NI KITU GANI TUNAJIFUNZA KWA RISPA, BINTI AYA?

NI KITU GANI TUNAJIFUNZA KWA RISPA, BINTI AYA?

Jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, Natumai u mzima, karibu tujifunze Maneno ya Uzima kama ilivyo wajibu wetu, maadamu siku ile inakaribia.

Leo tutatazama kwa ufupi juu ya aliyoyatenda mwanamke mmoja aliyeitwa Rispa, mwanamke huyu alikuwa ni suria wa mfalme Sauli. Sasa ilitokea siku moja Israeli ilipitia katika njaa ya mfulilizo wa miaka mitatu, hakuna mvua yoyote juu, mpaka wakajiuliza ni nini hiki? Maandishi ya zamani tofauti na biblia yanasema Daudi akajiuliza pengine kuna watu wanaabudu miungu kwa siri, wakaangalia wakaona mbona sio, wakaangalia kwa kila namna, na wakachunguza kila kitu lakini bado hakuna kilichowapa jibu,

Ndipo Daudi akaona aende moja kwa moja kumuuliza Mungu, pengine labda ni yeye kamkosea, Lakini Mungu akamjibu na kumwambia kuwa kosa lipo katika nyumba ya mfalme Sauli, kwa kuwa yeye alikwenda kuwaua watu ambao walishaingia nao maagano tangu zamani kwamba hawatawaua kwa kinywa cha akina Yoshua (Yoshua 9:15)

Lakini mfalme Sauli hilo hakulijali, akawaua hao watu (wagibeoni), ndipo Mungu akaliona hilo na kuifanya nchi ya Israeli ikae katika njaa kwa miaka mitatu mfufulizo..

Sasa Daudi alichokifanya ni kuwaendea wale wagibeoni, na kuwauliza wawafanyie nini, ili hiyo laana indoke juu yao, ndipo Wagibeoni hawakutaka kitu kingine chochote, bali walitaka tu kumlipizia kisasi Sauli kwa uzao wake, hivyo wakamwomba wapewe wazao wa Sauli waliobaki wawaue kwa kuwatundika kwenye miti milimani. Ndipo Daudi akawajalia haja yao, akawapa wana 7 wa Sauli.

Sasa wawili kati ya hao wana 7 walikuwa wa huyu suria mmoja wa Sauli aliyeitwa Rispa. Tusome.

2Samweli 21:9 “akawatia mikononi mwa Wagibeoni, nao wakawatundika mlimani mbele za Bwana, nao wakaangamia wote saba pamoja; wakauawa siku za mavuno, za kwanza, mwanzo wa mavuno ya shayiri.

10 Naye Rispa, binti Aya, akatwaa nguo ya magunia akajitandikia mwambani, tangu mwanzo wa mavuno hata waliponyeshewa mvua toka mbinguni; wala hakuacha ndege wa angani kukaa juu yao mchana, wala wanyama wa mwitu usiku”.

Unaweza kutengeneza picha mama anayeona watoto wake wakiuliwa kikatili mbele ya macho yake, kwa makosa ya watu wengine, halafu hawazikwi, wameachwa pale msalabani ni uchungu kiasi gani, anausikia..

Lakini kama tunavyosoma hapo huyu Rispa, hakuondoka pale mlimani, bali tangu siku hiyo watoto wake walipotundikwa, alikaa pale pale, kuhakikisha kuwa maiti za wanawe zinaheshimiwa, hakuruhusu ndege aje kula mizoga yao, wala usiku fisi waje kula mifupa.. Na zamani zile ilikuwa mizoga haiondolewi kwenye miti, mpaka hapo Mungu atakapojibu maombi, hivyo kama majibu yakija baada ya wiki moja, ndipo inashushwa pale mtini, yakija baada ya mwezi mmoja ndipo itakaposhushwa, vivyo hivyo hata yakija baada ya mwaka mzigo hiyo itaendelea kubakia pale mtini kwa mwaka mzima.

Na maandiko yanatuambia, mama yule hakuondoka pale mchana wala usiku tangu mwanzo wa mavuno ya shayiri mpaka mvua iliponyesha.. Mwanzo wa mavuno ya yashiri ni mwenzi wa 3-4, na mvua kunyesha ni mwezi 10..Hivyo mwanamke huyu alikaa pale mlimani kwa kipindi kisichopungua miezi 6..

Tengeneza picha, usiku na mchana, unafanya kazi ya kulinda, kuhakikisha maiti za wanao hazivunjiwi heshima kama mizoga ya wanyama, kwa kuliwa na ndege au fisi..alikaa pale mpaka ikawa ni mifupa tu imening’inia lakini hakuruhusu fisi achukue hata kidole cha wanawe.

Lakini tukirudi huku upande wa pili, Daudi akashangaa japokuwa tumewatimizia Wagibeoni haja zao, lakini mbona kama mvua inachelewa tena kwa miezi kadhaa?

Ndipo akasikia kuwa kumbe mama wa wale watoto wawili, tangu kipindi kile cha mauaji, hakuondoka pale mlimani akilinda maiti za wanawe.

Hilo likamfikirisha sana Daudi,, akawaza, kama mama huyu anazithamini maiti na mifupa ya wanawe waliotundikwa mitini na wao sio kitu kikubwa sana, Si zaidi mimi kuthamini mifupa ya Mfalme Sauli aliyeuliwa vivyo hivyo kama wao, (1Samweli 31:10-13) isitoshe ni mtiwa mafuta wa Mungu, mfalme wa Israeli na mimi sijui hata mifupa yake ilipo, Ndipo Daudi akatuma watu kwenda kuichukua mifupa ya Sauli iliyokuwa mbali sana, ng’ambo ya mto Yordani, akaileta Israeli, wakaifanyia maombolezo ya kitaifa, akaichanganya akaichukua ni mifupa ya wale watoto 7 waliouliwa, wakaenda kuzikiwa pamoja.

2Samweli 21:11 “Kisha akaambiwa Daudi hayo aliyoyafanya huyo Rispa binti Aya, suria wa Sauli.

12 Akaenda Daudi, akaitwaa mifupa ya Sauli na mifupa ya Yonathani mwanawe mikononi mwa watu wa Yabesh-gileadi; waliyoiiba katika njia ya Bethshani, hapo Wafilisti walipowatungika, katika siku hiyo waliyomwua Sauli huko Gilboa;

13 naye akaileta toka huko hiyo mifupa ya Sauli, na mifupa ya Yonathani mwanawe; nao wakaizoa mifupa yao waliotundikwa.

14 Kisha wakaizika mifupa ya Sauli na ya Yonathani mwanawe katika nchi ya Benyamini, huko Zela, kaburini mwa Kishi babaye; wakafanya yote aliyoyaamuru mfalme. Na baadaye Mungu aliiridhia hiyo nchi”

Na kwa tukio hilo likapelekea Mungu kuileta mvua juu ya nchi.

Ni nini tunajifunza?

Bidii ya mwingine, na kujali kwa mwingine, kunaweza kukawa sababu ya wewe Mungu kukuzuilia baraka zako. Unasema wewe ni mkristo, umeokoka, Lakini Mungu akimtazama mtu mwingine ambaye hamwabudu Mungu mkuu unayemwabudu wewe lakini ana bidii usiku na mchana ya kumtafuta mungu wake, ujue kuwa mbingu itazuliwa juu yako.. Haijilishi utasema umeokoka kiasi gani.

Ikiwa watu wa dini nyingine wanamfanyia mungu wao dua mara 5 mpaka 10 kwa siku, lakini wewe unaambiwa uombe lisaa limoja kwa siku, huwezi unategemea vipi mbingu isifungwe juu yako?, Hata kama utakuwa umetimiza vigezo vingine vyote, yule mwingine atabakia kuwa hukumu tu kwako.

Yatupasa tujirekebishe, ikiwa wao wanafunga siku 30 kila mwaka, sisi tunapaswa tuende zaidi ya hapo, lakini kama inapita mwaka mzima hujawahi kufunga hata wiki moja, mbingu zitafunga tu juu yako.

Ikiwa wanazingatia kushika aya za vitabu vyao vya dini kwa bidii, lakini wewe mkristo hujui hata biblia inavitabu vingapi, hujawahi hata kusoma kitabu kimoja cha biblia ukakimaliza chote, unasubiria tu kuhubiriwa, mbingu zitafungwa juu yako. Mpaka siku utakapojua tatizo ni nini.

Hivyo sote tujitathmini, Na Bwana atusaidie.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

JE TATIZO LA KULA KUCHA NI ISHARA YA KUWA NA MAPEPO?

SAUTI AU NGURUMO?

CHOCHOTE UMFANYIACHO KRISTO KINA THAMANI.

JINSI YA KUJIWEKA KARIBU NA MUNGU.

HATUTAACHA KUJIFUNZA NENO KILA INAPOITWA LEO.

IJUE NGUVU YA IMANI.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments