USIWE MKRISTO WA KUKAA TU GHALANI,

USIWE MKRISTO WA KUKAA TU GHALANI,

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Karibu tujifunze maneno ya uzima ya mwokozi.

Watu waliomwamini Yesu Kristo, yaani waliopokea ondoleo la dhambi zao. Hutambulika kama NGANO, lakini watu ambao bado wapo kwenye dhambi, hujulikana kama MAKAPI.

Sasa kazi ya kwanza ambayo Yesu anaifanya kwa mwamini, ni kumtenganisha yeye na makapi, kisha humweka katika ghala lake.

Mathayo 3:12  Ambaye pepeto lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake; na kuikusanya ngano yake ghalani, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.

Ghalani ni uweponi mwa Mungu, yaani kutengwa na udunia.

Soma pia..Mathayo 13:29-30.

Sasa kama wewe unafahamu ukulima, unajua kabisa si mbegu zote zinawekwa ghalani kwa matumizi ya chakula, zipo nyingine, zinachukuliwa na kurudishwa shambani ili kwenda kuzalisha nyingine. Na baadaye huongeza ghala la mkulima.

Tofauti kabisa na ile inayobakia pale ghalani, itaendelea kubakia vilevile hata miaka 10, lakini ile inayokwenda shambani, ndani ya hicho kipindi cha miaka 10, yaweza kuongeza magunia mengi sana ya ngano nyingine.

Ndio maana Bwana Yesu alisema maneno haya;

Yohana 12:24  Amin, amin, nawaambia, CHEMBE YA NGANO ISIPOANGUKA KATIKA NCHI, IKAFA, HUKAA HALI IYO HIYO PEKE YAKE; BALI IKIFA, HUTOA MAZAO MENGI. 25  Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele. 26  Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu.

Umeona hapo? Kumbe isipoanguka na kuoza basi itaendelea kubakia katika hali ile ile. Lakini ikikubali kuanguka na kuoza, ardhini, basi itachipuka kama shina, na mwisho wa siku itazaa sana.

Na hapa ndipo waamini wengi, hawataki kuingia gharama. Wanatamani wamzalie Mungu matunda, lakini hawawezi, kwasababu hawajakubali “kufa na kuoza” kwa habari ya huu ulimwengu.

Hawajakubali kuziangamiza  nafsi zao kwa ajili ya Kristo. Sasa hiyo ndio inayopelekea wabakie tu kama wakristo wa ghalani,wasioweza kuzalisha chochote.

Yesu alitoa sifa za mbegu yenye kuzaa katika ule mfano wa mpanzi,  akasema nyingine ziliangukia njiani, nyingine kwenye miamba, nyingine kwenye miiba, na nyingine kwenye udongo mzuri. Akasema vilizoangukia kwenye udongo mzuri ziliweza kuzaa kwa tendo moja tu la “kuvumilia”

Kuvumilia nini?

Kuvumilia dhiki, na udhia kwasababu ya Kristo, kuvumilia vishawishi vya anasa, udanganyifu wa mali, na shughuli za ulimwengu huu zilizopitiliza, lakini pia kwa unyofu wa moyo walikuwa wanalitendea kazi Neno ili walilolisikia lisiwe bure adui akaliiba ndani yao. (Luka 8:11-15). Hao ndio wakristo wasio wa ghalani, ni wakristo waliokubali kutoka nje, kumletea Bwana matunda.

Je! Na sisi tunaweza kupiga hatua nyingine? Umeokoka ndio, lakini ni lazima wokovu wako uwe na matokeo kwa wengine, uwavute na wengine kwa Kristo, kama wewe ulivyovutwa. Hivyo kubali kumaanisha kumfuata Yesu na kukaa mbali na udunia kwa kadiri uwezavyo.

Jitoe pia kwa Bwana, mali zako, zitumike kuhubiri injili, tenga fungu lako kwa Bwana, penda kusapoti kazi za Mungu, usiwe msomaji tu na kusema Amen!. Onyesha kuwa na wewe ni mtendaji kazi ili thawabu yenu iwe ni  moja, na yule mtendaji kazi mwingine.

Bwana atusaidie, tutoke ghalani.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

NI YESU YUPI UMEMPOKEA?, NI ROHO IPI UMEIPOKEA? NA INJILI IPI UMEIPOKEA?

ANGALIA JINSI USIKIAVYO:

SEMA KWA LUGHA NYINGINE.

Je Mungu ana njia ngapi za kuzungumza?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments