FUMBO ZA SHETANI.

FUMBO ZA SHETANI.

Kati ya yale makanisa 7 tunayoyasoma katika kitabu cha Ufunuo, Kanisa la Thiatira, lilikuwa ni la tofauti sana, kwani lenyewe lilisifiwa sana na Bwana kwa jinsi lilivyokuwa linapanda viwango, siku baada ya siku, kiimani, kihuduma, pamoja na kiupendo, tofauti na makanisa mengine sita, hadi Bwana Yesu alilipongeza kwa  kuliambia, matendo yake ya mwisho yamezidi yale ya kwanza..(Ufunuo 2:18-29)

Lakini pamoja na kuwa lilienda katika uaminifu huo, Shetani naye hakukaa nyuma. Bali alibuni njia ya kitofauti sana ya kuliangamiza, na njia yenyewe ndio hiyo ya kutumia MAFUMBO.  Alibadili mbinu zake za kawaida, akawa anakuja tofauti na walivyotarajia. Na kwa njia hiyo alifanikiwa kulishusha kwa spidi kubwa kanisa lile, kwasababu  baadhi yao walidhani kwamba wanaendelea vizuri na Mungu, kumbe wanamwabudu shetani moja kwa moja.

Leo kwa neema za Bwana tutajifunza baadhi ya FUMBO za shetani, wengi wetu hatuzijui ambazo anazitumia hata leo, na hizo zimewafanya watu wengi warudi nyuma, kama sio kuanguka kabisa kiroho.

Hizi ndio fumbo zake;

  1. Shetani anataka tudhani kuwa hawezi kusema ukweli:

Wakati ule mtume Paulo anafika kwa mara ya kwanza, Mji huo wa THIATIRA, alikutana na kijakazi mmoja aliyekuwa  na pepo la utambuzi, na lilipomwona Paulo, lilimshuhudia Paulo ukweli, kwamba yeye ni mtumishi wa Mungu aliyejuu, na liliendelea kufanya  hivyo kwa muda mrefu tu, lengo lake likiwa ni kumpumbaza Paulo adhani ile ni roho ya Mungu ikimshuhudia, ili tu lisisumbuliwe kutenda kazi zake, Lakini mtume Paulo kwa kufunuliwa na Roho akatambua kuwa Yule sio Roho wa Mungu bali ni shetani, ndipo akalikemea likamtoka.

Mtendo 16:16 “Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua.

17 Akamfuata Paulo na sisi akipiga kelele, akisema, Watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya wokovu.

18 Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile.

19 Basi bwana zake walipoona ya kuwa tumaini la faida yao limewapotea, wakawakamata Paulo na Sila, wakawakokota mpaka sokoni mbele ya wakuu wa mji;

Hata leo, Shetani anawajia watu kwa namna hii, na wao bila kujua kumbe tayari wameshanaswa katika mitego yake. Ndugu si kila habari ya kweli inatoka kwa Mungu, Nabii kukueleza habari sahihi za maisha yako, hata ibilisi anaweza kufanya hivyo. Mpime kwa Neno la Mungu, na matunda anayoyatoa ndani yake.  Hicho ndio kigezo. Usiridhishwe na maneno tu, ridhishwa na maisha nyuma ya hayo maneno.

     2)  Anataka tudhani kuwa hawezi kuwepo kanisani:

Hili hili kanisa la Thiatira, lilidhani hivyo, Mpaka Bwana Yesu alipolifumbua macho na kuliambia kuna mwanamke Yezebeli katikati yao, (Ambaye anawakilisha watumishi wa uongo waletao mafundisho mageni ndani ya kanisa),  Anawafundisha njia potofu.

Ufunuo 2:18 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Thiatira andika; Haya ndiyo anenayo Mwana wa Mungu, yeye aliye na macho yake kama mwali wa moto, na miguu yake mfano wa shaba iliyosuguliwa sana.

19 Nayajua matendo yako na upendo na imani na huduma na subira yako; tena kwamba matendo yako ya mwisho yamezidi yale ya kwanza.

20 Lakini nina neno juu yako, ya kwamba wamridhia yule mwanamke Yezebeli, yeye ajiitaye nabii na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ili wazini na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu.

21 Nami nimempa muda ili atubu, wala hataki kuutubia uzinzi wake.

22 Tazama, nitamtupa juu ya kitanda, na hao wazinio pamoja naye, wapate dhiki kubwa wasipotubia matendo yake;

23 nami nitawaua watoto wake kwa mauti. Na makanisa yote watajua ya kuwa mimi ndiye achunguzaye viuno na mioyo. Nami nitampa kila mmoja wenu kwa kadiri ya matendo yake.

24 Lakini nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, wowote wasio na mafundisho hayo, WASIOZIJUA FUMBO ZA SHETANI, kama vile wasemavyo, Sitaweka juu yenu mzigo mwingine”.

Hata leo, wapo watu wa Mungu wazuri, wanabidii kweli katika kumtafuta Mungu, lakini hawajui kuwa viongozi wao wanawakosesha kwa Mungu pasipo wao kujua, kwamfano, wambiwapo bikira Maria anaweza kuwa mpatanishi wako na Mungu, hayo ni machukizo, ufundishwapo mafundisho ya kutumia mafuta ya upako, chumvi, sabuni n.k. kana kwamba hivyo vitu vinatosha kumponya mtu, hizo ni ibada za sanamu. Lakini kwasababu unamwamini kiongozi wako kwamba hawezi kukosea, unamtii, ukidhani Mungu atakuridhia na wewe. Kuwa makini na kila fundisho geni unaloletewa na kiongozi wako.

         3) Tudhani kuwa sikuzote anatisha na mwenye mapembe:

Wengi ukiwaambia shetani  yupoje moja kwa moja, wanachowaza katika akili yao ni kitu cha kutisha chenye mapembe, na kichwa cha nyoka. Ni kweli hivyo vitu vinamwakilisha yeye. Lakini yeye hayupo hivyo, kumbuka, alikuwa ni malaika kama malaika wengine, na alipofukuzwa hakuondolewa chochote alichokuwa nacho, hata nguvu zake, bali alifukuzwa tu kwenye makao yake mbinguni.

Kwahiyo sasa alipo bado anatumia njia yake ya uzuri kuwadanganya watu wengi. Hii imewafanya watu wadhani shetani yupo katika vitu vichafu chafu, au vibaya baya, na shida na umaskini, vichaa, na wagonjwa.. Lakini  Siku ile alimpofuata Bwana Yesu ili kumjaribu alikuja kama tajiri, mwenye milki zote za ulimwengu. Biblia inasema anaweza kujibadilisha kuwa malaika wa Nuru,

Kwahiyo usitazamie kuwa wakati wote atakufuata tu katika ndoto mbaya usiku au katika uchawi, au katika magonjwa. Wakati mwingine atakuja na amani feki, na utulivu, na utajiri. Ukadhani ni Mungu huyo kumbe ni shetani, anakutega ili kukuangamiza. Usikurupukie kila mafanikio mazuri, au fursa iliyopo mbele yako.

          4) Tudhani kuwa hawezi kuzitetea njia za Mungu.

Tunaweza kudhani shetani hawezi, kujifanya anaisapoti kazi ya Mungu, au kuitetea, unafki huo anao. Wakati ule Bwana Yesu alipowaambia wanafunzi wake kuhusiana na mateso yake, utaona wakati huo huo shetani akamwingia Petro kujifanya, yeye ni mtetezi wa Bwana..

Mathayo 16:22 “Petro akamchukua, akaanza kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata.

23 Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu”.

Ni kawaida yake, hata wakati akina Zerubabeli wanajenga hekalu la Bwana, maadui zao walijitokeza kwa kivuli cha kuwa wanataka kuwasaidia ujenzi, lakini walipofukuzwa ndio hapo wakaonyesha makucha yao, wao ni akina nani.(Ezra 4)

Shetani akishaona una kitu ndani yako cha ki-Mungu atakuja kwa njia ya msaada au utetezi, kuwa makini sana, na misaada unayoipokea katika utumishi wako au unachokifanya. Hakikisha unaifahamu na unaelewa kwa undani nyuma yake kuna roho gani. Vinginevyo utaingia katika matatizo makubwa sana.

         5) Tudhani kuwa hawezi kukubali kushindwa.

Si kila wakati ibilisi atakuja kama mpingamizi, au mharibifu, hapana, lengo lake litakuwa ni hilo ndio, lakini atakuja kwa ujanja wa kujionyesha ameshindwa wewe una nguvu nyingi, atajiweka chini yako, ajifanye kuwa yeye siku zote ni mnyonge tu.. lakini kumbe ameshakuweza. Ndicho kilichomtokea Yoshua alipovuka Jordani, sababu mojawapo ya yeye kushindwa kuwaondoa wenyeji  wote wa Kaanani ilikuwa ni hiyo, ya kumsikiliza shetani unyonge wake .  Pale walipojifanya, wametokea nchi ya mbali, wanaomba sharti ya amani wasidhuriwe, kwasababu wamesikia ushujaa wao,  kumbe ni watu wa karibu tu (Yoshua 9)

Leo hii mapepo yanaweza kukusifia sana, kujishusha, kusema wewe ni mkuu, unatisha,una upako, una nguvu,  yakajifanya yanatetemeka mbele zako, ili tu uchukulie mambo rahisi rahisi, lakini kumbe tayari yanatenda kazi kwa nguvu ndani yenu bila kujua.. Usikisikilize kilio cha shetani. Ni mwongo.

       6) Tudhani kuwa hajui mambo mengi.

Shetani anayotabia ya kujifanya mjinga, hajui  kila kitu. Pale Edeni alimfuata mwanamke na kuanza kumwambia Ati, hivi ndivyo Mungu alivyosema, msile “matunda ya miti yote”?. Anajifanya kama hajui, ni matunda gani yaliyokatazwa, na ndio maana anasema “miti yote”. Anakusubiria utiririke, ndipo akunasie mahali fulani.

Hila hii anayo hata sasa, huyo kijana anakuja anajifanya hajui uzinzi ni nini..anataka taarifa kwako, umwambie kwa muhtasari, ndipo hapo akupeleke mpaka kwenye vilindi vya dhambi. Kila jambo baya, kabla ya kukuingiza, atataka wewe ndio umfundishe kwanza.

Kwahiyo hiki ni kipindi cha kuishi kwa umakini, tuzijue FUMBO ZA IBILISI. Ili asifanikiwe kutunasa popote pale. Tuzitambue fikra zake, tumpinge.

Swali ni je! Umeokoka? Je! Unaouhakika kuwa Kristo akirudi leo hii, utakwenda naye mbinguni? Kumbuka hizi ni siku za mwisho kweli kweli, siku yoyote unyakuo utapita, na ibilisi analijua hilo, na ndio maana anafanya kazi kwa nguvu nyingi sana kutafuta watu wa kuwameza.

Hivyo tubu dhambi zako kwa kumaanisha kabisa kumfuata Yesu. Ili akuweke huru.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Elisante Nnko
Elisante Nnko
1 year ago

Shalom mwl aomba kupata mafunfisho Zaid Asante