Swali: Katika biblia tunasoma sehemu kadha wa kadha zikiwataja “wana wa manabii”.. Je! Hawa wana wa manabii walikuwa ni watu gani?, na kazi yao ilikuwa ni ipi? Na kwanini waliitwa hivyo?.. Na je hata leo kuna wana wa manabii?
Jibu: Ni kweli Katika Agano la kale lilikuwepo kundi la watu waliojulikana kama Wana wa Manabii. (Soma 1Wafalme 20:35, 2Wafalme 6:1, 2Wafalme 4:1, na 2Wafalme 2:5).
Watu hawa walikuwa ni “manabii wa Mungu”, ambao walijitia katika kifungo cha kujifunza juu ya Nabii zilizotangulia kabla yao..
Kumbuka sio kujifunza jinsi manabii wanavyoishi au wanavyokula au wanavyoona maono!… La! Hakuna mwanadamu yeyote anayeweza kumfundisha mtu mwingine namna ya kuona maono!…hivyo ni vipawa vya Mungu ambayo ni Mungu mwenyewe anaviweka ndani ya mtu, na hatujifunzi wala hatufundishwi.. Ni sawa na ndoto…
Hakuna mtu anayeweza kumfundisha mwenzake jinsi ya kuota!.. Ndoto zinakuja zenyewe, kwasababu ni vipawa vya asili ambavyo Mungu kaviweka kwetu sote.. Na nabii za Mungu, zinawajia watu maalumu ambao Bwana kawachagua, na si kupitia kujifunza!.
Kwahiyo hawa wana wa manabii, au kwa lugha nyingine “Wanafunzi wa manabii” walikuwa ni watu waliojikita kujifunza Nyakati na Majira, Pamoja na Nabii zilizotangulia kutolewa na manabii wengine waliowatangulia..(kumbuka walikuwa wanajulikana kama wana wa manabii, na sio wana wa NABII!)..
Na lengo la kufanya hivyo (yaani kupokea maarifa hayo) ni ili wawe salama, na wawe na uhakika wa Nabii watakazozitoa isije wakapotoka na kutoa unabii wa uongo.
Kwa mfano Nabii anaweza kuona maono au kupata ujumbe kuhusu Taifa la Israeli, sasa ili authibitishe ujumbe ule au ono lile kama kweli ni kutoka kwa Bwana, ni sharti awe na Nabii nyingine za kutosha, za waliomtangulia zinazosapoti ono lake hilo jipya!.. Na akija kugundua kuwa Nabii mwingine, mkuu aliyetangulia alishatabiri jambo kama hilo au linalokaribiana na hilo… basi ndipo Ono lake hilo linathibitika… lakini akija kukuta ono lake linakinzana na maono ambayo manabii wakuu waliyatoa, ndipo analiacha, kwasababu sio kutoka kwa Bwana… (kwasababu kamwe Bwana hawezi kujipinga katika maneno yake).
Hivyo ndio maana ilihitajika shule ya manabii, ambayo lengo lake ni kujifunza kujua Nabii zilizotangulia juu ya watu, na mataifa…
Ili tuzidi kuelewa vizuri, utakumbuka kipindi cha Nabii Yeremia wakati anatabiri kwamba Israeli watachukuliwa utumwani kwenda Babeli.. utaona Yeremia alikuwa ni mtu mwenye elimu ya kutosha kuhusu Nabii zilizotangulia, alihakiki jumbe anazozipokea katika maono, kwa nabii za waliomtangulia kama wakina Isaya, na wengineo..
Na jambo moja utaona alilojifunza ni kuwa “Manabii karibia wote, hawakuwahi kutabiri juu ya amani kwa mataifa, manabii wengi walikuwa wanatabiri juu ya Vita na Mabaya na Tauni”.. Na Yeremia alijua Mungu hawezi kujipinga.. Hivyo maono yake aliyahakiki kwa namna hiyo..
Lakini utaona alitokea mtu anaitwa Hanania, ambaye alijitokeza na kuanza kutabiri juu ya Amani kwa Israeli kwamba hawataenda utumwani, watakuwa salama, ni ilihali Taifa zima limemwacha Mungu..jambo ambalo linakinzana na Nabii Mungu alizozitoa kupitia manabii wakuu waliotangulia… Na Yeremia kuliona hilo akamwambia Hanania maneno yafuatayo…
Yeremia 28:7 “Lakini lisikilize sasa neno hili nilisemalo, masikioni mwako, na masikioni mwa watu wote,
8 MANABII WALIOKUWAKO KABLA YA ZAMANI ZANGU, NA ZAMANI ZAKO, WALITABIRI JUU YA NCHI NYINGI, NA JUU YA FALME KUBWA, HABARI YA VITA, NA YA MABAYA, NA YA TAUNI”.
Umeona jambo Yeremia alilomwambia huyu Hanania?…
Yeremia alikuwa ni Mwana wa manabii, lakini Hanania alikuwa ni mtu tu aliyejizukia na kujiita Nabii, hana elimu yoyote ya Nabii za Mungu.. na akaanza kuwafariji watu kwa maneno ya uongo!..Jambo ambalo lilimchukiza sana Mungu, na hata kumwua Hanania.
Yeremia 28:15 “Kisha nabii Yeremia akamwambia nabii Hanania, Sikia sasa, Ee Hanania; Bwana hakukutuma; lakini unawatumainisha watu hawa maneno ya uongo. 16 BASI BWANA ASEMA HIVI, TAZAMA, NAKUTUMA UENDE ZAKO TOKA JUU YA USO WA NCHI; MWAKA HUU UTAKUFA, KWA SABABU UMENENA MANENO YA UASI JUU YA BWANA.17 BASI NABII HANANIA AKAFA, MWAKA UO HUO, MWEZI WA SABA”.
Yeremia 28:15 “Kisha nabii Yeremia akamwambia nabii Hanania, Sikia sasa, Ee Hanania; Bwana hakukutuma; lakini unawatumainisha watu hawa maneno ya uongo.
16 BASI BWANA ASEMA HIVI, TAZAMA, NAKUTUMA UENDE ZAKO TOKA JUU YA USO WA NCHI; MWAKA HUU UTAKUFA, KWA SABABU UMENENA MANENO YA UASI JUU YA BWANA.
17 BASI NABII HANANIA AKAFA, MWAKA UO HUO, MWEZI WA SABA”.
Lakini leo hii shetani kaligeuza hili Neno “Wana wa Manabii”. Leo hii kuna watu wamefungua vyuo vyao, wakiwa wenyewe wanajiita Manabii wakuu, na vijana wao wanawaita “wana wao (yaani wana wa manabii)”.. Lakini ukiingia katika madara yao na kusikia wanachofundishwa, ni huzuni tupu!.
Utasikia wanachofundishwa ni jinsi ya kuona maono, jinsi ya kutumia na kutengeneza mafuta na chumvi na mengineyo, utaona wanafundishwa mtindo wa maisha na mtindo wa kuongea, na kuvaa kama nabii mkuu wao, na jinsi ya kumwogopa na kumtukuza baba yao, nabii mkuu..
Na watasomea hata miaka 5 na wakitoka hapo wanapewa na vyeti, tayari wakufunzi!!!..
Ndugu! Huo ni uongo wa shetani…
Wana wa manabii katika Agano la kale, hawakufundishwa wala hawakuwa wanajifunza mitindo ya kuongea ya manabii waliowatangulia…wala walikuwa hawajifunzi jinsi ya kuona maono! (kwasababu tayari walikuwa na hiyo karama, ndio maana wakaitwa manabii)..Walichokuwa wanajifunza ni Nabii zilizotangulia zinazohusu wakati waliopo wao, na za mataifa mengine, kuanzia zilizoandikwa katika Torati ya Nabii Musa, mpaka wakati waliopo wao, ili kusudi wasije wakapotoka na maono waliyokuwa wanayapokea.
Na sisi leo hii wote ni wana wa Manabii.. ambao manabii wetu si baba zetu wa kiroho!!! Wala si maaskofu wetu, bali ni MITUME WA KWENYE BIBLIA, na MANABII WA KWENYE BIBLIA!!!...Tunatembea katika Nabii walizozitoa hao, wakina Musa, Isaya, Yeremia, Habakuki, na mitume wakina Petro, Yohana, Paulo n.k.. (Na nabii zao hazijawahi kukinzana),Kwasababu walikuwa na Roho mmoja.
Kwamfano Nabii Isaya alitoa unabii ufuatao..
Isaya 13:6 “Pigeni kelele za hofu; maana siku ya Bwana i karibu; itanyesha kama maangamizi yatokayo kwa Mwenyezi Mungu”.
Nabii Yoeli naye alitoa unabii kama huo huo katika Yoeli 3:14, na manabii wengine wote walitabiri hayo hayo…
Kwahiyo ili sisi tuhesabike kuwa “Wana wa manabii” ni lazima maono yetu tunayoyaona katika ndoto, au kwa wazi, ni lazima yapatane na huo unabii wa Isaya, na Yoeli na wengineo katika biblia!… usipopatana na huo unabii wa Isaya basi hilo Ono au huo Unabii ni wa UONGO!!! Ni kutoka Kuzimu!!!...
Tukiota au tukiona maono ambayo yanatuonyesha au kutuambia kuwa “Tufurahi, tupige kelele za shangwe, kwasababu siku ya Bwana bado sana”..basi hilo ni Ono kutoka kuzimu!!!..
Kwahiyo kwa hitimisho ni kwamba wana wa manabii, ni manabii ambao walikuwa wamejikita katika kusoma Nabii za manabii wa Mungu waliowatangulia, ili wasifanye makosa katika kutoa nabii zao.
Na sisi ni lazima tuwe wanafunzi wa biblia, turejee biblia katika kuhakiki kila kitu, na hatupaswi kuamini tu kila jambo ambalo tunalipokea katika ndoto au maono.
Bwana Yesu na atusaidie sana.
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp: Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
UJUE UCHAWI WA MANABII WA UONGO?.
Nini maana ya “Torati na manabii”?
Nini maana ya “Roho za manabii huwatii manabii?
UNAWAFAHAMU MANABII WA UONGO?
MJUMBE ASIYEKUWA NA UJUMBE.
Rudi nyumbani
Print this post