SWALI: Nini maana ya “saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada?”
Jibu: Unabii huo Bwana Yesu aliutoa kwa wanafunzi wake, pamoja na wote ambao watakuja kumwamini baadaye, kwamba utafika wakati kila ambaye atawaua, au kuwatesa atadhani kuwa anamtolea Mungu ibada. Hiyo ni kuonyesha kwamba mateso ya watu wa Mungu, yanaanzia ndani ya dini, au Imani, na si penginepo. Na Bwana Yesu alisema tena, adui za Mtu ni watu wa nyumbani kwake mwenyewe (Mathayo 10:36).
Sasa tukirudi kwenye swali kwanini Bwana Yesu aseme, “saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada”. Ni kwasababu dhiki ya wakristo, itaanzia kwa watu wanaojiita wa dini.
Tukianza na Bwana wetu Yesu mwenyewe, watu waliomsulubisha ni Makuhani na wakuu wa dini, Hao ndio waliohusika wa kwanza katika dhiki zote za Bwana, mpaka Golgotha..Hawa makuhani, ndio waliomshawishi Pilato Mrumi, amsulubishe Bwana. Na walipokuwa wanafanya hayo, walidhani wanamfanyia Yehova ibada, (yaani wanampendezesha Mungu) kwasababu Torati ya Musa ilisema..
Kutoka 31:15 “Kazi itafanywa siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, takatifu kwa Bwana; kila mtu atakayefanya kazi yo yote katika siku ya Sabato, hakika yake atauawa”.
Kwahiyo walipomwona Bwana Yesu, anatembea huko na huko kuifanya kazi ya Mungu, ikiwemo kuponya wagonjwa na kuwafungua, wakaamini anaivunja torati, hivyo ili kumpendezesha Mungu, ni lazima Bwana Yesu auawe kulingana na hilo andiko la Kutoka 31:15. Hivyo walimuua Yesu mioyoni mwao wakiamini kwamba wamelitimiza Neno la Mungu, kwamba kila mtu atakayefanya kazi yoyote siku ya sabato auawe.. kumbe wamepotea!.
Na sio tu Bwana Yesu, tunaona pia mitume wake na wanafunzi wake waliofuata baada yake, Mfano tunamwona mtu mmoja anayeitwa Stefano. Huyu aliuawa na wale waliomwua walidhani wanaitimiza torati.
Matendo 6:8 “Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu.
9 Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano;
10 lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye.
11 Hata wakashawishi watu waliosema, Tumemsikia mtu huyu akinena maneno ya kumtukana Musa na Mungu.
12 Wakawataharakisha watu na wazee na waandishi, wakamwendea, wakamkamata, wakampeleka mbele ya baraza.
13 Wakasimamisha mashahidi wa uongo waliosema, Mtu huyu haachi kusema maneno ya kufuru juu ya mahali hapa patakatifu na juu ya torati;
14 maana tumemsikia akisema kwamba Yesu huyo Mnazareti atapaharibu mahali hapa, na kuzibadili desturi tulizopewa na Musa.
15 Watu wote walioketi katika ile baraza wakamkazia macho yao, wakamwona uso wake kuwa kama uso wa malaika”.
Sheria ya mtu aliyemtukana/kumlaani Mungu, ilikuwa ni kifo.
Walawi 24:15 “Nawe nena na wana wa Israeli na kuwaambia, Mtu awaye yote atakayemlaani Mungu wake atachukua dhambi yake.
16 Na yeye atakayelikufuru jina la Bwana hakika atauawa; mkutano wote watamwua kwa kumpiga kwa mawe; kama ni mgeni, kama ni mzalia, hapo atakapolikufuru jina la Bwana atauawa”.
Kwahiyo kulingana na hilo andiko Stefano alistahili kupigwa mawe, kwasababu tayari walikuwa wamemwambia kuwa amemtukana Mungu (Ingawa alisingiziwa), hivyo wote walioshiriki kumuua waliamini kuwa wanalitimiza hilo andiko kwamba “yeyote atakayemlaani Bwana Mungu wake, sharti mkutano wote wampige kwa mawe mpaka afe”. Hivyo hao kwa kumuua Stefano walidhani wanamtolea Mungu ibada.
Kadhalika na vifo vya mitume karibia wote, ni hivyo hivyo, wote walioshiriki kuwaua walidhani kuwa wanamtolea Mungu ibada, na yote hayo yametokea ili litimie hilo Neno Bwana Yesu alilolisema. “saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada”.
Lakini pamoja na hayo, unabii huo wa Bwana haukuishia tu kwa mitume au wakristo wa kanisa la kwanza, bali pia unaendelea mpaka leo. Leo watu wa kwanza wanaotumika na shetani bila kujua kuwaletea wakristo wa ukweli dhiki ni watu wanaojiita watu wa imani, hao ndio shetani anaowavaa kuwaletea wakristo wa kweli dhiki, na hata kuwaua.
Leo hii akitokea mtu wa Mungu kajikana nafsi, na kaenda kasimama mahali Fulani anahubiri, kwa adabu yote, labda kwenye gari, au mahali Fulani penye watu, utaona watakaotokeza wa kwanza kwenda kumshitaki kwa wenye mamlaka, na hata kumweka ndani, kwamba anawapigia kelele na hana kibali ni watu Fulani wanaojiita wakristo, tena wanaoyajua maandiko au hata pengine ni kiongozi Fulani mkubwa wa kanisa. Na anafanya hivyo akitumia andiko linalosema…
Warumi 13: 1 “Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu”
Na tena anafurahi kuona au hata akisikia Yule mtu kapotea kabisa, huku moyoni akiamini kwamba “anamfanyia Mungu ibada”, kumbe anamfanyia ibada shetani. Wakati yeye anafurahia Yule mtu kutiwa ndani, upande wa pili kuna mtu yale maneno yamemgusa na anakwenda kutubu..
Wakati Fulani Petro na Yohana walisimama hekaluni kuhubiri, wakakamatwa na wakuu wa dini, na kutiwa gerezani, wakiwa kule gerezani malaika akaja kuwatoa, na huyo huyo malaika akawaambia warudi kuhubiri kule kule hekaluni walikokamatiwa. Sasa huyo malaika hakujua kwamba wanapaswa watii mamlaka iliyo kuu, na wawe na vibali?? Kasome Matendo 5:17-21.
Bwana Yesu alisema katika Mathayo 28:18 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.
19 Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi…”
Hivyo ni lazima tujihakiki kila siku, na tuwe makini tusije tukajikuta tunafanya mambo tukidhani kuwa tunampendezesha Mungu kumbe ndio tunakwenda mbali naye, na kumuudhi. Ukikuta mahali popote jina la Yesu linatajwa ni vyema ukafunga mdomo wako na kutulia, kwasababu hujui ni nini Mungu anafanya kwa wakati huo.
Bwana atusaidie.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp
Mada Nyinginezo:
Shalom, Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe daima.
Siku ya leo, dunia inaadhimisha tukio kuu lililotokea takribani miaka 2000 iliyopita, Na tukio lenyewe ni lile la kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo kaburini.
Lakini lipo jambo nataka tujifunze, juu ya mazingira yaliyokuwa yanaendelea siku ile. Lakini kabla ya kuingia katika kiini cha somo letu, nikurudishe nyuma kidogo ili tuweke msingi. Naomba ufuatilie mpaka mwisho lipo jambo kubwa utajifunza leo.
Siku mbili kabla ya Kristo kusulibiwa alikuwa ameketi katika nyumba ya mtu mmoja aliyeitwa Simoni mkoma, kama tunavyojua habari akiwa anawafundisha alitokea mwanamke mmoja, akiwa amebeba kibweta cha Marhamu ya Nardo, akakifungua, akamwagia Yesu kichwani, lakini wale watu waliokuwa karibu walipoona tukio lile walianza kumnung’unikia yule mwanamke sana, kwanini anapoteza fedha nyingi katika mambo yasiyo ya msingi. Sasa mpaka unaona watu wanakinung’unikia kitendo kile ujue kuwa marhamu ile ilikuwa si ya bei ya kawaida.
Kwani kama ingeuzwa wenyewe wanasema wangepata dinari 300, na dinari moja kwa enzi za kibiblia ni mshahara wa kibarua wa siku nzima, (Soma Mathayo 20:1-15), hivyo tukijaribu kubadilisha kwa wakati wetu huu, mshahara wa kibarua kwa siku nzima tunajua ni kama sh. Elfu 20 hivi, ukiizidisha kwa 300, hiyo ni sawa na milioni 6.
Hivyo marhamu hiyo kwasasa ingeuzwa sh. Milioni 6. Kwahiyo unaweza kuona hapo mwanamke yule alijitoa kimasomaso kweli kuinunua, pengine aliuza kila kitu alichokuwa nacho ili tu, amnunulie Kristo marashi yale mazuri ya kupendeza. Na matokeo yake ni kuwa Bwana Yesu akampa thawabu kubwa sana, ya kumbukumbu lisilofutika daima..
Tusome.
Marko 14:3 “Naye alipokuwapo Bethania, nyumbani mwa Simoni mkoma, ameketi chakulani, alikuja mwanamke mwenye kibweta cha marhamu ya nardo safi ya thamani nyingi; akakivunja kibweta akaimimina kichwani pake.
4 Palikuwa na watu waliochukizwa katika nafsi zao wakisema, Kwani kupoteza marhamu namna hii?
5 Maana marhamu hii ingaliweza kuuzwa kwa dinari mia tatu na kuzidi, wakapewa maskini. Wakamnung’unikia sana yule mwanamke.
6 Yesu akasema, Mwacheni; mbona mnamtaabisha? Amenitendea kazi njema;
7 maana sikuzote mnao maskini pamoja nanyi, na kila mpendapo mwaweza kuwatendea mema; lakini mimi hamnami sikuzote.
8 Ametenda alivyoweza; ametangulia kuupaka mwili wangu marhamu kwa ajili ya maziko
9 Amin, nawaambia, Kila ihubiriwapo Injili katika ulimwengu wote, na hili alilotenda huyu litatajwa kwa kumbukumbu lake”.
Sasa mpaka hapo tutakuwa tumeshajenga msingi wa somo letu la leo, Sasa tuzidi kusonga mbele.
Wakati Bwana Yesu anashushwa pale msalabani baada ya kufa kwake, biblia inatuambia kulikuwa na wanawake waliotoka naye Galilaya wakifuatilia kwa karibu, kujua ni wapi watakapokwenda kuulaza mwili wa Bwana (Soma Luka 23:55-56 ).
Na walipoona na kupamaki, wakaondoka kwenda nyumbani, kuandaa, Manukato na Marhamu. Lengo lao lilikuwa ni kwenda kuipaka maiti ya Bwana marhamu hiyo. Lakini kwasababu siku hiyo ilikuwa ni maandalio ya sabato hawakuweza, ikawabidi, wayaweke tayari wasubiri mpaka siku ya jumapili asubuhi ambapo sabato itakuwa imeshakwisha, waende kuupaka mwili wake manukato hayo.
Marko 16:1-3
“1 Hata sabato ilipokwisha kupita, Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yakobo, na Salome walinunua manukato wapate kwenda kumpaka.
2 Hata alfajiri mapema, siku ya kwanza ya juma, wakaenda kaburini, jua lilipoanza kuchomoza;
3 wakasemezana wao kwa wao, Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe mlangoni pa kaburi”?
Lakini tunapaswa tujifunze, katika habari hiyo, kulikuwa hakuna umuhimu wowote wa kwenda kuupamba na manukato mwili ambao tayari upo kaburini, tena umeshakaa siku 3 mule, uzingatia tena kaburi lenyewe limetiwa muhuri na walinzi, kiashirio kuwa hakuna mtu yoyote aliyeruhusiwa kusogelea mahali pale.
Kwa namna ya kawaida Marhamu ile ilistahili kumwagiwa Yesu akiwa hai, kama alivyofanya yule Mwanamke wa kwanza nyumbani kwa Simoni mkoma, au kama alivyofanya Miriamu nduguye Martha siku ile Yesu alipokwenda kwao (Yohana 12:3)..
Au wangemwagia, wakati bado hajazikwa, yaani mwili ukiwa bado haujaenda kaburini ili kuufanya usiotoe harufu, kama alivyofanya Nikodemo wakati ule walipomshusha msalabani ili kwenda kumzika
Yohana 19:39 “Akaenda Nikodemo naye, (yule aliyemwendea usiku hapo kwanza), akaleta machanganyiko ya manemane na uudi, yapata ratli mia.
40 Basi wakautwaa mwili wake Yesu, wakaufunga sanda ya kitani pamoja na yale manukato, kama ilivyo desturi ya Wayahudi katika kuzika”.
Lakini tunaona hawa wanawake, hawakujali upotevu wowote, waliindaa kwa ajili ya maiti iliyokwisha kuzikwa tayari,..Hilo ni tendo kuu sana la Upendo kwa Bwana wao.
Japokuwa walijua kuwa watakumbana na kikwazo cha Jiwe kubwa pale kaburini, japokuwa walijua kwa namna ya kawaida zoezi lao wanalojaribu kulifanya haliwezi kufanikiwa lakini walijitoa ufahamu, wakaanza safari yao hivyo hivyo, ya kwenda kupoteza marhamu zao za thamani nyingi, kwa ajili ya maiti iliyokwisha kuzikwa siku chache nyuma..
Lakini kwa tukio lao lile la upendo usio wa kawaida, walipofika tu pale kaburini, biblia inatuambia waliona kaburi limeshakuwa wazi tayari, malaika wa Bwana alitangulia kuwafungulia, tena akiwa mule ndani ya kaburi tayari anawangojea,… Embu Tuendelee kusoma..
Marko 16:3-8
“3 wakasemezana wao kwa wao, Ni nani atakayetuvingirishia lile jiwe mlangoni pa kaburi”?
4 Hata walipotazama, waliona ya kuwa lile jiwe limekwisha kuvingirishwa; nalo lilikuwa kubwa mno.
5 Wakaingia kaburini wakaona kijana ameketi upande wa kuume, amevaa vazi jeupe; wakastaajabu.
6 Naye akawaambia, Msistaajabu; mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyesulibiwa; amefufuka; hayupo hapa; patazameni mahali walipomweka.
7 Lakini enendeni zenu, mkawaambie wanafunzi wake, na Petro, ya kwamba awatangulia kwenda Galilaya; huko mtamwona, kama alivyowaambia.
8 Wakatoka nje, wakakimbia kutoka kaburini; kwa maana wameingia tetemeko na ushangao; wala hawakumwambia mtu neno, maana waliogopa”.
Unaona? Na baadaye wakati wanarudi walitokewa na Bwana Yesu mwenyewe, wakamsujudia, na kupewa maagizo ya kwenda kuwaambia mitume wake yawapasayo kufanya (Soma Mathayo 28:1-10)
NI UJUMBE GANI TUNAFUNDISHWA?
Kuna wakati Yesu atakuwa hai anatambea, na pia kuna wakati Yesu atajifanya kama amekufa..Tunapaswa tuonyesha upendo wetu dhati, na wa hali na mali kwake nyakati zote, kwasababu zote zina thawabu zake kubwa.
Wapo wale wanawake walimtia Yesu marhamu wakati akiwa hai, na Kristo akawapa thawabu zao, lakini tunaona wanawake hawa wengine watatu nao walikuwa radhi hata kwenda kufukua kaburi la Yesu ili tu wautie mwili wake mafuta ya thamani, japokuwa walijua kuwa hakuna matumaini yoyote, masaa machache baadaye yatageuka kuwa harufu mbaya, kutokana na kuwa Bwana alikaribia kwenda kutoa harufu, lakini hawakujali, kutoa walichokuwa nacho maadamu ni kwa ajili ya Bwana wao waliyempenda walifanya hivyo kwa furaha tele, na matokeo yake walipofanya hivyo, walikuwa wa kwanza kabisa kutokewa na Bwana, na kupewa maagizo ya kuwapelekea wale wengine, ambao hawakujishughulisha na chochote.
Na sisi pia, kuna wakati tunaweza kuona kazi ya Mungu imekufa, au inakaribia kufa, au haina thamani sana machoni petu, pengine unaweza kuona hata kama ukiisaidia au kutoa msaada wako ni kama unapoteza nguvu zako tu, au mali zako tu.. Lakini katika mazingira kama hayo, wewe jitoe kwenye kazi ya Mungu, kama ni fedha peleka, kama ni nguvu zako zipeleke, kama ni utumishi wako uachie hapo, hata kama kutakuwa hakuna matumaini yoyote ya kazi hiyo kufanikiwa kwasasa.. Wewe mfanyie Kristo kwa moyo wako wote..
Na matokeo yake ni kuwa utakuwa wa kwanza kumwona Kristo aliyefufuka, katika kanisa lake. Na yeye ndiye atakayekupa ujumbe wa kuwapelekea wengine..Hiyo yote ni kwasababu ulimthamini hata angali akiwa maiti inayokaribia kuoza na kunuka.. Hivyo na yeye atakuthamini na kukujalia kumuona katika utukufu wa kufufuka kwake.
Hivyo ujumbe wa leo ni kuwa tunapoadhimisha, kufufuka kwa Kristo, tukumbuke kuwa waliomwona wa kwanza walikuwa ni wale wanawake watatu, Na kilichowafanya wamwone Yesu ni moyo wao ule wa kumtendea jambo bila kujali, kupotea kwa tumaini lao.
Injili kama hizi, zinazohubiriwa na wanawake wacha Mungu kama hawa, zinamatokeo makubwa sana rohoni, kama tutazizingatia katika maisha yetu ya ukristo.
Bwana akubariki sana.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, nakukaribisha katika kuyatafakari maandiko. Leo tutajifunza mbinu nyingine ambayo adui shetani anaitumia kuwapunguzia watu kasi ya kumtafuta Mungu.
Ni wazi kuwa kila mtu ana kiu ya kusikia sauti ya Mungu katika maisha yake, na ana kiu ya kujua ni nini kinamzunguka, ni hatari gani iliyopo sasa na iliyopo mbele yake. Na kutokana na wengi kukosa kufahamu ni namna gani wanaweza kuisikia sauti ya Mungu, wameishia kujikita kuishi kwa ndoto wanazoota, wakiamini kuwa kila ndoto wanayoota ni Mungu anazungumza nao.
Leo nataka nikuambie ndugu, ambaye pengine una kiu ya kutafuta kuisikia sauti ya Mungu katika maisha yako, nataka nikuambie sauti ya Mungu haipo katika ndoto unazoota kila siku, njia pekee ya kuisikia sauti ya Mungu si ndoto unazoota bali ni NENO LA MUNGU linalokaa ndani yako. Sauti ya Mungu ni Neno lake katika biblia na si ndoto!.
Si kila ndoto ni sauti ya Mungu kwako. Nyingi zinakuja kutokana na shughuli zako za kila siku na mambo yaliyoujaza moyo wako.
Kwa mfano kama maisha yako yamejaa kutazama filamu za kidunia, na kusikiliza miziki, basi ndoto zako zitajaa hayo mambo, kama moyo wako umeujaza kutukana na maisha ya anasa, na ndoto zako pia zitakuwa hivyo hivyo, kama maisha yako yamejaa kufanya shughuli nyingi kutwa kuchwa, basi na ndoto zako zitakuwa zinahusiana na hizo hizo shughuli unazozifanya..
Mhubiri 5:3 “Kwa maana ndoto huja kwa sababu ya shughuli nyingi;….”.
Sasa inapotokea mtu anaacha kulisoma Neno, na kuishi kwa ndoto zake, na kwamba kila anachoota anatafsiri kwamba ni ujumbe kutoka kwa Mungu, mtu namna hiyo ni rahisi sana kupotezwa na uongo wa shetani. Kwasababu ameacha kujua njia sahihi ya kuisikia sauti ya Mungu, na amekijita kwenye ndoto anazoota kila siku.
Sauti ya Mungu, ni Neno lake ndani ya biblia takatifu. Ukitaka kujua Mungu anataka kuzungumza nawe nini kwa wakati huu, au kwa wakati ujao, nenda kasome biblia, na utaisikia sauti ya Mungu kwa wakati huo..inakuambia nini, (Ni kweli Mungu anaweza kuzungumza na mtu kwa ndoto, lakini hiyo ni mara chache sana..ukilinganisha na jinsi anavyoweza kuzungumza na sisi kwa kupitia Neno lake).
Yusufu japokuwa alikuwa na kipawa hicho cha Mungu kuzungumza naye kwa ndoto, lakini biblia inarekodi mara tatu tu, katika maisha yake yote. Lakini leo utaona mtu kila ndoto anayoota kwake ni ujumbe kutoka kwa Mungu!!. Na huku kaisahau kabisa biblia, hafahamu chochote kuhusu maneno ya Mungu.
Ndugu, Kama unaishi kwa ndoto, (Na kwamba kila asubuhi unapoamka wewe ni kutafuta tafsiri ya ndoto yako kwa watumishi), fahamu kuwa upo mbali sana na sauti ya Mungu, na ndoto unazoota umepofushwa macho ukidhani kuwa Mungu anazungumza na wewe kila siku huko kwenye ndoto zako. Mifano wa sauti ya Mungu kwako na kwangu ni hii >>
Mathayo 5:21 “Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue, na mtu akiua, itampasa hukumu.
22 Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto”.
Mathayo 5:38 “Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho, na jino kwa jino;
Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili”.
Na..
Mathayo 5:43 “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako;
44 lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,
45 ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki”.
Hiyo ndio mifano ya sauti na maonyo ya Mungu kwetu, ambayo ipo moja kwa moja isiyo na mafumbo yoyote. Lakini tukizutumainia ndoto tunazoota kila siku, na kufikiri huo ndio mlango wa kwanza wa Mungu kuzungumza na sisi, tutakuwa tumepotea njia pakubwa sana.
Hivyo tusiishi kwa ndoto, bali kwa Neno la Mungu!
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp
Mada Nyinginezo:
Nini maana ya “Tumejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii”?
Nakusalimu katika jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo, karibu tuyatafakari maneno ya uzima, ambayo ndio chakula cha kweli kutupacho afya roho zetu.
Lipo jambo moja nataka tujifunze leo linalohusiana na utendaji kazi wa shetani pale anapopata nafasi ya kumwingia mtu. Katika biblia tunaona Yuda ndiye mtu wa kwanza aliyerekodiwa kwa uwazi kabisa kuingiliwa na shetani. Tunalisoma hilo katika
Luka 22:3 “Shetani akamwingia Yuda, aitwaye Iskariote, naye ni mmoja wa wale Thenashara.
4 Akaondoka, akaenda akasema na wakuu wa makuhani na majemadari, jinsi atakavyoweza kumtia mikononi mwao”.
Na matokeo ya yeye kuingiliwa kule na shetani ilipelekea kutiwa moyo mwingine na ibilisi ambao yeye mwenyewe hakuwa nao kabisa.. Na moyo wenyewe ulikuwa ni moyo wa kusaliti.
Yohana 13:1 “Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye ali amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo.
2 Hata wakati wa chakula cha jioni; naye Ibilisi amekwisha kumtia Yuda, mwana wa Simoni Iskariote, moyo wa kumsaliti;”
Sasa moyo kama huu ukishaingia ndani yako, huwa haujali kitu kingine chochote, huwa haufikirii kwamba huyu ni ndugu yangu, au huyu ni mama yangu, au huyu ni jirani yangu, au huyu ni mwenye haki,au nani n.k. wenyewe kazi yake ni kuvuruga, kuharibu, kusaliti, kuchinja kama sio kuua kabisa. Kwasababu si moyo wa mwanadamu tena unaofanya kazi ndani ya mtu bali ni moyo wa ibilisi mwenyewe ule wa kuasi.
Ndicho kilichomtokea Yuda, alipoingiwa na moyo huo, hakujali kuwa Yesu alimpenda Upeo kama tulivyosoma hapo juu, mpaka akamfanya kuwa msiri wake, na kumpa tonge lake alilolipenda yeye peke yake.. Lakini kinyume chake ni kuwa alimwinulia kisigino chake, akaenda kumsaliti kwa maadui zake, tena mbele ya macho yake kwa kumbusu. Usifikiri ule ulikuwa ni moyo wa Yuda.. Haukuwa moyo wake hata kidogo, na ndio maana baadaye shetani alipomwacha, alijuta sana na mwisho wa siku akaenda kujinyonga.
Zaburi 41:9 “Msiri wangu tena niliyemtumaini, Aliyekula chakula changu, Ameniinulia kisigino chake”
Moyo huu huu ndio utakaomwingia mpinga-Kristo siku ile ya mwisho, ambaye kazi yake itakuwa ni kuchinja tu wale wote ambao hawana ile chapa ya mnyama. Na baadaye itamtoka na kuyaendea mataifa ili kuleta vita duniani.
Ufunuo 16:13 “Nikaona roho tatu za uchafu zilizofanana na vyura, zikitoka katika kinywa cha yule joka, na katika kinywa cha yule mnyama, na katika kinywa cha yule nabii wa uongo.
14 Hizo ndizo roho za mashetani, zifanyazo ishara, zitokazo na kuwaendea wafalme wa ulimwengu wote kuwakusanya kwa vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi.
Leo hii unaona watu wanafanya mauaji makubwa ya kinyama, na kuchinja watu, au kuwatoa ndugu zao kafara usidhani ni mioyo yao inafanya hivyo. Hao ni watu ambao tayari walishamfungulia milango shetani tangu zamani ya kuwaingia, na matokeo yake shetani naye akawawekea mioyo mingine ndani yao, ambayo haijali utu tena, au haithamini kitu chochote, haijalishi itaonyeshwa upendo mkubwa kiasi gani.
Na kwa kawaida mwisho wa siku watu hawa huwa wanaishia katika majuto makubwa sana, pale ambapo wanajiona wameishia katika dhiki, au vifungo, au kukaribia kuuliwa, kutokana na makosa yao, wakati huo shetani ameshawaacha..ndipo wanaposhangaa ilikuwaje walijihusisha katika mambo kama hayo.
Mpaka mtu anafikia hatua ya kuzini zini ovyo hajali chochote, hajali huyu ni mke wa mtu, au mume wa mtu, hajali maradhi, hajali kuwa ni machukizo kwa Mungu, hata wakati mwingine anafanya hivyo na wanyama, au watu wa jinsia moja na yeye, huo ni moyo mwingine wa ibilisi umeshakwisha kuingia ndani yake. Na mwisho wa siku itakuwa ni majuto tu kwake.
Tukumbuke kuwa Yuda alikuwa ni mtume aliyechaguliwa na Yesu mwenyewe, lakini kwa uzembe wake, yalimkuta mambo kama yale, hiyo ni kutufundisha kuwa hata sisi tunaosema tumeokoka yanaweza kutukuta endapo tutakuwa ni watu wa kumpa ibilisi nafasi au upenyo ndani ya maisha yetu.
Tusidhani kuwa tukishafikia hatua hiyo itakuwa ni rahisi kumshinda ibilisi, hilo haliwezekani. Hivyo tuwe makini sana. Tukisema tumeokoka tumaanishe kweli kweli, Yuda alianza na tabia ndogo sana ya wizi, ambayo hakuna mtu aliyejua ingempelekea hata kusaliti na mwisho wa siku kujinyonga. Na sisi mambo madogo madogo tunayoyakumbatia hayo ndiyo yatakuwa upenyo wa ibilisi kutuingia na kuweka mioyo mingine ndani yetu.
Bwana atutie nguvu sote katika safari yetu hii ya wokovu.
Swali ni je, umemwamini Yesu? Je amekusafisha dhambi zako kwa damu yake?. Kama sivyo, unasubiri nini? Una habari kuwa hizi ni nyakati za mwisho? Na shetani naye analijua hilo na ndio maana anafanya kazi zake kwa bidii kukuingia mtu kama wewe mwenye mawazo mawili, kukutia moyo mwingine ndani yako, kwasababu anajua wakati alionao ni mchache?.
Ufunuo 12:12 “..Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu”.
Huu ni wakati wa kuamka katika usingizi wa mauti, na kumgeukia Kristo, na kumaanisha kweli kumfuata yeye, hivyo tubu dhambi zako kwa kumaanisha kabisa kuziacha, kisha kuwa tayari kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo ikiwa hukubatizwa hapo kabla. Na baada ya hapo Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu, atakayekulinda na kukuongoza katika kweli yote.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
SWALI: Biblia ina maana gani inaposema “Mwenye hekima huvuta roho za watu”?
JIBU: Tusome.
Mthali 11:30 “Mazao ya mwenye haki ni mti wa uzima; Na mwenye hekima huvuta roho za watu”
Zipo hekima nyingi, lakini hekima inayozungumziwa katika biblia ni hekima ya rohoni, ambayo ndiyo kuu kuliko hekima zote, ndio hekima aliyonayo Mungu mwenyewe. Sasa hapo aliposema mwenye hekima huvuta roho za watu, anamaanisha kuwa yeye anayewavuta watu kwa Mungu au watu wamjue Mungu, huyo anatambulika kama mtu mwenye hekima sana.
Hekima hii ilianza kuonekana kwa Bwana wetu Yesu Kristo, Kama tunavyojua yeye aliacha enzi na nguvu na mamlaka huko mbinguni akashuka hapa duniani kwa lengo moja tu, na kuturejeshea sisi ule uhusiano tuliokuwa tumeupoteza na Mungu, na ndio maana akawa radhi kuhubiri injili na kama hiyo haitoshi kuutoa uhai wake kwa ajili yetu.
Vivyo hivyo na sisi pia, tukisema tumeokoka, ni lazima tuwavute na wengine kwa Mungu, ili na wao pia waokoke kama sisi, Hapo ndipo tutatambulika na mbingu kuwa tuna hekima, lakini kama hatuonyesha bidii ya namna hiyo, haijalishi tutasema sisi ni wa rohoni kiasi gani, bado tutakuwa hatuna hekima, kwa mujibu wa maandiko.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp
Mada Nyinginezo:
Je kuna uthibitisho wowote wa kimaandiko kwamba kutakuwa na mateso baada ya kifo kwa wale watakaokufa katika dhambi?.
Jibu ni ndio.. Tusome,
Luka 16:22 “Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa.
23 Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, ALIPOKUWA KATIKA MATESO, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake.
24 Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu NINATESWA KATIKA MOTO HUU.
25 Ibrahimu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe UNAUMIZWA.”
Watu wote ambao watamkataa Yesu katika maisha haya, watakapokufa wataenda kuzimu kwenye mateso, watu wote wanaoliharibu hekalu la Roho Mtakatifu (yaani miili yao) kwa kuvaa vimini, nguo za utupu, zinazochora maungo yao, wanaopaka wanja, wanaopaka hina, wanaoweka kucha za bandia, na wigi ili wafanane na wanawake wa ulimwengu huu, biblia imesema, wote wataingia katika lile ziwa la moto.
Na biblia inazidi kusema kuwa kuzimu haishibi watu na wala haijai,.. ni kubwa kuliko hii dunia tunayoishi.
Mithali 27:20 “KUZIMU NA UHARIBIFU HAVISHIBI;….”.
Mithali 30:15 “……………Kuna vitu vitatu visivyoshiba kamwe, Naam, vinne visivyosema, Basi!
16 KUZIMU; na tumbo lisilozaa; Nchi isiyoshiba maji; na moto usiosema, Basi!“.
Kuzimu haishibi!!..Inapokea tu watu kila siku kila saa… Ipo nafasi kubwa mno kuzimu na watu wanaingia huko kila siku. Biblia haidanganyi.
Watu wote wanaofanya uasherati, na wanaopenda ulimwengu kuliko kumpenda Mungu, ikiwemo kutazama filamu za kidunia, na tamthilia za kidunia, wote wataenda katika ziwa la moto kama hawatatubu na kuacha njia zao mbaya, hiyo ni kulingana na Neno la Mungu.
Wote wanaocheza kamari, ikiwemo kubeti, na michezo yote ya bahati nasibu. Wakifa katika hiyo hali wataenda kuzimu.
Watu wote wanaoishi na wanawake/wanaume ambao si wake zao/waume zao, na wote wanaotazama picha za utupu katika mitandao, na wanaojichua, na walawiti wote.. hao wakifa sehemu yao itakuwa ni katika lile ziwa la moto, hiyo ni kulinga na Neno la Mungu.
Na wote watakaoingia kuzimu, hakuna mlango wa kurudi tena au kutoka huko, wakiwa katika mateso huko kuzimu watatamani kutubu lakini itakuwa wameshachelewa, watalia lakini hakuna atakayesikia, mateso yao yatakuwa makali usiku na mchana, watakuwa tu katika hali ya majuto, wakijutia kiburi chao, uchafu wao waliokuwa wanaufanya kwa siri au kwa wazi, uasherati wao waliokuwa wanaufanya bila hofu, ulevi wao waliokuwa wanaufanya kila siku, anasa zao N.k
Kwa uchungu na mateso mengi wakiwa huko, watajigundua kuwa shetani alikuwa amewapofusha macho na hivyo watamchukia shetani kwa ukomo wa chuki, lakini watakuwa wameshachelewa, wangepaswa wafanye hivyo kabla hawajaingia huko.
Ndugu hakuna maombi yoyote yanayopanda kutoka kuzimu kwenda kwa Mungu, hakuna kilio chochote kinachotoka kuzimu na kwenda kwa Mungu, wala hakuna utukufu wowote wa Mungu unaotoka kuzimu, hivyo Mungu hasikii kilio cha watu wanaolia kuzimu, wala kelele zao hazimfikii, wala sifa zao kwa Mungu, hakuna mtandao kati ya kuzimu na mbingu. Walioingia huko ndio wamesahaulika hivyo.
Isaya 38:18 “Kwa kuwa kuzimu hakuwezi kukusifu; mauti haiwezi kukuadhimisha; Wale washukao shimoni hawawezi kuitarajia kweli yako. 19 Aliye hai, naam, aliye hai, ndiye atakayekusifu..”
Zaburi 6:5 “Maana mautini hapana kumbukumbu lako; Katika kuzimu ni nani atakayekushukuru?”
Shetani kanyanyua mahubiri, yanayosema kuwa kuna tumaini baada ya kifo, yaani wale watu waliokufa katika dhambi na kuingia kuzimu, wanaweza kutolewa kutoka katika hayo mateso na kuingia peponi, kwasababu Mungu anasikia mateso yao na maumivu yao huko.. USIDANGANYIKE!!. Hakuna nafasi ya pili baada ya kifo, wala hakuna mageuzi wala mashauri kuzimu!!.. Wala hatuwezi kumwombea mtu aliyeshuka kuzimu, wala kumshauri Mungu juu ya hao waliopo kuzimu.
Mhubiri 9:10 “ Lo lote mkono wako utakalolipata kulifanya, ulifanye kwa nguvu zako; kwa kuwa hakuna kazi, wala shauri, wala maarifa, wala hekima, HUKO KUZIMU UENDAKO WEWE”.
Kaka/Dada unayesoma huu ujumbe, Iepuke kuzimu! Kwasababu kuzimu ipo kweli, sio nadharia, ni kitu halisi kabisa. Na mtu akishuka huko hatatoka tena milele, na ndilo lengo kubwa la shetani, hataki kwenda mwenyewe kwenye moto wa milele, anataka kwenda na wengi.
Hivyo tusiruhusu hilo, aende peke yake na mapepo yake… Leo hii unapoisikia hii sauti nenda kachome hivyo vimini, na nguo zote za kikahaba, ikiwemo suruali, tupa hayo mawigi na mahereni unayovaa (mwili wako ni hekalu la Roho Mtakatifu).. usiangalie ni kundi kubwa kiasi gani linakiuka Neno la Mungu. Kuzimu utashuka peke yako, wala hutakuwa na jopo kubwa la watu, kama hutatubu. Wale funza wa kuzimu, ambao Bwana Yesu alisema hawafi watakutesa kule kuzimu usiku na mchana, na utalia wala sauti yako haitasikika popote, utakuwa peke yako, katikati ya giza nene, ukiungua tu, kwenye moto usiozimika.
Siku hiyo utasema heri ningesikia na kutubu, nisingekuwepo huku..lakini haitasaidia chochote.
Hivyo geuka leo na kutubu kwa vitendo, hiyo miziki unayoisikiliza ya kidunia itakupeleka kuzimu, futa yote leo katika simu yako, na itoe katika nyumba yako, hizo filamu acha kuzitazama kuanzia muda huu, haijalishi zinapendwa na kusifiwa na wangapi. Kuanzia leo anza kumfuata Yesu kwa kumaanisha, na wala usiwe mshabiki wa Kristo, bali uwe mfuasi wake.
Kama umeamua kumfuata Yesu leo kwa kutubu, na kudhamiria kuacha vyote.. Bali uamuzi huo ni bora kuliko kitu kingine chochote ambacho ungeweza kukifanya, hivyo ili usirudi tena nyuma na uukulie wokovu, hakikisha unakishikilia kile ulicho nacho kwa bidii sana, kwa kusoma Neno la Mungu kwa bidii, na kutafuta kuzijua habari zake kwa bidii, mahali popote pale anapohubiriwa.
Na pia ili kuukamilisha wokovu wako, ni lazima ukabatizwe ubatizo sahihi kama bado hujabatizwa, Ubatizo sahihi ni ule wa maji mengi (Yohana 3:23), na kwa jina la YESU KRISTO, ambalo ndio jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu kulingana na Matendo 2:38, Matendo 8:16, na Matendo 19:5, kwaajili ya ondoleo la dhambi.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Je! kuna maombi yoyote ya kumtoa mtu aliyekufa kwenye mateso ya kuzimu?