Title June 2021

Ni nani aliye kipofu, ila mtumishi wangu?

SWALI: Nini maana ya hii mistari?

Isaya 42:19 “Ni nani aliye kipofu, ila mtumishi wangu? Au aliye kiziwi, kama mjumbe wangu nimtumaye? Ni nani aliye kipofu, kama yeye aliye na amani? Naam, kipofu kama mtumishi wa Bwana?

20 Unaona mambo mengi, lakini huyatii moyoni; masikio yake ya wazi, lakini hasikii”.


JIBU: Maneno hayo hayamaanishi kuwa watumishi wa Mungu wote ni vipofu na viziwi kwamba wanaona mambo mengi lakini hawayatilii maanani, hapana.

Bali Isaya kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu aliandika kwa wayahudi, Ambao  hao ndio waliokuwa kwanza kumjua Mungu, kufahamu sheria zake, kuona miujiza yake na matendo yake makuu, tangu zamani, na ndio maana akawafananisha na watumishi / wajumbe wake. Lakini kinyume chake wao ndio wakawa wa kwanza kukimbilia kuabudu miungu mingine, na kufuata mambo maovu, kuliko hata mataifa ambayo hayamjui Mungu.

Jambo kama hilo liliendelea mpaka kipindi cha kutokea kwa Masihi duniani(Yesu Kristo), mafarisayo na waandishi ambao ndio wangepaswa wawe wa kwanza kumtambua Kristo wao, na kumwamini, kutokana na kuwa walishajua unabii wake katika torati tangu zamani, lakini kinyume chake ndio waliokuja kumpinga, na kumuua.

Na ndio maana Bwana Yesu akawaambia maneno haya..

Yohana 9:39 “Yesu akasema, Mimi nimekuja ulimwenguni humu kwa hukumu, ili wao wasioona waone, nao wanaoona wawe vipofu.

40 Baadhi ya Mafarisayo waliokuwapo pamoja naye wakasikia hayo, wakamwambia, Je! Sisi nasi tu vipofu?

41 Yesu akawaambia, Kama mngekuwa vipofu, msingekuwa na dhambi; lakini sasa mwasema, Twaona; basi dhambi yenu inakaa”.

Unaona? Hata sasa, inasikitisha kuona baadhi ya watu wanaojiita ni watumishi wa Mungu ni vipofu rohoni. Kwasababu kama tutashindwa kujua kiini cha Kristo kuja hapa duniani ni nini. matokeo yake tunaigeuza injili ya Kristo kuwa sehemu ya biashara, na mahali pa kutafutia tu mafanikio, na sio wokovu tena, hakuna cha kukemewa dhambi, wala mafundisho ya mbinguni. Huo ni upofu wa hali ya juu sana.

Tunakuwa hatuna tofauti na wale mafarisayo na masadukayo, na wale watumishi wa mishahara ambao Bwana Yesu aliwataja katika. Yohana 10:12-13

Bwana atusaidie sana, tusiwe vipofu na viziwi, kwa kubaki katika misingi ya Neno la Mungu..

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

WANA WA MAJOKA.

WAPE WATU WANGU RUHUSA ILI WAPATE KUNITUMIKIA.

Ngome ni nini?  Kwanini Mungu anafananishwa na ngome?

TAFAKARI SANA KABLA YA KUAMUA HATIMA YAKO.

Mharabu ni nani katika biblia?

Rudi nyumbani

Print this post

Makuruhi ni nini, kama tunavyosoma katika biblia?

Makuruhi; Ni neno linalomaanisha “kuchukiza kuliko pitiliza”, Kwa mfano mtu akisema mabeberu ni makuruhi kwa waafrika. Anamaanisha kuwa mabeberu ni watu wanaochukiza sana/ au ni harufu mbaya sana kwa waafrika, hawapendwi hata kidogo. Na hiyo yote ni kwasababu ya maumivu ambayo pengine walishawahi kuyapata kutoka kwao enzi za utumwa.

Vivyo hivyo neno hili katika biblia utalisoma katika mstari huu;

1Samweli 13:4 “Waisraeli wote wakasikia habari ya kwamba Sauli ameipiga hiyo ngome ya Wafilisti, na ya kwamba Waisraeli wamepata kuwa MAKURUHI kwa Wafilisti. Basi hao watu wakakusanyika pamoja kumfuata Sauli huko Gilgali.

5 Nao Wafilisti wakakusanyana ili wapigane na Waisraeli, magari thelathini elfu, na wapanda farasi sita elfu, na watu kama mchanga ulio ufuoni mwa bahari kwa wingi wao; wakapanda juu, wakapiga kambi yao katika Mikmashi, upande wa mashariki wa Beth-aveni”.

Habari hiyo ni baadaya ya Israeli kuwaivamia kambi mojawapo ya wafilisti na kuipiga, na kisha kujigamba baada ya hapo, Hivyo wafilisti walivyosikia hivyo ikawabidi wawachukie Israeli kupitiliza, mpaka ikawabidi wafilisti wote waungane na idadi yao ikawa kama mchanga wa bahari ili waifutilie Israeli mbali, hiyo yote ni  kwasababu tayari wameshafanyika kuwa makuruhi kwao.

Lakini kama tunavyoijua habari ni kuwa, walikuja kuuliwa wote, na waisraeli kwa msaada wa Mungu.

Jambo kama hili linajirudia leo hii, Vita kati ya Israeli na Palestina.  Wapalestina (ambao ndio wafilisti wa kipindi kile), sasa wanawachukia wayahudi kupitiliza, Israeli imekuwa harufu mbaya kwao, na hiyo yote ni kutimiza maandiko. Ili baadaye Mungu aje kujichukulia utukufu kutoka katika vita ambavyo vitakavyopiganwa siku za hivi karibuni pale Israeli ( Soma Ezekieli 38 &39).

Na sio tu ni makuruhi kwa  wapalestina peke yao. Hapana bali wataendelea kuwa hivyo, mpaka kwa dunia nzima. Ili kutimiza unabii wa vita ile kuu ya Har Magedoni ambayo itapiganwa pale Israeli, siku za mwisho. Vita hiyo itakuwa kati ya Israeli na mataifa yote duniani.

Zekaria 12:3 “Tena itakuwa siku hiyo, nitafanya Yerusalemu kuwa jiwe la kuwalemea watu wa kabila zote; wote watakaojitwika jiwe hilo watapata jeraha nyingi; na mataifa yote ya dunia watakusanyika pamoja juu yake”.

Kwa urefu wa vita hiyo na mambo hayo yatakayotokea fungua link hii > https://wingulamashahidi.org/2018/07/17/siku-ya-bwana-inayotisha-yaja/

Hivyo ndugu, unapoona migogoro inayoendelea Israeli leo hii, usidhani ni ishara nzuri kwako wewe mwenye dhambi. Hiyo ni ishara ya Israeli kurudiwa na Mungu. Na moja ya hizi siku tutaona mabadiliko ya ghafla katika hii dunia. Na mabadiliko hayo yakishatokea tujue kuwa Unyakuo utakuwa umeshapita wakati huo, kanisa lipo mbinguni kwenye karamu ya mwana-kondoo.

1Wathesalonike 5:3 “Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa”.

Jiulize, mabadiliko hayo yakitokea leo, wewe utakuwa wapi?

Majibu yote yapo moyoni mwako.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

JE NI KWELI SAMAKI NGUVA YUPO?

NAYE AKASIMAMA JUU YA MCHANGA WA BAHARI.

Nini maana ya Dirii, Chepeo na Utayari?

Rudi nyumbani

Print this post

MUNGU ATAKUUA UKIWA MBAYA MACHONI PAKE.

Mwanzo 38:6 “Yuda akamwoza mke Eri, mzaliwa wake wa kwanza, na jina lake huyo mke ni Tamari.

7 Naye Eri, mzaliwa wa kwanza wa Yuda, alikuwa mbaya machoni pa Bwana; na Bwana akamwua”.

Lazima tukumbuke kuwa Mungu anatazama matendo ya kila mmoja wetu katika hii dunia, Na pale yanapovuka mipaka yake aliyoiweka tujue kuwa tunayahatarisha maisha yetu sisi wenyewe.

Vifuatavyo ni vitu ambavyo, havimpendezi Mungu, na kama vipo ndani yako, basi hakikisha vinaondoka mapema sana. Tulishajifunza huko nyuma lakini ni vizuri tujikumbushe tena, ili visiondoke mioyoni mwetu. Tunavisoma katika..

Mithali 6:16 “Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana; Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake.

17 Macho ya kiburi, ulimi wa uongo, Na mikono imwagayo damu isiyo na hatia;

18 Moyo uwazao mawazo mabaya; Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu;

19 Shahidi wa uongo asemaye uongo; Naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu.

MACHO YA KIBURI:

Kiburi ni kujiona wewe ni bora kuliko wengine, upo juu wa wengine wote, hivyo unawadharau , hutaki kurekebishwa, hutaki kuonywa, hutaki kuwasaidia wengine. watu wa namna hii, ni machukizo mbele za Mungu, katika biblia kulikuwa na mtu aliyeitwa Nabali, ni mfano wa mtu aliyekuwa na kiburi, japokuwa alisaidiwa na Daudi kuangaliwa mifugo yake, lakini bado alimdharau na kumtukana, kisa tu ana mali, na mafanikio, na mwisho wa siku Mungu akamuua. (1Samweli 25:1-38)

Kiburi pia kinachozungumziwa hapo ni kiburi cha uzima. Kisa una afya, ni mzuri, una nguvu, una mafanikio, basi ukielezwa habari za Mungu, wewe ni kudharau, na kudhihaki, na kukebehi, unasema watu wanaomtafuta Mungu ni watu wajinga, wavivu, hawana akili. Kama wewe ni mmoja wapo wa hili kundi la watu, jirekebishe mapema sana, upo hatiani kuuliwa na Mungu.

ULIMI WA UONGO: 

Kilichomfanya shetani apewe adhabu ya kutupwa katika ziwa la moto, ni pamoja na uongo aliokuwa nao tangu mwanzo. Bwana Yesu alisema..

Yohana 8:44 “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; KWA SABABU YEYE NI MWONGO, NA BABA WA HUO”.

Embu fikiria na wewe pale unapokuwa mwongo mwongo kwa kila jambo, unadhani Mungu atapendezwa na wewe? Hawezi kinyume chake unajitafutia kifo tu na hukumu. Uongo unaharibu mahusiano ya mtu na Mungu kwa kiasi kikubwa sana. Tuziponye ndimi zetu.

MIKONO IMWAGAYO DAMU ISIYO NA HATIA:

Kundi lingine ambalo Mungu halipendi kabisa, ni la wauaji. Wengi wanadhani kuwa muuaji ni mpaka utimilize  tendo lenyewe. Hapana, kitendo tu cha kusema nashika silaha,nashika kisu, panga, n.k. na kwenda kuvamia kuiba, tayari wewe ni muuaji, kwasababu hiyo silaha uliyobeba tayari ulishawaza kichwani mwako, endapo ikitokea shida utaitumia kujihamu, ikiwezekana hata kuua. Mambo kama hayo, yanavuta kifo chako cha kiroho na kimwili kwa haraka sana.(Mathayo 5:21-22). Acha matendo yenye harufu za uuaji nyuma yake. Zitakupunguzia maisha yako hapa duniani.

MOYO UWAZAO MAWAZO MABAYA:

Ni moyo ambao hauna fikra chanya kwa Mungu, au katika kuuendeleza ufalme wa Mungu. Badala yake ni moyo ambao unawaza uzinzi wakati wote, unafikiria mbinu ambazo unaweza kupata pesa ukatumie katika anasa. Moyo ambao unaamka asubuhi unafikiri ukafanye kazi ile baadaye ukamalizie siku yote baa.

Moyo ambao unafikiria utapeli, uporaji, dhulma, hauna nafasi hata mara moja kufikiria hatma ya maisha yake ya baadaye, haumfikirii muumba wake, haufikirii kumtolea Mungu, haufikirii kuifanya kazi ya Mungu. Watu kama hawa Mungu anawaua mapema sana, aidha rohoni au mwilini.

MIGUU ILIYO MYEPESI KUKIMBILIA MAOVU;

Kwa kawaida mwanadamu yoyote ni lazima aone ugumu Fulani, katika kutekeleza jambo ambalo sio la haki, ni lazima ashtuke pale anapoletewa habari ya kwenda kuzini na mke wa mtu, anapoambiwa tule rushwa n.k. Lakini kama wewe ni mwepesi wa kukimbilia maovu, mtu anakwambia twende Disko na wewe unakurupuka kuongozana naye, twende tukaibe, unakurupuka kuenda, twende tukazini mume wangu kasafiri, na wewe unaenda, Ujue mwisho wako utakuwa ni mbaya sana, kwasababu miguu hiyo ni mepesi kukimbilia maovu. (Mithali 1:16 , 7:5-27)

SHAHIDI WA UONGO ASEMAYE UONGO;

Huyu ni zaidi ya mtu anayesema uongo. Huyu anaushuhudia kabisa uongo  kuwa ni kweli. Kipindi kile Yezebeli aliajiri watu wamshuhudie uongo Nabothi kwamba amemkufuru Mungu, ili watu wampige mawe afe ili arithi kiwanja chake 1Wafalme 21:1-16

Hata leo hii, wapo watu ni hodari wa kushuhudia uongo, wanafundishwa kusema uongo ili wasitiri dhambi zao, au za wengine, hilo ni jambo baya sana, ambalo linamchukiza Mungu. Bwana atusaidie tusifanyike mashahidi wa uongo.

NAYE APANDAYE MBEGU ZA FITINA KATI YA NDUGU:

La mwisho ndio hili, unatunga uchonganishi katikati ya ndugu wanaomwamini Mungu, ili wachukiane, wagombane, wasiongee, unavunja umoja wao na upendo wao, ambao Bwana Yesu aliwaombea wawe nao katika Yohana 17. Lakini wewe furaha yako ni kuona hivyo. Jambo hilo linamchukiza sana Mungu.

Wakati Mungu anasema,Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu. Wewe unakuwa mchonganishi..kinyume chake ni kuwa utaitwa mwana wa Ibilisi.

Hivyo tunapoishi hapa duniani tuwe watu wenye Hofu kwa Mungu. Tusiishi kana kwamba Mungu hatuoni.. Anatuona, na tunavyozidi kuwa wabaya ndivyo tunavyoyaweka maisha yetu hatarini. Ni wazi kuwa mtoto wa Yuda, alifanya mojawapo ya dhambi hizo na ndio maana Mungu akamuua. Vivyo hivyo na sisi tujichunguze kama mambo hayo yapo basi tuyaweke mbali na sisi.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

TABIA KUU TATU ZA WAHUBIRI WALIORUDI NYUMA NA KUMWACHA MUNGU.

VIKAANGUKA MACHONI PAKE VITU KAMA MAGAMBA.

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

Rudi nyumbani:

Print this post

Je! kuna madhara kuchukiwa na kila mtu kwasababu huna mali?. Kama biblia inavyosema katika Mithali 14:20?.

Jibu: Tusome,

Mithali 14:20 “Maskini huchukiwa hata na jirani yake; Bali tajiri ana rafiki wengi”.

Na  pia

Mithali 19:4 Inasema  “Utajiri huongeza rafiki wengi; Bali maskini hutengwa na rafiki yake”.


Hizi ni Mithali ziliyoandikwa na Mfalme Sulemani, kwa hekima alizopewa na Mungu, na zipo Mithali nyingine nyingi alizoandika kwa mafunzo na maonyo. Lakini tofauti na inavyodhaniwa na wengi, Kuwa kila Mithali Sulemani aliyoiandika ilikuwa ni agizo! Hapana!. Sio kila mithali tunayoisoma katika kitabu cha Mithali ilikuwa ni agizo!. Mithali nyingi Sulemani alizoziandika zilikuwa zinahusu uhalisia wa jambo Fulani, na si agizo la jambo Fulani.

Kwamfano mimi leo nikisema “Watu wengi walio wapole wanaonewa na kudhulumiwa”. Hapo sijatoa agizo kwamba wapole wasiendelee kuwa wapole tena, waanze kuwa wakali na wakorofi. bali nimezungumza “uhalisia, jambo fulani ambalo lipo!”. Na huo umetokana na mimi kuchunguza mpaka nikaja na jawabu hilo.

Kadhalika Mithali nyingi Sulemani alizoziandika hazikuwa ni maagizo, bali ni uhalisia wa mambo fulani, ambayo yapo!!!  na huo unatokana na uchunguzi alioufanya!..Na mfano mmojawapo alioutoa ambao ulikuwa ni uhalisia na si agizo ndio huu tunaousoma..

Mithali 14:20 “Maskini huchukiwa hata na jirani yake; Bali tajiri ana rafiki wengi”.

Sasa hapa sio kwamba Sulemani, alitoa agizo kwamba.. “kuwa maskini watafute utajiri ili wawe na marafiki wengi”. Hapana hakumaanisha hivyo, Kwasababu ingekuwa ndivyo mbeleni asingekuja kusema tena haya maneno..

Mithali 28:6 “Afadhali maskini aendaye katika unyofu wake, Kuliko mpotofu wa njia angawa ni tajiri”

Umeona! alisema maneno kwasababu alichunguza na kuona kuwa Walikuwepo Maskini wenye busara na hekima, ambao katika haki yao yote bado hawakupendwa, walichukiwa… Na hapo hapo akaona walikuwepo matajiri wengi ambao katika udhalimu wao walipendwa na wengi. Jambo ambalo ni kawaida hata sasa, mtu aliye na mali hata kama ni mali za haramu atapata marafiki wengi!..(lakini ni marafiki wasiofaa)

Hebu tusome tena mahali pengine Sulemani alipochunguza jambo kama hilo..

Mhubiri 9:14 “Palikuwa na mji mdogo, na watu ndani yake walikuwa wachache; akaja mfalme mkuu juu yake, akauhusuru, akajenga ngome kubwa ili kuupiga.

 15 Basi, kulionekana humo MTU MASKINI MWENYE HEKIMA, naye kwa hekima yake akauokoa mji ule lakini hata hivyo HAPAKUWA NA MTU YE YOTE ALIYEMKUMBUKA YULE MTU MASKINI.

 16 NDIPO NILIPOSEMA, BORA HEKIMA KULIKO NGUVU; walakini hekima ya maskini hudharauliwa, wala maneno yake hayasikilizwi.

 17 Maneno ya wenye hekima yanenwayo taratibu husikiwa, Zaidi ya mlio wake atawalaye katikati ya wapumbavu.

18 Hekima NDIYO BORA KUPITA SILAHA ZA VITA; Lakini mkosaji mmoja huharibu mema mengi”

Umeona hapo?.. Sulemani anamsifu Maskini mwenye hekima, ambaye kwa hekima yake ameuokoa mji, anasema “Bora hekima kuliko nguvu, na hekima ni bora kuliko silaha za vita”.

Mithali 16:16 “Si afadhali kupata hekima kuliko dhahabu? Naam, yafaa kuchagua ufahamu kuliko fedha.

Na japokuwa anamwona maskini huyo hakumbukwi, wala hatapendwa na wengi, wala marafiki wengi, wala hakuna mtu aliyemkumbuka.. Lakini kwa hekima yake ameuokoa mji, na hivyo ipo thawabu yake baada ya maisha haya…

Mhubiri 4:13 “Heri kijana maskini mwenye hekima Kuliko mfalme mzee mpumbavu”.

Kwahiyo  ni vizuri kuzichambua vyema hekima za Sulemani na kuzielewa, kwasababu si kila kitu kilichoandikwa kule ni agizo!..

Tukirudi katika ukristo pia hatujaahidiwa kwamba tukimpokea Yesu tutakuwa na marafiki wengi, au ndio tutapendwa na watu wengi..la! kinyume chake ndio tutachukiwa.. Na kuchukiwa huko sio laana!, bali ndio muhuri wa wito wetu.

Luka 21:16  “Nanyi mtasalitiwa na wazazi wenu, na ndugu zenu, na jamaa zenu, na rafiki zenu, nao watawafisha baadhi yenu.

17  Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu”

Vile vile hatujaahidiwa kuwa tunapozaliwa mara ya pili ndio hatutapitia dhiki za hapa na pale.. vipindi vya dhiki vitakuwepo, lakini Bwana ameahidi kuwa atakuwa na sisi hatatuacha.

Bwana Yesu alisema maneno haya..

Ufunuo 2:9 “Naijua dhiki yako NA UMASKINI WAKO, (lakini u tajiri) najua na matukano ya hao wasemao ya kuwa ni Wayahudi, nao sio, bali ni sinagogi la Shetani.

10  Usiogope mambo yatakayokupata; tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima”

Mathayo 16:2  “Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada. Na hayo watawatenda kwa sababu hawakumjua Baba wala mimi”.

Bwana atubariki na kutusaidia.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

TENDA AGIZO LA YESU, HILO NDIO LITAKALOKULINDA.

LISHIKILIE SANA LILE AGIZO LA KWANZA.

Mego ni nini kama tunavyosoma katika biblia? (Mithali 17:1)

Mpumbavu ni nani katika biblia? (Zaburi 14:1, Mithali 10:14)

Nini maana ya Mungu amemfanya mwanadamu mnyofu?

Rudi nyumbani

Print this post

Ni yupi aliyekuwa mkwe wa Musa kati ya Reueli na Yethro?

JIBU: Ukisoma katika kitabu cha Kutoka, utaona kuna habari kama inajichanganya kuhusiana na baba-mkwe halisi wa Musa, Kwamfano Kutoka 2:18 Inasema aliitwa Reueli, lakini sehemu nyingine zote zilizosalia kama vile Kutoka 3:1,4:18, inamtaja kama ni Yethro. Je Kuna kuna makosa ya kiuandishi?

Embu tusome baadhi ya vifungu hivyo;

Kutoka 2:15 “Basi Farao alipopata habari, akataka kumwua Musa; lakini Musa akakimbia mbele ya Farao, akakaa katika nchi ya Midiani; akaketi karibu na kisima.

16 Basi kuhani wa Midiani alikuwa na binti saba, nao wakaja wakateka maji, wakazijaza birika maji, wapate kunywesha kundi la baba yao.

17 Wachungaji wakaja wakawafukuza; lakini Musa akasimama, akawasaidia, akalinywesha kundi lao.

18 Walipofika kwa Reueli baba yao, akasema, Imekuwaje hata mkarejea mapema leo?

19 Wakasema, Mmisri mmoja alituokoa katika mikono ya wachungaji, tena zaidi ya hayo, akatutekea maji, akalinywesha kundi.

20 Akawaambia binti zake, Yuko wapi basi? Mbona mmemwacha mtu huyo? Mwiteni, ale chakula.

21 Musa akawa radhi kukaa kwake mtu yule, naye akampa Musa binti yake, Sipora.

Kutoka 3:1 “Basi huyo Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu”.

Jibu ni kuwa hakuna hitilafu, yoyote ya kiuandishi isipokuwa zamani ilikuwa ni jambo la kawaida mtu mmoja kuwa na jina zaidi ya moja, Kwamfano tukimtazama Yakobo, Mungu alimwambia utaitwa Israeli, Hivyo majina yake yote mawili utayakuta yakiandikwa sehemu mbalimbali katika biblia Lakini mtu ni Yule Yule mmoja.

Vivyo hivyo na Yethro mkwewe Musa, aliitwa pia Reueli, na kwasababu alikuwa ni kuhani, hatushangai kuona akiwa na majina mawili, moja la kwake la asili na lingine la kikuhani.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

UTAJI ULIOKUWA JUU YA USO WA MUSA.

Je Musa yupo anawashitaki watu..kulingana na Yohana 5:45?

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 1

NJIA YA KUPATA WOKOVU.

Je Musa kumwoa Sipora, Mkushi alifanya dhambi?

USIKATE TAMAA UNAPOPITIA MAGONJWA.

Rudi nyumbani

Print this post

TABIA ZA WATAKAOMKARIBIA SANA MUNGU SIKU ILE.

Kwa mara ya kwanza Yohana alionyeshwa maono ya jinsi mbinguni kulivyo, na mfumo wake mzima wa utawala ulivyojiunda.

Tukisoma mambo yale tusidhani, Mungu alikuwa anamuonyesha Yohana sinema tu ya mbinguni jinsi kulivyo, Hapana zipo siri kubwa sana zinazotuhusu sisi, endapo tutazitambua.

Leo kwa ufupi tutazama ngazi hizo, na ni jinsi gani zilivyoficha siri za sisi kumkaribia Mungu..

Ukisoma kile kitabu cha Ufunuo, sura ya 4 yote, utaona Yohana alionyeshwa mbingu zikifunga. Na moja kwa moja macho yake yakakiona kile kiti cha Enzi cha Mungu kilichojaa utukufu mwingi.

Lakini kiti hichi hakikusimama peke yake, bali alionyeshwa pia viti 24 ambavyo vimekizunguka kile kiti cha enzi ambavyo vimekaliwa na wale wazee 24, na katikati ya vile viti 24 aliona pia wenye uhai 4 ambao wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi. Na nyuma ya wale wazee 24 kulikuwa maelfu kwa maelfu ya malaika mbinguni  wamemzunguka Mungu, wakimsifu na kumtukuza. Soma Ufunuo sura ya 4 yote.

Embu tusome baadhi ya vifungu kidogo; Tafadhali soma kwa utulivu,usiviruke.

Ufunuo 4:1 “Baada ya hayo naliona, na tazama, mlango ukafunguka mbinguni, na sauti ile ya kwanza niliyoisikia kama sauti ya baragumu ikinena nami, ikisema, Panda hata huku, nami nitakuonyesha mambo ambayo hayana budi kuwako baada ya hayo.

2 Na mara nalikuwa katika Roho; na tazama, kiti cha enzi kimewekwa mbinguni na mmoja ameketi juu ya kile kiti;

3 na yeye aliyeketi alionekana mithili ya jiwe la yaspi na akiki, na upinde wa mvua ulikizunguka kile kiti cha enzi, ukionekana mithili ya zumaridi.

4 Na viti ishirini na vinne vilikizunguka kile kiti cha enzi, na juu ya vile viti naliona wazee ishirini na wanne, wameketi, wamevikwa mavazi meupe; na juu ya vichwa vyao walikuwa na taji za dhahabu.

5 Na katika kile kiti cha enzi kunatoka umeme na sauti na ngurumo. Na taa saba za moto zilikiwaka mbele ya kile kiti cha enzi, ndizo Roho saba za Mungu.

6 Na mbele ya kile kiti cha enzi kulikuwa na mfano wa bahari ya kioo, kama bilauri; na katikati ya kile kiti cha enzi, na pande zote za kile kiti, walikuwako wenye uhai wanne, wamejaa macho mbele na nyuma”.

Ufunuo 5:11 “Nikaona nikasikia sauti ya malaika wengi pande zote za kile kiti cha enzi, na za wale wenye uhai, na za wale wazee, na hesabu yao ilikuwa elfu kumi mara elfu kumi na elfu mara elfu,

12 wakisema kwa sauti kuu, Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na baraka.

13 Na kila kiumbe kilichoko mbinguni na juu ya nchi na chini ya nchi ya juu ya bahari, na vitu vyote vilivyomo ndani yake, nalivisikia, vikisema, Baraka na heshima na utukufu na uweza una yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na yeye Mwana-Kondoo, hata milele na milele.

14 Na wale wenye uhai wanne wakasema, Amina. Na wale wazee wakaanguka, wakasujudu.

Sasa ni vizuri ukajiuliza kwanini walivyozidi kumkaribia Mungu, walionekana na maumbile tofauti tofauti. Ikumbukwe kuwa hao wote wanaozungumziwa hapo ni malaika, hakuna mwanadamu hata mmoja. Jiulize ni kwanini wawe ni wazee, na si vijana, na vilevile kwanini wale wenye Uhai wanne wawe na maumbile kama yale na si vinginevyo.?

Hiyo ni kufunua kuwa rohoni, na sisi tukitaka kumkaribia sana Mungu, basi hatuna budi kupitia hatua kama za wale wanaoonekana wapo karibu sana na Mungu.

Kwamfano tukiwatazama wale wazee 24, wanafunua kuwa ili mtu aweze kumkaribia Mungu sana, ni lazima awe ni mzee rohoni, awe amekomaa siku za wokovu ndani yake. Awe kama Ibrahimu, awe kama Henoko aliyetembea na Mungu kwa miaka 300 bila kumwacha, awe kama Eliya aliyemtumikia Mungu mpaka uzee wake, awe kama Ayubu, Hana, na Simoni, Zekaria na Elizabeti. Ambao hao walitembea katika haki yote na Mungu wao bila kumwacha. Watu wa namna hiyo, wanapomaliza siku zao hapa duniani, na wametembea na Mungu tangu ujana wao, mpaka kufa kwao, basi ni wazee rohoni. Na hivyo watakapovuka kule ng’ambo watakuwa karibu sana na Mungu.

Kwasababu Mungu naye, anajitambulisha kama mzee wa siku (Danieli 7:9). Hivyo na wale watakaomkaribia ni lazima wawe wameshiba siku za wokovu, Lakini ikiwa wewe unataka kuwa mkristo tu wa kufa ili uende mbinguni, hutaki kutenda mapenzi ya Mungu angali ukiwa hapa duniani, hutaki kukua kiroho, ujue kuwa ukifa leo hii, kamwe hutakaa umkaribie Mungu kule mbinguni, utakuwa mtu baki tu, haijalishi umeikwepa hukumu

Kwa urefu wa somo hilo fungua link hii>>

https://wingulamashahidi.org/2021/02/22/tutamkaribia-mungu-kwa-idadi-ya-mvi-zetu-rohoni/

Sasa tupige hatua mbele kidogo, kumbuka hawa malaika 24 ambao walifanana sana na wanadamu wazee 24 ni kweli walikuwa karibu na sana na Mungu, lakini wapo waliokuwa karibu zaidi ya Mungu kuliko wao. Na hao si wengine zaidi ya wale wenye uhai 4.

Wenye Uhai 4 walisimama moja kwa moja mbele ya kiti cha enzi cha Mungu, mbele ya wale wazee 24, Ndio makerubi wa Mungu. Hawa walikuwa na nyuso 4 kila mmoja. Uso wa kwanza upande wa kulia ulikuwa ni wa simba, upande wa kushoto ulikuwa ni wa ndama, upande wa nyuma ulikuwa ni wa Tai, na upande wa  mbele ulikuwa ni kama wa binadamu. Ndivyo Ezekieli alivyoonyesha kwa uwazi wote viumbe hai hao  jinsi walivyo (Ezekieli 1:1-26)

Japokuwa Yohana alionyeshwa upande mmoja mmoja wa kila kiumbe hai huyo kwasababu kulikuwa na sababu ya yeye kuonyeshwa vile, Lakini wote hao walikuwa na sura 4 kila mmoja wao (Soma Ufunuo 4).

Sasa kama tulivyotangulia kusema, haikuwa sinema tu, kwamba Mungu anataka kutuonyesha viumbe hao jinsi walivyo wa ajabu hapana. Bali alikuwa anatuonyesha kuwa na sisi tukitaka kumkaribia zaidi yeye. Ni lazima tuwe kama wao Rohoni, kwamba ni lazima uwe na sura hizo nne, ili ukidhi vigezo vya kuwa karibu sana na Mungu. hivyo tu.

Na leo kwa ufupi tutatazama kila uso wa hao makerubi, unawakilisha nini kwa leo. Tukianzana na ule..

USO WA SIMBA:

Kama tunavyojua simba ni mnyama jasiri asiye na woga,

Mithali 30:29 “Kuna watatu wenye mwendo wa kupendeza, Naam, wanne walio na mwendo mzuri.

30 Simba aliye hodari kupita wanyama wote; Wala hajiepushi na aliye yote;”

Kuonyesha kuwa kama mkristo, ni lazima uvae sura ya ujasiri kwa ajili ya imani yako na injili, kama Yesu Kristo alivyokuwa, na ndio maana anaitwa Simba wa Yuda (Ufunuo 5:6). Yeye hakuogopa mwanadamu yoyote, ilipofika suala la wokovu hata Herode alipotaka kumkamata, aliwaambiwa wale watu akisema “mwambieni Yule MBWEHA”!.. kuonyesha kuwa yeye hababaishwi na mwanadamu yoyote kuhubiri injili.

Vilevile na sisi ni lazima tuwe kama simba tukiwa hapa duniani kwasababu shetani naye hatufuati kama kondoo, bali kama Simba, biblia inasema hivyo katika 1Petro 5:8, Unategemea vipi na sisi tumwendee kwa upole katika kuuharibu ufalme wake?

USO WA NDAMA:

Upande wa kushoto wa vile viumbe walikuwa na uso wa ndama. Kama tunavyojua ndama ni wanyama wa kafara, wa kuchinjwa, wa kuchukua  dhambi za watu n.k. Hivyo hiyo ni kuonyesha kuwa unapokuwa mkristo ni lazima uso wa ndama/mwana kondoo, uwe nao pia. Yaani ukubali kuteseka kila siku kwa ajili ya manufaa ya wengine, na si yako tu peke yako. Ukubali hata kujinyima kwa ajili ya injili,

Paulo alisema..”Ninakufa kila siku”.. 1Wakor 15:31. Hata Bwana wetu Yesu Kristo alikuwa tayari kuutoa uhai wake kwa ajili yetu, ili sisi tupate ondoleo la dhambi. Vivyo hivyo na sisi kama wakristo, tunapaswa tuwe na uso huu wa ndama ndani yetu. Tuwe tayari kufa kila siku kwa ajili ya injili ya Kristo. Kujitoa ikiwemo na mali zetu  na nguvu zetu kwa ajili ya injili., kama alivyofanya Kristo na mitume wake.

USO WA TAI:

Wenye uhai 4 walikuwa na uso wa Tai kwa nyuma. Tai ni ndege anayeiona mbali sana, Jicho lake linaweza kuona chakula kutokea mbali sana, mahali ambapo wewe huwezi hata kumuona juu. Na sio tu chakula, bali pia maadui.

Na ndio maana Bwana Yesu alisema katika siku za mwisho, ni Tai tu ndio watakaoweza kuona chakula cha kweli cha roho kilipo. Wengine wote watakuwa kama kuku, wakisikia Kristo yupo huku wanakimbilia, yupo kule wanakimbilia, manabii wa uongo na imani potofu zikiwachanganya, wanabahatisha kwasababu macho yao hayawezi kuona mbali.

Luka 17:37 “Wakajibu, wakamwuliza, Wapi, Bwana? Akawaambia, Ulipo mzoga, ndipo watakapokutanika tai”.

USO WA MWANADAMU:

Wenye uhai 4 hawa walikuwa pia na nyuso wa binadamu kwa mbele.

Kumbuka mwanadamu, ndiye aliyejuu ya zaidi ya wanyama wote ambao Mungu alishawahi kuwaumba. Mwanadamu anao ujuzi, hekima, utashi, fikra, elimu, ujuzi, maarifa. Kwa kutumia tu utashi aliopewa na Mungu anaweza kubuni na kuvumbua mambo makubwa sana, ambayo yanaweza kumletea matokeo chanya au matokeo hasi. Inategemea na dhima yake ni nini.

Hivyo, Na sisi pia ni lazima tutumie utashi wetu tuliopewa na Mungu, kumpendeza Mungu. Sio kila mahali, tutatumia maombi tu peke yake hapana. Wakati ule Mungu anampa Musa maagizo ya kutengeneza vitu vya hemani, alimwambia akamtafute mtu aliyeitwa Bazaleli, ambaye Mungu atampa  ujuzi na utashi wa uchongaji wa vitu hivyo.

Kutoka 31:1 “Bwana akanena na Musa, na kumwambia,

2 Angalia, nimemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila ya Yuda;

3 nami nimemjaza roho ya Mungu, katika hekima, na maarifa, na ujuzi, na mambo ya kazi ya kila aina,

4 ili abuni kazi za ustadi, kuwa fundi wa dhahabu, na wa fedha, na wa shaba”,

Tujiulize je! Sisi tulishawahi kumbunia nini Mungu?  Watu wa ulimwengu wanatushinda, wao kila siku wanambunia mungu wao shetani, mambo mapya kila siku, mengi ya kuwavutia wao, wanamtungia kila aina ya nyimbo za miundo tofauti tofauti, lakini sisi kama wakristo, ujuzi wetu tuliopewa na Mungu tumeuweka kapuni, tukimwimbia Mungu badala tufikirie ni jinsi gani nyimbo zetu zitakuwa zimejaa Roho, sisi tunawaiga wale wa kidunia staili zao.

Bwana atusaidie sana.

Hivyo Bwana atusaidie sana. Nyuso zote hizo 4 tuwe nazo. Yaani tuwe jasiri kama Simba, tuwe wa kujitoa kama ndama, tuwe na jicho la kuona mbali chakula chetu kilipo kama Tai, na pia tuwe na hekima na ujuzi kama mwanadamu.

Tukiweza hayo, basi tujue kuwa tutakuwa karibu sana Mungu, kuliko tunavyodhani, kwasababu shetani anakuwa hana upenyo wa kutuingilia. Kwasababu kila upande kuna uso tunamwona.

Mwisho, kabisa, upako wa wenye uhai hawa wanne ulitembea pia katika nyakati saba za kanisa. Hivyo kama utapenda kufahamu kwa urefu juu ya nyakati hizo na jinsi mihuri ile ilivyofunguliwa basi fungua link hii utakutana na mfufulilizo wa maelezo hayo.

https://wingulamashahidi.org/2018/07/19/mihuri-saba/

Bwana akubariki sana.

Je! Umeokoka ndugu? Je! Una habari kuwa tunaishi katika kipindi ambacho tutashuhudia tukio la kurudi kwa pili kwa Kristo duniani?  Unalifahamu hilo? Kwasababu hakuna dalili hata moja Kristo aliyoizungumzia haijatimia. Ni heri ukayasalimisha maisha yako leo kwake, ili siku ile isikukute pabaya.

Tubu kwa kumaanisha kabisa, kisha kabatizwe katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo upate ondoleo la dhambi zako.

Jina la Bwana libarikiwe.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

UNYAKUO.

UFUNUO: Mlango wa 4

PINDO LA VAZI LAKE SASA LIMEREFUSHWA.

IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.

KAMA MKRISTO FAHAMU ZIPO HATUA UTAPIGISHWA NA MUNGU.

NYAKATI SABA ZA KANISA NA WAJUMBE WAKE.

Rudi nyumbani

Print this post

Mahali pa juu palikuwa ni wapi kama tunavyosoma katika biblia?

“Mahali pa juu” ni mahali palipoinuka ambapo watu walikwenda kutengeneza madhabahu na kutoa dhabihu zao.. Mahali hapo panaweza kuwa ni mlimani au mahali  penye mwinuko. Ilikuwa ni heshima kwa Mungu kutengeneza madhabahu mahali palipoinuka, kuonyesha kuwa yeye ni juu ya yote.

Ibrahimu ni moja ya watu wa kwanza kutenengeneza madhabahu mahali pa juu.. Wakati anamtoa Isaka mwanawe, alipanda juu ya Moria, na kutengeneza madhabahu pale, sasa mahali pale alipojenga madhabahu ile ndio mfano wa “mahali pa juu”..

Ifuatayo ni baadhi ya mifano michache juu ya mahali pa juu…

1Samweli 9:11 “Hata walipokwea kwenda mjini, wakakutana na wasichana, wanatoka kwenda kuteka maji; wakawaambia, Je! Mwonaji yuko?

12 Nao wakawajibu, wakasema, Yuko; tazama, yuko huko mbele yako; fanyeni haraka sasa, maana hivi leo amekuja mjini; kwa sababu WATU WANA DHABIHU LEO KATIKA MAHALI PA JUU”

Na pia tunaona kabla Mfalme Sulemani kujenga hekalu lile juu ya mlima Moria, naye pia alikuwa anatoa dhabihuu katika mahali pa juu..

1Wafalme 3:2 “Ila watu walikuwa wakichinja dhabihu katika MAHALI PA JUU, kwa sababu haikuwapo nyumba iliyojengwa kwa jina la Bwana, hata siku zile.

 3 Sulemani naye akampenda Bwana, akienda katika amri za Daudi babaye, ila hutoa dhabihu na kufukiza uvumba katika MAHALI PA JUU”

Mistari mingine inayozungumzia mahali pa juu ni pamoja 1Nyakati 16:39, 1Nyakati 21:29.

Lakini pamoja na hayo, walikuwepo pia watu waliotengeneza madhahabu katika mahali pa juu kwaajili ya miungu yao… popote walipopaona pameinuka walizitengeneza madhabahu hizo, na kuitolea dhabihu miungu hiyo, jambo ambalo lilikuwa ni chukizo kubwa sana kwa Bwana.

1Wafalme 14:22 “Basi Yuda wakafanya maovu machoni pa Bwana; wakamtia wivu, kwa makosa yao waliyoyakosa, kuliko yote waliyoyafanya baba zao.

23 Maana hao pia wakajijengea MAHALI PA JUU, na nguzo, na maashera, juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi”.

Unaweza pia kusoma 2Wafalme 16:4, 2Wafalme 17:9-11,29, utaona jambo hilo hilo..

Swali ni je! Mahali petu pa juu pa leo ni wapi?..mahali ambapo tunaweza kumtengenezea Mungu wetu madhahabu inayompa heshima yeye?.

Tusome,

Yohana 4:19  “Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii!

20  Baba zetu waliabudu katika MLIMA HUU, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia.

21  Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu.

22  Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi.

23  LAKINI SAA INAKUJA, NAYO SASA IPO, AMBAYO WAABUDUO HALISI WATAMWABUDU BABA KATIKA ROHO NA KWELI. KWA MAANA BABA AWATAFUTA WATU KAMA HAO WAMWABUDU

24  Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli”

Umeona mahali petu palipoinuka leo ni wapi?..Si milimani, wala si mahali penye miinuko, bali ni katika roho zetu. Huko ndiko madhabahu za Mungu aliye juu zinapotengenezwa.

Je ndani ya roho yako ipo madhabahu ya Mungu?..au ya miungu?..Haijalishi utakuwa unakwenda kanisani, au unatoa sadaka lakini kama mahali pa juu (yaani ndani ya roho yako), hakuna madhabahu ya Mungu, basi fahamu kuwa bado unaitumikia miungu migeni. Kama moyoni mwako kuna anasa, ulevi, wizi, uasherati, na mengineyo, bado wewe ni najisi mbele za Bwana.

Mathayo 15:19  “Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati; wivi, ushuhuda wa uongo, na matukano”.

Bwana atusaidie tumjengee madhabahu bora katika roho zetu.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Nini maana ya “heri mtu asiyekaa barazani pa wenye mizaha?”

Kwanini madhabahu zilitengenezwa kwa mawe yasiyochongwa?

Mungu anaposema “nitaliweka jina langu” ana maana gani?

Swali: Kurushwa upesi kunakozungumziwa katika Danieli 9:21 ndio kupi?

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

Rudi nyumbani

Print this post