Category Archive Home

Pambaja ni nini katika Biblia kama tunavyosoma katika kitabu cha Wimbo ulio bora 1:2?

Jibu: Pambaja ni neno linalo maanisha “upendo” (ule wa mwanaume na mwanamke).  Upo upendo wa ndugu kwa ndugu, mfano upendo wa Mzazi na mtoto, dada na kaka wa familia moja na pia upo upendo wa mwanamke na mwanamke. Sasa upendo huu wa mwanaume na mwanamke kwa lugha nyingine ndio unaoitwa PAMBAJA. Neno hili linaweza kutumika kama wingi, lakini linamaanisha vile vile upendo.

Wimbo ulio Bora 1: 2 “Kubusu na anibusu kwa kinywa chake. Maana pambaja zako zapita divai”

Wimbo ulio Bora 4: 10 “Jinsi zilivyo nzuri pambaja zako, umbu langu, Bibi arusi, ni nzuri kupita divai; Na harufu ya marhamu yako Yapita manukato ya kila namna”

Pia unaweza kulipata neno hilo kwenye mistari hii; Wimbo 1:4, Wimbo 7:12.

Sasa ni kwanini upendo huu umetajwa hapo?, je una umuhimu wowote kwetu sisi wakristo?. Ndio una umuhimu mkubwa, kwanza kwa wana-ndoa na Pili kwa Kristo na Kanisa lake.

Kumbuka Sisi wakristo katika roho tunafananisha na bibi-arusi na Kristo ndiye Bwana Arusi. Hivyo jinsi Kristo anavyolipenda kanisa upendo wake ni kama wa mke na mume (yaani Pambaja).  Na kama unavyojua wivu ni mbaya kuliko ghadhabu..Na ndivyo Kristo anavyotuonea wivu, tunapoiacha njia ya haki na kuufuata ulimwengu.. Tunamtia wivu.

Wimbo 8: 6 “Nitie kama muhuri moyoni mwako, Kama muhuri juu ya mkono wako; Kwa maana upendo una nguvu kama mauti, Na wivu ni mkali kama ahera. Mwako wake ni mwako wa moto, Na miali yake ni miali ya Yahu”

Hivyo sisi tuliookoka ni watu wa thamani mbele ya Kristo, ni bibi-arusi wake, anayetupenda na kutujali na katuandalia mambo mengi mazuri mbinguni katika karamu yake aliyotuandalia..

Ufunuo 21: 9  “Akaja mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na vile vitasa saba vilivyojaa yale mapigo saba ya mwisho, naye akanena nami, akisema, Njoo huku, nami nitakuonyesha yule Bibi-arusi, mke wa Mwana-Kondoo.

10  Akanichukua katika Roho mpaka mlima mkubwa, mrefu, akanionyesha ule mji mtakatifu, Yerusalemu, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mwenyezi Mungu”

Je utaikosa hiyo Yerusalemu mpya iliyoandaliwa mahususi kwa bibi-arusi?. Kama hujampokea Kristo hutaurithi uzima huo wa milele. Hivyo mpokee leo, kwa kutubu na kwenda kubatizwa na yeye atakupokea.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

UPENDO NI NINI NA JE! KUNA AINA NGAPI ZA UPENDO?

SI MAPEPO YOTE NI YA KULIPUKA.

JE! UKIMWI UNATIBIKA?

JIKANE NAFSI MTEULE WA MUNGU.

BWANA SI MWEPESI WA HASIRA, LAKINI BWANA NI MWINGI WA HASIRA.

Rudi nyumbani

Kwanini  vizazi vya ukoo wa Yesu vinajipinga katika Mathayo na Luka.

Kwamfano tukisoma katika injili ya  Mathayo, tunaona, mwandishi anaanza kueleza ukoo wa Yesu tangu Ibrahimu Mpaka Yusufu, lakini alipofika kwa  Daudi, aliendelea na kusema Daudi akamzaa Sulemani, (Mathayo 1:6)..Lakini tukirudi tena kwenye Luka hapo hapo tunaona Daudi alimzaa Nadhani (Luka 3:31), Hiyo ni kuonyesha kuwa Yesu alipitia uzao wa Nathani na sio wa Sulemani, kulingana na Luka. Lakini Mathayo anasema alipitia kwenye uzao wa Sulemani, kwanini iwe hivyo?

Pia ukisoma tena mwishoni utaona kulingana na Injili ya Mathayo, baba yake Yusufu alikuwa ni  Yakobo, lakini Luka anatuambia baba yake Yusufu alikuwa ni Eli (Luka 3:23).. Naomba ufafanuzi juu ya hili.

JIBU: Ni wazi kuwa ukisoma kitabu cha Mathayo na kile cha Luka utaona kuna tofauti kubwa kwenye vizazi vya ukoo wa Yesu. Luka anatuambia baba wa Yusufu alikuwa ni Eli, na Mathayo inasema babaye alikuwa ni Yakobo. Lakini je! Hilo linamaanisha biblia inajipinga?

Jibu ni la! Ikumbukwe kuwa zamani katika taifa la Israeli walikuwa na desturi  ya mtu kumnyanyulia ndugu yake uzao, na mtoto huyo kuitwa kwa jina la marehemu ikiwa mtu huyo atakufa kabla hajapata mtoto.. Soma. Kumbukumbu 25:5-6,

Kwamfano, kama wewe ni mwanaume umezaliwa katika familia, na ukaoa, lakini kwa  bahati mbaya ukafa bila kupata mtoto, basi anatafutwa ndugu yako wa karibu aidha katika familia au katika ukoo, Yule aliye karibu zaidi  na wewe, kisha anakwenda kumuoa huyo mke wako uliyemwacha, kisha anamzalia mtoto, lakini huyo mtoto hataitwa kwa jina lake, bali ataitwa kwa jina lako wewe marehemu, haijalishi kuwa watoto huyo watakuwa wametoka katika viungo vya mtu mwingine. Na Wanafanya hivyo ili kulitunza jina lako lisipotee.

Na ndicho walichokifanya Israeli wakati ule, ndicho alichokifanya Boazi kwa Ruthu, (ukisoma Ruthu 4:6-9)

Sasa tukirudi katika Injili. Mathayo aliandika Uzao wa Yusufu (Babaye Yesu), akifuata ubaba  wa kibaolojia, na Luka aliandika uzao wa Yusufu akifuata ubaba wa kijina.

Ikiwa na maana kuwa Eli pengine alikufa kabla ya kupata mtoto, hivyo Yakobo akamchukua mke wake, na kuzaa naye ili kumtunzia jina, ndipo akamzaa Yusufu. Hivyo kibaolojia Yusufu alikuwa ni mtoto wa Yakobo lakini kisheria alikuwa ni mtoto wa Eli.

Na ndio maana Yakobo hatajwi katika injili ya Luka, bali ni Eli.. Lakini Mathayo anamtaja Yakobo Kama baba wa Yusufu lakini kibaolojia. Hivyo maandiko yapo sawa.

Kwafaida ya asiyekuwa na biblia anaweza kuvipitia, vifungu hivyo vya biblia hapa chini:

Mathayo 1:1-16

1 Kitabu cha ukoo wa Yesu Kristo, mwana wa Daudi, mwana wa Ibrahimu.

2 Ibrahimu alimzaa Isaka; Isaka akamzaa Yakobo; Yakobo akamzaa Yuda na ndugu zake;

3 Yuda akamzaa Peresi na Zera kwa Tamari; Peresi akamzaa Esromu; Esromu akamzaa Aramu;

4 Aramu akamzaa Aminadabu; Aminadabu akamzaa Nashoni; Nashoni akamzaa Salmoni;

5 Salmoni akamzaa Boazi kwa Rahabu; Boazi akamzaa Obedi kwa Ruthu; Obedi akamzaa Yese;

6 Yese akamzaa mfalme Daudi.

7 Sulemani akamzaa Rehoboamu; Rehoboamu akamzaa Abiya; Abiya akamzaa Asa;

8 Asa akamzaa Yehoshafati; Yehoshafati akamzaa Yoramu; Yoramu akamzaa Uzia;

9 Uzia akamzaa Yothamu; Yothamu akamzaa Ahazi; Ahazi akamzaa Hezekia;

10 Hezekia akamzaa Manase; Manase akamzaa Amoni; Amoni akamzaa Yosia;

11 Yosia akamzaa Yekonia na ndugu zake, wakati wa ule uhamisho wa Babeli.

12 Na baada ya ule uhamisho wa Babeli, Yekonia akamzaa Shealtieli; Shealtieli akamzaa Zerubabeli;

13 Zerubabeli akamzaa Abihudi; Abihudi akamzaa Eliakimu; Eliakimu akamzaa Azori;

14 Azori akamzaa Sadoki; Sadoki akamzaa Akimu; Akimu akamzaa Eliudi;

15 Eliudi akamzaa Eleazari; Eleazari akamzaa Matani; Matani akamzaa Yakobo;

16 Yakobo akamzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa YESU aitwaye Kristo.

Na..

Luka 3:23-38

23 Na Yesu mwenyewe, alipoanza kufundisha, alikuwa amepata umri wake kama miaka thelathini, akidhaniwa kuwa ni mwana wa Yusufu, wa Eli,

24 wa Mathati, wa Lawi, wa Melki, wa Yana, wa Yusufu,

25 wa Matathia, wa Amosi, wa Nahumu, wa Esli, wa Nagai,

26 wa Maathi, wa Matathia, wa Semei, wa Yusufu, wa Yuda,

27 wa Yoana, wa Resa, wa Zerubabeli, wa Shealtieli, wa Neri,

28 wa Melki, wa Adi, wa Kosamu, wa Elmadamu, wa Eri,

29 wa Yoshua, wa Eliezeri, wa Yorimu, wa Mathati, wa Lawi,

30 wa Simeoni, wa Yuda, wa Yusufu, wa Yonamu, wa Eliakimu,

31 wa Melea, wa Mena, wa Matatha, wa Nathani, wa Daudi,

32 wa Yese, wa Obedi, wa Boazi, wa Salmoni, wa Nashoni,

33 wa Aminadabu, wa Aramu, wa Hesroni, wa Peresi, wa Yuda,

34 wa Yakobo, wa Isaka, wa Ibrahimu, wa Tera, wa Nahori,

35 wa Serugi, wa Ragau, wa Pelegi, wa Eberi, wa Sala,

36 wa Kenani, wa Arfaksadi, wa Shemu, wa Nuhu, wa Lameki,

37 wa Methusela, wa Henoko, wa Yaredi, wa Mahalaleli, wa Kenani,

38 wa Enoshi, wa Sethi, wa Adamu, wa Mungu.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

MWANZO WA INJILI YA YESU KRISTO.

Bwana Yesu alimaanisha nini kusema “Saa yangu haijawadia?”

JE BWANA WETU YESU ALIKUWA NI MZUNGU?

Je! Bwana Yesu alitumwa kwa Waisraeli tu peke yao?

JE! SISI KAMA WAKRISTO NI DHAMBI KUSHEHEREKEA KRISMASI?.

Rudi nyumbani

Je! Kuna malaika wangapi mbinguni?

Biblia haijatoa idadi kamili ya malaika Mungu aliowaumba, inatumia neno “MAJESHI” ambayo majeshi yenyewe  hayo yapo maelfu kwa maelfu.

Waebrania 12:22 “Bali ninyi mmeufikilia mlima Sayuni, na mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni, na MAJESHI ya malaika ELFU NYINGI”,

Umeona ni wengi sana kiasi kwamba hata mwandishi ameshindwa kutoa idadi kamili ya majeshi hayo, anaishia kusema tu elfu NYINGI..maana yake hayahesabiki.

Sehemu nyingine, inasema  idadi yake ni elfu mara elfu na elfu kumi mara elfu kumi..utaona hapo mwandishi bado  anapata shida kuelezea idadi hiyo  kamili ya malaika hao, jinsi walivyo wengi, Ni malfu mengi yanayojizidisha, na kujizidisha na kujizidisha..

Ufunuo 5:11 “Nikaona nikasikia sauti ya malaika wengi pande zote za kile kiti cha enzi, na za wale wenye uhai, na za wale wazee, na hesabu yao ilikuwa elfu kumi mara elfu kumi na elfu mara elfu,”

Katika biblia Malaika wapo wa aina tofauti tofauti,

Wapo malaika wa Sifa: Hawa wapo mbele za Mungu usiku na mchana kuilinda enzi yake, ndio wale Maserafi na makerubi; ambao tunawasoma kwenye biblia. Ezekieli 1:4-28, Isaya 6:2-6

Wapo malaika wa vita: Mfano wa hawa ni Mikaeli na malaika zake: 2Wafalme 6:17, Ufunuo 12:7, Yeremia 5:14, 38:17, Hosea 12:5

Wapo malaika wajumbe: Mfano wake ni  Gabrieli. Danieli 8:16, 9:21, Luka 1:19,26.

Wapo malaika wa vitu vya asili tu: kama vile moto, maji n.k. Ufunuo 16:5, 14:18

Wapo malaika wa ulinzi, (Mji, na mataifa): Danieli 4:13

Wapo malaika wa ulinzi (wanadamu): Mathayo 18:10, Zaburi 34:7

Wapo malaika wa Huduma (watumishi):  Matendo 5:19, 7:30, 8:26, 12:15, 27:23,Waebrania 1:14,

Wapo malaika wa mapigo: Zaburi 78:49, Ufunuo 16

Wapo malaika wa uponyaji: Yohana 5:4, Isaya 6:7

Pamoja na hayo wapo pia malaika walioasi. Ambao biblia inatuambia walikuwa ni theluthi tu ya malaika wote waliokuwa mbinguni. Na hao idadi yao haihesabiki, katikati yao kuna ambao wapo vifungoni saa hii wanasubiria hukumu ya mwisho, (Yuda 1:6)  

Wengine wapo  vifungoni lakini watakuja kuachiliwa kwa muda kidogo wafanye kazi duniani kwa muda mfupi kisha wataondolewa(Ufunuo 9:1-11),

na wengine wapo  bado hapa hapa duniani wakizurura zurura tu kuwaharibu watu, na kusababisha maovu duniani..

Jaribu tu kutengeneza picha tu  yale mapepo yaliyomwingia Yule kichaa, kule makaburini, Yesu alipowauliza jina lako nani, yakasema LEGIONI, yaani jeshi, yakimaanisha hatuhesabiki..Sasa Kama ndani ya mtu mmoja yanaweza kukaa mapepo yasiyohesabika, jiulize mapepo yaliyopo ndani ya watu wote ambao hawajampa Kristo maisha yao leo hii yapo mangapi?

Hivyo hiyo inafanya idadi ya malaika  ambao Mungu aliwaumba kuwa nyingi sana isiyoweza kuhesabika, hata zaidi ya idadi ya wanadamu wote walioishi na wanaoishi duniani tangu dunia iumbwe.

Hiyo ni kutuonyesha jinsi Mungu alivyojawa na uweza na nguvu na utukufu.

Zaburi 139:17 “Mungu, fikira zako zina thamani nyingi kwangu; Jinsi ilivyo kubwa jumla yake!

18 KAMA NINGEZIHESABU NI NYINGI KULIKO MCHANGA; NIAMKAPO NIKALI PAMOJA NAWE”.

JINA LA BWANA LIHIMIDIWE DAIMA.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Nitaitofautishaje sauti ya Malaika na ya Roho Mtakatifu?

Kwanini Mungu anasema “Afanyaye malaika zake kuwa pepo”?

MALAIKA WAPELELEZI WA HUKUMU WANAPITA SASA.

 KUWAHUDUMIA MALAIKA PASIPO KUJUA.

UTAWALA WA MIAKA 1000.

Rudi nyumbani

BWANA AYAGANGE NA MACHO YETU PIA.

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tulitafakari Neno la Mungu pamoja, kwani ndicho chakula pekee kinachoweza kuziponya roho zetu kabisa kabisa.

Lipo swali tunaweza kujiuliza ni kwanini kuna wasaa ilimgharimu Bwana wetu kulia sana na kutoa machozi ? Tunajua alikuwa ni mkamilifu , alikuwa hana hofu na chochote, na lolote alilomwomba Mungu, dakika hiyo hiyo alipewa, lakini ni kwanini wakati mwingine ilimpasa atoe machozi mengi, na kulia ili apoke?

Kitabu cha Waebrania kinatuambia hivyo;

Waebrania 5:7 “Yeye, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja NA KULIA SANA NA MACHOZI, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu”;

Wakati  mwingine Bwana wetu Yesu alilia sana kama katoto kadogo, mbele za Mungu wake, alitoa machozi mengi, Yesu huyo ambaye leo hii  tunamwita Bwana wa Mabwana na Mfalme wa Wafalme, na kama hilo halitoshi tunamwita mwanaume wa wanaume.

Lakini mwanaume huyu alilia, alitoa machozi katika kumwomba Mungu wake, na kwasababu hiyo Mungu akamsikia, japokuwa hata asingefanya hivyo angesikiwa tu, lakini hisia zake zilizidi uwezo wake, na mamlaka yake, na nguvu zake..alipokuwa mbele za Baba yake machozi yalimtoka mwenyewe  tu, pale alipoutafakari uwezo wake jinsi ulivyo mkuu, yalimtoka mwenyewe alipoona Upendo wa Baba yake unavyozidi upeo, yalimtoka mwenyewe pale alipowahurumia watu aliopewa na Baba yake.

Jambo hilo halikuishia tu kwake, tunaona pia aliwaambukiza mpaka na mitume wake waliomtumikia baadaye..Kwa mfano utamwona Paulo wakati mwingi sio tu alilia katika kuomba bali hata alipokuwa anawahubiria watu alitoa machozi, kwa vile alivyokuwa anawahurumia roho zao.

Matendo 20:31 “Kwa hiyo kesheni, mkikumbuka ya kwamba miaka mitatu, usiku na mchana, sikuacha kumwonya kila mtu kwa machozi”.

Soma tena..

2Wakoritho 2:4 “Maana katika dhiki nyingi na taabu ya moyo niliwaandikia na machozi mengi; si kwamba mhuzunishwe, bali mpate kujua upendo wangu nilio nao kwenu jinsi ulivyo mwingi”.

Na…

Wafilipi 3:18 “Maana wengi huenenda, ambao nimewaambieni mara nyingi habari zao, na sasa nawaambia hata kwa machozi, kuwa ni adui za msalaba wa Kristo”;

Unaona hisia hizo nyingi za Paulo ndizo zilizochangia pia hata huduma yake duniani kuwa na mafanikio makubwa. Kwasababu aliyachukulia mambo ya Mungu kwa uzito mkubwa, aliithamini neema katika hisia za hali ya juu sana, ambazo zilimpelekea hata  kutoa machozi wakati mwingi alipokuwa anafanya kazi ya Mungu.

Na sisi pia, tuziamshe hisia zetu kwake. Mwingine anaweza kusema mimi siwezi! Ndio huwezi kulia kwasababu hujakaa chini na kuutafakari kwa makini uweza wake wote kwako, aliokufanyia tangu umekuja hapa duniani.

 Ungetafakari kwa undani ni kwanini Mungu amekupa uhai mpaka leo hii, na hujampa chochote, ni kwanini unavuta hewa yake bure, na hajawahi kukuchaji hata senti, ni kwanini umekuchagua wewe na kukupa wokovu na muda huo huo kuna wengine hawataki hata kusikia habari za mUNGU, ukidhani kwamba wewe kichwa chako ni chepesi sana kuelewa kuliko wale?, Hilo ondoa akilini, ni kwamba Mungu kachagua tu kukuvuta wewe kwake, hilo tu, huna cha ziada ulichomfanyia.  Ukikumbuka siku ile ulikuwa katika jaribu fulani akakuvusha, kama sio yeye ungekuwa ni marehemu sana.. Ukikumbuka hayo yote, hutabaki kama ulivyo,

Ukikumbuka ni  kwanini mwaka huu unakwisha, wewe hujafa na KORONA, wakati mamilioni ya watu wamekufa na bado wanaendelea kufa duniani leo hii.. nakwambia utabaki kama ulivyo.. utalia tu, na kutoa machozi kwa kumpa Mungu shukrani, kwa kulibariki jina lake.

Unapoumaliza huu mwaka, usizizuie hisia zako kwa Mungu. Huu ni mwaka ambao sote tunahitaji kumshukuru Mungu, kwa nguvu zaidi kuliko hata miaka mingine yote iliyowahi kututangulia.

“Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema; Kwa maana fadhili zake ni za milele”. (1Nyakati 16:34)

Mungu atujalie kulijua hilo, ayagange macho yetu.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312 Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group

Mada Nyinginezo:

 Rudi nyumbani

Fadhili ni nini? Nini maana ya “fadhili zake ni za milele” kibiblia?

Biblia inapozungumza juu ya fadhili za Mungu, ni zaidi ya zile fadhili ambazo tunazojua  ambazo mtu anaweza kuzifanya kwa mtu mwingine, yaani kumuonyesha ukarimu na wema..

Kibiblia Fadhili za Mungu ni Neno pana sana, kwa kiebrania linatamkwa “Hesed”, ambalo tafsiri yake huwezi kuelezea kwa neno moja, au kwa maneno machache.

Fadhili za Mungu sio tu wema na ukarimu Mungu anaotufanyia sisi, bali linamaanisha pia Upendo wa Mungu usioelezeka, upendo wa kusaidia, upendo wa kuvumilia, Upendo wa kuokoa upendo wa kutoa,..

Ni wema usio na masharti, kwamba hatutendei fadhili zake kisa sisi tumemfanyia kitu kwanza, au tumekuwa marafiki zake, Hapana. Anatenda kama vile ni wajibu wake kufanya, Wema huo hauwezi kuelezeka, kwasababu unagusa kila Nyanja, ambazo haziwezi kufikiwa na mwanadamu yoyote Yule, au kiumbe chochote kile mbinguni au duniani., umeingia ndani kabisa.

Na ndio maana Neno hili utalisoma sehemu nyingi sana katika biblia,  Na pia utaona Daudi kila alichokiona  au alichokitaja alihitimisha na neno “kwa maana fadhili zake ni za  milele”..

ZABURI 136

1 Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

2 Mshukuruni Mungu wa miungu; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

3 Mshukuruni Bwana wa mabwana; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

4 Yeye peke yake afanya maajabu makuu; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

5 Yeye aliyefanya mbingu kwa fahamu zake; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

6 Yeye aliyeitandaza nchi juu ya maji; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

7 Yeye aliyefanya mianga mikubwa; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

8 Jua litawale mchana; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

9 Mwezi na nyota zitawale usiku; Kwa maana fadhili zake ni za milele. 10 Yeye aliyewapiga Wamisri kwa kuwaua wazaliwa wa kwanza wao; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

11 Akawatoa Waisraeli katikati yao; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

12 Kwa mkono hodari na mkono ulionyoshwa; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

13 Yeye aliyeigawa Bahari ya Shamu; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

14 Akawavusha Israeli katikati yake; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

15 Akamwangusha Farao na jeshi lake katika Bahari ya Shamu; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

16 Yeye aliyewaongoza watu wake jangwani; Kwa maana fadhili zake ni za milele.

Vipo vifungu vingi sana Soma pia.. 1Nyakati 16:34, Zaburi 106:1 n.k.

Utaona pia Musa alipofumbuliwa macho yake na kumwona Mungu kwa sehemu, alipokuwa kule mlima alitangaza na kusema;

Kutoka 34:6 “Bwana akapita mbele yake, akatangaza, Bwana, Bwana, Mungu mwingi wa huruma, MWENYE FADHILI, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli;

Vivyo hivyo kilichomchea Mungu kumtuma mwanawe duniani kuja kutuokoa, hakikuwa kingine zaidi ya Fadhili zake za milele zinazodumu kwetu daima..

Alikuwa tayari kumtoa mwanawe wa pekee kafara ili sisi tupate wokovu, Jiulize wewe unaweza kumtoa mwanao, tena yule unayempenda kuliko wote awe sadaka ili jirani yako ambaye hakusaidii chochote apone au afaidike? Unaweza kufanya hilo?  Huwezi kwasababu hujafikia kiwango hicho cha fadhili za Yehova.

Hivyo kama  tukiyajua hayo ni wajibu wetu kumwimbia usiku na mchana, kumshukuru juu ya wema wake aliotuonyesha na anaotufanyia kila siku. Na Tunampa Mungu sifa za vinywa vyetu, pamoja na kwa MATOLEO YETU.

Jina la Yesu Kristo libarikiwe daima.

 Haleluya.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

ZIKUMBUKE FADHILI ZA MUNGU

NI NANI ATAKAYETUTENGA NA UPENDO WA KRISTO?

KWA KUWA NGUVU ZA MBINGUNI ZITATIKISIKA.

NJIA YA KUPATA WOKOVU.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Rudi nyumbani

Kikuku/vikuku ni nini katika biblia?

Vikuku ni vitu mfano wa bangili ambavyo vinavaliwa aidha mikononi au miguuni, kwa lengo la urembo. Tazama picha juu. Katika enzi za zamani vikuku vilivaliwa na jinsia zote, yaani wanaume na wanawake.

wanawake wanavaa vikuku miguuni

Katika biblia tunaona neno hilo likitokea mara kadhaa..

2 Samweli 1:10 “Basi, nikasimama karibu naye, nikamwua, kwa sababu nalijua hakika ya kuwa hawezi kupona baada ya kuanguka; kisha nikaitwaa ile taji iliyokuwa kichwani mwake, na kikuku kilichokuwa mkononi mwake, nami nimevileta hapa kwa bwana wangu”.

Na pia unaweza kusoma mistari ifuatayo binafsi iliyozungumzia juu ya vikuku Mwanzo 24:47, Isaya 3:19,  Ezekieli 16:11 na Ezekieli 23:42.

Lakini sio hilo tu, vikuku pia vilitumika katika kutengenezea mishikio ya masanduku. Kwa mfano utaona sanduku la Agano lilitengenezwa kwa vikuku katika pande zake za chini ili kuwezesha upitishaji wa zile fimbo zake, na kufanya ubebaji wake uwe mrahisi… Tazama picha chini.

vikuku katika sanduku la agano

Kutoka 25: 14 “Nawe tia hiyo miti katika vile vikuku vilivyo katika pande mbili za sanduku ili kulichukua hilo sanduku.

15 Hiyo miti itakaa katika vile vikuku vya sanduku; haitaondolewa.

16 Kisha tia ndani ya sanduku huo ushuhuda nitakaokupa”.

Lakini je! Katika agano tunaruhusiwa kuvaa vikuku?

Jibu ni la!. Mwanaume au mwanamke wa kikristo hapaswi kutoboa pua na kuweka hazama, hapaswi kujiharibu ngozi kwa kujichubua, hapaswi kuvaa vikuku katika mikono yake au miguu yake..Kwasababu miili yetu ni hekalu la Roho Mtakatifu.

1Petro 3:3 “Kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi;

4  bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu.

5  Maana hivyo ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu, na kuwatii waume zao”

Mwanamke anayevaa kikuku mguuni, anakuwa hana tofauti na kahaba. Matumizi ya vikuku yabaki katika kutengenezea masanduku na bidhaa nyingine lakini si kuivalisha miili yetu.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

Hazama ni nini katika biblia?(Ezekieli 16:12, Kutoka 24:47)

KUJIPAMBA NI DHAMBI?

UUMBAJI BORA WA MUNGU, UPO NDANI YA MWANADAMU.

UFUNUO NI NINI, NA NITAPOKEAJE UFUNUO KUTOKA KWA MUNGU?

UFUNUO: Mlango wa 3 part 3

Rudi nyumbani

NJIA YA KUPATA WOKOVU.

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, Ni neema tumeiona tena siku ya leo, hivyo nakukaribisha katika kuyatafakari Maneno ya uzima wa roho zetu.

Leo tutajifunza jinsi wokovu unavyopatikana.. Tunapozungumzia wokovu maana yake ni tunazungumzia Uponyaji wa Roho zetu. Upo uponyaji wa mwili na uponyaji wa roho. Sasa njia ya uponyaji wa mwili ni tofauti na ile ya roho.

Sasa kama utakumbuka katika hatua za mwanzo kabisa za wana wa Israeli kutolewa Misri, utaona Farao alikuwa akipigwa kwa mapigo kadha wa kadha…Utaona alikuwa analetewa makundi ya nzige, mara nzi, mara Vyura na chawa n.k.  Na kila walipomlilia Bwana awaondolee hayo mapigo Mungu alikuwa anayaondoa katikati yao..

Kutoka 8: 8 “Ndipo Farao akawaita Musa na Haruni na kuwaambia, Mwombeni Bwana, ili awaondoe vyura hawa kwangu mimi na kwa watu wangu; nami nitawapa watu ruhusa waende zao, ili wamtolee Bwana dhabihu.

9 Musa akamwambia Farao, Haya, ujitukuze juu yangu katika jambo hili; sema ni lini unapotaka nikuombee wewe, na watumishi wako, na watu wako, ili hao vyura waangamizwe watoke kwako wewe na nyumba zako, wakae ndani ya mto tu.

10 Akamwambia, Kesho, Akasema, Na yawe kama neno lako; ili upate kujua ya kwamba hapana mwingine mfano wa Bwana, Mungu wetu.

11 Hao vyura wataondoka kutoka kwako wewe na nyumba zako, na watumishi wako, na watu wako; watasalia mtoni tu.

12 Basi Musa na Haruni wakatoka kwa Farao; Musa akamlilia Bwana katika jambo la hao vyura aliokuwa amewaleta juu ya Farao.

13 Bwana akafanya sawasawa na neno la Musa; na hao vyura wakafa kutoka katika zile nyumba, na katika viwanja, na katika mashamba”

Na Mainzi ni hivyo hivyo na mapigo mengine yote… Wamisri walipomwomba Mungu awaondolee, Mungu aliwasikia na kuliondoa lile tatizo…soma Kutoka 8:29-30.

Lakini tunakuja kuona mbele kidogo tu, wakati wana wa Israeli tayari wameshavuka bahari ya Shamu, walipomuudhi Mungu, na Mungu alipowaletea zile nyoka za moto…Walimlilia Mungu aziondoe lakini hakuziondoa…badala yake aliwatafutia dawa ili kila aliyeumwa, wanapoitazama ile nyoka ya shaba wapate kupona.

Hesabu 21: 5 “Watu wakamnung’unikia Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu.

6 Bwana akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa.

7 Watu wakamwendea Musa, wakasema, Tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung’unikia Mungu, na wewe; utuombee kwa Bwana, atuondolee nyoka hawa. Basi Musa akawaombea watu.

8 Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo ataishi.

9 Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi”.

Hapo Bwana hakuwaondoa hao nyoka, kama alivyoondoa wale vyura, au nzige, au chawa wakati wa Farao. Badala yake aliwaacha nyoka waendelee kuwepo (maana yake waendelee kuuma watu)..Na mtu mwenyewe achague aidha UZIMA au MAUTI. Kama atachagua uzima basi atajinyenyekeza na kwenda kuitazama ile nyoka wa shaba, lakini kama hatataka na kuamua kutafuta njia zake yeye mwenyewe anazozijua za kujitibu, basi atakufa.

Sasa Jambo hilo ufunuo wake ni upi?

Bwana Yesu mwenyewe alitufumbua macho na kutupa ufunuo wa tukio hilo katika kitabu cha Yohana. Anasema;

Yohana 3:14  “Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa;

15  ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye”

Umeona?.. Yule nyoka wa shaba ni mfano wa Yesu Kristo pale msalabani, na wale nyoka ni dhambi iletayo mauti. Hivyo kila mtu anayetumikishwa na dhambi ambayo mshahara wake ni mauti, Akitaka tiba ya hiyo dhambi ni kumtazama Kristo tu.

Kristo kazi yake hakuja kuiondoa dhambi katikati ya jamii yetu, hapana, dhambi ipo ndio maana unaona mpaka leo watu wanaitenda. Alichokuja kukileta ni dawa ya hiyo dhambi. Na sio lazima mtu kupokea uponyaji, ni uchaguzi wa mtu, kuchagua uzima au kifo. Kwa namna ile ile, jinsi wale nyoka walivyoendelea kuachwa katikati ya wana wa Israeli, hawakuondolewa..ili kila mtu ajue kifo kipo na hivyo achague uzima au kifo.

Ndugu usomaye ujumbe huu. Kama hujayakabidhi maisha yako kwa Yesu,  biblia inasema..

Kumbukumbu 30:15 “Angalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya”

Wokovu sio wa kuchaguliwa na mtu, au kuletewa na mtu, ni jukumu la wewe binafsi kuchagua.. Mungu hawezi kulazimisha wokovu uingie ndani yako kama wewe hutaki. Hivyo ni jukumu lako aidha kuchagua kuishi katika dhambi siku zote ambapo mshahara wake ni mauti ya mwilini na rohoni, au umtazame Kristo pale msalabani upate uzima wa milele. Uchaguzi ni wako.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

KWANINI YESU KRISTO NI WA MUHIMU KWETU SASA?

WAPE WATU WANGU RUHUSA ILI WAPATE KUNITUMIKIA.

UMUHIMU WA KUZALIWA MARA YA PILI.

Bwana Yesu alikuwa anamaanisha nini kusema Marko 2:19″walioalikwa harusini wawezaje kufunga maadamu bwana-arusi yupo pamoja nao?”

JE UPENDO WAKO UMEPOA?

Rudi nyumbani

Maashera na Maashtorethi ni nini?

Ashera au kwa jina lingine anajulikana kama Ashtorethi, Ni mungu-mke wa kipagani ambaye alikuwa anabudiwa katika nchi ya wakaanani, Waashuru na mataifa mengine ya kando kando pale mashariki ya kati..

Ashera pamoja na Baali ni moja ya miungu ambayo ilikuwa ni maarufu sana duniani kwa wakati huo.

Katika nchi ya Kaanani walikuwa wanamwabudu katika mfumo wa mti, ambao ulipandwa chini, na kuchongwa katika maumbile ya mwanamke, kumwakilisha yeye. Wakimwona kama ndiye mti wa uzima.

Sasa tunaona katika maandiko, Wana wa Israeli wakiwa bado jangwani Mungu aliwaonya sana, juu ya miungu ya nchi hiyo ya Kaanani wanayoiendea, kwamba wasijichanganye nayo, badala yake wakifika huko  waivunje vunje, na kuiondoa, kwasababu yeye ni Mungu mwenye wivu;

Kutoka 34:12 “Ujihadhari nafsi yako, usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi ile unayoiendea, lisiwe mtego katikati yako.

13 Bali utabomoa madhabahu zao, na kuvunja-vunja nguzo zao, na kuyakata-kata maashera yao.

14 Maana hutamwabudu mungu mwingine, kwa kuwa Bwana, ambaye jina lake ni mwenye wivu, ni Mungu mwenye wivu”.

Lakini tunaona walipofika nchi ya ahadi hilo hawakulizingatia badala yake, nao wao pia wakaanza kuiga desturi za wale wafiisti ambao hawakuwamaliza wote, wakaanza na wao kuabudu Maashera..

2Wafalme 17:9 “Tena, wana wa Israeli wakafanya kwa siri mambo yasiyokuwa mema juu ya Bwana, Mungu wao, wakajijengea mahali pa juu katika miji yao yote, kutoka mnara wa walinzi hata katika miji yenye boma.

10 Wakajisimamishia nguzo na maashera juu ya kila mlima mrefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi”;

Ikafikia hatua mpaka wafalme wengine wakawa sio tu wanaibudia nje kwa siri, bali waliichukua kabisa nguzo zake na kuipeleka katika hekalu la Mungu, mahali ambapo Mungu ameliweka jina lake, watu wamwabudu na kumfanyia dua, wao wanaingiza miungu migeni, Matokeo yake wakamtia Mungu wivu mkubwa zaidi, wakapewa adhabu ambayo isiyosameheka, na adhabu yenyewe ilikuwa kuuliwa, mji kuteketezwa na kuchukuliwa utumwani Babeli.

Mfalme ambaye alifanya kitendo hicho aliitwa Manase;

2Wafalme 21:7 “Akaiweka sanamu ya kuchongwa ya Ashera aliyoifanya ndani ya nyumba, ambayo Bwana alimwambia Daudi, na Sulemani mwanawe, Katika nyumba hii, na katika Yerusalemu, niliouchagua miongoni mwa kabila zote za Israeli, nitaliweka jina langu milele”;

Utasoma habari za maashera katika vifungu hivi;

2Nyakati 14:2,17:6, 19:3, 24:18, 23:14

Je hadi leo kuna maashera yanayoabudiwa?

Hata sasa Mambo hayo yanatendeka katika Kanisa la Kristo hata leo, na cha kusikitisha zaidi ni kuwa wanajua kabisa Mungu amekataza lakini wao wanafanya.

Unapoliweka sanamu la mtakatifu fulani (tuseme bikira Mariamu), na kuanza kulihusianisha na ibada, unaomba kwa kupitia hilo, unaeleza shida zao kwa kutazama sanamu hilo, ujue kuwa unamwabudu Ashera moja kwa moja.

Na tendo hilo linamtia wivu Mungu sana, wivu ambao unaweza kukusababishia mauti.  Ni heri ukutane na hasira ya Mungu kuliko Wivu wake..Kwasababu wivu unakula na hivyo mapigo yake ni makali zaidi.

Wimbo 8:6b..Kwa maana upendo una nguvu kama mauti, Na wivu ni mkali kama ahera.

Biblia inasema tena…

Mithali 27:4 “Ghadhabu ni kali, na hasira ni gharika; Lakini ni nani awezaye kusimama mbele ya wivu”.

Unaona?, shida inakuja ni pale mtu anapoelezwa ukweli kama huu, anadhani dini yake inashutumiwa..Nakwambia ni heri dini ishutumiwe roho yako ipone, kuliko roho iangamie dini yako iendelee kumtia Mungu wivu, faida yake itakuwa ni nini sasa?  Tubu mgeukie Kristo, uokoke. Hizi ni nyakati za mwisho.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

HISIA YA MUNGU ILIYO MBAYA KULIKO ZOTE.

USIIGEUZE NYUMBA YA MUNGU KUWA PANGO LA WANYANG’ANYI.

KUABUDU SANAMU/IBADA ZA SANAMU.

JIEPUSHE NA MANENO YA MANABII WA UONGO.

Nini maana ya uvuvio?.

Rudi nyumbani

MTEGO HUTEGWA BURE, MBELE YA MACHO YA NDEGE YE YOTE.

Shalom, karibu tujifunze maneno ya uzima.. Lipo swali ambalo linaulizwa na watu wengi, kwamba kama Mungu anajua kuna jambo litakwenda kutokea mbeleni ambalo litanisababishia mauti, kwanini basi asinizuie kwenda kulifanya badala yake ananiacha mpaka naingia, na mwisho wa siku napotea na kwenda kuzimu? Mbona kama vile atakuwa sio Mungu wa upendo?

Kama na wewe swali hili lipo ndani yako basi tuzidi kutafakari pamoja somo letu la leo,

Kitabu cha Mithali kinasema..

“Kwa kuwa mtego hutegwa BURE, Mbele ya macho ya ndege ye yote”.( Mithali 1:17).

Embu jiulize, mtu anayetega mtego wa kumshika ndege kwa ajili ya kitoweo chake, Je! Unadhani Mungu hampendi ndege yule? Au unadhani Mungu hajampa uwezo wa kuwakimbia maadui zake kiwepesi?

Au mtu anayetega mtego wa kunasa panya, unadhani Mungu anawachukia panya, na hivyo kawaondolea uwezo wa kuwakimbia adui zao?

Au mtu anayetega ndoano kuvua samaki, unadhani Mungu hawapendi samaki wake,?

Sikuzote mpaka umeona kitu fulani kinaundiwa mitego, basi ujue kuwa kitu hicho kilishashindikana  kukamatika kwa njia rahisi, au ya kawaida, hivyo kimetafutiwa njia mbadala, kwamfano leo hii unaweza kumuona ndege katua hapo pembeni yako, hatua kadhaa tu pembeni, lakini embu kajaribu kwenda kumkamata kwa mikono yako kama utaweza,? Au umwone panya anakatiza kwenye kona ya nyumba, au store, halafu fanya mazoezi ya kwenda kumkata kwa mikono kama vile unavyokamata chura uone kama itakuwa ni kazi rahisi kwako.

Au umwone samaki anaelea juu ya maji, hivyo unatakwenda kwenda kumchota haraka kwa mikono yako, jaribu zoezi hilo kama litakuwa rahisi. Huwezi kuwapata kwasababu Mungu tayari kashawekea uwezo ndani yao wa kujiangua kutoka kwa maadui zao kivyepesi sana.. na wenyewe wanajua kabisa maadui zetu ni ngumu kutushika kwasababu hawana wepesi tulionao sisi, au hawana uhodari tulionao sisi wenyewe.. Na  sisi tunaowawinda tunajua kuwa ili waendelee kuwa salama ni wajibu wao, kutotuamini sisi kwa kitu chochote siku zote za maisha yao hapa duniani, haijalishi tutawavutia kwa vitu vingi kiasi gani wanavyovipenda.

Vivyo hivyo na sisi wanadamu, Mungu ameshatupa uwezo mkubwa sana ndani yetu wa kumshinda adui yetu shetani, na yeye analijua hilo, hawezi kuja na kukukamata hivi hivi kama anavyotaka, hana uwezo huo, anajua kabisa hawezi kukupata, lakini anachokifanya ni kijiundia mitego yake mbalimbali, ambayo hiyo  ikishakunasa, basi  hapo ndipo anakuwa na uwezo wa kukufanya chochote anachotaka ikiwemo hata kukuua.

Kwamfano mtego mmojawapo maarufu , ni uasherati, shetani anaweza kukuletea kahaba, ili mkazini, lengo lake sio ukutane na kahaba au uzini tu halafu basi, hapana, bali  ni ukosane na Mungu wako kwa kitendo hicho, ili apate nafasi ya kuyaachilia mapepo yake yaingie katika maisha yako kukuharibu kirahisi katika kila nyanja, ikiwemo upate na magonjwa ya zinaa kama vile ukimwi ili ufe kabla ya wakati wako.

Lakini hayo anajua hayawezi kuja hivi hivi, ni mpaka akuwekee mtego, ndipo hapo   anakuletea kahaba mzuri, au mwanaume mwenye pesa, anakulaghai na wewe bila kufikiri kuwa ule ni mtego umewekwa mbele yako unakwenda kuuva, ukidhani kuwa Mungu atakuepusha nao.. Hilo Mungu hawezi kulifanya ndugu yangu.

Kwa nafasi yako soma kitabu cha Mithali sura ya 7 yote, uone jinsi, kijana mpumbavu aliyetegwa na mwanamke mzinzi, na hatma yake inavyokuwa; hatuwezi kusoma vyote lakini vile vifungu vya mwisho mwisho vinasema..

Mithali 7:21 “Kwa maneno yake mengi na ulaini akamshawishi, Kwa ubembelezi wa midomo yake akamshinda.

22 Huyo akafuatana naye mara hiyo, KAMA VILE NG’OMBE AENDAVYO MACHINJONI; Au mpumbavu kuadhibiwa katika pingu;

23 Hata mshale umchome maini; KAMA NDEGE AENDAYE HARAKA MTEGONI; Wala hajui ya kuwa ni hasara ya nafsi yake.

24 Basi, wanangu, nisikilizeni sasa, Mkayaangalie maneno ya kinywa changu.

25 Moyo wako usizielekee njia zake, Wala usipotee katika mapito yake.

26 Maana amewaangusha wengi waliojeruhi, Naam, JUMLA YA WALIOUAWA NAYE NI JESHI KUBWA.

27 Nyumba yake ni njia ya kwenda kuzimu, Hushuka mpaka vyumba vya mauti.

Ndege anayenaswa kwenye mtego ni kajitakia mwenyewe na sio kwamba alikuwa ni dhaifu, tamaa zake ndizo zilizompeleka pale,. Leo hii, unapojikuta kwenye matatizo mazito, ambayo unajua kabisa ni kwasababu ya dhambi Fulani uliyoifanya ndio yakakukuta, usianze kumlaumu Mungu ni kwanini hakukuepusha nayo hapo kabla. Mungu alishakupa uwezo huo tangu zamani,  Na Mungu naye hawezi kumlaumu shetani, kwasababu shetani naye analo la kujitetea, anasema mimi sikumuita mtu aje kwenye mtego wangu, wala sikumlazimisha mtu, kufuata kile nilichokiweka kwenye mtego, ni yeye mwenyewe alinifuata, ni ndio hapo akanasikia akaangamia, ilikuwa ni wajibu wake kuchukua tahadhari anapoishi duniani.

Na ndio maana biblia inasema..

Hosea 4: 6 “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa;..”

 Tukikosa maarifa ya kuzijua njama za shetani, au kuyajua mafumbo ya shetani, tutajikuta tunaingia katika matatizo ambayo tutajiuliza ilikuwaje kuwaje tumejikuta hapa,

Ufunuo 2:24 “Lakini nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, wo wote wasio na mafundisho hayo, WASIOZIJUA FUMBO ZA SHETANI, kama vile wasemavyo, Sitaweka juu yenu mzigo mwingine.

25 Ila mlicho nacho kishikeni sana, hata nitakapokuja”.

Hivyo kila mmoja anao wajibu wa kupata maarifa sahihi ya kuitambua mitego ya adui. Na maarifa hayo utayapata kutoka katika Neno la Mungu tu basi, biblia imejaa siri za kuepukana na hila za adui. Na ndio maana shetani hapendi watu waisome.

Kuwa msomaji wa biblia kila siku, tafakari , usiisome kama gazeti, hiyo tu ndio itakayokuwa nuru yako katika zama hizi za kumalizia, kumbuka mitego ni mingi, vishawishi ni vingi, na ipo ya aina tofauti toauti, uwezo umepewa, pengine umepungukiwa tu na maarifa. Hivyo ni wajibu wako kuyatafuta maarifa hayo, ambayo utayapata katika Neno la Mungu. Yaani BIBLIA.

Hakuna jaribu lolote linalotendeka leo hii, ambalo halijawahi kuandikwa katika biblia na njia ya kuepukana nalo., Hivyo jijengee desturi ya kusoma Neno la Mungu. Ili usiwe wa kumlaumu Mungu, kwanini hiki, kwanini kile, wakati ni wewe mwenyewe uliyakataa maarifa, hivyo ukanasika kirahisi.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

UFUNUO NI NINI, NA NITAPOKEAJE UFUNUO KUTOKA KWA MUNGU?

ZIFAHAMU HUDUMA KUU (10) ZA SHETANI DUNIANI.

Uga ni nini? Na kazi yake ni ipi kibiblia?

TAZAMA, NASIMAMA MLANGONI.

Kwanini Mungu awachome watu kwenye ziwa la moto na hali yeye ndiye aliyewaumba?

JINA LAKE KWA KIEBRANIA NI ABADONI, NA KWA KIYUNANI NI APOLIONI.

Rudi nyumbani

UFUNUO NI NINI, NA NITAPOKEAJE UFUNUO KUTOKA KWA MUNGU?

Ufunuo ni kitu kilichofunuliwa.. Maana yake ni kwamba kilikuwa kimefichika/kimefichwa  sasa kimefunuliwa.

Tunaposoma maandiko na kupata kitu kipya ambacho hatukuwa tunakijua hapo kwanza, hapo ni sawa na hicho kitu kimefunuliwa kwetu.

Kwamfano unaposoma biblia kuhusu damu ya Yesu, na ukagundua kitu kipya kuhusu damu hiyo, hicho ulichokipata ndio ufunuo. Sasa hicho ndicho kinachoelezea ukubwa wa Imani yako, Ukipata kujua/kugundua kitu kikubwa zaidi kuhusu damu ya Yesu, ndivyo Imani yako inavyozidi kuwa kubwa. Maana yake ni kwamba kwa ufunuo huo unaweza kutatua matatizo makubwa ya kiroho, au kufanya mambo makubwa, tofauti na yule mtu ambaye bado hajapata ufunuo wowote kuhusu damu ya Yesu.

Na maneno mengine yote ya Mungu ni hivyo hivyo, Ukipata kugundua kitu cha kipekee kumhusu Yesu, ambacho hapo kwanza ulikuwa hukijui.. Hicho ulichokigundua ndicho shetani kinachomwogopesha na ndicho hicho kinachoweza kukupa matokeo makubwa ya rohoni.Na kugundua huko kunaletwa na Roho Mtakatifu mwenyewe ndani ya mtu.

Sasa Ufunuo upo wa uongo, na Pia upo wa ukweli.

Unaweza kusoma neno ukapata kitu au ukagundua kitu ambacho ulikuwa hujakijua hapo kwanza.. Sasa hicho kitu ulichokigundua kama ni cha ukweli (maana yake kama kimetokana na Mungu kupitia Roho wake Mtakatifu) basi kitakubaliana na mistari mingine au habari nyingine za kwenye biblia. 

Lakini kama si cha ukweli basi kitakinzana na mistari mingine ya biblia. Maana yake si cha kukipokea wala kukiamini. 

Sasa ni kwa namna gani tutapokea Ufunuo?. Zipo njia kuu Mbili.

  1. Kwanza ni kwa kulisoma Neno la Mungu:

Wengi hawapendi kulisoma Neno la Mungu wao binafsi, na badala yake wanapenda kufundishwa,  au kutazama filamu fulani tu  za kikristo, Lakini pasipo kujua kuwa kuna hatari kubwa sana ya kudanganywa kama usipojijengea tabia ya kulisoma mwenyewe Neno. 

Kwasababu wanaofundisha uongo ni wengi kuliko wanaofundisha ukweli. Bwana Yesu alisema Njia ni nyembamba, maana yake mimi na wewe hakuna namna tunaweza kuifanya iwe nene, na alisema Manabii wengi wa uongo watatokea watawadanganya hata yamkini walio wateule, hakuna namna tunaweza kuwafanya wawe wachache hawa manabii wa uongo. Kwahiyo Njia itakayobakia kuwa bora siku zote ni ile ya mtu binafsi kutafuta kulisoma Neno yeye binafsi maadamu anao uwezo wa kusoma na kuandika. Na hapo hapo Roho Mtakatifu anapata nafasi ya kumfunulia maandiko.

Na kumbuka tunapozungumzia kusoma Neno hatumaanishi kwenda kuchukua mstari mmoja hapa kwenye Mathayo na kisha kwenda kuruka kutafuta mstari mwingine wa faraja kwenye Isaya, Na kurudi kuunganisha mwingine kwenye Yeremia..na hivyo kujikuta kwa siku umesoma mistari mia, tofauti tofuati kwa masaa mawili na kujipongeza kuwa umelisoma Neno..Nataka nikuambia hapo utakuwa hujasoma biblia bali umeiperuzi biblia, wanaoiperuzi biblia ni wahubiri, na wanafanya hivyo kwa lengo la kufundisha, somo lipate kueleweka kwa muda mfupi. Hivyo wewe usiiperuzi biblia, hutaelewa chochote na wala hutapata kitu cha kudumu cha kukusaidia roho yako.

Kusoma Neno kunakofaa ni huku, kushika kitabu kimoja kimoja…kukisoma chote pasipo kuruka…sio lazima ukisome chote kwa siku moja hapana, Mfano unaweza kuanza kusoma kitabu cha Mwanzo, sura 10 za kwanza na kisha kupata muda mrefu wa kuzitafakari, na hata kuzirudia tena hizo mpaka utakapoona umeelewa vya kutosha kusonga mbele.. lakini ukisoma sura 4, 5 ukafika sehemu inazungumzia vizazi ukaboreka na kisha ukarukia kitabu cha kutoka hutakaa uielewe biblia..

Soma kitabu cha Mwanzo chote kimalize, haijalishi itakuchukua wiki au mwezi, kisha nenda kitabu kinachofuata… Ukifanya hivyo utaielewa biblia sana, na Ndio chanzo kikubwa cha KUPATA UFUNUO WA KWELI wa Neno . Na pia unaposoma biblia, hakikisha unafungua kule nyuma kwenye ramani, uielewe pia ramani kama biblia yako inayo ramani..fuatilia kwenye ramani zile hatua Ibrahimu alizopita, Wana wa Israeli walizopita, miji Bwana Yesu aliyokuwa anatembea n.k.

  1. Njia ya pili ni ile ya Kusikiliza Mahubiri:

Sasa kama tulivyotangulia kusema, Kuna hatari kubwa sana katika kutegemea njia hii kupata ufunuo wa Neno la Mungu. Lakini njia hii ikitumika sahihi pia ni rahisi kupata mengi. 

Sasa njia bora sio kufungulia redio au internet na kwenda kusoma au kusikiliza mahubiri yanayoendelea kila siku, na huku huna habari kabisa na biblia yako, hapo nakuambia utakwenda na maji, haijalishi mhubiri huyo umemwamini kiasi gani.

Njia bora ni ya kupata ufunuo wa Neno la Mungu kupitia watumishi wa Mungu, ni wewe kwenda kusoma Neno kwanza, labda mada fulani katika biblia.. Na kisha ukishaisoma hiyo mada na ukaielewa, isipokuwa kuna vipengele vichache ambavyo hukuvielewa na ungehitaji kuviongezea maarifa, ndipo unamtafuta Mtumishi na kumuuliza kulingana na ile mada uliyoisoma, au unakwenda katika internet na kukitafuta kitu kile, uone maoni ya watumishi mbali mbali kuhusu jambo hilo.

Hiyo ni njia bora ambayo itakusaidia kutokudanganywa kirahisi, kwasababu utakuwa unakwenda kutafuta kujua kitu ambacho tayari una ufahamu nacho angalau kidogo, hivyo ni ngumu kudanganyika…Kamwe usiende kutafuta kuuliza kitu ambacho hata wewe mwenyewe hujui kinapatikana wapi kwenye biblia.

Ni sawa umekwenda kwenye mji uliochanganyikana kama Kariakoo, na kuanza kuuliza uliza, bila ya wewe kuwa na angalau taarifa ndogo ya kile unachokitafuta au unakokwenda, kwasababu kama hujui kabisa ni rahisi kutapeliwa na kupoteza kila kitu ulichonacho..Unaweza kuomba kuelekezwa benki ukaelekezwa kichochoro cha vibaka, ukaibiwa kila kitu hata nauli uliyokuwa umebakiwa nayo.

Ndio maana Bwana Yesu alisema katika Luka..

Luka 8:8 “Jiangalieni basi jinsi msikiavyo; kwa kuwa mwenye kitu atapewa, na yule asiye na kitu atanyang’anywa hata kile ambacho anadhaniwa kuwa nacho.”

Bwana anatuonya tujiangalie jinsi TUNAVYOSIKIA.  Maana yake ukienda kutafuta kusimuliwa vitu bila wewe mwenyewe kutafuta kusoma kile kitu kwanza, angalau kidogo, kuna hatari kubwa ya wewe kupoteza kila kitu hata kile kidogo kizuri ulichokuwa nacho moyoni mwako. Ni rahisi hata kama kulikuwa na kitu cha ukweli moyoni mwako, ni rahisi kukipoteza hicho, Kwasababu utakayekutana naye kama atakuwa ni mwalimu au nabii wa uongo, atakutoa kabisa kwenye mstari (huko ndio kunyang’anywa hata kile kidogo ulicho nacho).

Kwamfano unakwenda kumuuliza Mwalimu/Nabii (wa uongo) kuhusu habari fulani kwenye biblia ambayo ulisikia tu watu mtaani wakisimuliana, ili hali wewe hujawahi hata kwenda kuifuatilia kwenye biblia inasemaje, yule nabii atakudanganya, na wewe utamwamini..na zaidi ya hayo, kama pia kama ulikuwa unaamini kuwa si sahihi kuoa wake wengi, huyo nabii atakupa maandiko na maandiko pia ya kukuambia ni ruksa kuoa wake wengi, na wewe utamwamini. Pasipo kujua kuwa tayari umeshanyang’anywa hata kile kidogo ulicho nacho.

Roho Mtakatifu anataka kutufundisha mengi, lakini sisi ndio hatutaki kumpa nafasi ya yeye kutufundisha, kwasababu tunakuwa wavivu wa kusoma (Waebrania 5:11). Tujitahidi kumpa nafasi.

Bwana atubariki.

Kama hujampokea Yesu, Basi fahamu kuwa ANARUDI. 

Waebrania 10:37  “Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia”.

Hivyo mkaribie leo naye atakukaribia.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

JIFUNZE NENO LA MUNGU KWA BIDII ZOTE.

Uga ni nini? Na kazi yake ni ipi kibiblia?

MWILI NA DAMU YA YESU KRISTO.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 10 (Kitabu cha Zaburi).

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Rudi nyumbani