Category Archive Home

Ni kweli hakuna mtu aliyewahi kuuona uso wa Mungu Zaidi ya Bwana Yesu?

SWALI: Musa alikuwa na mawasiliano ya ana kwa ana na Mungu, hata kuuona uso wake lakini katika Yohana 1:18, inaonekana Yohana anakanusha kuwa hakuna mtu aliyewahi kumwona Mungu isipokuwa Kristo pekee.


Jibu: Kumwona Mungu kunakozungumziwa hapo sio KUMTAZAMA USONI, kwamba anaonekanaje, mwonekano wake ukoje, uso wake unafananaje fananaje n.k. La! Sio kwa namna hiyo. Bali kumwona kunakozungumziwa hapo ni kwa ufahamu.

Kwamfano tunaposema TUMEUONA MKONO WA BWANA, haimaanishi tumeenda mbinguni tukauona mkono wake jinsi ulivyo, au umeshuka chini tukauona jinsi ulivyo, rangi yake na idadi ya vidole alivyo navyo! N.k. La! Bali tunamaanisha tumeona uweza wake mkuu!. Vile vile tunaposema tumemwona Bwana katika maisha yetu, haimaanishi ameshuka mbele yetu na tukamwona sura yake, bali tunamaanisha tumeona uwepo wake na kuutambua.

Kadhalika maandiko hapo yanaposema hakuna aliyemwona Mungu haimaanishi “aliyemwona Uso wake jinsi ulivyo” bali inamaanisha “hakuna aliyemjua Mungu na kumfahamu, kiuweza na kimamlaka kikamilifu” isipokuwa Kristo peke yake. Wengine wamemwona na kumwelewa lakini si kwa kiwango ambacho Mungu mwenyewe, alikuwa anataka watu wamwelewe.. Hivyo ni sawa na hawakumwona kabisa! Au kumwelewa. Ni Bwana Yesu pekee ndiye aliyemwelewa na kumfunua Baba, kikamilifu…

Luka 10:22 “Akasema, Nimekabidhiwa vyote na Baba yangu, wala hakuna amjuaye Mwana ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba ila Mwana, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia”.

Umeona? Kristo pekee ndiye aliyemjua Mungu, jinsi inavyopaswa kumjua.. Musa hakumjua Mungu, ndio maana torati ya Musa havikuweza kumkamilisha mwanadamu!.. Kristo ndiye aliyekuja kumfunua Mungu kwetu jinsi inavyopaswa, na kutuonyesha mapenzi yake kamili..

Yohana 1:17 “Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo”.

Kwamfano Wanafunzi wa Yesu walikuwa wanamwona Bwana Yesu kila siku, lakini walikuwa hawamjui, macho ya mioyo yao yalikuwa yamefumbwa. Ndio maana alipowauliza Yeye ni nani, wakawa wanakosa jibu sahihi, mpaka Petro ambaye alifunuliwa na Baba, aliposema yeye ni Mwana wa Mungu, ili litimie hilo neno “WALA HAKUNA AMJUAYE MWANA ILA BABA”; WALA HAKUNA AMJUAYE BABA ILA MWANA, na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia”.

Hivyo Bwana Yesu(Mwana wa Mungu).. ndio kila kitu katika haya maisha. Hakuna mtu mwingine yeyote, au nabii mwingine yeyote ambaye tunaweza kumfuata au kumtegemea maneno yake tukafika mbinguni. Injili ya Musa haikumhaidia mtu kufika kule Baba aliko, wala ya Nabii mwingine yeyote.. Ni Yesu pekee ndiye aliyetoa njia ya Watu kumfikia Baba Mbinguni!!..kwasababu yeye ndiye anayemjua.. Na njia hiyo ya kumfikia Baba ni YEYE MWENYEWE, yaani maisha yake na Neno lake.

Yohana 14:5 “Tomaso akamwambia, Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia?

6 Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi”

Je! Unataka kwenda mbinguni kwa Baba?

Kama ni ndio!, basi tambua NJIA NI YESU. Hakuna elimu nyingine yeyote, wala dini nyingine yeyote, wala maarifa mengine yeyote, ambayo yataweza kukufikisha mbinguni.. isipokuwa ni YESU TU!. Huyo ndiye aliyemwona Baba na Baba mwenyewe akamthibitisha.. hivyo hakuna njia ya mkato ya kufika mbinguni.

Hivyo kama hujampokea, mpokee leo na utubu na kubatizwa, ili aingia maishani mwako na kukuongoza katika njia ya uzima wa milele.

Maran atha!

[embedyt] https://www.youtube.com/embed?listType=playlist&list=PLIIhnDzXkeEcXSNPlq09Q5yonU3MOLI0h&v=kuCSAZcnM80&layout=gallery[/embedyt]

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Mlima Gerizimu na Ebali ni ipi, na umuhimu wao rohoni ni upi?

MJUE SANA YESU KRISTO.

Kama Mungu ndiye kaumba kila kitu, je ni yeye huyo huyo ndiye aliyeumba dhambi pia?

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

KWANINI TUNAPASWA TUJIZUIE?

Rudi nyumbani

Print this post

Je! Karamu za ‘Idi’ ndio zipo hizo tunazozisoma katika Hosea (12:9)

Hosea 12:9 Lakini mimi ni Bwana, Mungu wako tangu ulipotoka katika nchi ya Misri; nitakukalisha tena katika hema, kama siku za KARAMU YA IDI.


JIBU: Tofauti na inavyodhaniwa hapo, na watu wa dini tofauti, kwamba Biblia inazitambua sherehe za kiislamu!. Jambo ambalo si kweli.

Ni vizuri kufahamu kuwa lugha yetu ya Kiswahili imetohoa maneno mengi sana kutoka katika lugha ya kiharabu, hata wakati ambapo biblia inatafsiriwa katika Kiswahili ilifuata mkondo huo huo. Kwamfano Sehemu nyingine utaona neno “shehe” likitajwa (1Samweli 5:8), na hapa unaona pia Neno “Idi” .

Kulingana na lugha ya  kiharabu neno IDI, linamaanisha “Sherehe”. Haijalishi ni sherehe ya aina gani, inaweza ikawa ni ya kidini au ya kitaifa, au ya kitamaduni, au ya kimuungano..

Hivyo imezoeleka na watu wengi wasioilewa lugha ya kiharabu kudhani kuwa Idi ni neno la sikukuu ya kiislamu, kumbe sio.

Katika biblia ya kiharabu, mahali popote, kulipotajwa sherehe ya kiyahudi, Neno Idi liliandikwa pale. Mfano, palipoandikwa sikukuu ya pasaka, iliandikwa “idi ya pasaka” n.k..

Hivyo, hatushangai na Neno hilo kuonekana katika baadhi ya vifungu kwenye biblia. Hiyo yote ni kwasababu lugha yetu ya Kiswahili, imeundwa kutoka katika lugha nyingi mbalimbali. Kwahiyo inayozungumziwa hapo sio sikukuu ya kiislamu, bali ni sikukuu ya vibanda, ambayo wana wa Israeli walikuwa wakiisheherekea kwa katika vibanda pindi walipokuwa jangwani.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

SIKUKUU 7 ZA KIYAHUDI ZINAFUNUA NINI KWETU?

UFUNUO: Mlango wa 19

ESTA: Mlango wa 5, 6 & 7

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

Je kunena kwa Lugha mpya kukoje?.Na hizi lugha ni zipi, na je! ni lazima kila mkristo aliyepokea Roho Mtakatifu anene kwa lugha mpya?

Rudi nyumbani

Print this post

MWANAMKE, BINTI, MAMA. (Sehemu ya 2)

Hii ni sehemu ya pili ya mfululizo wa masomo kwa wanawake, katika sehemu ya kwanza tumeona, ni kwanini Bwana alipokutana na yule mwanamke mwenye dhambi, alimtambua kwa jinsia yake (Yaani “mwanamke”) na sio kwa mwonekano wake wa kike pengine wa kiumri au  wa kimaumbile. Hiyo ni kufunua kuwa ujumbe alioubeba yule mwanamke ulikuwa ni wa kijinsia.. yaani maalumu kwa wanawake. Hivyo kama hukupata maelezo yake, unaweza kunitumia ujumbe inbox nikakutumia.

Leo tutaenda katika sehemu ya pili: ya BINTI.

Mahali pengine, Bwana Yesu, aliwatambua wanawake wengine kama, binti zake.. Na cha ajabu ni kuwa, wengine walikuwa pengine wana umri mkubwa kuliko yeye, lakini bado aliwaita BINTI zake, akifunua kuwa kutazama kwake hakukuwa katika jicho la kimwili bali la rohoni. Embu tusome, kisa hiki kimoja..kisha tuone ni ujumbe gani Bwana alitaka kuupitisha kwa ulimwengu kupitia mwanamke huyu.

Mathayo 9:20 “Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake.

21 Kwa maana alisema moyoni mwake, Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona.

22 Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu, BINTI YANGU; imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile.”.

Swali la kujiuliza ni kwanini alimtambua mwanamke huyu kama binti na sio pengine kama Mama, au bibi?

Ni kwasababu ya Imani yake ya kipekee aliyokuwa nayo kwake..Ambayo hakuiona kwa watu wengine wote waliomfuata, ijapokuwa alihangaika kwa miaka 12 kutafuta suluhu la matatizo yake asipate, lakini alipofika kwa Yesu kwa mara ya kwanza tu hakumuhesabia kama mmojawapo wa wale matapeli aliokutana nao, huko nyuma, waliomchukulia fedha zake.

Bali alimwamini moja kwa moja kwa asilimia 100, akasema, nitakapoligusa tu pindo la vazi lake, muda huo huo nitakuwa mzima, kumbuka hakusema sio “naamini nitapona, au pengine nitapona” hapana, bali alisema “NITAPONA” kuonyesha kuwa alikuwa na uhakika wa yule aliyekutana naye sio mbabaishaji au tapeli…. Na ndio maana akaona hata hakuna sababu ya kwenda kumsumbua kuzungumza naye, au kumwomba aje kumtembelea, Bali aliona pindo la vazi lake, tu linatosha yeye kuwa mzima..

Na Yesu alipoiona Imani yake saa ile ile akamgeukia na kumwita “Binti yangu”.. Akampa nafasi ya kipekee sana Kama Mtoto wa kike aliyemzaa yeye mwenyewe, ambaye ana haki zote za kupokea mema yote ya Baba yake.

Tujiulize ni wanawake wangapi leo Bwana anaweza kuwaita binti zangu? Usidhani Kristo kukuita binti yake, kwasababu ya umri wako mdogo, au mrembo wako, au utanashati wako, hilo halipo, yeye hana jicho la mwilini, kama sisi tulilonalo, haangalii umri wala umbile.

Kama wewe ni mwanamke lakini unafika kwa Kristo ili kujaribu jaribu tu, uone kama Bwana atakujibu au la!,atakusaidia au la! unamlinganisha na wale waganga wa kienyeji uliowahi kuwatembelea huko nyuma.. uone kama atajibu au la!. Ujue kuwa wewe sio binti wa Yesu.

Mabinti wa Yesu, tangu walipokutana na Yesu utawakuta wametulia kwa Bwana hadi sasa, wanaouhakika na waliyemwendea, hawahitaji kusaidiwa na mtu, kuelewa kuwa Yesu ni muweza, wanafanya mambo yao wakiwa wame-relax, huwezi kuwakuta leo kanisani Kesho, disco,  leo wamevaa magauni, Kesho wanakatiza barabarani na visuruali na vikaptura, leo kwa nabii huyu Kesho kwa yule..huwezi kuwakuta wapo namna hiyo.

Hao ndio binti za Mungu. Na faida yao ni kuwa kwasababu wameshaitwa binti za Mungu, tayari wanaourithi kutoka mbinguni. Jambo ambalo wengi hawajui wakidhani kila mtu atakuwa mrithi wa kila baraka ya Mungu mbinguni.

Dada/mama/bibi tambua ni nini Kristo anatamani kuona kwako, acha kutangatanga na huu ulimwengu, Acha kujaribu jaribu, maanisha kumfuata Kristo.. Yeye mwenyewe anasema.

2Wakorintho 6:17 “Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha.

18 Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu WANANGU WA KIUME NA WA KIKE”,

Kumbuka hizi ni siku za mwisho, Kristo anarudi siku yoyote. Bado tu hujatulia kwa Bwana? Injili tuliyobakiwa nayo sasa hivi sio ya kubembelezewa tena wokovu, ni wewe mwenyewe aumke usingizini, umtafute Mungu wako. Kwasababu muda umeshaisha.

Maran atha..

Usikose sehemu ya tatu na ya mwisho ya Makala hii, ambayo, tutaona pia ni kwanini Bwana Yesu aliwatambua wanawake wengine kama MAMA.

Bwana akubariki..

Maran atha

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

Print this post

Biblia inasema tusiwe kwazo kwa yeyote, je! inawezekanikaje kwa dunia hii ya sasa?(2Wakorintho 6:3).

Jibu; Tusome,

2 Wakorintho 6:3 “Tusiwe kwazo la namna yo yote katika jambo lo lote, ili utumishi wetu usilaumiwe”

Leo hii ukizungumzia neno “kukwaza” moja kwa moja akili za wengi zinalenga katika “kuudhi au kumuudhi mtu”.

Hivyo andiko hilo ni rahisi kulitafsiri, kuwa tusiwakwaze watu (yaani tusiwaudhi) kwa namna yoyote ile.

Lakini kiuhalisia andiko hilo halimaanishi hivyo.

Tafsiri ya neno kikwazo/kwazo ni kitu chochote ambacho kinaweza kumzui mtu asisonge mbele, kwamfano mtu anayesafiri kwa gari na akakuta jiwe kubwa katikati ya barabara, limezuia barabara jiwe lile ni kikwazo kikwazo kwake kwa safar yake.

Sasa kibiblia KWAZO ni kitu chochote kinachomzuia mtu kuingia katika Imani au kusonga mbele katika imani..

Hivyo hapo biblia inaposema kwamba tusiwe KWAZO la namna yoyote..imemaanisha kuwa TUSIWE KIKWAZO KWA MTU YEYOTE KUINGIA KATIKA IMANI.

Vipo vitu vingi ambavyo vinaweza kuwa kikwazo kwa watu wengine kuvutiwa na imani ya kikristo. Na mfano wa vitu hivyo ni maisha ya kianasa na kiulimwengu watu wanayoishi.

Kwamfano uvaaji wako unaweza kuwa kwazo kwa mwingine kumpokea Yesu, huwezi kwenda kumhubiria mtu ampokee Yesu na huku akikuangalia wewe unavaa vimini, Unatembea nusu uchi, au unajiuza, au ni mtukanaji, au mlevi.. Hapo ni lazima utakuwa KWAZO tu la yeye kuingia katika Imani na hata wakati mwingine kusababisha jina la Mungu kutukanwa.

Warumi 2:21 “basi wewe umfundishaye mwingine, je! Hujifundishi mwenyewe? Wewe uhubiriye kwamba mtu asiibe, waiba mwenyewe?

22 Wewe usemaye kwamba mtu asizini, wazini mwenyewe? Wewe uchukiaye sanamu, wateka mahekalu?

23 Wewe ujisifuye katika torati, wamvunjia Mungu heshima kwa kuiasi torati?

24 Kwa maana jina la Mungu latukanwa katika Mataifa kwa ajili yenu, kama ilivyoandikwa”.

Katika hali kama hiyo biblia ndio inatuonya tusiwe Kwazo la namna yoyote ile kwa watu, ili utumishi wetu pia usilaumiwe.
Lakini haimaanishi kuwa tusiwaudhi watu kwa namna yoyote ile!.

Katika haya maisha haiwezekani kuishi maisha ambayo hutawaudhi watu kabisa..kwasababu hata ukitenda mema yote bado utawaudhi tu baadhi ya watu..hivyo hilo ni jambo lisiloepukika.

Lakini kuishi maisha ambayo hatutakuwa KWAZO la mtu kuingia katika ufalme inawezekana kwa asilimia zote, endapo tukijikana nafsi kweli kweli, na tukimtegemea Roho Mtakatifu.

Bwana azidi kutusaidia katika hilo ili tusiwe kwazo kwa yeyote!

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

USIMLAANI KIZIWI, WALA USITIE KWAZO MBELE YA KIPOFU.

INJILI YA MANENO LAINI ITAKUGHARIMU.

 

ZIKIMBIE TAMAA ZA UJANANI! NA MTU YEYOTE ASIUDHARAU UJANA WAKO.

KUSAMBAA KWA ROHO YA MPINGA-KRISTO.

 

Rudi nyumbani

Print this post

Misukule ni nini? ni kweli ipo? Na je! inaweza kurudishwa?

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe.

Misukule kwa tafsiri inayojulikana na wengi, ni watu waliotekwa kichawi, kwa lengo la kutumikishwa..ambapo kabla ya kutekwa huko, mtu yule anakuwa anatengenezewa kifo bandia, na kuonekana kama amekufa, na hata kuzikwa kabisa..lakini anakuwa hajafa, na kile kilichozikwa kinakuwa si yeye, bali ni kipande kidogo cha gogo, au mgomba.

Ambapo kipande hicho kinageuzwa kimazingara na kuchukua taswira ya yule mtu aliyetekwa. Na hivyo ndugu wa huyu aliyechukuliwa wanakuwa wanadhani wamemzika mpendwa wao kumbe sio.

Sasa swali ni Je! Ni kweli hiyo aina ya ushirikina ipo?.

Jibu ni ndio ipo!. Shetani anao uwezo wa kufanya jambo hilo na mengine Zaidi ya hayo, aliweza kugeuza fimbo kuwa nyoka aliye hai mbele ya Farao, si zaidi fimbo kuwa nyoka aliyekufa?, au fimbo kuwa maiti ya mtu aliyekufa!!..hivyo hilo ni jambo ambalo linawezekana.

Lakini pamoja na kwamba anaweza kufanya hayo,  lakini si rahisi kwake yeye kufanya hivyo, kuna ugumu mkubwa sana kwake….tofauti na wengi tunavyodhani kuwa shetani mambo yote kwake ni mteremko, kwamba lolote atakalojiamulia kwake ni rahisi kulifanya. Nataka nikuambie hata kwa shetani mambo mengine si rahisi kwake bali anapambana sana ili afanikiwe.

Ingekuwa kila kitu kwake ni mteremko, sidhani mpaka leo dunia ingekuwepo..vile vile angewafanya watu wote leo kuwa wabaya kupindukia, lakini utaona ijapokuwa kuna watu wengi walio waovu na ambao hawajampokea Yesu, LAKINI BADO SI WABAYA KUPINDUKIA!!. Si kwamba shetani hapendi kuwafanya wawe wabaya sana!.. anatamani kuwafanya kuwa wabaya kupindukia..Lakini anashindwa na kukwama kwa wengi.. Kwasababu si kila mlango ni mrahisi kwake kuuingia.

Ndio maana utaona ataweza kumshawishi na kumfanya mtu kuwa mwasherati, na mlevi lakini kumshawishi kuwa mkatili na gaidi inakuwa ni ngumu!.. Hiyo ni kwasababu kuna milango ambayo si mirahisi kwa shetani kuiingia kwa mwanadamu.. ataweza kumshawishi mtu kuwa mwongo na mtukanaji na mzinzi wa kupindukia lakini akashindwa kumfanya awe Jambazi linaloua watu kikatili!..utaona ni watu baadhi tu miongoni mwa watu wake anaofanikiwa kufawanya magaidi.

Vivyo hivyo ni watu baadhi tu ndio ataweza kuwateka na kuwageuza kuwa Misukule, na kuwatumikisha, lakini si jambo rahisi kwake, ambalo linaweza kufanyika kwa jinsi anavyotaka yeye au kwa mtu yeyote.

Jambo la mtu kuchukuliwa msukule, ni gumu sana kutokea kwa mtu, kama vile, ilivyo ngumu kwa kahaba, au mlevi kuwa gaidi yule wa kuchinja watu!.. Mtu anaweza asiwe hata ndani ya imani ya kikristo na ikawa ngumu kwa shetani kumchukua msukule. Ni kwasababu kuna ulinzi Fulani ambao upo duniani wa Roho Mtakatifu.

Ni watu wachache sana ambao ndio wanaweza kuchukulika msukule na kutekwa kwa namna hiyo.. (tutakuja kuliona hilo kundi mbele kidogo)..Kama tu vile ilivyo ni watu wachache sana walio katika ufalme wa giza wanaoweza kufanywa kuwa magaidi na shetani…

Wapo wengi walio waovu duniani, wazinzi, waongo, lakini bado isiwe rahisi kwao kuchukuliwa msukule..

Hivyo msukule sio jambo kubwa na linalofanyika kirahisi kama linavyotukuzwa leo. Kiasi kwamba leo hii kati ya misiba 10 inayotokea kiajabu ajabu.. basi 2 au 3 katika hiyo, utasikia watu wakisema huyo mtu kachukuliwa msukule, hajafa!.

Jambo ambalo si kweli!.. ambalo lengo lake ni kuukuza ufalme wa giza na kupachika hofu..

Ingekuwa hivyo ndivyo nadhani shetani angeshamaliza watu wote duniani, kuwachukua misukule..Maana walio nje ya Imani, ni wengi kuliko walio ndani ya Imani. Nchi ya  India na China tu zina mabilioni ya watu wanaoabudu miungu, ambao hata hawamjui Mungu wa kweli, hao nadhani angeshawamaliza wote.. Lakini wengi wa hao wapo salama tu!.

Nchi za Ulaya na Marekani, zina idadi kubwa  ya watu wasioamini kama Mungu yupo, lakini wengi wao wapo huru, hawajachukuliwa misukule. Hata katika jamii zetu, wapo wengi walio waovu lakini wapo wanaishi.. Je! Unadhani shetani hawaoni na kuwatamani??.. anawaona na kuwatamani sana… lakini si rahisi kwake, kwasababu yupo Roho Mtakatifu duniani ambaye anamzuia shetani kujiamulia kufanya baadhi ya mambo.. Maandiko yanasema baada ya huyo kuondolewa duniani ndipo mambo yatabadilika ulimwenguni (2Wathesalonike 2:7).

Sasa wengi wa wanaochukuliwa Msukule, wanakuwa ni watu wanaoangukia katika mojawapo ya makundi haya matatu

1. Wachawi na Washirikina.

Hili ni kundi la kwanza, ambalo ni rahisi sana kuchukuliwa msukule. Wengi wa wanaochukuliwa msukule ni aidha wao wenyewe walikuwa wachawi, au washirikina. Hivyo kama ni mshirikina au mchawi basi, ni rahisi kwako kutekwa na adui.

2. Watu wanaohudhiria kwa waganga wa kienyeji.

Mtu yeyote ambaye anakwenda kwa mganga wa kienyeji, maana yake kamsogelewa shetani kwa hiari yake mwenyewe, hivyo kajiuza kwa shetani na shetani anaweza kumfanya lolote, ikiwemo kumchukua msukule.

3. Watu wanaoyadharau Maneno ya Mungu kwa makusudi.

Hili ni kundi lingine ambao li karibu sana na kuchukuliwa msukule. Mtu yeyote anayeidharau injili kwa muda mrefu, na makusudi, huyo anajiondolea ulinzi wa kiMungu kwa haraka sana pasipo yeye kujijua..na anakuwa amejiuza kwa shetani bila yeye kujua.

Utauliza kivipi?

Kuna mfano mmoja wa mtu aliyechukuliwa Msukule na shetani mwenyewe kwenye biblia..huyo alikuwa ni mtu wa kuyadharau maneno ya Mungu, alipoonywa mara nyingi atubu alishupaza shingo..na ndipo walinzi wa mbinguni ambao kazi yao ni kuwalinda wanadamu, waliopoondoa ulinzi juu yake.. na kumruhusu shetani amchukue. Na huyo si mwingine zaid ya Mfalme Nebukadneza..

Danieli 4:23 “Tena, kwa kuwa mfalme alimwona mlinzi, naye ni mtakatifu, akishuka kutoka mbinguni, akisema, Ukateni mti huu, mkauangamize; ila kiacheni kisiki cha shina lake katika ardhi, pamoja na pingu ya chuma na shaba, katika majani mororo ya kondeni; kikatiwe maji kwa umande wa mbinguni, na sehemu yake iwe pamoja na wanyama wa kondeni, hata nyakati saba zipite juu yake;

24 tafsiri yake ni hii, Ee mfalme, nayo ni amri yake Aliye juu, iliyomjia bwana wangu, mfalme

25 ya kuwa utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa kondeni, nawe utalazimishwa kula majani kama ng’ombe, nawe utatiwa maji kwa umande wa mbinguni, na nyakati saba zitapita juu yako; hata utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa yeye amtakaye, awaye yote.

26 Na kwa kuwa waliamuru kukiacha kisiki cha shina lake; ufalme wako utakuwa imara kwako, baada ya wewe kujua ya kuwa mbingu ndizo zinazotawala.

27 Kwa sababu hiyo, Ee mfalme, shauri langu lipate kibali kwako; ukaache dhambi zako kwa kutenda haki, ukaache maovu yako kwa kuwahurumia maskini; huenda ukapata kuzidishiwa siku zako za kukaa raha.

28 Hayo yote yakampata mfalme Nebukadreza.

29 Baada ya miezi kumi na miwili, alikuwa akitembea ndani ya jumba la kifalme katika Babeli.

30 Mfalme akanena, akasema, Mji huu sio Babeli mkubwa nilioujenga mimi, uwe kao langu la kifalme, kwa uwezo wa nguvu zangu, ili uwe utukufu wa enzi yangu?

31 Hata neno lile lilipokuwa katika kinywa cha mfalme, sauti ilikuja kutoka mbinguni, ikisema, Ee mfalme Nebukadreza, maneno haya unaambiwa wewe; Ufalme huu umeondoka kwako.

32 Nawe utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa kondeni; utalishwa majani kama ng’ombe, na nyakati saba zitapita juu yako, hata utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, awaye yote.

33 Saa iyo hiyo jambo hilo likatimizwa, likampata Nebukadreza; alifukuzwa mbali na wanadamu, akala majani kama ng’ombe, na mwili wake ulilowa maji kwa umande wa mbinguni, hata nywele zake zikakua, zikawa kama manyoya ya tai, na kucha zake kama kucha za ndege”

Umeona?.. huyu alitekwa na shetani mwenyewe kwa ruhusa ya Mungu.. kwasababu alikuwa anayadharau wazi maneno ya Mungu, akachukuliwa msukule, maandiko yanasema akalishwa majani kama ng’ombe. Misukule ya siku hizi inalishwa pumba, na vitu visivyofaa..

Hiyo inatufundisha na sisi kutoyadharau maneno ya Mungu na kutokuwa na kiburi. Mungu akitukataa hakuna atakayetukubali.. Na Mungu akiondoa ulinzi wake juu yetu, kama alivyoondoa kwa Nebukadneza, unadhani ni nini shetani atakachokuwa amebakiwa nacho kwetu, Zaidi ya kutuchukua mateka?.

Na Mwisho, je! mtu anatokaje kama tayari kashachukuliwa Msukule?

Mtu anapokuwa katika kutekwa huko, akili zake zinakuwa zimefungwa anakuwa kama kichaa.. Hivyo kama hatakutana na mtu atakayemwombea huko basi atabaki katika hali hiyo hiyo mpaka Bwana atakapomfungua mwenyewe, kama alivyomfungua Nebukadneza..

Na kumbuka watu hawa(Misukule) wanakuwa wapo katika mwili, na si katika roho, kwasababu hawajafa.. Ni ngumu kuwaona kwasababu waliowashika wanawaficha katika nyumba zao..kama mtu anayeficha almasi ndani kwake….hivyo ni ngumu kujua, lakini wapo katika mwili na wanaonekana kwa macho kabisa.. hivyo wanapoonekana ni kama vile kichaa aliyeonekana barabarani.. hivyo anaweza kuchukuliwa na kufanyiwa maombezi, ili akili zake zimrudie..na anapofunguka anarudia hali yake ya kawaida, kama mtu aliyepona ukichaa. kwasababu alikuwa hajafa. (lakini kumbuka si kila kichaa ni msukule)… Na si kila misiba ni misukule.

Na vile vile hakunaga huduma ya kwenda kutafauta misukule, au kuichimbua..au kuiita huko iliko na kuirudisha.. kwasababu hujui ni nani na nani ndio kachukuliwa. Roho Mtakatifu ndiye anayefunua kwamba mahali Fulani katika nyumba Fulani kuna mtu kafungwa, anahitaji kuombewa afunguliwe..Hivyo!, na si kwenda kuzunguka na kutafuta msukule!.

Na Ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko ufalme wa giza. Roho ya Mungu duniani ni KUU kuliko roho ya shetani.

Hivyo hatuhitaji kuishi kwa hofu ya kuchukuliwa msukule, wala watoto wetu kuchukuliwa msukule, wala hatuhitaji kufuatilia sana habari za kichawi, kama tayari tupo ndani ya Kristo. Tunapokuwa ndani ya Kristo, tunapaswa tuongeze bidii katika kumjua sana Mungu Zaidi ya shetani.. Tukimjua sana Yesu na neema yake na utukufu wake..maarifa hayo yanatosha kutulinda na kutuhifadhi, hata kama hatujawahi kusikia neno uchawi katika maisha yetu.

Jambo la hatari shetani analolifanya katika siku hizi za mwisho, ni kuhakikisha anaupandisha hadhi ufalme wake, ambao tayari upo chini. Ndio hapo atanyanyua hata watu wahubiri ili kusifia kazi za shetani, na uchawi wake. Wakati kiuhalisia uchawi, si kitu kwa walio ndani ya Kristo, na wala Bwana Yesu hajawahi kutupa maagizo tukajifunze juu ya uchawi, ili tumwelewe yeye, au tumpendeze yeye. Anachotaka kwetu ni SISI tumjue yeye, na si tujue majina ya mapepo na elimu ya kuzimu.

Hivyo kama umempokea Yesu, tafuta kumjua Zaidi Yesu, na kama bado basi mpokee leo. Na tafuta kumjua.

Bwana akubariki.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Jiunge na Group letu ya whatsapp, la masomo ya kila siku kwa kubofya hapa > Group-whatsapp


Mada Nyinginezo:

KUOTA NYOKA.

EDENI YA SHETANI:

EDENI YA SHETANI:

Kwa maana kahaba ni shimo refu; Na malaya ni rima jembamba.

Kwanini Mungu awachome watu kwenye ziwa la moto na hali yeye ndiye aliyewaumba?

Rudi nyumbani

Print this post

Nini maana ya ‘Hukumu haina huruma kwake yeye asiyeona huruma’?

SWALI: Nini maana ya  “hukumu haina huruma kwake yeye asiyeona huruma”?(Yakobo 2:13)


 Yakobo 2:13 Maana hukumu haina huruma kwake yeye asiyeona huruma. Huruma hujitukuza juu ya hukumu.

JIBU: Ukianzia kusoma tokea ule  mistari wa kwanza utaona Yakobo, anajaribu kulionya kanisa juu ya Upendo, yaani kufanya mambo bila upendeleo, akatolea mfano wa waaminio wawili, mmoja Tajiri mwingine maskini, halafu, ikatokea kanisa limstahi yule Tajiri kwa kumpa heshima kubwa ya viti vya mbele, na yule maskini likamweka sehemu mbaya, Yakobo anahoji anasema; Kanisa halioni kama litakuwa linahukumu vibaya?

Ndipo hapo sasa akaja kusema mbeleni, kuwa hukumu huwa haina huruma kwake yeye asiye na huruma.. Ikiwa na maana kuwa, mfano wewe ukampiga mwenzako mpaka akafa bila kumuhurumia, usitegemee kuwa sheria itakusamehe kwa kosa hilo?  Haiwezi kukuhurumia, hata kama utaomba msamaha vipi, kinyume chake ni lazima itakuwajibisha kulingana na kosa ulilolifanya..

Vivyo hivyo, mbele za Mungu, ikiwa hatutawahurumia wengine naye Mungu hatatuhurumia sisi, ikiwa tutawependelea wengine naye Mungu atawapendelea wengine badala yetu sisi siku ile itakapofika..

Bwana Yesu alisema katika

Luka 6:36 “Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma.

37 Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa.

38 Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa”.

Unaona,  tukiwa na huruma, maana yake ni kuwa hukumu haiwezi kuwa na nguvu juu yetu. Ndipo linapotimia hili neno “Huruma hujitukuza juu ya hukumu”.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

BASI, IWENI NA HURUMA, KAMA BABA YENU ALIVYO NA HURUMA

Biblia inamaanisha nini inaposema “Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake”?

Kwanini Paulo, alihukumu wakati hukumu hairuhusiwi?

NINI KINATOKEA BAADA YA KIFO?

Rudi nyumbani

Print this post

MWANAMKE, BINTI, MAMA.( Sehemu ya 1)

Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo, karibu katika sehemu ya kwanza ya  mfululizo wa masomo ya wanawake.

Yapo masomo mengine kwa wanawake yameshapita nyuma , ikiwa yalikupita na utapenda kuyapata, basi utanitumia msg inbox nikutume.

Lakini leo tutatazama, namna ambavyo Bwana Yesu alivyowatambua wanawake aliokutana nao, katika kipindi chote cha huduma yake alipokuwa hapa duniani.

  • Kuna wakati alipokutana na mwanamke Fulani, alimtambua kama BINTI
  • Kuna wakati tena alipokutana na mwanamke Fulani, alimtambua kama MAMA
  • Na kuna wakati pia alipokutana na mwanamke Fulani alimtambua kama MWANAMKE.

Haya ni mambo ambayo unapaswa uyaelewe, na kuyazingatia sana unaposoma biblia. Kwasababu kila utambulisho ulibeba ujumbe maalumu kwa kundi husika.

1) Leo tutaangazia Utambulisho wa kwanza wa Bwana ambao ni  MWANAMKE.

Unajua mpaka mtu akuite “mwanamke” ni wazi kuwa halengi kitu kingine Zaidi ya “jinsia” yako, halengi umri wako, au ukubwa wako, au umbo lako, hapana bali jinsia. Ndicho alichokifanya Bwana Yesu alikupokutana na baadhi ya wanawake, hakuwa na nia ya kuwaita kwa vyeo vyao au kwa  mionekano yao labda ni wadogo au wakubwa, au wazee au vijana hapana bali aliwaita “mwanamke” kulenga jinsia yao Zaidi..

Kufunua kuwa, ujumbe ulio nyuma yake, ni mahususi kwa watu wa jinsi hiyo. Hivyo, embu tusome kwa pamoja habari ya yule mwanamke aliyekuwa na dhambi nyingi, tuone ni nini alikifanya mpaka ikampelekea Bwana Yesu kumtambua kama mwanamke na sio, kitu kingine..

Tusome..

Luka 7:37 “Na tazama, mwanamke mmoja wa mji ule, aliyekuwa mwenye dhambi, alipopata habari ya kuwa ameketi chakulani katika nyumba ya yule Farisayo, alileta chupa ya marimari yenye marhamu.

38 Akasimama nyuma karibu na miguu yake, akilia, akaanza kumdondoshea miguu machozi yake, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake, akiibusu-busu miguu yake na kuipaka yale marhamu.

39 Basi, yule Farisayo aliyemwalika alipoona vile, alisema moyoni mwake, Mtu huyu kama angekuwa nabii, angemtambua mwanamke huyu amgusaye, ni nani, naye ni wa namna gani, ya kwamba ni mwenye dhambi.

40 Yesu akajibu akamwambia, Simoni, nina neno nitakalo kukuambia. Akasema, Mwalimu, nena.

41 Akasema, Mtu mmoja mkopeshaji alikuwa na wadeni wawili; mmoja amwia dinari mia tano, na wa pili hamsini.

42 Nao walipokuwa hawana cha kumlipa, aliwasamehe wote wawili. Katika hao wawili ni yupi atakayempenda zaidi?

43 Simoni akajibu akasema, Nadhani ni yule ambaye alimsamehe nyingi. Akamwambia, Umeamua haki.

44 Akamgeukia yule mwanamke, akamwambia Simoni, Wamwona mwanamke huyu? Niliingia nyumbani kwako, hukunipa maji kwa miguu yangu; bali huyu amenidondoshea machozi miguu yangu, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake.

45 Wewe hukunibusu; lakini huyu tangu nilipoingia hakuacha kunibusu sana miguu yangu.

46 Hukunipaka kichwa changu mafuta; bali huyu amenipaka miguu yangu marhamu.

47 Kwa ajili ya hayo nakuambia, Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana; lakini asamehewaye kidogo, huyo hupenda kidogo.

48 KISHA ALIMWAMBIA MWANAMKE, UMESAMEHEWA DHAMBI ZAKO”.

Unapoitafakari habari hiyo unaona nini kwa huyu mwanamke aliyekuwa gwiji wa dhambi, aliyefahamika mji mzima..? Utagundua kuwa Toba au kibali chake hakikuja katika maneno yoyote? Bali katika vitendo ambavyo Bwana Yesu aliona hata wakuu wa dini waliomwalika karamuni, hawakuvitenda.

Mwanamke huyu alitoa mafuta yake yenye thamani nyingi sana, akaanza kuusafisha mwili wa Kristo, ambao aliouna umechafuka sana, alianza kujitoa bila kujali ni nini anapoteza, na kikubwa Zaidi akatumia na nywele zake za thamani, jambo ambalo si la kawaida kwa wanawake wa kidunia wapendao urembo kufanya, kama tu mvua ikimdondokea atatafuta kibanda ajifiche ili tu nywele zake zisiharibike, sembuse kupangusa miguu michafu kwa nywele zake?

Lakini huyu mwanamke alikuwa radhi kufanya hivyo..Na kwa kitendo kile, moyo wa Bwana uliguswa sana, hadi kumsamehe dhambi zake, japokuwa hakutoa Neno lolote kinywani mwake…akasema “mwanamke” umesamehewa dhambi zako.

Na wewe kama mwanamke kabla hujafikiria kujifunza kwa akini Petro, embu chukua muda kwanza, ujifunze kwa wanawake kama hawa, ambao mpaka sasa tunasoma habari zao, ambao Bwana Yesu aliwaona wanathamani kubwa kuliko hata yule Farisayo tajiri (Simoni), aliyemwalika nyumbani kwake, kula chakula..

Mwanamke Ikiwa utatamani, Kristo akusamehe, au akupe kibali, au akufungue, au akuponye,  Maisha yako. Basi Jibidiishe, kuusafisha mwili wa Kristo, kwa kumaanisha kweli, kweli. Tukisema mwili wa Kristo, tunamaanisha, Kanisa lake, na kazi yake. Jitoe kwa hali na mali zako. Hata kama huna chochote, kapige deki, kasafishe hiki au kile.. Lakini usiwe mwombaji tu wa maneno.

Hichi ndicho Bwana alichokiona wa wanadamu wa jinsia hii, (wanawake). Kumjali Kristo ni sehemu ya wito wao hapa duniani, na unathamani kubwa kama tu karama nyingine za kitume zilivyo mbele ya Kristo.

Muhudumie Bwana mwanamke..

Luka 8:2 “na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba,

3 na Yoana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao”.

Bwana akubariki.

Maran atha

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Mwendelezo wa sehemu ya pili unakuja…ambapo tutaona kwanini Bwana aliwatambua baadhi ya wanawake na kuwaita binti zake, na sio, kwa vyeo vyao au ukubwa wao..

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

Print this post

Ni mlima gani Yule Mwanamke Msamaria aliokuwa anaumaanisha? (Yohana 4:19)

Jibu: Tusome,

Yohana 4:19 “Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii!

20 BABA ZETU WALIABUDU KATIKA MLIMA HUU, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia”.

Mlima Mwanamke Msamaria aliokuwa anaumaanisha ni MLIMA GERIZIMU.

Katika Mji wa Samaria kulikuwa na milima mikuu miwili mikubwa iliyokuwa inaangaliana, ambapo katikati ya milima hiyo kulikuwa na bonde.. Na milima hiyo ndio Mlima Gerizimu, na Mlima Ebali.

Mwanzo wa milima hii kutajwa katika biblia, ilikuwa ni kipindi wana wa Israeli wanatoka Misri kuelekea Kaanani, ambapo Mungu alimpa Musa maagizo na kumwambia atakapovuka mto Yordani, Nusu ya kabila ya Israeli (Yaani kabila 6) wapande juu ya mlima Gerizimu, kwaajili ya kuitikia Baraka na nusu nyingine iliyobakia (yaani kabila 6), zipande juu ya mlima Ebali kwaajili ya kuitikia laana.

Na katikati ya milima hiyo miwili, (yaani katika lile bonde lililokuwepo katikati) makuhali walisimama na kusoma Baraka na Laana kama zilivyoandikwa katika Torati ya Musa.. Ziliposomwa laana wale waliokuwa juu ya Mlima Ebali waliitika kwa sauti, AMEN!.. Na ziliposomwa baraka wale waliokuwa juu ya mlima Gerizimu waliitika AMEN kwa sauti!

Kumbukumbu 27:11 “Musa akawaagiza wale watu siku iyo hiyo, akasema,

12 Hawa na wasimame juu ya MLIMA WA GERIZIMU kwa kuwabarikia watu, mkiisha vuka Yordani; Simeoni, na Lawi, na Yuda, na Isakari, na Yusufu, na Benyamini;

13 na hawa na wasimame juu ya mlima wa Ebali kwa laana; Reubeni, na Gadi, na Asheri, na Zabuloni, na Dani, na Naftali.

14 Kisha Walawi na wajibu, wawaambie watu wote wa Israeli kwa sauti kuu,

15 Na alaaniwe mtu afanyaye sanamu ya kuchonga, au ya kusubu, machukizo kwa Bwana, kazi ya mikono ya fundi, akaisimamisha kwa siri. Na watu wote wajibu, waseme, Amina.

16 Na alaaniwe amdharauye baba yake au mama yake. Na watu wote waseme, Amina.

17 Na alaaniwe aondoaye mpaka wa jirani yake. Na watu wote waseme, Amina”.

Unaweza kulisoma jambo hilo hilo tena katika kile kitabu cha Yoshua 8:33-34

Hivyo mlima Gerizimu, ukajulikana na Wasamaria kama mlima wa Baraka, na Ebali Mlima wa laana.

Kumbukumbu 11: 29 “Tena itakuwa, atakapokuleta Bwana, Mungu wako, na kukutia katika nchi uendeayo kuimiliki, ndipo uiweke baraka juu ya mlima wa Gerizimu, na laana uiweke juu ya mlima wa Ebali”.

Kwa maelezo marefu kuhusu milima hii na ujumbe iliyoubeba katika roho unaweza kufungua hapa >>> MLIMA GERIZIMU NA EBALI

Kwahiyo Wasamaria wakaamini huo mlima GERIZIMU ndio MLIMA WA MUNGU, ambao Bwana ataliweka jina lake, jambo ambalo linapishana na Imani ya kiyahudi, inayoamini kuwa mlima wa Bwana ni MLIMA MORIA ulipo Yerusalemu, mahali pale Ibrahimu alipotaka kumtoa sadaka mwanawe, na ndipo Mfalme Daudi alipomwona Yule malaika wa uharibifu, na ndipo ambapo mwanae Sulemani alikuja kutengeneza Hekalu la Mungu.

Kwahiyo huyu mwanamke Msamaria alipokutana na Bwana Yesu kisimani, alijaribu kumweleza kuwa wao (yaani Bwana Yesu na wayahudi wengine) wanaamini kuwa sehemu ya kuabudia ni katika ule mlima Moria kule Yerusalemu, pale palipojengwa hekalu… Na wakati wao Wasamaria wanaamini ni katika mlima Gerizimu ambapo Mungu alipaagiza kuwa watu Wabarikiwe.

Lakini katika hayo yote tunaona jibu la Bwana Yesu lilikuwaje..

Yohana 4:20 “Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia.

21 Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo HAMTAMWABUDU BABA KATIKA MLIMA HUU, WALA KULE YERUSALEMU.

22 Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi.

23 LAKINI SAA INAKUJA, NAYO SASA IPO, AMBAYO WAABUDUO HALISI WATAMWABUDU BABA KATIKA ROHO NA KWELI. KWA MAANA BABA AWATAFUTA WATU KAMA HAO WAMWABUDU”.

Ikimaanisha kuwa Mungu haabudiwi tena katika vilele vya milima ya damu na nyama.. bali katika vilele vya milima ya Roho zetu.

Tunapomwamini Yesu, na kujazwa Roho wake Mtakatifu.. na kuifahamu kweli hiyo..Basi tunapokwenda kumfanyia Mungu ibada, tunakuwa tunamwabudu katika Roho na Kweli.

Je na wewe leo unamwabudu Baba katika roho na kweli?.. au katika Uzuri wa Kanisa lako na Mapokeo yako?.. au katika dini yako na dhehebu lako?..

Kumbuka maandiko yanasema wale wote wasio na Roho wake hao sio wake (Warumi 8:9), na hakusema wale wote wasio na dhehebu, au dini ndio sio wake..

Swali ni je!, unaye umempata huyo Roho?..Kama bado basi ni rahisi sana kumpata kama unamhitaji katika maisha yako, kwasababu yeye ndio muhuri wa Mungu kwetu.

Matendo 2:37 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?

38 Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.

39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.

40 Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi”.

Marana atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Mlima Gerizimu na Ebali ni ipi, na umuhimu wao rohoni ni upi?

Wasamaria walikuwa ni watu gani?

KATIKA MLIMA WA BWANA ITAPATIKANA.

Mahali pa juu palikuwa ni wapi kama tunavyosoma katika biblia?

Rudi nyumbani

Print this post

IIGE RATIBA YA MUNGU YA WIKI IKUSAIDIE

Nakusalimu katika jina kuu sana la Bwana wetu Yesu Kristo, karibu tujifunze maneno ya uzima.

Tunaposoma kile kitabu cha Mwanzo sura ya kwanza , wengi wetu tunachokiona pale ni tendo la uumbaji tu lakini hatuoni mikakati na ratiba alizojipangia Mungu ili kuukamilisha huo mpango wake mzima wa uumbaji.

Walimwengu wanasema, mtu mwenye akili huwa anajifunza kwa waliofanikiwa.. Sasa sisi wanadamu hatuna aliyefanikiwa Zaidi ya Mungu wetu si ndio?. Tunapoziangalia mbingu na nchi tunachokiona ni kazi stadi iliyobuniwa kwa  umakini  sana isiyokuwa na mapungufu au madhaifu yoyote, hivyo na sisi pia kama tunataka tuwe na mafanikio makubwa hatuna budi kujifunza ratiba ya Mungu jinsi alivyoweza kupangilia mambo yake. Mpaka tukakiona hichi tunachokiona sasa hivi.

Sasa katika zile siku 7 za uumbaji, Mungu alizigawanya shughuli zake katika vipengele vikuu vitatu.

Kipengele cha kwanza: Alijikita katika kufanya kazi ya utenganisho

Kipengele cha pili :Kilikuwa ni uumbaji

Na kipengele cha  tatu: Kupumzika.

Tukianza na kipengele cha Kwanza: Kufanya utenganisho.

Ukisoma Mwanzo 1:2 Utaona utenganisho wa kwanza alioufanya Mungu katika siku ya kwanza ulikuwa ni kati ya Nuru na giza.

Mwanzo 1:3 Mungu akasema, Iwe nuru; ikawa nuru.

4 Mungu akaiona nuru, ya kuwa ni njema; Mungu akatenga nuru na giza.

Siku ya pili tena akaendelea na kazi hiyo hiyo.. akayatenga maji ya juu ya chini, na ya chini ya nchi kwa kuweka kitu kinachoitwa anga katikati..

Mwanzo 1:7 Mungu akalifanya anga, akayatenga yale maji yaliyo juu ya anga na yale maji yaliyo chini ya anga; ikawa hivyo.

8 Mungu akaliita lile anga Mbingu. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya pili.

Unaona Kama hiyo haitoshi, bado aliendelea hadi siku ya tatu kufanya matenganisho, kati ya maji na ardhi, ili nchi kavi ionekane

Mwanzo1:9 Mungu akasema, Maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, ili pakavu paonekane; ikawa hivyo.

10 Mungu akapaita pale pakavu Nchi; na makusanyiko ya maji akayaita Bahari; Mungu akaona ya kuwa ni vyema.

Na Siku ya Nne pia, akatenganisha, siku na siku, na mwezi na mwezi, na mwaka na mwaka,..kwa kuumba jua na mwezi na nyota..

Soma Mwanzo 1:16-19 utalithibitisha hilo

Sasa mpaka anafikia siku ya nne, alikuwa bado hajaumba mnyama yoyote, ni kazi tu ya utenganisho tukiachilia mbali mimea ambayo iliumbwa siku ya tatu..

Mungu kuanzana na utenganisho ni kutufundisha nini?

Hii ni kutufundisha kuwa, hatupaswi kukimbilia kufanya jambo lolote,kwanza  kama kuna mambo ambayo bado hayajatenganishwa na sisi rohoni. Tutumie nguvu kubwa kutenganisha nuru na giza kwenye wiki yetu, ..Usianze tu wiki yako hivi hivi, bila kuiambia kwanza iwe nuru kwako,kwa kwenda ibadani nyumbani kwa Bwana usianze wiki bila kuomba, hakikisha unayatenga mambo maovu mbali na wewe kwa kadiri uwezavyo. Ndicho Mungu alichokuwa anakifanya katika siku za mwanzo.

Kama kuna mtu umemdhulumu mlipe..kama una madeni ya watu yasawazishe..kama kuna dhambi ulitenda ziungame mbele za Bwana.

Kipengele cha  Pili: Ni uumbaji,

baada ya pale ndipo utaona Mungu anaanza kuumba, samaki , na wanyama wa kila namna wa mwituni na wa kufungwa pamoja na ndege wote angani..na mwisho kabisa akamwuumba na mwanadamu, katika siku ile ya sita.

Hii ni kutufundisha kuwa, mara baada ya kutenganisha mambo yasiyofaa mbali nasi ndipo hapo sasa tuwe na uhakika kuwa kila tunachotia mkono kukifanya, kitakuwa ni chema sana.. Kisichokuwa na mapungufu au kasoro..Kama Mungu alivyoona jinsi uumbaji wake ulivyokuwa vema sana usio na mapungufu yoyote.

Mwanzo 1:31 Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita.

Kipengele cha Tatu: Kupumzika.

Sasa alipomaliza kazi yake yote, kwa siku 6, akaona ni vema atenge siku moja apumzike. Akatenga muda wa saa 24 wa kutofanya kazi yoyote.

Hii ni kutufundisha pia, kuwa sisi tusijifanye tupo buzy sana kuliko Mungu, ikiwa yeye alipumzika, wewe ni nani usipumzike? Kama unatenda kazi kama mashine wiki nzima, usiku na mchana huna muda wa kupumzika, wiki nenda wiki rudi, miaka nenda miaka rudi.. Tambua kuwa hata hicho unachokifanya hakiwezi kuwa na ubora wowote. Hivyo na wewe ukienenda kwa ratiba kama hii ya Mungu katika wiki yako, jiandae kukutana na matokeo chanya katika mambo yako yote unayoyasumbukia. Uwe ni mtumishi wa Mungu katika huduma yako, au mwanafunzi, au mfanyakazi, au kiongozi, ijaribu ratiba hii ya Mungu uone.Lakini kama wewe  ibada si kitu cha muhimu kwako, unachowaza siku zote ni kazi tu, hujitenganishi, na kazi haramu, au marafiki wabaya, au mazungumzo mabaya, hujitengi na dhambi, huna muda na kuomba, au kujifunza Neno la Mungu, au kujirekebisha, unachowaza ni pesa tu ujue kuwa wiki yako, na masumbuko yako ni hasara tu. Kwasababu unapanda katika giza..unaumba katika maji..mahangaiko yako uwe na uhakika yatakuwa ni bure tu..

Kumbuka tunapoizungumzika ratiba hii ya Mungu, haimaanisha na wewe uifuate hivyo hivyo kwamba siku ya 1-4 ufanye hivi au vile, hapana, bali, walau katika wiki yako nzima, uhakikishe kila kipengele umekigusua, kwa muda unaolingana na huo Mungu alioutumia. Kama ni kupumzika, unaweza usiwe na saa 24 mfululizo, lakini hakikisha walau kwa wiki hukosi hizo saa 24 za kupumzika, vivyo hivyo na hayo mengine yote.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

MWANZO WA INJILI YA YESU KRISTO.

NAMNA YA KUITAMBUA SAUTI YA MUNGU INAPOZUNGUMZA NA WEWE

AHADI YA ROHO ILIYOSALIA SASA KWA KIPINDI CHETU.

JE UNAIFANYA KAZI YA MUNGU?

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 1

Rudi nyumbani

Print this post

Wasamaria walikuwa ni watu gani?

Baada ya Israeli kuondolewa na Waashuru kutoka katika nchi yao, Mfalme wa Ashuru aliwaleta watu wengine, wakakae katika nchi hiyo,waliyoondolewa.. ili kwamba nchi hiyo , isibakie mapori.

Watu hao walioletwa kukaa katika nchi ya Israeli, hawakuwa Wayahudi bali walikuwa ni wapagani, wanaoabudu miungu yao.
Na walipoletwa walienda kukaa mahali pajulikanapo kama Samaria, huku wakiwa bado na miungu yao.

Lakini maandiko yanasema walipofika katika nchi takatifu, walisumbuliwa sana na simba (simba walikuwa wanaua watu sana).

Mpaka Mfalme wa Ashuru alipotuma kuhani mmoja wa kiyahudi kwenda kuwafundisha desturi za hiyo nchi..kwamba ni nchi takatifu hivyo hawana budi kuishi kulingana na kanuni za Mungu wa Israeli na si kulingana na kanuni za miungu yao.
Hivyo walupopelekewa Kuhani walivipokea vitabu vitano tu vya Musa, pamoja na kitabu cha Yoshua, lakini vitabu vingine vilivyosalia vya manabii hawakuviamini wala kuvipokea.

Hivyo wakawa ni jamii ya watu wanaozishika sheria za Mungu wa Israeli nusu..na nusu wanaitumikia miungu yao.

2 Wafalme 17:24
“Naye mfalme wa Ashuru akaleta watu kutoka Babeli, na Kutha, na Ava, na Hamathi, na Sefarvaimu, akawaweka katika miji ya Samaria badala ya wana wa Israeli; wakaumiliki Samaria, wakakaa katika miji yake.

25 Basi ikawa, wakati ule walipoanza kukaa huko, hawakumcha BWANA; kwa hiyo BWANA akapeleka simba kati yao, nao wakawaua baadhi yao.

26 Kwa hiyo wakamwambia mfalme wa Ashuru, wakasema, Wale wa mataifa uliowahamisha, na kuwaweka katika MIJI YA SAMARIA, hawaijui kawaida ya Mungu wa nchi; kwa hiyo amepeleka simba kati yao, na tazama, wanawaua, kwa sababu hawaijui kawaida ya Mungu wa nchi.

27 Ndipo mfalme wa Ashuru akatoa amri, akasema, Mpelekeni mmojawapo wa makuhani, mliowachukua kutoka huko; aende akakae huko, akawafundishe kawaida ya Mungu wa nchi.

28 Basi mmoja wa makuhani waliochukuliwa kutoka Samaria akaenda akakaa katika Betheli, akawafundisha jinsi ilivyowapasa kumcha BWANA.

29 Lakini pamoja na hayo watu wa kila taifa wakajifanyia miungu yao wenyewe, wakaiweka katika nyumba za mahali pa juu, walipopafanya Wasamaria, kila taifa katika miji yao walimokaa.

30 Watu wa Babeli wakafanya Sukoth-benothi kuwa mungu wao, watu wa Kutha wakafanya Nergali, watu wa Hamathi wakafanya Ashima,

31 Waavi wakafanya Nibhazi na Tartaki; nao Wasefarvi wakawaunguza wana wao katika moto kwa Adrameleki na Anameleki, miungu ya Sefarvaimu.

32 Basi hivyo wakamcha BWANA, nao wakijifanyia wengine wao kuwa makuhani wa mahali pa juu, ambao waliwafanyia dhabihu katika nyumba za mahali pa juu.

33 WAKAMCHA BWANA, NA KUITUMIKIA miungu YAO WENYEWE, sawasawa na kawaida za mataifa ambao wao walihamishwa kutoka kwao.

34 Hata siku hii ya leo hufanya sawasawa na kawaida za kwanza; wala hawamwogopi BWANA, wala hawazifuati sheria zao, wala hukumu zao, wala ile torati, wala ile amri BWANA aliyowaamuru wana wa Yakobo, ambaye alimpa jina la Israeli”

Umeona hapo, mstari wa 33..maandiko yanasema wakamca Bwana na kuitumikia miungu yao wenyewe..

Yaani walifanya mambo mawili kwa wakati mmoja..

Kwa tabia hiyo basi wayahudi ambao walikuwa wanaishika sheria ya Mungu wa Israeli kwa ukamilifu wote,..wakawa hawachangamani na hawa Wasamaria.

Mpaka wakati wa kuja kwa Bwana, Wayahudi walikuwa bado hawachangamani na Wasamaria (Yohana 4:9).

Lakini Bwana Yesu alipokuja, alikiondoa hicho kiambaza cha kati,

Hata mahali pa kuabudia pakawa si tena Yerusalemu katika mlima Moria (katika hekalu la Sulemani) wala si Samaria katika mlima Gerizimu, ambao Wasamaria ndio waliamini mahali oanapowapasa wao kuabudia..bali pakawa ni KATIKA ROHO NA KWELI.. Hapo ndipo mlimani pa Bwana alipopachagua.

Yohana 4:21 “Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu.

22 Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi.

23 Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, AMBAYO WAABUDUO HALISI WATAMWABUDU BABA KATIKA ROHO NA KWELI. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu”.

Je na wewe leo unamwabudu Baba katika Roho na Kweli? Yaani katika Roho Mtakatifu na katika Neno lake?

Kama bado mpokee leo Kristo, na ukabatizwe ubatizo sahihi wa maji mengi na kwa jina la Yesu, upate ondoleo la dhambi na upokee kipawa cha Roho Mtakatifu.

Maran atha!.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

MSAMARIA MWEMA.

BASI, IWENI NA HURUMA, KAMA BABA YENU ALIVYO NA HURUMA

OLE WAKO KORAZINI NA BETHSAIDA.

NI NINI KITAKACHOTUFANYA TUPIGE MBIO BILA KUPUNGUZA MWENDO?

Mlima Gerizimu na Ebali ni ipi, na umuhimu wao rohoni ni upi?

Rudi nyumbani

Print this post