Category Archive Mafundisho

USIKWEPE CHUO CHA UTAKATIFU.

Zawadi kubwa Mungu aliyompa mwaminio ni UTAKATIFU. 

Utakatifu ni ile hali ya kuwa mkamilifu kama Mungu, kutokuwa na dosari au kasoro yoyote, msafi asilimia mia moja, bila kosa lolote ndani yako. 

Sasa heshima hii tumetunukiwa na Mungu, jambo ambalo hapo zamani halikwepo, ilihitaji matendo ya haki ya Mtu kuufikia, lakini hapakuwahi kutokea mwanadamu yoyote aliyeweza kufikia cheo hicho cha juu sana cha Mungu, yaani kutokuwa na dhambi kabisa.

Lakini pale tunapomwamini Bwana Yesu, siku hiyo hiyo, Mungu anatufanya Watakatifu kama yeye, haijalishi bado tutakuwa na asili ya dhambi nyingi kiasi gani. Hiyo ndio maana ya neema. Tunaitwa watakatifu bila ya kujisumbua kwa lolote.

Lakini sasa lengo la Mungu sio tuwe “watakatifu katika dhambi” Bali “tuwe watakatifu katika utakatifu”. Hivyo kuanzia huo wakati anaanza kumfundisha mtu kuusomea hadi kuuhitimu Utakatifu wake, aliopewa ili aendane na cheo alichotunukiwa tangu mwanzo.

Na hapo mtu akishindwa kupiga hatua, basi anaondolewa heshima hiyo kwake, na hivyo hawezi tena kuwa kama Mungu, na matokeo yake wokovu unampotea.

Mwaka Fulani hapa nchini kwetu kulikuwa na askari mmoja aliyeonyesha kitendo cha kishujaa kukataa rushwa ya milioni 10, ambapo alishawishiwa aipokee ili aifute kesi ya watuhumiwa wawili waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka,. Lakini yeye hakukubali, na ilipokuja kubainika, mkuu wa jeshi la polisi (IGP) akafurahishwa naye, Akampandisha cheo (kwani alikuwa ni askari wa chini). Lakini cha kushangaza baada ya kama miaka miwili tukaja kusikia Yule askari aliyepandishwa cheo ameshushwa cheo kile. Kufuatilia ni kwanini imekuwa hivyo? Jeshi la polisi likatoa taarifa kuwa alionyesha utovu wa nidhani, wa kukataa kwenda kwenye mafunzo ya cheo chake kipya.  Akidhani kwasababu IGP amempandisha basi inatosha hakuna haja ya mafunzo tena. Akasahau kuwa ufahamu wake wa kielimu ni lazima uendane na cheo chake, kwamba akiwa bado na cheo kikubwa, wakati huo huo anapaswa aendelee kusoma,na kujifunza kimatendo, ili aweze kutumika ipasavyo. Lakini akashushwa cheo na kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa kukataa kutii amri ya jeshi.

Ndivyo ilivyo katika UTAKATIFU tunaopewa na Mungu bure, ni lazima tuutendee kazi kwa kila siku kupiga hatua mpya ya mabadiliko. Huwezi kusema umeokoka (wewe ni mtakatifu), halafu maisha yako ya mwaka jana na mwaka huu ni yaleyale wewe sio mtakatifu.  Kila siku lazima uwe na mabadiliko, ulikuwa unabeti, unaacha kubeti, ulikuwa unavaa mavazi ya uchi uchi, unayachoma moto, ulikuwa unajichubua, unaacha, ulikuwa unasengenya unakaa mbali na wasengenyaji, ulikuwa unakesha kwenye muvi usiku kucha unaacha hayo, unatumia muda wako mwingi kwenye kujisomea biblia, ulikuwa ni mtu wa rushwa unaanza kuondoa vitendo hivyo kwenye biashara yako. Ulikuwa huwezi kufunga na kuomba unaanza kujizoeza kuwa mtu wa rohoni, unafunga, unaomba, na kukesha, Huko ndiko Mungu anakokutaka. Anaona umekiheshimu cheo alichokupa.

Ukiwa ni mtu wa kupiga hatua kila siku, basi Mungu atazidi kukuona wewe ni MTAKATIFU na hivyo utakuwa karibu na yeye. Lakini ukiishi hoe hae, hutambuliki kama umeokoka, au vipi, tabia zilezile za zamani unaendelea nazo, wala hujihangaishi kuziondoa. Usijidanganye wewe umeokoka.

Bwana atusaidie..

Je! Upo ndani ya Kristo? Je unataarifa kuwa hizi ni siku za mwisho? Yesu amekaribia kurudi? Ni nini utamweleza Mungu siku ile endapo leo utaukataa wokovu unaoletwa kwako bure..  Tubu dhambi zako, mgeukie Bwana, akupe Roho Mtakatifu, akupe heshimu hiyo ya utakatifu. Hivyo Ikiwa upo tayari kufanya hivyo basi fungua hapa kwa ajili ya mwongozo wa sala ya toba >>>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618 Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mada Nyinginezo:

FUNDISHO KUU LA NEEMA YA MUNGU KWETU.

MATUNDA 9 YA ROHO MTAKATIFU

UTAKASO NI SEHEMU YA MAISHA YA MKRISTO YA KILA SIKU.

USITAZAME NYUMA!

Kwanini hatuirithi neema kama tunavyoirithi dhambi?

HATARI YA KUHUBIRI INJILI TOFAUTI NA ILIYOANDIKWA KWENYE BIBLIA.

Wakili ni nani kibiblia? Uwakili ni nini?

Rudi nyumbani

Print this post

JUA HALITAKUPIGA MCHANA, WALA MWEZI WAKATI WA USIKU.

Nakusalimu katika jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo. Nakukaribisha katika kuyatafakari maneno ya uzima.

Ulishawahi kuutafakari vema huu mstari?

Zaburi 121:5 Bwana ndiye mlinzi wako; Bwana ni uvuli mkono wako wa kuume.  6 Jua halitakupiga mchana, Wala mwezi wakati wa usiku.  7 Bwana atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako.  8 Bwana atakulinda utokapo na uingiapo, Tangu sasa na hata milele.

Ni rahisi kumwelewa mtu anayekuambia, “leo jua limenipiga”, lakini si rahisi kumwelewa mtu anayesema “leo mwezi umenipiga” Ni wazi kuwa utamwona anakuchezea akili.  Si ni kweli?..Lakini hapa katika vifungu hivi ambavyo Mungu anaeleza ulinzi wake kwa watu wake jinsi ulivyo, anatumia mifano hiyo miwili  ya jua na mwezi. Na anaonyesha kuwa kama vile jua linavyompiga mtu, ndivyo na mwezi nao unavyompiga mtu.

Akiwa na maana gani?  

Tunajua kuwa mwezi hauna nguvu yoyote ya kumuunguza mtu au kumchosha, tofauti na jua. Lakini Mungu anaona hata mwangaza tu  huo wa mwezi ni pigo kwa mtu. Akiwa na maana  si katika mateso magumu, au dhiki kubwa zinazoonekana kwa macho ndio anazoshughulika nazo Mungu, lakini pia hata katika zile ndogo sana, ambazo unaweza kuona zikiendelea kuwepo hazina madhara yoyote kwako, Bwana anakulinda nazo.

Kwamfano wewe huwezi kuona umepata hasara pale nywele yako moja imepungua kichwani mwako, tena si rahisi kugundua,  lakini yeye anaithamini na ndio maana amezihesabu zote. Ikidondoka moja tu, anaona mapungufu, umekutana na mateso..

Mathayo 10:30  lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote.,

Vivyo hivyo rohoni, unaweza kumwomba Mungu, niepushe na majaribu, kichwani kwako ukafikiri hili na hili labda magonjwa, umaskini, vita, vifungo,ajali,  kuteswa kwasababu ya imani, N.K. ndio Bwana anashughulika navyo hivyo kukulinda, au kukupa nguvu ya kuvishinda. Lakini anahakikisha hata zile honi za magari unazopishana nazo barabarani, haziyaharibu masikio yako, jani ulilokanyaga jana, halijaharibu mguu wako, bacteria walio katika mikono yako, hawaui seli za ngozi, idadi ya minyoo walio tumboni mwako, hawaendi kula maini na figo zako, kiwembe kinachopita kichwani mwako kila siku haking’oi mizizi ya nywele, n.k…Haya mambo unaweza kuona ni ya kawaida tu, lakini Bwana akitoa mkono wake umeisha.

Kwa ufupi ni kuwa zipo Nyanja nyingi sana za hatari, ambazo Bwana anatuepusha nazo, Ndio maana tunapaswa tuwe waombaji sikuzote, unapojiona upo salama, omba, unapojiona upo kwenye matatizo omba, muda wote dumu uweponi mwa Bwana. Hata kama utaona kama majaribu yamekulemea, Bwana ameahidi ushindi mwishoni, Ayubu alilemewa na mateso lakini mwishoni alirejeshewa mara dufu.

Ulinzi wa Mungu ni uhakika kwa watu wake, dumu katika katika maombi ili Bwana apate nafasi ya kutulinda vema, nyakati za jua na nyakati za mwezi. (Mathayo 26:41)

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618 Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mada Nyinginezo:

MAJARIBU MATANO (5) YA MKRISTO.

Je! Siku ilihesabiwaje kabla ya jua na mwezi kuumbwa?

MIEZI 13 YA KIYAHUDI.

UWEZA WA MUNGU UNAONEKANA WAPI?

Mwandamo wa mwezi/Mwezi mpya Ni nini kibiblia?

Kumaka ni nini katika biblia? (Mathayo 8:27)

Rudi nyumbani

Print this post

Kumaka ni nini katika biblia? (Mathayo 8:27)

Jibu: Neno “kumaka” limeonekana mara mbili katika biblia na maana yake ni “kushangaa/ mshangao”. Mtu anapokutana na jambo au anapoona kitu au tukio la ajabu ambalo hajawahi kuliona au kukutana nalo hapo kabla huwa anapatwa na mshangao! Sasa huo mshangao ndio unaoitwa “kumaka”.

Mathayo 8:27  “Wale watu WAKAMAKA wakisema, Huyu ni mtu wa namna gani hata pepo na bahari zamtii?”

Hapa wanafunzi walipomwona Bwana Yesu anazikemea pepo za bahari na kumtii, waliingiwa na mshangao wa ajabu kujiuliza yule ni mtu wa namna gani?

Utalisoma tena tukio hilo katika Luka 8:27, Lakini pia utaona Bwana Yesu alifanya mambo mengi makubwa ambayo yaliwashangaza watu wengi, (soma Marko 5:42, na Luka 4:36).

Hiyo ni kuonesha uweza wa Bwana Yesu Kristo wa kutenda miujiza ulivyokuwa Mkuu. Lakini uweza Mkuu na Muujiza Mkuu Bwana Yesu alioufanya na anaondelea kufanya leo, ambao hakuna mwingine yeyote awezaye kuufanya ni Muujiza wa KUFUTA DHAMBI!.

Miujiza mingine yote Bwana Yesu alisema nasi pia tunaweza kuifanya, lakini ule wa kusamehe dhambi ni yeye tu ndiye anayeweza kuufanya.

Marko 2:9 “Vyepesi ni vipi, kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende?

10  Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (hapo amwambia yule mwenye kupooza)”

Kwahiyo na sisi tunapaswa kuutafuta na kuupokea huu muujiza mkuu anaotoa Bwana Yesu wa kusamehewa dhambi, kwasababu kama hatutasamehewa dhambi na tukaponywa magonjwa peke yake bado haitatufaidia chochote, lakini tukipata msamaha wa dhambi hata kama tusipopokea uponyaji wowote katika mwili bado ni faida kubwa kwetu, kwasababu tutaurithi uzima wa milele.

Je! Umepokea msamaha wa dhambi zako?.. na je unaijua kanuni ya kupokea msamaha mkamilifu kutoka kwa Bwana?

Kanuni ya kupokea msamaha wa dhambi ni rahisi, nayo ni Kutubu kwa kumaanisha kuacha dhambi, kubatizwa na kupokea Roho Mtakatifu. Hatua hizo tatu ukizifuata, utapokea muujiza ambao hujawahi kuupokea katika maisha yako yote.

Matendo 2:36  “Basi nyumba yote ya Israeli na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyemsulibisha kuwa Bwana na Kristo.

37  Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?

38  Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

39  Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie”

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618 Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mada Nyinginezo:

NI NINI BWANA ANATAKA KUTOKA KATIKA MUUJIZA ALIOKUFANYIA?

BABA UWASAMEHE

NINI MAANA YA KUTUBU

UMEONDOLEWA DHAMBI?

TAFUTA MSAMAHA HALISI, NA SI MSAMAHA TU!

Rudi nyumbani

Print this post

KUWA NA  MAFUTA YOTE YA ROHO MTAKATIFU NDANI YAKO.

Moja ya maeneo ambayo yamekuwa na uelewa mchanga katika ukristo, ni pamoja na eneo la Roho Mtakatifu. Wengi tunachofahamu kuhusiana na huduma ya Roho Mtakatifu ni kunena kwa lugha tu! Basi. Lakini hilo ni tone moja kati ya bahari kubwa, tunahitaji kumwelewa kwa mapana na marefu ili tujue utendaji kazi wake ulivyo kwa wanadamu na ulimwengu.

Kipo kitabu cha Roho Mtakatifu, ikiwa utapenda kukipata wasiliana nasi kwa namba zilizo chini ya chapisho hili/ au tutumie ujumbe whatsapp.

Leo  tutaona sehemu mojawapo ambayo inahusiana na mafuta ya Roho Mtakatifu.  Unaweza ukajiuliza, kwanini kila mara watu waliposhukiwa na Roho Mtakatifu, maandiko yanatumia neno “wakajazwa”, na sio neno kama ‘wakavikwa’  au labda ‘wakalishwa’. Kwasababu tukisema wakavishwa maana yake tunamfanya yeye kuwa kama nguo, au tukisema wakalishwa tunamfanya yeye kuwa kama chakula. Lakini tukisema wakajazwa tunamfanya yeye kuwa kama kimiminika, na hicho si kingine zaidi ya MAFUTA. Roho Mtakatifu anakuja kwetu kama MAFUTA. Ni vema kulitambua hilo!

Sasa si watu wote wanayo mafuta yote ya Roho Mtakatifu kama Bwana Yesu alivyokuwa,. Leo tutaona aina mbalimbali za mafuta hayo, kisha tujitahidi tuyapokee yote kwa msaada wa Roho.

1.Mafuta ya nguvu

Haya yanapatikana katika UMOJA.

Zaburi 133:1 Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja.  2 Ni kama mafuta mazuri kichwani, Yashukayo ndevuni, ndevu za Haruni, Yashukayo mpaka upindo wa mavazi yake.

Maana yake ni kuwa jinsi watakatifu wanavyoshirikiana  pamoja kwa umoja, rohoni, yanaonekana ni mafuta mengi yanashuka katikati yao, mengi kiasi cha kufika hata katika upindo wa mavazi. Wanatiwa mafuta, na hayo ni ya nguvu. Kwasababu palipo na umoja ndipo penye nguvu.

Na ndio maana siku ile ya pentekoste, Mungu aliwakutanisha kwanza mahali pamoja wakawa wapo orofani pale sio katika kupiga zoga, hapana, bali katika kusali na kuomba, na kutafakari maneno ya Bwana(Matendo 1:12-14). Na ghafla, wakashangaa, katika siku ya kumi, Roho Mtakatifu amewashukia wote wakajazwa nguvu. Wakawa mashahidi wa Bwana tangu siku ile  na kuendelea (Matendo 2).

Jambo kama hilo utalithibitisha tena katika Matendo 12:14, walipokuwa wamekaa pamoja kumwomba Mungu, mahali pale pakatikiswa, wajazwa Roho Mtakatifu wakanena Neno la Mungu kwa ujasiri. Hivyo hivyo na sisi  tupenda ushirika na wengine, hususani katika kuomba na kufunga. Tukiwa watu wa namna hii tutajazwa mafuta haya na tutapokea ujasiri mwingi sana katika wokovu wetu.

Soma (Mhubiri 4:12)

2. Mafuta ya shangwe

Haya yanapatikana katika usafi na utakatifu.

Waebrania 1:8  Lakini kwa habari za Mwana asema, Kiti chako cha enzi,Mungu,ni cha milele na milele; Na fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya adili. 9  Umependa haki, umechukia maasi; Kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekutia mafuta, Mafuta ya shangwe kupita wenzio

Shangwe ni ile furaha iliyopitiliza, inayodhihirika hata mpaka kwa nje. Halikadhalika Roho Mtakatifu naye anayo shangwe yake, ambayo hiyo inazidi hata hii ya kidunia, kwasababu ya kwake inakufanya ufurahi sio tu katika raha bali mpaka katika majaribu. (Luka 10:21)

Kwamfano utaona Bwana Yesu alikuwa nayo hata pale msalabani.

Wakolosai 2:15  akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.

Tukiwa watu wa kupenda haki(utakatifu), mafuta haya Roho anayaminina, mioyoni mwetu. Maisha yetu yanakuwa ni ya furaha tu, daima, vipindi vyote. Haijalishi mauvimu, kero, udhia, yataonekana kwa nje, lakini rohoni ni shangwe nyingi za Roho Mtakatifu, ndivyo Mungu alichokiweka ndani ya Kristo na kwa wakatifu wa kale ( Matendo 13:52, Waebrania 11:13, , Mathayo 5:12).

Hivyo Tuchague kupenda maisha ya haki ili tuyapate mafuta haya. Ni muhimu sana, ukipoteza furaha ya wokovu, huwezi kusonga mbele.

3. Mafuta ya upambanuzi

Haya yanaachiliwa katika kulitunza Neno la Mungu ndani yako.

1Yohana 2:26  Nimewaandikia haya katika habari za watu wale wanaotaka kuwapoteza. 27  Nanyi, mafuta yale mliyoyapata kwake yanakaa ndani yenu, wala hamna haja ya mtu kuwafundisha; lakini kama mafuta yake yanavyowafundisha habari za mambo yote, tena ni kweli wala si uongo, na kama yalivyowafundisha, kaeni ndani yake.

Kumbuka biblia ni sauti ya Mungu katika maandishi, hivyo unavyoiweka moyoni mwako, ndivyo inavyoumbika  na kuwa sauti kamili ya Mungu. Na hiyo ndio itakayokufudisha, na kukusaidia kupambanua, ikiwa wewe ni mkristo na una miaka  mingi katika wokovu halafu hujawahi kuisoma BIBLIA yote, bado kuna viwango Bwana hawezi kusema na wewe.  Lakini Unavyozidi kujifunza Neno ndivyo mafuta haya yanavyoachiliwa ndani yako kukufundisha. “Huna Neno, huna sauti ya Mungu”

4. Mafuta ya kuhudumu

Haya huachiliwa katika kuwekewa mikono na wakufunzi wako, au kuombewa na kanisa (wazee wa kanisa).

Huu ni utaratibu mwingine Mungu ameuachilia, katika kanisa, vipo vitu ambavyo huwezi kuvipokea wewe tu mwenyewe. Bali kutoka kwa waliokutangulia kiimani.

Elisha alitiwa mafuta na Eliya, akasimama mahali pake kihuduma (1Wafalme 19:15-16)

Musa aliwatia mafuta wale wazee 70, sehemu ya roho yake ikawaingia (Hesabu 11:16-25)

Daudi na Sauli wote walitiwa mafuta ya Samweli, ndipo wakapokea nguvu kutoka kwa Mungu, kutumika. (1Samweli 15:1, 16:12,)

Vilevile Timotheo, aliwekewa mikono na mtume Paulo  (2Timotheo 1:6), akapokea neema ya kuyasimamia makanisa ya Kristo, mahali pa Paulo.

Vivyo hivyo na wewe usikwepe, wala usimdharau kiongozi wako wa kiroho, hata kama atakuwa ana madhaifu. Anayo sehemu yake aliyopewa na Mungu kwa ajili yako. Jinyenyekeze omba akuwekee mikono neema ya Mungu ijae ndani yako ya kuhudumu, ili Bwana akunyanyue katika viwango vya juu zaidi.

Hivyo kwa kuzingatia aina hizo 4, tukazipokea basi tutamsogelea Bwana katika mafuta mengi sana ya juu. Mfano wa Bwana wetu Yesu Kristo. Roho Mtakatifu atajifunua zaidi ndani yetu.

Bwana akubariki.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mada Nyinginezo:

TUUTAFUTE UMOJA WA ROHO.

NITAUVUTAJE UWEPO WA ROHO MTAKATIFU KARIBU NAMI?

Nini maana ya’Shangwe ya waovu ni kwa muda kidogo’Ayubu 20:4

Wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza

Je tunaruhusiwa kujipaka mafuta au kujipulizia marashi?

Masihi ni nani?

Rudi nyumbani

Print this post

Je! Wapalestina ni watu gani, na sehemu yao katika biblia ni ipi?

Jina Palestina limetoka na Neno la kiyunani Filistia,  lenye maana ya ardhi ya wafilisti. Kwahiyo ile Filisti inayotajwa kwenye biblia ndio Palestina unayoisikia sasa.

Lakini Jambo ambalo wengi wanachanganya ni kudhani kuwa wafilisti walikuwa ni waarabu. Si kweli, kwani waarabu walikuwa ni watoto wa Ishmaeli kutoka kwa Ibrahimu, lakini wafilisti walikuwepo kabla hata ya Ibrahimu, na walitokea katika uzao wa Hamu.

Mwanzo10:14 na Wapathrusi, na Wakasluhi; huko ndiko walikotoka Wafilisti na Wakaftori.

Watu hawa walikuwa ni wapagani moja kwa moja, na waliabudu miungu yao mikuu mitatu iliyoitwa Ashtorethi, Baal-zebubu, na Dagoni.(Waamuzi 16:23, 2Wafalme 1:2, 1Samweli 31:10,)

Wafilisti walikwenda kuweka makazi yao, katika nchi ya Kaanani. Upande wa kusini, kutoka mto Yordani mpaka ule wa ile habari kubwa (Bahari ya Mediterenia). Na baadaye kipindi cha akina Samweli wakawa na miji yao mitano imara iliyoitwa Gaza, Ashdodi, Gathi, Ashkeloni, Ekroni (1Samweli 6:17, Yoshua 13:3)

Hivyo Ibrahimu alipoitwa na Mungu na kuambiwa aindee nchi ile aliwakuta tayari wapo, na wameshajiwekea ngome zao (Mwanzo 21:32, 34, 26:1).

Na wana wa Israeli walipokuwa wanavuka kuingia nchi yao ya ahadi Waliambiwa wawaangamize wakaanani wote, kwasababu wamepewa nchi yote. Lakini tunaona walipuuzia, na kule kukawia kawia kwao na kuridhika, Mungu akawaambia watu hawa watakuwa “mwiba” kwao .  

Waamuzi 2:1 Kisha malaika wa Bwana alikwea juu kutoka Gilgali kwenda Bokimu. Akasema, Mimi nimewaleta ninyi mkwee juu kutoka nchi ya Misri, nami nimewaleta hata nchi niliyowaapia baba zenu; nami nilisema, Mimi milele sitalivunja hilo agano langu nililoagana nanyi;  2 nanyi msifanye agano lo lote na hawa wenyeji wa nchi hii; zipomosheni nchi madhabahu zao; lakini hamkuisikia sauti yangu; je! Mmefanya haya kwa sababu gani?  3 Basi kwa ajili ya hayo mimi nilisema zaidi, Mimi sitawafukuza watoke mbele zenu; lakini watakuwa kama miiba mbavuni mwenu, na miungu yao itakuwa ni tanzi kwenu.

Na ndivyo ilivyokuwa Yoshua hakuweza kuwatoa wenyeji wote wa Filisti(Yoshua 11:20-23). Na ndio hao wakaja kuwasumbua baadaye.

Ni wazi kuwa Israeli walipigana vita vingi, lakini moja wa maadui zao waliokuwa wanawasumbua sana basi ni hawa wafilisti, kwasababu walikuja kupata nguvu, sio tu ya wingi wa watu, bali pia ya kiteknolojia katika silaha, kiasi kwamba Israeli ilitegemea kunolewa silaha zao kutoka Filisti.(1Samweli 13:19-23). Na zaidi sana waliwazidi Israeli hata kimaendeleo, kwa kipindi kirefu hawakuweza kuwashinda

Na wana wa Israeli walipomkosea Mungu aliwaweka kwenye mikono yao, wakataabishwa kwa muda mrefu, kisha walipomlilia Bwana, walinyanyuliwa mkombozi. Ndio hapo tunawaona waamuzi kama wakina Samsoni, Shamgari, Samweli, Sauli, Daudi.Wakipigana vita vingi sana na watu hawa.Ambavyo tunavyosoma katika biblia (Waamuzi, Samweli 1&2, Wafalme 1&2,)

Kuanguka kwa wafilisti.

Lakini wakati Israeli inachukuliwa utumwani taifa hili nalo halikupona lilianguka, katika mkono wa mfalme Nebukreza wa Babeli, na kupotea kabisa. (Yeremia 47:47, Ezekieli 25:15-17, Sefania 2:4-7).

Tangu huo wakati hakukuwa na taifa rasmi la wafilisti, wala haikuwa rahisi kuwatambua kwa miaka zaidi ya 2500.  Mpaka ilipofikia mwaka 1948, Taifa la Israeli kuundwa tena kwa mara ya kwanza, eneo hilo la wafilisti, kusini mwa Israeli, lilikuwa tayari linajulikana kama “Palestina”

Palestina ya leo ni mahali palipo na mchanganyiko wa jamii mbalimbali za watu, walio wa asili ya kifilisti wakiwa ni wachache sana, lakini wengi wao sasa ni waislamu waliohamishiwa hapo na waturuki, kutoka katika mataifa mbalimbali kati ya karne ya 16-19, pamoja waarabu katika karne ya 20 ambao nao waliletwa na waingereza.

Hivyo mpaka sasa tunavyoona, ni kwamba Palestina imemezwa zaidi na dini ya kiislamu na jamii kubwa ya waharabu. Na cha kushangaza ni kwamba ijapokuwa  jamii ya sasa ni tofauti kabisa,na wafilisti wa zamani, bado migororo ile ile ya zamani inanyunyuka tena. Kuonyesha kuwa Neno la Mungu halipiti milele.

Ule mwiba bado utawasumbua wayahudi.

Nini kinaendelea rohoni?

Lakini ipo sababu nyingine ya Rohoni. Kumbuka kuwa hatma ya huu ulimwengu, itakuwa ni Dunia nzima kusimama kinyume na taifa teule la Mungu Israeli. Ili Yesu Kristo atokee mawinguni na kuwapigania watu (Matendo 1:6, Ufunuo 19) .  Na tayari Mungu alishaahidi kuwa atafanya mataifa yote kuwa kama kikombe cha kulemea,. Ili tu ayachonganishe, kisha mwisho wake uwe ni yeye kulitetea taifa lake, ndipo huo mwisho ufike.

Wewe huoni mvuragano huu, unayagusa mataifa yote duniani.

Zekaria 12:3 Tena itakuwa siku hiyo, nitafanya Yerusalemu kuwa jiwe la kuwalemea watu wa kabila zote; wote watakaojitwika jiwe hilo watapata jeraha nyingi; na mataifa yote ya dunia watakusanyika pamoja juu yake

Unaweza kuona ni jinsi gani tupo mwishoni kabisa mwa dunia. Hii neema tuliyonayo huku katika mataifa, ndio inafikia ukomo wake, na kurejea Israeli. Maana Mungu anasema atawarudia watu wake (Warumi 10&11), na kuwaokoa, wakati huo yatakapokuwa yanatendeka unyakuo utakuwa umeshapita huku kwetu.

Zekaria 12:9 Hata itakuwa siku hiyo, ya kwamba nitatafuta kuwaangamiza mataifa yote watakaokuja kupigana na Yerusalemu.  10 Nami nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, roho ya neema na kuomba; nao watamtazama yeye ambaye walimchoma; nao watamwombolezea, kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao wataona uchungu kwa ajili yake, kama vile mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya mzaliwa wake wa kwanza.  11 Siku hiyo kutakuwa na maombolezo makuu huko Yerusalemu, kama maombolezo ya Hadadrimoni katika bonde la Megido

Je! Unaishije sasa hivi, Umehubiriwa injili mara ngapi, bado unashupaza shingo yango? Huko uendako unatarajia ukawe mgeni wa nani. Na ukweli umeshaujua kuwa tunaishi katika siku za kumalizia, Unyukuo wa kanisa ni wakati wowote. Huu ni wakati sasa ya kuyathimini maisha yako ya rohoni, angalia dunia inapoelekea, kufumba na kufumbua mambo yanabadilika. Uamuzi ni wako. Lakini ikiwa utapenda Yesu akuokoe, akufanye kiumbe kipya basi fungua hapa upate mwongozo wa sala ya toba. >>>>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Bwana akubariki.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mada Nyinginezo:

NIMEAZIMIA KUWAKUSANYA MATAIFA. NIPATE KUWAMWAGIA GHADHABU YANGU

KUNA NGUVU YA ZIADA KATIKA KULING’ANG’ANIA KUSUDI LA MUNGU.

Konzo la Ng’ombe ni nini? (Waamuzi 3:31).

Bahari mbalimbali zilizoorodheshwa kwenye biblia.

USIMPE NGUVU SHETANI.

Mataifa ni nini katika Biblia?

UAMINIFU NI KIGEZO KIKUBWA CHA KUTUMIWA NA MUNGU.

Rudi nyumbani

Print this post

Nchi iligawanyikaje kama tunavyosoma katika Mwanzo 10:25?

Swali: Je katika Mwanzo 10:25 tunasoma kuwa nchi/dunia iligawanyika? Swali ni Je! Iliwaganyikaje? Na je ule ndio ulikuwa mwanzo wa mabara saba (7) tuliyonayo leo?.

Jibu: Tusome,

Mwanzo 10:25 “ Eberi akazaliwa wana wawili wa kiume; jina la wa kwanza ni Pelegi maana KATIKA SIKU ZAKE NCHI ILIGAWANYIKA; na jina la nduguye ni Yoktani”.

Kama ukiendelea mbele kidogo kusoma Mlango wa 11 wa kitabu hiko cha Mwanzo utaona kuna tukio lilitokea ambalo ndio lile la kujengwa kwa Mnara wa Babeli, ambapo watu wale walipokuwa katika hatua za awali za kuujenga Mungu alishuka na kuchafua lugha zao na Semi zao, ili wasisikilizane. Na hiyo ikawafanya waache kuujenga ule mnara na kila mmoja kutawanyika na njia yake.

Mwanzo 11:1 “Nchi yote ilikuwa na lugha moja na usemi mmoja. 

2 Ikawa watu waliposafiri pande za mashariki waliona nchi tambarare katika nchi ya Shinari; wakakaa huko. 

3 Wakaambiana, Haya, na tufanye matofali tukayachome moto. Walikuwa na matofali badala ya mawe, na lami badala ya chokaa.

4 Wakasema, Haya, na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike mbinguni, tujifanyie jina; ili tusipate kutawanyika usoni pa nchi yote.

5 Bwana akashuka ili auone mji na mnara waliokuwa wakiujenga wanadamu.

6 Bwana akasema, Tazama, watu hawa ni taifa moja, na lugha yao ni moja; na haya ndiyo wanayoanza kuyafanya, wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya. 

7 Haya, na tushuke huko, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao.

 8 BASI BWANA AKAWATAWANYA KUTOKA HUKO WAENDE USONI PA NCHI YOTE; wakaacha kuujenga ule mji.

 9 Kwa sababu hiyo jina lake likaitwa Babeli; maana hapo ndipo Bwana alipoichafua lugha ya dunia yote; na kutoka huko Bwana akawatawanya waende usoni pa nchi yote”.

Hapo Mstari wa 8  unasema “BWANA AKAWATAWANYA KUTOKA HUKO WAENDE USONI PA NCHI YOTE”.

Sasa huo Mtawanyiko waliotawanywa wanadamu ndio “mgawanyiko wa nchi” unaozungumziwa katika Mwanzo 10:25 na unarudiwa tena katika 1Nyakati 1:19, Na ulitokea katika nyakati za mtu mashuhuri aliyeitwa “Pelegi” aliyekuwa mwana wa Eberi.

Hivyo mgawanyiko wa nchi haukuwa wa kiografia bali wa watu!.. na wala mabara 7 hayakuzaliwa hapo!, na Zaidi sana biblia haijataja mahali  popote kuwa dunia iligawanyika na kuwa mabara 7, huenda yalikuwa hivi hivi saba tangu uumbaji, au huenda yalizalika kipindi Fulani baada ya uumbaji, tusichokijua sisi lakini  si hiko kilichotajwa katika Mwanzo 10:25. Mgawanyiko huo wa Mwanzo 10:25 unahusu watu na si mabara.

Kujua ufunuo uliopo nyuma ya mnara wa Babeli basi fungua hapa >>TUUTAFUTE USEMI MMOJA. TUUJENGE MNARA WA MUNGU

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mada Nyinginezo:

MNARA WA BABELI

Babeli ni nchi gani kwasasa?

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 12 (Kitabu cha Isaya)

Shokoa ni nini katika biblia?

YESU KATIKA USINGIZI WAKE.

Rudi nyumbani

Print this post

Kuota upo uwanjani (uwandani)

Nini maana ya kuota upo uwanjani/uwandani?

Jibu: Kiroho uwanja au uwanda unawakilisha mahali pa mapambano.Wanamichezo wote wanaoshindania tuzo, huwa mashindano hayo yanafanyikia viwandani/uwandani.

Kwahiyo unapoota kuwa upo Uwandani na shughuli zako hazihusiani na viwanja, basi fahamu kuwa upo katika mapambano. Na mapambano hayo yanaweza kuwa mazuri au mabaya.
Mapambano Mazuri:

Mapambano mazuri ni yale ya imani, hivyo kama umeokoka vizuri na umesimama kisawasawa na ukapata ndoto au ono unashindana na watu wengi au wachache katika uwanja/uwanda basi fahamu kuwa huenda Mungu anakuonyesha, au kukukumbush vita vya kiimani vilivyopo mbele yako. Hivyo huna budi kupiga mbio..sawasawa na kile kitabu cha Waebrania 12:1

Waebrania 12:1”Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu”.

Soma pia Wafilipi 1:30, Wafilipi 1:27, na 1Wakorintho 9:24.

Lakini kama umejiona upo uwandani peke yako, basi kuna jambo la lingine Mungu anataka kusema nawe. Na hilo huenda ni jambo la tahadhari.

Na tahadhari yenyewe ni kama ile ya Kaini.

Wakati Kaini alipotaka kumwua Habili, alimtenga na kumpeleka uwandani. Na hiyo ni kanuni ya adui anapotaka kumdhuru mtu, anampeleka kwanza uwandani, mahali ambapo hapana watu, wala msaada wa kitu chochote..

Hivyo unapojiona upo uwandani/uwanjani peke yako, au upo na mtu mmoja, basi fahamu kuwa adui anatafuta kukuharibu au kuharibu mambo yako ya kiroho na kimwili.

Mwanzo 4:8 “Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani].
Ikawa walipokuwapo uwandani, Kaini akamwinukia Habili nduguye, akamwua”.

Kwahiyo uotapo ndoto hiyo, kama hujaokoka zingatia kuokoka, na pia kama una wokovu usio thabiti (maana yake wewe ni vuguvugu) basi zingatia kuwa moto, ili adui asipate nafasi ya kukumaiza.

Lakini kama tayari upo dhani ya wokovu ulio thabiti, basi zingatia Maombi, omba maombi ya kuharibu hila zote na njama za adui, na kutakuwa shwari.
Bwana akubariki.

Tafadhalishea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mada Nyinginezo:

KUOTA UPO UCHI.

Kuota unasubiriwa mahali fulani uhutubie, halafu unachelewa.

Kuota mbwa kunamaanisha nini?

UZAO WA NYOKA.

MWIMBIE BWANA ZABURI KATIKA NYAKATI ZA FURAHA.

Rudi nyumbani

Print this post

USILIPIZE KISASI.

Kwanini hatupaswi kujilipiza kisasi?… Kwasababu maandiko yanatufundisha kuwa kisasi ni juu yake yeye atalipa.

Warumi 12:19 “Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, KISASI NI JUU YANGU MIMI; MIMI NITALIPA, ANENA BWANA.

20 Lakini, Adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake”.

Tabia ya kujilipiza kisasa Bwana Mungu aliikataa tangu Mwanzo na Bwana Yesu akaja kuithibitisha tena katika Mathayo 5.

Tunaona baada ya Kaini kumwua ndugu yake Habili kwasababu ya wivu, Mungu alimlaani Kaini kwa kosa lile..

Lakini Mungu hakumwua Kaini bali alimlaani juu ya ardhi kwamba ataendelea kuishi lakini ardhi itamkataa… Kila kilimo atakachokifanya juu ya ardhi hakitafanikiwa, ndio maana baada ya pale hatuoni Kaini na uzao wake wakiendelea na kazi yake ya ukulima badala yake tunasoma wanaanza kutengeneza vyuma, na wapiga filimbi (Mwanzo 4:17-22).

Sasa baada ya Bwana Mungu kumlaani Kaini alijua kabisa kuna watu watakuja kusikia habari zake kwamba ni mwuaji, na pia kalaaniwa na Mungu, hivyo watataka wajichukulie hukumu aidha ya kumwua au kumnyanyasa…

Sasa Mungu kwa kulijua hilo, akamwekea Kaini alama, ili kila mtu atakayemwona asimguse…

Na alama hiyo ikaendelea kuwepo juu ya Kaini na uzao wake, iliyowatofautisha uzao wa Kaini na uzao mwingine.

Na Bwana akasema mtu atakayemwua Kaini, basi atalipwa kisasi mara 7,

Mwanzo 4:13 “Kaini akamwambia BWANA, Adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki.

14 Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua.

15 BWANA akamwambia, Kwa sababu hiyo ye yote atakayemwua Kaini atalipizwa kisasi mara saba. BWANA akamtia Kaini alama, mtu amwonaye asije akampiga”

Hivyo watu walivyosikia hivyo wakaogopa kumnyooshea mikono yao Kaini, kwasababu walijua kuna adhabu kubwa sana katika kufanya hayo…

Umeona?..Kumbe kisasi na hasira ndani ya maisha ya mtu ni machukizo makubwa sana mbele za Mungu..
Ndivyo maandiko yanasema…

Mithali 24:17 “Usifurahi, adui yako aangukapo; Wala moyo wako usishangilie ajikwaapo;

18 BWANA asije akaliona hilo, likamkasirisha; Akageuzia mbali naye hasira yake”.

Ikiwa na maana kuwa kama adui yako amekutenda mabaya na wewe usimrudishie yale mabaya, mwombee Bwana ambadilishe, itakuwa heri kwako…na utasikia ule mzigo umeondoka ndani yako…

Lakini kama ukifikiri kwamba njia ya kuondoa mzigo (uchungu) ndani yako ni wewe kujilipiza kisasi, nataka nikuambie kuwa ndio utauongeza badala ya kuupunguza, kwasababu utakayemlipa kisasi utakuwa umeweka uadui naye hivyo shetani anaweza kumtumia tena kufanya jambo lingine kwa wakati mwingine kwa njia nyingine…lakini lililo baya zaidi ni kwamba utakuwa umekosana na Mungu pia.

Sasa nini kifanyike ili kuishinda nguvu ya kisasi ndani yako?

1. Wokovu.

Wokovu ndio mlango wa Imani. Ni lazima kumwamini Yesu na kumkiri.


2. Maombi (yanayoambatana na mifungo).

Baada ya kuokoka ni lazima uwe mtu wa maombi. Maombi yatakufanya uwe na nguvu za kiroho ambazo zitakusaidia wewe kushinda dhambi.

3 .Kusoma Neno.

Neno la Mungu (biblia) litakusaidia kukujenga utu wako wa ndani. Kwamfano Neno lifuatalo ukilijua litakusaidia wewe kutolipiza kisasi.

Mhubiri 7:21 “Tena, usitie moyoni mwako maneno yote yaliyosemwa; usije ukamsikia mtumwa wako mwenyewe ali anakutukana.

22 Kwa kuwa mara nyingi moyo wako pia unajua ya kwamba wewe mwenyewe umewatukana watu wengine”.

Mambo haya matatu ukiyazingatia sana basi Nguvu ya kisasi haiwezi kufanya kazi ndani yako, utakuwa mtu wa kusamehe na kuombea wanaokuudhi, na mengine kumwachia Bwana, na hivyo utu wako wa ndani utajengeka sana.

Maran atha!.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618 Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mada Nyinginezo:

Biblia inaposema Kaini akatoka mbele za uso wa Bwana, Inamaana gani?

KISASI NI JUU YA BWANA.

Mtu wa kwanza kufa alikuwa nani?

SADAKA INAKOMESHA LAANA!

JE! Kaini alimpatia mke wake wapi?

Rudi nyumbani

Print this post

MAJARIBU MATANO (5) YA MKRISTO.

Safari ya wokovu ya mkristo inafananishwa na safari ya Wana wa Israeli kutoka Misri kwenda Kanaani. 

Na kama vile maandiko yanavyotuonyesha walikombolewa wote Kwa damu ya Mwana kondoo, Kisha Wakabatizwa katika bahari ya Shamu, wakawa chini ya wingu la Roho Mtakatifu kule jangwani,.. Lakini katika hayo yote bado tunaambiwa wengi wao hawakuweza kuiona Ile nchi ya ahadi. Isipokuwa wawili tu, (yaani Yoshua na Kalebu), waliotoka nchi ya Misri.

Biblia inatuonyesha walipishana na majaribu 5, ambayo yaliwafanya waangamie jangwani. Na majaribu yenyewe tunayasoma katika 1Wakorintho 10:1

1 Wakorintho 10:1-12

[1]Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari; [2]wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari;

[3]wote wakala chakula kile kile cha roho; [4]wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo. [5]Lakini wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani.

[6]Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani. [7]Wala msiwe waabudu sanamu, kama wengine wao walivyokuwa; kama ilivyoandikwa, Watu waliketi kula na kunywa, kisha wakasimama wacheze.

[8]Wala msifanye uasherati, kama wengine wao walivyofanya, wakaanguka siku moja watu ishirini na tatu elfu. [9]Wala tusimjaribu Bwana, kama wengine wao walivyomjaribu, wakaharibiwa na nyoka.

[10]Wala msinung’unike, kama wengine wao walivyonung’unika, wakaharibiwa na mharabu. [11]Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. [12]Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke.

Kama tunavyosoma hapo. Makosa hayo yalikuwa ni haya;

  1. Kutamani mabaya
  2. Kuabudu sanamu
  3. Kufanya uasherati
  4. Kumjaribu Mungu
  5. Kunung’unika

1) Kutamani mabaya

Mungu aliwapa MANA kama chakula pekee ambacho wangekula jangwani, wao na mifugo Yao, lakini, baadaye waliikinai wakataka NYAMA, na vyakula vingine (Hesabu 11:4-35), matokeo yake ikiwa Mungu kuwaua, wengi wao.

Kama wakristo tuliookoka MANA yetu ni NENO LA MUNGU, Hatupaswi kulikinai, tukakimbilia chakula kingine kisicho Cha kiMungu. Tukataka tuongozwe na mifumo ya kidunia. Ndugu ni hatari mbaya sana. Kumbuka Ile mana ijapokuwa kilikuwa ni chakula Cha aina Moja, lakini hawakuwahi kuumwa, Wala kudhoofika, Wala miguu yao kupasuka, tofauti na walivyokuwa Misri penye vyakula vingi, lakini vimegubikwa na magonjwa. 

Ndugu Lipokee Neno la Mungu, ishi Kwa hilo, hata kama halitavutia (kidunia), lakini limebeba virutubisho vyote vya kimwili na kiroho. Wanaotembea Kwa Neno la Mungu, hawatikisiki hustawi milele.

2) kuabudu sanamu:

Walipomwona Musa amekawia mlimani, na Mungu hazungumzi chochote Kwa wakati ule  wakajiundia sanamu zao za ndama waziabudu. Wakacheza, wakala na kinywa (Kutoka 32). Hii ni kuonesha kuwa kitu chochote kinachokufanya ushangilie  tofauti na Mungu wako, ni ibada ya sanamu.

Rafiki kuwa makini Kwa wakati wa Leo mkristo kushabikia mipira, kwenda Disko, kutumikia Mali, kufuatilia vipindi vya sinema kulikopitiliza, chattings, kupenda anasa. Ni ibada za sanamu waziwazi.

 Kwasababu gani?. Kwasababu ndio bubujiko lako la roho lilipo kama ilivyokuwa Kwa Wana wa Israeli, Kwa sanamu zile. Ikapelekea watu wengi kufa siku Ile. Ibada Yako iwe Kwa Bwana. Mungu ni mwenye wivu. Mpira ukichukua nafasi zaidi ya Mungu wako ni kosa.

3) Kufanya uasherati

Walipokuwa jangwani Mungu aliwakataza wasitangamane na wageni, kwasababu watawageuza mioyo na kuiabudu miungu Yao. Lakini wao walipowaona wanawake wa taifa la Moabu, wakaenda kuzini nao, Kisha wakageuzwa mioyo wakaabudu miungu Yao. Hiyo ikawa sababu ya Mungu kuwaua waisraeli wengi sana idadi yake 23,000.

Na sisi kama wakristo tulishapewa tahadhari kwenye maandiko. Tusifungwe nira na wasioamini isivyo sawasawa (2Korintho 6:14-18). Kwasababu hakuna ushirika kati ya Nuru na Giza. Hivyo hatuna budi kuwa makini na ulimwengu, tushirikiane nao kwenye mambo ya kijamii na ya msingi, pale inapokuwa na ulazima, lakini ya kiroho, hatupaswi hata kidogo kuwa na urafiki nao kwasababu ni rahisi kugeuzwa moyo na kuambatana nao kitabia, na matokeo yake tukamwasi Mungu.

Sulemani aligeuzwa moyo, Wana wa Mungu tunaosoma kwenye Mwanzo 6 nao pia waligeuzwa mioyo Kwa jinsi hiyo hiyo, na wewe pia usipojiwekea mipaka na watu ambao ni wa kidunia, Unaweza kupoteza taji lako. Pendelea zaidi kuwa na kampani ya waliookoka. Ni Kwa usalama wako. Usijikute unafanya uasherati wa kiroho.

4) Kumjaribu Bwana

Wana wa Israeli walimjaribu Bwana, wakati Fulani wakamnun’gunikia Mungu na Musa, wakisema chakula hiki dhaifu, wakitaka Kwa makusudi Bwana awafanyie Tena muujiza mwingine, Mungu akakasirishwa nao, akawaangamiza Kwa nyoka (Hesabu 21:4-9).

Kama mkristo tambua kuwa Mungu haendeshwi kama “robot”. Kwamba ni lazima afanye jambo Fulani Kila tutakapo ndio tuthibitishe yeye yupo na sisi. Ndugu ukristo wa hivi ni hatari, wengi wameishia kuanguka kwasababu hii. Jaribu kama hili aliletewa Bwana Yesu na shetani jangwani. Ajitupe kutoka kinarani, kwasababu maandiko yanasema Mungu atamuagizia malaika wake wamchukue salama. lakini Bwana Yesu alimwambia shetani usimjaribu Bwana Mungu wako.

Kamwe usimwendeshe Mungu, mwache yeye ayaendeshe maisha Yako. Tuwe na hofu na Mungu wetu.

5) Kunung’unika.

Wana wa Israeli tangu mwanzo wa safari Yao Hadi karibia na mwisho, waligubikwa na manung’uniko tu,(Kutoka 23:20-21) wengi wao hawakuwa watu wa shukrani. Ijapokuwa walilishwa mana, waliouna utukufu wa Mungu Kwa wingi. Lakini bado manung’uniko yalizidi shukrani.

Biblia inatuasa sisi tuliookoka tuwe watu wa Shukrani (Wakolosai 3:15), Kwa kazi aliyoimaliza Yesu pale msalabani ya kuondolewa dhambi ni fadhili tosha zaidi hata ya wale Wana wa Israeli kule jangwani. Hata tukikosa Kila kitu, maadamu tumeahidiwa uzima wa milele. Hatuhitaji kuwa na hofu na jambo lolote. Wokovu wetu ndio uwe faraja.

Epuka Maisha ya manung’uniko.

Bwana akubariki.

Ikiwa tutashinda majaribu haya MATANO katika safari yetu ya wokovu. Basi tutalipokea taji timilifu Kwa Bwana  siku Ile mfano wa Yoshua na Kalebu.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618 Au jiunge na makundi yetu ya mafundisho ya kila siku kwa kwa njia ya Whatsapp kwa kubofya hapa >>>> WHATSAPP GROUP

Mada Nyinginezo:

Nini maana ya Mhubiri 10:16, inaposema Ole wako, nchi, akiwa mfalme wako ni kijana?

Wale Nyoka wa Moto jangwani, walikuwa ni wa namna gani?

Nimekuwa kama mwari nyuni wa jangwani

JE! JICHO LAKO LINAONA NINI KATIKATI YA MAJARIBU?

NI KWA NAMNA GANI TUTASHINDA MAJARIBU?

JIHADHARI NA UONGO WA SHETANI UNAOKARIBIANA NA UKWELI.

MLANGO MWINGINE WA ADUI KUTULETEA MAJARIBU.

Rudi nyumbani

Print this post

TUUTAFUTE UMOJA WA ROHO.

Umoja wa Roho Mtakatifu upo katika vifungo 7, ambavyo kama kanisa ni lazima tujifunge katika vifungo hivyo.

Lakini kabla ya kuvitazama hivi vifungo 7 vya Roho Mtakatifu, ni vizuri tuweke msingi kidogo kumhusu Roho Mtakatifu.

Biblia inatufundisha kuwa kuna Roho 7 za Mungu, ambazo ndizo zinazotajwa kama Macho 7 ya Mungu.

Ufunuo 5:6  “Nikaona katikati ya kile kiti cha enzi na wale wenye uhai wanne, na katikati ya wale wazee, Mwana-Kondoo amesimama, alikuwa kana kwamba amechinjwa, mwenye pembe saba na macho saba, AMBAZO NI ROHO SABA ZA MUNGU zilizotumwa katika dunia yote”

Vile vile inazitaja Roho hizi 7 kama TAA SABA ZA MUNGU, ikiwa na Maana kuwa hizo ndizo mwanga mbele ya kiti cha Enzi.

Ufunuo 4:5 “Na katika kile kiti cha enzi kunatoka umeme na sauti na ngurumo. NA TAA SABA ZA MOTO ZILIKIWAKA MBELE YA KILE KITI CHA ENZI, NDIZO ROHO SABA ZA MUNGU”.

Hii yote ikimaanisha kuwa Roho Mtakatifu anatenda kazi katika Nafasi zake 7, au hatua zake 7 katika kuwakamilisha watu wake, lakini haina maana kuwa Roho Mtakatifu wapo 7.

Kwa msingi huo basi twende tukazitazame jinsi anavyolikamilisha kanisa katika kifungo cha UMOJA katika hatua zake saba.

Tusome,

Waefeso 4:3 “ na kujitahidi kuuhifadhi UMOJA WA ROHO katika kifungo cha amani.

MWILI MMOJA, na ROHO MMOJA, kama na mlivyoitwa katika TUMAINI MOJA la wito wenu.

BWANA MMOJA, IMANI MOJA, UBATIZO MMOJA.

MUNGU MMOJA, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote”.

Tutazame moja baada ya nyingine:

1.MWILI MMOJA.

Mwili unaozungumziwa hapa ni Mwili wa Yesu, (Soma Waefeso 4:12 na Wakolosai 3:15), na Mwili huu unajengwa kupitia Vipawa na Karama ambazo Roho Mtakatifu ameziweka ndani yetu, ambapo kila mmoja ni kiungo ndani ya mwili huo.. Hivyo ili tuufikie umoja wa Roho kama kanisa ni lazima tuenende katika msingi huu kwamba kanisa linaongozwa katika karama za Roho Mtakatifu, na si itikadi, mapokeo au siasa.

1Wakorintho 12:13  “Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.

14  Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi”.

2. ROHO MMOJA.

Anaposema Roho mmoja, zipo roho nyingi, hata shetani naye ni roho.. ikiwa na maana kuwa ndani ya kanisa ni lazima tuwe na Roho mmoja anayezaa matunda yanayofanana kwa wote. Na matunda ya Roho ni yale yanayotajwa katika Wagalatia 5:22, kupitia hayo, tutakuwa tumekamilka katika kifungo cha pili cha Roho. Ndio maana biblia inatufundisha kuzichunguza roho, kwamaana zipo roho nyingi..

2Wakorintho 11:4 “Maana yeye ajaye akihubiri Yesu mwingine ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea ROHO NYINGINE MSIYOIPOKEA, au injili nyingine msiyoikubali, mnatenda vema kuvumiliana naye”

3. TUMAINI MOJA

Tumaini linalozungumziwa hapa ni “Tumaini la Utukufu ujao”.. Kwamba kila aliyeokoka analo tumaini la kuingia katika utukufu wa Mungu ujao,(Mbingu mpya na nchi mpya). Hili ni tumaini ambalo Kanisa lazima liufikie, na si kila mmoja anaamini analoliamini, kwasababu wapo wengine wanaosema hakuna ufufuo, mtu akifa amekufa!, jambo ambalo ni kinyume kabisa na maandiko. Ufufuo upo, na watakatifu watafufuliwa na kuingia katika utukufu wa milele.

Wakolosai 1:26  “siri ile iliyofichwa tangu zamani zote na tangu vizazi vyote, bali sasa imefunuliwa kwa watakatifu wake;

27  ambao Mungu alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo utajiri wa utukufu wa siri hii katika Mataifa, NAO NI KRISTO NDANI YENU, TUMAINI LA UTUKUFU”

4. BWANA MMOJA

Yupo Bwana mwingine (yesu mwingine), anayehubiriwa tofauti na yule wa kwenye maandiko matakatifu.

2Wakorintho 11:4 “Maana yeye AJAYE AKIHUBIRI YESU MWINGINE ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea roho nyingine msiyoipokea, au injili nyingine msiyoikubali, mnatenda vema kuvumiliana naye”.

Yesu mwingine ni yule anayesema Mungu haangalii mwili anaangalia Roho, ni yule anayesema mchukie adui yako, n.k. Lakini yule halisi anasema Mwombee adui yako, waombeeni wale wanaowaudhi, na wasameheni wale wanaowaudhi (Mathayo 5:43).

5. IMANI MOJA

Imani moja ni sahihi ni ile inayosema mpatanishi kati ya Mungu na mwanadamu ni mmoja (naye ni YESU KRISTO), Lakini Imani nyingine inasema “watakatifu waliokufa pia wanaweza kuwa wapatanishi” hivyo wanaweza kutuombea…

1Timotheo 2:5  “Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu”.

Vile vile inasema, mwombezi wetu kwa Baba ni yeye mmoja Yesu Kristo ( 1Yohana 2:1) na wala hakuna mwingine, lakini Imani nyingine inasema waombezi wanaweza kuwa wengi mbinguni. Hivyo kanisa ni lazima lifikie umoja wa Imani ya kweli ya kwenye biblia, kwamba mpatanishi ni mmoja na mwombezi ni mmoja, ambaye ni Yesu Kristo, na wala hakuna mwingine wa kumsaidia.

6. UBATIZO MMOJA.

Ubatizo mmoja wa kimaandiko ni ule wa Maji mengi (Yohana 3:23) na kwa jina la Bwana Yesu Kristo (Matendo 2:38, Matendo 10:48, Matendo 19:5). Ni lazima kanisa lifikie huu umoja, na si kila mmoja kuamini ubatizo wake.

7. MUNGU MMOJA.

Mungu mmoja wa kweli  ni yule aliyeumba mbingu na nchi, ambaye ni Baba wa yote, aliyeko juu mbinguni na si sanamu, wala miti, wala wanadamu. Hivyo ni lazima ndani ya mwili wa Kristo wote tufikie umoja huu wa kumwamini na kumwabudu Mungu mmoja, na kuchanganya ibada na miungu mingine au sanamu.

Adui anafanya kazi kwa nguvu, kuuvunja UMOJA HUU WA ROHO, kwasababu anajua ndio NGUVU YA KANISA, anataka kuweka umoja wake mwingine wa kidunia ndani ya kanisa, na kuutafsiri kama ndio umoja wa roho. Hivyo hatuna budi kuwa makini na kuyaishi maandiko.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mada Nyinginezo:

JE UNAMHUBIRI KRISTO KATIKA KWELI YOTE?.

Roho Mtakatifu ni nani?.

NI KWASABABU YA YESU KRISTO.

TUMAINI NI NINI?

Dinari ni nini na Rupia ni nini (Mathayo 20:2,Ufunuo 6:6)

Rudi nyumbani

Print this post