Category Archive Home

INJILI YA KRISTO HAITANGAZWI KWA HATI MILIKI.

Ni kitu cha kushangaza jinsi injili ya Kristo, Bwana wetu  inavyogeuzwa leo hii kutoka katika kitu cha kutolewa bure hadi kuwa kitu cha kutolewa kwa masharti,.Tunaweza tukadhania ni ustaarabu mzuri kufanya hivyo lakini kibiblia huo haukuwa mpango wa Kristo tangu zamani alipowaita mitume wake..kwasababu ni jambo linalozuia injili ya Kristo kusonga mbele. Na leo tutaona ni kwa namna gani.

Embu tafakari kwa utulivu jambo hili walilolifanya mitume, na majibu Bwana YESU aliyowapa,

Marko 9:38 “Yohana akamjibu, akamwambia, Mwalimu, tulimwona mtu akitoa pepo kwa jina lako, ambaye hafuatani nasi; tukamkataza, kwa sababu hafuatani nasi.

39 Yesu akasema, Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya mwujiza kwa jina langu akaweza mara kuninenea mabaya;

40 kwa sababu asiye kinyume chetu, yu upande wetu”.

Mitume walipomwona mtu huyu anatenda kazi zile zile wanazozifanya wao, wanatumia jina lile lile wanalolitumia wao, tunaweza kusema pia anawabatiza watu vilevile kama wanavyowabatiza wao, anafufua wafu vilevile kama wanavyofufua wao, badala ya wao kumfurahia na kumchukua wafanye naye kazi pamoja, kinyume chake wanamkemea na kumkataza kwamwe asikae kufanya kitu kama hicho tena, pengine walimtisha na kuahidi kumshitaki endapo atarudia kutumia jina hilo bila idhini yao…Na hiyo yote ni kwasababu moja tu, kwamba HAFUATANI NAO basi! Hakuna kingine, wala hakuna ubaya wowote waliuona ndani yake…ni kwasababu tu HAFUATANI NAO! Embu jaribu kufikiria mtu yule alipotoka pale alivunjika moyo kiasi gani..ule moto uliokuwa ndani yake ulizimishwa ghafla kwa kiasi gani, alikuwa anahubiri injili kwa kujifichaficha akiogopa labda pengine wale watu watamwona tena na kumkamata na kumpeleka kwa kadhi.

Na Zaidi ya yote alitegemea pengine hao Mitume ndio wangekuwa wakwanza kumsapoti lakini kinyume chake wakawa wakwanza kumpinga.

Hata leo hii, Hicho ndio kikwazo cha watumishi wengi wa Mungu, wapo watu wengi wanaotamani kumhubiri Kristo kwa mafundisho yao, au vitabu vyao, au nyimbo zao, lakini wanatishwa na vikwazo vya namna hiyo, wanaogopa wakifanya tu, watakamatwa na kuambiwa ni nani kakupa ruhusu ya kusambaza hiki au kile.

Wameiwekea injili hati miliki kwamba mtu huwezi kufundisha wanachokifundisha wao, mpaka upewe kibali fulani kutoka kwao, huwezi kuziimba nyimbo zao mahali fulani mpaka upewe kibali fulani kutoka kwao, ili ulipie kwanza kiwango fulani cha fedha..Injili ya Kristo nayo imegeuzwa na kuwa kama staili ya kibiashara hivi, kwamba mtu fulani amegundua aina yake ya mafundisho basi hataki mwingine aibe aifundishe sehemu nyingine, ameimba nyimbo fulani, hataki mwingine aiimbe mahali pengine kwa utukufu wa Mungu..lengo tu ni ili nyimbo yake isichuje haraka au aitwe yeye aimbe ili apate faida kidogo..Ndivyo ilivyo sasa hivi.

Kipindi fulani nyuma, kuna ndugu nilimuhubiria akakata shauri la kuokoka, hivyo akawa anahitaji abatizwe pia, kwa kuwa mkoa aliokuwepo ni mbali kidogo na mimi nilipo ikanibidi nimtafutie kanisa la kiroho liliokaribu naye abatizwe na adumu katika fundisho la pale, lakini nilipopiga simu na mhudumu mmojawapo wa kanisa alipokea, ili nimkabidhishe huyo mtu kwake, kuzungumza naye tu maneno machache na kugundua mimi sio mshirika wa makanisa yao, akasema mimi ni ndugu wa uongo, ni nani aliyenipa ruhusu hiyo, hawakutaka kusikia habari yangu, hata na huyo kondoo ambaye alikuwa anatafuta malisho..Nilihuzunika na kushangaa sana,..kwani hawakuangalia faida ya Kristo bali waliangalia je kama hichi kitu kinatoka katika jumuiya yao ya kidini kama mitume walichokuwa wanajaribu kukifanya.

Vitabu au Makala za Kikristo tunazozichapishwa, tunachopaswa kuzuia tu kwa wale wanaofanya na kuuza kwa biashara, lakini kama ni mtu ameona upo ujumbe mzuri ndani yake ambao unaweza kuwabadilisha wengine, hivyo akaamua kwenda kuchapisha Makala hizo nyingi na kwenda kuzitoa bure kwa watu wengine bila hata ya kukueleza, au kupata idhini yako, wewe unakwazika nini katika hilo? wewe hofu yako ni nini? Kwani kazi hiyo ni yako au ya Kristo?. Kwanini kila kitu unawaza kukiwekea mipaka na vizuizi, hujui kuwa kazi ya Kristo inasimama kwa ajili yako. Mwingine akisikia kuna mtu kahubiri mahali pengine kitu alichokihubiri yeye na hajatajwa jina anapata wivu?.

Kwanini upate wivu? Kuna umuhimu gani wa kukutaja wewe kama kweli una Nia ya Kristo ndani yako? Unapaswa ufurahi kwasababu ulichokizaa wewe kimekwenda kuzaa vingine vingi, sasa hiyo si ni faida? Wengine mpaka wanawapa masharti wanaowahubiria kwamba watakapohubiri mafundisho yao mahali pengine wawataje!.

Yule mtu aliyekuwa anatenda miujiza kwa jina la YESU alitambua kabisa kuwa Kristo mwenyewe yupo duniani, na kwamba angetaka kwenda kumwomba ruhusa angekwenda, lakini yeye hakuona hata ulazima wa kumwomba Ruhusa mwenye jina lenyewe badala yake aliliondoka kimya kimya na kwenda kuuendeleza ufalme,..Na Kristo hakumkemea kwa hilo wala kumwita kutaka kumjua, aliona ni sawa tu..aendelee..

Iweje sisi ambao hata hatumwoni Kristo tuwazuie wengine wasimtangaze Kristo kwa kazi zetu?. Jitafakari vizuri wewe unayejiita kiongozi wa dini, wewe unayejiita mchungaji, wewe unayejiita mwalimu, wewe unayejiita mwandishi, wewe unayejiita MWIMBAJI WA NYIMBO ZA INJILI wewe unayejiita mwinjilisti, wewe unayejiita mshirika…

Usiwe kikwazo cha injili ya Kristo kuhubiriwa.

Shalom.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

HATARI YA KUHUBIRI INJILI TOFAUTI NA ILIYOANDIKWA KWENYE BIBLIA.

KIWANGO CHA TATU CHA IMANI.

SADAKA YA MALIMBUKO.

Yeshuruni ni nani katika biblia?

Rudi Nyumbani:

Print this post

NINI MAANA YA KUSAGA MENO?

NINI MAANA YA KUSAGA MENO?

Kusaga meno ni kitendo cha kung’ata meno kwa nguvu kutokana na maumivu fulani au uchungu fulani. Kwamfano mtu aliyejikata na kisu au kujikwaa kwenye kidole utaona atang’ata meno kwa nguvu kutokana na maumuvi anayoyasikia au uchungu au hasira fulani (Soma Matendo 7:54).

Na hata wakati mwingine mpaka kung’ata huku yanasuguana. Sasa kitendo hicho ndicho kinachoitwa kusaga meno.

Katika biblia kuna sehemu kadha wa kadha zimezungumzia tendo hilo. Kwamfano utaona Bwana Yesu alipozungumzia juu ya  mateso yaliyopo Jehanum hakuacha kuhusisha tendo la usagaji wa meno. Ikifunua kuwa Jehanamu sio mahali pa raha. Bali pa mateso makali sana.

Alisema.

Mathayo 13:41  “Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi,

42  na kuwatupa katika tanuru ya moto, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno”.

Mathayo 25:30 “Na mtumwa yule asiyefaa, mtupeni mbali katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno”. 

Mistari mingine inayofanana na hiyo, inayozungumzia kitendo cha kusaga meno ni pamoja na Zaburi 37:12, Mathayo 8:12, Mathayo 13:50. Mathayo 22:13, 25:30, Marko 9:18 na Luka 13:28.

Hiyo yote inalenga kutuonyesha ukali wa mateso yaliyopo Jehanum. Kwamba si sehemu nzuri, kutakuwa na maumivu makali na mateso kwa wale wote ambao hawajampokea Kristo na waliorudi nyuma.

Kama hujampa Yesu Kristo maisha yako, ni vyema ukafanya hivyo kabla muda wako wa kuishi duniani haujaisha. Unachopaswa kufanya ni kutubu tu mahali ulipo. Unatubu dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kisha unatafuta ubatizo sahihi wa maji tele na kwa jina la YESU KRISTO kulingana na Matendo 2:38. Kwa ajili ya kukamilisha wokovu wako.

Na kama ulishabatizwa katika vigezo hivyo hapo juu basi hauhitaji kubatizwa tena. Na mwisho kabisa Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu atakayekusaidia kushinda dhambi.

Bwana akubariki.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

USIZITEGEMEE NGUVU ZAKO KUKUSAIDIA!

KWA KUWA NGUVU ZA MBINGUNI ZITATIKISIKA.

JE ! BWANA YESU ALIKUJA DUNIANI KUAMUA NINI?

Kwanini Bwana Yesu alisema pale msalabani naona kiu?

Rudi Nyumbani:

Print this post

USIZITEGEMEE NGUVU ZAKO KUKUSAIDIA!

usizitegemee nguvu zako kukusaidia katika jambo lolote!

Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze Biblia, Neno la Mungu ambalo ni Taa iongozayo miguu yetu na mwanga wa njia zetu (Zab.119:105).

Leo tutajifunza kwa ufupi, ni jinsi gani Bwana hapendezwi na sisi kuzitegemea nguvu zetu wenyewe, au kuwategemea wanadamu katika matatizo yanayotukabili. Au kutegemea vitu tulivyojiwekezea.

Tutajifunza kwa kumtazama Mtu anayeitwa Daudi. Ambaye wakati Fulani alikengeuka kidogo na kutaka kuzitegemea nguvu zake mwenyewe badala ya kumtegemea Mungu. Jambo ambalo lilimchukiza sana Mungu..Ingawa aliwahi kwenda kutubu lakini tayari lilikuwa limeshaleta madhara makubwa sana katika Taifa la Israeli.

Kama ni msomaji mzuri wa Biblia utakumbuka kuna wakati Mfalme Daudi wazo lilimwingia la kwenda kuwahesabu watu. Na kama utakumbuka jambo hilo lilimchukiza sana Mungu na kusababisha watu wengi kufa Israeli. Ingawa jambo hilo Mungu aliliruhusu makusudi ili kuwalipiza kisasi wana wa Israeli kwa makosa yao. Lakini bado halikuwa mpango kamili wa Mungu.

Tunasoma Daudi alikwenda kuwahesabu watu wote na kupata jumla ya mashujaa laki 8 wenye kufuta upanga katika Israeli na mashujaa laki 5 katika Yuda..Hivyo jumla ya mashujaa waliokuwa ni milioni moja na laki tatu.(1,300,000) Hiyo ni idadi kubwa sana ya watu.

Tusome.

2Samweli 24:1 “Tena hasira ya Bwana ikawaka juu ya Israeli, akamtia Daudi nia juu yao, akisema, Nenda, ukawahesabu Israeli na Yuda.

2 Basi mfalme akamwambia Yoabu, jemadari wa jeshi la askari, waliokuwa pamoja naye, Zunguka sasa katikati ya kabila zote za Israeli, tangu Dani mpaka Beer-sheba, mkawahesabu watu, nipate kujua jumla ya hao watu………..”

8 Nao walipokwisha kuzunguka nchi yote, wakaja Yerusalemu mwisho wa miezi kenda na siku ishirini.

9 Naye Yoabu akamtolea mfalme jumla ya hesabu ya watu; nao walikuwa wa Israeli mashujaa wenye kufuta panga mia nane elfu; nao wa Yuda walikuwa watu mia tano elfu.

10 Ndipo moyo wake Daudi ukamchoma baada ya kuwahesabu hao watu. Naye Daudi akamwambia Bwana, Nimekosa sana kwa haya niliyoyafanya; lakini sasa, Ee Bwana, nakusihi uuondolee mbali uovu wa mtumishi wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa.

11 Na Daudi alipoondoka asubuhi, neno la Bwana likamjia nabii Gadi, mwonaji wake Daudi, kusema,

12 Nenda, ukanene na Daudi, Bwana asema hivi, Nakuwekea mambo matatu; katika haya uchague moja, nikutendee hilo.

13 Basi Gadi akamwendea Daudi, akamweleza, akamwambia, Basi, miaka saba ya njaa ikujie katika nchi yako? Au miezi mitatu ukimbie mbele ya adui zako, huku wakikufuatia? Au siku tatu iwe tauni katika nchi yako? Fanya shauri sasa, ufikiri, ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma.

14 Naye Daudi akamwambia Gadi, Nimeingia katika mashaka sana; basi sasa na tuanguke katika mkono wa Bwana; kwa kuwa rehema zake ni nyingi; wala nisianguke katika mkono wa wanadamu”.

Sasa ukichunguza Nia ya Daudi hasa haikuwa kujua idadi ya watu wote waliokuwemo Israeli, bali utagundua kuwa Nia yake kuu ilikuwa ni kujua idadi ya wanajeshi au mashujaa alionao wa vita waliokuwepo kwenye ufalme wake wote. Kumbuka Daudi alikuwa ni mtu wa Vita. Muda wote alikuwa amezungukwa na maadui hivyo alitaka kwenda kuwahesabu wanajeshi wake ili ajiwekee matumaini katika jeshi hilo.

Hapo kabla Daudi alikuwa hajui anao idadi ya wanajeshi wangapi, alikuwa anamtegemea tu Mungu asilimia 100, ikitokea vita anaita idadi ya wanajeshi waliopo, bila kujali watakuwa ni wachache kiasi gani ukilinganisha na maadui zao kwasababu Bwana ndiye aliyekuwa jemedari wake.

Ndio maana utaona karibia kila mahali Daudi alikuwa anasema..

Zaburi 20: 7 “Hawa wanataja magari na hawa farasi, Bali sisi tutalitaja jina la Bwana, Mungu wetu.

8 Wao wameinama na kuanguka, Bali sisi tumeinuka na kusimama.

9 Bwana, umwokoe mfalme, Utuitikie siku tuitayo”.

1Samweli 17: 45 “Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana.

46 Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli.

47 Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya Bwana, naye atawatia ninyi mikononi”

Lakini Daudi Mtu ambaye alikuwa hategemei majeshi kumwokoa. Sasa hapa anaanza kujitumainisha katika hayo. Alikuwa hategemei mikuki, panga wala fumo sasa anaanza kuvitegemea kwa kutaka kujua idadi ya wanajeshi walioshika upanga. Amesahau kuwa miaka yote Mungu hakuwahi kumwokoa kwa wingi wa jeshi au silaha alizonazo.

Hiyo ikawa ni dhambi kubwa sana ikasababishia Mungu kuyapunguza hayo majeshi yake aliyoyahesabu, kwa kuleta Tauni, wakafa watu elfu 70. Na tena hapo ni kwasababu tu ya Rehema za Mungu kuwa nyingi, endapo Bwana asingeachilia Rehema zake. Watu milioni kadhaa wangekufa. Na hayo majeshi aliyojitumainia nayo yatakuwa wapi?…Usizitegemee nguvu zako.

Ndio maana Bwana Yesu alisema mfano huu katika kitabu cha Luka.

Luka 12:19 “Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi.

20 Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?

21 Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu”.

Je! Tumaini lako liko wapi? Kwenye mali ulizo nazo?. Au hazina ulizo nazo, au vitega uchumi vyako?. Au watoto wako?, au idadi ya wafanyakazi ulio nao? Au Bwana?. Usianze kusema sasa nina mali nyingi au fedha nyingi au salio kubwa kwenye akaunti yangu basi kesho yangu itakuwa safi, kesho yangu itakuwa ya ushindi, bali useme Ninaye Bwana moyoni mwangu kesho yangu itakuwa safi, kesho yangu itakuwa ya Baraka na ya mafanikio haijalishi niacho hiki au sina, kwasababu Bwana ndiye ngome yangu na jabali langu.

Kama ni Bwana ndiye tegemeo lako, basi umechagua fungu jema ambalo hutakuja kujutia kamwe! usizitegemee nguvu zako..Wakati wengine wanataja hazina zao wewe utalitaja jina la Bwana wa Majeshi, wakati wengine wanatumaini vitu vya ulimwengu huu, wewe unamtumainia Bwana.

Lakini kama humtumainii Bwana na unajitumainisha katika vitu ulivyowekeza hapa duniani. Kumbuka Yaliyompata Daudi yanaweza kukupata na wewe. Watu aliojitumainia Daudi kwa kwenda kuwahesabu walipunguzwa kwa Tauni ya siku tatu tu. Kadhalika Bwana atasambaratisha kila kitu unachojitumainisha kwacho leo hii. Atapunguza mali ulizonazo, atapunguza hata kile kidogo ambacho ulikuwa umeshakianza. Kwasababu yeye anasema ni Mungu mwenye wivu. Hawezi kuruhusu Vitu vya Ulimwengu huu vichukue nafasi yake yeye. Usizitegemee nguvu zako.

Bwana akubariki sana. Kama hujampa Yesu Kristo maisha yako, ni vyema ukafanya hivyo leo. Kwasababu saa ya wokovu ni sasa na si Kesho. Tubu kwa kumaanisha kuacha dhambi na Bwana atakusamehe na kukuokoa.

Maran atha! jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

UNYAKUO.

Ni sahihi kumuita Mariamu mama wa Mungu?

JISHUSHE ILI MUNGU AKUHUDUMIE.

TIMAZI NI NINI

Rudi Nyumbani:

Print this post

HATUTAACHA KUJIFUNZA NENO KILA INAPOITWA LEO.

Je! Kuna umuhimu wowote wa kujifunza Neno kila siku?

Unajua ni kwasababu gani leo hii tunaomwona Mtume Paulo ni mtu aliyekuwa amejaa mafunuo ya ndani kabisa yamuhusuyo Mungu na YESU KRISTO kiasi cha Mungu kufikia hatua ya kuyafanya mafundisho yake kuwa muhamala mkuu wa kanisa hadi sasa, ni kwasababu mtume Paulo hakuwa mtu wa kuchoka kusoma na kujifunza neno kila iitwapo leo,..Hakuwa mtu wa kulizoelea Neno la Mungu…

Tunaweza kuona mpaka wakati wa kukaribia kufa kwake, wakati anampa Timotheo maagizo ya kuliongoza na kulichunga kanisa, ameshakuwa mzee kabisa amebakisha kipindi kifupi sana cha kuishi, lakini bado anamwagiza Timetheo ampelekee vitabu vya nyaraka za maandiko avisome, kwasababu alijua bado anayo mengi ya kujifunza..

2Timotheo 4:6 “Kwa maana, mimi sasa namiminwa, na wakati wa kufariki kwangu umefika.

7 Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda;

8 baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake.

……… 13 Lile joho nililoliacha kwa Karpo huko Troa, ujapo ulilete, na vile vitabu, hasa vile vya Ngozi’

Paulo mtu aliyehubiri Injili tangu ujana wake, Aliyekutana na Yesu uso kwa uso, alifunuliwa siri za ndani kabisa ambazo hata Mitume wengine hawakufunuliwa wakati wakiwa na Bwana Yesu hapa duniani.,..Aliyenyakuliwa mpaka mbingu ya tatu, na kuonyeshwa mambo ambayo hayaelezeki kwa namna ya kibinadamu, lakini bado mtu kama huyo hakuchoka kujifunza neno mpaka siku ya kufa kwake…Bado aliendelea kusoma kwa bidii, akitazamia Mungu kumfunulia mambo mpya ambayo hakuwahi kuyafahamu..Anamwambia Timotheo, Ujapo uvilete vile vitabu vya ngozi..

Hii inatufundisha kuwa kupokea mafunuo ni kitendo endelevu, hatupaswi kuridhika tu na kile tunachokifahamu au tulichopewa kukijua sasa na Mungu bali kila siku tunapaswa tumwombe Mungu azidi kutufumbua macho Zaidi na zaidi katika Neno lake, na kutia bidi katika kusoma Neno lake.

Ndicho alichokifanya Danieli, yeye mwanzoni kabisa ukisoma ile sura ya pili ya kitabu cha Danieli, utaona Mfalme Nebukadneza aliota ndoto ya ile sanamu kubwa yenye kichwa cha dhahabu, kifua cha fedha, kiuno cha shaba na miguu ya chuma..Ambayo Danieli alipewa tafsiri yake inayohusiana na falme 4 zitakazotawala ulimwenguni mpaka mwisho wa dunia..

Lakini utaona Danieli hakuridhika na ufunuo ule peke yake, utaona kwenye sura ya 7 anaonyeshwa mambo ya ndani Zaidi kuhusiana na zile falme 4, ambayo hakufunuliwa katika ile njozi ya kwanza ya Mfalme Nebkadneza, alionyeshwa tabia ya zile falme jinsi zitakavyosimama na kuanguka…Ukiendelea kusoma sura ya 8 utaona tena anaelezwa mambo ya ndani Zaidi jinsi falme zile zitakavyokuwa..Ukizidi kusoma kuanzia ile sura ya 11 hadi ya 12 sasa Ndivyo utakavyooona jinsi Danieli anafunuliwa mambo yote kwa uwazi anaelezwa tukio baada ya tukio kikitoka hichi kinafuata hichi, kuanzia ule ufalme aliokuwepo mpaka ule unaomfuata baada yake…

Ndipo Danieli akaelewa sasa, na ukisoma pale utaona alitamani kuendelea kufahamu Zaidi juu ya matukio ya siku za mwisho, lakini malaika yule alimwambia aache hayo si ya wakati wake bali ayatie muhuri yatafunuliwa siku za mwisho..Ni wazi kuwa kama asingeambiwa vile basi Danieli angetusaidia kujua kila tendo litakalotokea katika siku zetu hizi za mwisho.

Lakini kama angesema Ah! Huu ufunuo Mungu atakaonipa wa ziada kuhusu ndoto ya Mfalme Nebukadneza. Ule alionipa unatosha hakuna haja ya kujifunza neno na kumwomba Mungu anifunulie Zaidi basi Danieli angebakia kujua tu zipo falme 4 zitakazotawala mpaka mwisho wa dunia basi, lakini habari za chukizo la uharibifu asingezijua, habari za hukumu ya mwisho asingezijua, habari za kuja kwa masihi asingezijua, habari za Kristo kusulibiwa asingezijua, habari za majuma sabini asingejua, habari za dhiki kuu asingezijua…Endapo tu angeridhika na hali ile ile ya ufunuo aliyopewa. Na hata ukizidi kusoma utagundua Danieli alikuwa mtu msomaji sana wa vitabu, mpaka akafikia kugundua miaka Israeli waliyotabiriwa kukaa Babeli.

Danieli 9:2 “katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danielii, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la Bwana lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini”

Vivyo hivyo na sisi Mungu atusaidie tujifunze, juu ya mambo haya, tusiridhike katika hali tuliyopo, tukaona kwamba kwasababu tumeisoma biblia nzima basi hakuna jambo jipya tunaweza kujifunza tena, kwasababu tumeshausoma mstari huu au ule, basi huyu muhubiri hawezi kutuambia tena jambo jipya hapo..Neno la Mungu halina ubobeaji..

Mungu anataka sisi tukue kifikra, tukue kiimani, vilevile tukue kiroho, kutoka katika hali ya uchanga hadi hali ya utu uzima kuelewa mambo ya ndani kabisa ya rohoni.. Mafumbo magumu na hiyo yote ni kama tutakuwa tayari kujifunza neno kila siku maneno ya Mungu pasipo kuyazoelewa.

Mungu akubariki sana. Ikiwa bado hujaokoka, nadhani utakuwa unafahamu kuwa hizi ni siku za mwisho, na kwamba moja ya hizi siku parapanda italia, na wafu watafufuliwa, na kuungana na watakatifu waliopo duniani na kwa pamoja kwenda kumlaki Bwana YESU mawingu. Kuelekea katika karamu ile ya mwanakondoo, ambayo Mungu aliindaa tangu enzi na enzi kwa wale waliookolewa..Sasa utajisikiaje ikiwa wewe utakosekana katika karamu hiyo? Mimi sitaki kukosa wewe je?..Utajisikiaje umebaki huku duniani kwenye dhiki ya mpinga kristo halafu baada ya hapo uishie kwenye ziwa la moto?..Angalia jinsi Mungu alivyotupenda, kutupa YESU KRISTO ili atuokoe sisi bure kwa damu yake.

Hivyo anakuita na wewe ayaokoe Maisha yako. Tubu popote pale ulipo, ukabatizwe kisha atakupa amani ambayo utadumu nayo hadi siku ya kuja kwake.

Ubarikiwe sana.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

RUDIA, TENA NA TENA KUMWOMBA MUNGU USIKATE TAMAA.

TABIA YA KIPEKEE USIYOIJUA KUHUSU NENO LA MUNGU.

JISHUSHE ILI MUNGU AKUHUDUMIE.

UNATAKA KUBARIKIWA? BASI USIKWEPE GHARAMA ZAKE.

Ni sahihi kumuita Mariamu mama wa Mungu?

Rudi Nyumbani:

Print this post

Roho Mtakatifu ni nani?.

Watu wengi wanajiuliza Roho Mtakatifu ni nani? Jibu  rahisi ni kuwa Roho Mtakatifu ni Roho ya Mungu, Mungu anayo Roho kama vile mwanadamu alivyo na roho, hakuna mwanadamu yeyote asiye na roho.

Na Biblia inasema katika Mwanzo 1:26 kwamba Mwanadamu aliumbwa kwa mfano na sura ya Mungu. Ikiwa na maana kuwa kama mwanadamu ana nafsi halikadhalika Mungu naye anayo nafsi, na kama mwanadamu anayo roho vilevile na Mungu naye anayo Roho. Kwasababu tumeumbwa kwa sura yake na kwa mfano wake. Na kama vile mwanadamu anao mwili halikadhalika Mungu naye anao mwili.

Na Mwili wa Mungu si mwingine zaidi ya ule uliodhihirishwa pale Kalvari miaka 2000 iliyopita. Nao ni mwili wa Bwana Yesu Kristo, hivyo Yesu Kristo ndiye Mungu mwenyewe aliyedhihirishwa katika Mwili. Hivyo aliyemwona Yesu amemwona Mungu (Yohana 14:8-10)

1Timotheo 3:16 “Na bila shaka siri ya utauwa ni kuu. Mungu alidhihirishwa katika mwili, Akajulika kuwa na haki katika roho, Akaonekana na malaika, Akahubiriwa katika mataifa, Akaaminiwa katika ulimwengu, Akachukuliwa juu katika utukufu”.

Huyo ni Yesu anayezungumziwa hapo.

Na kadhalika roho iliyokuwepo ndani ya Mwili wa Bwana Yesu Kristo ndio Roho ya Mungu na ndiye ROHO MTAKATIFU MWENYEWE. Tunalithibitisha hilo katika kitabu cha.

Matendo 16:6 “Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia.

7 Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa,

8 wakapita Misia wakatelemkia Troa”.

Sasa utauliza kama Roho wa Yesu ndiye Roho Mtakatifu iweje mahali pengine Bwana Yesu anaonekana amejaa Roho Mtakatifu?. Na mahali pengine anaonekana Roho Mtakatifu akishuka juu yake?

Jibu ni kwamba, Roho wa Mungu hana mipaka kama roho zetu sisi wanadamu zilivyo na mipaka, sisi wanadamu Mungu alivyotuumba roho zetu mipaka yake ni katika miili yetu.

Haziwezi kutenda kazi nje ya fahamu zetu au miili yetu.Haiwezekani niongee na wewe hapa na wakati huo huo roho yangu ipo China. Hilo haliwezekani kwetu sisi wanadamu, isipokuwa kwa Mungu linawezekana. Roho wake anauwezo wa kuwa kila mahali, ndio maana wewe uliopo Tanzania utasali muda huu na mwingine aliyepo China atasali na mwingine aliyeko Amerika atakuwa anamwabudu Mungu muda huo huo na wote Roho Mtakatifu akawasikia na kuwahudumia kila mtu kivyake. Huyo huyo anao uwezo wa kuwepo mbinguni, na duniani ndani ya Mwili wa Bwana Yesu na wakati huo huo kuzimu, hakuna mahali asipofika.

Ndio maana utaona alikuwa ndani ya Kristo, na bado akashuka juu ya Kristo, na akaachiliwa juu yetu siku ile ya Pentekoste.

Hiyo ndiyo tofauti ya Roho wa Mungu na roho ya mwanadamu. Roho zetu zina mipaka lakini Roho wa Yesu hana mipaka.

Na ni kwanini Roho wa Yesu anajulikana kama Roho Mtakatifu?

Ni kwasababu yeye ni Roho Takatifu, hiyo ndio sifa kubwa na ya kipekee Roho wa Yesu aliyoibeba..Yeye ni mtakatifu na hachangamani na uchafu.

Na ndio maana uthibitisho wa Kwanza kabisa wa Mtu aliyempokea Roho Mtakatifu ni kuwa Mtakatifu. Umepokea uwezo wa kufanyika mwana wa Mungu, unakuwa kama YESU. Naamini mpaka hapo utakuwa umeshafahamu Roho Mtakatifu ni nani?

Je! Umepokea moyoni mwako? kama bado ni kwanini? Biblia imesema ahadi hiyo ni ya bure na tunapewa bila malipo, kwa yeyote atakayemwamini.

Matendo 2:39 “Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie”.

Gharama za kumpata huyo Roho si fedha bali ni Uamuzi tu! Ukimtafuta Mungu kwa bidii utampata Neno lake linasema hivyo..

Hivyo kanuni rahisi sana ya kumpata ni KUTUBU kwanza: Yaani unamaanisha kuacha dhambi kwa vitendo, kisha kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi wa maji tele (Yohana 3:23) na kwa jina la Yesu kwaajili ya ondoleo la dhambi kulingana na Matendo 2:38 ili kuukamilisha wokovu wako. Na Roho Mtakatifu ataingia ndani yako, atakayekupa uwezo wa kuwa kama yeye alivyo yaani Mtakatifu. Vilevile atakushushia na karama zake za Roho kwa jinsi apendavyo yeye juu yako. Hapo ndipo utakapopokea uwezo wa kuwa shahidi wake

Kumbuka biblia inasema wote wasio na Roho Mtakatifu hao sio wake (Soma Warumi 8:9), Hivyo ni wajibu wetu sote kumtafuta Roho Mtakatifu kwa bidii sana. Kwasababu hutaweza kumjua Mungu, wala kupokea uwezo wa kuishinda dhambi kama huna Roho Mtakatifu ndani yako.

Bwana akubariki.

Maran Atha !jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

KWANINI YESU KRISTO ALIKUJA DUNIANI?

JE UNATAMANI KUMJUA MUNGU, NA HUJUI PA KUANZIA?

KWANINI YESU KRISTO NI MWANA WA DAUDI?

ROHO HUTUOMBEA KWA KUUGUA KUSIKOWEZA KUTAMKWA!

KAMA MUNGU ANABORESHA KAZI ZAKE, KWANINI WEWE USIBORESHE ZA KWAKO?.

Rudi Nyumbani:

Print this post

KWA KUWA NGUVU ZA MBINGUNI ZITATIKISIKA.

Kwanini nguvu za mbinguni zitikisike?.

Bwana Yesu alitabiri na kusema kipindi kifupi karibu na mwisho wa dunia kutaanza kuonekana baadhi ya ishara za kutisha kutoka mbinguni, na mambo ya ajabu sana, Na hiyo itawafanya watu wengi waingie katika hofu sana, wakijiuliza nini maana ya mambo haya na nini kitatokea baada ya hayo..

Luka 21:25 “ Tena, kutakuwa na ishara katika jua, na mwezi, na nyota; na katika nchi dhiki ya mataifa wakishangaa kwa uvumi wa bahari na msukosuko wake;

26 watu wakivunjika mioyo kwa hofu, na kwa kutazamia mambo yatakayoupata ulimwengu. Kwa kuwa nguvu za mbinguni zitatikisika”.

Kama tunakumbuka  Octoba 1 mwaka 2016, kulitokea Ishara ya ajabu pale Yerusalemu Israeli, sauti kama za baragumu nyingi zilisikika zikipigwa angani (tarumbeta zikilia Israeli angani)kwa umbali mrefu sana.. Na pale ambapo sauti zilipokuwa zinatokea kulionekana mduara mkubwa sana wa wingu lililozunguka kama pete..Jambo ambalo liliwashtua wakazi wengi wa mji wa Yerusalemu sio tu Israeli peke yake, bali hata dunia nzima. Kama hujalifahamu hilo bofya link hii utazame baadhi ya video zilizo rekodi tukio hilo(youtube).

https://www.youtube.com/watch?v=AwCc45T38SU

Haikuishia hapo lakini Inaripotiwa miaka ya hivi karibuni mambo kama hayo ya ajabu yamekuwa yakitokea angani, karibu dunia nzima, mambo ambayo hayajawahi kusikika wala kuonekana siku za huko nyuma,..hata wanayansi wanakosa majibu ya maswali hayo, wengine wanadai dunia inatembelewa na viumbe kutoka sayari nyingine (Aliens), wengine wanasema hivi, wengine vile, lakini biblia imeweka wazi kabisa katika siku za mwisho nguvu za mbinguni zitatikisika, na ishara kama hizo zitaendelea kuwa nyingi, na hiyo yote tunapaswa tujiulize ni kwanini hayo yote yanatokea?..Ni kwasababu Mungu anatukumbusha kuwa ule mwisho upo karibu na hivyo tujiweke tayari kwasababu saa ya ukombozi wetu imekaribia..

Amosi 3: 6 ”Je! Tarumbeta itapigwa mjini, watu wasiogope?…”

Kusikika kwa matarumbeta kama hayo, ni kutuonyesha kuwa Upo wakati parapanda halisi ya mwisho italia na wafu waliokufa katika Kristo watafufuliwa na kupewa ile miili ya utukufu pamoja na watakatifu waliokuwa hai kisha wote kwa pamoja watanyakuliwa na kwenda kumlaki Bwana Yesu mawinguni, kisha wataenda katika karamu ya mwana kondoo waliyoandaliwa mbinguni,

Lakini kumbuka kwa wakati huo ambao tutakuwa mbinguni, huku chini dhiki kuu itakuwa inaendelea,. Kumbuka hizi ni saa za majeruhi, Injili ya Kristo iliyotabiriwa ya siku hizi za mwisho sio ile ya kuwavuta tena waje kwa Kristo hapana bali ni injili ya kuhimiza, kumtia moyo yule ambaye tayari ni mtakatifu ili azidi kuwa mtakatifu na kumuhimiza yule ambaye ni mwovu na azidi kuwa mwovu (Soma Ufunuo 22:11), …

Kwasababu wakati wa mavuno umekaribia na magugu na ngano tayari yameshajitenga..Hivyo hakuna tena muda wa kuanza kutafuta magugu ni yapi na ngano ni zipi katika shamba la Mungu…

Hivyo ndugu kama bado unasuasua ni heri ukayajenga Maisha yako sasa upya, mkaribishe Kristo katika Maisha yako, ulimwengu huu usioisha masumbufu na mahangaiko, ukiendelea nao, utajikuta unaendelea hivyo hivyo mpaka unakufa au unyakuo unakukuta kwa ghafla..Hivyo kama upo tayari leo, hapo ulipo tafuta nafasi yako mwenyewe, upige magoti, umweleze Mungu dhambi zako zote, kisha mwombe akusamehe, unafanya hivyo huku ukiwa umemaanisha na umekusudia kuacha dhambi zako kabisa kwamba kuanzia leo unataka kuishi Maisha yale Kristo anayotaka..

Na kama utakuwa umefanya hivyo kwa Imani basi fahamu kuwa Umeshasamehewa,..Amani ya Bwana itaingia ndani ya moyo wako, (Huo ndio uthibitisho wa Msamaha wako), sasa unachopaswa kufanya baada ya hapo ni kwenda kubatizwa kama hujabatizwa, Hivyo tafuta kanisa linaloamini katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi na uwe kwa jina la YESU KRISTO ubatizwe sawasawa na Matendo 2:38,..Ili kuukamilisha wokovu wako, Na Bwana mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake Mtakatifu. Kwasababu hiyo ni ahadi aliyoiahidi kwa wale wote wanatakao mpokea. Roho Mtakatifu atakusaidia kushinda dhambi na kukupa uelewa wa maandiko kwa namna isiyokuwa ya kawaida.

Bwana akubariki sana.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Maran Atha.

Mada Nyinginezo:

Rudi Nyumbani:

Print this post

Uasherati wa Kiroho maana yake nini?

Uasherati wa Kiroho maana yake nini?

JIBU: Mtu yeyote aliyejiingiza katika mahusiano na Yesu Kristo, mtu huyo katika roho anajulikana kama ni Mpenzi wa Yesu Kristo, Na mtu anajiingiza katika mahusiano hayo kwanza kwa kumwamini YESU KRISTO, kwamba alikuja kufa kwaajili ya dhambi zake, na kwamba yeye ndiye mwokozi wa ulimwengu, Na kumwamini huko kunatokana na kuisikia Injili ya Kweli inayohubiriwa na watumishi wake (Soma 2Wakorintho 11:2)..na baada ya kumwamini anatubu kwa kumaanisha kuziacha dhambi zake na kwenda kubatizwa kwa maji na kwa Roho Mtakatifu, sasa mtu aliyepitia hatua hizo zote katika ulimwengu wa roho anajulikana kama mpenzi wa YESU KRISTO au kwa jina lingine anaitwa Bibi arusi wa Kristo.

Yeremia 3:14 “Rudini, enyi watoto wenye kuasi, asema Bwana; MAANA MIMI NI MUME WENU; nami nitatwaa mtu mmoja wa mji mmoja, na wawili wa jamaa moja, nami nitawaleta hata Sayuni;”

Sasa ikitokea Mtu wa namna hii akiacha mahusiano yake haya na Kristo na kurudia tena kuishi maisha ya dhambi, na kumdharau Roho Mtakatifu, akaenda kuzini, au kuabudu sanamu, akaenda kwa waganga wa kienyeji…kibiblia mtu kama huyo ni anafanya uasherati wa kiroho, ambao ndio unaomtia Mungu wivu, ambao unaweza kupelekea hata kifo cha ghafla kwa huyo Mtu.

Waebrania 10:28 “Mtu aliyeidharau sheria ya Musa hufa pasipo huruma, kwa neno la mashahidi wawili au watatu.

29 Mwaonaje? Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, na kumfanyia jeuri Roho wa neema?

30 Maana twamjua yeye aliyesema, Kupatiliza kisasi ni juu yangu, mimi nitalipa. Na tena, Bwana atawahukumu watu wake.

31 Ni jambo la kutisha kuanguka katika mikono ya Mungu aliye hai.”

Unaweza kupitia binafsi mistari hii inaeleza zaidi juu ya uasherati huu wa kiroho (Soma 1Nyakati 5:25-26, Zaburi 106:39, Yeremia 13:27, Ezekieli 6:9, Walawi 17:7, Ezekieli 16:27,)

Waamuzi 2:16 “Kisha Bwana akawainua waamuzi, waliowaokoa na mikono ya watu hao waliowateka nyara.

17 Lakini hawakuwasikiliza hao waamuzi wao, maana walifanya uasherati kwa kuifuata miungu mingine, wakajiinamisha mbele yao; wakageuka upesi, na kuiacha njia ile waliyoiendea baba zao, waliozitii amri za Bwana bali wao hawakufanya hivyo”.

Hivyo uasherati wa kiroho sio ndoto za kufanya mapenzi usiku na mtu au viumbe visivyojulikana, kama zinavyotafsiriwa na wengi leo, bali ni kufanya kitendo chochote kilicho kinyume na Imani yako ya kikristo, ambacho ni machukizo mbele za Mungu, na Mungu alisema yeye ni Mungu mwenye wivu,(Soma Nahumu 1:2 na Kutoka 20:4).

Wivu huo ni wivu anauona pale mtu anapokwenda kufanya vitu kinyume na ile Imani aliyokuwa nayo.

Bwana atusaidie sana.

Ubarikiwe.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

UFUNUO: Mlango wa 13

UFUNUO: Mlango wa 17

UFUNUO: Mlango wa 18

TIMAZI NI NINI

Rudi Nyumbani:

Print this post

Biblia inamaana gani kusema;aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi?

SWALI: Kwanini biblia sehemu moja inasema mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, na sehemu nyingine inasema tukisema hatuna dhambi tunajidanganya wenyewe?. Je! Ni lipi hapo lipo sahihi kati ya hayo mawili?.


JIBU: Tukisoma 1Yohana 3:9 inasema..

“Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu”.

Tukisoma pia 1Yohana 1:8-10 inasema..

“Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.

9 Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.

10 Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu”.

Hivyo ukisoma kwa juu juu mistari hiyo utaona kama inajichanganya yenyewe lakini ukweli ni kwamba haijichanganyi na yote miwili ipo sawa, isipokuwa tunapaswa tuelewe Mtume Yohana alikuwa anaizungumzia hiyo mistari katika Nyanja ipi?, kwamfano kama ukiutazama vizuri huo mstari wa pili unaosema,“Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.,” Utagundua kuwa Mtume Yohana alikuwa analenga katika eneo la mtu kujiona kuwa mkamilifu asilimia mia kama Mungu mwenyewe, suala ambalo halipo, hakuna mwanadamu ambaye ni mkamilifu kwa asilimia zote, anayesema hana chembe ya dhambi hata kidogo ndani yake, vinginevyo basi neema itakuwa ni bure…..yapo makosa madogo madogo ambayo mtu anayatenda pasipo hata yeye kujua kama ameyafanya sasa haya ndio yanayotufanya tusijigambe kuwa hatuna dhambi hata kidogo.

Na tukiwa na ufahamu huo kichwani mwetu basi, tutajinyenyekeza mbele zake, na kuungama makosa yetu kila siku kwa yale ambayo tunamkosea Mungu pasipo kujua na kwa yale tunayoyajua.

Lakini sasa tukirudi katika ule mstari wa kwanza unaosema.. “Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu”.

Ni kwamba hakuna mtu yeyote anayesema amezaliwa mara ya pili kwa akili zake na kwa ufahamu wake akaenda kutenda dhambi…Hicho kitu hakiwezekani kabisa, kutokuwa wakamilifu asilimia 100 kama Mungu hakumaanishi kuwa ndio tufanye dhambi kwa makusudi, wanaoweza kufanya hivyo ni watu ambao hawajazaliwa mara ya pili, wao ndio wanaweza kutamani na muda huo huo wakaenda kuzini au kufanya mustarbation, au kutazama pornography, wanaweza wakakasirika na muda huo huo wakaleta madhara na wakati mwingine hata kuua, wanaweza wakatamani mali ya mwingine na muda huo huo wakaiba, wanaweza kuudhiwa na muda huo huo wakaporomosha matusi, au kulipiza kisasi..

Lakini kwa mtu aliyezaliwa mara ya pili jambo hilo haliwezekaniki kabisa, ni kwasababu gani?. Ni kwasababu biblia inasema,uzao wake wakaa ndani yake, (yaani Uzao wa Mungu) na kama uzao wake wakaa ndani yake, basi mtu huyo ataonyesha tabia za yule aliyemzaa, ataonyesha tabia za YESU ndani yake..Kwamfano haiwezekani, mtoto akazaliwa na mtu halafu siku hiyo hiyo akaanza kula majani kama ng’ombe,tutajiuliza ni nini kimetokea,.. lakini tukimwona ndama aliyezaliwa leo anakula majani hatushangai kwasababu uzao wa ng’ombe upo ndani yake..Vivyo hivyo na sisi tuliozaliwa mara ya pili, hatuwezi sisi wenyewe kutenda dhambi kwa makusudi halafu tukasema tumezaliwa na Mungu, huo ni uongo…

Ukiona mtu anakwenda kuzini halafu anasema nimepitiwa huyo bado hajazaliwa mara ya pili, ukiona mtu anafanya mustarbation halafu anasema ameokoka huyo bado hajazaliwa mara ya pili, ukiona anakwenda disko bado hajazaliwa mara ya pili..ukiona mtu ni mlevi, au mvutaji sigara au mvaaji vimini, mzinzi, mtukanaji, na bado anasema amezaliwa mara ya pili fahamu kuwa huyo bado yupo ulimwenguni. Uzao wa Mungu haupo ndani yake. Hivyo anahitaji kutubu na kuzaliwa mara ya pili.

Ubarikiwe.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

DHAMBI YA MAUTI

DHAMBI ISIYO NA MSAMAHA.

IELEWE SAUTI YA MUNGU.

Katika Yakobo 1:13 Biblia inasema Mungu hamjaribu mtu, lakini tukirudi kwenye kitabu cha Mwanzo 22:1 tunaona Mungu alimjaribu Ibrahimu. Hapo naomba mwanga zaidi.

Rudi Nyumbani:

Print this post

TUMAINI NI NINI?

Tumaini ni moja ya nguzo tatu kuu katika Ukristo, Ya kwanza ikiwa ni UPENDO, Ya pili ni IMANI na ya tatu ni Tumaini. (1Wakorintho 13:13). Sasa hivi viwili vya mwisho vinatabia ya kwenda sambamba, kwani biblia inatumbia Imani ni kuwa na uhakika wa mambo YATARAJIWAYO, ni bayana ya mambo yasiyoonekana…(Waebrania 11:1)

Lakini kibiblia tumaini ni tarajio, au tazamio Fulani ambalo tayari unao uhakika nalo. Tofauti na tafsiri za kawaida kwamba tumaini ni tarajio la jambo ambalo pengine unaweza ukawa hata huna uhakika nalo, kwamfano, mtu anayeishi na virusi vya ukimwi, ipo kauli inayosema, watu wa namna hiyo huwa wanaishi kwa matumaini…Wakiwa na maana kuwa wanatumainia siku moja dawa itatokea, na kwamba isipotekea ndio basi tena…kwasababu wapo katika tarajio lisilo na uhakika.

Lakini katika ukristo ni kinyume  chake, hatusemi tunatumainia tukifa tutakwenda mbinguni, kana kwamba hatuna uhakika huo kuwa tutakwenda mbinguni au la,  hapana…Au hatusemi tunatumai Bwana Yesu atakuja hapana bali tunaamini kuwa atakuja, uhakika huo tunao kabisaa na hiyo ndio inayoitwa Imani…sasa katika kuamini huko ndipo tumaini halisi linazaliwa hapo ndipo tunaweza kusema   tunatumai moja ya hizi siku tutamwona Bwana Yesu akitokea mawinguni…Unaona hapo tunaamini kuwa ni lazima aje, isipokuwa tunatazamia atakuja hivi karibuni, na kama asipokuja leo wala kesho, basi ni sawa lakini mwisho wa siku ni lazima aje tu…

Kila mkristo ni lazima awe na kiwango kikubwa cha Tumaini ndani yake, katika safari hii ngumu na ya majaribu mengi hapa duniani ni lazima TUMAINI liumbike ndani yetu kwamba siku si nyingi Bwana wetu atatuokoa…Na ndio maana tunaimba..’’Ni salama rohoni mwangu, Bwana Himiza siku ya kuja,’’ ..tunatumai siku moja hayo yote yatakwisha, tunapopitia misiba ya ndugu zetu tunatumai siku moja tutawaona tena utukufuni uso kwa uso, na hivyo hiyo inatupa nguvu ya kuendelea mbele tusikate tamaa, tunapopitia mateso, na njaa na kuchukiwa na kutengwa, na kudharauliwa tunajua ni kwa muda tu tunatumai siku moja tutafutwa machozi na BWANA na hayo yote hatutayaona tena…Hilo ndilo tumaini hasaa linalotoka katika uhakika Fulani…ambao bado hatujaufikia maadamu tupo hapa duniani.

Bila tumaini, katika safari hii hatuwezi kufika mbali kama vile tu, bila Imani na Upendo, hakuna chochote tunachoweza kufanya.Kwasababu tumaini linavutwa na subira na uvumilivu.

Warumi 5:1  Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na mwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo,

2  ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu.

3  Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi;

4  na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini;

5  na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi.

Biblia inaendelea kusema…

Wagalatia 5:5  Maana sisi kwa Roho tunalitazamia tumaini la haki kwa njia ya imani.

Wafilipi 3:20  Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena TUNAMTAZAMIA Mwokozi, Bwana Yesu Kristo;

21  atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake.

Inasema tena…

2Petro 3:13  Lakini, kama ilivyo ahadi yake, MNATAZAMIA mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake. 14  Kwa hiyo, wapenzi, kwa kuwa mnatazamia mambo hayo, fanyeni bidii ili mwonekane katika amani kuwa hamna mawaa wala aibu mbele yake.

Hivyo kwa ufupi  tumaini ni matarajio au matazamio ya ahadi tulizoahidiwa, Lakini Imani ni uhakika wa matarajio hayo. Au tunaweza kusema uhakika wa tumaini letu.

Ubarikiwe sana. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

UPENDO NI NINI NA JE! KUNA AINA NGAPI ZA UPENDO?

PENGINE MUNGU ALISHASEMA NAWE KWA NJIA HII.

UMEPATANISHWA NA MAADUI ZAKO?

Biblia inamaanisha nini kusema Yeye aliye na sikio, na asikie?

Rudi Nyumbani:

Print this post

KUTAHIRIWA KIBIBLIA

Kutahiriwa Ni nini?

Kutahiriwa kibiblia ni kitendo cha Sehemu ya nyama ya mbele ya uume wa mwanamume kukatwa. Mtoto yeyote wa kiume anapozaliwa anakuwa na sehemu ya nyama iliyozidi katika uume wake. Sehemu hiyo ya nyama ndiyo inayoitwa GOVI na ndiyo iliyokuwa inakatwa.

Katika Biblia Mungu alimpa Ibrahimu maagizo ya kufanya Tohara yake (Yaani kuiondoa hiyo sehemu ya nyama iliyozidi katika kila mtoto wa kiume) kuanzia yeye  binafsi na wazao wake pamoja na wote waliokuwepo katika malango yake. Na Tohara hiyo Mungu aliiruhusu ifanyike  kama Ishara ya Agano Mungu aliloingia nao.

Mwanzo 17:9 “Mungu akamwambia Ibrahimu, Nawe ulishike agano langu, wewe na uzao wako kwa vizazi vyao baada
yako.

10 Hili ndilo agano langu utakalolishika, kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, Kila mwanamume wa kwenu atatahiriwa.

11 Mtatahiriwa nyama ya magovi yenu, na jambo hilo litakuwa ishara ya agano kati ya mimi na ninyi.

12 Mtoto wa siku nane atatahiriwa kwenu, kila mwanamume katika vizazi vyenu, mzaliwa nyumbani, na mnunuliwa kwa fedha, kila mgeni asiyekuwa wa uzao wako.

13 Mzaliwa nyumbani mwako, na mnunuliwa kwa fedha yako, lazima atahiriwe; na agano langu litakuwa katika mwili wenu, kuwa agano la milele.

14 Na mwanamume mwenye govi asiyetahiriwa nyama ya govi lake, mtu yule atatengwa na watu wake; amelivunja agano langu”

Hivyo Tohara ilikuwa ni Ishara ya Agano la Mungu katika miili ya wana wa Israeli.

Na ni kwanini ifanyike katika kiungo cha Uzazi? 

Jibu ni kwamba sehemu ya uzazi, ni sehemu ya siri na ya muhimu sana kwa mtu.Ni sehemu ambayo inafunikwa kwa mavazi mengi. Jambo hilo linafunua kitu fulani katika Tohara ya pili ambayo tutakwenda kuiona hapo mbele.

Lakini sasa tukirudi katika Agano jipya la Yesu Kristo. Tohara ya mwilini sio tena ISHARA YA AGANO Mungu aliloingia nasi. Ipo tohara nyingine ya Rohoni ambayo ndiyo ya Muhimu kuliko zote. Ambayo ndio ISHARA Pekee ya Agano la Mungu. Na hiyo si nyingine zaidi ya TOHARA YA MOYONI.

Warumi 2:29 “bali yeye ni Myahudi aliye Myahudi kwa ndani, na tohara ni ya moyo, katika roho, si katika andiko; ambaye sifa yake haitoki kwa wanadamu bali kwa Mungu”. 

Tunapoisikia Injili na kuitii, Roho Mtakatifu anaondoa kile kipande cha nyama kilichozidi katika mioyo yetu. Kiburi kilichozidi ni govi, Uongo ambao haukupaswa uwepo ndani yako ni govi, hivyo Roho Mtakatifu anaukata. Kadhalika uasherati, ulevi, wizi na mambo mengine yote mabaya. Yanaondolewa na Roho Mtakatifu mwenyewe.

Wakolosai 2:10 “Na ninyi mmetimilika katika yeye aliye kichwa cha enzi yote na mamlaka.

11 Katika yeye mmetahiriwa kwa tohara isiyofanyika kwa mikono, kwa kuuvua mwili wa nyama, kwa tohara ya Kristo”

Tunasoma pia katika..

Matendo 7:7.51 Enyi wenye shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, siku zote mnampinga Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo.

Hivyo kutahiriwa kibiblia ni kuondolewa sehemu isiyostahili kuwepo katika moyo wa mtu. Na kama vile jinsi ilivyofanyika kwenye viungo vya uzazi vilivyojificha. Kadhalika inafanyika pia katika MOYO ambao ndio umeficha mambo yote ya siri za mtu.

Je! Umetahiriwa moyoni mwako?..ulevi umeondolewa? rushwa imeondolewa?.. uasherati umeondolewa?. Kumbuka Tohara ya kwanza ilikuwa inawahusu wanaume tu..Lakini hii ya pili inahusu jinsia zote!.

Kama wewe bado unatoa mimba bado hujatahiriwa. Kama wewe mwanamke unasengenya na kuishi na mwanamume ambaye hamjafunga ndoa hapo bado unahitaji tohara ya moyoni.

Hivyo kama hujampa Yesu Kristo maisha yako. Ni wazi kuwa bado hujapokea Tohara hii ya moyoni yenye umuhimu mkubwa sana. Maana hiyo ndio ishara ya Agano la Mungu kwako. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

JE! KUNA UMUHIMU WOWOTE WA KULIPA ZAKA?

Je! msalaba kaburini una umuhimu wowote?

SIKU ILE NA SAA ILE.

ROHO HUTUOMBEA KWA KUUGUA KUSIKOWEZA KUTAMKWA!

JE BIKIRA MARIAMU ALIZAA WATOTO WENGINE?

Rudi Nyumbani:

Print this post