TENDA JAMBO LA ZIADA.

TENDA JAMBO LA ZIADA.

(Masomo maalumu yahusuyo kazi na uchumi).


Tunahitaji kujua kanuni chache ili tuweze kufungua milango yetu ya kiuchumi. Leo tutaangalia kanuni nyingine ambayo mkristo akiitumia basi anaweza kupata kibali mahali pale afanyiapo kazi.

Si wakati wote maombi tu pekee yanatosha kukuletea kibali katika maisha ya kazi/kuwajibika. Ni lazima pia uongeze na maarifa ili uweze kufungua milango hiyo ya Baraka.

Sasa ukitaka upate kibali kazini au kwa aliye juu yako, basi FANYA JAMBO LA ZIADA HAPO UFANYIAPO KAZI.

Kwa mfano Mshahara wako unaoupokea kwa siku, wiki au mwezi, ni kiasi Fulani…. baada ya kutoa sehemu ya Mungu (yaani sadaka pamoja na Zaka) kiasi kilichosalia  usikitumia chote katika mahitaji yako..bali toa sehemu kidogo ya hicho na ufanye jambo jipya na la kipekee hapo ufanyiapo kazi!.

Kwa mfano kama umeajiriwa na unafanya kazi ya usafi hapo kazini, badala ya kusubiri mwajiri wako akupe fedha ya kwenda kununua kifaa cha usafi, hebu wewe TENDA JAMBO LA ZIADA… toa kiasi kidogo cha pesa yako na nenda kununua kifaa hicho.

Kwa kufanya hivyo utaonekana mjinga mbele ya wafanyakazi wenzako na watu wengine walio karibu nawe pengine hata kwa mke wako/mume wako… lakini si kwa Mwajiri wako!, yeye atakusifu kama si kwa kinywa chake basi katika moyo wake, na hiyo itakuongezea kibali kikubwa sana katika maisha yako ya kazi… Utakuwa umepata nafasi katika moyo wake, na kiwango cha kukuamini na kukupenda kitaongezeka..

Au labda umeajiriwa katika mgahawa, hebu TENDA JAMBO LA ZIADA…badala ya kusubiri boss wako akupe fedha za kwenda kununua sahani za biashara, au akupe fedha za kwenda kununua sufuria, au sabuni.. hebu mara moja moja wewe toa kiasi chako kidogo cha mshahara kanunue zile sahani, au sufuria au kitu kingine chochote cha muhimu kinachohitajika pale..

Wala usianze kuangalia mahitaji uliyonayo (hayo yataendelea kuwepo tu)… wewe fanya hivyo kwasababu  unajua ni mbegu gani unayoipanda wakati huo!… wengine watakuona huna akili, au umechanganyikiwa, wewe usiangalie hayo bali angalia yanayokuja..

Pengine umeajiriwa kama mhasibu katika ofisi fulani, hebu TENDA JAMBO LA ZIADA, Toa kidogo katika mshahara wako kanunue kiti kingine cha ofisi au saa ya ofisi nzuri, au pamba kwa chochote kile pale ufanyiapo kazi.. weka mbali matatizo yako kwa muda, na mahitaji yako na ufanye hayo.. nakuhakikishia matokeo yake utakuja kuyaona baadaye.. Utapata kibali ambacho utakishangaa.

Wakati unafanya hayo, wengine watakuona ni mjinga, kwasababu hayo unayoyafanya yangepaswa kutekelezwa na boss wako au kampuni, na sio wewe…ndio maana watakuona umerukwa na akili, lakini Mwajiri wako atakuona ni shujaa..

Katika biblia Bwana YESU alitoa mfano wa wakili dhalimu, ambaye alitoa mali zake za wizi na kuwalipa wadeni wa Boss wake, na kupitia mali ile ya udhalimu alijipatanisha na boss wake pamoja na wadeni wa boss wake…na hivyo akasifiwa hata na yule yule aliyemwibia (yaani bosi wake). Soma Luka 16:1-12

Sasa huyu alijipatia kibali kwa mali ya udhalimu (maana yake mali ya wizi).. vipi wewe ambaye una mali ambayo sio ya wizi (halali), halafu ukaitumia katika kutafuta kibali?.. unadhani hutakipata??.

Lakini ukisema mimi nitaomba tu!, na kutumia kiasi chako kwa mahitaji yako tu…na huku hutaki kutenda jambo la ziada,  hapo unapofanyia kazi, utakuwa unajiwikwamishia Baraka zako tu!… kwasababu hayo uyafanyayo ni kila mtu anayafanya, na yameshazoeleka…lakini ukitenda TENDA TENDO LINGINE ZA ZIADA ambayo halifanywi na wengine wote, hapo utajipatia kibali.

Hata katika kumtumikia MUNGU, Bwana YESU alitufundisha kuwa ni lazima tujifunze kutenda tendo lingine la ziada ili tupokee kibali.

Mathayo 5:46 “Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?

47  Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo?”

Hivyo pata maarifa na TENDA TENDO LA ZIADA, na utaona jinsi utakavyopokea kibali katika yote uyafanyayo!.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

TENDA HAKI KWA FAIDA YAKO MWENYEWE.

Mfano wa wanawali kumi(Mathayo 25), unaelewekaje?

Mistari ya biblia kuhusu kibali.

NJIA NYINGINE YA KUPATA REHEMA NA KIBALI KUTOKA KWA MUNGU.

MAPAMBO YA WANAWAKE WALIOUKIRI UCHAJI WA MUNGU.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments