Je! Ule Unabii wa mifupa mikavu una maana gani kwetu?
Ezekieli alionyeshwa maono,ambayo yalimshangaza sana, maono yenyewe yalihusu mifupa ya watu ambao walionekana kama walishakufa kipindi kirefu sana nyuma, na inavyoelekea yalikuwa ni mauaji ya halaiki, (watu wengi waliouawa kwa wakati mmoja).Kwasababu mifupa hiyo ilikuwa mingi sana katika bonde kavu.
Hivyo alipopitishwa kwenye bonde hilo, alisikia sauti ya Mungu ikimuuliza Ezekieli Je! Mifupa hii inaweza kuwa hai tena?, Ezekieli akajibu wewe Bwana wajua, yaani wewe ndiye unayejua kama yaweza kuwa hai tena au la.
Lakini kama tunavyosoma Habari muda huo huo aliambiwa aitabirie uhai, na alipofanya vile alishuhudia uumbaji wa Mungu kwa mara nyingine tena. Jinsi mifupa ilivyopata mishipa, mara nyama, mara uhai na kutembea na kuongea tena..
Tusome.
EZEKIELI: MLANGO 37
1 Mkono wa Bwana ulikuwa juu yangu, naye akanichukua nje katika roho ya Bwana, akaniweka chini, katikati ya bonde; nalo limejaa mifupa;
2 akanipitisha karibu nayo pande zote; na tazama, palikuwa na mifupa mingi katika ule uwanda! Nayo, tazama, ilikuwa mikavu sana.
3 Akaniambia, Mwanadamu, je! Mifupa hii yaweza kuishi? Nami nikajibu, Ee Bwana MUNGU, wajua wewe.
4 Akaniambia tena, Toa unabii juu ya mifupa hii, uiambie, Enyi mifupa mikavu, lisikieni neno la Bwana.
5 Bwana MUNGU aiambia mifupa hii maneno haya; Tazama, nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi.
6 Nami nitatia mishipa juu yenu, nami nitaleta nyama iwe juu yenu, na kuwafunika ngozi, na kutia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.
7 Basi nikatoa unabii kama nilivyoamriwa; hata nilipokuwa nikitoa unabii, palikuwa na mshindo mkuu; na tazama, tetemeko la nchi, na ile mifupa ikasogeleana, mfupa kwa mfupa mwenziwe.
8 Nikatazama, kumbe! Kulikuwa na mishipa juu yake, nyama ikatokea juu yake, ngozi ikaifunika juu yake; lakini haikuwamo pumzi ndani yake.
9 Ndipo akaniambia, Tabiri, utabirie upepo, mwanadamu, ukauambie upepo, Bwana MUNGU asema hivi; Njoo, kutoka pande za pepo nne, Ee pumzi, ukawapuzie hawa waliouawa, wapate kuishi.
10 Basi nikatabiri kama alivyoniamuru; pumzi ikawaingia, wakaishi, wakasimama kwa miguu yao, jeshi kubwa mno.
11 Kisha akaniambia, Mwanadamu, mifupa hii ni nyumba yote ya Israeli; tazama, wao husema, Mifupa yetu imekauka, matumaini yetu yametupotea; tumekatiliwa mbali kabisa.
12 Basi tabiri, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitafunua makaburi yenu, na kuwapandisha kutoka katika makaburi yenu, enyi watu wangu, nami nitawaingizeni katika nchi ya Israeli.
13 Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapoyafunua makaburi yenu, na kuwatoa ninyi katika makaburi yenu, enyi watu wangu.
14 Nami nitatia roho yangu ndani yenu, nanyi mtaishi, nami nitawawekeni katika nchi yenu, nanyi mtajua ya kuwa mimi, Bwana, nimesema hayo, na kuyatimiza, asema Bwana.
Hii ni mistari ya Faraja, kwasababu inaeleza ukuu wa Mungu, kwenye matumaini ambayo yalishakwisha potea. wana wa Israeli walipopelekewa unabii huu walipata nguvu mpya,kwasababu wakiwa Babeli walikuwa wameshapoteza matumaini ya kurudi katika taifa lao tena, kuishi na kumwabudu Mungu. Lakini Mungu akawaambia japokuwa mmekuwa kama mifupa mikavu iliyokauka, mimi nitawafufua tena na kuwarudisha katika nchi yenu, na kupanda na kujenga na kunitumikia tena.
Na kweli jambo hilo lilikuja kutokea vilevile, Bwana aliwarejesha tena katika taifa lao.
Hata sasa, unaweza ukawa umekufa, kwa namna nyingi, mpaka umekata tamaa ya kuishi au ya kuendelea mbele katika Imani, pengine afya yako imepoteza matumaini kabisa, labda unaugonjwa wa kiharusi huwezi kutembea umelala tu kitandani miaka mingi au una kansa hatua ya nne, umeambiwa na daktari una wiki chache tu za kuishi, au umeishi na virusi vya ukimwi kwa muda mrefu sasa, na kinga yako imeshuka sana, siku yoyote umeambiwa unaondoka, usiogope, Bwana anaweza kukurejesha ukawa mzima tena, kama zamani.
Ibrahimu alikuwa na matumaini hayo, na ndio maana hakuona shida kumtoa mwanaye kafara kwa ajili ya Bwana, mpaka Mungu akamuita baba wa Imani,
Waebrania 11:17 “Kwa imani Ibrahimu alipojaribiwa, akamtoa Isaka awe dhabihu; na yeye aliyezipokea hizo ahadi alikuwa akimtoa mwanawe, mzaliwa pekee;
18 naam, yeye aliyeambiwa, Katika Isaka uzao wako utaitwa,
19 akihesabu ya kuwa Mungu aweza kumfufua hata kutoka kuzimu; akampata tena toka huko kwa mfano”.
hivyo na wewe kuwa na Imani na Mungu wako, hakuna linalomshinda yeye.
Mwingine, unaweza ukawa hata chakula ni shida, hujui kesho utaamkaje, familia inakutegemea, kazi huna, umekuwa mifupa mikavu kwelikweli, kumbuka uwezo wa Mungu ni mkubwa sana. Anaweza kukufufua kutoka huko tena, na kukutajirisha.
Unachopaswa kufanya ni kutulia katika mapenzi yake. Yaani, kama hujaokoka basi OKOKA leo, na kama umeshaokoka, basi zidi kumwamini yeye, na hakika atakutengenezea njia pasipo na njia.
Ikiwa wewe ni mmojawapo wa mifupa hii mikavu, ningependa tusali Pamoja sala hii;
Basi magoti mahali ulipo kisha nyanyua mkono wako mmoja juu kisha sema sala hii kwa Imani na Bwana atakusaidi.
Baba yangu, Nimejua hakika wewe ni Mungu, wala hapana mwingine mwenye ishara kuu na za ajabu kama wewe. Nimesoma maneno yako, nami nimeamini, kuwa wewe MUNGU unaweza kurejesha uhai tena kwa watu waliokwisha kufa na kuoza na kubakia mifupa tu. Naomba Bwana wangu, unisamehe makosa yangu yote, niliyokukosea kwa kujua na kutokujua. Naomba Damu ya mwanao Yesu Kristo initakase kuanzia sasa, nami nakiri kuwa nitatembea katika maisha ya utakatifu, sikuzote za Maisha yangu.
Naomba unisaidie tatizo langu hili (Taja tatizo lako, kama ni ugonjwa, shida, n.k. mwambie ), Unifufue upya, nisimame, nikutukuze, nikutumikie, nikuabudu Mungu wangu. Asante kwa kunisamehe, Asante kwa kunisaidia, asante kwa kuniweka huru.
Amen.
Irudie sala hiyo kwa mara nyingine tena, hadi usikie amani ndani ya moyo yako.
Na amini kuwa Bwana ameshaanza kutenda jambo katika Maisha yako,.
Ubarikiwe sana.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali./Ubatizo
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?
Bwana Yesu asifiwe, nakukaribisha katika Makala zinazoeleza juu ya thawabu mbalimbali za Mungu, na vigezo ambavyo Mungu atavitumia kuzitoa thawabu hizo. Tumeshatazama vigezo vya thawabu kadha wa kadha huko nyuma, na sasa, tutaendelea na sehemu yetu ya tano (5)
5) Zipo thawabu za kumiliki miji mingi Zaidi katika ule ufalme wa Mungu.
Mungu ameahidi,kuwapa utawala mkubwa, wale watu ambao watatumika kwa uaminifu wakiwa hapa duniani.
Tuupitie mfano huu tutaelewa zaidi;
Luka 19:12 “Basi akasema, Mtu mmoja, kabaila, alisafiri kwenda nchi ya mbali, ili ajipatie ufalme na kurudi.
13 Akaita watu kumi katika watumwa wake, akawapa mafungu kumi ya fedha, akawaambia, Fanyeni biashara hata nitakapokuja.
14 Lakini watu wa mji wake walimchukia, wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatumtaki huyu atutawale.
15 Ikawa aliporudi, ameupata ufalme wake, aliamuru waitwe wale watumwa aliowapa fedha, ili ajue faida aliyopata kila mtu kwa biashara yake.
16 Akaja wa kwanza, akasema, Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi zaidi.
17 Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi.
18 Akaja wa pili, akasema, Bwana, fungu lako limeleta mafungu matano faida.
19 Akamwambia huyu naye, Wewe uwe juu ya miji mitano.
20 Akaja mwingine akasema, Bwana, hili ndilo fungu lako, ambalo nililiweka akiba katika leso.
21 Kwa maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; waondoa usichoweka, wavuna usichopanda.
22 Akamwambia, Nitakuhukumu kwa kinywa chako, mtumwa mwovu wewe. Ulinijua kuwa ni mtu mgumu, niondoaye nisichoweka, na kuvuna nisichopanda;
23 basi, mbona hukuiweka fedha yangu kwa watoao riba, ili nijapo niipate pamoja na faida yake?
24 Akawaambia waliosimama karibu, Mnyang’anyeni hilo fungu, mkampe yule mwenye mafungu kumi.
25 Wakamwambia, Bwana, anayo mafungu kumi.
26 Nawaambia, Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang’anywa hata alicho nacho”.
Mfano huo unajieleza wenyewe.. Ikiwa Bwana amekupa kiwango Fulani cha neema umtumikie hapa duniani, anatarajia kuona umekizalisha kwa wingi kwa jinsi uwezavyo. Mfano amekupa neema ya kufagia uwanja wa kanisa, anatarajia, kuona na vyoo pia, ni visafi, na madirisha na viti vinakaa katika hali ya usafi siku zote.
Kwasababu siku atakayokuja, atatazama, kama kile alichokupa mwanzo, na utawajibikaji wako je! vinaendana, lakini ikiwa utaona kazi ya kufagia kanisa, haina maana yoyote, ukaendelea na shughuli zako, atakuja kukuambia kama uliona uvivu kufagia basi si ungemwajiri mtu akusaidie kuifanya hiyo kazi umlipe, kuliko kuuacha uwanja wangu ukiwa na vichaka na matakataka namna ile? Unaona Kama tu alivyomwambia yule aliyepewa fungu moja, si ungeweka kwa watoa riba, ili nijapo nikute na faida yangu?. Ndivyo atakavyotuambia na sisi!
Lakini kama tutakuwa waaminifu wa kile alichotupa, tukazalisha na Zaidi ya pale, tujue kuwa, uaminifu wetu, utaamua umiliki wetu katika ufalme ule…Kama ni miji basi tutamiliki hiyo miji kulingana na uaminifu wetu sasa.
Hivyo hiyo inatupa hamasa, tuitende kazi ya Bwana bila kutoa visingizio, bila kudharau, tena tutende Zaidi ya pale kwa kadiri tuwezavyo, kwasababu hivyo hivyo vidogo ndivyo vitakavyopima utajiri wetu.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312 Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > WHATSAPP-Group
Mada Nyinginezo:
Jibu: Hii ni moja ya hoja ambayo ni muhimu sana mkristo yeyote kuijua.
Ukweli ni kwamba shetani hawezi kuingia kwenye ufahamu wa mtu na kujua anachokifikiri au kukiwaza au kukipanga.
Huo uwezo hana, na hajawahi kuwa nao. Na sio yeye peke yake bali hata malaika hawana huo uwezo, wala wanadamu hawana huo uwezo.
Ni Mungu peke yake na mtu mwenyewe ndio wenye Nywila (password) ya kuingia ndani ya mawazo yako.
Maana yake ni kwamba kile unachokiwaza sasahivi ni wewe peke yako ndiye unayekijua na Mungu, shetani hakijui, wala malaika wala mwanadamu mwenzako.
Labda wewe ndio uamue kuwafunulia yaliyopo ndani yako.
Sasa swali hili; kama ni hivyo inakuwaje shetani anaonekana kama anajua mambo yetu hata yale ya siri?.
Jibu ni kwamba, anajua mambo yetu kwa kuzisoma fahamu zetu.
Hata wewe unaweza kumsoma mtu na kujua anachowaza kwa wakati huo, kama una utashi wa kutosha, lakini hiyo haijamaanisha kwamba umeingia katika ubongo wake na kuyaona mawazo yake kama Tv. Hapana!
Vivyo hivyo na shetani, ana uwezo mkubwa wa kumsoma mwanadamu na hata kujua anachowaza.. kwasababu amekabiliana na mwanadamu kwa miaka mingi, tangu Edeni anazijua tabia za wanadamu, hivyo ni rahisi pia kuyasoma mawazo yao lakini si kuingia ndani ya mawazo yao.
Kama vile wewe mtu mzima unavyoweza kuyasoma mawazo ya mtoto mdogo na kujua kila kitu anachokifikiri kwa wakati huo na shetani ni hivyo hivyo.
Lakini pamoja na kwamba shetani ana uwezo wa kuyasoma mawazo ya mtu, lakini bado anapata shida sana kuyasoma na kuwaelewa mawazo ya watu waliozaliwa mara ya pili kwa Roho.
Maandiko yanasema kuwa hali ya mtu aliyezaliwa mara ya pili ni kama upepo, haujulikani unapoanzia wala unapoishia.
Yohana 3:8 “Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho”.
shetani anapata wakati mgumu sana kuyasoma mawazo ya mtu aliyezaliwa mara ya pili.
Kwasababu atadhani yale majaribu aliyomjaribu nayo jana, yatamfanya leo asiendelee na wokovu, kinyume chake anashangaa ndio kwanza anasonga mbele.
Au anategemea vile vitisho alivyomtisha navyo jana usiku, vitamfanya leo sidhubutuu kuendelea kuhubiri, au kuendelea na shughuli zake za kawaida, kinyume chake anaona yule mtu anaendelea kuhubiri kwa raha au anaendelea na shughuli zake.
Anategemea ule uchumi alioutikisa jana, utamfanya huyu mtu leo awe katika dimbwi kubwa la mawazo na hata kukufuru kinyume chake anamwona hata hawazi.
Kila anachojaribu kukifanya ili kumtikisa mtu aliyezaliwa mara ya pili, anakutana na matokeo tofauti na anayoyategemea.
Mtu aliyezaliwa mara ya pili anakuwa hatabiriki katika upeo wa shetani na mapepo yake. Tofauti na mtu ambaye hajazaliwa mara ya pili ambapo akitishiwa na wachawi kidogo tu ndani ya nyumba yake, tayari kashatishika kiasi kwamba shetani na mapepo yake wanajua kesho huyo mtu hatalala tena kwenye hiyo nyumba..Na kweli kesho yake halali tena huko ndani.
Mtu na namna hiyo shetani anakuwa anaweza kumsoma kirahisi na vile vile anakuwa anampangia maisha.
Swali ni je! Mimi na wewe tumezaliwa mara ya pili kwa Roho?. Kama bado basi tufahamu kuwa maneno haya yafuatayo yanatuhusu.
Yohana 3:3 “Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu”.
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
JINSI MUNGU ATAKAVYOTOA THAWABU ZAKE, NA VIGEZO ATAKAVYOTUMIA. (Sehemu ya 4)
Nakusalimu katika jina kuu sana la Bwana wetu Yesu Kristo, karibu katika kujifunza Neno la Bwana. Bado tupo katika mwendelezo wa thawabu mbalimbali za Mungu, na vigezo anavyovitumia kuzitoa. Hii sehemu ya 4.
4) Zipo thawabu kwa wanaowasadia maskini na wasiojiweza.
Bwana Yesu alimwambia yule Farisayo Tajiri aliyemwalika katika karamu yake maneno haya;
Luka 14:12 “Akamwambia na yule aliyemwalika, Ufanyapo chakula cha mchana au cha jioni, usiwaite rafiki zako, wala ndugu zako, wala jamaa zako, wala jirani zako wenye mali; wao wasije wakakualika wewe ukapata malipo.
13 Bali ufanyapo karamu waite maskini, vilema, viwete, vipofu,
14 nawe utakuwa heri, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa wenye haki.
15 Basi aliposikia hayo mmojawapo wa wale walioketi chakulani pamoja naye alimwambia, Heri yule atakayekula mkate katika ufalme wa Mungu”.
Ikiwa wewe ni mtakatifu Umeokoka, usisahau, kuwakumbuka watu wenye mahitaji, na wasiojiweza kwa kile Mungu alichokujalia, kwasababu kina thawabu yake kubwa mbinguni siku ile Bwana atakapowafufua wateule wake ili kuwapa thawabu.
Unapotoa msaada, au unapofanya sherehe, usiwaalike tu, watu wenye uwezo, bali tafuta na wengine wasio na kitu cha kukurudishia, tusiwaalike watu tu waliotuchangia, bali tuwaalike pia, na wasioweza kuchangia, kwasababu, tutakuwa tumejiwekea hazina nzuri mbinguni.. Mtume Paulo alikuwa na bidii kulifanya hilo, pale alipousiwa na mitume waliomtangalia. Alisema..
Wagalatia 2:9 “tena walipokwisha kuijua ile neema niliyopewa; Yakobo, na Kefa, na Yohana, wenye sifa kuwa ni nguzo, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kuume wa shirika; ili sisi tuende kwa Mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara;
10 ila neno moja tu walitutakia, tuwakumbuke maskini; nami neno lilo hilo nalikuwa na bidii kulifanya”.
Unaona? Hivyo na sisi tuwaonapo maskini, na mayatima, na wenye mahitaji, basi tujue hapo ni mahali petu pa kujichumia thawabu zetu nyingi, tufanye bidi kuwasaidia. Kwasababu tukifika mbinguni, utajiri wetu, utapimwa kwa matendo kama haya, lakini kama kila tulichokuwa tunakipata, tunakula wenyewe, au na watu wenye uwezo kama sisi, tujue kuwa tunapunguza kiwango cha utajiri wetu mbinguni. Kutoa si mpaka tuwe na vingi, ukipata sh.100, inatosha, kuwaga 50, kwa maskini na nyingine ukatumia wewe.
Bwana atusaidie tulione hilo, tuanze sasa kuwakumbuka na watu wengine wenye uhitaji.
Bwana akubariki.
Usikose mwendelezo..
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp
Mada Nyinginezo:
Kristo atukuzwe! Kama dhambi ilikuja kupitia mtu mmoja (Adamu), na kila aliyezaliwa ameirithi, kwanini Neema iliyoletwa na Bwana Yesu hatujairithi, yaani wote wanaozaliwa wasiwe na dhambi?
Jibu: Ni kweli maandiko yanasema katika Warumi 5:12-21, Kwamba kwa kupitia mtu mmoja Adamu dhambi iliingia, na hivyo na sisi uzao wake wote tukaingia katika hali ya kukosa (yaani tukazaliwa huku tumerithi dhambi)..
Lakini swali ni je kwanini haipo hivyo kwa Bwana, kama yeye anafananishwa na Adamu wa pili, kwanini na sisi tusizaliwe hali tumeirithi hiyo neema bila kupitia hatua nyingine hizo za wokovu?.
Jibu ni kwamba, hatujairithi Neema kwa namna ya kimwili kwasababu Bwana Yesu hajatuzaa katika mwili kama Adamu alivyotuzaa sisi katika mwili.
Endapo Bwana angetuzaa upya watu wote katika mwili, kama vile Adamu alivyotuzaa kupitia Hawa, basi na sisi tungeirithi hiyo neema kwa njia ya mwili na kungekuwa hakuna haja ya kupitia hizo hatua za wokovu.
Lakini kwasababu Bwana hakuwa na mke, na wala hajazaa kwa namna ya mwili, kwasababu kama angekuja kwa njia hiyo ya kuzaa katika mwili basi wangezaliwa wanadamu wengine ambao ni uzao wa Bwana ulio mkamilifu kama Bwana, na hivyo sisi wengine ambao ni uzao wa Adamu ambao tumekwishazaliwa tayari tungekuwa bado tupo kwenye dhambi..na hapo kungekuwa hakuna wokovu.
Lakini ashukuriwe Mungu, Kristo hakuja kuleta uzao mwingine duniani bali kuukomboa ule ambao tayari upo, (yaani sisi tulio uzao wa Adamu).
Hivyo ni lazima Bwana aje na mpango mwingine wa kutuzaa katika roho na si katika mwili, ili tuwe uzao wake katika roho, na tuzirithi ahadi zake hizo katika roho..Ndio maana Bwana Yesu alisema hatuna budi kuzaliwa mara ya pili katika Roho.
Yohana 3:3 “Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.
4 Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa?
5 Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu.
6 Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.
7 Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili”.
Umeona hapo?
Na tunazaliwa mara ya pili kwa maji na kwa Roho, yaani kwa Ubatizo wa maji na Kwa Ubatizo wa Roho Mtakatifu.
Maana yake ni kwamba mtu aliyebatizwa ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu (Matendo 2:38, Yohana 3:23), na akapokea Roho Mtakatifu anakuwa tayari amezaliwa mara ya pili, na hivyo ni mzao wa Bwana Yesu katika Roho. (Na tayari kapata ukombozi wa roho yake).
Ukombozi wa miili yetu utakuja siku ile ya unyakuo itakapofika (Waefeso 4:30), wakati parapanda itakapolia tutakapovikwa miili mipya ya utukufu isiyo na kasoro.
Swali ni je!. Mimi na wewe tumezaliwa mara ya pili kwa maji na kwa Roho, kumbuka Bwana anasema mtu asiyezaliwa mara ya pili hawezi kuurithi uzima wa milele.
Maran atha!.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Karama ya pili inayozungumziwa katika 2Wakorintho 1:15 ndio ipi?
JE! USIPOTIMIZA NADHIRI ZAKO ZOTE KWA BWANA. HAWEZI KUKUSAMEHE?
Shalom, huu ni mfululizo, wa Makala ambazo zinaeleza vigezo ambavyo Mungu, atavitumia kuwapa watu wake thawabu mbalimbali, au atakavyovitumia kuwakaribisha katika ufalme wake, hii ni sehemu ya tatu, ikiwa hukupitia sehemu zilizotangulia utatumia ujumbe inbox tukutumie chambuzi zake.
3) Biblia inatuonyesha kuna watu watu wataingizwa katika ufalme wa Mungu, bila kutambua sababu.
Inashangaza lipo kundi la watu ambalo litapewa neema ya kuungia ufalme wa Bwana wetu Yesu Kristo, bila lenyewe kutambua sababu mpaka litakapofunuliwa na Kristo mwenyewe siku ile.
Tunalisoma kundi hilo katika vifungu hivi.
Mathayo 25:31 “Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake;
32 na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi;
33 atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto.
34 Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu;
35 kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha;
36 nalikuwa uchi, mkanivika nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia.
37 Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha?
38 Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika?
39 Ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au kifungoni, tukakujia?
40 Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.
41 Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake;
42 kwa maana nalikuwa na njaa, msinipe chakula; nalikuwa na kiu, msininyweshe;
43 nalikuwa mgeni, msinikaribishe; nalikuwa uchi, msinivike; nalikuwa mgonjwa, na kifungoni, msije kunitazama.
44 Ndipo hao pia watajibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona wewe una njaa, au una kiu, au u mgeni, au u uchi, au u mgonjwa, au u kifungoni, tusikuhudumie?
45 Naye atawajibu, akisema, Amin, nawaambia, Kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo, hamkunitendea mimi.
46 Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele”.
Kundi hili, ni lile, lilowahifadhi, watumishi wa Kristo, wakiwa hapa duniani, wasijue kuwa walikuwa wanamtendea Kristo mwenyewe, hapa hazungumzii maskini, na omba omba, au mayatima hapana, wanaowahudumia hao wanayothawabu yao, ambayo tutaiona katika Makala inayofuata, bali wanaozungumziwa hapa ni watakatifu wa Bwana, ambao kutokana na maisha yao ya utumishi, walipitia kupungukiwa, kuumwa, kukosa chakula, nguo, makazi n.k. Sasa wapo ambao waliwaona na kuwahifadhi, wasijue kuwa wanamtendea Kristo mwenyewe.
Sasa siku ile itakapofika, hawa watumishi wa Bwana watasimama na kuwataja mbele ya Kristo, na kwasababu hiyo Kristo atawapa neema ya kuuingia ufalme wake. Sawasawa na ule mfano wakili dhalimu tunaousoma katika Luka 16:1-12.
Mtume Paulo aliwaombea rehema ndugu wa mtu mmoja aliyeitwa Onesiforo, kwa jinsi walivyomtunza na kumuhudumia kwa mahitaji mbalimbali alipokuwa anahubiri.
2Timotheo 1:16 “Bwana awape rehema wale walio wa mlango wake Onesiforo; maana mara nyingi aliniburudisha, wala hakuuonea haya mnyororo wangu;
17 bali, alipokuwapo hapa Rumi, alinitafuta kwa bidii akanipata.
18 Bwana na ampe kuona rehema machoni pa Bwana siku ile. Na jinsi alivyonihudumia kwa mengi huko Efeso, wewe unajua sana”.
Vivyo hivyo, na wale ambao, wanawaona watu wanaomtafuta Mungu, ni kama mizigo kwao, wanawadhihaki, wanawatukana, wanawafukuza, hata wakiomba maji wanawaona ni wavivu. Watu ambao wanaposikia watumishi wa kweli wa Mungu ni kama kero kwa kwao, Watu kama hawa upo wakati Kristo naye atawakana.
Inatufundisha nini?, tukisema tunampenda Kristo, tunamaanisha kuwa tunawapenda na wale wampendao, kama unawachukia watakatifu, utampendaje Kristo?. Hivyo, wapo watu ambao Kristo atawakaribisha kwa namna hii,. Vilevile wapo watu ambao Kristo atawafukuza kwa namna hii. Kwasababu hawakumkaribisha Kristo kwao.
Shalom.
Usikose mwendelezo..
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
JINSI MUNGU ATAKAVYOTOA THAWABU ZAKE, NA VIGEZO ATAKAVYOTUMIA. (Sehemu ya 1)
JINSI MUNGU ATAKAVYOTOA THAWABU ZAKE, NA VIGEZO ATAKAVYOTUMIA. (Sehemu ya 2)
Tumetazama, wapo watu ambapo siku ile ya hukumu, watalipwa thawabu sawa na wale ambao wameteseke Maisha yao yote katika kumtumikia Mungu. Na kigezo chenyewe kwanini Mungu afanye hivyo, tumeshakiona katika maandiko, ikiwa hujapata uchambuzi wake, tutumie ujumbe, inbox tukutumie..
Tutaendelea, na vigezo cha pili cha thawabu, za Mungu. Hichi tunakisoma katika Mathayo 24:44-51
2) Kwamba wapo watu watawekwa juu ya kazi yote ya Mungu, mbinguni.
Unaweza kujiuliza, Je! Inamaana kuna watu ambao hawatawekwa, juu ya kazi za Mungu siku ile? Jibu ni ndio, twende moja kwa moja katika Habari hii, tuone ni kigezo gani, Kristo anakitumia, katika kutoa thawabu kama hiyo.
Mathayo 24:44 “Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja.
45 Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake?
46 Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo.
47 Amin, nawaambieni, atamweka juu ya vitu vyake vyote.
48 Lakini mtumwa yule mbaya akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia;
49 akaanza kuwapiga wajoli wake, na kula na kunywa pamoja na walevi;
50 bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani, na saa asiyojua,
51 atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wanafiki; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno”.
Katika Habari hiyo, tunaona, mtu mmoja Tajiri aliondoka bila kutoa taarifa ya lini atarudi, lakini akamwacha mtumwa wake mmoja awe mwangalizi wa watu wake, ahakikishe anawahudumia, pasipo kusimamiwa. Lakini anasema kama mtumwa huyo atadhani kuwa Bwana wake atachelewa. akaanza kuwa mzembe, mara hawapi watu chakula, mara anawapiga, mara anaamrisha vibaya. Siku asiyodhani atakuja, na kumkata vipande vipande.
Lakini akimkuta yupo katika majukumu yake, basi ameahidi, kuwa atamweka juu vitu vyake vyote.
Leo hii kama wewe ni mtumishi wa Mungu, aidha mchungaji, nabii, mwalimu, mtume, mwimbaji, au unafanya kazi yoyote ile ya kuujenga ufalme wa Mungu..Fahamu kuwa Bwana anataka kukuona, wakati wote, muda wote, ukitumika kwa uaminifu katika hiyo kazi, ili siku atakapokujia ghafla (aidha kwa kifo au unyakuo ) akukute katika utumishi wako.
Lakini ukianza kuidharau kazi ya Mungu na kuigeuza kama vile biashara, hutaki kutumika mpaka ulipwe, hutaki kusimamia kundi lako kama mchungaji, unazini na washirika, hutaki kuwafundisha watu kama mwalimu, unaona uvivu wa kuwahubiria wengine Habari njema, kama mwinjilisti, unamgeuza Mungu kama mtu baki, unamtumikia tu pale unapojisikia, ukiwa huna mudi, unaendelea na mambo yako.
Ndugu, thawabu kama hii itakupita, Kazi ya Mungu inapasa iwe ni sehemu ya Maisha yako, ikiwa umeitwa kweli na Bwana, usiruhusu mapengo pengo yasiyokuwa na lazima yakusonge, mpaka kusudi lote liyeyuke ndani yako.
Lakini ukisimama katika nafasi yako, kama vile, huyu ambaye Bwana Yesu alimzungumzia hapo kwamba alimkuta anawapa watu wake chakula kwa wakati, aliahidi kumweka juu ya kazi yake yote.
Katika huo ufalme wa milele unaokuja huko, zitakuwepo kazi na majukumu, na hivyo, tangu sasa Bwana anatafuta watakaozisimamia kama viongozi kazi hizo za kimbinguni tukufu sana. Na watakaopewa nafasi hizo za kipekee ni wewe na mimi endapo tutakuwa tunagawa posho la Bwana kwa wakati.
Hivyo tuamke, kama tulikuwa tunalegea mahali, tuanze kuitenda kazi ya Bwana kwa bidii mpya.
Bwana akubariki.
Usikose mwendelezo..
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
JINSI MUNGU ATAKAVYOTOA THAWABU ZAKE, NA VIGEZO ATAKAVYOTUMIA. (Sehemu ya 1)
Bwana Yesu asifiwe, katika Makala hizi, tutazama vigezo ambavyo Mungu atavitumia kutoa thawabu zake, tutakapofika kule ng’ambo, Hii itatusaidia kuzidisha hamasa zetu katika kumtumikia Mungu, kama vile mtume Paulo, alivyoliona hilo, mpaka akasema..
Wafilipi 3:14 “nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu”.
Tutapitia baada ya vifungu, ambavyo vitatupa picha jinsi thawabu hizo Mungu atakavyozigawa; Kigezo cha thawabu ya kwanza tunakisoma katika Mathayo 20:1-16
Unaweza ukasema ni kwanini Mungu afanye hivyo? Embu tupitie Habari hii, tutapata majibu yote.
Mathayo 20 : 1-16
“1 Kwa maana ufalme wa mbinguni umefanana na mtu mwenye nyumba aliyetoka alfajiri kwenda kuajiri wakulima awapeleke katika shamba lake la mizabibu.
2 Naye alipokwisha kupatana na wakulima kuwapa kutwa dinari, aliwapeleka katika shamba lake la mizabibu.
3 Akatoka mnamo saa tatu, akaona wengine wamesimama sokoni wasiokuwa na kazi;
4 na hao nao akawaambia, Enendeni nanyi katika shamba langu la mizabibu, na iliyo haki nitawapa. Wakaenda.
5 Akatoka tena mnamo saa sita na saa kenda, akafanya vile vile.
6 Hata kama saa kumi na moja akatoka, akakuta wengine wamesimama, akawaambia, Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi?
7 Wakamwambia, Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri. Akawaambia, enendeni nanyi katika shamba la mizabibu.
8 Kulipokuchwa, yule bwana wa shamba akamwambia msimamizi wake, Waite wakulima, uwalipe ujira wao, ukianzia wa mwisho hata wa kwanza.
9 Na walipokuja wale wa saa kumi na moja, walipokea kila mtu dinari.
10 Na wale wa kwanza walipokuja, walidhani kwamba watapokea zaidi; na hao pia wakapokea kila mtu dinari.
11 Basi wakiisha kuipokea, wakamnung’unikia mwenye nyumba,
12 wakisema, Hao wa mwisho wametenda kazi saa moja tu, nawe umewasawazisha na sisi tuliostahimili taabu na hari za mchana kutwa.
13 Naye akamjibu mmoja wao, akamwambia, Rafiki, sikudhulumu; hukupatana nami kwa dinari?
14 Chukua iliyo yako, uende zako; napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe.
15 Si halali yangu kutumia vilivyo vyangu kama nipendavyo? Au jicho lako limekuwa ovu kwa sababu ya mimi kuwa mwema?
16 Vivyo hivyo wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho”.
Lakini ni wakina nani hawa, ambao, watakuja kulipwa sawasawa na wale waliotaabika katika kazi ya Mungu kwa muda mrefu.
Ukitazama, utaona, wale wa mwisho, hawakuwa wanashughulika mahali popote hapo kabla.. Bali mwenye shamba alipowafuata na kuwauliza kwanini mmesimama hapa mchana kutwa wakasema “Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri”.. Hii ikiwa na maana kama wangebahatika kufuatwa na mwenye shamba tangu asubuhi nao pia wangefanya kazi kubwa tu kama wale wengine, lakini hakutokea mtu wa kuwaajiri mpaka jioni.
Ikifunua kuwa, kuna watu mpaka sasa bado hawajafikiwa na neema ya wokovu, na pengine umri umeenda, labda tuseme mpagani Fulani mwabudu ng’ombe, lakini akiwa na miaka 80, ndio anahubiriwa injili na kuokoka kwa kumaanisha, na baada ya hapo anakuwa tayari kumtumikia Mungu kwa moyo wake wote, pengine akamtumikia Mungu kwa uaminifu kwa mwaka 1 tu akafa.
Au mwingine, neema imemkuta katika ujana wake, labda miaka 20 tu, lakini akatumika miaka 2 tu, alipofikisha miaka 22 akafariki.
Sasa watu kama hawa, kama walitumika kwa uaminifu kwa muda huo mfupi tu. Usishangae kuwakuta kule ng’ambo wamepewa thawabu sawa mitume. Ni kwanini? Ni kwasababu wakati neema inawafikia, na muda wao wa kutumika ulipokuja, waliandikiwa muda mchache sana. Hivyo kama wangekutwa tangu zamani ni wazi kuwa wangemtumikia Mungu kwa uaminifu.
Lakini,ikiwa wewe leo hii unaisikia neema, unaichezea, leo upo na Kristo, kesho upo na shetani, yaani hueleweki, usitazamie, Kristo atakupa thawabu yoyote, ikiwa utakufa leo katika hali kama hiyo, yaani umezaliwa katika familia ya kikristo, unajua kabisa misingi ya kiimani kwamba, pasipo wokovu huwezi kwenda popote, usitazamie, utalingana na yule mpagani au mtu wa dini nyingine ambaye kaokoa hivi karibuni, halafu akafa.
Bwana alisema wamwisho watakuwa wa kwanza, na kwanza watakuwa wamwisho. Ithamini neema uliyopewa , hizi ni siku za mwisho.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Ni muda gani Bwana Yesu alisulibiwa. Je! Ni saa 3 au saa 6?
KWANINI MTINI KATIKATI YA MIZABIBU?
NI NANI ATAKAYEUCHUKUA MSALABA WA YESU?
AINA TATU ZA WAKRISTO.
Bwana Yesu alimaanisha nini kusema “Saa yangu haijawadia?”
Jibu: Tusome,
Yohana 11:32 “ Basi Mariamu alipofika pale alipokuwapo Yesu, na kumwona, alianguka miguuni pake, akamwambia, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa.
33 Basi Yesu alipomwona analia, na wale Wayahudi waliofuatana naye wanalia, aliugua rohoni, akafadhaika roho yake,
34 akasema, Mmemweka wapi? Wakamwambia, Bwana, njoo utazame.
35 Yesu akalia machozi.
36 Basi Wayahudi wakasema, Angalieni jinsi alivyompenda.
37 Bali wengine wao wakasema, Je! Huyu aliyemfumbua macho yule kipofu, hakuweza kumfanya na huyu asife?”
Ukisoma kwa makini habari hiyo utaona Bwana Yesu hakulia machozi kwa sabababu ya uchungu wa msiba, bali alilia kwasababu ya ugumu wa mioyo yao katika kumwamini Mungu.
Bwana hakuwa na uchungu na msiba kwasababu yeye ndiye ufufuo na uzima, alijua dakika chache mbeleni Lazaro atakuwa hai.
Lakini kitendo cha wale wafiwa walivyokuwa wanahuzunika, na kutokuamini kama Lazaro anaweza kuwa hai tena, na walivyokuwa wanalia kwa uchungu kama watu waliopoteza tumaini, kitendo hicho kilimuhuzunisha sana Bwana mpaka akalia machozi.
Amekaa nao mara nyingi, wamesikia akifufua wafu mara nyingi lakini bado walikuwa hawaaamini kama Mungu anaweza kumfanya akawa hai tena, ni jambo la kuhuzunisha sana..
Yohana 11:38 “Basi Yesu, hali akiugua tena nafsini mwake, akafika kwenye kaburi. Nalo lilikuwa ni pango, na jiwe limewekwa juu yake.
39 Yesu akasema, Liondoeni jiwe. Martha, dada yake yule aliyefariki, akamwambia, Bwana, ananuka sasa; maana amekuwa maiti siku nne.
40 Yesu akamwambia, Mimi sikukuambia ya kwamba ukiamini utauona utukufu wa Mungu?
41 Basi wakaliondoa lile jiwe. Yesu akainua macho yake juu, akasema, Baba, nakushukuru kwa kuwa umenisikia.
42 Nami nalijua ya kuwa wewe wanisikia sikuzote; lakini kwa ajili ya mkutano huu wanaohudhuria nalisema haya, ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma.
43 Naye akiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje”.
Utaona pia mara kadhaa, Bwana alihuzunishwa na Mafarisayo..
Marko 3:1 “Akaingia tena katika sinagogi; na palikuwako huko mtu mwenye mkono uliopooza;
2 wakamvizia ili kuona kama atamponya siku ya sabato; wapate kumshitaki.
3 Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, Simama katikati.
4 Akawauliza, Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya? Kuponya roho au kuiua? Wakanyamaza.
5 Akawakazia macho pande zote kwa hasira, AKIONA HUZUNI KWA AJILI YA UGUMU WA MIOYO YAO, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Naye akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena.
6 Mara wakatoka wale Mafarisayo, wakawa wakifanya shauri juu yake pamoja na Maherodi, jinsi ya kumwangamiza”.
Na hata sasa Bwana analia machozi, kwasababu ya ugumu wa mioyo yetu, Hata sasa tunamhuzunisha Mungu kwa kutomwamini kwetu, na hata wakati mwingine tunapomjaribu.
Hivyo hatuna budi kuishi maisha ya Imani, ili tumpendeze Mungu.
Waebrania 11:6 “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza…”
Maran atha!.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Unaweza ukajiuliza Je shetani anaweza kuwazuia watu wasihubiri injili?
Jibu ni ndio Tusome,
1 Wathesalonike 2:17 “Lakini ndugu, tukiwa tumefarakana nanyi kwa kitambo, kwa uso si kwa moyo, tulizidi kutamani kwa shauku nyingi kuwaona nyuso zenu.
18 Kwa hiyo tulitaka kuja kwenu, naam, mimi Paulo, mara ya kwanza, na mara ya pili, na Shetani akatuzuia”.
Kulingana na maneno hayo ya Mtume Paulo, ni wazi kuwa shetani anahusika pakubwa sana katika kuizuia injili.
Siku zote shetani ni adui wa injili hakuna mahali alishawahi kukubaliana na watu kuipeleka injili. Hataki injili ihubiriwe kwasababa anajua ni uweza wa Mungu uletao wokovu. (Warumi 1:16).
Na yeye hataki kamwe watu wapate wokovu, anataka wasiisikie injili ili wafe katika dhambi zao na wajikute katika hukumu kama yeye siku ile ya mwisho.
Kwahivyo atafanya juu chini aizuie injili.
Sasa swali anaizuiaje?.
Anaizuia kwa kunyanyua matukio ambayo yataikwamisha safari ya kwenda kuhubiri.
Kwamfano akina Paulo labda walipanga kwenda huko Thesalonike lakini tarehe walizopanga kwenda hakukuwa na mashua za kuelekea huko au tufani zilianza kiasi kwamba haiwezekani kuanza safari kwa kipindi hicho.
Au wakati wameanza tu safari kufika maili kadhaa mbelen baharini ikachafuka, jahazi likavunjika, hivyo safari kuishia pale.
Au unakuta wamepanga safari vizuri tu inatokea wanapoteza nauli au wanaibiwa, hivyo safari inakuwa imeisha hapo.
Au wamepanga safari, ghafla mmojawao anaugua n.k.
Hayo ndio mambo shetani anayoyafanya kuizuia injili, na zaidi ya yote Mtume Paulo mwenyewe aliyashuhudia hayo mambo wanayokutana nayo katika safari zao za kwenda kuhubiri.
2 Wakorintho 11:25 “Mara tatu nalipigwa kwa bakora; mara moja nalipigwa kwa mawe; mara tatu nalivunjikiwa jahazi; kuchwa kucha nimepata kukaa kilindini;
26 katika kusafiri mara nyingi; hatari za mito; hatari za wanyang’anyi; hatari kwa taifa langu; hatari kwa mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za jangwani; hatari za baharini; hatari kwa ndugu za uongo;
27 katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi”.
Mambo hayo pia yaliwatokea wanafunzi wa Bwana Yesu walipokuwa wanavuka kwenda nchi ya Wagerasi, wakiwa katikati ya safari baharini, shetani alijaribu kuwazuia kwa kuwaletea tufani kubwa, shetani alitaka kuwazuia kwasababu aliona kuna watu wawili kule nga’ambo wenye pepo wanaishi makaburini, wanakwenda kufunguliwa, hivyo hilo jambo hawezi kuliruhusu, ndipo akawaletea tufani njiani, mpaka Bwana alipoamka na kuinyamazisha.(Mathayo 8:23-34).
Hivyo kilichomtokea Paulo na Wanafunzi wa Bwana Yesu kinaweza kumtokea mhubiri yeyote yule, haijalishi umeitwa kwa wito gani kamwe shetani hawezi kuruhusu wewe uhubiri injili kirahisi, ni lazima atakupinga tu.
Sasa swali kama hivyo ndivyo tunapaswa tufanyeje kila tunapotaka kwenda kuhibiri injili?.
Bwana Yesu alitupa dawa ya kuepukana na majaribu ya namna hiyo, na hiyo si nyingine zaidi ya kuomba kwa bidii.
Bwana Yesu aliwaambia wanafunzi wake mara kadhaa waombe ili wasije wakaingia majaribuni, kwasababu alijua silaha moja kubwa ya kudhoofisha vizuizi vya shetani ni kuomba, ndio maana ijapokuwa yeye mwenyewe alikuwa ni Mungu lakini alikuwa anakesha kuomba, ili kutufundisha sisi.
Na jukumu la kuomba sio tu la Mhubiri, au mchungaji, au Muinjilisti, au Mtume.
Jukumu la kuomba ni la kila mtu aliye mkristo, kila mtu anapaswa kuiombea ili injili iweze kupelekwa bila kizuizi chochote, unapotenga muda na kuiombea injili ya Bwana Yesu, hujui ni mchango gani mkubwa uliouchangia.. Kwa kuomba kwako huko unaharibu mipango ya shetani ya kumvunjia jahazi mhubiri fulani mahali fulani.
Kwa kufunga kwako kuiombea injili ya Bwana Yesu, umeharibu mipango ya wizi na magonjwa shetani aliyoipanga juu ya wahubiri fulani waliopanga kwenda kupeleka injili mahali fulani. Hivyo na wewe unakuwa ni mojawapo ya jeshi la Bwana katika kuipeleka injili mbele.
Lakini ukiacha tu na kusema.. Aaah mimi sio mhubiri, sio muinjilisti hiyo sio karama yangu, huombi, hufungi, huchangii, hufanyi chochote, basi fahamu kuwa unaupa nguvu ufalme wa giza.
Ndio maana Mtume Paulo baada ya kuwaandikia waraka hawa Wathesalonike kwamba ameshindwa kuja kwao shetani kamzuia, alimalizia na kuwaambia hao Wathesalonike kwamba WAMWOMBEE.
Wasikae tu wakasubiri, kwani vita ni vikali.
1 Wathesalonike 5:24 “Ndugu, tuombeeni”
Na zaidi ya yote katika waraka wake wa pili aliwakumbusha tena jambo hilo hilo..
2 Wathesalonike 3:1 “Hatimaye, ndugu, tuombeeni, neno la Bwana liendelee, na kutukuzwa vile vile kama ilivyo kwenu ”.
Je na wewe unaiombea Injili ya Bwana Yesu?.
Bwana atubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Ni madhara gani yatampata mtu yule anayetafsiri Neno isivyopaswa!
Ni kweli Paulo alipuuzia maonyo aliyopewa ya kwenda Yerusalemu?