USITAZAME NYUMA!

USITAZAME NYUMA!

Je! Ni kosa tu la kugeuza shingo na kutazama nyuma ndilo lililomgharimu mke wa Lutu maisha?.. Bila shaka Mungu asingeweza kumhukumu kwa kosa hilo, ni wazi kuwa kuna jambo lingine la ziada alilifanya..

Leo tutajifunza nini maana ya kugeuka nyuma, na mke wa Lutu aligeukaje nyuma hata ikamgharimu maisha yake..

Awali ya yote hebu tusome mstari ufuatao…

Luka 9:61 “Mtu mwingine pia akamwambia, Bwana, nitakufuata; lakini, nipe ruhusa kwanza nikawaage watu wa nyumbani mwangu.

62 Yesu akamwambia, Mtu aliyetia mkono wake kulima, KISHA AKAANGALIA NYUMA, hafai kwa ufalme wa Mungu”.

Kwa mfano huo Bwana alitafsiri kuwa “kitendo cha kuamua kurudi nyuma baada ya kukusudia kumfuata yeye” ni sawa na “kutazama nyuma baada ya kudhamiria kwenda shambani”. Hivyo kutazama nyuma hapo, ni kumwacha Bwana Yesu kwa kitambo, kwenda kurekebisha mambo fulani kisha kumrudia.

Sasa mpaka kufikia hapo tutakuwa tumeshaanza kupata kuelewa nini maana ya mke wa Lutu kutazama nyuma.. Kwamba alimwacha Lutu na kurudi nyuma..

Lakini ili tulithibitishe hilo vizuri, hebu tusome tena maneno ya Bwana Yesu mahali pengine, ambapo aliieleza habari hiyo ya Mke wa Lutu vizuri zaidi..

Luka 17:28 “Na kadhalika, kama ilivyokuwa katika siku za Lutu, walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakinunua na kuuza, wakipanda na kujenga;

29 lakini siku ile Lutu aliyotoka Sodoma kulinyesha moto na kibiriti kutoka mbinguni vikawaangamiza wote.

30 Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile atakayofunuliwa Mwana wa Adamu.

31 Katika siku ile, aliye juu ya dari, na vyombo vyake vimo ndani ya nyumba, asishuke ili kuvitwaa; NA KADHALIKA, ALIYE SHAMBANI ASIREJEE NYUMA.

32 MKUMBUKENI MKEWE LUTU”.

Hapo Bwana anaifananisha siku za kufunuliwa kwake na siku za Lutu, na anaelezea au anatoa ushauri jinsi ya kuokoka na ghadhabu ya Mungu kipindi itakapokaribia kumwagwa duniani kote, kama ilivyomwagwa katika miji ya Sodoma na Gomora.

Anasema siku hiyo “mtu aliye shambani asirejee nyuma”.. “maana akirudi huku atakutana na hatari itakayomgharimu maisha, hivyo abaki huko huko, au akimbie mbali zaidi”…na baada ya Bwana kusema maneno hayo anahitimisha kwa kusema “MKUMBUKENI MKEWE LUTU”.

Sasa jiulize kwanini aseme “Mkumbukeni mkewe Lutu”.. Maana yake kuna somo la kujifunza kutoka kwake, ili na sisi kipindi ghadhabu hiyo inakaribia kumwagwa duniani, tusiangamie kama yeye… Maana yake ni kwamba “mke wa Lutu alirejea nyuma”..aliangukia kwenye hilo kundi ambalo  Bwana alisema, “aliye shambani asirejee nyuma”.. yeye alirejea nyuma na kukumbana na ghadhabu ya Mungu, ule moto na kiberiti na ile ardhi ya chumvi, ya Sodoma ambayo biblia inasema haiwezi kupandwa wala kumea, (Kumbukumbu 29:22-23), vikagandamana na mwili wake na kutengeneza umbile kama la mtu aliyesimama, kama nguzo, ambapo hata baada ya moto ule kuisha katika hiyo miji, na kila kitu kiteketea umbile lake lilibaki kama sanamu za kumbukumbu zinazotengenezwa na kuwekwa kwenye maingilio ya miji.

Hiyo yote ni kwasababu alirejea nyuma.. alianza kuitamani mikoba yake ya fedha aliyoiacha kule nyumbani.. Hakuwa na lengo la kurudi kuishi Sodoma, bali alivitamani vyombo vyake, mali zake, akazichukue na kisha aondoke nazo…ili huko aendako ziweze kumsaidia kuendesha maisha, lakini mambo yakabadilika, kabla ya kumaliza safari moto ulikuwa umeshamzunguka kila mahali.

Hiyo inatufundisha na sisi, tulioianza safari ya wokovu. Hii dunia tayari imeshatamkiwa hukumu, hakuna maombi yoyote yanayoweza kuifuta hukumu ya huu ulimwengu. Yaliyotamkwa na kuandikwa yatatimia kama yalivyo..

 Hivyo kilichobaki kwetu ni sisi kuondoka na kujiokoa nafsi zetu, na katika safari yetu, hatupaswi kurejea nyuma..tunapaswa tukazane kuzidi kusonga mbele, kwasababu nyuma yetu, moto unazidi kusogea huku tuendako, hivyo tunakaza mwendo.

Kurejea nyuma ni kitendo cha kupiga hatua kabisa kuurudia ulimwengu.. ulikuwa umeshaushinda uzinzi lakini sasa umeurudia, ulikuwa umeshaishinda pombe na ulevi, na utukanaji, ulikuwa umeshaanza kumtumikia Mungu, lakini sasa umeacha, ulikuwa umeshaanza mambo yote ya ulimwengu, ikiwemo uvaaji mbaya, na kujipodoa..lakini sasa umerejea nyuma, umeanza kuyafanya hayo tena na ziaid ya hayo.. Bwana anakuambia.. “mkumbuke mkewe Lutu”..mkumbuke..mkumbuke..

Hakuna mtu mwingine yeyote Bwana aliyetuambia tumkumbuke katika biblia nzima… Ni huyu tu! Mke wa Lutu, ndiye aliyetuasa tumkumbuke…tusimsahau, maana yake tujifunze kwake.

Kama bado hujampokea Yesu maishani mwako mpokee leo, na kama tayari ulikuwa umeanza kurejea nyuma, basi ahirisha hiyo safari kabla hujafika mbali, kwasababu kuna wakati utatamani kumrudia Bwana lakini utashindwa, unyakuo wa kanisa upo karibu sana.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

SI MAPEPO YOTE NI YA KULIPUKA.

NI LIPI KATI YA MAKUNDI HAYA, WEWE UPO?

JIHADHARI NA UONGO WA SHETANI UNAOKARIBIANA NA UKWELI.

Je! “Mke wa ujana wako” ni yupi kibiblia?

JIHADHARI NA UONGO WA SHETANI UNAOKARIBIANA NA UKWELI.

KUSAMBAA KWA ROHO YA MPINGA-KRISTO.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments