NI NINI KITAKACHOTUFANYA TUPIGE MBIO BILA KUPUNGUZA MWENDO?

NI NINI KITAKACHOTUFANYA TUPIGE MBIO BILA KUPUNGUZA MWENDO?

Paulo akijua kuwa anakaribia ukingoni kabisa mwa safari yake, hakujali taarifa yoyote mbaya iliyoletwa mbele yake, utaona yeye mwenyewe anasema, mji kwa mji Roho Mtakatifu alimshuhudia kuwa vifungo na dhiki nyingi vinamngojea kule Yerusalemu alipokusudia kwenda, lakini bado alisema, siachi kupiga mbio nimalize mwendo wangu.

Matendo20:23 “isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja.

24 Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu”.

Kama hilo halitoshi alipofika Kaisaria, karibu kidogo na Yerusalemu, Nabii mmoja aliyeitwa Agabo, alitokea na kumtolea unabii kwa uweza wa Roho Mtakatifu akisema, Paulo atakwenda kufungwa, na kupata dhiki, hivyo asiende, Yerusalemu.

Lakini hilo nalo halikumfanya Paulo, aache kwenda Yerusalemu, badala yake aliwaambia;

Matendo 21:13 “Ndipo Paulo alipojibu, Mnafanya nini, kulia na kunivunja moyo? Kwa maana mimi, licha ya kufungwa, ni tayari hata kuuawa katika Yerusalemu kwa ajili ya jina lake Bwana Yesu”.

Unaona, alifikia hatua, mawazo yake yote yalikuwa  ni kuimalizia kazi yake kwa kishindo, kiasi cha kutojali dhiki zozote atakazokumbana nazo mbele yake

Sasa usifikirie ni jambo rahisi kuchukua maamuzi hayo kama asingekuwa ni mtu anayefahamu ni nini anakitafuta.. Paulo alikuwa ni mtu mwenye malengo, ni mtu aliyekuwa anatazama vya mbali sana, alijua kupiga mbio huko kuna tuzo Fulani kubwa mbeleni, hivyo ni sharti aishindanie kwa nguvu ili asiikose.

1Wakorintho 9:24 “Je! Hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate.
25 Na kila ashindanaye katika michezo hujizuia katika yote; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo; bali sisi tupokee taji isiyoharibika.
26 Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; napigana ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa;
27 bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa”

Unaona alijua sikuzote mkimbiaji ambaye anajua lengo la kukimbia kwake ni nini huwa hakimbii kwa kuubembeleza mwili, bali anakimbia huku mawazo yake yakuwa kweney tuzo iliyowekwa mbele yake, hilo ndilo linalomfanya asitembee tembee njiani, asikubali kuusikiliza mwili, kwamba umechoka, hivyo apunguze mwendo.

Hali kadhalika mkimbiaji mzuri kwa namna ya kawaida, anapokaribia mzunguko wake wa mwisho ndio huwa anaongeza mwendo Zaidi, na ndicho alichokifanya Paulo.

Embu tumtazame mtu mwingine wa mwisho ambaye safari yake sikuzote ilikuwa ni ya mwendo tu, mtu ambaye yeye hakujali kikwazo chochote alipokuwa anamalizia mwendo wake hapa duniani. Na huyo si mwingine Zaidi ya Bwana wetu Yesu Kristo.

Biblia inatuambia wakati wa kupaa kwake ulipokaribia, “ALIUKAZA” uso wake kwenda Yerusalemu.

Luka 9:51 “Ikawa, siku za kupaa kwake zilipokuwa karibu kutimia, yeye aliukaza uso wake kwenda Yerusalemu;
52 akatuma wajumbe kutangulia mbele ya uso wake; wakaenda wakaingia katika kijiji cha Wasamaria, ili kumtengenezea mahali.
53 Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu”.

Kuukaza uso maana yake, ni kutokuwa tayari kuambiwa chochote, au kushauriwa chochote au kukwamishwa na chochote mpaka utimize malengo yako uliyoyakusudia mbele yako. Ndivyo ilivyokuwa kwa Bwana Yesu, wakati ambapo anajua amebakiwa na kipindi kifupi sana, amalize mwendo wake pale Yerusalemu, huku akijua moyoni mwake kuwa Mateso makali anakwenda kukumbana nayo, kusulibiwa, yeye hakujali chochote, Zaidi ndio alilazimisha kwenda huko huko.

Yohana 10:7 Kisha, baada ya hayo, akawaambia wanafunzi wake, Twendeni Uyahudi tena.
8 Wale wanafunzi wakamwambia, Rabi, juzijuzi tu Wayahudi walikuwa wakitafuta kukupiga kwa mawe, nawe unakwenda huko tena?

Je na sisi kipindi hichi cha kufunga majira, bado tunapiga mbio au tumepunguza mwendo wetu wa Imani ? Pengine tumeacha kukimbia kwasababu hatujajua malengo yetu ni nini? tunakumbana na milima mrefu, tunakata tamaa, lakini pia tunapaswa tujue jambo moja ili uitwe mlima ni lazima utakuwa na upande wa pili wa mteremko pia.

Ni heri maisha mafupi ya hapo duniani, tuyaishie kupanda mlima, lakini tutakapofika kule ng’ambo kwenye umilele tuyaishie kwenye mteremko,..

Hizi ndizo nyakati za kuzidisha mwendo, kutojali vitisho vyovyote vya kiimani, vitisho  vya ndugu, au rafiki, au majirani, kwasababu kama unyakuo hautatukuta, basi pia siku zetu za kuishi duniani zinapungua siku baada ya siku.

Hivyo tupige mbio tukijua kuwa zipo tuzo mbele yetu zinatungojea, lakini tukiwa walegevu hatutazipata.

2Timotheo 2:5 “Hata mtu akishindana katika machezo hapewi taji, asiposhindana kwa halali”.

Shalom

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

DAMU YA ZAKARI BIN BARAKIA.

HEKIMA YA KIMUNGU, INAINGIAJE MIOYONI MWETU?

NITAFANYA YERUSALEMU KUWA JIWE LA KUWALEMEA .

JINSI PAULO ALIVYOPAMBANA NA UJINGA WA ROHONI.

Nini maana ya neno ‘Kuabiri’ kama linavyotumika katika  biblia?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments