Title April 2023

TUUTAFUTE USEMI MMOJA. TUUJENGE MNARA WA MUNGU

Nakusalimu katika jina tukufu sana la mwokozi wetu Yesu Kristo, Nakualika katika kuyatafakari maneno ya uzima.

Leo tutajifunza siri mojawapo iliyokuwa nyuma ya watu wa zamani, ambayo tukiitumia na sisi italeta mageuzi makubwa sana katika ulimwengu huu tunaoishi. Wengi wetu tunadhani watu wa leo wanayoakili zaidi ya kuwashinda wale, lakini ukweli ni kwamba yapo mambo mengi yalifanywa na watu wa kale, ambayo mpaka leo hatuwezi kuyafanya. Mfano mmojawapo ni yale mapiramidi yaliyopo Misri (ambayo yapo katika maajabu saba ya dunia), teknolojia iliyotumika pale, hadi sasa hakuna ujenzi unaoweza kuwa kama ule, ijapokuwa tunazo teknolojia kubwa na za kisasa.

Tukisoma katika maandiko tunaona, Jinsi Babeli ilivyoanza kujengwa na kusitawi. Lakini hilo halikuwa jambo zito, kwasababu miji mingi pia ilikuwa inajengwa. Jambo lililoipelekea Babeli kuwa tofauti na miji mingine ni pale watu walipotaka kuunda Mnara, ndani ya mji ule, lengo lao likuwa ni kufika MBINGUNI, ili wajipatie jina. Sasa wengi wetu tunaona kama walikuwa ni wajinga kuunda hiyo Projekti yao. Tunadhani walikuwa wanafanya jambo la masiara au walikuwa hawaelewi kitu wanachokifanya. Ni sawa na leo mtu akumbie ninaunda ndege, ambayo itanifikisha mbinguni, ni rahisi kusema amerukwa na akili. Lakini maandiko yanatuonyesha watu hawa, walikuwa wanajua wanachokifanya mpango huo wangeweza kufanikiwa kama Mungu asingeingilia kati. Embu tusome habari hiyo tuombe jambo hilo;

Mwanzo 11:1 “Nchi yote ilikuwa na lugha moja na usemi mmoja.  2 Ikawa watu waliposafiri pande za mashariki waliona nchi tambarare katika nchi ya Shinari; wakakaa huko. 

3 Wakaambiana, Haya, na tufanye matofali tukayachome moto. Walikuwa na matofali badala ya mawe, na lami badala ya chokaa.  4 Wakasema, Haya, na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike mbinguni, tujifanyie jina; ili tusipate kutawanyika usoni pa nchi yote. 

5 Bwana akashuka ili auone mji na mnara waliokuwa wakiujenga wanadamu.  6 Bwana akasema, Tazama, watu hawa ni taifa moja, na lugha yao ni moja; na haya ndiyo wanayoanza kuyafanya, WALA SASA HAWATAZUILIWA NENO WANALOKUSUDIA KULIFANYA. 

7 Haya, na tushuke huko, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao.  8 Basi Bwana akawatawanya kutoka huko waende usoni pa nchi yote; wakaacha kuujenga ule mji.  9 Kwa sababu hiyo jina lake likaitwa Babeli; maana hapo ndipo Bwana alipoichafua lugha ya dunia yote; na kutoka huko Bwana akawatawanya waende usoni pa nchi yote”.

Umeona hapo? Mungu hakusema hawa watu wamerukwa na akili, wanafanya kazi isiyokuwa na faida, bali alisema hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya. Maana yake ni kuwa watafanikiwa, Hivyo Mungu akaangalia NGUVU yao ya kufikia adhma yao ipo wapi? Akaona kuwa sio katika ile teknolojia, bali katika ule USEMI MMOJA waliokuwa nao.

Usemi maana yake ni NIA. Hawa watu waliingia maagano,wakapatana kwa moyo mmoja, kwamba kila mmoja atajitoa kwa akili, hali na mali, kuhakikisha Mnara huo unajengeka na kilele chake kinafika mbinguni, hata kama itawagharimu miaka 1000, lakini mwisho wa siku ni lazima wafike mbinguni. Lakini Mungu akaenda kuuchafua usemi wao wakawa hawaelewani baada ya pale, kwasababu walichokuwa wanakijenga ni kwa ajili ya JINA LAO na sio jina la MUNGU. Hivyo Usemi wao ukachafuliwa wakawa hawaelewani, mpaka na lugha zao zikageuzwa pia.

Ni nini Bwana anataka tuone hapo,

Ni nguvu ya USEMI MMOJA.

Na sisi kama kanisa la Kristo lililo hai. Nafasi yetu ya kuufikia utukufu WOTE wa Mungu ulio mbinguni tunao.

Kwasababu Tayari siku ile ya Pentekoste, Roho Mtakatifu alirudisha USEMI HUU mmoja katikati yetu. Na ndio maana siku ile utaona watu walianza kunena kwa lugha za mataifa mengine magheni, kuonyesha kuwa Sasa Mungu anataka mataifa yote wakaribie waliunde taifa la Mungu haijalishi lugha zao, jinsia zao, rangi zao. Alikuwambusha tukio lile la Babeli, kwamba sasa lianze kufanyika tena kwa jina la Bwana.Watu wale wakatii na siku ile ile kanisa likaanza. Mnara wa Mungu ukaanza kujengwa duniani.

Matendo 2:1  “Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja.

2  Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. 3  Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.

4  Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka. 5  Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu. 6  Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe.

7  Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? 8  Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? 9  Warparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia.

10  Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu,.11  Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.

12  Wakashangaa wote wakaingiwa na shaka, wakiambiana, Maana yake nini mambo haya?

Na ndio maana hatushangai kwanini Kanisa la kwanza lilikuwa na mapinduzi makubwa sana. Kwa kipindi kifupi sana injili ilinea duniani kote, na walikuwa hawana vyuo vya biblia. Ni kwasababu walikuwa na USEMI mmoja.

Lakini leo kanisa limevunjika vunjika, shetani kalisambaratisha, kachafua lugha yetu. Hata ndani ya kanisa moja kila mmoja anao usemi wake. Ijapokuwa wote mnaliamini Neno hilo hilo moja. Kwasababu gani, ni kwasababu tunatafuta utukufu wetu wenyewe na sio ule wa Mungu.

Ni kweli tutaunganishwa na Neno lakini tusipotaka kujishusha na kutii, ili tumwinue Kristo na sio sisi wenyewe, kamwe hatutaona utukufu wa Mungu kama vile inavyopaswa. Hatutaufikia moyo wa Mungu mbinguni, hatutaona udhihirisho wa wazi wa Miujiza mikubwa ya Mungu katika kanisa. Ni sharti tujikane nafsi zetu kila mmoja tumfuate Yesu , ili tuujenge mnara huu wa Bwana.

Luka 14:27  “Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. 28  Maana ni nani katika ninyi, KAMA AKITAKA KUJENGA MNARA, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? 29  Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki”.

Tufahamu kuwa kanisa sio shirika la kijamii, sio huduma, wala sio chuo Fulani, bali ni udhihirisho wa Mungu duniani kupitia watu wake aliowakomboa. Hivyo ni lazima sisi kama viungo vya Kristo tujishikamanishe tuwe mwili mmoja Ili Kristo atende kazi zake duniani kama alivyokuwa anatenda zamani. Na hii inaanza na mtu mmoja mmoja, pale tunapodhamiria kuyatii maneno ya Kristo.

Bwana atujalie kuliona hilo.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Mada Nyinginezo:

NITAUVUTAJE UWEPO WA ROHO MTAKATIFU KARIBU NAMI?

Je kunena kwa Lugha mpya kukoje?

Pentekoste ni nini?

NI NINI TUNAJIFUNZA KWA YOANA NA MANAENI?

USIIKARIBIE DHAMBI, KAA NAYO MBALI.

Kibiriti ni kitu gani? kama kinavyozungumziwa kwenye maandiko?

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

Rudi nyumbani

Print this post

Nini tofauti ya kushuhudia na kuhubiri?

Jibu: Kushuhudia kunatokana na neno “Ushuhuda”. Mtu anayetoa taarifa ya jambo fulani alilolishuhudia au aliloshuhudiwa basi hapo anatoa ushuhuda.

Kwamfano mtu anaweza kuona ajali ya gari na akaenda kuwaelezea watu wengine tukio zima jinsi lilivyokuwa, hapo ni sawa na ametoa ushuhuda au amewashuhudia watu ajali ile.

Vile vile katika Ukristo, mtu anayewaelezea wengine mambo aliyoyaona au kuyasikia kumhusu Yesu…yani wema wake aliomtendea, au aliowatendea watu wengine, hapo ni sawa na kusema anawatolea ushuhuda au anawashuhudia wengine habari za Yesu.

Lakini tukija katika neno “Kuhubiri”…lenyewe ni neno pana linalojumuisha kushuhudia, kufundisha, kuonya, na kutoa maoni.

Kwamfano mtu aliyeshuhidia tukio la ajali ya gari na akaenda kulielezea/kulishuhudia kwa watu.. na baada ya hapo akaanza kutoa mafundisho na tahadhari kuhusiana na ajali kama hizo na jinsi ya kuziepuka..mtu huyo anakuwa ameihubiri ile habari za ajali.

Vile vile mtu anayeenda kutoa ushuhuda wa wema wa Yesu na habari za kufa na kufufuka kwake na mwishoni akaanza kuelezea faida za kumpokea Yesu, na hasara za kutompokea…ni nini Yesu anataka na nini hakitaki…Mtu huyo anakuwa amevuka kutoka hatua ya kushuhudia mpaka ya kuhubiri.
Na sisi kama wakristo ni lazima tuzishuhudie habari za Yesu na pia tuzihubiri

2 Timotheo 4:5 “Bali wewe, uwe na kiasi katika mambo yote, vumilia mabaya, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiliza huduma yako”

Maran atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Je kauli ya Bwana Yesu inajichanganya? Katika Yohana 8:14 na Yohana 5:31?

UTARATIBU WA KUTOA FUNGU LA 10 UPOJE?.

KUOTA AJALI, KUNAMAANISHA NINI?

Je! Mungu anasababisha ajali au Majanga?

Karama ya pili inayozungumziwa katika 2Wakorintho 1:15 ndio ipi?

Rudi nyumbani

Print this post

Ni sahihi kwa mkristo kupokea fedha kutoka kwa mtu anayefanya kazi haramu?

Je! ni sahihi kwa mkristo kupokea fedha kutoka kwa mtu anayefanya kazi haramu kama za uuzaji wa dawa ya kulevya, wizi au bangi?

Jibu: Kama wewe ni mtu uliyeokoka, aidha mchungaji, au mwalimu, au muimbaji au mshirika wa kawaida, sio sahihi kupokea fedha zozote kutoka kwa mtu anayefanya kazi haramu kama za ujambazi au wizi, au uuzaji wa madawa ya kulevya, kwasababu kwa kufanya vile ni sawa na kushiriki zile kazi.

Kwasababu huwezi kupenda fedha za mtu mwovu, halafu ukachukia na kazi zake.. Huwezi kupenda boga halafu ukachukia ua lake.. Mpaka umekikibali kitu maana yake tayari umekikubali na chanzo chake..

Hivyo kama utapokea fedha kutoka kwa mtu anayeuza madawa ya kulevya, au jambazi, tayari moja kwa moja umehakikia chanzo chake na kukikubali!, lakini kama umekikataa chanzo chake pia huwezi kukubali matunda ya chanzo hicho, Kama Bwana Yesu alivyosema katika…

Luka 6:43 “Kwa maana hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala mti mbaya uzaao matunda mazuri;

44  kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana, katika miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu”

Kwahiyo kibiblia sio sahihi kwa mtu aliyeokoka kupokea fedha kutoka kwa mtu anayefanya kazi haramu, aidha kwa lengo la kuendeleza huduma, au kwa lengo la kujiendeleza yeye mwenyewe. Ni sharti kwanza mtu huyo ageuzwe njia zake kwa kumpokea Yesu kikamilifu na kubadili kazi yake hiyo kwa kufanya kazi halali, ndipo fedha zake ziwe safi. (Hapo atakuwa ameufanya mti wake kuwa mzuri na matunda yake kuwa mazuri)

Na sio tu kupokea, vilevile watu hao wafanyao kazi haramu kibiblia hawaruhusiwi kuzipeleka fedha zao kama sadaka au zaka katika nyumba ya Mungu, kwani ni machukizo makubwa sana..

 Mithali 15:8 “Sadaka ya mtu mbaya ni chukizo kwa Bwana; Bali maombi ya mtu mnyofu ni furaha yake”.

Soma pia Kumbukumbu 23:18 na Mithali 21:27.

Kwahiyo ni lazima kuvifanya vyanzo vyetu kuwa safi, ndipo na matunda ya vyanzo hivyo yawe safi, lakini kama vyanzo ni vichafu hata matunda yake yatakuwa machafu tu, kwa anayetoa na anayepokea. Ndio maana asilimia kubwa ya wanaopokea fedha kutoka kwa watu wanaofanya biashara haramu, zile fedha wanazozipokea ni lazima zitakuja kuwaletea madhara kwa namna moja au nyingine, kwasababu zinakuja na roho na maagizo ya ibilisi nyuma yake.

Bwana atusaidie.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Mwana haramu ni nani kibiblia? (Kumbukumbu 23:2).

Nini maana ya “kila tendo lisilotoka katika imani ni dhambi?”

KANUNI RAHISI YA KUPOKEA BARAKA MARA DUFU.

JINSI YA KUMSIKIA MUNGU, NA KUPOKEA MAFUNUO AU JUMBE KUTOKA KWAKE.

Atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani? Maana yake nini?

Rudi nyumbani

Print this post

Bawa la mbuni hufurahi; Lakini mabawa yake na manyoya yake, je! Yana huruma? 

SWALI: Nini maana ya haya maneno Mungu aliyomwambia Ayubu kuhusiana na  tabia za Mbuni?

Ayubu 39:13 Bawa la mbuni hufurahi; Lakini mabawa yake na manyoya yake, je! Yana huruma?  14 Kwani yeye huyaacha mayai yake juu ya nchi, Na kuyatia moto mchangani,  15 Na kusahau kwamba yumkini mguu kuyavunja, Au mnyama wa mwitu kuyakanyaga.  16 yeye huyafanyia ukali makinda yake, kana kwamba si yake; Ijapokuwa taabu yake ni ya bure, hana hofu;  17 Kwa sababu Mungu amemnyima akili, Wala hakumpa fahamu.  18 Wakati anapojiinua juu aende, Humdharau farasi na mwenye kumpanda. 


JIBU: Ukianzia kusoma mistari michache ya juu katika hiyo hiyo  sura  ya 39, Utaona Mungu anamweleza Ayubu baadhi ya wanyama ambao wanauwezo fulani mkubwa lakini hauwasidii kufanya mambo ya msingi, kwamfano mstari wa 5-8, anamtaja punda-milia, ni mnyama anayefanana na punda, ana nguvu na uwezo wa kukimbia zaidi hata ya punda, lakini je! Anamuuliza Ayubu unaweza kumkamata na kumfanya mtumwa wako akubebe mizigo? Au akulimie. Jibu ni la!

Mstari wa 9-12, anamtaja tena, Nyati, anamsifia nguvu zake, kwamba ni nyingi sana, lakini je utaweza kumfunga nira na kumwambia akulimie shamba lako kama ufanyavyo kwa ng’ombe? Jibu ni la kwasababu jambo hilo halipo ndani yake.

Na hapa kwenye mstari wa 13-18 Anamtaja tena Ndege mbuni na sifa zake. Anasema mabawa yake ni bora na mazuri, kiasi cha kuweza kuyatamia vema mayai ardhini zaidi ya ndege wengine wote duniani. Lakini kinyume chake ni kuwa mbuni ni ndege asiyejali mayai wala vifaranga vyake kuliko ndege wote unaowafahamu. Japokuwa anaouwezo mkubwa wa kuwashinda maadui zaidi ya ndege wote, lakini uwezo wake hautumii katika mambo yaliyo na faida. Mbuni anataga popote tu, hata kando ya njia,

hawezi kutafuta sehemu iliyo salama kama ndege wengine ambao huenda sehemu za maficho na kutaga huko ili watoto wao wawe salama pindi wazaliwapo lakini yeye hilo halijali, anataga popote apaonapo, matokeo yake ni aidha mayai yake kukanyagwa na wanyama wakubwa au kuibiwa na kenge au wanyama wengine wezi. Mbuni anaouwezo wa kutaga mpaka mayai 60 na kutamia yote yakatotolewa, lakini kwa tabia yake ya kutokujali anaweza kuambulia vifaranga viwili au vitatu tu. Anaweza kuyasahau mayai yake mchangani, jua au joto la mchangani likamsaidia kotolesha.

Na akishazaa, watoto wake awahudumii, kama wafanyavyo ndege wengine wadogo, ambao huakikisha wanazunguka huko na huko kutafuta vyakula vya watoto wao. Lakini bado maandiko haya yanaonyesha jinsi gani alivyomshapu kuliko hata farasi. Mwendo wa mbuni unauzidi mwendo wa farasi yoyote duniani. Kuonyesha jinsi alivyo mwepesi kujipigania lakini sio watoto wake.

Ni nini Mungu alikuwa anamwonyesha Ayubu ni kwamba, uwezo wa kufanya jambo Fulani sio tija ya mtu huyo kulitenda, kama Mungu hakumpa moyo huo. Wapo wenye mali nyingi, lakini hawana moyo wa kusaidia wanyonge, wapo wenye vipawa vizuri lakini hawezi kumwimbia Mungu. Nguvu zao ni bure hazina faida, wapo wenye uwezo wa kufundisha lakini hawewezi kujinyenyekeza chini ya makusudi ya Mungu watumiwe ili kuujenga ufalme wa Mungu, wanakuwa tu kama punda-milia wa nyikani.

Wapo wenye uwezo wa kulichunga kundi la Mungu lakini wanakuwa kama mbuni, nguvu zao, ukubwa wao hauwasaidii katika kujali kazi ya Mungu. Lakini Bwana akikupa moyo huo, basi utafanya hata kama utakuwa ni dhaifu, utafanya tu. Na hili ndio jambo ambalo tunapaswa tumwombe Bwana . ATUPE MOYO WA KUMTUMIKIA YEYE. Tusitazame kwamba mpaka tupate kitu Fulani ndio tuweze, mpaka tukasomee uchungaji ndio tuweze kuchunga, mpaka tupate pesa ndio tuweze kuisapoti kazi ya Mungu, Bwana atupe moyo huo tangu sasa wakati hatuna uwezo wowote. Kwani huo ndio utakaotusukuma kufanya makubwa.

Lakini pia yapo mambo matatu tunaweza kujifunza:

Jambo la kwanza ni sisi wenyewe, tusiwe kama mbuni ambao hatujali kuhudumia vinavyozalika ndani ya roho zetu. Kwa kutengeneza viota vyetu mahali salama,kinyume chake tunamwachia shetani azichukue mbegu zetu rohoni zinazopandwa, tunaziacha juu juu na matokeo yake ibilisi anakuja kuzila sawasawa tu na mfano wa mpanzi ambao Yesu aliutoa juu ya zile mbegu zilizoangukia njiani ndege wakazila. Ndivyo ilivyo maisha ya wengi, wanapolisikia Neno la Mungu badala walitunze na kulipalilia ndani yao  ili liwazalie matunda wao wanazembea tu, wanaishi kama wanavyotaka. Hivyo tunakuwa wapumbavu kama mbuni, kwa kutokuzalisha chochote.

Jambo la pili: Linahusu familia: Wazazi wasiowajali watoto wao, Ni wajibu kwa mzazi kuwatunza wanawe, kwa kuwahudumia kimwili na kiroho. Imekuwa rahisi leo hii wazazi kujali sana Elimu za watoto wao jambo ambalo ni zuri, lakini kuhusiana na maisha yao ya kiroho wamewaweka nyuma . Hiyo ni hatari kubwa sana, usipompa Mungu watoto wako awalee, shetani atakusaidia kuwaelea. Na matokeo yake utayaona baadaye watakapokuwa watu wazima. Kama mzazi jali sana maisha ya kiroho ya watoto wako, wapeleke Sunday school, wapeleke katika semina za watoto kanisani, wahubirie, wafundishe kuomba, kufunga, kuimba nyimbo za wokovu n.k.

Jambo la tatu: Ni kuhusu watumishi wa Mungu. Bwana hataki tuwe kama Mbuni katika eneo la kulichunga kundi lake. Tunachowaza ni kujijali sisi tu, lakini kuwafuatilia na kuwachunga kondoo wa Bwana tunaona uvivu. Tunasahau kuwa shetani huko nje! Anafanya kazi usiku na mchana kuwarudisha tena ulimwenguni. Hivyo ni angalizo kwetu sisi watumishi wa Mungu. Popote ulipo hakikisha unalilisha na kulichunga kundi la Mungu dhidi ya Yule mwovu. Tuwe na hekima za ‘chungu’

Bwana akubariki sana.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Hawa ndege katika Walawi 11:13-19 ndio ndege gani kwasasa?

NI NINI KINATOKA KINYWANI MWA MTOTO WAKO?

“Humfukuza punda wake asiye baba”, nini maana ya mstari huu? (Ayubu 24:3)

HUDUMA YA (ELIFAZI, SOFARI, NA BILDADI).

Kuvyaza ni nini katika biblia? (Ayubu 21:10).

KWANINI NI NUHU, AYUBU NA DANIELI?

Marijani ni nini katika biblia(Ayubu 28:18,Mithali 8:11)?

Santuri ni nini? (Danieli 3:5,10)

HUTATAMBUA LOLOTE, SIKU YA UNYAKUO IKIFIKA.

Rudi nyumbani

Print this post

Je! Bwana Yesu alisulubiwa juu ya msalaba au juu ya mti uliokuwa wima?

Swali: Katika Wagalatia 3:13 maandiko yanasema Bwana Yesu alisulubiwa juu ya mti, lakini tukirejea tena Yohana 19:19, tunaona biblia inasema Bwana alisulubishwa juu ya msalaba.. je maumbile ya huo msalaba au huo mti yalikuwaje?.. je ulikuwa ni mti uliosimama kama nguzo au miti miwili iliyokutana kama alama ya kujumlisha?

Jibu: Tuirejee mistari hiyo..

Wagalatia 3:13 “Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu AANGIKWAYE JUU YA MTI”.

Na tena..

Yohana 19:19 “Naye Pilato akaandika anwani, akaiweka juu ya msalaba, imeandikwa, YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI”.

Bwana Yesu alisulubiwa juu ya msalaba ambao ulikuwa ni wa malighafi ya mti, na si wa malighafi ya chuma, au ya shaba, hiyo ndio maana ya “kuangikwa juu ya mti”,

Lakini tukirudi katika umbile la msalaba wa Bwana kama ulikuwa ni wa wima mfano wa nguzo au wa kukutana mfano wa alama ya kujumlisha, ili tujue maumbile yake yalikuwaje ni lazima turejee historia kidogo, kwasababu biblia haijatoa maelezo juu ya umbile la msalaba, maelezo iliyotoa ni malighafi ya msalaba tu!.. kuwa ni malighafi ya mti kama tulivyosoma hapo katika Wagalatia 3:13.

Tukirudi katika Historia sote tunajua kuwa wakati Bwana yupo duniani, utawala uliokuwa unatawala dunia nzima ulikuwa ni utawala wa Rumi, na ndio uliomsulubisha Bwana Yesu.

Sasa kulingana na historia, warumi walikuwa na adhabu nyingi walizowahukumu nazo wahalifu. Na mojawapo wa adhabu walizozitoa kwa wahalifu wakuu ilikuwa ni kumtundika mtu juu ya msalaba, na msalaba huo haukuwa nguzo moja ndefu, hapana bali ulikuwa ni nguzo mbili zilizokutana! (kafuatilie historia).

Hivyo mtu alining’inizwa mikono ikielekezwa katika nguzo mlalo na miguu na kichwa vikielekezwa katika nguzo wima, na mwili huo ukishikiliwa na misumari, na watu walisulubiwa uchi wa mnyama pasipo hata kuwa na  kipande chochote cha kuzuia hata sehemu za siri.

Lengo la adhabu hiyo ilikuwa ni kumtesa mtu huyo kwa mateso na maumivu makali, na pia kumwua kwa kifo cha aibu, kutokana na kosa lake alilolifanya. Lakini si wahalifu wote waliokuwa wanahukumiwa adhabu hiyo, bali wale waliokutwa na kosa la kustahili kusulubiwa hivyo.

Kwahiyo Bwana Yesu aliangukia katika hukumu ya namna hii ya kusulubiwa  juu ya msalaba, ingawa hakufanya kosa la kustahili kuuawa!,  Lakini kwasababu ilikuwa ni kwa makusudi ya ukombozi wetu ilimbidi afe kifo cha aibu kama hicho ili sisi tupone!.

Lakini swali ni je! Wale wanaoamini kuwa Bwana Yesu alisulubiwa katika Nguzo ya wima, je hawataokolewa ikiwa wameshika na kuzitenda kanuni nyingine za imani?

Jibu ni la!.. Mtu akiamini kuwa Bwana Yesu alisulubiwa katika mti uliokuwa wima, au katika Miti miwili iliyokatana kwa mfano wa alama ya kujumlisha.. haimwongezei chochote wala haimpunguzii chochote katika vigezo vyake vya kuokolewa… Suala la msingi ni kuamini kuwa Yesu aliteswa na kusulubiwa kwaajili yetu, na akazikwa na kufufuka na akapaa mbinguni, na siku ya mwisho atarudi tena kutuchukua, hivyo tutubu na kuacha dhambi, lakini Mambo mengine hayana msingi sisi kuyajua…

Aina ya mti Bwana aliosulubiwa nao kama ni mshita, au mkoko hauna maana yoyote sisi kujua… vile vile na urefu wa mti au maumbile yake hivyo havitusaidii chochote wala havituongezei kitu katika vigezo vya kuokolewa, kama tu vile sura ya Bwana isivyoweza kutuongezea kitu kwa wakati huu (kwani hakuna anayeijua sura yake lakini bado wokovu tunapata) vivyo hivyo na maumbile ya msalaba hayatuongezei chochote, bali kuzaliwa mara ya pili.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Mada Nyinginezo:

Shekina ni nini? Na Je! Utukufu wa shekina unamaana gani?

UTHAMINI WITO WA PILI WA YESU ZAIDI YA ULE WA KWANZA.

BASI MUNGU ALIMWADHIMISHA MNO.JE! NI KWELI UMEMFUATA YESU?

NI NANI ATAKAYEUCHUKUA MSALABA WA YESU?

Wapelelezi wa uhuru wa wakristo ni watu gani (Wagalatia 2:4)?

Rudi nyumbani

Print this post

NINYI AKINA BABA MSIWACHOKOZE WATOTO WENU

Majukumu ya Mzazi ni kumlea mtoto katika njia inayompasa, kwasababu hekima ya Mungu inasema, hataiacha njia hiyo hata atakapokuwa mzee.

Mithali 22:6 “Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee”

Lakini pamoja na kumlea mtoto katika njia impasayo ya kiMungu, mzazi pia hapaswi kumchokoza mwanae sawasawa na maandiko yafuatayo…

Waefeso 6:4  “Nanyi, akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana”.

Wakolosai 3:21 “Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa”

Sasa utauliza nini maana ya kuchokoza?

Kuchokoza kama ilivyotumika hapo, ni “kitendo cha kumfanya mtoto awake hasira, pasipo kuwa na sababu ya msingi”

Na baadhi ya sababu hizo ambazo zinaweza kumfanya mtoto awake hasira, hata kufikia hatua ya kukata tamaa au kufanya dhambi  kama za kutoa maneno mabaya mdomoni au moyoni..ni kama zifuatazo.

1.Ukali wa mzazi uliopitiliza.

Mzazi anapokuwa mtu wa kufoka mara kwa mara, na kushutumu kwa ukali mambo yasiyo na mashiko ni rahisi kumfanya mtoto akate tamaa au awake hasira, na kitendo hicho kibiblia kinatafsirika kama “Mzazi kamchokoza mwanae”.

2. Kumwadhibu mtoto mara kwa mara bila kuwa na sababu ya msingi.

Wapo wazazi ambao mtoto akifanya kosa dogo tu, tayari wamekamata kiboko na kutoa adhabu kali. Ni lazima mzazi apime kosa, kama linastahili adhabu au linastahili kuonya tu!.. Lakini sio kila kosa hukumu yake iwe viboko!. Hilo linaweza kumfanya mtoto achukizwe sana badala ya kujengeka, na kibiblia ikahesabika kama umemchokoza mwanao na si kumjenga.

3. Kumdhalilisha mtoto

Wapo wazazi wasiowatia moyo watoto wao, badala yake wanawadhalilisha mbele ya watoto wenzao, au mbele ya jamii.. Jambo kama hili pia kibiblia linatafsirika kama mzazi kamchokoza mwanae.

Tunapaswa siku zote kuwathaminisha watoto wetu mbele ya watoto wengine, vile vile kuwatia moyo katika mambo mazuri wanayoyafanya.

Na wazazi wengi hawajui kama wanawachokoza watoto wao, na kuwaharibu utu wao wa ndani kwa ukali wao.

Hivyo kama mzazi, zingatia mambo hayo (Usiwachokoze watoto wako) na Bwana atakubariki na vile vile kuwabariki watoto wako.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Mada Nyinginezo:

NINI MAANA YA SISI KUWA WATOTO WA MUNGU?

MZAZI, JALI MAISHA YA KIROHO YA MTOTO WAKO.

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

Je! Wana wenu huwatoa kwa nani? maana yake ni nini?

KILEMBA CHA NEEMA, JE! UMEMVIKA MWANAO?

Rudi nyumbani

Print this post

MSIWE NA UCHUNGU NAO!

Usiwe na Uchungu na Mke wako!.

(Masomo maalumu kwa Wanandoa)-UPANDE WA WANAUME/ MAJUKUMU YA WANAUME.

Neno la Mungu linasema..

Wakolosai 3:19  “Ninyi waume, wapendeni wake zenu MSIWE NA UCHUNGU NAO”

Hapo biblia imetoa maagizo mawili; 1)Kupenda na 2)Kutokuwa na uchungu.

1.Kupenda:

Kila mwanaume analo jukumu la kumpenda Mke wake kuanzia siku ile alipofunga naye ndoa mpaka siku ile kifo kitakapowatenganisha!. (Na hiyo ni Amri sio ombi). Tena anapaswa ampende kwa viwango vile vile vya kama Kristo alivyolipenda kanisa..

Waefeso 5:25  “Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake”

Kwahiyo kila Mwanaume ana wajibu wa kumpenda Mke wake siku zote za maisha yake… Ukiona upendo kwa mke wako unapungua, basi tafuta kuurejesha huo upendo kwa gharama zote!.(Jambo hilo linawezekana kabisa endapo ukimwomba Mungu, na wewe ukitia bidii katika kuurejesha upendo)

2. Kutokuwa na uchungu nao:

Amri ya pili waliyopewa wanaume juu ya wake zao, ni “KUTOKUWA NA UCHUNGU NAO” . Na mpaka biblia inasema “wanaume wasiwe na uchungu na wake zao” maana yake ni kwamba “wanawake wana mambo mengi ambayo wakati mwingine yanaleta machungu mengi”.

Kwamfano Matumizi mabaya ya Pesa… Hili ni moja ya jambo ambalo linaweza kumletea Mwanaume uchungu, hususani kama sehemu kubwa ya fedha anazitoa yeye, na pia tabia ya kuzungusha maneno ya siri ya familia kwa marafiki au kwa watu wasio na uhusiano wowote na familia,  jambo hili pia linaweza kuleta uchungu kwa mwanaume. Na pia tabia ya kurudia makosa yale yale, na tabia ya kutokusikia au kukosa umakini wa baadhi ya mambo na hivyo kusababisha hasara Fulani,  au kuwa wazito kufanya baadhi ya mambo, hizi zinaweza kuleta uchungu kwa mwanaume.

Lakini kwa sababu hizo au nyingine zozote, ni amri wanaume wote kutokubali uchungu ndani yao kwasababu ya kasoro hizo za wanawake.

Sasa Kwanini ipo hivyo?

Biblia imeweka wazi kuwa ni kwasababu “wanawake ni vyombo visivyo na nguvu”..

1Petr3:7 “Kadhalika ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, KAMA CHOMBO KISICHO NA NGUVU; na kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe”

Kwahiyo kama mwanamke ni chombo dhaifu, ni lazima tu kitakuwa hivyo siku zote!.. hivyo ni lazima kuchukuliana nacho katika hali hiyo.. Lakini usipokichukulia kama ni vyombo dhaifu, na kukifanya kuwa ni chombo chenye nguvu, basi utakuwa ni mtu wa kuumia moyo kila wakati, na kujikuta unakuwa mtu uliyejaa uchungu na hasira na hata kufikia kuwa mtu wa ugomvi na makelele ndani ya nyumba. Jambo ambalo ni dhambi!!

Waefeso 4:31 “UCHUNGU WOTE NA GHADHABU NA HASIRA NA KELELE na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya”

Hivyo ni wajibu wa kila mwanaume aliyeoa kutokuwa na uchungu na Mke wake.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Mada Nyinginezo:

Neno “Uchungu wa mauti” lina maana gani kibiblia?

Mshahara wa Mbwa ni upi? Kama tunavyousoma katika Kumbukumbu 23:18

SHINA LA UCHUNGU, LISICHIPUKE NDANI YETU.

Nini maana ya msiwe waalimu wengi (Yakobo 1:3)?

MAJARIBU 10 WANA WA ISRAELI WALIYOMJARIBU MUNGU.

Rudi nyumbani

Print this post

Uishi kwa furaha pamoja na mke umpendaye, siku zote

SWALI: Naomba kufahamu maana ya hivi vifungu katika maandiko

Mhubiri 9:7-10

[7]Wewe enenda zako, ule chakula chako kwa furaha, unywe mvinyo yako kwa moyo wa kuchangamka; kwa kuwa Mungu amekwisha kuzikubali kazi zako.

[8]Mavazi yako na yawe meupe sikuzote; wala kichwa chako kisikose marhamu.

[9]Uishi kwa furaha pamoja na mke umpendaye, siku zote za maisha yako ya ubatili, ulizopewa chini ya jua; siku zote za ubatili wako, kwa maana huo ni sehemu yako ya maisha; na katika taabu zako ulizozitaabika chini ya jua.

[10]Lo lote mkono wako utakalolipata kulifanya, ulifanye kwa nguvu zako; kwa kuwa hakuna kazi, wala shauri, wala maarifa, wala hekima, huko kuzimu uendako wewe.

JIBU: Kitabu Cha mhubiri ni kitabu kinachoelezea uhalisi wa maisha, mambo mazuri lakini pia mambo mabaya yaliyopo duniani mwanadamu anayoyasumbukia, yasiyokuwa na faida. Pamoja na siri nyingi mwanadamu asizoweza kuzivumbua, isipokuwa Mungu tu peke yake

Kwamfano anasema Dunia imejaa uchovu usioneneka, mambo yote ni ubatili kwasababu hakuna jipya chini ya jua mwisho wa siku tutayaacha yote hapa duniani.(Mhubiri 1:8)

Lakini pia pamoja na hayo hatupaswi kuyakinai maisha, kwani pia Yana mambo mazuri ambayo mwanadamu anaweza kuyafurahia endapo ataishi katika kumcha Mungu, 

Ndipo hapo anasema.ule chakula chako, uvae mavazi meupe, uishi Kwa furaha pamoja na mke umpendaye siku zote za maisha Yako, ufurahie matunda ya kazi uliyoifanya maadamu tayari Mungu ameshakuridhia…yaani tayari upo ndani ya Kristo.

Hivyo Kama Mahali Mungu alipokuweka panastahili kufurahi basi furahi tu, kwasababu ni Mungu kakubariki, huku ukiwa ndani ya Bwana, kama ni mke Bwana kakupa mfurahie, kama ni mavazi mazuri vaa..Kwani mambo hayo ni ya hapa hapa tu duniani, Bwana ametukirimia,.Hatutakwenda nayo kule ng’ambo.

Sehemu nyingine anasema.

Mhubiri 8:15

[15]Kisha nikaisifu furaha, kwa sababu mwanadamu hana neno lo lote lililo jema chini ya jua, kuliko kula, na kunywa, na kucheka; na yakuwa hilo likae naye katika amali yake, siku zote za maisha yake alizompa Mungu chini ya jua.

Hivyo mhubiri anatuambia tuhakikishe kwanza Bwana ameziridhia njia zetu. Kisha furaha ya maisha ifuate baada ya hapo, Ndio kiini cha hivyo vifungu. lakini ikiwa tutafurahia maisha, lakini Mungu yupo nyuma, hiyo inageuka na kuwa anasa na tujue mwisho wetu utakuwa ni upotevu.

Zaidi sana sehemu nyingine anasema heri, “Heri konzi moja pamoja na utulivu, Kuliko konzi mbili pamoja na taabu; na kujilisha upepo” Mhubiri 4:6  Maana yake ni kwamba ikiwa umejaliwa kimoja, lakini upo katika amani ni bora kuliko kuwa na vingi lakini katika masumbufu.

Bwana atusaidie, tuishi kwa hekima katika dunia yake aliyotupa. Pastahilipo furaha tufurahi, pastahilipo kujizuia tujizuie kwelikweli. Mambo yote yawe katika uwiano ndani ya Kristo.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

JE! NINAWEZA KUPOTEZA FURAHA YA WOKOVU?

Mithali 24:17 inamaana gani kusema Tengeneza kazi yako huko nje?

Furaha ni nini?

Mithali 14:4 ‘Zizi ni safi ambapo hapana ngombe;

IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.

“Humfukuza punda wake asiye baba”, nini maana ya mstari huu? (Ayubu 24:3)

Nini maana ya “mtakayoyafunga duniani, yatakuwa yamefungwa mbinguni”?

NINI MAANA YA KUWA MKRISTO?

Rudi nyumbani

Print this post

Nini maana ya kupwita-pwita? (Zaburi 38:10)

Jibu: Turejee,

Zaburi 38:10 “Moyo wangu unapwita-pwita, Nguvu zangu zimeniacha; Nuru ya macho yangu nayo imeniondoka”.

Kupwita-pwita maana yake, ni “kudunda kwa haraka”, hivyo hapo biblia iliposema “kuwa moyo wangu unapwita pwita”, maana yake ni kuwa “moyo wa mwandishi unaenda mbio” kutokana na mateso aliyokuwa anayapitia.

Mtu anayepitia katika hali ya mateso, kutoka kwa watu wabaya.. ni kawaida kuumia moyo, Tuwapo katika hali kama hiyo, biblia imetufundisha kuwa waombaji na kujinyenyekeza kwa Mungu ili Bwana aiponye mioyo yetu na kutuokoa na mikono ya watesi.

Zaburi 17:14 “Ee Bwana, kwa mkono wako uniokoe na watu, Watu wa dunia hii ambao fungu lao li katika maisha haya”.

Zaburi 59:1 “Ee Mungu wangu, uniponye na adui zangu, Uniinue juu yao wanaoshindana nami. 

2 Uniponye nao wafanyao maovu, Uniokoe na watu wa damu. 

3 Kwa maana wanaiotea nafsi yangu; Wenye nguvu wamenikusanyikia; Ee Bwana, si kwa kosa langu, Wala si kwa hatia yangu.

 4 Bila kosa langu huenda mbio, hujiweka tayari; Uamke uonane nami, na kutazama”.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa >> WHATSAPP-GROUP

Mada Nyinginezo:

Nitajuaje kuwa nimesamehewa dhambi zangu?

SALA YA UPONYAJI/MAOMBI YA UPONYAJI.

MWIMBIE BWANA ZABURI KATIKA NYAKATI ZA FURAHA.

BWANA UNIJULISHE MWISHO WANGU.

Mtima ni nini kibiblia?.

Rudi nyumbani

Print this post

FAHAMU MAISHA YA YESU KABLA YA HUDUMA.

Jina la mwokozi wetu Yesu Kristo litukuzwe milele na milele. Nakualika Tena wakati huu tujifunze maneno ya uzima wa Roho zetu.

Wengi wetu tunavutiwa na maisha ya Yesu alipoanza huduma, tunafurahishwa na jinsi alivyokuwa anafanya miujiza mikubwa, alivyokuwa anahubiri kwenye miji na vijiji, alivyokuwa anaponya wagonjwa,kutoa Pepo na kufufua wafu n.k.

Lakini ni Wachache sana wanaweza kuyatafakari maisha ya Yesu kabla ya huduma. Na hayo ndio Yana umuhimu sana kwetu kuliko Yale aliyoyadhihirisha baadaye.

Maandiko yanasema Yesu alimpendeza Mungu kabla hata hajaanza huduma yoyote ya kuhubiri, kutoa Pepo, na kuokoa watu…alishampendeza Mungu kabla ya hayo yote, tunalithibitisha hilo katika kitabu Cha Mathayo 3 siku Ile anabatizwa na Yohana, 

Mathayo 3:16-17

[16]Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake;

[17]na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.

Umeona alishampendeza Mungu kabla hata ya utumishi wowote, kuanza..tofauti na Leo tunavyodhani kwamba ili tumpendeze Mungu, ni sharti tuwe wahubiri wakubwa, au tuwe na upako, au tuwe wachungaji..hiyo sio kanuni ya Mungu.

Hivyo ni lazima tujue Mungu alipendezwa na Yesu kwa kipi? Ni kitu gani alikuwa anafanya mpaka kimfanye akubaliwe na Mungu namna Ile?

JIBU lipo katika Maisha aliyokuwa anaishi Kwa ile miaka 30 kabla ya huduma. Na hapa ndipo tunapaswa tupaangalie sana. Na tujifunze ili na sisi tufanane naye.

Watu wengi wanaona kama maisha yake ya awali yalifichwa sana, zaidi ya Yale aliyoyatenda katika huduma. Ni kweli ukitazama Kwa jicho la nje sehemu kubwa ya injili imeandika juu ya huduma ya Yesu, yaani ile miaka mitatu na nusu ya mwisho ya maisha yake. Lakini ukweli ni kwamba maisha ya Yesu kabla ya huduma ndio yameandikwa kwa wingi zaidi kuliko Yale aliyoyafanya katika huduma.

Hivyo Kwa neema za Bwana tutaona  juu ya maisha yake yalikuwaje, tangu utotoni mpaka anakaribia kuanza huduma.

Sehemu ya kwanza tutaona Mahali ambapo maandiko yameeleza moja Kwa moja maisha yake yalivyokuwa. Na sehemu ya pili tutaona maandiko ambayo sio ya moja Kwa moja, lakini yalimwelezea Yesu maisha yake.

Tukianza na maandiko yanayoeleza moja Kwa moja juu ya maisha yake. Kama yafuatavyo;

1) YESU ALIISHI MAISHA YA KUMPENDEZA MUNGU PAMOJA NA WANADAMU.

Luka 2:52

[52]Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.

Maisha yake yote alikuwa ni mtu mwenye bidii sana kuhakikisha hafanyi jambo lolote ambalo ni kinyume na mapenzi ya Mungu. Alikuwa yupo makini sana na hilo, lakini zaidi sana alihakikisha katika jamii hawi na harufu mbaya. Alizingatia kuwa na adabu na heshima Kwa Kila mtu aliyekutana naye.

Si ajabu watu walipomuona walimsifia sana, na kusema yule kijana anaheshima, yule kijana ni mtaratibu, natamani watoto wangu wangekuwa kama yule, hatumuoni kwenye kampani za wahuni, hatumuoni akiruka ruka na mabinti barabarani, hatumuoni akitembea Kwa majigambo barabarani, muda wote anatabasamu, hakasiriki haraka, anahekima kama za mtu mzima wakati bado ni kijana..

Yesu alipata sifa isiyo ya kawaida katika jamii, alipoishi duniani, hakuna mtu alimchukia Kwa Tabia zake, alijitoa kwelikweli kuishi kikamilifu katika jamii yake.

Na sisi pia hichi ndio kitu Mungu anataka kukiona katika maisha yetu tunapookoka kabla hata ya kufikiria kuwa wahubiri ,je  mtaani kwako unaonekanaje, shuleni kwako Tabia zako zikoje? Mwonekano wako unawavutiaje watu, ofisini kwako kauli zako na wanyakazi wenzako Zina mvuto gani mpaka watu wakuone wewe ni mtu Bora kuliko wengine wote?

2) YESU ALIKUWA MTIIFU

Luka 2:51

[51]Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake.

Aliwatii wazazi wake, hakukuwa na kiburi ndani yake, Neno utiifu kwa Yesu lilikuwa ni kama pumzi kwenye mapafu. Alipoagizwa alifanya, alipotumwa alikwenda, maisha yake yalikuwa ni ya namna hiyo, ili kutunza hadhi yake aliyokuwa nayo ya kuwapendeza watu wote..

Na sisi je tunaweza tukawa watiifu Kwa wazazi wetu wa kimwili na wa kiroho? Tuwatii viongozi wetu wa kiroho hata kama tutakuwa tunafahamu jambo Fulani zaidi ya wao, maadamu Bwana katuweka chini Yao.Hatuna budi kufanana na Yesu. Bwana atusaidie juu ya hilo.

3) ALIPENDA KUKAA NYUMBANI MWA BABA YAKE

Hii ni sifa nyingine inayomwelezea Yesu Tabia yake.

Luka 2:41-49

[41]Basi, wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka.

[42]Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu;

[43]na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari.

[44]Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao;

[45]na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta.

[46]Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali.

[47]Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake.

[48]Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni.

[49]Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu?

Akiwa kijana mdogo wa miaka 12, hakujali atakula nini, atalala wapi, ataoga wapi..alinogewa na ibada na mafundisho hekaluni akaona hata ule muda wa sikukuu hautoshi yeye kukata kiu yake Kwa Mungu, akaendelea kubaki palepale siku tatu, akiwa amefunga, yeye ni kujifunza tu, na kuyatafakari maneno ya Baba yake..

Wazazi wake hawakujua kuwa angekuwa na kiu Kali namna ile, lakini baada ya pale walimzoea, ikawa ndiyo desturi ya maisha yake yote.

Yesu alikuwa ni mtu asiye mtoro wa ibada, alikuwa anatumia majira yake mengi, kwenda kwenye masinagogi na kutafakari Neno la Mungu pamoja na viongozi wake wa kidini. Hakuwa mtu wa kujitenga Tenga, kama watu wanavyodhani.

Lakini pia alikuwa ni jemedari wa maombi kweli kweli na Dua.

Alikuwa anaomba sana Kwa bidii, Kwa kulia na machozi sana, na kwa kujimimina sana. Maandiko yanasema hivyo;

Waebrania 5:7

[7]Yeye, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu;

Na sisi je tunaweza tukaiga Tabia hii ya Bwana. Je! Furaha yetu ni kuwepo uweponi MWA Bwana muda mwingi au kuwepo katika anasa za Dunia? Au katika biashara zetu? Ni lazima Bwana apewe kipaumbele Cha kwanza.

4) YESU ALIISHI MAZINGIRA YA KUFANYA KAZI

Pamoja na kuwa alikuwa ni mtiwa mafuta wa Bwana ameandaliwa Kwa kusudi moja tu la kuwaokoa watu. Lakini kipindi anasubiri wakati wa Bwana, hakukaa hivi hivi tu, Mungu aliruhusu afanye kazi.

Marko 6:3

[3]Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? Na maumbu yake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake.

Yesu hakuwa kama Yohana mbatizaji, Kukaa majangwani mbali na watu muda wote, lakini alikuwa ni mtu ambaye yupo katikati ya jamii, anayejulikana, anafahamika, alifanya kazi pamoja na baba yake ya useremala. 

Kwasasa tunaweza kusema alikuwa kariakoo akiuza vifaa vya majumbani na baba yake.

Lakini katika hayo yote aliishi maisha makamilifu ya kujichunga na kuwa na kiasi. 

Hii ni kutuonyesha kuwa unapookoka, uwapo popote pale iwe ni kazini, au kwenye biashara Yako, bado unaweza kumpendeza tu Mungu. Hivyo tusiruhusu kazi ziwe kisingizio cha sisi kutoishi maisha makamilifu. Yesu alikuwa ni mtu wa kujichanganya, lakini hakuruhusu dhambi iwe juu yake. Alipouza kabati hakukwepa kulipa Kodi, hakumuuzia mtu meza Kwa bei isiyoendana na thamani yake.  Hivyo ikampelekea Mungu ampende sana

Hayo ni maandiko ya moja Kwa moja yanayoeleza maisha ya Yesu yalivyokuwa.

Lakini maandiko mengine tunayapata wapi?

JIBU ni kuwa tunayapata katika kinywa Cha Yesu mwenyewe. Kwa kawaida mtu hawezi kusema maneno ambayo yeye hayaishi. Vinginevyo atakuwa ni mnafki, na Yesu yupo mbali sana na unafki, aliukemea sana, hata alipouona ndani ya mafarisayo na waandishi,walipowafundisha watu mambo ambayo wao hawayaishi.(Mathayo 23:1-5)

Hivyo ukitaka kufahamu Kwa kina maisha ya Yesu yalikuwaje sikikiza maagizo yote aliyokuwa anayatoa katika vitabu vyote vya injili.

Kwamfano. Mathayo soma sura yote ya 5-7 utaona maneno kadha wa kadha aliyokuwa anawafundisha makutano.

Anasema wapendeni adui zenu na kuwaombea(Mathayo 5:43-44): Yesu alikuwa anawaombea watu wote waliokuwa wanamchukia Kwa kumwonea wivu. Badala ya kuwatakia mapigo anawatakia maisha marefi, kuwaombea toba wageuzwe.

Anasema mtu akupigaye shavu la kuume mgeuzie la kushoto(Mathayo 5:38-40). Kuonyesha kuwa hakuwa mtu wa Shari, sikuzote alipotukanwa, au alipoaibishwa hakurudisha majibu, Bali alikubali kuaibishwa zaidi, ili aipushe malumbano zaidi.

Anasema amtazamaye mwanamke Kwa kumtamani amekwisha kuzini naye(Mathayo 5:28). Hakuwa na uvumilivu na macho yake, hakuwahi kuruhusu tamaa itawale maisha yake. Alijitenga na vichocheo vyote vya uzinzi, na mazungumzo yote yasiyofaa.

Alikuwa ni mtu wa kusamehe mara Saba sabini, hakuwa anawahukumu watu, au kuwalaumu(Mathayo 7:1-4)

Alikuwa si mtu wa kuruhusu hasira, aliona ukiwa hivyo adhabu Yako inakupasa ziwa la moto (Mathayo 5:21).

Bado alijishuhudia kuwa yeye ni mpole na mnyenyekevu (Mathayo 11:29), aliishi Kwa kujishusha, bila kumdharau yoyote, watu wote walikuwa na nafasi sawa kwake..

Na maandiko mengine mengi, aliyotuelekeza. Hivyo itoshe kusema maisha ya Yesu yaliyomfanya Mungu ampende kabla hata ya huduma ndiyo haya tunayoyasoma katika vitabu vya injili…

Hivyo ndugu Mimi na wewe yatupasa,. Tufikie hapo, acha kumuomba Mungu upako. Utakuja wenyewe tu endapo utampendeza Mungu kwanza kama Bwana Yesu, ukiwa unauhitaji. Penda mema chukia maasi..ndivyo Yesu alivyokuwa hapa duniani, hakuivumilia dhambi kwa namna yoyote, na matokeo yake Bwana akamtia nguvu kuliko mwanadamu yoyote aliyewahi kutokea hapa duniani.

Waebrania 1:9

[9]Umependa haki, umechukia maasi; Kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekutia mafuta, Mafuta ya shangwe kupita wenzio.

Bwana atusaidie sasa tuishi kama Kristo, ili baadaye tutende kama Kristo.

Bwana akubariki.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa >> WHATSAPP-GROUP

Mada Nyinginezo:

Ni kweli hakuna mtu aliyewahi kuuona uso wa Mungu Zaidi ya Bwana Yesu?

Kibiriti ni kitu gani? kama kinavyozungumziwa kwenye maandiko?

Nini maana ya Ukuta uliopakwa chokaa (Matendo23:3)?

FANYA MAAMUZI KABLA HAZIJAKARIBIA SIKU ZA HATARI.

NAFASI YA MWANAMKE KATIKA KANISA

MAUMIVU  NYUMA-YA-HUDUMA.

WITO WA MUNGU

Rudi nyumbani

Print this post