HAKI HAIMWACHI KUISHI.

HAKI HAIMWACHI KUISHI.

…Japokuwa ameokoka katika bahari,haki haimwachi kuishi…


Ikiwa wewe ni mtoto wa Mungu, unapaswa ujue kuwa kuna wakati sio mambo yote yataenda vizuri kama unavyofikiri, Hilo ni vizuri ukaliewa kwasababu watu wengi wameishia njiani na kuona kama wokovu ni mgumu wakidhani kuwa ndio utaendaelea kuwa hivyo hivyo wakati wote.

Biblia ni kitabu ambacho kimeturahisishia kuielewa vizuri hii njia ya imani, kiasi kwamba yale ambayo tunaona kama sisi ndio wa kwanza kuyapitia, Kumbe tayari wengine walishayapitia zamani sana huko nyuma, na hivyo Habari zao zikaandikwa ili kututia moyo na kutupa nguvu sisi tuliotokea huku mwishoni.

Sasa tusipokuwa watafakariji wazuri wa maandiko namna hiyo, hapo ndipo shetani anapata njia rahisi ya kutuangusha katika hatua za awali kabisa za wokovu wetu.

Leo tutakiangazia kile kisa cha Mtume Paulo, baada ya kufungwa na kusafirishwa kupelekwa Rumi kutoka Yerusalemu, sasa Ili kuifanya Habari kuwa fupi, ni kwamba safari ile ilikuwa ni ya kufa na kupona, bahari iliwachafukia katikati ya vilindi, dhorubu kali iliwakumba, kaisi kwamba hawakuona jua wala nyota kwa siku nyingi..Yeye akiwa kama mmojawapo wa mfungwa, wakiwa wameishiwa chakula kutokana na kwamba shehena nyingi za hazina zilitupwa baharini ili kuifanya meli iwe nyepesi, sasa wakiwa katikati ya njaa kali ,anasema walifikia hatua wakakata tamaa ya kuokoka.. kwa jinsi hali ilivyokuwa mbaya, mpaka kuvunjikiwa meli yao, na kunusurika kibahati bahati kwa neema za Mungu..(Soma Habari hiyo yote katika Matendo 27&28).

Lakini walipofika kwenye kisiwa kimoja walichotulia, wakiwa wamepewa hifadhi kwa muda na wenyewe wa pale, wakati wa usiku wanaota moto, Paulo akiwa ameshika mzigo wa kuna, ghafla akatokea nyoka (jamii ya kifutu), akajifiringisha na kujikaza kwa nguvu mkononi mwake, Wenyeji kuona vile wakasema huyu ni lazima atakuwa Muuaji tu, japokuwa kanusurika kule baharini, lakini haki haimwachi aishi, ..Tusome..

Matendo 28:3 “Paulo alipokuwa amekusanya mzigo wa kuni, na kuuweka motoni, nyoka akatoka kwa ajili ya ule moto akamzonga-zonga mkononi.

4 Wenyeji walipomwona yule nyoka akilewa-lewa mkononi, wakaambiana, Hakosi mtu huyu ni mwuaji; ambaye ijapokuwa ameokoka katika bahari haki haimwachi kuishi.”

Jaribu kutengeneza picha, jinsi Paulo alivyokuwa anaonekana mbele za watu wakati huo, kwasasa watu wanaweza kusema, Ana Nuksi huyu, ana mikosi, ni laana za wazazi wake zinamwandama, au za ukoo.. haiwezekani apitie shida tu yeye sikuzote..

Kwanini afilisike, kwanini nyumba yake iinguliwe na moto, kwanini aibiwe mali zake, kwanini afiwe na Watoto wake wote watatu kwa mpigo.. Kama Mungu yupo naye, si angemuepusha na mambo hayo yote? Mungu gani huyo.. Kwanini akose mahali pa kulala, n.k.n.k.

Maneno mengi sana yanaweza kuzuka, kwa njia hizo, Lakini Paulo alipoumwa na nyoka yule mwenye sumu kali, kwasababu nyoka wale wanakufanya uvimbe kwa haraka, na baadaye damu inaganda, na kisha kukutwa na kifo cha ghafla kama hutawahishiwa matibabu.. Lakini Paulo hakuhitaji matibabu yao, bali alimtupa motoni akatulia kimya..

Muda ukapita, masaa yakapita, siku ikapita wakaona mbona havimbi, mbona haonyeshi hata dalili ya kuumwa.. Ndipo zile shutma zao zikageuka kuwa kitu kingine.

Matendo 28:5 “Lakini yeye akamtukusia motoni asipate madhara.

6 Wao wakadhani ya kuwa atavimba au kuanguka chini kwa kufa ghafula; na wakiisha kumwangalia sana, na kuona kwamba halimpati dhara lo lote, wakageuka, wakasema kwamba yeye ni mungu”.

Jambo tunalopaswa tujifunze (Sisi kama watakatifu), ni kuwa si kila tatizo ni Mkosi, au laana, au mapigo wala matokeo ya uchawi..…

Hapana, mengine Mungu anayaruhusu tu, kwasababu lipo kusudi anataka kulipitisha nyuma yake.. Kama Paulo asingeumwa na nyoka , wasingemwamini pale alipokuwa anawahubiria Habari za Kristo na uponyaji wa kiungu. Lakini kwa tukio lile baada ya muda Mungu alitukuzwa.

Vivyo hivyo na sisi, tukijijua maadamu hatuna tatizo lolote na Mungu wetu, basi tutulie kimya tuiache mitazamo ya watu ipite, lakini wakati utafika watagundua kuwa haukuwa na nuksi, au mkosi, bali ulikuwa katika njia ya mafanikio yako rohoni.

Lakini ikiwa wewe ni mwenye dhambi, hilo ni jambo lingine. Hapo Mungu hausiki, ni vizuri ukampa Kristo Maisha yako, shetani hana urafiki na wewe, ukifa leo mwisho wako utakuwa ni kuzimu na ndicho anachokitafuta na kukifurahia..Biblia inasema..

1Petro 4:18 “Na mwenye haki akiokoka kwa shida, yule asiyemcha Mungu na mwenye dhambi ataonekana wapi?”

Jiulize utaonekania wapi siku ile? Kama leo hii hutampokea Kristo?

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

 

YA KALE YAMEPITA, TAZAMA YAMEKUWA MAPYA

Mtu astahiliye hofu ni yupi?

KILA KIUNGO LAZIMA KISHUGHULIKE.

WAKAKAA KWAKE SIKU ILE. NAYO ILIKUWA YAPATA SAA KUMI.

KWANINI TUNAPASWA TUJIZUIE?

TAHADHARI YA NEEMA YA MUNGU.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments