MALIPO YA UPOTEVU.

MALIPO YA UPOTEVU.

Upotevu una malipo. Pale mtu anapoufahamu ukweli, lakini hataki kuufuata, pale mtu anaposikia kila kukicha acha dhambi, mpe Yesu Maisha yako, dunia hii inakwenda kuisha, dalili zote zinaonyesha, magonjwa ya Tauni Bwana Yesu aliyoyazungumzia kuwa yatatokea nyakati za Mwisho yanaonekana sasa, watu kupenda pesa, watu kupenda anasa kuliko kumpenda Mungu yanaonekana sasa ulimwenguni kote, tetesi za vita, manabii wa uongo kuzuka, Injili kuhubiriwa ulimwenguni kote, Israeli kama mtini kuchipuka tena, yote hayo yameshatimia lakini ni kama kelele kwake..

Mpaka sasa hakuna mtu anayejiita mkristo ajiyejua kuwa tunaishi katika siku za kumalizia, dakika za majeruhi, majira ya parapara kulia, na lakini mtu huyo huyo anayeyafahamu hayo yote hataki kuchukua hatua yoyote rohoni mwake, anaposikia injili anaona ni kama ya watu fulani hivi waliokata tamaa ya Maisha wajulikanao kama walokole, kila siku anasema moyoni “nita”….“nita” nitaacha siku moja, nitatubu siku moja, na huku bado anatazama picha za ngono mitandaoni, anazini, anajijua kabisa yupo upotevuni, lakini bado anaendelea kufanya hivyo, na kusahau kuwa Upotevu huo ulio ndani yake unao malipo yake..

Na malipo yenyewe, sio yale ya kwenda motoni hapana, kabla hujafika huko, Mungu anachofanya kwanza katika Maisha haya ni kukuacha..Ni heri ukaachwa na ulimwengu mzima lakini sio kuachwa na Mungu..ukishaachwa tu wakati huo huo maroho mengine mabaya ya kuzimu yanakuingia, na ndio hapo unajikuta kiwango chako cha kufanya maasi kinaongezeka mara mbili Zaidi, kama ulikuwa ni mwasherati hutaishia kufanya na jinsia tofauti tu, utafika kutamani hata jinsia ya aina yako, au viumbe vingine, au vitu vingine,..hayo ndio malipo ya uovu wako..

Warumi 1:26 “Hivyo Mungu ALIWAACHA wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili;

27 wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, WAKAPATA NAFSINI MWAO MALIPO YA UPOTEVU wao yaliyo haki yao”.

Hapo mstari wa 27 unasema.. wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao..Unadhani walioishia kuwa mashoga walianzia wapi? Walianzia kwenye dhambi ya uzinzi na uasherati lakini wakakataa kumtii Mungu alipokuwa anaugua ndani ya mioyo yao, wakapata malipo ya upotevu wao..Vivyo hivyo na dhambi nyingine zote, huwa zinakwenda hatua nyingine iliyo ovu Zaidi, kama mtu huyo hatataka kumtii Mungu na kubadilika..

Biblia pale inaendelea kusema..

“28 Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa.

29 Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na tamaa na ubaya; wamejawa na husuda, na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya,

30 wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye kutakabari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao,

31 wasio na ufahamu, wenye kuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema;

32 ambao wakijua sana hukumu ya haki ya Mungu, ya kwamba wayatendao hayo wamestahili mauti, wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao”.

Ndugu tumtii Yesu Kristo ambaye alituokoa bure kwa damu yake. Anatuwazia mawazo yaliyo mema, ikiwa tutamwamini na kutubu dhambi zetu kwa kumaanisha kuziacha yeye mwenyewe atatusafisha na kutusamehe kabisa na kutufanya kuwa wapya tena haijalishi tulimkosea namna gani..

Hivyo Ikiwa leo hii utahitaji kumpa Yesu Maisha yako, basi uamuzi unaoufanya ni wa busara sana ambao hautakaa uujutie maisha yako yote kama ilivyokuwa hata kwetu sisi. Unachopaswa kufanya, hapo ulipo, chukua muda mchache ujitenge peke yako. Kisha piga magoti, kisha fuatisha sala hii kwa Imani, ukijua kuwa Mungu yupo hapo karibu na wewe pembeni yako kukusikia..Kisha ukiwa sasa katika utulivu Sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, . NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Sasa ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani ..Hatua iliyobakia kwako ni kuithitisha toba yako kwa Vitendo ikiwa ulikuwa unafanya mambo yote ambayo hayampendezi Mungu unayaacha na kujitenga nayo, Sasa Mungu akishaona umegeuka kwa vitendo basi toba yako anaipokea na atakuja ndani yako wakati huo huo na kufanya makao ya milele kwako. Vile vile unahitaji, kutafuta kanisa la kiroho ambalo utajumuika na wakristo wengine katika kumwambudu Mungu katika roho na kweli, na kujifunza biblia ili uukulie wokovu. Na vilevile ili upate ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la YESU KRISTO kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako.

Fanya hayo yaliyo ya msingi na yaliyosalia Bwana atashughulika nayo maishani mwako.

Ubarikiwe sana

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

NDUGU,TUOMBEENI.

MTANGO WA YONA.

HAKI HAIMWACHI KUISHI.

Mbona Mungu anaruhusu watu wapate shida, ilhali ana uwezo wa kutuepusha?

MAOMBI YA YABESI.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments