SWALI: Nini maana ya huu mstari?
Mithali 22:2
[2]Tajiri na maskini hukutana pamoja; BWANA ndiye aliyewaumba wote wawili.
JIBU: Pamoja na kwamba kutakuwa na kutokuelewana baina ya makundi haya ya watu..Maskini atamwonea wivu tajiri, na tajiri atamdharau maskini..Lakini katika hayo yote bado tu kila mmoja atamhitaji mwenzake…atakutana na mwenzake mahali fulani tu katika maisha..
Maskini atamfuata tajiri ampe kazi, vilevile tajiri atamtegemea maskini amwoshee gari lake, amfulie nguo zake, amlimie bustani yake.n.k Hivyo kila mahali uendapo makundi yote utayapata .. Na sababu tayari biblia imeshaitoa..”Kwamba Bwana ndiye aliyewaumba wote wawili”Akawaweka hapa duniani..wala mmoja hakumweka mawinguni, mwingine ardhini.
Hii ni kufunua kuwa tumewekwa kusaidiana, wala hakuna mtu anaweza kujikidhi yeye mwenyewe kwa kile alichonacho pasipo mwingine..zaidi sana yule ambaye unamwona hakufai ndiye atakayekufaa sana wakati fulani. Kwasababu ni Mungu ndiye aliyetuumba sote, mmoja hakuumbwa na shetani, na mwingine Mungu.
Hivyo hekima inatufundisha tukae kwa utulivu, tuthaminiane sisi kwa sisi
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
KWA KUWA WASEMA MIMI NI TAJIRI.
Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.
Azidishaye mali yake kwa riba, Humkusanyia mtu awahurumiaye maskini.
JE! NINAWEZA KUPOTEZA FURAHA YA WOKOVU?
Mimi ni mweusi-mweusi, lakini ninao uzuri.
Swali: Katika 1Petro 2:13 Tumeambiwa tutii kila kitu tunachoamriwa na wafalme, lakini katika Matendo 5:29, tunaona Petro huyo huyo hawatii wenye mamlaka, anasema imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu..Je hapo panakaaje?
Jibu:Tusome
1 Petro 2:13 “Tiini kila kiamriwacho na watu, kwa ajili ya Bwana; ikiwa ni mfalme, kama mwenye cheo kikubwa;
14 ikiwa ni wakubwa, kama wanaotumwa naye ili kuwalipiza kisasi watenda mabaya na kuwasifu watenda mema”
Tusome tena…
Matendo 5:29 “Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu”.
Ni kweli tumeamriwa kutii mambo yote, lakini si hata yale yasiyofaa. Kwamfano inatokea mkuu wa nchi au mwenye mamlaka anatoa amri ya watu kuabudu kitu fulani ambacho si Mungu wa mbingu na nchi (yaani Yehova).. Hapo hatuwezi kumtii, kwasababu kavuka mipaka, au mkuu anatoa amri hakuna kuhubiri injili, au kuomba au kufunga, hapo tumepewa ruhusa ya kutotii maagizo yake hayo.
Lakini mambo mengine, ambayo hayaathiri imani yetu, hayo hatuna budi kutii..
Kwamfano sheria imetolewa na wakuu wa nchi kuwa siku fulani itakuwa ni siku ya usafi nchi nzima, kwamba watu wote watoke wafanye usafi, hapo hatuna budi kutii, kwasababu jambo hilo haliathiri imani yetu, na zaidi sana litatuongezea ushuhuda mzuri katika jamii na linafaa kwa afya zetu. Na sheria nyingine zote mfano wa hizo, hatuna budi kuzitii.
Lakini ikitoka sheria ya kutukataza kumwabudu Mungu, au sheria ya kutulazimisha kufanya mabaya, sheria hiyo tumepewa ruhusa ya kuivunja, na tukawa hatujafanya dhambi, bali kinyume chake tukawa tumempendeza Mungu.
Ndio maana Petro ijapokuwa alilihubiri suala hilo la kuwatii wenye mamlaka, (Katika hiyo 1Petro 2:13) lakini ilipofika wakati hao wenye mamlaka walipowakataza wasihubiri habari njema za ufalme wa mbinguni… Petro na Yohana hawakukubaliana na hiyo sheria..ndipo wakasema imewapasa kumtii Mungu kuliko wanadamu, wakisaidiwa na Malaika wa Mungu.
Matendo ya Mitume 5:18 “wakawakamata mitume wakawaweka ndani ya gereza;
19 lakini malaika wa Bwana akafungua milango ya gereza usiku, akawatoa, akasema
20 Enendeni mkasimame hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya Uzima huu.
21 Nao waliposikia wakaenda alfajiri hekaluni, wakaanza kufundisha. Akaja Kuhani Mkuu nao waliokuwa pamoja naye, wakawakutanisha watu wa baraza, na wazee wote wa wana wa Israeli, wakatuma watu gerezani ili wawalete.
25 Mtu mmoja akaja akawapasha habari ya kwamba, Watu wale mliowaweka gerezani wako ndani ya hekalu, wamesimama wakiwafundisha watu.
26 Ndipo yule jemadari akaenda pamoja na watumishi, wakawaleta, lakini si kwa nguvu, kwa maana waliogopa watu wasije wakawapiga kwa mawe.
27 Walipowaleta, wakawaweka katika baraza. Kuhani Mkuu akawauliza,
28 akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu.
29 Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu”.
Na sio tu kwa wafalme na wenye mamlaka, tuliopewa ruhusa ya kuvunja amri zao zilizozidi mipaka, bali hata katika familia..endapo Mume katoa sheria ya mke au watoto kuabudu miungu, hapo tumepewa ruhusa ya kutomtii mzazi huyo au mume kwa agizo hilo..Kwasababu ni agizo lililovuka mipaka..
Mathayo 10:37 “Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili”.
Lakini mume akitoa amri au sheria ambazo haziathiri imani zetu, hizo hatuna budi kuzitii, mfano mzazi anatoa amri ya kufanya shughuli fulani ya nyumbani iliyo halali hapo hatuna budi kutii hata kama hatutaki..
Kwahiyo kwa ufupi tumepewa amri ya kutii yote yaliyo mema lakini hatujapewa amri ya kutii mambo mabaya. Lakini yote hatuna budi kuyafanya kwa hekima.
Bwana atusaidie.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312.
Mada Nyinginezo:
JE NI KUTII AU KUPATA KWANZA MAARIFA?
NINI TOFAUTI KATI YA MATENDO YA SHERIA NA MATENDO YA IMANI?
SWALI: Je! maneno tunayoyasoma katika Mhubiri 7:24, yana maana gani?
[24]Mambo yale yaliyo mbali, na yale yaendayo chini sana, ni mtu yupi awezaye kuyatafuta?
JIBU: Hapo Kuna vitu viwili..
1) Yale yaliyo mbali.
2) Yale yaendayo chini sana.
Akimaanisha yaendayo mbali na upeo wa mwanadamu..na hayo si mengine zaidi ya mambo ya mbinguni, na kuzimu na ya maisha baada ya hapa..yatakuwa na mwonekano gani..picha yake halisi ipoje, miaka bilioni moja kutoka sasa watakatifu watakuwa wanafanya nini?..Hayo hakuna mtu anayeweza kuyavumbua isipokuwa Mungu tu peke yake.
Na yale yaendayo chini sana, maana yake ni yale yaliyositirika kama madini n.k. ambayo yenyewe yanapatikana chini sana. Hivyo vitu vilivyositirika/ siri za Mungu, ni mwanadamu gani anaweza kuzivumbua..
Kwamfano Siku ya unyakuo itakuwa lini, kabla ya uumbaji Mungu alikuwa anafanya nini, maji yanajaaje kwenye mawingu, yaliyo hewa tu, halafu baadaye yanamwagika chini kama mvua, mifupa unajiumbaje ndani ya tumbo la mama mjamzito, mapigo ya moyo yanadundishwa kwa nishati gani, mpaka hayachoki n.k Siri hizo anazo Mungu tu hakuna awezaye kuzivumbua..
Ayubu 11:7 inasema..
[7]Je! Wewe waweza kuuvumbua ukuu wa Mungu? Waweza kuufikilia upeo wa huyo Mwenyezi?
Soma Kitabu cha Ayubu kuanzia sura ya 38-41, utaona Mungu anamuuliza mwanadamu maswali magumu ambayo mpaka sasa hakuna hata moja lililopatiwa jibu lake.
Hiyo ndio maana ya huo mstari;
Mhubiri 7:24
[24]Mambo yale yaliyo mbali, na yale yaendayo chini sana, ni mtu yupi awezaye kuyatafuta?
Yatosha sisi kumwamini yeye na kulitii Neno lake tu. Kwasababu hata tukijitahidi vipi kwa akili zetu kamwe hatutaweza kuzivumbua siri za ndani za Mungu wetu, isipokuwa yeye mwenyewe atufunulie.
Jina lake BWANA lihimidiwe. milele na milele. Amen.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Birika ni nini?, na yale Matao matano katika birika la Bethzatha ni nini?.
MUME / MKE BORA KUTOKA KWA BWANA UTAMWONA UKIWA KATIKA MAZINGIRA GANI?
nini maana ya kujikana nafsi na kujitwika msalaba?
HUJAPEWA MBAWA ZA KUKIMBIA MATATIZO
Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze na kuyatafakari maandiko pamoja.
Leo napenda tujifunze juu ya lile tukio maarufu lililotokea siku ile ya Pentekoste, ambapo tunasoma Roho Mtakatifu alishuka juu ya Wanafunzi wa Bwana Yesu 11, pamoja na wanafunzi wengine wengi, jumla yao ni watu 120 (Matendo 1:15).
Ilipotimia siku ya Pentekoste tunasoma kuwa Watu wote walishukiwa na “Ndimi zilizogawanyikana kama ndimi za moto”.
Matendo 2:1 “Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja.
2 Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi.
3 Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao”
Napenda tuyafakari hayo maneno kabla hatujaendelea mbele.
Neno la Kwanza ni “Ndimi”.. Ndimi ni wingi wa neno “ulimi”, Na mtu anapozungumzia Ulimi, anamaanisha “lugha”... Kwamfano tukitaafsiri neno “lugha mama” kwenda kwenye lugha ya kiingereza itakuwa ni “Mother tongue” na tafsiri ya “tongue” kwa Kiswahili ni “ulimi”.. Hivyo badala ya kusema “lugha mama” pia ni sahihi kusema “ulimi mama” (ni kitu kimoja).
Kwahiyo hapo biblia iliposema kuwa zilitokea “ndimi za moto” ilimaanisha kuwa ni “lugha za moto”.. Lakini haiishi hapo, biblia inaendelea kusema kuwa “zilikuwa ni ndimi zilizogawanyikana” maana yake ni kuwa zilikuwa ni “lugha zilizogawanyikana/tofautitofauti”.. kila mmoja alishukiwa na lugha yake tofauti na ya mwenzake.. Na lugha hizo hazikuwa za kimbinguni, bali za duniani kama vile Kiswahili, kiarabu, kihindi, kichina, kisukuma n.k
Matendo 2:4 “Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.
5 Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu.
6 Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe.
7 Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya?
8 Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo?
9 Warparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia, 10 Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu,
11 Wakrete na Waarabu; TUNAWASIKIA HAWA WAKISEMA KWA LUGHA ZETU MATENDO MAKUU YA MUNGU.
12 Wakashangaa wote wakaingiwa na shaka, wakiambiana, Maana yake nini mambo haya?
Mstari wa 11, biblia inasema… “TUNAWASIKIA HAWA WAKISEMA KWA LUGHA ZETU MATENDO MAKUU YA MUNGU”.
Kumbe Wanafunzi hawa waliojazwa Roho Mtakatifu, walikuwa wananena matendo makuu ya Mungu.. Kumbe walisikika wakiyatangaza matendo makuu ya Mungu, na si mambo mengine..
Sasa mfano wa matendo hayo ni yapi?
Ndio kama yale ya Mungu kupasua bahari na wana wa Israeli kupita salama, ndio kama yale ya Mana kushushwa kutoka mbinguni kwa miaka 40, ndio kama yale ya Bwana kuziangusha kuta za Yeriko, ndio kama yale ya Eliya kushusha moto n.k n.K (Hayo ndio matendo ambayo mitume walisikika wakiyatangaza kwa lugha nyingine)…Na watu waliposikia wakikumbushwa matendo makuu hayo ya Mungu, tena kwa lugha za ndani kabisa..mioyo yao iliwaka, kutaka kumrudia Mungu na kutaka kujua zaidi.
Hebu tengeneza picha unamwona mzungu aliyetoka Ulaya anazungumza lugha yako ya kikabila tena ile ya ndani kabisa, ambayo hata wewe pengine huipati vizuri, na ukizingatia yeye ni mgeni kabisa, na hajawahi kufika huko kijijini kwenu.. halafu maneno anayoyasema ni ya kumtukuza Mungu, kwa matendo makuu aliyoyafanya katika biblia.
Bila shaka utaduwaa na kushangaa!! Na kujiuliza maswali mengi, na jibu la mwisho utakalolipata ni kusema “huu ni muujiza” na zaidi sana hata kile mzungu huyo anachokisema kitakuja kwa uzito kwako, tofauti na kama angeongea kwa lugha yake ile ile ya kiingereza.
Ndicho kilichotokea siku ya Pentekoste, wanafunzi walisikika wakimtangaza Mungu kwa lugha mbalimbali, hivyo watu wakashangaa na kutenga muda kuwasikiliza, na siku hiyo wakaongezeka waongofu elfu 3.
Na sisi hatuna budi wakati mwingine, tuzungumze kwa lugha nyingine.. Kuzungumza kwa lugha nyingine si lazima kuwe kwa lugha ambayo huijui!, hapana! Hata kwa lugha yako hiyo hiyo lakini Bwana aibadilishe itoke kwa namna nyingine, ambayo italeta mageuzi kwa wale watakaokusikiliza.
Na si lazima kuwe kunena tu, bali hata KUIMBA, Bwana akabadilishe lugha na sauti yako iwe na uvuvio wa Roho ambao utawabadilisha watu wasikiao, na si katika kuimba tu, bali hata katika KUOMBA!. Bwana akabadili lugha yako, na kuwa lugha nyingine kusudi maombi yakolee munyu, mbele zake.
1Wakorintho 14:15 “Imekuwaje, basi? Nitaomba kwa roho, tena nitaomba kwa akili pia; mtaimba kwa roho, tena nitaimba kwa akili pia”.
Na si katika kuomba, na kuimba tu, bali hata katika MAISHA YETU YA KAWAIDA YA MAZUNGUMZO. Lugha zetu zinapaswa zibadilishwe.
Tukiwa watu wa lugha mbaya, maandiko yanasema tunaziharibu tabia zetu njema !(1Wakorintho 15:33). Na lugha mbaya ndizo zinazotukosesha kibali, lakini kauli mbaya huuwasha moto (Yakobo 3:6).
Siku ya leo ni siku ya kuomba BWANA AIBADILISHE LUGHA YAKO..Na kuwa lugha nyingine ya kuwafaa watu na kufaa mbele za Mungu.
Ikiwa bado hujaokoka, Bwana Yesu hawezi kuibadilisha lugha yako.. lakini leo hii ukiamua kumpokea Yesu maishani mwako kwa kumaanisha kabisa kwa dhati, basi Bwana atakupa lugha mpya.. Na hivyo utakuwa mtu mwingine wa kuzaa matunda siku zote..
Basi ikiwa umeshampokea Yesu, au leo hii umeshafanya maamuzi ya kumpokea Yesu na kutubu dhambi zako, basi pata muda jitenge binafsi mahali pa utulivu, na kisha piga magoti kwa utulivu na uombe na mwombe Bwana akupe kipawa hicho cha lugha mpya, naye ni mwaminifu atakupa, na tangu siku hiyo utaona mabadiliko makubwa sana katika maisha yako..
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?
Je Mungu ana njia ngapi za kuzungumza?
NINI TOFAUTI KATI YA MATENDO YA SHERIA NA MATENDO YA IMANI?
IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.
Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo, ni wasaa mwingine tena Bwana ametupa neema ya kuutafuta uso wake. Karibu tujifunze Neno la Mungu.
Lipo funzo kubwa sana Bwana anatufundisha nyuma ya wale malaika wake wawili aliowatuma sodoma kwa ajili ya kuuangamiza ule mji. Habari tunaifahamu, hakuna haja ya kulitazama tukio lote, lakini tutatazama huduma yao ya mwisho ambayo waliifanya kwa familia ya Lutu.. Hiyo itatufanya na sisi leo hii tuwe makini sana na hii neema ya Mungu tuliyopewa kwa kitambo.
Malaika wale walipomwambia Lutu atoke sodoma, maandiko yanasema, Lutu akawa ‘anakawia kawia’,..Hata baada ya “kuhimizwa sana” bado akawa anakawia kawia..hapo ndipo ikabidi wale malaika wachukue jukumu wenyewe la kuwatoa kwa nguvu sodoma, kana kwamba ndio wao wenye shida. Tusome;
Mwanzo 19:15 Hata alfajiri ndipo malaika WAKAMHIMIZA LUTU, wakisema, Ondoka, mtwae mkeo na binti zako wawili waliopo hapa, usipotee katika maovu ya mji huu. 16 AKAKAWIA-KAWIA; nao wale watu wakamshika mkono, na mkono wa mkewe, na mkono wa binti zake wawili, kwa jinsi Bwana ALIVYOMHURUMIA, wakamtoa wakamweka nje ya mji..
Biblia inatuambia Kwa jinsi Mungu ‘alivyomhurumia’ Lutu na familia yake, ikampelekea amtoe kwa nguvu kama katoto kanacholazimishwa kupelekwa shuleni kwa kubembelezwa.. Hivyo waliendelea kuvutwa kwa umbali mrefu kidogo.. Lutu na mke wake wakashikwa na malaika mmoja, halikadhalika mabinti zake wawili wakashikwa na malaika mwingine.. Wakati wanatembea Walikuwa wanaweza kuangalia nyuma kama watakavyo na wasiambiwe kitu. Pengine walifika mahali wakawa wanasema tumechoka, wanabembelezwa watembee tu hivyo hivyo, wanafarijiwa, wanatiwa nguvu, Kwani jukumu la wao kuokolewa halikuwa katika uwezo wa mikono yao, bali wa wale malaika wawili.
Lakini hali hiyo haikuendelea sana… biblia inatuambia, walipofika nje tu kidogo ya mji..Wakaachwa, na kuambiwa zamu hii, sasa kipengele kilichobakia ni juu yao wenyewe..sisi tumemaliza kazi yetu.
Mwanzo 19:17 “Ikawa walipomtoa nje, mmoja alisema, Jiponye nafsi yako usitazame nyuma, wala usisimame katika hilo bonde po pote; ujiponye mlimani, usije ukapotea”.
Ndipo safari ya kukimbia, ikaanza..Lakini mkewe lutu, akidhani wakati huu ni kama ule wa mwanzo akageuka nyuma akidhani watakuwepo malaika tena wa kumshika mkono,na kumvuta vuta, na kumbembeleza bembeleza kama mwanzoni.. saa ile ile akageuka kuwa jiwe la chumvi.
Maana yake ni nini?
Saa tunayoishi ni wakati ambao sio tena kubembelezewa wokovu kama ilivyokuwa miaka ya kale.. Bali tunaishi ukingoni sana mwa neema ya wokovu. Wakati ambapo tunapaswa tujiokoe nafsi zetu na huu ulimwengu mbovu unaokaribia kuisha.. Pengine utasema umejuaje tupo katika zama hizo za kujiokoa nafsi zetu wenyewe, zama za kukimbia bila kuangalia nyuma, na sio za kuvutwa na Mungu? ,..Ni kutokana na kauli ya Bwana Yesu mwenyewe aliyoisema katika vifungu hivi;
Luka 17:32 “Mkumbukeni mkewe Lutu. 33 Mtu ye yote atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; na ye yote atakayeiangamiza ataiponya”.
Maana yake ni kuwa hakuna kusubiria tena, Mungu akuambie hivi, au akuambie vile, au akufanyie hiki kwanza au kile.. Tayari alishasema na wewe kwamba usiangalie nyuma, kuna kuna kuwa jiwe la chumvi..jiokoe nafsi yako. Hivyo unapokuwa mkristo vuguvugu, unakapokuwa mkristo-jina, ujue upo hatarini sana wakati huu.. unyakuo ukipita leo au ukifa katika hali hiyo usidhani kwamba utakuwa na nafasi ya pili.
Mlango wa neema unakaribia kufungwa kwa watu wa mataifa, na hivi karibuni Yesu anarudi, dalili zote zinaonyesha huwenda kizazi tunachoishi tutayashuhudia yote. Sasa ya nini kuendelea kuufanyia mzaha wokovu,..Yanini kuendelea kuupenda ulimwengu? Ya nini kushikamana na mambo ya sodoma kama mke wa Lutu…
Usipoupokea wokovu wa kweli leo, ujue kesho itakuwa ngumu sana kwako, kuliko siku moja nyuma. Kwasababu neema ya Mungu haidumu milele kwa mwenye dhambi..litambue hilo!
Luka 13:24 “Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze.
25 Wakati mwenye nyumba atakaposimama na kuufunga mlango, nanyi mkaanza kusimama nje na kuubisha mlango, mkisema, Ee Bwana, tufungulie; yeye atajibu na kuwaambia, Siwajui mtokako;
26 ndipo mtakapoanza kusema, Tulikula na kunywa mbele yako, nawe ulifundisha katika njia zetu.
27 Naye atasema, Nawaambia, Siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu.
28 Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno, mtakapomwona Ibrahimu na Isaka na Yakobo na manabii wote katika ufalme wa Mungu, nanyi wenyewe mmetupwa nje.
29 Nao watakuja watu toka mashariki na magharibi, na toka kaskazini na kusini, nao wataketi chakulani katika ufalme wa Mungu”.
Isikize sauti ya Mungu..ikuambiayo jiokoe nafsi yako, mkumbuke mke wa Lutu.
Nyakati zetu ni za hatari sana kuliko nyakati za kale.
Bwana atusaidie.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
JINSI SODOMA NA GOMORA ILIVYOKUWA INAVUTIA SANA.
Roho, Nafsi, na Mwili vina utofauti gani?
Ni SIRI gani Paulo aliyokuwa anaimaanisha katika Waefeso 5:32?
Sefania 3:8 “Basi ningojeni, asema Bwana, hata siku ile nitakapoondoka kuteka mateka; maana nimeazimia kuwakusanya mataifa, ili nizikutanishe falme, nipate kuwamwagia ghadhabu yangu; naam, ukali wote wa hasira yangu; kwa maana dunia yote itateketezwa kwa moto wa wivu wangu”.
Majira yaliyopo mbele yetu, si rafiki kabisa ndugu yangu, bali ni majira ya vita. Fahamu kuwa hii dunia haitaisha katika amani..Vipo vita vikubwa na vibaya vinavyokuja mbele yetu… Hilo haliepukiki kwasababu biblia ilishatabiri. Na sasa zipo vita kuu mbili(2), ambazo zitapiganwa kinyume na Mungu kabla ya huu ulimwengu kuisha..
Tukisema ‘kinyume na Mungu’ Tunamaanisha kinyume na Israeli, kwasababu Mungu yupo katika taifa lake Israeli..Ndilo taifa pekee Mungu aliloliunda kwa lengo la kuyabariki mataifa na pia kwa lengo la kuyakomesha mataifa.
Vita ya kwanza itakuwa ni ile tunayoisoma katika kitabu cha Ezekieli 38&40, Hii itapiganwa kipindi kifupi sana kabla ya unyakuo, au kipindi kifupi sana baada ya unyakuo. Kwaufupi ni kwamba taifa hili la Urusi, ndilo litakalosimama kama kichwa cha vita hiyo, likiyaongoza na mataifa mengine machache ya kando kando ,lakini litapigwa na habari yao itakuwa imeishia hapo. Ikiwa utataka kupata maelezo zaidi kuhusiana na vita hii tutumie ujumbe inbox (+255693036618 / +255789001312), tukutumie somo lake.
Lakini vita nyingine, ni vita ijulikanayo kama vita ya Harmagedoni.. Hii haitakuwa tena ya mataifa machache tu..Hapana, bali itahusisha mataifa yote duniani. Yataungana, yakiwa na lengo moja la kuifuta Israeli katika uso wa dunia..Na sababu ambayo itapelekea ni kwamba Mungu ataitumia Israeli, kuyaudhi mataifa haya..aidha kwa kupitia manabii atakaowanyanyua, au kwa kupitia watawala watakaokuwepo. Na itapiganwa mwishoni kabisa mwa ulimwengu.
Zekaria 12:2 “Angalia, mimi nitafanya Yerusalemu kuwa kikombe cha kuyumba-yumba kwa watu wa kabila zote, wazungukao pande zote; tena kitakuwa juu ya Yuda pia wakati wa kuhusuriwa Yerusalemu.
3 Tena itakuwa siku hiyo, nitafanya Yerusalemu kuwa jiwe la kuwalemea watu wa kabila zote; wote watakaojitwika jiwe hilo watapata jeraha nyingi; na mataifa yote ya dunia watakusanyika pamoja juu yake”.
Hata taifa lako unaloishi wewe litahusika wakati huo, watakuwa wamejiandaa na mabomu yao ya nyuklia na majeshi, ili kwenda kuisambaratisha nchi ile ndogo. Wakati huo Israeli wakiwa wanyonge, na wamezingirwa na majeshi, Ndipo Kristo mkombozi wao atakapotokea mawinguni. Na atashuka katika ule mlima wa Mizeituni, na kuanzia hapo, atafanya vita ya kuyateketeza mataifa yote ulimwenguni..halitasalia hata moja litakalokosa kunywa kikombe hicho cha ghadhabu ya Mungu.
Pitia kwa utulivu maandiko haya;
Ufunuo 19:11 “Kisha nikaziona mbingu zimefunuka, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda, aitwaye Mwaminifu na Wa-kweli, naye kwa haki ahukumu na kufanya vita.
12 Na macho yake yalikuwa kama mwali wa moto, na juu ya kichwa chake vilemba vingi; naye ana jina lililoandikwa, asilolijua mtu ila yeye mwenyewe.
13 Naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa, Neno la Mungu.
14 Na majeshi yaliyo mbinguni wakamfuata, wamepanda farasi weupe na kuvikwa kitani nzuri, nyeupe, safi.
15 Na upanga mkali hutoka kinywani mwake ili awapige mataifa kwa huo. Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, naye anakanyaga shinikizo la mvinyo ya ghadhabu ya hasira ya Mungu Mwenyezi.
16 Naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, MFALME WA WAFALME, NA Bwana WA MABwana.
17 Kisha nikaona malaika mmoja amesimama katika jua; akalia kwa sauti kuu, akiwaambia ndege wote warukao katikati ya mbingu, Njoni mkutane kwa karamu ya Mungu iliyo kuu;
18 mpate kula nyama ya wafalme, na nyama ya majemadari, na nyama ya watu hodari, na nyama ya farasi na ya watu wawapandao, na nyama ya watu wote, waungwana kwa watumwa, wadogo kwa wakubwa.
19 Kisha nikamwona huyo mnyama, na wafalme wa nchi, na majeshi yao, wamekutana kufanya vita na yeye aketiye juu ya farasi yule, tena na majeshi yake”.
Pitia tena hili andiko, uone Kristo atakavyoshuka juu ya mlima wa mizeituni na kuanza maangamizi kwa watu waovu.
Zekaria 14:2 “Kwa maana nitawakusanya mataifa yote walete vita juu ya Yerusalemu; na huo mji utapigwa, nazo nyumba zitatekwa, nao wanawake watatendwa jeuri; na nusu ya watu wa mji watatoka kwenda utumwani; ila mabaki ya watu wa mji hawatakatiliwa mbali.
3 Hapo ndipo atakapotokea Bwana, naye atapigana na mataifa hayo, kama vile alipopigana zamani siku ya vita.
4 Na siku hiyo miguu yake itasimama juu ya mlima wa Mizeituni, unaoelekea Yerusalemu upande wa mashariki, nao mlima wa Mizeituni utapasuka katikati yake, upande wa mashariki na upande wa magharibi; litakuwako huko bonde kubwa sana; na nusu ya mlima ule utaondoka kwenda upande wa kaskazini, na nusu yake itaondoka kwenda upande wa kusini”.
Hapa ndipo utakapokuwa mwisho wa mataifa yote ulimwenguni.
Leo hii umeshaanza kuona ni jinsi gani, dunia inavyopata shida kwa taifa la Israeli?. Taifa hili kwasasa lina maadui wengi kuliko marafiki, limeshaonekana kama taifa asi la dunia. Na hapo Bwana hajalirudia taifa hili. Utafika wakati, hii neema itaisha kwetu sisi mataifa, ndipo watakapogeukiwa wao, na watatubu, kwa makosa waliyoyafanya ya kumsulubisha Bwana wao..
Soma..
Zekaria 12:9 “Hata itakuwa siku hiyo, ya kwamba nitatafuta kuwaangamiza mataifa yote watakaokuja kupigana na Yerusalemu.
10 Nami nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, roho ya neema na kuomba; NAO WATAMTAZAMA YEYE AMBAYE WALIMCHOMA; nao watamwombolezea, kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao wataona uchungu kwa ajili yake, kama vile mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya mzaliwa wake wa kwanza.
11 Siku hiyo kutakuwa na maombolezo makuu huko Yerusalemu, kama maombolezo ya Hadadrimoni katika bonde la Megido.
12 Nayo nchi itaomboleza, kila jamaa peke yake; jamaa ya nyumba ya Daudi peke yao, na wake zao peke yao; jamaa ya nyumba ya Nathani peke yao, na wake zao peke yao;
13 jamaa ya nyumba ya Lawi peke yao, na wake zao peke yao; jamaa ya nyumba ya Shimei peke yao, na wake zao peke yao.
14 Jamaa zote zilizosalia, kila jamaa peke yake, na wake zao peke yao”.
Ndugu, Wakati huu upo karibuni kutokea.. Je! Umejipangaje/Tumejipangaje? Neema ndio tunaiaga hivyo? Inawarudia wayahudi, ilipoanzia.. kama wewe unasubiri kila siku kupigiwa kelele za injili utubu..Fahamu kuwa zama hizo zimeshaisha..jicho la Mungu linaanza kurudi Israeli sasa.. Na siku sio nyingi, UNYAKUO, utapita, watakaobakia ndio watakaoshuhudia hayo yote. Lakini tuliokoka tutakuwa mbinguni kwenye karamu ya mwanakondoo.
Tubu leo mpe Yesu maisha yako, ukabatizwe katika ubatizo sahihi, na kupokea Roho Mtakatifu. Huu Ulimwengu si rafiki, yasalimishe maisha yako kwa Bwana.
Maran Atha.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
WATAMTAZAMA YEYE AMBAYE WALIMCHOMA; NAO WATAMWOMBOLEZEA.
Nini maana ya ombeni kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi wala siku ya sabato?.
Swali: Lile Konzo la Ng’ombe Shamgari alilowapigia Wafilisti mia sita lilikuwa ni nini?
Jibu: Tusome,
Waamuzi 3:30 “Basi Moabu alishindwa siku hiyo chini ya mikono ya Israeli. Nayo nchi ikawa na amani muda wa miaka themanini
31 Tena baada yake huyo alikuwapo Shamgari mwana wa Anathi, aliyepiga katika Wafilisti watu mia sita KWA KONZO LA NG’OMBE; yeye naye aliwaokoa Israeli”
“Konzo” ni lugha nyingine ya “Mchokoo”. Na mchokoo ni kipande kifupi cha fimbo ya chuma, ambayo mwishoni ina ncha kali, fimbo hii ilitumika enzi za kale kuongozea ng’ombe wakati wa kulima. Wakati ambapo Ng’ombe waligoma kulima au kutembea kwa kasi inayohitajika na mkulima, basi fimbo hiyo ya chuma yenye ncha iliwekwa nyuma yao, na kuwachoma migongo yao.. Hivyo walipoguswa na ncha hiyo ya chuma na kusikia maumivu, basi walisonga mbele…
Mchokoo tunaweza kuusoma katika
Matendo 26:14 “Tukaanguka nchi sote, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya kiebrania, Sauli! Sauli! Mbona waniudhi? NI VIGUMU KWAKO KUUPIGA MATEKE MCHOKOO.
15 Nami nikasema, Wewe u nani, Bwana? Bwana akaniambia, Mimi ni Yesu, ambaye wewe unaniudhi”.
Paulo alikuwa anashindana na maagizo ya Mungu, na ndipo Bwana Yesu akampa hiyo mithali, kumwonyesha jinsi hali yake ya kiroho ilivyo..
Sasa kwa maelezo marefu zaidi kuhusu Mchokoo, na jinsi leo hii watu wanavyopiga mateke mchokoo wa Bwana Yesu unaweza kufungua hapa >>USIPIGE MATEKE MCHOKOO!
Lakini tukirudi kwa Shamgari, Mwamuzi aliyetiwa mafuta na Mungu kuwaokoa wana wa Israeli, maandiko yanatuambia alitumia hilo Konzo/Mchokoo kuwapiga wafilisti mia sita.
Hiyo ni kuonyesha ushujaa aliokuwa nao katika Bwana, na kuonyesha kuwa Mungu haokoi tu kwa mapanga na majeshi, bali anaokoa kwa jina lake kupitia vitu vilivyo dharaulika, Kama alivyofanya kwa Daudi.
Daudi alimwangusha Goliathi kwa jiwe moja tu, ambalo alilirusha kwa Goliathi na kumwua shujaa yule wa Wafilisti. Na ndivyo Mungu alivyomtumia huyu Shamgari kwa Konzo moja la Ng’ombe kuangusha mashujaa 600 wa kifilisti.
Hiyo ikitufundisha kuwa na sisi hatuna budi kumtegemea Bwana asilimia zote..pasipo kutegemea uwezo wetu, wala nguvu zetu wala uwezo wetu, kwasababu siku zote vita ni vya Bwana… Na Bwana anavitumia vitu vidhaifu kuviabisha vile vyenye nguvu. (sawasawa na 1Wakorintho 1:27-29).
1Samweli 17:42 “Hata Mfilisti alipotazama huku na huku, akamwona Daudi akamdharau; kwa kuwa ni kijana tu mwekundu, tena ana sura nzuri.
43 Mfilisti akamwambia Daudi, Je! Mimi ni mbwa hata umenijia kwa fimbo? Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake.
44 Mfilisti akamwambia Daudi, Njoo huku kwangu; nyama yako nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni.
45 NDIPO DAUDI AKAMWAMBIA YULE MFILISTI, WEWE UNANIJIA MIMI NA UPANGA, NA FUMO, NA MKUKI, BALI MIMI NINAKUJIA WEWE KWA JINA LA BWANA WA MAJESHI, MUNGU WA MAJESHI YA ISRAELI ULIOWATUKANA.
46 Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli.
47 NAO JAMII YA WATU WOTE PIA WAJUE YA KWAMBA BWANA HAOKOI KWA UPANGA WALA KWA MKUKI; MAANA VITA NI VYA BWANA, NAYE ATAWATIA NINYI MIKONONI MWETU”.
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
KUNA NGUVU YA ZIADA KATIKA KULING’ANG’ANIA KUSUDI LA MUNGU.
Nini maana ya usimfunge ng’ombe kinywa apurapo nafaka!.(Kumbukumbu 25:4)
Kwanini Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi wake wasichukue chochote isipokuwa fimbo tu?
Maji ya Farakano ni nini katika biblia?
SWALI: Wale wachawi walikuwa na maana gani waliposema..”Miungu wasio na kikao pamoja na wenye mwili”?.
Danieli 2:11
[11]Ni neno la ajabu, hili analolitaka mfalme, wala hapana mwingine awezaye kumwonyesha mfalme neno hilo, ila miungu, wasio na kikao pamoja na wenye mwili.
JIBU: Hiyo ni baada ya Mfalme Nebukadneza kutoa mtihani mzito wa kukumbushwa na kupewa tafsiri wa ndoto aliyoiota,..lakini tunaona wale wachawi wote walishindwa kupokea taarifa yoyote kutoka kwa miungu yao..ndipo wakakiri wazi kuwa fumbo hilo, si kila aina na mungu ilimradi mungu tu anaweza kulifichua, bali ni miungu wengine isiyofanya kikao na wanadamu.
Sasa hawa wachawi walitumia neno “miungu”..kwasababu waliamini katika miungu mingi, ndio màana utaona wanatumia neno miungu na sio Mungu asiyefanya kikao na wanadamu…lakini walimaanisha Mungu mmoja ( ambaye ni Yehova) yeye peke yake, ambaye huwa hafanyi vikao na wanadamu.
Sasa aliposema…asiyefanya vikao na wanadamu” maana yake ni kuwa asiyeishi pamoja na wanadamu..yaani Mungu ambaye makazi yake si duniani, bali ni mbinguni.
Miungu yote ya kipagani, makao yao ni hapa duniani, mizimu, mapepo, vibwengo, majini, n.k. vyote hivyo vinaishi katikati ya watu, na vinawategemea watu kutenda kazi zao..vinazurura zurura huku duniani kukusanya taarifa za matukio mbalimbali…havina kitu cha ziada zaidi ya kupeleleza peleleza, kama baba yao shetani (Ayubu 1:7)..
Haviwezi kujua mambo yajayo, haviwezi kutambua siri za ndani za mioyo ya watu..wakati mwingine hata vikitaka taarifa fulani ya mtu vitakuambia niletee kwanza unyayo, au nywele, jinsi gani vilivyo vidhaifu, havijui, wala havipo kila mahali..na ndio maana wale wachawi walitaka kwanza wasimuliwe ile ndoto..ndio walau wakisie kisie tafsiri yake..
Lakini Yehova peke yake ndiye ambaye hategemei, mwanadamu, au kiumbe chake chochote kufahamu au kutenda jambo alitakalo,
Hii ni kutuonyesha kuwa Mungu pekee(Yehova) ndio tumaini la kweli, shetani au vipepo haviwezi kueleza hatma ya mtu. Unapotazama utabiri wa nyota, ujue kuwa umedanganyika, unapokwenda kwa waganga ujue kuwa ndio umekwenda kujitafutia matatizo, unapofanya mila na kuamsha mzimu, ujue unajifungulia milango mwenyewe wa kupelekwa kuzimu.
Zaburi 115:3-9
[3]Lakini Mungu wetu yuko mbinguni, Alitakalo lote amelitenda.
[4]Sanamu zao ni fedha na dhahabu,
Kazi ya mikono ya wanadamu.
[5]Zina vinywa lakini hazisemi, Zina macho lakini hazioni,
[6]Zina masikio lakini hazisikii, Zina pua lakini hazisikii harufu,
[7]Mikono lakini hazishiki, miguu lakini haziendi, Wala hazitoi sauti kwa koo zake.
[8]Wazifanyao watafanana nazo, Kila mmoja anayezitumainia.
[9]Enyi Israeli, mtumainini BWANA; Yeye ni msaada wao na ngao yao.
Amen.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Bwana aliposema kuwa yeye ni “Mungu wa miungu” alikuwa na maana gani?..je! yeye ni Mungu wa sanamu?
JE! PAKA KULIA USIKU NI ISHARA YA UCHAWI?
Kuwiwa maana yake nini katika biblia?
Wasamaria walikuwa ni watu gani?
Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia Neno la Mungu wetu…
Yakobo baada ya kuondoka kwa Labani, alipokuwa njiani maandiko yanasema alikutana na Jeshi la Malaika wa Bwana…
Mwanzo 32:1 “Yakobo akashika njia yake na malaika wa Mungu wakakutana naye.
2 Naye Yakobo alipowaona, alisema, Hili ni jeshi la Mungu. Akapaita mahali pale, MAHANAIMU”.
Maana ya Neno “Mahanaimu” ni “Kambi mbili”…Yakobo alipaita mahali pale kwa jina hilo, kwasababu kaliona jeshi la Bwana likiwa pamoja naye.. Na hivyo kufanya jumla ya majeshi Mawili; jeshi lake yeye mwenyewe (yaani yeye na watumishi wake na watu wake wote) na la Bwana (malaika watakatifu).
Baada ya kuona jeshi hilo la Mbinguni likifuatana naye, ndipo alipojua kuwa hayupo mwenyewe, hivyo nguvu mpya na hofu yote ikamwondoka, Na hofu ya kwanza ambayo ilikuwa inamsumbua kwa muda mrefu ni ile ya kukutana na ndugu yake Esau, maana alikiri kabisa mwenyewe kuwa anamwogopa ndugu yake Esau (Mwanzo 32:11).
Lakini baada ya kujua kuwa lipo Jeshi lingine kubwa la mbinguni linamzungukan na kufuatana naye, ndipo akapata ujasiri mpya na kuamua kumtafuta ndugu yake..
Mwanzo 32:1 “Yakobo akashika njia yake na malaika wa Mungu wakakutana naye.
2 Naye Yakobo alipowaona, alisema, Hili ni jeshi la Mungu. Akapaita mahali pale, Mahanaimu.
3 Basi, Yakobo akapeleka wajumbe mbele yake kwenda kwa Esau nduguye mpaka nchi ya Seiri katika nyika ya Edomu
4 Akawaagiza akisema, Mwambieni hivi bwana wangu, Esau, Hivi ndivyo asemavyo mtumwa wako, Yakobo; Nimekaa ugenini kwa Labani, na kukawia huko hata sasa,
5 nami nina ng’ombe, na punda, na kondoo, na watumwa, na vijakazi; nami nimepeleka watu nimpashe bwana wangu habari, nipate neema machoni pako.
6 Wale wajumbe wakarudi kwa Yakobo wakisema, Tulifika kwa ndugu yako, Esau, naye anakuja kukulaki, na watu mia nne pamoja naye”.
Jambo kama hilo hilo lilitokea pia kwa Elisha, kipindi Mfalme wa Shamu alipotuma majeshi kwenda kumkamata Elisha pamoja na mtumishi wake, walipoamka asubuhi Elisha na mtumishi wake waliona jeshi la Washami limezunguka lile eneo lote.. Na Yule mtumishi wa Elisha akaishiwa nguvu kwa hofu, lakini Bwana akamfumbua macho na kuona jeshi kubwa la Malaika wa mbinguni, lililo kubwa kuliko jeshi la Washami limezunguka kile kilima chote..
2Wafalme 6:15 “Hata asubuhi na mapema mtumishi wake yule mtu wa Mungu alipoondoka, na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi la watu, na farasi na magari, wameuzingira mji ule. Mtumishi wake akamwambia, Ole wetu! Bwana wangu, tufanyeje?
16 Akamjibu, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.
17 Elisha akaomba, akasema, Ee Bwana, nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona. Bwana akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote”.
Jeshi hilo hilo pia limewazunguka leo watu wa Mungu(Waliompokea Yesu), wakati mwingine unaweza kuwa na hofu na kudhani Mungu hayupo na wewe, hata Yakobo alidhani hivyo, hata Mtumishi wa Elisha alidhani hivyo.. Lakini hawakujua kuwa lilikuwepo jeshi lingine kubwa la mbinguni lililofuatana nao, kuhakikisha kuwa wanafanikiwa katika njia zao.
Leo hii unaweza usifumbuliwe macho kama Mtumishi wa Elisha au kama Yakobo, lakini amini kuwa lipo jeshi lingine kubwa sana la mbinguni limekuzunguka.. hivyo usiogope siku zote kuendelea mbele, wala usiogope maadui…
Yakobo alimwogopa ndugu yake Esau kwa miaka mingi, lakini siku alipotambua kuwa Lipo jeshi la pili pamoja naye (Mahanaimu)..alisonga mbele kwa ujasiri na Bwana akampatanisha na Adui yake, Yule Yule adui yake akageuka kuwa kipenzi chake.. Vile vile yale majeshi yaliyotumwa kumkamata Elisha na Mtumishi wake, yaligeuka kuwa marafiki wa Elisha..(kwani baada ya lile tukio hayakurudi tena Israeli kwa kipindi kirefu sana 2Wafalme 6:23).
Na wewe kama umeokoka, songa mbele usikwamishwe na vitisho vya shetani, kwasababu walio upande wako ni wengi kuliko walio upande wa adui.
Bwana akubariki.
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
BWANA AWEZA KUKUPA ZAIDI SANA KULIKO HIZO.
SINA PESA SASA, YESU ATANISAIDIA NINI?
Je Elisha alimdanganya Ben-hadadi kuwa hatakufa kwa ugonjwa wake?
SWALI: Je huduma za mitume na manabii, zinaendelea kufanya kazi hadi sasa? Kwani kunaendelea mabishano baina ya wakristo baadhi, wengine wanasema kwasasa huduma hizo hazitendi kazi tena kufuatana na andiko la Paulo katika
Waefeso 2:20 linalosema;
[20]Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni.
…Lakini wengine wanasema huduma hizo hadi sasa zipo katika kanisa. Je ukweli ni upi?
JIBU: Kabla hatujafahamu kwanza kama huduma za mitume na manabii zinaendelea hadi sasa au la!…tutazame kwanza aina za manabii wa mwanzo, na mitume wa mwanzo walikuwaje..
1)Manabii wa kutia msingi wa wakati wote
2)Manabii wa kuthibitisha misingi.
1 ) Hawa manabii wa kutia misingi; Ndio wote waliotiwa mafuta na Mungu kaandika biblia takatifu…mfano wa hawa ndio kama Yeremia, Isaya, Nahumu, Malaki, Yoeli, Yona, Habakuki..n.k. Kwamba nabii zao zisimame kama msingi na mwongozo wa daima wa kuliongoza kanisa la Mungu wakati wote..
2 ) Manabii wa kuthibitisha: Hawa Mungu aliwanyanyua kutoa mwongozo wa wakati fulani tu mahususi.. Walikuwa wanasema Neno la Mungu lakini la wakati fulani tu ambapo ukishapita basi, unabii huo hauna umuhimu tena kwa vizazi vijavyo.
Mfano wa hawa utawasoma wengi sana..wakina Mikaya, Aguri, Odedi, Azuri, Ahiya, pia katika agano jipya walikuwepo wakina sila, agabo..n.k
Vivyo hivyo tukirudi na katika Mitume wa Kristo.
Wapo ambao waliotiwa mafuta kwa lengo la kuweka misingi ya daima. Hawa ndio wote tunaosoma nyaraka zao katika maandiko..mfano Paulo, Petro, Yakobo, Yohana, Yuda, Mathayo, Luka.
Na wapo waliowekwa kwa ajili ya kutihibitisha / kutia misingi midogo.midogo. Mfano wa hawa ni Epafrodito Wafilipi 2:25..
Sasa tukishafahamu…hilo…tunaporudi katika lile andiko linalosema..mmejengwa juu ya misingi ya mitume na manabii tunaweza kuelewa
Tusome;
Waefeso 2:20
[20]Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni.
Maana yake ni kuwa sisi kama kanisa tumejengwa juu ya mafunuo ya manabii watangulizi na mitume watangulizi wale waliochaguliwa kuweka misingi ya daima..(Yaani kwa lugha rahisi tumejengwa juu ya BIBLIA TAKATIFU)…
Hakuna namna tutajengwa juu ya misingi mingine mipya zaidi ya hiyo yao.. Hivyo kwasasa hatuna manabii na mitume kama wale watangulizi, ambao walipokea mafunuo ya moja kwa moja ya namna ya kulijenga kanisa la Kristo..ni sawa na kusema hatuna mitume mfano wa Paulo au Petro au manabii mfano wa Yeremia au Isaya, kwasasa.
Lakini wapo mitume na manabii wa nyakati ndogo ndogo, ambao wanafanya kazi za kuthibitisha misingi ambayo tayari ipo lakini sio wa kuleta jambo jipya duniani..
Kwamfano kazi mojawapo ya mitume ilikuwa ni kwenda kupanda makanisani mapya maeneo mapya..hivyo, mtu yeyote mwenye huduma.hii ndani yake, ni mtume lakini kazi yake itakuwa ni kutembea katika mstari ule ule wa mitume wa kwanza..hapaswi kuja na jambo lake jipya..anapaswa ahubiri kilekile mitume walichokifundisha, hapo atakuwa amekidhi kuitwa mtume.
Ni sawa na mtu anayejenga nyumba ya gorofa..msingi mkuu ni mmoja..ule uliopo chini…lakini akitaka aweke nyumba juu yake ni sharti afuata ramani ya msingi wa chini….
Ndivyo ilivyo kwa huduma hizi za kitume na kinabii.. Ni lazima zirejee katika biblia takatifu chochote kitolewacho lazima kionekane katika biblia sio katika maono yao wenyewe wanayojitungia.
Paulo aliandika maneno haya;
1 Wakorintho 3:10-15
[10]Kwa kadiri ya neema ya Mungu niliyopewa, mimi, kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima, naliuweka msingi, na mtu mwingine anajenga juu yake. Lakini kila mtu na aangalie jinsi anavyojenga juu yake.
[11]Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, Yesu Kristo.
[12]Lakini kama mtu akijenga juu ya msingi huo, dhahabu au fedha au mawe ya thamani, au miti au majani au manyasi, kazi ya kila mtu itakuwa dhahiri.
[13]Maana siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani.
[14]Kazi ya mtu aliyoijenga juu yake ikikaa, atapata thawabu.
[15]Kazi ya mtu ikiteketea, atapata hasara; ila yeye mwenyewe ataokolewa; lakini ni kama kwa moto.
Hivyo kwa kuhitimisha ni kuwa tofauti ya wale na hawa ni kwamba wote kazi yao ni moja ya upandaji wa kanisa la Kristo,mahali na mahali, isipokuwa wasasa hawaleti fundisho jipya, au maono mapya isipokuwa yale ambayo tayari yameshaanzishwa na mitume.
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Nitamjuaje nabii wa Uongo?
Wana wa Manabii walikuwa ni watu gani?
Hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu.
JINSI MTUME PAULO ALIVYOUTHAMINI WITO WAKE, JUU YA WENYE VYEO.