MAANA HUFUMBA MACHO YAO WASIONE!

MAANA HUFUMBA MACHO YAO WASIONE!

Karibu tunayatafakari maandiko…

2Petro 3:3 “Mkijua kwanza neno hili ya kwamba katika siku za mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki, wafuatao tamaa zao wenyewe,

4  na kusema, Iko wapi ahadi ile ya kuja kwake? Kwa maana, tangu hapo babu zetu walipolala, vitu vyote vinakaa hali iyo hiyo, tangu mwanzo wa kuumbwa.

MAANA HUFUMBA MACHO YAO WASIONE neno hili ya kuwa zilikuwako mbingu tangu zamani, na nchi pia, imefanyizwa kutoka katika maji, na ndani ya maji, kwa neno la Mungu;

6  kwa hayo dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia

7  Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu”.

Maandiko yanatuambia watu wa siku za mwisho watafumba macho yao WASIKUMBUKE KILICHOTOKEA WAKATI WA NUHU. Kwamba Mbingu zilikuwepo na nchi pia ilikuwepo, na watu walikuwa wanaendelea na mambo yao, wakidhihaki mahubiri ya Henoko na Nuhu kuhusiana na hukumu ya Mungu, na wakati ulipotimia wa kikombe cha ghadhabu ya Mungu kujaa, hakuna hata mmoja aliyesalia Zaidi ya Nuhu na wanawe na wake zao, jumla watu 8 kati ya dunia iliyokuwa imejaa mabilioni ya watu.

Sasa mambo hayo yalishawahi kutokea katika rekodi za wanadamu.. lakini watu WANAFUMBA MACHO YAO!, Wasione hilo, wala kulitafakari.. na hatimaye wanadhihaki wakisema mbona Yesu harudi!.. mbona tumesubiri na kusubiri!..

Lakini hao hao wanaelewa kilichotokea wakati wa Nuhu kuwa dunia iligharikishwa yote..na wanajua kabisa kuwa walikuwepo watu wenye dhihaka kama za kwao, wakisema hakuna Mungu, na hakuna mtakatifu duniani.. Lakini siku ilipofika ya kuokoka Nuhu peke yake na familia yako, ndipo walipoelewa kuwa walikuwepo wacha Mungu duniani, na tena Mungu haangalii wingi.

Ndugu usidanganyike!. KRISTO ANARUDI! Na wala hatakawia..

Waebrania 10:37 “Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia”.

Baada ya Kristo kuwachukua watu wake, kitakachofuata duniani ni gharika ya Moto wa ghadhabu ya MUNGU juu ya wote wasiomcha Mungu, kama tu ilivyokuwa nyakati za Nuhu.

2Petro 3:7 “Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu.

Hivyo kamwe usifikiri wala kuwaza, wala kutia wasiwasi juu ya ujio wa BWANA YESU KRISTO.. Kama ulishawahi kudanganywa, au kulaghaiwa basi ni wanadamu ndio waliokudanganya na kukulaghai, lakini MUNGU muumba wa mbingu na nchi, kamwe hajawahi kusema uongo, na hatakaa aseme uwongo..

Kizazi chetu kitahukumiwa zaidi kuliko kile cha Nuhu kwasababu laiti watu wa kipindi cha Nuhu, wangepata mfano wa wengine waligharikishwa kabla yao, huenda wangeyatii mahubiri ya Nuhu lakini hawakuwa na mifano kabla yao, lakini sisi tunao mfano, wa watu hao.. ni kitu gani kinatutia kiburi!.

Ni nini kinachotufumba macho, na kinachowafumba watu macho????

Unadhani ni shetani????... nataka nikuambie shetani anahusika kwa sehemu ndogo sana, (Na adui anapenda kila kitu asingiziwe yeye ili watu waendelee kujifariji namna hiyo)…..kinachowafanya watu KUFUMBA MACHO YAO, wasitafakari yaliyotokea nyakati za Nuhu na Sodoma na Ghomora ni KIBURI CHA UZIMA, na watu kwa mioyo yao wenyewe KUCHAGUA GIZA na KUIKATAA NURU.

Yohana 3:19 “Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu”.

Siku hizi za Mwisho watu wameyafumba macho yao, wasione na wanajiaminisha ni shetani, kumbe si shetani bali ni wao…tupo! kizazi cha hatari sana..

Mathayo 13:15 “Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya”

Kwa hitimisho usilisahau andiko lifuatalo…

2Petro 3:8 “Lakini, wapenzi, msilisahau neno hili, kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja.

9 Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba”.

Ikiwa bado hujampokea BWANA YESU, bali mlango wa wokovu sasa upo wazi, na tunaishi ukingoni kabisa mwa wakati. Hatuna muda mwingi KRISTO anarudi!. Ni wakati wa kutubu na kuishi maisha masafi yanayoendana na toba yetu.

Ufunuo 22:12 “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.

13  Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho.

14  Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake”

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

NUHU WA SASA.

UMEFUNULIWA AKILI?

KWANINI NI NUHU, AYUBU NA DANIELI?

Kuna tofauti gani kati ya uso wa Bwana na macho ya Bwana?

NI WAKATI UPI UTAUONA USO WA KRISTO?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments