NI WAKATI UPI UTAUONA USO WA KRISTO?

NI WAKATI UPI UTAUONA USO WA KRISTO?

Habari ya huyu kipofu unaweza ukawa umeshaisoma mara nyingi sana, lakini lipo jambo limejificha ambalo kila mtu anapaswa alijue, tafadhali soma tena kwa utaratibu na kwa utulivu kisha tutatazama ni wapi tunapaswa tuzingatie sana sana pale tunapodhani kuwa Mungu kutufanikisha au kutuwezesha katika mambo yetu ni uthibitisho kuwa tumemwona yeye.

Embu tusome tena pamoja kwa utulivu:

Yohana 9:1-41 
“1 Hata alipokuwa akipita alimwona mtu, kipofu tangu kuzaliwa. 

2 Wanafunzi wake wakamwuliza wakisema, Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu? 

3 Yesu akajibu, Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake. 

4 Imetupasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenipeleka maadamu ni mchana, usiku waja asipoweza mtu kufanya kazi. 

5 Muda nilipo ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu. 

6 Alipokwisha kusema hayo, alitema mate chini, akafanya tope kwa yale mate. Akampaka kipofu tope za macho, 

7 akamwambia, Nenda kanawe katika birika ya Siloamu, (maana yake, Aliyetumwa). Basi akaenda na kunawa; akarudi anaona. 

8 Basi jirani zake, na wale waliomwona zamani kuwa ni mwombaji, wakasema, Je! Huyu siye yule aliyekuwa akiketi na kuomba? 

9 Wengine wakasema, Ndiye. Wengine wakasema, La, lakini amefanana naye. Yeye mwenyewe alisema, Mimi ndiye. 

10 Basi wakamwambia, Macho yako yalifumbuliwaje? 

11 Yeye akajibu, Mtu yule aitwaye Yesu alifanya tope, akanipaka macho akaniambia, Nenda Siloamu ukanawe; basi nikaenda na kunawa, nikapata kuona. 

12 Wakamwambia, Yuko wapi huyo? Akasema, Mimi sijui. 

13 Basi wakampeleka kwa Mafarisayo yule aliyekuwa kipofu zamani. 

14 Nayo ilikuwa sabato, hapo Yesu alipofanya zile tope na kumfumbua macho. 

15 Basi Mafarisayo nao wakamwuliza tena jinsi gani alivyopata kuona. Akawaambia, Alinitia tope juu ya macho, nami nikanawa, na sasa naona. 

16 Basi baadhi ya Mafarisayo wakasema, Mtu huyo hakutoka kwa Mungu, kwa sababu haishiki sabato. Wengine wakasema, Awezaje mtu mwenye dhambi kufanya ishara kama hizo? Kukawa matengano kati yao. 

17 Basi wakamwambia yule kipofu mara ya pili, Wewe wasemaje katika habari zake kwa vile alivyokufumbua macho? Akasema, Ni nabii. 

18 Basi Wayahudi hawakusadiki habari zake, ya kuwa alikuwa kipofu, kisha akapata kuona; hata walipowaita wazazi wake yule aliyepata kuona. 

19 Wakawauliza wakisema, Huyu ndiye mwana wenu, ambaye mnasema kwamba alizaliwa kipofu? Amepataje, basi, kuona sasa? 

20 Wazazi wake wakawajibu, wakasema, Tunajua ya kuwa huyu ndiye mwana wetu, tena ya kuwa alizaliwa kipofu; 

21 lakini jinsi aonavyo sasa hatujui; wala hatujui ni nani aliyemfumbua macho. Mwulizeni yeye mwenyewe; yeye ni mtu mzima; atajisemea mwenyewe. 

22 Wazazi wake waliyasema hayo kwa sababu waliwaogopa Wayahudi; kwa maana Wayahudi walikuwa wamekwisha kuafikiana kwamba mtu akimkiri kuwa ni Kristo, atatengwa na sinagogi. 

23 Ndiyo sababu wale wazazi wake walisema, Ni mtu mzima, mwulizeni yeye. 

24 Basi mara ya pili wakamwita yule mtu aliyekuwa kipofu, wakamwambia, Mpe Mungu utukufu. Sisi tunajua ya kuwa mtu huyo ni mwenye dhambi. 

25 Basi yule mtu akajibu, Kwamba yeye ni mwenye dhambi sijui. Najua neno moja, kuwa mimi nalikuwa kipofu na sasa naona. 

26 Basi wakamwambia, Alikutendea nini? Alikufumbua macho jinsi gani? 

27 Akawajibu, Nimekwisha kuwaambia, wala hamkusikia; mbona mnataka kusikia tena? Ninyi nanyi mnataka kuwa wanafunzi wake? 

28 Basi wakamshutumu, wakasema, Wewe u mwanafunzi wake yule; sisi tu wanafunzi wa Musa. 

29 Sisi tunajua ya kuwa Mungu alisema na Musa; bali yule hatujui atokako. 

30 Yule mtu akajibu, akawaambia, Hii ni ajabu! Kwamba ninyi hamjui atokako, naye alinifumbua macho! 

31 Twajua ya kuwa Mungu hawasikii wenye dhambi; bali mtu akiwa ni mcha Mungu, na kuyafanya mapenzi yake, humsikia huyo. 

32 Tokea hapo haijasikiwa ya kuwa mtu ameyafumbua macho ya kipofu, ambaye alizaliwa hali hiyo. 
33 Kama huyo asingalitoka kwa Mungu, asingeweza kutenda neno lo lote. 

34 Wakajibu, wakamwambia, Ama! Wewe ulizaliwa katika dhambi tupu, nawe unatufundisha sisi? Wakamtoa nje. 

35 Yesu akasikia kwamba wamemtoa nje; naye alipomwona alisema, Wewe wamwamini Mwana wa Mungu? 

36 Naye akajibu akasema, Ni nani, Bwana, nipate kumwamini? 

37 Yesu akamwambia, Umemwona, naye anayesema nawe ndiye. 

38 Akasema, Naamini, Bwana. Akamsujudia. 

39 Yesu akasema, Mimi nimekuja ulimwenguni humu kwa hukumu, ili wao wasioona waone, nao wanaoona wawe vipofu. 

40 Baadhi ya Mafarisayo waliokuwapo pamoja naye wakasikia hayo, wakamwambia, Je! Sisi nasi tu vipofu? 

41 Yesu akawaambia, Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi; lakini sasa mwasema, Twaona; basi dhambi yenu inakaa.”

Amen!

Katika habari hiyo kuna maswali kadhaa ya kujiuliza,

La kwanza ni kwa nini Bwana hakumponya huyu kipofu wakati ule ule alipokutana naye hadi kumwambia kwanza aende kunawa katika birika la ALIYETUMWA ( yaani SILOAMU?) ndipo atakapofunguliwa macho yake.?Unadhani alishindwa kumfungua macho muda ule ule?.

Pili Kulingana na habari baada ya kufunguliwa macho yake ni kweli alipata kuona kwa namna ile Kristo aliyokuwa anaitarajia?.

Ukichunguza kwa makini utaona kuwa Yule mtu hakumjua YESU ni nani, wala alipotokea wala alipoenda wala hakumwona uso wake hata baada ya kufunguliwa macho yake. Haikujalisha alifunguliwa macho kiasi gani yeye alichoweza kufanya ni kwenda tu kuendelea kufanya shughuli zake za nyumbani kwao za kila siku mpaka ilipofikia wakati majirani zake walipoanza kumuuliza habari za kufunguliwa macho yake..Ndipo akaanza tena kunena habari za YESU.

Kama tunavyosoma alianza kupitia mitikisiko pindi tu alipoanza kumkiri Kristo maishani mwake. Hapo ndipo vita kutoka kwa watu mbali mbali, kutoka kwa wakuu wa dini vikaanza, kukanwa na wazazi, kupuuziwa na majirani kulipoanza. Kwasababu kumbuka kwa wakati ule wayahudi wote walikuwa wameshakwisha kupatana kuwa akitokea mtu yeyote atakayemkiri Kristo kuwa ni mwokozi adhabu yake itakuwa ni kutengwa na sinagogi daima, kwa leo tunaweza kusema kutengwa na kanisa. Na kumbuka kutengwa na sinagogi kwa wakati ule ni zaidi ya hapo, kulikuwa ni sawa na kutengwa na jamii nzima ya wayahudi kwasababu Taifa zima lilikuwa na DINI moja na Utamaduni mmoja..Tofauti na sasahivi ambapo mtu akitengwa na jamii yake anaweza akakubaliwa na jamii nyingine kwasababu tamaduni zipo nyingi na kuna haki nyingi za kibinadamu mtu kuishi anavyotaka…Hivyo mtu aliyekuwa anadhubutu kufanya vile alikuwa hachukui uamuzi mwepesi, bali ni uamuzi wa kujikana kweli kweli, ulikuwa ni uamuzi mzito mno.. Na ndio maana ukisoma wapo wengi waliomwamini YESU lakini pale ilipofikia hatua ya kumkiri walishindwa

Yohana 11: 42 “WALAKINI HATA KATIKA WAKUU WALIKUWAMO WENGI WALIOMWAMINI; LAKINI KWA SABABU YA MAFARISAYO HAWAKUMKIRI, WASIJE WAKATENGWA NA SINAGOGI.

43 Kwa maana walipenda utukufu wa wanadamu kuliko utukufu wa Mungu.

44 Naye Yesu akapaza sauti, akasema, Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi”

Na kama tunavyosoma baada ya Yule kipofu kujadiliana na wale mafarisayo kwa muda mrefu ndipo waakamua kumchukua kwa nguvu na kumtupa nje ya Sinagogi…Maskini mtu Yule akitazama wazazi wake hawakutaka kusimama upande wake japo walijua ukweli kuwa ni Yesu ndiye aliyemponya, wale majirani zake hakuweza kumtetea kwa wakati ule wakiogopa kutengwa na jamii nzima, wala mtu yeyote aliyefahamu ukweli hakudhubutu kusimama upande wake, wote walikaa kando wakiogopa kumkiri BWANA, Hivyo Yule mtu akafukuzwa asionekane tena katikati ya mikusanyiko ya waaminio iliyokuwa katika miji ile, ilikuwa bado nusu tu apigwe kwa mawe kama angeendelea kudumu eneo lile na kushindana na wale viongozi wa dini,..

Lakini tunasoma alipokuwa mwenyewe pale nje ndipo Kristo AKAMJIA. Haleluya, na kwa kuwa yeye hakuwahi kumwona uso wake hata siku moja japo alifunguliwa macho na yeye, alipokuja Bwana hakuweza hakumtambua, mpaka Bwana alipomuuliza “WEWE WAMWAMINI MWANA WA MUNGU? Ndipo Yule mtu akajibu: Ni nani, Bwana, nipate kumwamini?..Bwana akamwambia “UMEMWONA, NAYE ANAYESEMA NAWE NDIYE.” Akasema, Naamini, Bwana. Akamsujudia.

Na mwishoni Bwana akamalizia na kumwambia maneno haya..

“39 MIMI NIMEKUJA ULIMWENGUNI HUMU KWA HUKUMU, ILI WAO WASIOONA WAONE, NAO WANAOONA WAWE VIPOFU.

40 Baadhi ya Mafarisayo waliokuwapo pamoja naye wakasikia hayo, wakamwambia, Je! Sisi nasi tu vipofu?

41 Yesu akawaambia, Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi; lakini sasa mwasema, Twaona; basi dhambi yenu inakaa.” 

Kaka/dada inawezekana Bwana alishakufungua katika vifungo vyako kule “KWA ALIYETUMWA (SILOAMU)”..Siloamu wako anaweza akawa mchungaji Fulani, mtumishi Fulani, huduma Fulani vyovyote vile. Inawezekana ulipokwenda ulipokea majibu ya maombi yako uliyokuwa umemwomba Mungu siku nyingi, ulipokwenda uliponywa, ulipokwenda ulifunguliwa, ulipokwenda upata kile ulichokuwa unakihitaji kwa muda mrefu..Lakini je! Ni KWELI ULIKUTANA NA KRISTO?. ULIUONA USO WAKE?

Yule kipofu japo alifanyiwa muujiza mkubwa kama ule lakini hakuwahi kumjua Kristo, wala kumwona sura yake..Lakini baada ya kuanza kumkiri tu na kuichagua ile njia ILIYOOGOPWA NA WENGI, iliyokuwa ya hatari ya kujikana maisha kwa ajili ya jina lake. Ndipo alipokwenda kukutana na YESU uso kwa uso kule nje! Na kumfahamu vizuri yeye ni nani. Unadhani alishindwa kumkana kusema tu vile ili kuwaridhisha mafarisayo. Hakushindwa lakini alitaka kutafuta kitu kilicho bora zaidi ya aliyotendewa, Alipotengwa kando ndipo Yesu akamjia.

Ni wengi leo hii, wanadai wamemwona Mungu katika maisha yao kisa tu wamefanikishwa katika mambo yao na shughuli zao. Lakini ukiyatazama maisha yao je ni kweli wameiendea njia ya msalaba, ya kujikana nafsi na kujitwika msalaba wako kwa ajili ya Kristo, na kuamua kuishi maisha matakatifu, utagundua hawajafanya hivyo na bado wanadai wamemwona Mungu.

Wanaogopa wakijaribu kufanya hivyo watatengwa na wazazi wao, wanaogopa kudharauliwa na marafiki zao, wanaogopa kuonekana ni watu wa ajabu washamba, wakiogopwa kuchukiwa na watu wa ulimwengu huu… Hawajui kuwa kule kufanikiwa kwao ilikuwa ni kwa ajili ya kulikiri jina la Kristo kwa maisha yao na si kwa midomo tu. Na pia ni kwa ajili ya wao kujitengenezea njia nzuri ya kwenda kukutana na Kristo lakini wao wanaikwepa. Dada/Kaka Kristo anapatikana katika njia iliyokataliwa, hapatikani kwa  wakuu wa dini,wala wa madhehebu anapatikana nje kule mahali palipokataliwa..Yule kipofu hakukutana na Kristo alipokuwa na wale mafarisayo, na wakuu wa dini, hapana badala yake alikutana na Yesu mahali ambapo hata yeye mwenyewe hakutarajia, mahali walipokuwa wamemtenga.

Kumbuka Kristo leo hii ametupwa nje na ulimwengu, Na ndio maana anasema Ufunuo 20: 20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.

Ili uwe na mahusiano binafsi na YESU katika maisha yako ni lazima uchukue uamuzi wa kujitwika msalaba wako na kumfuata.

Ni wale tu watakaokubali kutupwa na wao nje ndio watakaokutana na Kristo huko vinginevyo utabakia kumsikia tu, haijalishi ni kwa namna gani utakuponya magonjwa yako, haijalishi ni kwa namna gani atakufanikisha katika biashara zako, haijalishi ni kwa namna gani atakukirimia mahitaji yako. Kama hutakubali kutupwa nje na ulimwengu kwa ajili ya jina lake, hutakaa UMWONE YESU KAMWE!

Ndio maana sehemu nyingine Bwana Yesu anajulikana kama JIWE KUU LA PEMBENI ambalo limekataliwa na waashi wengi. Kristo hapatikani kwa Padre, kwa Mchungaji, kwa Papa, kwa Watumishi, au kwa mtu yoyote anayejiita Mtu wa Mungu.. Kristo anapatikana mahali palipokataliwa na Ulimwengu..Mahali penye njia nyembamba.. 

Luka 13: 22 “Naye alikuwa akipita katika miji na vijiji, akifundisha, katika safari yake kwenda Yerusalemu. 

23 Mtu mmoja akamwuliza, Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache? Akawaambia, 

24 JITAHIDINI KUINGIA KATIKA MLANGO ULIO MWEMBAMBA, KWA MAANA NAWAAMBIA YA KWAMBA WENGI WATATAKA KUINGIA, WASIWEZE”.

Njia ni nyembamba ndugu iendayo uzimani..Tujitahidi uipite hiyo sasa, kabla Mlango wa Neema haujafungwa, kwa kumwamini Yesu Kristo, Mkuu wa Uzima, na MSHIKAJI WA MAMLAKA YOTE, Kwa kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji mengi na Kwa Jina lake, na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

Bwana akubariki sana.Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Zinazoendana:

UKIAMINI NA UKIMKIRI YESU KWA KINYWA CHAKO, UTAOKOKA.

NJIA YA MSALABA

IKO NJIA IONEKANAYO KUWA SAWA MACHONI PA MTU.


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments