Jina kuu la Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia, Neno la Mungu ambalo ndio mwanga wa njia yetu na Taa iongozayo miguu yetu. (Zab.119:135).
Kitabu cha Filemoni ni waraka ulioandikwa na Mtume Paulo wakati akiwa gerezani, Kwa mtu mmoja anayejulikana kama Filemoni. (Ikumbukwe kuwa waraka ni kama barua tu), hivyo Mtume Paulo aliandika waraka huo/barua hiyo kwa Filemoni, na waraka huo kwa uongozo wa Roho, ukawekwa kwenye orodha ya vitabu vya biblia kwasababu una maonyo makubwa na mafunzo makubwa kwa wakristo. Na pia ni mojawapo ya vitabu vifupi katika agano jipya.
Sasa huyu Filemoni alikuwa ni nani?
Filemoni alikuwa ni mmoja wa watu waliompokea Yesu, kupitia injili iliyokuwa inahubiriwa na wakina Paulo katika mji wa Efeso, hivyo huyu Filemoni alikutana na injili hiyo na kumpokea Yesu, na kuanza kumtumikia kwa moyo wake wote, mpaka kufikia hatua ya kuwa askofu wa kanisa, ambalo lilikuwa linakusanyika nyumbani kwake mwenyewe (Filemon 1:2), huko Kolosai.Lakini pamoja na hayo, mtu huyu alikuwa ana uwezo na alikuwa anamiliki watumwa nyumbani kwake (yaani wafanyakazi).
Na mmoja wa watumwa wake aliyekuwa anaitwa Onesimo, siku moja alitoroka kwake na kumwibia baadhi ya mali zake, na kukimbia nazo Rumi. Wakati akiwa njiani kuelekea Rumi, alikutana na Paulo akihubiri injili, na Maneno ya Mungu yakamgusa na kumfanya kutubu kwa dhati kabisa. Na alipotubu ndipo baadaye Paulo akajua alikuwa ni mtumwa wa Filemoni yule wa Efeso, mtenda kazi kazi katika shamba la Mungu. Na kwasababu Paulo amemhakiki Onesimo kuwa ni kweli katubu kwa dhati, na kageuka kuwa mkristo, na kaacha wizi na mambo yote mabaya, na zaidi ya yote alikuwa anataka kufuatana na Paulo katika injili kila anakokwenda na hata katika vifungo vyake.
Lakini Paulo hakuruhusu afuatane naye badala yake kwa kuongozwa na hekima ya Roho akaamua amsafirishe amrudishe kwanza kwa Bwana wake, lakini asimrudishe mikono mitupu bali ampeleke na waraka kutoka kwake, wa ushuhuda wake kwa Onesimo, kwamba kijana wake si yule aliyemwacha, bali amebadilika na kuwa mtu mwingine, (kawa kiumbe kipya), na katika waraka huo pia kulikuwa na mambo machache ya kumshauri Filemoni juu ya Onesimo mtumwa wake….
Kwasababu kwa wakati huo, kulingana na sheria za kirumi, endapo mtumwa akimtoroka bwana wake, na akipatikana, sheria kwake ilikuwa ni kifo. Kwahiyo Paulo alilijua hilo na ndio maana akaazimu kumrudisha Onesimo kwa bwana wake pamoja na waraka.
Na katika waraka huo aligusia vipengele vikuu 3 vifuatavyo.
1. Kwanza aliomba ampokee kwasababu kashatubu na kubadilika..
Filemoni 1:9 “lakini, kwa ajili ya upendo nakusihi, kwa kuwa ni kama nilivyo, Paulo mzee, na sasa mfungwa wa Kristo Yesu pia. 10 Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo vyangu, yaani, Onesimo; 11 ambaye zamani alikuwa hakufai, bali sasa akufaa sana, wewe na mimi pia; 12 niliyemtuma kwako, yeye mwenyewe, maana ni moyo wangu hasa”
Filemoni 1:9 “lakini, kwa ajili ya upendo nakusihi, kwa kuwa ni kama nilivyo, Paulo mzee, na sasa mfungwa wa Kristo Yesu pia.
10 Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo vyangu, yaani, Onesimo;
11 ambaye zamani alikuwa hakufai, bali sasa akufaa sana, wewe na mimi pia;
12 niliyemtuma kwako, yeye mwenyewe, maana ni moyo wangu hasa”
2. Baada ya kumpokea asimfanye tena kama mtumwa, bali kama ndugu katika Kristo.
Filemoni 1:16 “ tokea sasa, si kama mtumwa, bali zaidi ya mtumwa, ndugu mpendwa; kwangu mimi sana, na kwako wewe zaidi sana, katika mwili na katika Bwana.” 3 Na pia kama alimdhulumu, basi Paulo atamrudishia na kulipa pale alipodhulumiwa,
Filemoni 1:16 “ tokea sasa, si kama mtumwa, bali zaidi ya mtumwa, ndugu mpendwa; kwangu mimi sana, na kwako wewe zaidi sana, katika mwili na katika Bwana.”
3 Na pia kama alimdhulumu, basi Paulo atamrudishia na kulipa pale alipodhulumiwa,
Filemoni 1:17 “Basi kama ukiniona mimi kuwa mshirika nawe, mpokee huyu kama mimi mwenyewe. 18 Na kama amekudhulumu, au unamwia kitu, ukiandike hicho juu yangu. 19 Mimi Paulo nimeandika kwa mkono wangu mwenyewe, mimi nitalipa. Sikuambii kwamba nakuwia hata nafsi yako”
Filemoni 1:17 “Basi kama ukiniona mimi kuwa mshirika nawe, mpokee huyu kama mimi mwenyewe.
18 Na kama amekudhulumu, au unamwia kitu, ukiandike hicho juu yangu.
19 Mimi Paulo nimeandika kwa mkono wangu mwenyewe, mimi nitalipa. Sikuambii kwamba nakuwia hata nafsi yako”
Filemoni 1:20 “Naam, ndugu yangu, nipate faida kwako katika Bwana; uniburudishe moyo wangu katika Kristo. 21 Kwa kuwa nakuamini kutii kwako ndiyo maana nimekuandikia, nikijua ya kuwa utafanya zaidi ya hayo nisemayo”.
Filemoni 1:20 “Naam, ndugu yangu, nipate faida kwako katika Bwana; uniburudishe moyo wangu katika Kristo.
21 Kwa kuwa nakuamini kutii kwako ndiyo maana nimekuandikia, nikijua ya kuwa utafanya zaidi ya hayo nisemayo”.
Katika waraka huu, biblia inatufundisha jinsi ya kuishi na watumwa wetu, ambao kwasasa tunaweza kusema watu tuliowaajiri. Na pia inatufundisha majukumu ya kila mtumishi wa Mungu (kwamba anapaswa awe mpatanishi).
Unaweza kuwa umeokoka na kumwamini Yesu, na nyumbani unaye mfanya kazi wa ndani, au mlinzi wa geti, au unafanya kazi katika ofisi na chini wako kuna watumishi umewaajiri,…kumbuka huyo mtumishi wako, au mfanyakazi wako anapookoka na kuwa na Imani kama yako, fahamu kuwa huyo kwako ni kama ndugu, hupaswi kumfanya kama mtumwa wako tena…Ndio anaweza kuendelea na kazi yake ya nyumbani, au ya kulinda lakini, mchukulie kama ni ndugu yako..maana yake, kazi anayoifanya iendane sana na mshahara wake, kiasi kwamba ajihisi kama vile analipwa bure, ukilinganisha na kazi anayoifanya…
Pia utu wake uendane sawa na kazi anayoifanya…Maana yake anapofanya kazi yako ajihisi kama na yeye ni sehemu ya ile kazi, kwa kupendwa, kusikilizwa, kupewa muda wa kupumzika, na si ajihisi ni kama mnyama, au mtumwa Fulani anayetumikishwa ili mwisho wa siku tu alipwe mshahara, na pia wewe kama bwana wake unapaswa uwe mvumilivu na mtu wa kusamehe kama Filemoni.
Wakolosai 4:1 “Ninyi akina bwana, wapeni watumwa wenu yaliyo haki na ya adili, mkijua ya kuwa ninyi nanyi mna Bwana mbinguni”.
Na pia kama wewe ni mtumwa huna budi kuwa mnyenyekevu, na kuwa na busara na hekima. Kwasababu biblia inasema pia..
Wakolosai 3:22 “Ninyi watumwa, watiini hao ambao kwa mwili ni bwana zenu, katika mambo yote, si kwa utumwa wa macho, kama wajipendekezao kwa wanadamu, bali kwa unyofu wa moyo, mkimcha Bwana.”
Maana yake ni kwamba, ijapokuwa boss wako ni ndugu yako katika Kristo, hupaswi kumkosea heshima, wala kumdharau. Ukimvunjia heshima, au ukimdharau na kumfanya boss wako ahuzunike tayari umemkosea Mungu.
Pia katika kitabu hichi tunajifunza, majukumu yetu kama watumishi wa Mungu, kwamba tuwe wapatanishi, hapo tunamwona Mtume Paulo, baada ya kumbadilisha Onesimo kwa injili yake, hakumchukua na kuanza ziara za kutembea naye, ingawa Onesimo alikuwa tayari na alitamani sana awe anatembea na Paulo, lakini Paulo aliona si vyema kutembea naye katika utumishi, na ilihali bado ni mtumwa wa mtu mwingine, hivyo ni vizuri kwanza akarudi kwa bwana wake, na kupatana naye, na kama bwana wake kama atampa ruhusa basi ndipo arudi na kuzunguka na wakina Paulo katika kuhubiri. Lakini si hekima kumchukua na ilihali katoroka kwa bwana wake, isingeleta picha nzuri, Filemoni asikie kwamba yule mtu aliyemuibia na kutoroka yupo huko anatembea na Paulo katika kuhubiri.
Vivyo hivyo hata katika wakati huu, wapo watu wamewaibia maboss zao, na wametubu kwa dhati kabisa, lakini hawataki kwenda kupatana na waliowaibia…wanataka watubu tu kimoyo moyo, na zaidi ya yote wanapokelewa makanisani na hata katika huduma na kupewa nafasi ya kuhudumu. Pasipo kujua kuwa huko nje wameacha sifa gani.
Wapo wengine wamekutwa katika udunia, na wameisikia injili na kuamua kutubu, lakini hapo kabla walikuwa wameshawakimbia wake zao, au waume zao, au familia zao…sasa kabla ya kuwapokea watu kama hao katika utumishi, ni vizuri kwanza wakapatane na ndugu zao, na wake zao au waume zao…Huku sisi tuliowahubiria tukiwasaidia, kama Paulo alivyomsaidia Onesimo kurudi kwa bwana wake kwa waraka, ili watakapoingia katika utumishi wasilete picha mbaya kwa walio nje.
Hivyo kama mchungaji, au mtumishi yeyote wa Mungu, tunapaswa tuchunguze kwanza historia ya mtu, kabla ya kuanza naye kazi ya huduma, hata kama ametubu kwa dhati, hiyo pekee haitoshi, anapaswa atengeneze machache ya nyuma, ambayo ameyaharibu, ili isipatikane dosari yoyote katika injili atakayoihubiri, au watakaoihubiri wale waliomhubiria.
Bwana atubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali. Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA KITABU CHA RUTHU:
MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA WARAKA WA PILI WA YOHANA.
JINSI YA KUEPUKA KUUMIZWA MOYO KUSIKOKUWA NA SABABU.
NI NINI TUNAJIFUNZA KWA DEMA NA MARKO?
JINSI MTUME PAULO ALIVYOUTHAMINI WITO WAKE, JUU YA WENYE VYEO.
Rudi nyumbani
Print this post