ELIMA MCHAWI, ANAFANYA KAZI HADI SASA.

ELIMA MCHAWI, ANAFANYA KAZI HADI SASA.

Sikuzote roho haiji hivi hivi tu, bila kuwa na chanzo Fulani, na chanzo hicho kinaweza kuwa mtu, au kitu au sehemu, Sasa pale yule mtu anapoondoka, huwa anaacha tabia yake Fulani inayoendelea na tabia hiyo ikishakita mizizi vizuri ndio inaitwa roho,..

Kwamfano kwenye biblia utamwona mwanamke anaitwa Yezebeli, huyu mwanamke alikuwa ni mchawi, na mzinzi, na tabia zake tunazijua vizuri kwenye biblia, jinsi alivyoiharibu Israeli na kuigeuzwa kuwa nchi ya kichawi. Lakini tunasoma mara baada ya kufa kwake, roho yake iliendelea kutembea duniani, na ndio maana miaka mingi baadaye utaona Bwana Yesu anamzungumzia tena habari zake kana kwamba bado yupo duniani, katika kitabu cha Ufunuo,

Ufunuo 2:19 “Nayajua matendo yako na upendo na imani na huduma na subira yako; tena kwamba matendo yako ya mwisho yamezidi yale ya kwanza.
20 Lakini nina neno juu yako, ya kwamba wamridhia yule mwanamke Yezebeli, yeye ajiitaye nabii na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ili wazini na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu”

Utamwona pia Eliya, pindi alipoondoka roho yake ilianza kutembea tena wakati baada ya wakati, Kumbuka hawi Eliya mwenyewe kama Eliya, Au Yezebeli kama Yezebeli, bali ile tabia  ya rohoni iliyokuwa juu ya Eliya, ndiyo inayotembea juu ya watu kadha wa kadha, Roho hiyo ilikuja juu ya Elisha, baadaye Yohana Mbatizaji n.k. na itaendelea kutembea hadi wakati wa nyakati za mwisho kabisa.(Malaki 4:5)

Halikadhali Na Bwana wetu Yesu Kristo, yeye alitembea hapa duniani, kwa miaka 33 na nusu, lakini alipoondoka, hakuondoka hivi hii ilikuwa ni sharti aichalie Roho yake katikati yetu, na ndio Roho Mtakatifu tuliye naye sasa. Kiasi kwamba mtu akiyaamini maneno yote ya Bwana Yesu moja kwa moja anampokea Roho wake ambaye atamsaidia aisha maisha kama ya Yesu.

Sasa tukishaweka msingi kama huo, tuende moja kwa moja katika somo letu la leo ambalo linamzungumzia yule Elima mchawi aliyekutana na Paulo na Barnaba  pindi walipokuwa wanahubiri injili huko Pafo, tusome.

Matendo 13:6 “Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake Bar-Yesu;
7 mtu huyu alikuwa pamoja na liwali Sergio Paulo, mtu mwenye akili. Yeye liwali akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno la Mungu.
8 Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani.
9 Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho,
10 akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka?
11 Basi, angalia, mkono wa Bwana u juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza, akazunguka-zunguka na kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza.
12 Ndipo yule liwali, alipoyaona yaliyotendeka, akaamini, akiyastaajabia mafundisho ya Bwana”`.

Huyu mtu alikuwa ni mchawi, na wakati huo huo ni nabii wa Uongo. Kazi yake na lengo lake, lilikuwa ni kuwafanya watu wasiiamini njia ya wokovu, pale tu wanapokutana na injili ya kweli ya msalaba. Ni mchawi aliyebobea kwenye kitendo cha kupinga tu, na kushawishi watu kuiacha imani, na ndio maana mtume Paulo alimwambia “Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka?”

Kwa kazi yake hii, mpaka akawa ameshawafikia kabisa na watu wakubwa na wenye akili kama huyu Sergio Paulo, ikiwa na maana kuwa  huku chini tayari alishaburuza.

Kama tunavyoona hapo, Paulo alipoanza kumuhubiria huyu liwali, yeye bila kupoteza muda alianza kuwabishia wakina Paulo, na kutoa hoja zake za uongo, na pengine kumwambia yule liwali hawa watu ni waongo, wapiga dili, hakuna kitu kuokoka hapa duniani, huyo Yesu aliibiwa hajafufuka, hawa ni wapotoshaji n.k.

Lakini Paulo kulijua hilo, akamkemea saa ile ile akawa kipofu kwa muda.

Sasa huyu mtu alishakufa lakini aliiacha roho yake hapa duniani, na roho hiyo inatembea kwa kasi sana, sasa hivi duniani imewavaa watu wengi, na wenyewe hawajijui kuwa wanafanyika kuwa wachawi, pasipo wao kujijua.

Kuna watu kazi yao ni kupinga tu kila habari ya Kristo, wakiona kila mtumishi wa Mungu anahubiri, au kushuhudia, wanasema ni nabii wa uongo, wanasema ni wazinzi, wakisikia injili ya kweli inahubiriwa wanasema anapotosha,

Sasa kibiblia watu kama hao ni wachawi, hawajijui tu kama wameshafikia hiyo hatua

Katika nyakati hizi za kumalizia ni kujiangalia sana, si kila wazo la kila mtu la kulisikiliza, au kulipokea haijalishi atakuwa ni ndugu yako, au rafiki yako, au mfanyakazi mwenzako. 

Bwana Yesu alisema, angalieni jinsi msikiavyo (Luka 8:18)

Kaa mbali nao, ikiwa unaona kila wakati tu wanakosoa habari za Mungu au watumishi wa Mungu, hakuna kipengele hata kimoja watakisifia, kaa mbali nao, wanakuwekea tu moyo mgumu wa kutokuamini.

Ukikutana na watu kama hao ujue unaongea na wachawi, jiupushe nao. Leo hii duniani utakutana nao wengi sana akina Elimu, Bar Yesu. Wewe jikite katika kumtafuta Muumba wako kwa bidii, mpende Mungu wako, sikiliza na soma Neno la Mungu, achana na hao wanaoipuuzia, au kukejeli kila kitu cha ki Mungu kinachokatiza mbele yao.

Jiepushe nao.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

JINSI PAULO ALIVYOPAMBANA NA UJINGA WA ROHONI.

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

Nini maana ya neno ‘Kuabiri’ kama linavyotumika katika  biblia?

ILI NIWE KIELELEZO KWA WALE WATAKAOMWAMINI BAADAYE.

KUMTUMIKIA MUNGU, KUNAWEZA KUWE KINYUME NA MATARIJIO YAKO.

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments