyingi (maana yake watumie kidogo)..kwaajili ya magonjwa ambayo yatakuwa yanawapata mara kwa mara.

1 Timotheo 3:8 “Vivyo hivyo mashemasi na wawe wastahivu; si wenye kauli mbili, SI WATU WA KUTUMIA MVINYO SANA, si watu wanaotamani fedha ya aibu”.

Kwasababu madhara ya kutumia mvinyo nyingi ni kulewa. Na maandiko yanasema ulevi ni dhambi.

Waefeso 5:18 “Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho”.

Sasa swali la kujiuliza ni je, hata leo tunapopatwa na magonjwa ya tumbo, au majeraha ya mwili tutumie Divai kujitibu?.

Jibu ni la!.. Sasahivi tunayo madawa mengi, yanayotibu tumbo na majeraha kwa ukamilifu wote. Ni sehemu chache sana za dunia zilizosalia zinazotumia njia hiyo ya matumizi ya divai kidogo kwaajili ya tiba ya tumbo au vidonda.

Kwahiyo kwa hitimisho ni kwamba ULEVI NI DHAMBI, na walevi wote hawataurithi uzima wa milele.

Wagalatia 5:19 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi,

20 ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,

21 husuda, ULEVI, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu”.

Kama bado hujampokea Yesu, kumbuka hizi ni siku za Mwisho, kama bado ni mzinzi, au MLEVI, au mtukanaji, au mwizi, au muuaji, tambua kuwa upo hatarini!..hivyo suluhisho ni kumpokea Yesu ili akuoshe dhambi zako na kukusafisha.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

Je! ni halali kwa mtu wa Mungu kutumia njia za uzazi wa mpango,ikiwamo mipira?

Je tunaruhusiwa kutumia vidonge wakati wa kufunga?

Nini maana ya “Andiko huua, bali Roho huhuisha (2Wakorintho 3:6)

Kula uzao wa tumbo lako maana yake nini? (Kumbukumbu 28:53)

Je! mabalasi Bwana Yesu aliyoyatumia kugeuzia maji kuwa divai, yalitumika tu kwa kazi hiyo?

Rudi nyumbani

Print this post

Hapana hata mmoja aliyethubutu kuambatana nao;

SWALI: Biblia ina maana gani kusema maneno haya kwa habari ya mitume?

Matendo 5:13 “hapana hata mmoja aliyethubutu kuambatana nao; ila watu waliwaadhimisha;”

JIBU: Tusome habari hiyo tena;

Matendo ya Mitume 5:12-16

[12]Na kwa mikono ya mitume zikafanyika ishara na maajabu mengi katika watu; nao wote walikuwako kwa nia moja katika ukumbi wa Sulemani;

[13]na katika wote wengine hapana hata mmoja aliyethubutu kuambatana nao; ila watu waliwaadhimisha;

[14]walioamini wakazidi kuongezeka kwa Bwana, wengi, wanaume na wanawake;

[15]hata ikawa katika njia kuu hutoa nje wagonjwa, na kuwaweka juu ya majamvi na magodoro, ili Petro akija, ngawa kivuli chake kimwangukie mmojawapo wao.

[16]Nayo makutano ya watu wa miji iliyoko kandokando ya Yerusalemu wakakutanika, wakileta wagonjwa, nao walioudhiwa na pepo wachafu; nao wote wakaponywa.

Japokuwa Mungu alidhihirisha uweza mwingi na maajabu kwa mikono ya mitume, lakini kulikuwa na aina maisha/ mwenendo ambao haukuwa mwepesi kwa watu wengine kuufuata kama wao.

Na ndio maana maandiko yanasema hapo “hapana hata mmoja aliyethubutu kuambatana nao, japokuwa walikuwa  wanawaadhimisha, yaani wanawaonea fahari kama maaskari wa Bwana, waaminifu.

Na mwenendo wenyewe ambao uliwafanya watu wasiweze kufuatana nao, ndio huo wa kutokuogopa vifo, mapigo, mabaraza ya makuhani, mashutumu, na sura za watu.

 Ikumbukwe kuwa mitume walipoitwa hawakutumwa kwanza nchi za mbali bali waliagizwa waanzie kwanza pale pale Yerusalemu ambapo palikuwa na ukinzani mkubwa sana kutoka kwa wafalme na viongozi wa kidini,

na cha hatari zaidi mitume walikuwa wanaongozwa kwenda kuhubiri katika hekalu lile lile ambalo, Kristo alipindua meza zao, hata baadaye tena Petro na Yohana walipofungwa, kwasababu ya kuhubiria watu, mule hekaluni..utaona malaika aliwatoa na kuwaaagiza warudi kule kule hekaluni kuhubiri.

Matendo ya Mitume 5:18-21

[18]wakawakamata mitume wakawaweka ndani ya gereza;

[19]lakini malaika wa Bwana akafungua milango ya gereza usiku, akawatoa, akasema,

[20]Enendeni mkasimame hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya Uzima huu.

[21]Nao waliposikia wakaenda alfajiri hekaluni, wakaanza kufundisha.

Akaja Kuhani Mkuu nao waliokuwa pamoja naye, wakawakutanisha watu wa baraza, na wazee wote wa wana wa Israeli, wakatuma watu gerezani ili wawalete.

Unaona, Hata wakati kanisa linapitia dhiki Yerusalemu, na kuwafanya  watakatifu wote watawanyike, ni mitume peke yao waliendelea kubaki Yerusalemu.

Matendo ya Mitume 8:1

[1]Siku ile kukatukia adha kuu ya kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao mitume.

Hivyo kwa utumishi wa namna hiyo wa kuhatarisha maisha, haikuwa vyepesi kwa watu wengi, kuufuata..japokuwa watu walikuwa pamoja nao bega bega, wakifurahia ushujaa wao, wakitamani waendelee kumtumikia Mungu kwa ujasiri, injili ienee.

Jambo kama hilo tunaliona pia katika huduma ya  Bwana Yesu..

Biblia inasema wengi wa wakuu wa kidini walimuamini lakini hawakuweza kumkiri kwasababu ya hofu wa watu..

Yohana 12:42

[42]Walakini hata katika wakuu walikuwamo wengi waliomwamini; lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakumkiri, wasije wakatengwa na sinagogi.

Watu wengi hawakuweza kuambata na Yesu katika mapito yake lakini aliaminiwa na wengi.

Hii ni kufunua nini kwa watumishi wa Mungu?

Ikiwa umeitwa kama mtumishi wa Mungu..Ni lazima maisha yako yajikite katika utumishi wa Mungu kwelikweli, yaani viwango vyako vya kujikana lazima viwe juu zaidi ya watu wengine..

Ndivyo Mungu atakavyokutumia na ndivyo watu watakavyokuadhimisha kama ilivyokuwa kwa mitume.

Chachu yetu ni lazima izidi ya watu wengine. Bwana atusaidie sana.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

THAWABU ZA SIRI, ZA WATAKATIFU MBINGUNI.

SIKUJA KULETA AMANI DUNIANI, BALI MAFARAKANO.

KWANINI MITUME WAMUULIZE BWANA FARAGHANI?

Nini maana ya msiwe waalimu wengi (Yakobo 1:3)?

Kama tunaokolewa kwa neema kwanini wokovu tuupate kwa nguvu?

Ulafi ni nini kibiblia?

Rudi nyumbani

Print this post

Neno Kupatiliza maana yake nini katika biblia?

Kupatiliza ni neno lenye maana ya “kupiga/kuadhibu ”..mfano badala ya kusema “fulani, kapigwa na Mungu, unaweza kusema fulani kapatilizwa na Mungu”

Lakini swali la kujiuliza ni je!..Mungu huwa anapiga watu (anapatiliza)?

Jibu ni ndio!. Huwa anatoa adhabu, anawapatiliza waovu vile vile na wema endapo wakitoka nje ya mstari.

Lakini siku zote adhabu za Mungu lengo lake ni ili sisi tutubu na si kutukomoa au kutukomesha, kama sisi wanadamu tunavyokomeshana.

Tunapopatwa na majanga tofauti tofauti, ni ili tutubu tuache njia zetu mbaya na tulitafute kusudi la Mungu juu ya maisha yetu. Na pale tunapopata ufahamu na kugeuka kuiacha ile njia mbaya tuliyokuwa tunaiendea basi moja kwa moja, Bwana anaondoa yale mapatilizo na kutupatia mema.

Mfano wa mtu aliyepigwa baada ya kuliacha kusudi la Mungu ni nabii Yona.
Yeye alidhani kuacha kuitii sauti ya Mungu ataendelea kuwa salama!…kumbe kinyume chake ndio anazidi kuielekea ile hatari.

Akajikuta amekaa tumboni mwa samaki siku 3, bila kula wala kunywa.

Vile vile Bwana anawapatiliza Waovu hata kizazi cha tatu na cha nne..

Kutoka 20:4 “Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia.

5 Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, BWANA, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; NAWAPATILIZA wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao”.

Umeona?..ukiabudu sanamu, kama babu yako au kama baba yako au bibi yako au mama yako…Bwana atakupatiliza wewe mzao wake kama na wewe utaendelea na kuabudu sanamu kama wao.

Vile vile na wakristo wote waliomwamini Yesu wamepewa mamlaka na nguvu za kuvamia kambi za adui katika ulimwengu wa roho na kupatiliza (kupiga) kila kazi zote za giza, na kuyaacha huru mateka..

Tunaweza kuyasoma hayo katika…

2 Wakorintho 10:3 “Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili;

4 (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;)

5 tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo;

6 tena TUKIWA TAYARI KUPATILIZA maasi yote, kutii kwenu kutakapotimia”.

Na tunazipiga/patiliza Ngome za Adui kwa KUOMBA, KUHUBIRI na KUSOMA NENO.

Maran atha!.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp group:
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

Nini maana ya kupiga Kite! Katika biblia.

Je ni halali kupiga kura kanisani kuchagua viongozi?

KWANINI UPIGE MISHALE CHINI?

NENO LA MUNGU KATIKA UTIMILIFU WOTE.

Ngome ni nini?  Kwanini Mungu anafananishwa na ngome?

Rudi nyumbani

Print this post

KUNA AINA NGAPI  ZA MAOMBI?

Yapo maombi ya namna tofauti tofauti, lakini yote  ni lazima yaangukie katika mojawapo ya makundi haya Matano (5).

1)   Kusifu na Kuabudu.

Wengi hawafahamu kama sifa zetu ni maombi yanayojitegemea kwa Mungu, haya ni maombi yanayomwasilia Mungu katika mfumo wa nyimbo, halikadhalika pia kwa kumwadhimisha kwa matendo yake makuu aliyoyafanya kwa kuzungumza kwa vinywa vyetu.. ndio maombi ya kwanza yenye nguvu. Tunapomsifu Mungu katika Roho na kweli, ni Zaidi ya maombi mengine yote tunayoweza kuyapeleka kwake.,

Biblia inasema Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu;(1Nyakati 16:29), Na pia Mataifa yote yamsifu yeye. Mambo mengi, na vifungo vingi huwa vinafunguka, pale tu tunapomsifu Mungu kwa kumaanisha katika Roho na kweli, Kwasababu ni maombi yanayouvuta uwepo wa Mungu kwa haraka sana juu ya mtu, Na ndio maana ibada zote lazima zitanguliwe na maombi haya.

2) Maombi ya Upatanisho.

Ni maombi ya kuwaombea wengine, Zaidi ya kwako mwenyewe. Kuwaombea watakatifu,  kuwaombea, wanyonge, kuliombea taifa, viongozi, hata maadui zako n.k. Haya ni maombi ambayo yanampendeza Mungu sana. Danieli alifunga na kuomba kwa ajili ya taifa lake Israeli, na dhambi zao, Na Mungu akamsikia akamrehemu (Danieli 9:1-27).

 Bwana Yesu alipokuwa duniani, sehemu kubwa ya maombi yake ilikuwa ni kutuombea sisi (Yohana 17) hivyo akasema pia, tuombeane sisi kwa sisi ili tupate kuponywa (Yakobo 5:16). Ikiwa na maana wengi hawawezi kuokoka/kufunguliwa wenyewe, ikiwa sisi hatutawaombea, Na pale maombi haya yanapokuwa ya muda mrefu (ya dua), basi huwa yana nguvu Zaidi, kupelekea kutupa kibali cha kupendwa na Mungu, kama ilikuwa kwa Danieli.

3) Maombi ya Mahitaji.

Ni maombi ya kupeleka haja zetu kwa Mungu, ikiwemo, kumwomba Roho wake, rizki, amani, furaha,  uponyaji, kibali, fursa, gari n.k. Bwana Yesu alisema pia, tuombapo tuombe Bwana atupe rizki zetu,(Mathayo 6:11). Na pia alisema tuombe nasi tutapewa. Haya ndio maombi yanayojulikana na kuombwa na watu wengi sana.

Luka 11:11 “Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki atampa nyoka?

12 Au akimwomba yai, atampa nge?

13 Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?”

4) Maombi ya Shukrani.

Ni maombi muhimu kwa kila mwanadamu, ni maombi ya wakati wote, ya asubuhi, ya mchana, na jioni, tunamshukuru Mungu, kwa uhai, afya, chakula, makazi, Malazi, familia,

Wakolosai 3:15 inasema “….tena iweni watu wa shukrani.”. Ulishawahi kushukuriwa kwa wema Fulani uliomtendea mtu, ukaona hali unayojisikia ndani ya moyo wako kwa shukrani ile..Ndivyo ilivyo kwa Mungu anapoona Sio kila majira tunaenda kumpelekea tu mahitaji yetu..Bali wakati mwingine tunamkaribia kumshukuru kwa vile anavyotufanyia. Inampendeza sana moyo. Na wakati mwingine kupelekea hata kupewa vile vilivyosalia, kwasababu tunaonyesha kuthamini neema yake.

5) Maombi ya Vita.

Ni maombi ya kushindana, na nguvu za giza, kwa mamlaka ya rohoni tuliyopewa katika damu ya Yesu, Hapa tunatangaza ushindi, na pia kutamka kwa Imani katika Neno la Mungu. Yapo mambo mengine ibilisi hawezi kuyaachia kirahisi rahisi. Hivyo inahitaji kukemea, kuamuru, kuvunja, na kubomoa, kwa Imani.

Ufunuo 12:10 “Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku.

11 Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa”.

Hivyo kama watakatifu tukijifunza kutumia aina hizi tano za maombi, bila kupuuzia hata moja, basi, tutakuwa ni askari wazuri sana katika roho.

Shalom

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

NJIA SAHIHI YA KUFUNGA.

Nifanyeje niwe mwombaji mzuri, wa masafa marefu?

YAFUATAYO NI MAWAZO YA ADUI HIVYO USIYASIKILIZE.

WALA TUSIACHE KUKUSANYIKA PAMOJA

LAKINI SISI HATUKUIPOKEA ROHO YA DUNIA.

Matulizo ya mapenzi ni nini? (Wafilipi 2:1)

Rudi nyumbani

Print this post