Category Archive Wanawake

MWANAMKE ULIYEKOMAA KI-UMRI, ITAMBUE HUDUMA YAKO.

Ni kwanini wakati mwingine tunaona kama kuna mambo hayaendi sawa katika kanisa la Kristo, kwasababu tunafiri mambo yote yanatatuliwa na mchungaji, au mwalimu au mwinjilisti peke yake..

Kila kiungo katika mwili wa Kristo kinayo kazi yake, hivyo kimoja kisipowajibika ipasavyo ni lazima tu mapungufu yataonekana haijalishi vile vingine vitawajibika kiasi gani…

Leo hii utajiuliza ni kwanini wanawake wengi wanayo malezi mabaya ya watoto.. utakuta mwanamke anaye mtoto lakini hana heshima au maadili, au anaye mtoto lakini kichwani pamejaa miziki ya kidunia na wakati huo huo hajui hata mstari mmoja wa biblia..Unadhani hiyo inatokana na nini? Inatokana na mtu mmoja kushindwa kutimiza jukumu lake katika kanisa la Kristo.

Au utakuta mwanamke hamuheshimu mume wake, anajibizana naye kama mtoto, hajui kuwa ni agizo la Mungu kila mke amuheshimu mume wake, kama vile sisi tunavyomuheshimu Kristo na kila mume ampende mke wake, kama vile Kristo anavyotupenda sisi..Lakini yeye hilo si kitu kwake, anaona ni kawaida tu, na bado anafahamika kama mkristo, unadhani kilichomfanya awe na tabia hizo ni nini? ni kwasababu mtu Fulani hakutimiza jukumu lake katika kanisa, alimwachia mchungaji, au mtumishi Fulani afanye yeye kila kitu.

Au kwanini wanawake wengine, hawatulii katika shughuli zao, majumbani mwao, kinyume chake, ni kujizungusha mitaani, kutafuta habari za wengine, wanakosa staha, wanavaa mavazi yasiyo na heshima, nusu uchi wanakatiza barabarani, na bado ni waimba kwaya,…Unadhani hiyo inatokana na nini wakati mwingine? Ni kwasababu mtu Fulani hakutimiza jukumu lake katika mwili wa Kristo..

Paulo alimwandikia Timotheo maneno haya, akamwambia..

Tito 2:3 “Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema;

4 ILI WAWATIE WANAWAKE VIJANA AKILI, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao;

5 na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe”.

Unaona hapo biblia inaeleza wazi kabisa huduma ya mwanamke mzee ni ipi kanisani…Kumbuka mwanamke mzee sio lazima awe ni mzee kikongwe, lakini walau mwanamke ambaye ameshafikia umri wa makamo, ameshapitia mambo mengi hususani katika ndoa, anajua jinsi gani ya kuishi na mume katika Kristo..

Ikiwa wewe ni mmojawapo na upo katika kanisa, basi fahamu kuwa unalo jukumu zito la kuwasimamia ipasavyo wanawake vijana, ukijionyesha kwanza wewe mwenyewe kama kielelezo, kwa mwenendo wako wa utakatifu na tabia. Kisha ndio uwafundishe na kuwasimamia mabinti, na wanawake vijana jinsi ya kuishi kama mwanamke wa Kikristo..

Vinginevyo usipofanya hivyo, ujue kuwa jina la Mungu linatukanwa kwa ajili yako.

Hi ni huduma kubwa sana katika kanisa, lakini cha kushangaza ni kwamba mwanamke huyu huyu mzee na yeye anataka awe mchungaji kwasababu anaona huduma aliyopewa kama vile ni ndogo haijulikani.. Hafahamu kuwa hata katika kanisa wanawake huwa ndio wengi kuliko wanaume, hivyo kama huduma basi yeye ndio mwenye huduma kubwa ya kuwaangalia watu kuliko mwanaume, lakini hilo halitaki, anataka yeye naye asimame mimbarani, ahubiri kama askofu mkuu Fulani, au mwalimu Fulani au nabii fulani..Na matokeo yake ndio unakuta migogoro mingi ya kifamilia mara mwanaume huyu kagombana na mkewe kwasababu hamuheshimu mara Yule kapigwa na memewe n.k..mwisho wa siku jina la Mungu linatukanwa kwasababu tu kiungo Fulani kanisani kilishindwa kutimiza kusudi lake.

Ikiwa wewe ni mama, leo hii tambua jukumu lako. Na ufahamu kuwa Kristo anaiheshimu sana huduma yako kama tu anavyoliheshimu lile la mchungaji, na askofu…na kama utafanya vizuri ina thawabu kuliko hata hizo zinazoonekana ni kubwa kuliko nyingine.

Bwana akubariki.

Shalom

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

NAFASI YA MWANAMKE KATIKA KANISA

JE NI DHAMBI KUWA NA MAHUSIANO KABLA YA NDOA?

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA WARAKA WA PILI WA YOHANA.

TUJIFUNZE JAMBO KWA WANAWAKE HAWA WAWILI:

USHAURI KWA MWANAMKE WA KIKRISTO.

Rudi Nyumbani:

Print this post

Je mama mjamzito anaruhusiwa kufunga?

Je mama mjamzito anaruhusiwa kufunga?..Na je watoto wadogo wanaruhusiwa kufunga na kusali? Na je inawezekana kufunga siku 40 bila kula?..

Kabla ya kufahamu kama mama mjamzito anaruhusiwa kufunga au la!..Hebu jiulize swali lifuatalo..{Je! Mtu katika hali ya kawaida anaruhusiwa kufunga siku 40 bila kula wala kunywa?..Au inawezekana mtu kufunga siku 40 bila kula wala kunywa na asife?}

Kama jibu ni ndio! basi Mjamzito naye anaweza kufunga.

Bwana Yesu alifunga siku 40 mchana na usiku bila kula wala kunya na hakufa…Na Mjaribu ibilisi alipomjia na kumwambia ageuze jiwe kuwa mkate..alimjibu na kumwambia imendikwa ..”mtu hataishi kwa mkate tu, bali kwa kila Neno litaokalo katika kinywa cha Mungu”

Mathayo 4:1 “Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ili ajaribiwe na Ibilisi.

2 Akafunga siku arobaini mchana na usiku, mwisho akaona njaa.

3 Mjaribu akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe mikate.

4 Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu

Kama imewezekana mtu kuishi  siku 40 bila kula wala kunya na hajafa basi inawezekana mjamzito au mtu mwingine yeyote yule kufunga bila kupatikana na madhara yoyote isipokuwa tu afunge kwa Imani na si kwa kutimiza wajibu fulani, au kulazimishwa…

Nimewahi kukutana na kumthibitisha mtu binafsi ambaye amemaliza siku 40, bila kunywa wala kunywa na hawajafa…na wapo wengi tu wengine wanaokwenda mfungo hata wa wiki 2, 3 hadi 4..bila kula wala kunywa na wanaishi vizuri tu…Shetani anachowadanganya watu wengi siku hizi ni kwamba “jambo la kufunga siku 40 kama Bwana Yesu siku hizi halipo”…Huo ni uongo wa shetani..

Hivyo mwanamke mjamzito anaweza kufunga hata katika hiyo hali ya ujauzito na isimuathiri yeye wala mtoto..

Lakini afunge tu kwa Imani, na si kwa dini wala mazoea, wala kulazimishwa..kama atafunga kwa dini na mazoea au kwa kulazimishwa basi ni afadhali asifunge kwa maana atapata madhara…lakini akifunga kwa Imani, huku binafsi akijiweka katika imani, utakatifu na ukamilifu,.. anaweza kumaliza hata siku 40 na mtoto akazaliwa akiwa na afya yake kamili na baraka tele.

Na sio tu mama mjamzito anaruhusiwa kufunga bali hata watoto..Wengi hawawaruhusu watoto wao wafunge wakihofia kwamba watadhoofika..Huo pia ni uongo wa shetani..mtoto kama anasukumwa ndani yake kufunga, hapaswi kuzuiliwa kwasababu “Mtu  hataishi kwa mkate tu bali kwa kila Neno litokalo katika kinywa cha Mungu”…Na Neno lenyewe ndio hilo kwamba ” mambo mengine hayawezekaniki isipokuwa kwa kufunga na kusali”. Hivyo watoto wadogo wanaruhusiwa kufunga kama watu wazima.

Maran atha!


Mada Nyinginezo:

MSIJISUMBUE KWA NENO LOLOTE.

Je! taratibu za kufunga ndoa [yaani harusi] ni agizo la Mungu au ni mapokeo tu ya kibinadamu?

SIKU ILE NA SAA ILE.

Adamu alikuwa na watoto wangapi?

Rudi Nyumbani:

Print this post

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA WARAKA WA PILI WA YOHANA.

Tukiachilia mbali ule waraka wa kwanza ambao Mtume Yohana aliuandika kwa watu wote, zile nyaraka mbili za mwisho zilizosalia hakuzielekezwa kwa watu wote, bali kwa watu husika, na tunaona ndio zimekuwa nyaraka fupi kuliko zote katika biblia nzima, lakini zimebeba ujumbe wa msingi sana, kwa makundi ya watu waliozungumziwa huko..Kwa mfano kama tukiutazama ule waraka wa tatu, tunasoma mtume Yohana aliuelekeza kwa ndugu mmoja anayeitwa GAYO.

Sasa wengi wanaupenda mstari mmoja maarufu sana unaotoka katika kitabu kile unaosema..”MPENZI NAOMBA UFANIKIWE KATIKA MAMBO YOTE NA KUWA NA AFYA YAKO, KAMA VILE ROHO YAKO IFANIKIWAVYO.(3YOHANA 1:2)”..Ni mstari unaopendwa na kila mmoja kwasababu ni mstari unatoa Baraka na mafanikio..Lakini tunashindwa kuelewa kuwa waraka ule haukuandikwa kwa watu wote bali kwa mtu anayeitwa GAYO peke yake ndio aliyeambiwa maneno yale ya baraka, na ni lazima ujue ni kwanini Baraka zile alizistahili yeye na si mwingine kutoka kwa Mungu, na kwa kujifunza kupitia yeye na sisi ndio tunaweza kustahili kupata Baraka kama zile, kwa ufupi kama ukisoma pale utagundua kuwa mtu huyu alikuwa na moyo wa kipekee sana, aliwakaribisha wageni waliokuwa wanasafiri kwa ajili ya kazi ya Mungu, alijitoa kwa ajili ya Bwana kweli kweli, aliwahudumia watumishi wa Mungu waliokwenda kuhubiri nchi za ugenini, kwa hali na mali kiasi cha kwamba hata watumishi hao waliosafirishwa na yeye wakawa hawana mahitaji yoyote kutoka kwa watu wasioamini, Hivyo sifa zake zikavuma katikati ya makanisa yote mpaka kuwafikia mitume..Na ndipo ukija kusoma utaona maneno hayo ya Baraka yanatamkwa mbele yake..

Sasa leo utamwona mtu ni mkristo lakini hata kutoa kitu kidogo kwa Mungu wake anaona shida, na huyo huyo bado ndio wa kwanza kumwambia Mungu, ulisema nifanikiwe katika mambo yote..Hajui kuwa ili Mungu akubariki kwa Baraka kama hizo kuu na nono sio hivi hivi tu..BALI KWA WATU WENYE TABIA KAMA ZA GAYO. Watu ambao hawapo tayari kuona kazi ya Mungu haikwamishwi na kitu chochote.

Vile vile na leo tutaona kwa ufupi juu ya ujumbe ulio katika huu Waraka wa PILI wa Yohana, je! Unamhuhusu nani?. Ni vema ukapata muda wa kuusoma wote peke yako. kwanza ni mfupi na pia itakusaidia tuende pamoja katika uchambuzi huu tunaokwenda kuuangalia..

Tunasoma…

3Yohana 1:1 “Mzee, kwa MAMA MTEULE, na watoto wake niwapendao katika kweli; wala si mimi peke yangu, bali na wote waijuao ile kweli;

Awali ya yote tunaona Hapa mtume Yohana anajitambulisha kama MZEE, na sio kama mtume, au mtumwa wa Kristo, kufikisha ujumbe kama mkomavu, mtu aliyekula chumvi nyingi, anafahamu mambo mengi yahusuyo kanisa na shamba la Mungu kwa ujumla, anayejua jinsi ya kupambanua mitego ya Yule mwovu aliyowahi kuiona katika maisha yake ya kikristo, na jinsi mitego hiyo inavyoweza kunasa makundi mbali mbali ya watu na namna yake, “kijana kwa wazee”, watoto kwa wakubwa, waume kwa wake, n.k.

Hivyo hapa waraka huu tunaona moja kwa moja anaulekeza kwa MAMA MTEULE..Na sio mama tu wa kawaida, Bali anasema mama MTEULE tena pamoja na watoto wake..Hivyo ni wazi kuwa ujumbe huu unawahusu WANAWAKE WOTE, WALE WALIO WATEULE WA KRISTO, ambao wameshaokolewa, ambao walishaoshwa dhambi zao kwa damu ya Yesu Kristo, ambao neema ya Mungu tayari ipo juu yao siku zote, ambao ni watakatifu tena wenye watoto,.

Sasa yapo mambo 3 makuu yalipaswa yazingatiwe au yameonekane katikati wanawake watuelu wa Mungu wa namna hiyo..Na ndio hayo tutayatazama leo katika vipengele vyake. Jambo la kwanza ni..

1) KUWAONGOZA WATOTO KATIKA KWELI:

Kama ukisoma hapo utaona mzee huyu alianza kwanza kwa kuchunguza hali ya watoto wa mama Yule mkristo,katika nyumba yake, na kutamani sana kuona jinsi alivyoweza kuwajali watoto wake au watu wa nyumbani kwake kwa kuhakikisha kuwa wanamcha Mungu, wanadumu katika utakatifu, alitamani kumwona mama huyu jinsi ambavyo angejitoa katika kuangalia hali ya kiroho ya watoto wake kuliko kitu kingine chochote wakifanyacho.. na kama tunavyosoma ni kweli mwanamke huyu mteule alikuwa nacho Tunasoma.

1:1 “Mzee, kwa mama mteule na watoto wake niwapendao katika kweli; wala si mimi peke yangu, bali na wote waijuao ile kweli;

2 kwa ajili ya hiyo kweli ikaayo ndani yetu, nayo itakuwa pamoja nasi hata milele.

3 Neema, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Yesu Kristo Mwana wa Baba, zitakuwa pamoja nasi katika kweli na upendo.

4 Nalifurahi mno kwa kuwa nimewaona baadhi ya watoto wako wanaenenda katika kweli, kama vile tulivyopokea amri kwa Baba”.

Unaona hapo mstari wa 4 anasema.

“4 Nalifurahi mno kwa kuwa nimewaona baadhi ya watoto wako wanaenenda katika kweli, kama vile tulivyopokea amri kwa Baba.”

Hivyo ikiwa wewe ni mama, na unataka kuitwa MTEULE wa Kristo, Swali ni je!.unahakikisha watoto wako wanaenenda katika misingi ya kumjua Mungu?, Unawakemea wanapotenda dhambi au unawaangalia tu, je! Unafuatia hali zao za kiroho, au kila wakati upo buzy kufuatilia tu mahudhurio yao ya shuleni na huku mahusiano yao na Mungu yanadorora kila siku. Watoto wako mstari mingapi ya biblia wanaifahamu mpaka sasa, lakini nyimbo za kidunia kila siku unawasikia wakiimba lakini huwasemeshi? Na bado unajiita MAMA MTEULE wa Kristo unayempenda Mungu….Huo sio uteule mama, siku ile hautakuwepo katikati ya wanawake wateule wa Kristo kama wakina SARA na HANA, na wengineo ikiwa utawaona watoto wako wanapotea na wewe huwasemeshi kitu, ikiwa utawaona hawamjui Mungu na wewe hutaki kuwafundisha, unawanunulia kila siku vitabu vipya vya shuleni lakini biblia huwanunulii, unawalipia tution kila siku lakini fellowship na bible study huwapeleki…Huo sio uteule mama…Hali kadhalika na wewe ambaye bado hujawa na watoto, je! Hayo malengo yapo kwenye kichwa chako?

2) KUWA NA UPENDO:

Jambo la pili Mzee huyu alilotamani kuliona katikati ya mwanamke huyu mteule wa Kristo ni UPENDO.

Tunasoma.

“5 Na sasa mama, nakuomba, si kwamba nakuandikia amri mpya, bali ile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo, kwamba tupendane.

6 Na huu ndio upendo: tuenende kwa kuzifuata amri zake. Hii ndiyo ile amri, kama mlivyosikia tangu mwanzo kwamba mwenende katika hiyo”.

Unaona hapo? Anasema Hii ndiyo ile amri, kama mlivyosikia tangu mwanzo kwamba mwenende katika hiyo. Sasa Amri hiyo aliyokuwepo tangu mwanzo ni ipi?

Marko 12:29 “Yesu akamjibu, Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja;

30 nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.

31 Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.”

Umeona hizo mbili zote alitazamia kuziona kwa mwanamke huyu, ahakikishe kuwa kumpenda Mungu kupo ndani yake siku zote, juu ya kulea watoto katika kweli lakini pia kumcha Mungu kuwepo ndani yake, awe na amani kuwepo uweponi mwa Bwana, awe mwombaji, au msomaji wa Neno.

Na pia awapende ndugu, kwa furaha kabisa kama vile biblia isemavyo upendo huvumilia, upendo hauhusudu, upendo haujivuni, upendo hauhesabu mabaya,.

Lakini mwanamke anayesema ameokoka, lakini hana habari na Mungu, hataki kujifunza maneno ya Mungu, hata kusali kwake ni shida, huruma hana, ni msengenyaji wakati wote, hana uvumilivu ndani yake, akiudhiwa kidogo tu, yeye naye anaanza kusengenya. Na suala hili limekuwa hafifu kwa wanawake wengi, na hivyo kimekuwa kikwazo kikubwa sana cha UTEULE WAO pasipo wao kujijua, Hivyo kama wewe ni mwanamke na unajiita mteule fanyia kazi hilo kwa bidii, shindana na usengenyaji huo mpaka uushinde.

3) KUJILINDA NA WADANGANYIFU. 

Hili ndio jambo la tatu na la mwisho mzee huyu mwenye hekima alimwomba mama huyu mteule alizingatie. Hapa anaendelea kusema..

“7 KWA MAANA WADANGANYIFU WENGI WAMETOKEA DUNIANI, wasiokiri ya kuwa Yesu Kristo yuaja katika mwili. Huyo ndiye yule mdanganyifu na mpinga Kristo.

8 Jiangalieni nafsi zenu msiyapoteze mliyoyatenda, BALI MPOKEE THAWABU TIMILIFU.

9 Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana Mungu. Yeyeadumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia.

10 Mtu akija kwenu, naye haleti mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani mwenu, wala msimpe salamu.

11 Maana yeye ampaye salamu azishiriki kazi zake mbovu”.

Tazama hapo anasema “KWA MAANA WADANGANYIFU WENGI WAMETOKEA DUNIANI”,…Sasa kumbuka kama wadanganyifu hawa walitokea wakati ule, watotokea na sasa, na pia zingatia jambo hili ili usichanganyikiwe roho ya mpinga-kristo ni ile ile, lakini utendaji wake kazi unabadilika kulingana na nyakati na majira. Wadanganyifu waliokuwepo wakati ule wa mitume walikuwa na kazi moja tu, yaani Kumkana Kristo kuwa hakufufuka..Kwasababu habari ya ukristo ndio kwanza zilikuwa zinaanza kuhubiriwa, Hivyo shetani ili kuuuwa ukristo usiaminiwe na wengi kwa wakati ule, alitumia udanganyifu wa kuwa Kristo hajafufuka, na pia hawezi kurudi katika mwili..Hao ndio walioitwa wapinga-kristo wa wakati ule, na ndio hao Mzee huyu alikuwa anamwonya mama huyu MTEULE ajitenge nao pamoja na mafundisho yao…Kwasababu kwa uzoefu wake wa rohoni Mungu aliompa aliona kuwa wanawake wengi wateule ndio wanaokuwa rahisi kuchuliwa na wimbi hili na wapinga-kristo zaidi ya wanaume wateule,.(sisemi kuwa wanaume hawadanganyiki), hapana bali wengi ni wanawake.

Lakini roho ile ile ya udanganyifu, inatenda kazi hata sasa isipokuwa kwa namna ya ujanja mkubwa zaidi, mpaka kufikia hatua Bwana Yesu kusema wakati huo watawadanganya yamkini hata walio WATEULE…Hivyo roho hii ya udanganyifu haiji tena kwa kusema Yesu hakufufuka, au haikuambii Yesu hatarudi, kwani mpaka sasa shetani anafahamu kuwa hakuna mkristo asiyejua kuwa Kristo alifufuka, na Yesu siku moja atarudi..kila mtu analijua hilo, lakini badala yake anakuja na udanganyifu mwingine nao ndio huu “Kushusha thamani ya wokovu na injili ya YESU KRISTO.”

Kuwafanya watu wasichukulie tena kwa uzito na umakini habari za wokovu, watu wajue kuwa ni kweli Yesu anaokoa lakini maisha yao yasiathiriwe na wokovu huo,anahakikisha kuwa mtu anakuwa vuguvugu, nusu kwa Mungu nusu kwa dunia, injili ya kisasa, injili ya I don’t care, injili ya “haijalishi!”..injili ya kutabiriwa tu mafanikio basi, lakini mambo ya toba yasigusiwe kabisa..Na hali hiyo inawalewesha hata wale ambao walikuwa wamesimama waanze kuwa vuguvugu.

Na roho hii inawakamata sana sana wakina mama, tena hata wale wateule, na ndio maana hapo Mtume Yohana anamwambia. “9 Kila apitaye cheo, wala asidumu katika MAFUNDISHO YA KRISTO, yeye hana Mungu”.

Umeona, njia pekee ya kuwatumbua hao ni kudumu katika mafundisho ya Kristo (Yaani Neno la Mungu)…

Webrania 12: 14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao;

Hivyo ikiwa wewe ni mwanamke mteule unayetaka kupokea THAWABU TIMILIFU kama huyu mama, hakikisha unaufanya imara uteule wako kama maandiko yanavyosema, kwa kuzingatia hayo mambo matatu kuwa yapo ndani yako.

2 Petro 10 “Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na UTEULE WENU; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe”.

Mungu akubariki. Tafadhali “Share” ujumbe huu kwa wengine. Na Bwana atakubariki zaidi.

Kwa maombezi/ Ushauri/ Ratiba za Ibada/Maswali/ Whatsapp/ Piga namba hizi: +255693036618/ +255789001312


Mada Zinazoendana:

TWEKA MPAKA VILINDINI.

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA WARAKA WA TATU WA YOHANA.

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA KITABU CHA RUTHU

TOA HUDUMA ILIYO BORA.


Rudi Nyumbani

Print this post

NAFASI YA MWANAMKE KATIKA KANISA

Nafasi ya mwanamke katika kanisa ni ipi? Je anaruhusiwa kuwa mchungaji, au askofu?

Mtume Paulo alisema,..

 1Wakoritho 14;34 “Wanawake na wanyamaze katika kanisa, maana hawana ruhusa kunena bali watii, kama vile inenavyo torati nayo. Nao wakitaka kujifunza neno lo lote, na wawaulize waume zao wenyewe nyumbani mwao; maana ni aibu wanawake kunena katika kanisa. Au je! Neno la Mungu lilitoka kwenu? Au kuwafikia ninyi peke yenu? Mtu akijiona kuwa ni nabii au mtu wa rohoni, na ayatambue hayo ninayowaandikia, ya kwamba ni maagizo ya Bwana”

Hapa maandiko yanaweka wazi kabisa mwanamke hana nafasi ya uongozi wowote katika kanisa, au kutatua tatizo lolote katika kanisa, Mungu aliuweka huu utaratibu, kulifundisha kanisa, maana mwanamke anawakilisha kanisa la Kristo, na kama vile kanisa limtiivyo Kristo katika kila Neno vivyo hivyo na wanawake wanapaswa kujitiisha chini ya waume zao ikiwemo kuongozwa kwa kila jambo kama maandiko yanavyosema kwenye..

 Waefeso 5:22-23Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. 

23 Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili.

24 Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo.   Kwahiyo mwanamke hajapewa mamlaka yeyote ya kumtawala mwanamume iwe kanisani au nyumbani, Kichwa cha mwanamke ni mwanamume na kichwa cha mwanamume ni Kristo.

Sasa zile huduma tano zilizozungumzwa katika waefeso 4:11( “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe”) hizi zilitolewa kwa wanaume tu ,ofisi hizi tano ni za uongozi katika kanisa hakuna hata moja inayomhusisha mwanamke. ikiwemo maaskofu na mashemasi wote wanapaswa wawe wanaume.

Na Bwana Yesu alitoa sababu katika

 1timotheo 2:11-14 ” Mwanamke na ajifunze katika utulivu, akitii kwa kila namna.Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe katika utulivu. Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye.Wala Adamu hakudanganywa, ila mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa.”

kwahiyo hapa tunaona kuwa Hawa ndiye aliyedanganywa na sio Adamu. Na Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, kama tu vile sisi tunavyowatii wazazi wetu pasipo shuruti na kuwaheshimu na kuwapa mamlaka yote katika familia ni kwasababu wao ndio waliotutangulia kwanza duniani na ndio waliotuzaa, lakini tunawapa heshima yao je! si zaidi kwa mwanamke kumtii Adamu aliyetoka katika ubavu wake na ndiye aliyeumbwa wa kwanza??..

Kuna baadhi ya wanaojiita watumishi wa Mungu wanaoingiza harambee za kijamii katika kazi ya Mungu na kufundisha kuwa kila kitu mwanaume anachofanya, mwanamke pia anaweza kufanya, hawajui kwamba wanaenda nje ya mpango wa Mungu kwa maana kila jambo Mungu aliweka kwa utaratibu na kwa kulifundisha kanisa.

Tunaona mitume 12 wote wa Bwana Yesu walikuwa ni wanaume, katika agano la kale hakuwahi kuwa na kuhani mwanamke, ilikuwa inafahamika hivyo tangu awali shughuli zote zinazohusu madhabahu ya Bwana zilikuwa zinafanywa na wanaume, lakini mambo haya yalianza kujitokeza ilipofika kuanzina karne ya 20 mpaka leo wanawake walipoanza kutafuta haki sawa ndipo hapo walipoanza kujiingiza katika siasa, na  leo hii shetani amefanikiwa kuingiza hiyo roho katika kanisa na kufanya madhabahu ya Mungu itawaliwe na wanawake. Haya ni machukizo mbele za Mungu, na ni dhambi yenye uzito ule ule sawa na wasiokuwa wa kabila la walawi kuhudumu katika nyumba ya Mungu kwenye agano la kale.

Swali ni je! wanawake wanaofanya hivyo Mungu hayupo nao??

Ni siri kubwa imekaa hapo ambayo watu wengi hawaijui, wanapoona mtu anatenda miujiza, vipofu wanaona, unabii unatolewa n.k. wakidhani ndio uthibitisho kuwa mtu huyo yupo katika njia sahihi biblia inasema

Mathayo 7:22-23 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.

22 Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?

23 Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.”

Kwahiyo tunaona haijalishi unatenda miujiza kiasi gani, uthibitisho pekee wa Mungu kuwa na wewe ni kuyatenda mapenzi ya Mungu ambayo ni kuishi katika Neno lake, na NENO lake ndilo hilo

Mwanamke na ajifunze katika utulivu, akitii kwa kila namna.Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe katika utulivu ” 

Kwahiyo yoyote aendaye kinyume na hayo anaenda nje ya maagizo ya Bwana haijalishi ni miujiza kiasi gani inatendeka kwenye huduma yake, anafanya kazi isiyokuwa na faida.

Je! kazi ya mwanamke ni ipi katika kanisa?
Kuna zile karama Mungu alizitoa kwa wote, kwa mwanaume na mwanamke. (ijulikane kuwa karama ni tofauti na huduma) ukisoma..

1wakoritho 12:4-10 ” Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule.

Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule.

Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote.

Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana. mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; ” 

 Hivyo basi Mungu anaweza kumtumia mwanamke kutoa unabii/ujumbe katika kanisa lakini sio kufundisha. Mungu anaweza kumtumia mwanamke kuponya wagonjwa, kunena kwa lugha, kutoa unabii, hizi zote ni karama za Mungu na anaweza kumtumia yeyote, lakini zile huduma ambazo ni ofisi kuu tano yaani, mitume, manabii, wainjilisti,waalimu na wachungaji, ikiwemo na mashemasi, hizi ni huduma za uongozi wa kanisa, na hazimuhusu mwanamke hata kidogo.

Wanawake wanapaswa kujifunza, kwa kuuliza maswali kwa mtu yeyote ikiwemo mchungaji wake yahusuyo masuala yake ya kiroho na pia kuruhusu karama za Mungu kutenda kazi ndani yake, ikiwemo, kunena kwa lugha, kutoa unabii, uponyaji, ishara na miujiza, ndoto,kumsifu na kumwimbia Mungu wao, na kushuhudia wengine katika nafasi uliyopo kwa jinsi Mungu atakavyokujalia.

Isipokuwa kufundisha au kuhubiri kanisani au kumtawala mwanaume kwa namna yoyote na kufungua huduma na kujiita mchungaji, au mwinjilisti au askofu au mwalimu au mtume ni makosa, kama ulishawahi kufanya hivyo pasipo kujua jirekebishe na ukae katika nafasi uliyoitiwa.

Mungu akubariki.


Mada Nyinginezo:

TUZO UTAPEWA KULINGANA NA NAFASI YAKO.

NJIA KUU YA KUINGIA KATIKA ULE MJI.

KWANINI MUNGU ANAMPA NABII HOSEA MAAGIZO YA KUMUOA MWANAMKE KAHABA? (HOSEA 3)

KUTOKA 10:1 “BWANA ANASEMA ATAMPA FARAO MOYO MGUMU, ASIMTII, JE! HAPO BWANA ATAMHUKUMU FARAO KAMA MKOSAJI SIKU ILE?”


Rudi Nyumbani

Print this post