Title March 2024

Yesu kuvishwa taji la miiba kichwani, kulifunua nini?

SWALI: Yesu kuvishwa taji la miiba kichwani alipokuwa anasulubiwa kulikuwa kuna funua nini rohoni?


JIBU: Kila tendo alilotendewa Yesu katika kipindi cha mateso yake lilikuwa lina ufunuo wake rohoni. Tunajua wale askari waliposikia kuwa yeye ni mfalme, muda ule ule walimvisha vazi la kifalme, kisha wakampa fimbo, na baada ya hapo wakasokota taji la miiba, wakamvisha kichwani, kisha wakaanza kumdhihaki, huku wakimpiga wakisema..  Salamu! Mfalme wa Wayahudi!

Yohana 19:2  “Nao askari wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani, wakamvika vazi la zambarau. 3  Wakawa wakimwendea, wakisema, Salamu! Mfalme wa Wayahudi! Wakampiga makofi”

Tunajua lengo la wale maaskari kumvisha miiba ni kumfanya aumie zaidi, lakini upo ufunuo mkubwa rohoni, pengine kwanini asingevishwa la matambara mabovu, au taji la udongo, au la vyuma vyenye ncha kali, badala yake wakaona miiba.

Kibiblia, miiba, huwakilisha “mahali palipolaaniwa”.

Adamu alipoasi, Mungu alimwambia ardhi imelaaniwa kwa ajili yako, hivyo itatoa miiba na michongoma. Na matokeo yake ni kwamba italimwa kwa shida

Mwanzo 3:17 Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako;  18 michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni;

Ndio maana shamba ambalo  halipaliliwi  au halitunzwi, matokeo yake ni kuwa linatoa miiba.

Mithali 24:30 Nalipita karibu na shamba la mvivu, Na shamba la mizabibu la mtu asiye na akili.  31 Kumbe! Lote pia limemea miiba; Uso wake ulifunikwa kwa viwawi; Na ukuta wake wa mawe umebomoka.  32 Ndipo nilipoangalia na kufikiri sana; Naliona, nikapata mafundisho.  33 Bado kulala kidogo, kusinzia kidogo, Bado kukunja mikono upate usingizi! 34 Hivyo, umaskini wako huja kama mnyang’anyi, Na uhitaji wako kama mtu mwenye silaha

Na vivyo hivyo rohoni, mioyo yetu inafananishwa na mashamba. 

Ukisoma ule mfano wa mpanzi, utaona mbegu(Neno la Mungu), lilipopandwa, zipo ambazo ziliangukia kwenye miiba (yaani mahali ambapo hapajafyekwa na kupapaliwa), ndipo pale kwenye miiba, na mwishowe zikakua na kumea. Lakini zikasongwa na ile miiba hazikashindwa kuzaa.

Yesu akatoa tafsiri yake, akasema, miiba ile ni “anasa, udanganyifu wa mali, na shughuli za ulimwengu huu”.

Luka 8:14  “Na zilizoanguka penye miiba ni wale waliosikia, na katika kuenenda kwao husongwa na shughuli na mali, na anasa za maisha haya, wasiivishe lo lote”.

Sasa Yesu alipokuja kufa msalaba, alishughulika na jambo hilo kubwa, kubeba laana hiyo kubwa kwenye kichwa chake.

Akimaanisha kuwa ile nchi iliyolaaniwa (yaani mioyo wa mtu), kuanzia sasa ni mwisho. Imekwisha.

Miiba iliyokuwa inatoka mimi nimeichukua kichwani mwangu.

Moyo wa mtu kuanzia sasa, utaanza kuzaa matunda, na wala hautasongwa na anasa, wala udanganyifu wa mali, wala shughuli za ulimwengu huu, usiivishe chochote.

Hii ikiwa ni kweli kabisa.

Sisi tunaomwamini Yesu, moja kwa moja tunapewa UWEZO wa kufanyika watoto wa Mungu (Yohana 1:12), na matokeo ya uwezo huo ni kuwa,  nguvu ya kusongwa na ulimwengu inakuwa ndogo, kwasababu Roho Mtakatifu aliyemwagwa ndani yetu anatusaidia, Kuukataa ulimwengu, na kuishi maisha ya utauwa. Utakuwa ulimwenguni lakini, hutasongwa na mambo yake. Kwasababu utafundishwa pia “kiasi” na Roho Mtakatifu.

Hivyo uwezo huu utakuja ndani yako, pindi tu unapomgeukia Kristo kwa kumaanisha kabisa, ambapo panaanza na kwa KUTUBU kwanza dhambi zako kwa kumaanisha kabisa kugeuka,na kumfuata Kristo tangu huo wakati, na kisha kubatizwa, na kupokea Roho wake. Lakini nje ya hapo, huwezi kwenda popote.

Je! Umempokea Yesu?

Pasipo yeye huwezi ndugu kuushinda ulimwengu kwa nguvu zako, haiwezekani hata kidogo, hata ufanyeje haiwezekani,miiba itakusonga tu, dunia itakulemea tu, Unahitaji nguvu zake, kwa Roho wake Mtakatifu. Ili kuzipata maanisha tu kumgeukia,  na kusudia kutembea naye moyoni mwako.

Utaushinda huu ulimwengu. Wala hakuna mwiba wowote utakaomea kwenye moyo wako. Kwasababu Kristo alishayakomesha yote. Je! upo tayari kuokoka leo? Basi fungua hapa kwa mwongozo wa kimaombi>>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Bwana akubariki

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

SHAMBA HUWA HALIMTAMBUI WALA KUMSUBIRIA MKULIMA.

Marhamu ni nini? Na Manukato ni nini?

Je vazi alilovikwa Bwana Yesu lilikuwa la Zambarau au Jekundu?

Mbaruti ni mmea gani? (Mathayo 7:16)

Rudi nyumbani

Print this post

Ipi tofuati ya “Kutakabari” na “kutakabali”?

Swali: Kuna tofauti gani ya “kutakabari” na “kutakabali”, sawasawa Warumi 1:30 na Mwanzo 4:4-5?


Jibu: Tuanze na 1) kutakabari..

Warumi 1:30  “wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye kutakabari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao”.

“Kutakabari” maana yake ni “kuwa na kiburi” kinachokuja kutokana na kuwa na kitu Fulani, au kujiamini sana..

Matokeo ya kutakabari ni kuanguka..

Mithali 16:18 “Kiburi hutangulia uangamivu; Na roho yenye kutakabari hutangulia maanguko.

19 Afadhali kuwa na roho ya unyenyekevu pamoja na maskini, Kuliko kugawanya nyara pamoja na wenye kiburi”.

Mfano wa mtu kwenye biblia aliyetakabari na akaanguka ni Mfalme wa Ashuru aliyeitwa Senakeribu.. Huyu alijiinua mbele za Mungu kwa kiburi kikuu na anguko lake likawa kubwa. (Soma 2Wafalme 19:28-37).

Unaweza kujifunza Zaidi juu ya kutakabari kwa kufungua hapa >>Kutakabari ni nini katika biblia?.

Mistari mingine inayozungumzia juu ya kutakabari ni pamoja na 1Samweli 2:3, Nehemia 9:10,  Isaya 13:3, na 1Wakorintho 13:4.

     2. KUTAKABALI.

“KUTAKABALI” ni tofauti na “kutakabari”…. Kutakabali ni “kukubali kitu”.. Utaona sadaka ya Habili Mungu aliitakabali (maana yake aliikubali na kuiheshimu zaidi ya ile ya Kaini).

Mwanzo 4:4 “Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. Bwana AKAMTAKABALI Habili na sadaka yake;

5 bali Kaini HAKUMTAKABALI, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana”

Na sisi tunapomtolea Mungu sawasawa na Neno lake, Sadaka zetu atazitakabali, lakini tukitoa nje na neno lake hatazitakabali kama vile sadaka ya Kaini alivyoikataa..

Yeremia 14:12 “Wafungapo, mimi sitasikia kilio chao; na watoapo sadaka za kuteketezwa na sadaka ya unga, sitazitakabali; bali nitawaangamiza kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni”

Vile vile tukimwomba Mungu sawasawa Neno lake basi Maombi yetu atayatakabali na kutujibu, lakini tusipoomba kulingana na Neno basi hata maombi yetu hayatajibiwa..

Zaburi 6:9 “Bwana ameisikia dua yangu; Bwana atayatakabali maombi yangu”.

Kujua kuomba kulingana na Neno la Mungu fungua hapa >>>>KWANINI MUNGU HAJIBU MAOMBI?

Mistari mingine inayohusu KUTAKABALI ni pamoja na Zaburi 20:3, Mhubiri 5:20, Ezekieli 20:41, Hosea 14:2 na Malaki 2:13.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

DHAMBI ILIYOMKOSESHA SHETANI:

Kiburi cha Uzima ni nini? (1Yohana 2:16)

UDHAIFU WA SADAKA!

Mtu wa kwanza kufa alikuwa nani?

MUNGU HUWAPINGA WENYE KIBURI.

Rudi nyumbani

Print this post

MAANA HUFUMBA MACHO YAO WASIONE!

Karibu tunayatafakari maandiko…

2Petro 3:3 “Mkijua kwanza neno hili ya kwamba katika siku za mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki, wafuatao tamaa zao wenyewe,

4  na kusema, Iko wapi ahadi ile ya kuja kwake? Kwa maana, tangu hapo babu zetu walipolala, vitu vyote vinakaa hali iyo hiyo, tangu mwanzo wa kuumbwa.

MAANA HUFUMBA MACHO YAO WASIONE neno hili ya kuwa zilikuwako mbingu tangu zamani, na nchi pia, imefanyizwa kutoka katika maji, na ndani ya maji, kwa neno la Mungu;

6  kwa hayo dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia

7  Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu”.

Maandiko yanatuambia watu wa siku za mwisho watafumba macho yao WASIKUMBUKE KILICHOTOKEA WAKATI WA NUHU. Kwamba Mbingu zilikuwepo na nchi pia ilikuwepo, na watu walikuwa wanaendelea na mambo yao, wakidhihaki mahubiri ya Henoko na Nuhu kuhusiana na hukumu ya Mungu, na wakati ulipotimia wa kikombe cha ghadhabu ya Mungu kujaa, hakuna hata mmoja aliyesalia Zaidi ya Nuhu na wanawe na wake zao, jumla watu 8 kati ya dunia iliyokuwa imejaa mabilioni ya watu.

Sasa mambo hayo yalishawahi kutokea katika rekodi za wanadamu.. lakini watu WANAFUMBA MACHO YAO!, Wasione hilo, wala kulitafakari.. na hatimaye wanadhihaki wakisema mbona Yesu harudi!.. mbona tumesubiri na kusubiri!..

Lakini hao hao wanaelewa kilichotokea wakati wa Nuhu kuwa dunia iligharikishwa yote..na wanajua kabisa kuwa walikuwepo watu wenye dhihaka kama za kwao, wakisema hakuna Mungu, na hakuna mtakatifu duniani.. Lakini siku ilipofika ya kuokoka Nuhu peke yake na familia yako, ndipo walipoelewa kuwa walikuwepo wacha Mungu duniani, na tena Mungu haangalii wingi.

Ndugu usidanganyike!. KRISTO ANARUDI! Na wala hatakawia..

Waebrania 10:37 “Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia”.

Baada ya Kristo kuwachukua watu wake, kitakachofuata duniani ni gharika ya Moto wa ghadhabu ya MUNGU juu ya wote wasiomcha Mungu, kama tu ilivyokuwa nyakati za Nuhu.

2Petro 3:7 “Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu.

Hivyo kamwe usifikiri wala kuwaza, wala kutia wasiwasi juu ya ujio wa BWANA YESU KRISTO.. Kama ulishawahi kudanganywa, au kulaghaiwa basi ni wanadamu ndio waliokudanganya na kukulaghai, lakini MUNGU muumba wa mbingu na nchi, kamwe hajawahi kusema uongo, na hatakaa aseme uwongo..

Kizazi chetu kitahukumiwa zaidi kuliko kile cha Nuhu kwasababu laiti watu wa kipindi cha Nuhu, wangepata mfano wa wengine waligharikishwa kabla yao, huenda wangeyatii mahubiri ya Nuhu lakini hawakuwa na mifano kabla yao, lakini sisi tunao mfano, wa watu hao.. ni kitu gani kinatutia kiburi!.

Ni nini kinachotufumba macho, na kinachowafumba watu macho????

Unadhani ni shetani????... nataka nikuambie shetani anahusika kwa sehemu ndogo sana, (Na adui anapenda kila kitu asingiziwe yeye ili watu waendelee kujifariji namna hiyo)…..kinachowafanya watu KUFUMBA MACHO YAO, wasitafakari yaliyotokea nyakati za Nuhu na Sodoma na Ghomora ni KIBURI CHA UZIMA, na watu kwa mioyo yao wenyewe KUCHAGUA GIZA na KUIKATAA NURU.

Yohana 3:19 “Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu”.

Siku hizi za Mwisho watu wameyafumba macho yao, wasione na wanajiaminisha ni shetani, kumbe si shetani bali ni wao…tupo! kizazi cha hatari sana..

Mathayo 13:15 “Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya”

Kwa hitimisho usilisahau andiko lifuatalo…

2Petro 3:8 “Lakini, wapenzi, msilisahau neno hili, kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja.

9 Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba”.

Ikiwa bado hujampokea BWANA YESU, bali mlango wa wokovu sasa upo wazi, na tunaishi ukingoni kabisa mwa wakati. Hatuna muda mwingi KRISTO anarudi!. Ni wakati wa kutubu na kuishi maisha masafi yanayoendana na toba yetu.

Ufunuo 22:12 “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.

13  Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho.

14  Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake”

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

NUHU WA SASA.

UMEFUNULIWA AKILI?

KWANINI NI NUHU, AYUBU NA DANIELI?

Kuna tofauti gani kati ya uso wa Bwana na macho ya Bwana?

NI WAKATI UPI UTAUONA USO WA KRISTO?

Rudi nyumbani

Print this post

Anaposema zijapokuwa nyekundu kama bendera, ana maana gani?

SWALI: Mungu anaposema dhambi zetu zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu. Ana maana gani, kwenye hilo neno bendera?

Isaya 1:18 Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu.  19 Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi;


JIBU: Hapa ni Mungu anaeleza mambo mawili hayuhuso dhambi walizotenda watu wake.

  • Jambo la kwanza ni ukubwa/wingi wa dhambi walizonazo. Ndio hapo anafananisha rangi nyekundu sana, ukilinganisha na kitu kilicho cheupe sana mfano wa theluji.

Tunajua theluji inang’aa sana mfano wa jua, Kuonyesha ni jinsi gani hawa watu walivyokuwa mbali sana na ukamilifu, yaani jinsi gani walivyokuwa hawakaribii hata kidogo kuwa wema mbele za Mungu, walau wangeonekana wa rangu ya kijani, basi wangekuwa na afadhali, lakini ni mbali sana, wana rangi ya damu. Ndivyo ilivyokuwa Israeli yake.

  • Jambo la pili ni usugu wa dhambi uliokuwa ndani yao.Ndio hapo anafananisha na Bendera, ukilinganisha ni sufu nyeupe.

Zamani bendera nyingi zilichovywa katika rangi nzito nyekundu, inayodumu sana, kwasababu ni kitu cha kudumu muda mrefu, hivyo haikuhitajika rangi inayofubaa haraka. Sio tu bendera, lakini mpaka mavazi ya kifalme, au nguo za thamani za sufu.

Hivyo unaposoma habari za bendera hapo, si bendera ya kila rangi, mfano wa bendera tulizonazo sikuhizi zina rangi mbalimbali, zamani nyingi zilichovya kwa rangi  nyekundu. Hivyo Mungu anawaambia ijapokuwa ni nyekundu kama bendera, basi zitageuzwa na kuwa nyeupe kama Sufu, (akiwa na maana ambayo haijachovywa), Yaani Mungu anaweza kuiondoa hiyo rangi sugu, kwenye hicho kitambaa kana kwamba hakijachovywa kabisa.

Kufunua nini,

Yesu Kristo mwokozi wetu ndiye aliyetimiza huo unabii. Kuonyesha kuwa dhambi zote tulizotenda haijalisha ni nyingi kiasi gani, haijalishi ni mbaya namna gani yeye kwa damu yake anaweza kuzifuta kabisa kabisa. Dhambi tulizotenda haijalishi hazisameheki namna gani, hazineneki, ni sugu namna gani, yeye anao uwezo wa kuziondoa, kwa neema yake.

Swali ni je! Umesamehewa dhambi zako? Kama ni la! Unangoja nini kuipokea neema hii, ya WOKOVU mkuu namna hii? Pokea sasa msamaha wa dhambi kwa kutubu dhambi zako, na kumaanisha kuishi maisha mapya ya wokovu. Kisha moja kwa moja atakupokea na kukupa ondoleo la dhambi zako. Na baada ya hapo unahesabiwa kuwa huna dhambi yoyote, umestahili uzima wa milele, bure.

Ikiwa upo tayari kufanya hivyo leo basi, fungua hapa kwa ajili ya mwongozo wa maombi mafupi, na kwa kupitia sala hiyo kwa imani utakuwa umeshampokea Yesu Kristo, na amekusamehe dhambi zako zote.>>>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Bwana akubariki.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

Wale Nyoka wa Moto jangwani, walikuwa ni wa namna gani?

ALAMA ZA BENDERA YA ISRAELI ZINAWAKILISHA NINI?

MAANA YA RANGI KIBIBLIA.

Maana Ya Maneno Katika Biblia.

Rudi nyumbani

Print this post

USIWE MKRISTO WA KUKAA TU GHALANI,

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Karibu tujifunze maneno ya uzima ya mwokozi.

Watu waliomwamini Yesu Kristo, yaani waliopokea ondoleo la dhambi zao. Hutambulika kama NGANO, lakini watu ambao bado wapo kwenye dhambi, hujulikana kama MAKAPI.

Sasa kazi ya kwanza ambayo Yesu anaifanya kwa mwamini, ni kumtenganisha yeye na makapi, kisha humweka katika ghala lake.

Mathayo 3:12  Ambaye pepeto lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake; na kuikusanya ngano yake ghalani, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.

Ghalani ni uweponi mwa Mungu, yaani kutengwa na udunia.

Soma pia..Mathayo 13:29-30.

Sasa kama wewe unafahamu ukulima, unajua kabisa si mbegu zote zinawekwa ghalani kwa matumizi ya chakula, zipo nyingine, zinachukuliwa na kurudishwa shambani ili kwenda kuzalisha nyingine. Na baadaye huongeza ghala la mkulima.

Tofauti kabisa na ile inayobakia pale ghalani, itaendelea kubakia vilevile hata miaka 10, lakini ile inayokwenda shambani, ndani ya hicho kipindi cha miaka 10, yaweza kuongeza magunia mengi sana ya ngano nyingine.

Ndio maana Bwana Yesu alisema maneno haya;

Yohana 12:24  Amin, amin, nawaambia, CHEMBE YA NGANO ISIPOANGUKA KATIKA NCHI, IKAFA, HUKAA HALI IYO HIYO PEKE YAKE; BALI IKIFA, HUTOA MAZAO MENGI. 25  Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele. 26  Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu.

Umeona hapo? Kumbe isipoanguka na kuoza basi itaendelea kubakia katika hali ile ile. Lakini ikikubali kuanguka na kuoza, ardhini, basi itachipuka kama shina, na mwisho wa siku itazaa sana.

Na hapa ndipo waamini wengi, hawataki kuingia gharama. Wanatamani wamzalie Mungu matunda, lakini hawawezi, kwasababu hawajakubali “kufa na kuoza” kwa habari ya huu ulimwengu.

Hawajakubali kuziangamiza  nafsi zao kwa ajili ya Kristo. Sasa hiyo ndio inayopelekea wabakie tu kama wakristo wa ghalani,wasioweza kuzalisha chochote.

Yesu alitoa sifa za mbegu yenye kuzaa katika ule mfano wa mpanzi,  akasema nyingine ziliangukia njiani, nyingine kwenye miamba, nyingine kwenye miiba, na nyingine kwenye udongo mzuri. Akasema vilizoangukia kwenye udongo mzuri ziliweza kuzaa kwa tendo moja tu la “kuvumilia”

Kuvumilia nini?

Kuvumilia dhiki, na udhia kwasababu ya Kristo, kuvumilia vishawishi vya anasa, udanganyifu wa mali, na shughuli za ulimwengu huu zilizopitiliza, lakini pia kwa unyofu wa moyo walikuwa wanalitendea kazi Neno ili walilolisikia lisiwe bure adui akaliiba ndani yao. (Luka 8:11-15). Hao ndio wakristo wasio wa ghalani, ni wakristo waliokubali kutoka nje, kumletea Bwana matunda.

Je! Na sisi tunaweza kupiga hatua nyingine? Umeokoka ndio, lakini ni lazima wokovu wako uwe na matokeo kwa wengine, uwavute na wengine kwa Kristo, kama wewe ulivyovutwa. Hivyo kubali kumaanisha kumfuata Yesu na kukaa mbali na udunia kwa kadiri uwezavyo.

Jitoe pia kwa Bwana, mali zako, zitumike kuhubiri injili, tenga fungu lako kwa Bwana, penda kusapoti kazi za Mungu, usiwe msomaji tu na kusema Amen!. Onyesha kuwa na wewe ni mtendaji kazi ili thawabu yenu iwe ni  moja, na yule mtendaji kazi mwingine.

Bwana atusaidie, tutoke ghalani.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

NI YESU YUPI UMEMPOKEA?, NI ROHO IPI UMEIPOKEA? NA INJILI IPI UMEIPOKEA?

ANGALIA JINSI USIKIAVYO:

SEMA KWA LUGHA NYINGINE.

Je Mungu ana njia ngapi za kuzungumza?

Rudi nyumbani

Print this post

TENDA JAMBO LA ZIADA.

(Masomo maalumu yahusuyo kazi na uchumi).


Tunahitaji kujua kanuni chache ili tuweze kufungua milango yetu ya kiuchumi. Leo tutaangalia kanuni nyingine ambayo mkristo akiitumia basi anaweza kupata kibali mahali pale afanyiapo kazi.

Si wakati wote maombi tu pekee yanatosha kukuletea kibali katika maisha ya kazi/kuwajibika. Ni lazima pia uongeze na maarifa ili uweze kufungua milango hiyo ya Baraka.

Sasa ukitaka upate kibali kazini au kwa aliye juu yako, basi FANYA JAMBO LA ZIADA HAPO UFANYIAPO KAZI.

Kwa mfano Mshahara wako unaoupokea kwa siku, wiki au mwezi, ni kiasi Fulani…. baada ya kutoa sehemu ya Mungu (yaani sadaka pamoja na Zaka) kiasi kilichosalia  usikitumia chote katika mahitaji yako..bali toa sehemu kidogo ya hicho na ufanye jambo jipya na la kipekee hapo ufanyiapo kazi!.

Kwa mfano kama umeajiriwa na unafanya kazi ya usafi hapo kazini, badala ya kusubiri mwajiri wako akupe fedha ya kwenda kununua kifaa cha usafi, hebu wewe TENDA JAMBO LA ZIADA… toa kiasi kidogo cha pesa yako na nenda kununua kifaa hicho.

Kwa kufanya hivyo utaonekana mjinga mbele ya wafanyakazi wenzako na watu wengine walio karibu nawe pengine hata kwa mke wako/mume wako… lakini si kwa Mwajiri wako!, yeye atakusifu kama si kwa kinywa chake basi katika moyo wake, na hiyo itakuongezea kibali kikubwa sana katika maisha yako ya kazi… Utakuwa umepata nafasi katika moyo wake, na kiwango cha kukuamini na kukupenda kitaongezeka..

Au labda umeajiriwa katika mgahawa, hebu TENDA JAMBO LA ZIADA…badala ya kusubiri boss wako akupe fedha za kwenda kununua sahani za biashara, au akupe fedha za kwenda kununua sufuria, au sabuni.. hebu mara moja moja wewe toa kiasi chako kidogo cha mshahara kanunue zile sahani, au sufuria au kitu kingine chochote cha muhimu kinachohitajika pale..

Wala usianze kuangalia mahitaji uliyonayo (hayo yataendelea kuwepo tu)… wewe fanya hivyo kwasababu  unajua ni mbegu gani unayoipanda wakati huo!… wengine watakuona huna akili, au umechanganyikiwa, wewe usiangalie hayo bali angalia yanayokuja..

Pengine umeajiriwa kama mhasibu katika ofisi fulani, hebu TENDA JAMBO LA ZIADA, Toa kidogo katika mshahara wako kanunue kiti kingine cha ofisi au saa ya ofisi nzuri, au pamba kwa chochote kile pale ufanyiapo kazi.. weka mbali matatizo yako kwa muda, na mahitaji yako na ufanye hayo.. nakuhakikishia matokeo yake utakuja kuyaona baadaye.. Utapata kibali ambacho utakishangaa.

Wakati unafanya hayo, wengine watakuona ni mjinga, kwasababu hayo unayoyafanya yangepaswa kutekelezwa na boss wako au kampuni, na sio wewe…ndio maana watakuona umerukwa na akili, lakini Mwajiri wako atakuona ni shujaa..

Katika biblia Bwana YESU alitoa mfano wa wakili dhalimu, ambaye alitoa mali zake za wizi na kuwalipa wadeni wa Boss wake, na kupitia mali ile ya udhalimu alijipatanisha na boss wake pamoja na wadeni wa boss wake…na hivyo akasifiwa hata na yule yule aliyemwibia (yaani bosi wake). Soma Luka 16:1-12

Sasa huyu alijipatia kibali kwa mali ya udhalimu (maana yake mali ya wizi).. vipi wewe ambaye una mali ambayo sio ya wizi (halali), halafu ukaitumia katika kutafuta kibali?.. unadhani hutakipata??.

Lakini ukisema mimi nitaomba tu!, na kutumia kiasi chako kwa mahitaji yako tu…na huku hutaki kutenda jambo la ziada,  hapo unapofanyia kazi, utakuwa unajiwikwamishia Baraka zako tu!… kwasababu hayo uyafanyayo ni kila mtu anayafanya, na yameshazoeleka…lakini ukitenda TENDA TENDO LINGINE ZA ZIADA ambayo halifanywi na wengine wote, hapo utajipatia kibali.

Hata katika kumtumikia MUNGU, Bwana YESU alitufundisha kuwa ni lazima tujifunze kutenda tendo lingine la ziada ili tupokee kibali.

Mathayo 5:46 “Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?

47  Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo?”

Hivyo pata maarifa na TENDA TENDO LA ZIADA, na utaona jinsi utakavyopokea kibali katika yote uyafanyayo!.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

TENDA HAKI KWA FAIDA YAKO MWENYEWE.

Mfano wa wanawali kumi(Mathayo 25), unaelewekaje?

Mistari ya biblia kuhusu kibali.

NJIA NYINGINE YA KUPATA REHEMA NA KIBALI KUTOKA KWA MUNGU.

MAPAMBO YA WANAWAKE WALIOUKIRI UCHAJI WA MUNGU.

Rudi nyumbani

Print this post

Chrislam ni nini?

Ni muungamaniko wa maneno makuu mawili. (Yaani Christian na Islamic). Likachukuliwa Neno la kwanza Chris katika Christian, likaunganishwa na Neno la katikati “slam” kutoka katika Islamic. Kuunda Christlam

Hii ni imani iliyozuka, katika taifa la Nigeria miaka ya 1970.  Kufuatana ni migongano ya kiimani baina ya makundi haya mawili ya dini, ikizingatiwa kuwa Taifa La Nigeria ndio lenye watu wengi barani Africa, na takribani Nusu kwa Nusu, dini hizi mbili ndio zimechukua jamii kubwa ya watu.

Hivyo waasisi ya umoja huu walikuwa na madhumuni ya kuondoa tofauti za kidini, husani zilizo katika mataifa ya magharibu na ya mashariki ya kati, Lakini pia kwasababu hizi ndio dini kubwa duniani, basi pia zikiungana zinaweza kusaidia kuushinda upagani kwa sehemu kubwa.Na ukweli ni kwamba imani hii imepata umaarufu mkubwa duniani, hususani kwa kipindi cha sasa.

Waanzilishi walisukumwa kuunda umoja huu, wakiamini kuwa, sehemu kubwa ya dini ya kikristo inatajwa katika Quran, wakimrejea Yesu mwenyewe pamoja na manabii wa kale, kama Ibrahimu na wengineo. Lakini pia uislamu unamwingiliano mkubwa wa kitamaduni ambao hata katika ukristo upo. Hivyo kwa mujibu wa hoja zao hakuna sababu ya kuwa na utofauti wowote katika mashindano ya kidini.

Lakini je! Umoja huu, mbele za Bwana unakubalika?

Imani ya Kikristo pamoja dini ya kiislamu haviwezi kuchangamana, ni sawa na chuma na udongo. Kwasababu kiini cha imani ya ukristo ni KRISTO mwenyewe, na kwamba mtu hawezi kwenda mbinguni pasipo kumwamini YESU kama mwokozi PEKEE anayewaokoa wanadamu. Jambo ambalo linakinzana na dini ya Kiislam, katika imani ya kufika mbinguni, ambapo kwao Kristo ni kama mmojawapo wa manabii tu wengine. Na hivyo mbingu si kupitia Kristo, bali kupitia matendo mazuri kama vile kukaa mbali na uovu n.k.

Uislamu haumtambua Kristo kama Mungu, huamini kuwa yoyote anayemfanya Yesu Mungu, ni makufuru, kwasababu Mungu hajazaa, wala hana mshirika. Hivyo aaminiye uungu wa Yesu, pepo haimuhusu.

Kwa vigezo hivyo, uislamu na ukristo ni imani mbili tofauti kabisa, ijapokuwa zitaonekana kushea baadhi ya desturi, lakini bado haziwezi kuletwa pamoja kuwa kitu kimoja.

Je! Hatupaswi kuwa waamini wa Chrislam

Ndio wewe kama Mkristo,, imani yako haipaswi kuchanganywa na nyingine yoyote, ukifanya hivyo ni Kosa kiimani. Sisi tunaamini, wokovu ni kwa kupitia Yesu Kristo anaotupa BURE kwa neema katika kumwamini Yeye, kwa kifo chake pale msalabani.

Tunamtegemea Kristo kutuokoa, kutupa nguvu ya kuishi maisha makamilifu, kutuongoza, kwa asili mia. Hivyo hatuna msingi au tegemeo lingine nje yake yeye. Na hata hivyo kibiblia, yoyote asiyekubaliana na Kristo Yesu, kama ndiye mwokozi pekee. Huyo ni mpinga-Kristo.

Hivyo kw hitimisho ni kuwa wewe kama mwana wa Mungu, usijihusishe ni imani yoyote nje ya Kristo Yesu mwokozi wako.

Matendo 4:12  Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

Dini ni nini, na Imani ya kweli ni ipi?

Praitorio ni nini? Na Kwanini ilikuwa ni najisi kwa wayahudi kuingia humo? (Yohana 18:28)

Uadilifu ni nini kibiblia?

Rudi nyumbani

Print this post

Merikebu ya Iskanderia kwanini itajwe jina lake ‘Ndugu Pacha’?

SWALI: Je kulikuwa na umuhimu wowote wa ile merikebu ya Iskanderia  walioipanda Paulo na wafungwa wengine kutajwa jina lake ‘ndugu Pacha’,?

Matendo 28:11  Baada ya miezi mitatu tukasafiri katika merikebu ya Iskanderia iliyokuwa imekaa pale kisiwani wakati wa baridi; na alama yake ni Ndugu Pacha. 12  Tukafika Sirakusa, tukakaa siku tatu. 13  Kutoka huko tukazunguka tukafikia Regio; baada ya siku moja upepo wa kusi ukavuma, na siku ya pili tukawasili Puteoli. 14  Huko tukakuta ndugu, wakatusihi tukae nao siku saba; na hivi tukafika Rumi.


JIBU: Safari ya mtume Paulo kama mfungwa, kutoka Kaisaria kwenda Rumi kuhukumiwa, haikuwa rahisi, iligubikwa na misuko suko mikubwa ambayo ilihatarisha maisha yao ukisoma Matendo 27, utaona mtume Paulo alionywa na Roho Mtakatifu kuhusu hatari hiyo lakini alipomwambia akida na manahodha, walipuuzia agizo lake, kwasababu watu wale hawakuamini habari za “miungu kabisa”. Maandiko yanasema walipoona upepo wa kusi umevuma kidogo tu, unaoruhusu kusafiri, wakadhani itakuwa hivyo mbeleni.

Lakini tunaona walipofika katikati, ghafla ile bahari iliwachafukia sana, upepo wa nguvu ukavuma merikebu yao ikawa karibu na kuzama, baadaye ilivunjika kabisa, na wakaokoka kwa shida kwasababu Mungu alimuhakikishia Mtume Paulo kuwa hakuna hata mmoja wao atakayeangamia.

Walipookoka na kufika kisiwa kile kilichoitwa Melita, walikaa miezi mitatu pale, kuruhusu hali ya hewa kutulia, kabla ya kuondoka. Lakini tunaona walipotaka kuondoka, safari hii wale mabaharia pamoja na maakida, hawakuichukulia safari yao kirahisi rahisi, yaani hivi hivi tu bila uongozo wowote. Ndipo walipojifunza kuchagua merikebu yenye “ulinzi wa kiroho”. Wakaipata hiyo ya Iskanderia iliyokuwa na nembo ya “Ndugu Pacha” kwa mbele.

Ndugu Pacha ni miungu ya kipagani ya kiyunani, ukisoma tafsiri nyingine za biblia imewataja moja kwa moja miungu hiyo kama Castor na Pollux. Ni miungu ambayo waliamini inahusika na ulinzi wa  safari za majini. Hivyo kwa imani yao ya kipagani, wakachukua nembo yao kuonyesha tunaiabudu na kuiheshimu hii miungu, na kutaka iwaongoze  salama katika safari yao, hawategemei tena elimu zao na nadharia zao.

Sasa tukirudi kwenye swali, linalouliza, kulikuwa ni umuhimu gani, hiyo merikebu ya Iskanderia kutajwa hadi nembo yake ya ndugu Pacha. Sababu ndio hiyo, Sio kwamba biblia inatufundisha, na sisi tukaweke miungu ya kipagani, kwenye vyombo vyetu vya usafiri kutuhakikishia ulinzi, hapana!

Bali inatufundisha Safari ya maisha hapa duniani. Kila mwanadamu anasafiri, lakini Je! Katika safari yako ni kitu gani kinakuongoza na kukulinda ili kukufikia ng’ambo yako salama?

Hakuna mwanadamu ambaye anaweza kujiongoza mwenyewe. Na ndio maana utaona hawa kwasababu hawakumjua Mungu wa kweli iliwabidi wakatafuta vinyago visivyoweza kuwasaidia kitu viwaongoze, na kama sio mtume Paulo kuwepo ndani ya Merikebu ile, safari yao ndio ingekuwa mbaya mara mbili zaidi. Hawakujua tu waliongozwa na Kristo Yesu pasipo wao kujua kwa neema tu!. Kwasababu watumishi wa Mungu walikuwa ndani.

Na sisi, hapa tulipo, fahamu kuwa maisha yako, bila KRISTO ni mauti mbele. Shetani hakuwazii mema, wala akili zako mwenyewe hazikusaidii ndugu, hiyo elimu ni kazi bure, huo uzoefu na ujuzi ulionao ni bure rafiki. Unamuhitaji Kristo, yeye ndio awe nembo  ya maisha yako. Mwamini leo akupe msamaha wa dhambi, mwamini leo akuokoe, safari yako iwe salama hapa duniani. Ukifa leo katika hali hiyo, fahamu ni jehanamu moja kwa moja. Umesikia injili ikihubiriwa mara ngapi, kwamba Yesu ni mwokozi lakini unapuuzia? Walio kuzimu wanatamani hata dakika moja, watubu hawawezi kwasababu kule hakuna maisha ya kuishi. Lakini wewe unaishi.

Usikiapo maneno haya, ugeuze moyo wako, umruhusu Kristo leo akuokoe, ikiwa upo tayari kumgeukia Bwana Yesu , na unatamani upate mwongozo wa kimaombi kwa ajili ya wokovu wako. Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo mwisho wa makala hii, bure.

Bwana akubariki.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

NA UPEPO WA KUSI ULIPOANZA KUVUMA KIDOGO,

MAJARIBU MATANO (5) YA MKRISTO.

Kalafati ni nini? (Ezekieli 27:9)

KWANINI DANI ALIKAA KATIKA MERIKEBU.

Rudi nyumbani

Print this post

Nini maana ya “Mvinyo hudhihaki na kileo huleta ugomvi? (Mithali 20:1)

Jibu: Turejee.

Mithali 20:1 “Mvinyo hudhihaki, kileo huleta ugomvi; Na akosaye kwa vitu hivyo hana hekima”.

Hili ni andiko linaloelezea mambo makuu mawili yanayowakosesha watu waliopungukiwa na Hekima.. na Mambo hayo ni “Mvinyo” pamoja na “Kileo”. Na vitu vyote hivi viwili vina madhara kwa mtu anayevitumia..

Sasa ni ipi tofauti kati ya Mvinyo na Kileo? Na madhara yake ni yapi kwa mtumiaji?.

“Mvinyo” (kwa lugha ya kiingereza ni “wine”) ni kilevi kinachotengenezwa kwa “Matunda yaliyosagwa” kama Zabibu, mananasi, maembe n.k Mfano wa mvinyo unaotengenezwa kwa zabibu ni “Divai”.

Wakati “Kileo” (Kwa lugha ya kiingereza Beer/Bia) ni kilevi kinachotengenezwa kwa nafaka kama Ngano, mahindi, ulezi, mtama, mchele n.k

Kikawaida Mvinyo ndio wenye kilevi kingi kuliko Kileo. Na matokeo ya mtu anayetumia mvinyo au kileo yanakaribiana. Hebu tuangalia madhara ya kimoja baada ya kingine kibiblia.

   1. MVINYO

Biblia anasema “Mvinyo hudhihaki”.. maana yake ni kuwa mtu anayetumia mvivyo anakuwa ni mtu wa kudhihaki na kudhihakiwa!.. kwasababu ya wingi wa maneno yao yasiyo na maana yatokayo midomoni mwao.

Ndio maana utaona kile kipindi cha Pentekoste, walipowasikia wanafunzi wa Bwana YESU wakinena kwa lugha, walidhani wamelewa kwa mvinyo mpya na hivyo wakaanza kuwadhihaki..

Matendo 2:12 “Wakashangaa wote wakaingiwa na shaka, wakiambiana, Maana yake nini mambo haya? 13  WENGINE WALIDHIHAKI, WAKISEMA, WAMELEWA KWA MVINYO MPYA.

14  Lakini Petro akasimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia, Enyi watu wa Uyahudi, na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, lijueni jambo hili, mkasikilize maneno yangu.

15  Sivyo mnavyodhani; watu hawa hawakulewa, kwa maana ni saa tatu ya mchana;

16  lakini jambo hili ni lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli”.

Umeona hapo?.. walianza kuwadhihaki wakidhani wamelewa kwa MVINYO MPYA, ikimaanisha kuwa Mvinyo huleta dhihaka kwa anayekunywa. Na mtu anayelewa kwa mvinyo atapokea dhihaka nyingi katika maisha yake..

    2. KILEO

Biblia inaendelea kusema kileo huleta “UGOMVI”. Asilimia kubwa ya watu wanaogombana mpaka kufikia hatua ya kudhuriana ni walevi wa pombe, mafarakano mengi yanatoka kwa watu waliolewa..

Hivyo kwa hitimisho ni kwamba, Ulevi wa aina yoyote ile uwe wa “Mvinyo” au wa “Kileo” matokeo yake ni mabaya katika maisha ya ulimwengu huu na ule ujao…. Kulingana na biblia walevi wote hawataurithi uzima wa milele (soma 1Wakorintho 6:9-10 na Wagalatia 5:19-20)..

Warumi 13:13 “Kama ilivyohusika na mchana na tuenende kwa adabu; si kwa ULAFI NA ULEVI, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu.

14  Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo, wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake”.

Maran atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

UPEPO WA KUSI HULETA MVUA;

“Si watu wa kutumia mvinyo sana”, je tunaruhusiwa kutumia mvingo kidogo?(1Timotheo 3:8).

Biblia ina maana gani inaposema akonyezaye kwa jicho huleta masikitiko?

Je! mwanadamu wa kwanza kuumbwa ni yupi?

JE! ULEVI NI DHAMBI?.

Rudi nyumbani

Print this post

 UNAUELEWA, HISOPO UMEAO UKUTANI?

1Wafalme 4:32 Naye akanena mifano elfu tatu, na nyimbo zake zilikuwa elfu moja na tano.  33 Akanena habari za miti tangu mwerezi ulioko Lebanoni hata HISOPO UMEAO UKUTANI; pia akanena habari za wanyama, na za ndege, na vitambaavyo, na samaki.

Salaam! karibu tujifunze na kutafakari bahari za mwokozi wetu Yesu Kristo na uzuri wake maishani mwetu.

Habari yetu itaanzia kwa mfalme Sulemani ambaye Mungu alimjalia hekima nyingi zaidi ya wanadamu wote waliokuwa duniani kwa wakati ule. Na moja ya mambo ambayo, aliyatafakari sana, hayawakuwa tu yanayowahusu wanyama na viumbe hai, lakini ni pamoja na mimea mbalimbali.

Hivyo kama tunavyosoma katika vifungu hivyo, aliweza kutambua hekima iliyokuwa imejificha nyuma ya miti mikubwa na yenye umaarifu kama mierezi, lakini, kilichomtafakarisha pia sio katika mimea mikubwa, lakini pia midogo  mfano wa Hisopo, na jinsi inavyomea. Na hapo tunaona anaeleza sifa yake, kwamba ni mmea unaomea ukutani.

Ikiwa na maana, mahali palipo na ardhi ngumu, au mwamba au jiwe, wenyewe unamea, na kukua na kuzaa bila shida yoyote. Tofauti na mimea mingine mingi yenye nguvu, itahitaji  udogo mlaini mwingi, tena tifutifu, lakini huu wa hisopo ni wa kipekee unahitaji mahali pagumu.

Kufunua nini?

Mmea huu unamfunua Bwana wetu Yesu Kristo,yeye  Hakuhitaji mahali palipoandaliwa pa kitajiri, ili kulitimiza kusudi la kifalme duniani,  hakuhitaji familia ya kidini maarufu, au kabila la kikuhani,  ili aishi maisha makamilifu, hakuhitaji kuishi mji mtakatifu Yerusalemu ili ampendeze Mungu. Bali alitokea mahali ambapo ni vijijini (Nazareti), familia maskini, tena nyakati za kipagani, ambazo imani ilikuwa imekongoroka sana, pia, kabila lisilojiuhusisha na mambo yoyote ya kikuhani kabisa. Hivyo Yesu aliishi katika jamii ya wapagani.

Wakati sisi katikati ya dhiki nyingi (yaani penye mwamba mgumu) tunanyauka. Yeye ndio alikuwa anasitawi. Aliweza kustahimili mapingamizi ya kila namna zaidi ya mwanadamu yoyote aliyewahi kutokea hapa duniani. Alichukiwa na ulimwengu, alisalitiwa, alikanwa, aliachwa peke yake, aliaibishwa, alipigwa mpaka kuuawa. Lakini hakuwahi kuanguka au kutenda dhambi yoyote. Haleluya! Anastahili hakika mwokozi wetu Yesu Kristo.

Ni hisopo umeao ukutani. Mahali ambapo mimea mingine imeshindwa, yeye ameweza.

Na ndio maana Neno linasema;

Waebrania 12:2  tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.

3  MAANA MTAFAKARINI SANA YEYE ALIYEYASTAHIMILI MAPINGAMIZI MAKUU NAMNA HII YA WATENDAO DHAMBI JUU YA NAFSI ZAO, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu.

4  Hamjafanya vita hata kumwagika damu, mkishindana na dhambi;

Umeona ni kwa namna gani Yesu alivyokuwa mwamba imara wa kutegemea sana?

Na ndio maana maandiko sasa yanasema, kwa kuwa alijaribiwa kama sisi, basi anaweza kuchukuliana na sisi pia katika mambo yetu ya udhaifu.

Waebrania 4:14  Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu.

15  Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi.

16  Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

Hivyo ndugu, ni nini unachongoja, usiokoke leo?. Wewe peke yako hutaweza, kuushinda huu ulimwengu, unaihitaji neema ya Yesu Kristo ikusaidie. Mpokee leo, upate ondoleo la dhambi zako,  Akupe na Roho wake mtakatifu ili kukusaidia sasa kuishi maisha ya ushindi kama yeye alivyoishi.

Ukipita katika miamba lakini unaendelea kumea.  Hivyo chukua uamuzi huo leo. Ikiwa upo tayari kuokoka basi fungua hapa kwa mwongozo wa sala ya Toba. >>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Bwana akubariki.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

ALIFANYIKA SADAKA KWA AJILI YETU!

VITA BADO VINAENDELEA.

TUKAZE MWENDO KWA TULIYOANDALIWA.

TUNAHESABIWA HAKI BURE KWA NJIA YA IMANI.

Rudi nyumbani

Print this post