Category Archive Home

UTOE MWILI WAKO KWA BWANA KWASABABU SI MALI YAKO.

Jambo linalotupa wengi kiburi ni kufikiri kwamba miili hii tuliyonayo ni mali yetu wenyewe..Lakini kama mtu ukitenga muda na kutafakari kwa kina utakuja kugundua kuwa mwili ulionao hauna mamlaka nao asilimia mia, na hivyo huo ni uthibitisho kwamba si mali yako kabisa..

Kama mwili ungekuwa ni mali yako ungekuwa na uwezo wa kujichagulia kimo, au rangi au jinsia…ungekuwa pia na uwezo wa kuyazuia mapigo ya moyo yasidunde pindi unapotaka, au ungekuwa na uwezo wa kuzuia damu isizunguke mwilini au mwili usitoe jasho wakati wa joto linapozidi kuwa kali. Lakini kama mojawapo ya mambo hayo huwezi basi ni uthibitisho kwamba huo mwili ni mali ya mtu mwingine ambaye wewe humjui. Kwa ujumla sio milki yako binafsi…Kama biblia inavyosema..

1Wakorintho 6:19 “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? WALA NINYI SI MALI YENU WENYEWE”

Kwasababu hiyo basi ndio maana ni lazima tuishi chini ya amri za mwenye miili hii…akisema miili hii haipaswi kufanywa kituo cha dhambi..basi tunatii kwasababu sio mali yetu..akisema hatupaswi kuitumia kwa zinaa, au ulevi, au uasherati basi ni lazima tutii kwasababu sio ya kwetu ni yake yeye. Sisi ni wageni waalikwa au wapangaji tu ndani ya hii miili yake..Hatuna uhuru asilimia 100 wa kuiweka tunavyotaka sisi. Akisema hatupaswi kuivisha mavazi yapasayo jinsia nyingine, hatupaswi kuhoji kwanini au kwasababu gani.

Sasa hebu tujifunze Zaidi juu Mmiliki wa hii miili tuliyonayo.

Kuna wakati Bwana wetu Yesu aliulizwa swali lifuatalo na Mafarisayo…

Mathayo 22:17 “Basi utuambie, Waonaje? Ni halali kumpa Kaisari kodi, ama sivyo?

18 Lakini Yesu akaufahamu uovu wao, akasema, Mbona mnanijaribu, enyi wanafiki?

19 Nionyesheni fedha ya kodi. Nao wakamletea dinari.

20 Akawaambia, NI YA NANI SANAMU HII, NA ANWANI HII?

21 Wakamwambia, Ni ya Kaisari. Akawaambia, Basi, mlipeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, NA MUNGU YALIYO YA MUNGU”

Ukisoma mstari huo wa 20 utaona Bwana anawauliza maswali mawili..1).Ni ya nani sanamu hii? Maana yake ile sura juu ya ile sarafu ni sura ya nani?…2).Na ni ya nani anwani hii?. Na wote wakajibu ni ya Kaisari..na yeye Bwana akawaambia vya Kaisari mpeni Kaisari na vya Mungu mpeni Mungu..

Sasa swali linakuja, vya Mungu ni vipi hapo?…Ndio vinaweza kuwa navyo pia ni fedha, (kama sadaka, zaka au malimbuko)..lakini hebu leo tuingie ndani Zaidi kujifunza vilivyo vya Mungu ni vipi.

Turudi kusoma kitabu cha Mwanzo..

Mwanzo 1: 26 “Mungu akasema, Na tumfanye MTU KWA MFANO WETU, KWA SURA YETU; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.

27 Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba”.

Mpaka hapo utakuwa umeona vya Mungu ni vipi?…Miili yetu ndio vya Mungu tunavyopaswa tumpe..kwasababu miili yetu ndio imebeba SURA na MFANO wa Mungu…Kwahiyo kama Bwana alivyowaambia watu wampe kodi Kaisari kwasababu tu sarafu ile imebeba sura yake na anwani yake..zaidi sana tunapaswa tumpe Kristo miili yetu kwasababu imebeba sura na mfano wa Mungu..

Kwahiyo tunapaswa tujipime kila siku je hii miili yetu tunaiweka jinsi Mungu anavyotaka?…Je tunaiweka katika utakatifu, je tunaishughulisha katika kufunga na kuomba na kuifikisha kwenye nyumba za Ibada?..Kama hufanyi hivyo, kila ukifika muda wa kuomba unasema umechoka!..ukifika muda wa kufunga unasema unaumwa, ikifika siku ya kwenda kwenye ibada unasema unapumzika…Kumbuka utatoa hesabu siku ile kwa mwenye huo mwili.

Kama unautumia mwili huo kuufanyia uzinzi, au uasherati…jitafakari sana, kama unafikiri ni mali yako hiyo anza kujitafakari tena upya, kama unafikiri una uhuru wa kuitembeza bila mavazi au kuichubua, au kuiweka kila aina ya matangazo anza kujitafakari tena upya, kama unafikiri ni ya kupokea mimba na kutoa tu jinsi utakavyo hilo nalo lifikirie…

Bwana atusaidie daima..

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

Mungu alikuwa anaongea na nani aliposema na “Tumfanye mtu kwa mfano wetu”,(Mwanzo 1:26)?

JINSI DHAMBI INAVYOMGHARIMU MTU SANA.

CHAPA YA MNYAMA

Maana ya ‘Usimjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake’

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita..

CHUKIZO LA UHARIBIFU

KAMA TUNATAKA KUWA ASKARI WA BWANA, NI LAZIMA TUJUE VIGEZO.

Kwanini kabila la Dani limeondolewa kwenye Ufunuo 7?

Rudi Nyumbani:

Print this post

OLE WAO WANAOJITAHIDI KUMFICHA BWANA MASHAURI YAO.

Jina la Bwana Yesu libarikiwe ndugu yangu..Karibu tuyatafakari kwa pamoja maneno ya uzima,

Biblia inasema..

Isaya 29:15 “Ole wao wanaojitahidi kumficha Bwana mashauri yao, na matendo yao yamo gizani, nao husema, Ni nani atuonaye? Nani atujuaye?.

Mungu hapa anatupa onyo sisi tunaodhani kuwa kwa nguvu zetu wenyewe tunajitosheleza kuyaendesha maisha yetu,..tunasema hakuna haja ya Mungu kuingilia mipango yetu..hatuhitaji kumwomba Mungu, kwani yeye ni nani mbona hatumwoni akituongozea kitu chochote, Sasa ya nini kumuhusisha katika mambo yetu., Tunaweza tusiseme hivyo kwa midomo lakini moyoni mwetu tunawaza hivyo,..

Leo ninataka kwenda kuoa/kuoelewa ya nini nimwombe Mungu kuhusu mchumba mwema, wacha nikatafute tu anayevutia machoni pangu..Leo ninataka kufungua biashara mpya wacha nifanye tu yoyote nipendayo hata kama si halali ya nini kumshirikisha Mungu, leo nimepataka kazi nzuri ya nini kupelekea sadaka ya shukrani kanisani kwa aliyonitendea..Leo ninapokea mshahara mzuri, ninapata faida kubwa, ya nini kutoa fungu la kumi kwa kila mapato yangu, tendo hilo linaniongezea nini mimi?..Ya nini kuwapelekea wale wachungaji wapiga-dili wanaowaza kula sadaka zetu tu kila siku?…

Ukiamka asubuhi unachowaza, ni mipango yako tu, unasema hakuna Mungu,..,.Lakini unajua kabisa ukiumwa leo karibu na kufa utataka msaada kutoka kwa Mungu, unajua kabisa ukifa leo katika dhambi hujui utajikuta upande upi, unajua kabisa, upo mashakani kwa hofu za magonjwa, ajali, vifo vya ghafla n.k lakini bado kwako wewe habari za Mungu ni kama habari wa wajinga..za watu waliokataa tamaa za maisha, watu maskini, watu wasiokuwa na elimu, watu wavivu wa kufikiri..walioathiriwa na dini za wazungu,..Hivyo ndivyo unavyoyachukulia masuala ya imani.

Ndugu, Bwana anasema Ole,.. kumbuka sisi wanadamu ni mvuke tu ndugu, tushushe viburi vyetu dunia hii sio yetu, hata pumzi tulizonazo si zetu, ni kama tu tumekopeshwa na muhusika. Sasa kwanini uishi tu kama utakavyo?

Yakobo 4:13 “Haya basi, ninyi msemao, Leo au kesho tutaingia katika mji fulani na kukaa humo mwaka mzima, na kufanya biashara na kupata faida;

14 walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka.

15 Badala ya kusema, Bwana akipenda, tutakuwa hai na kufanya hivi au hivi.

16 Lakini sasa mwajisifu katika majivuno yenu; kujisifu kote kwa namna hii ni kubaya”.

Tunapoishi maisha ya kama vile Mungu kwetu ni mtu-baki, hana umuhimu wowote, tujue kabisa tupo hatarini. Pale unapokutana na maneno ya Mungu halafu unatoa maneno ya mzaha,mzaha tu,au kejeli ni ujasiri gani unaokusukuma ufanye hivyo?

Unapokutana na Neno la Uzima, halafu unatukana, ni faida gani unapata, unaposhindana na sauti ya Mungu, hujui unajiharibu mwenyewe…Ayubu 40:2 “Je! Mwenye hoja atashindana na Mwenyezi? Mwenye kujadiliana na Mungu, na ajibu yeye”.

Kwasababu unaona Mungu amekaa kimya hafanyi chochote, ndio unajiamulia kuishi maisha unayotaka wewe,maisha yako yapo gizani, unaendelea kufanya dhambi kwa sirisiri ..Mungu amekuacha pasipo kujijua ndugu…Zaburi 81:12 “Nikawaacha wakaenda kwa ukaidi wa mioyo yao, Waenende katika mashauri yao”

Mithali 1:29 “Kwa kuwa walichukia maarifa, Wala hawakuchagua kumcha Bwana.

30 Hawakukubali mashauri yangu, Wakayadharau maonyo yangu yote.

31 Kwa hiyo watakula matunda ya njia yao, Watashiba mashauri yao wenyewe.

32 Maana kurudi nyuma kwao wajinga kutawaua, Na kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza”

Ndugu, hata sisi tulikuwa hivyo tu lakini siku tulipoona haya maisha ni tambara bovu, tulimpokea Kristo na sasa tumeokolewa tunamtumaini na kumtegemea yeye, na mashauri yetu yote yapo kwake.

Na wewe leo, badilisha aina ya maisha unayoishi, mguekie Kristo, au kama ulikuwa ndani ya Kristo na umemsahau Muumba wako kwa kiwango hicho, ni wakati sasa wa kujinyenyekeza na kumkabidhi njia zako zote na mashauri yako yote,

Mithali 16:3 “Mkabidhi Bwana kazi zako, Na mawazo yako yatathibitika”.

Hizi ni nyakati za kumalizia, tupo ukingoni kabisa wa muda, Kristo yupo mlangoni kurudi..Mguekie Yesu Mkuu wa uzima ayatawale maisha yako..Usimfiche mashauri yako, usimfiche chochote, hakikisha kila jambo lililo mbele yako Mungu ndio mshauri wako wa kwanza, hakikisha hufanyi chochote bila Bwana kuwa kiongozi wako.

Yeremia 17:7 “Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake.

8 Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda”.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

CHUKIZO LA UHARIBIFU

VIUNO VYENU VIWE VIMEFUNGWA NA TAA ZENU ZIWE ZINAWAKA

IFANYE KAZI YA MUNGU PASIPO HOFU!

USIJITAFUTIE KULAMBWA NA MBWA KWA DHAMBI YA KUTAMANI.

JINSI DHAMBI INAVYOMGHARIMU MTU SANA.

MWISHO WA DUNIA UTAKUJAJE?

 

Mwaloni ni nini? Na je unafunua nini rohoni?

Rudi Nyumbani:

Print this post

Maana ya ‘Usimjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake’

SWALI: Mstari huu una maana gani?…

Mithali 26:4 “Usimjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake; Usije ukafanana naye.
5 Umjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake; Asije akawa mwenye hekima machoni pake”.


JIBU: Katika huo mstari hilo neno “sawasawa” jinsi lilivyojirudia mara mbili..ndilo linalochanganya..lakini tukitafakari kwa kina tutagundua kuwa hilo Neno halijichanganyi, lipo sawasawa.

Sasa kabla ya kuendelea mbele hebu tujifunze mtu mpumbavu ni mtu wa namna gani,

Mpumbavu ni mtu asiyeweza kupambanua mambo vizuri hususani ya ki-Mungu. Mtu ambaye bado anafuata mambo ya ulimwengu au ambaye haamini kuhusu Mungu ni mpumbavu kulingana na biblia, kwasababu bado hajaweza kupambanua vizuri elimu ya maisha, ambayo ni kumjua muumba wake, na kuepukana na uovu….Hiyo ndiyo elimu ya kwanza ambayo kila mwanadamu anapaswa awe nayo..kwasababu hata wanyama na ndege kwa sehemu fulani wanayo. Wanajua kuwa kuna muumba..

Zaburi 14:1 “Mpumbavu amesema moyoni Hakuna Mungu”..

Na neno “upumbavu au mpumbavu” kama linavyotumika kwenye biblia sio tusi….bali ni hali mtu aliyonayo ya kushindwa “kupambanua mambo” kama tulivyotangulia kujifunza.

Sasa mtu asiyemjua Kristo anapokutana na wewe unayemjua Kristo na kukutukana matusi, na wewe unapomjibu kwa kurudisha matusi…hapo wewe na yeye hamna tofauti..wote wawili mmefanana na ni wapumbavu…hiyo ndio maana biblia inasema usimjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake ili usije ukafanana naye.

Lakini kama amekutukana…na wewe uliye ndani ya Kristo, ukatambua Yule mtu tatizo lake ni dhambi ndani ya moyo wake, na hivyo kulingana na biblia ni mpumbavu, na anamhitaji Yesu ili upumbavu wake uondoke…na hivyo kwa hekima ukaanza kumjibu kwa na kumuelekeza njia iliyo sahihi kwa upole na utaratibu..hapo atakapoona wewe umemzidi hekima, hujamrudishia tusi kama yeye alivyokutukana, yeye atajiona hana hekima..na hivyo atachomwa dhamira yake na kushawishika kugeuka kuacha njia yake mbaya.

Au pale mpumbavu anapotoa maneno ya kukulaani, lakini wewe ukambariki hapo ni sawa na umemjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake,
Ambapo kwa tendo hicho kitamfanya ajione hana hekima machoni pake mwenyewe.

Ubarikiwe.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAP

Mada Nyinginezo:

FAHAMU JINSI KRISTO ANAVYOPONYA WATU ROHO.

Je! Ni sahihi kwa mkristo kuoa/kuolewa na mtu wa imani nyingine?

MAMBO 5 AMBAYO KILA MKRISTO ANAPASWA KUFAHAMU.

UWEPO WA BWANA HATA KATIKATI YA MATESO.

Hapa ana maana gani kusema hivi? ” Usiseme moyoni mwako,Ni nani atakayepanda kwenda Mbinguni? (yaani ni kumleta Kristo chini), “au,Ni nani Atakayeshuka kwenda Kuzimu? (yaani, ni kumleta Kristo juu,kutoka kwa wafu.). {Warumi10:6-7.}

https://wingulamashahidi.org/2018/06/27/maswali-na-majibu/

Paulo alimwambia Timotheo atumie mvinyo kidogo kwa ajili ya tumbo lake, Je! tunaruhusiwa na sisi pia kutumia pombe?

USIINGIE MKATABA NA DHAMBI.

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

Rudi Nyumbani:

Print this post

FAHAMU JINSI KRISTO ANAVYOPONYA WATU ROHO.

Lipo tukio ambalo, wengi wetu tunalijua lihusulo yule kijana aliyepagawa na mapepo, ambapo tunaona baba yake alimchukua na kumpeleka kwa mitume wa Yesu, lakini walishindwa kulitoa lile pepo, lakini baadaye kidogo walipomwona Bwana anashuka milimani, baba yake yule kijana alimkimbilia Bwana, na kumwambia nisaidie mwanangu, nilimleta kwa wanafunzi wako lakini hawakuweza kumtoa..

Ndipo Bwana Yesu akawaambia wamlete kwake, sasa alipofika tu kwake, mambo yalikuwa nje ya matarajio ya watu wengi waliokuwepo mahali pale.. Embu tusome tena Pamoja Habari hiyo kwa utaratibu, lipo jambo jipya naamini tutalipata mwisho wa Habari hiyo.

Marko 9:17 “Mtu mmoja katika mkutano akamjibu, Mwalimu, nimemleta mwanangu kwako, ana pepo bubu;

18 na kila ampagaapo, humbwaga chini, naye hutoka povu na kusaga meno na kukonda; nikasema na wanafunzi wako wamtoe pepo, wasiweze.

19 Akawajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, nikae nanyi hata lini? Nichukuliane nanyi hata lini? Mleteni kwangu.

20 Wakamleta kwake; hata alipomwona, mara yule pepo alimtia kifafa; naye akaanguka chini, akagaa-gaa, akitokwa na povu.

21 Akamwuliza babaye, Amepatwa na haya tangu lini? Akasema, Tangu utoto.

22 Na mara nyingi amemtupa katika moto, na katika maji, amwangamize; lakini ukiweza neno lo lote, utuhurumie, na kutusaidia.

23 Yesu akamwambia, Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye.

24 Mara babaye yule kijana akapaza sauti, akasema, Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu.

25 Naye Yesu akiona ya kuwa mkutano unakusanyika mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akamwambia, Ewe pepo bubu na kiziwi, mimi nakuamuru, mtoke huyu, wala usimwingie tena.

26 Akalia, AKAMTIA KIFAFA SANA, akamtoka; naye AKAWA KAMA AMEKUFA; hata wengi wakasema, Amekufa.

27 Lakini Yesu akamshika mkono akamwinua naye akasimama”

Kama tunavyoona ule mstari wa 26 anasema, pepo yule akalia, halafu akamtia kifafa sana, Neno “sana” sio kitendo cha kawaida, ukitaka kujua si kitendo cha kawaida utaona kwa mahangaiko yake mtoto yule na kelele zake kuliwasababisha mpaka watu waliokuwa mbali wasogee karibu, wakisema kuna nini pale? Wakawa wanakuja kwa kasi..wengine walidhani pengine mtu anaungua moto, au kapewa sumu,..pengine baba yake yule kijana akafikiri mbona sasa hali hii ndio imekuwa mbaya Zaidi kuliko mwanzo..wale watu wengine wakafikiri na wao, afadhali alivyokuwa mwanzo, huyu mtu ndio kaharibu kabisa mambo, hali yake imekithiri zaidi..

Tengeneza picha, Na kibaya Zaidi ni kitendo kilichofuata cha yule kijana kutulia baada ya muda mfupi, akawa hapepesi midomo tena kama mtu mwenye kifafa anavyofanya siku zote, wala macho, wala haonekani kama anapumua, alikuwa kimya.. Unadhani jambo gani lingefuata kwa wale watu waliokuwa pale..Ni wazi kama tunavyosoma Habari walisema..Kijana AMESHAKUFA huyu..

wengine pengine wakakimbia saa hiyo hiyo wakisema hii ishakuwa kesi sasa, wengine pengine walianza kudondosha machozi..n.k.

Lakini ule upande wa pili Je! Bwana Yesu muda wote huo alikuwa anafanya nini?

Jibu ni alikuwa anaangalia uponyaji wa Mungu unavyofanya kazi ndani ya yule kijana.. alitulia kimya mpaka pale alipoona kazi ya Mungu imekamilika ndani ya yule kijana,…. Na ghafla tu wakati watu wanaendelea kufikiria tufanye nini?, Wanamwona Bwana anakwenda kumshika kijana mkono na kumnyanyua..

Alivyonyanyuka hakunyanyuka kama mgonjwa mwenye maruwe ruwe, hakunyanyuka kwa kuyumba yumba kama mtu ambaye hajapona vizuri, bali alinyanyuka kama vile mtu aliyeamka usingizini, asubuhi, akiwa fresh, akiona tabasamu zuri la Kristo likiyatazama macho yake.. Kijana akijiona mwepesi, mtulivu, kama vile sio yeye, na tangu huo wakati akawa mzima kabisa..

Sasa ni kwanini Kristo achague, njia kama ile kumponya yule kijana? Na sio zile zilizozoeleka kwamba anafika tu anamgusa mtu na saa hiyo hiyo anapona bila mateso yoyote wala mahangaiko kama yale..

Ni kuonyesha kuwa Kristo anavyowaponya watu wengine Roho zao kwa namna hiyo hiyo pasipo wao kujijua.. Kuna wakati mtu atamwomba Mungu niponye roho yangu..Niponye shida zangu, niponye vifungo vyangu, niponye magonjwa yangu.. Lakini baada ya kuomba vile mambo ndio yanakuwa tofauti, hali ndio inakuwa mbaya Zaidi kinyume na matarajio yake,.. mwingine ni mgonjwa, ugonjwa wake unaonekana kama ndio unazidi, mwingine ana mapepo, maroho hayo ndio yanaonekana kama yanazidi..wala usiogope maadamu ulishamwomba Kristo juu ya uponyaji wako, ujue kuwa hayo maroho yameshakutana na Kristo mwenyewe, hivyo ndio yanavyoungua ndani yako kwa Neno lake..na wakati si mwingi yatatoweka moja kwa moja.

Huo ugonjwa unaokusumbua muda mrefu, umemwomba Kristo akuponye, ameshakusikia na ameshakuponya, lakini hizo dalili za ugonjwa zinazoonekana kama zinazidi, zisikutishe, wakati utafika utaondoka kabisa..usiogope maneno au hisia za wanaokuzunguka, wamekukatia tamaa kiasi gani Kumbuka yule kijana alifikia hatua ya kuonekana amekufa kabisa..hana tumaini tena, lakini ghafla alishikwa mkono na kunyanyuliwa juu na Kristo..Ni nani anayeweza kufa mbele ya Kristo?..yeye ndiye UFUFUO NA UZIMA!

Hivyo na wewe maadamu umemkabidhi Kristo shida yako ujue kuwa hutakufa nayo..Utakufa na nyingi lakini sio hiyo, unachopaswa kufanya ni kuamini Tu.. Basi hicho tu, amini kuwa Kristo amekusikia na atameshakuponya…Lakini hakikisha upo ndani ya Kristo kwanza.

Vilevile katika roho, ukimwomba Kristo akuvushe katika daraja lingine, usishangae kuonekana na watu umekufa kabisa kiuelekeo machoni pa watu..Hiyo ni kawaida..Hivyo uwe tayari kwa hilo pia..kwasababu ni sharti aondoe yote yasiyofaa ndani yako, na ndipo alete mapya ndani yako, kwa Kristo ni lazima upoteze ndipo upate, usipokuwa tayari kufanya hivyo, ni huwezi kuvushwa hatua nyingine..Kwahiyo hilo nalo uwe nalo tayari.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAP

Mada Nyinginezo:

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita..

Je ni kweli huwezi kuijua karama yako mpaka uwekewe mikono na wazee?

CHUKIZO LA UHARIBIFU

MPINGA-KRISTO

USIMWOGOPE YEZEBELI.

Rudi Nyumbani:

Print this post

YATOE MAISHA YAKO KWA YESU.

Kuna tofauti ya kutoa uhai, kutoa mali, na kutoa maisha…Unapotoa uhai wako kwa Yesu maana yake unakuwa tayari kufa kwa ajili ya Kristo, unapotoa mali maana yake unatoa sehemu ya vile unavyomiliki kwa Kristo, na hivyo vinaweza kuwa fedha, hazina au milki yako yoyote ile….Lakini kuna kitu kingine cha muhimu ambacho ndicho tutakachokizungumzia leo…Na hicho ni kutoa maisha kwa Yesu.

Kuyatoa maisha yako kwa Yesu maana yake kuanzia huo wakati maisha yako sio milki yako wewe bali yake yeye…Hii ni sadaka kuu na ya kwanza na ya muhimu kuliko zote. Na maisha sio kipindi cha siku kadhaa, au wiki kadhaa bali ni kipindi chote chako cha kuishi ambacho kinaweza kikafika hata miaka 90. Ni kipindi cha kuweka chini mipango yako, na kuichukua mipango yake…ni kipindi si cha kuishi tena kama utakavyo wewe, bali atakavyo yeye..ni wakati wa kuvua nira zako ulizojivisha, na zile shetani alizokuvisha na kuzivaa nira za Yesu…ni wakati wa kutua mizigo yako binafsi uliyojitwisha na ile uliyotwishwa na shetani na kuibeba mizigo ya Yesu Kristo.

Unatoka kuwa mtumwa wa wanadamu na shetani na kuwa mtumwa wa YESU. Kitu kimoja kisichofahamika na wengi ni kwamba Yesu anapotutoa katika utumwa wa shetani..huwa hatuachi tu huru bila kuwa na shughuli yoyote…badala yake anatutwika mzigo wake,…maana yake tunaifanya kazi yake..na anapotuvua nira ya adui, ni ili atuvike nira yake yeye…ingawa yake ni laini na si ngumu kama ile ya Yule adui..Ndivyo maandiko yanavyosema katika..

Mathayo 11:28 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”.

Umeona?..Bwana na yeye anao mzigo wake..na vile vile anayo NIRA. Hivyo tunapompa Yesu maisha maana yake tunajiuza chini ya utumishi wake mpaka siku tutakayoondoka hapa duniani. Ndio maana Mtume Paulo karibia kila mwanzo wa nyaraka zake alianza na maneno haya…

Filemoni 1:1 “Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu, na Timotheo aliye ndugu yetu, kwa Filemoni mpendwa wetu, mtenda kazi pamoja nasi,…..9 lakini, kwa ajili ya upendo nakusihi, kwa kuwa ni kama nilivyo, Paulo mzee, na sasa mfungwa wa Kristo Yesu pia”…

Kasome pia Waefeso 3:1,4:1,Tito 1:1..

Mtume Paulo ni mfano wa watu walioyatoa maisha yao kwa Kristo…Na sisi hatuna budi tuwe vivyo hivyo…maana yake maisha yetu kuishi ni Kristo na kufa ni faida.

Lakini ukijiona unaishi lakini upo huru, kufanya dhambi…upo huru kuishi utakavyo basi jua bado hujawekwa huru na Kristo,kwasababu ukiwekwa huru na Kristo ni lazima akuvishe nira zake yeye na akutwishe mizigo yake…Sasa nira ya Yesu iko wapi Maishani mwako?..wewe ni mlevi ukiambiwa unasema Kristo kakuweka huru..bado hujawekwa huru…wewe ni mtumwa wa dhambi bado…maisha yako bado hujayatoa kwa Yesu.

Neno la Mungu leo linakufikia kwa njia hii, pengine ulishalisikia…Lakini sasa ni wakati wa kugeuka na kumpa Yesu maisha yako…Amua kuukataa utumwa wa shetani na kusudia kuuvaa utumwa wa Bwana Yesu, ambao amesema mzigo wake ni mwepesi na nira yake ni laini, tofauti na hiyo ya dhambi uliyoivaa..

Hivyo unachopaswa kufanya ni hapo ulipo ni kutenga muda mchache binafsi na kuomba rehema na kumwambia Bwana aingie maishani mwako, ayaongoze maisha yako na wewe uwe wake…usisome habari hizi kama hadithi tu ya kukusisimua, bali uchukue hatua…na baada ya kuomba kusudia kuacha yote uliyokuwa unayafanya yasiyompendeza Mungu..na baada ya hapo, katafute ubatizo sahihi, kwaajili ya kukamilisha wokovu wako…kabla ya kukitumia kijiko ni lazima ukioshe, na wewe kabla Bwana hajaanza kukutumia ni lazima akuoshe kwenye maji mengi kwanza kitakate…hivyo na wewe nenda katafute ubatizo sahihi kwa gharama zozote kwani ni wa muhimu sana, na ubatizo sahihi ni ule wa maji mengi na kwa jina la Yesu Kristo (Matendo 2:38,8;16,10:48,19:5) na Roho Mtakatifu atashuka juu yako kukufanya mtumishi wake…

Nakukumbusha kuwa tunaishi katika siku za mwisho, na Kristo yupo mlangoni kurudi.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAP

Mada Nyinginezo:

WAZAZI WA YOHANA NA YAKOBO.

KUTUBU SIO KUOMBA REHEMA.

NAMI NINAZO FUNGUO ZA MAUTI, NA ZA KUZIMU.

USIHUSISHE HISIA KATIKA KUMTOLEA MUNGU.

Je ni sahihi kumtenga mtu anapofanya dhambi kanisani?

 

USIHUSISHE HISIA KATIKA KUMTOLEA MUNGU.

NAMI NINAZO FUNGUO ZA MAUTI, NA ZA KUZIMU.

Rudi Nyumbani:

Print this post

KABLA YA MAANGAMIZI, KRISTO HUWA ANAONYESHA KWANZA NJIA YA KUTOROKEA.

Luka 21:20 “Lakini, hapo mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, ndipo jueni ya kwamba uharibifu wake umekaribia.

21 Ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani, na walio katikati yake wakimbilie nje, na walio katika mashamba wasiuingie.

22 Kwa kuwa siku hizo ndizo za mapatilizo, ili yatimizwe yote yaliyoandikwa.

23 Ole wao wenye mimba na wanaonyonyesha katika siku hizo! Kwa kuwa kutakuwa na shida nyingi katika nchi, na hasira juu ya taifa hili.

24 Wataanguka kwa ukali wa upanga, nao watatekwa nyara na kuchukuliwa katika mataifa yote; na Yerusalemu utakanyagwa na Mataifa, hata majira ya Mataifa yatakapotimia.”

Japokuwa mji wa Yerusalemu ulimkataa Kristo, kiasi cha kumsulibisha, lakini yeye hakuacha kuwaonya juu ya mabaya yaliyokuwa yanakuja mbele yao na sio tu kuwaonya bali pia aliwaonyesha na njia ya jinsi ya Kuyakwepa mabaya hayo.. Ni upendo wa namna gani huo..

Bwana Yesu aliona kuwa mji wa Yerusalemu utakuja kuzungukwa na majeshi ya Rumi, na baadaye kuja kuteketezwa na kuchomwa moto na kibaya Zaidi watu walio ndani ya mji watauliwa vibaya sana, wengine watatekwa nyara, na wengine watatawanywa katika mataifa yote duniani..

Luka 19: 41 “Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia,

42 akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako.

43 Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote;

44 watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako”

Lakini Pamoja na taarifa hiyo mbaya, hakuwaacha tu hivyo juu juu, bila suluhisho lolote.. Ndipo akawaambia sasa wakati huo watakapoyaona hayo majeshi tu yameuzunguka mji, basi wajue kuwa ndio ule wakati wa uharibifu umefika..Hivyo walio ndani ya mji huo wautoke haraka wakimbilie milimani (yaani makazi mengine yasiyokaliwa na watu)..Na walio katikati yake, yaani wale wanaoishi ndani yake, wenye manyumba basi wakatafute miji mingine ya kuishi, na wale walio katika mashamba( yaani wenye miradi yao, na biashara zao) wakatafute sehemu nyingine lakini sio pale Yerusalemu tena, kwasababu Yerusalemu unakwenda kuteketezwa siku si nyingi…

Jambo hilo lilikuja kutokea kama lilivyo miaka isiyozidi 33 baada ya Kristo kuondoka duniani..Ili kuelewa vizuri jinsi muda ulivyokuwa mfupi tangu alipotoa unabii huo hadi maangamizi yalipofika, tuseme kama leo mwaka (2020) ndio majeshi yametokea Tanzania basi Kristo alitoa unabii huo mwaka 1987… Hivyo kazazi kile chote kilichoyasikia yale maneno kilikuwepo hadi huo wakati ulipofika.

Sasa waliokuwa wameyazingatia maneno ya Kristo kwa wakati ule,walishangaa kweli kuyaona majeshi ya Rumi yamekuja kuuzingira mji, mwaka 66AD, Lakini hawakuleta madhara yoyote bado, Mungu aliruhusu iwe hivyo ili kupisha nafasi ya watu kuutoroka mji ule, sasa wale walioyasikiliza maneno ya Kristo walipoona vile, mara moja waliokuwa na miradi yao na mashamba yao, na mabenki yao, waliyaacha na kuondoka, wengine waliokuwa na majumba nao pia waliyaacha, wengine waliokuwa na mipango ya kuutembelea Yerusalemu msimu huo, wakaahirisha mipango yao..wakawa tayari kupata hasara ya mambo yao yote lakini sio hasara ya roho zao.

Lakini kulikuwa na wengine ambao waliona maneno ya Kristo kama hadithi za kizee tu, wakaendelea kubaki ndani ya mji ule na kuendelea na shughuli zao, wakitumai warumi wataondoka siku moja na kuuacha mji..na wengine wakajifariji kwamba hakutakuwa na vita yoyote, Lakini siku ya siku ilipofika, mwaka 70AD maangamizi yaliyokuwa Yerusalemu wakati ule, hadi leo kwenye historia tunayasoma..watu waliuliwa kikatili, hakuna hata mmoja aliyenusurika kutoroka, wale waliobahatika kuwa hai, walichukuliwa kama watumwa kwenda kufanyishwa kazi katika migodi sikuzote za Maisha yao, wengine wakatawanywa dunia nzima, na hekalu la pili likabomolewa halikusalia tofali juu ya tofali..(kutimiza unabii Bwana aliousema miaka 33 iliyopita)

Habari ya Israeli ilifutikia pale katika historia, mji uliharibiwa na kuchomwa moto, mpaka hekalu lile likaondolewa Yerusalemu pale..walipelekewa mbali kiasi kwamba iliwagharimu karibu miaka 1900 kurudi katika nchi yao tena..

Sasa kwanini Bwana Yesu aliwapa tahadhari ile kwanza, mpaka akaifananisha na dhiki kuu?

Ni kwasababu alikuwa anaonyesha mfano wa yatakayokuja kutokea huko mbele katika dhiki kuu HALISI, wapo wanaodhani kuwa Dhiki kuu ina muhusu kila mkristo..Biblia haifundishi hivyo..yapo makundi mawili katika kanisa, wapo wale wanaoyaishi bega kwa bega maneno ya Kristo, na hao ndio Bwana atakaowafungulia mlango wa kuikwepa dhiki kwa tendo linaloitwa UNYAKUO. Lakini wapo ambao wanafananishwa na wale wanawali wapumbavu, ambao hao wanaishi Maisha ya kubahatisha bahatisha tu, hawajishughulishi na mambo ya ufalme wa mbinguni, wapo tu, wanaridhika na hali zao za kiroho haijalishi wanazidi kuwa baridi au vuguvugu. Habari za dhiki kuu na unyakuo kwao ni kama stori za kilokole tu, na wakisikia mahubiri ya Neno la Mungu yanayowaonya, wananung’unika wanahukumiwa..

Bwana alishatupa tahadhari akasema kabisa, KESHENI,

Marko 13:32 “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba.

33 Angalieni, kesheni, [ombeni], kwa kuwa hamjui wakati ule utakapokuwapo.

34 Mfano wake ni kama mtu mwenye kusafiri, ameiacha nyumba yake, amewapa watumwa wake amri, na kila mtu kazi yake, naye amemwamuru bawabu akeshe.

35 Kesheni basi, kwa maana hamjui ajapo bwana wa nyumba, kwamba ni jioni, au kwamba ni usiku wa manane, au awikapo jimbi, au asubuhi;

36 asije akawasili ghafula akawakuta mmelala.

37 Na hilo niwaambialo ninyi, nawaambia wote, Kesheni”.

Siku ya Unyakuo hakuna anayeijua, lakini majira ya huo wakati tumeshapewa, tumeambia tukiona matetemeko makubwa ya ardhi, tetesi za vita duniani, tukiona magonjwa makubwa ya mlipuko yakitokea duniani kama vile CORONA. Basi tujue wakati wa mavuno umefika.

Hivyo tusishangae, moja ya hizi siku, wakati wowote, watakatifu wametoweka..Jiulize wewe ambaye hujajiweka tayari utakuwa wapi wakati huo?. Wakati wenzako wapo mbinguni kwenye karamu ya mwana kondoo, wewe utakuwa hapa chini duniani katika dhiki kuu ya mpinga-kristo, na wala usidhani ni rahisi kupona ndugu, hilo jambo halipo ikiwa leo hii unashindwa kumkiri tu Kristo, kwa mwenendo wako, kwa kukataa kuvaa vimini, na kuweka make-up, na kuvaa suruali utawezaye kumkiri kwa kifo kilichopo mbele yako..Yaani kwa ufupi ukishajiona umeachwa wewe, hukustahili katika ufalme wa mbinguni..wala hakuna tumaini lolote tena kwako. Sahau hili jambo linaloitwa nafasi ya pili. Mlango huo utakuwa kwa wengine kabisa..

Huu si wakati wa kuzidi kutanga tanga na dunia hii inayokaribia kuisha, kwasababu dunia inakwenda kuisha hii..Ni wakati wa kuyashika na kuyatunza maneno ya Yesu Kristo, kama yalivyoandikwa katika kitabu chake, Biblia takatifu.

Ufunuo 1:3 “Heri asomaye na wao wayasikiao maneno ya unabii huu, na kuyashika yaliyoandikwa humo; kwa maana wakati u karibu”.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAP


Mada Nyinginezo:

INJILI YA KRISTO HAITANGAZWI KWA HATI MILIKI.

Je ni kweli huwezi kuijua karama yako mpaka uwekewe mikono na wazee?

HEKIMA NI NINI? NA UFAHAMU UNAPATIKANA WAPI?

MAPAMBANO DHIDI YA SHETANI.

MAMBO YA KWANZA YAMEKWISHA KUPITA!

Rudi Nyumbani:

Print this post

KUMBUKUMBU LA DHAMBI.

Wakolosai 3:12 “Basi, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu,

13 mkichukuliana, na KUSAMEHEANA, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi”.

Kwanini tunapaswa tuwasamehe wale waliotukosea?…Ni kwasababu na sisi kila siku tunahitaji rehema na msamaha kutoka kwa Mungu wetu..Wengi hatujui nguvu iliyopo katika msamaha…Biblia inasema “achilieni nanyi mtaachiliwa (Luka 6:37)”…Maana yake tusipowaachilia watu na sisi pia hatutaachiliwa…

Na msamaha sio wa masaa machache au siku chache…bali ni wa milele…mtu akikukosea huda budi kumsamehe moja kwa moja…maana yake haitatokea siku ukamwekea kinyongo tena..lakini endapo umemsamehe leo na ikapita mwezi ukayakumbuka makosa yake na kuanza kuyatia tena moyoni…Biblia inasema hapo na wewe dhambi zako ulizozitenda huko nyuma zitakumbukwa na Mungu.

Kwamfano ulishaomba rehema na kutubia wizi ulioufanya huko nyuma kabla hujampa Yesu maisha yako…au kuna siku ulimrusha mtu kiasi Fulani cha pesa, au kuna siku ulimwibia boss wako pesa, au kuna kipindi ulimchomolea mtu simu n.k Na siku moja ukakutana na injili na ukatubu na kulia..na kuacha wizi…na ukaishi hivyo kwa zaidi ya miaka 10 bila kuiba tena…Lakini siku moja ikatokea mtu kakuchomolea simu yako, ambayo ndio hiyo tu ulikuwa nayo na uliinunua kwa gharama…ikakusababishia mpaka ukapoteza mambo yako ya muhimu sana uliyokuwa umeyahifadhi katika simu ile…na moyoni ukaudhika sana, na baadaye ukamgundua yule mtu aliyekuibia, ukamwekea kinyongo moyoni pasipo hata kumwambia..

Sasa katika hali kama hiyo…kama usipomsamehe Yule mtu, ukaendelea kumchukia vile vile moyoni mwako…hata kama huibi sasa, hata kama bado unaendelea kusali na kufanya mambo mengine ya Imani…Tayari Mungu anakuona wewe nawe ni mwizi…ule wizi wote uliokuwa unaiba kule nyuma unakumbukwa wote, kama vile umeufanya jana tu!!…Haijalishi imepita miaka mingapi hujaiba…Mbele zake unarudishwa na kuonekana kama umeufanya masaa machache tu nyuma…na hivyo hata ikitokea umekufa utaenda kuulizwa kwanini uliiba ile simu, kwanini ulimwibia Yule boss wako, kwanini ulimtapeli Yule mtu n.k n.K.

Hebu soma habari hii kwa makini na utaratibu…

Mathayo 18:21 “Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba?

22 Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.

23 Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake.

24 Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi.

25 Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo, ikalipwe ile deni.

26 Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema, Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia.

27 Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni.

28 Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari mia akamkamata,akamshika koo,akisema Nilipe uwiwacho.

29 Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake, akamsihi, akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia.

30 Lakini hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni, hata atakapoilipa ile deni.

31 Basi wajoli wake walipoyaona yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote yaliyotendeka.

32 Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa mwovu, nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi;

33 nawe, je! Haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe?

34 Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote.

35 Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake”.

Ndugu achana na biashara za kupambana pambana na maadui zako, jifunze kusamehe ndivyo na wewe utakavyosamehewa na Mungu Baba…Aliyekufundisha kwamba mlaani anayekukosea…huoni kwamba anataka na wewe ulaaniwe na Mungu?…anayekuzuia kusamehe huoni kama anakutakia mabaya?..huoni anakufungulia mlango wa kwenda jehanamu ya moto??…hebu soma tena mstari wa 35 hapo juu….na wewe binafsi unapojizuia kuwasamehe wanaokukosea hata baada ya kuelewa haya..huoni unajishitaki mwenyewe na kumkumbusha Mungu dhambi zako?.

Bwana atujalie kuyaelewa hayo.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAP


Mada Nyinginezo:

JE KUNA UISLAMU KATIKA BIBLIA?

Je! kuna maombi yoyote ya kumtoa mtu aliyekufa kwenye mateso ya kuzimu?

Mwaloni ni nini? Na je unafunua nini rohoni?

NAMI NINAZO FUNGUO ZA MAUTI, NA ZA KUZIMU.

Je! Ni sahihi kwa mkristo kuoa/kuolewa na mtu wa imani nyingine?

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 4

Rudi Nyumbani:

Print this post

MIGUU ILIYO MYEPESI KUKIMBILIA MAOVU, NI CHUKIO KWA BWANA.

Zipo dhambi za maandalizi, na zipo dhambi zisizo na maandalizi..

Hizi dhambi za maandalizi ni rahisi sana kuzishinda, kwasababu sio za kushtukiza kwani huwa zinaanzia mbali na hivyo mtu ni rahisi kuziona na kuzikwepa, na akizifanya mbele za Mungu adhabu yake inakuwa ni kubwa kuliko zile ambazo zinakuja bila maandalizi,

Mfano wa dhambi zisizo na maandalizi, ni kama vile hasira, hofu, mawazo mabaya, na mara chache sana kuzungumza maneno yasiyofaa..

Lakini Mfano wa dhambi zenye maandalizi, ni kama vile Uzinzi/Uasherati wa aina yoyote ile ikiwepo punyeto, ushoga, usagaji, ulevi, utoaji mimba, utapeli, wizi, n.k.

Hizi ni dhambi ambazo mtu hawezi kuzifanya bila kuwa na maandalizi Fulani, au kupitia hatua Fulani(process). Huwezi kusema nimepitiwa kufanya uzinzi wakati kitendo chenyewe kabla ya kufanya mlikutana mahali Fulani, mkakubaliana, na kabla hujafanya kile kitendo ndani yako kabisa kulikuwa na kipenga chekundu kinalia kikikuambia kuwa hicho kitendo unachokwenda kukifanya sio sawa ni dhambi, lakini wewe unakwenda tu, bila kujali..na mwisho wa siku unakifanya..vile vile na wizi,..n.k.

Fahamu kuwa mbele za Mungu dhambi kama hizo usidhani gharama zake ni ndogo kuziondoa.. kamwe usije ukasema ah, si nitatubu tu?..Fahamu kuwa Toba sio tiba ya dhambi, kama vile Panadol kwamba ukiumwa kichwa unakwenda kumeza kisha unapona, kesho tena ukiumwa unakwenda kumeza nyingine..

Ukadhani pia katika kila aina ya dhambi ya namna hii dawa ni kutubu tubu. Ujue kuwa Zipo dhambi biblia imeziita dhambi za Mauti..Hizi ukitenda na huku unajua hupaswi kuzifanya, hakuna msamaha, ndio unaweza ukasemehewa baada ya kutubu kwa muda mrefu sana lakini adhabu ya kifo bado itabakia pale pale..

(Kwa urefu wa somo hili la dhambi ya mauti,  utalipata chini kabisa mwisho wa somo hili),

Dhambi hii Hata ulieje, hata utubuje, adhabu ya kifo haiondoki..kwasababu uliitenda kwa makusudi,

Inawezekana wewe nawe leo ni mmojawapo wa walio mbioni kukimbilia kutenda maovu hayo..Embu geuka ujiepusha na hatari hiyo iliyopo mbele yako…Na wewe mwingine ambaye umekuwa ukiishi katika kutenda dhambi kama hizo za makusudi ukidhania kuwa utatubu tu, na kwamba neema itakuwepo kila siku kukuokoa..Embu futa mawazo hayo na kwa moyo mmoja leo hii umgeukie muumba wako, utubu leo dhambi zako kwa kumaanisha nawe pia Mungu atakusikia..

Kumbuku miguu ikimbiliayo maovu na machukizo kwake Bwana, ni moja ya mambo sita yanayomuudhi Bwana (Mithali 6:18).

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAP


Mada Nyinginezo:

DHAMBI YA MAUTI

KUTUBU SIO KUOMBA REHEMA.

MADHABAHU NI NINI?

MUUNGANIKO WA MADHEHEBU NI MPANGO WA MPINGA-KRISTO.

MAOMBI YA VITA

KAMA TUNATAKA KUWA ASKARI WA BWANA, NI LAZIMA TUJUE VIGEZO.

Rudi Nyumbani:

Print this post

USIINGIE MKATABA NA DHAMBI.

Laiti Yuda angefahamu yatakayokwenda kumpata Bwana ni makubwa kiasi kile, asingedhubutu hata kidogo kumsaliti, Yeye alijua tu watakwenda kumchukua na kumkemea asiwafundishe makutano mahubiri yake, na kumtishia kidogo na kisha kumwachia aende…Lakini mambo kule yalienda kuwa makubwa kuliko alivyotegemea…Kwani walikwenda kumpiga, na kumdhihaki, na kufikia hatua mpaka ya kumwua Bwana tena kwa kifo cha aibu na mateso…

Kwasababu ya tamaa ya fedha hakujua tayari ametumika kulitimiza kusudi la shetani…Pasipo kuwa na macho ya kuona mbali alijikuta kawa chombo maalumu cha shetani. Moto mdogo aliouwasha akidhani utateketeza karatasi tu, sasa umeteketeza msitu mkubwa…Ndio maana mwishoni aliishia kujuta kwa aliyoyafanya, alipoona kwamba ni busu lake dogo tu limemfikisha Bwana msalabani, alipoona vipande 30 tu vya fedha vimemwaibisha vile na kumtesa kiasi kile…alipojua atafikishwa salama na kutoka salama lakini mwisho wake anaishia kuvuliwa nguo na kuvishwa taji ya miiba kichwani…ni Dhahiri kuwa ilikuwa ni nje ya mapatano yao..

Marko 14:44 “Na yule anayemsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni, MKAMCHUKUE SALAMA.

45 Basi alipokuja, mara akamwendea, akasema, Rabi, akambusu.

46 Wakanyosha mikono yao wakamkamata”.

Mstari wa 44 hapo unasema “mkamchukue salama”…Lakini kule alipokwenda walikwenda kumtesa na kumwaibisha na kumuua, kinyume na mapatano yao. Na hiyo yote ni kutokana na kuingia mkataba na dhambi.

Na mwisho Yuda anasema maneno haya…

Mathayo 27: 3 “Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, alipoona ya kuwa amekwisha kuhukumiwa, alijuta, akawarudishia wakuu wa makuhani na wazee vile vipande thelathini vya fedha, akasema, Nalikosa nilipoisaliti damu isiyo na hatia.

4 Wakasema, Basi, haya yatupasani sisi? Yaangalie haya wewe mwenyewe.

5 Akavitupa vile vipande vya fedha katika hekalu, akaondoka; akaenda, akajinyonga”

Mambo machache tunaweza kujifunza hapo…unaweza kuuza wokovu wako kwa kitu kidogo..lakini mwishoni usijue kama kitakuletea au kitaleta madhara makubwa mbeleni…Umemwamini Yesu tayari, lakini unaingia tamaa ya kufanya zinaa..hivyo unatoka na kumwona mwanamke na kumtamani, na kusema nitatubu tu…siku unakutana naye kumbe kuna mwingine amewaona na kuwafuatilia mpaka nyumba mnayokwenda, na huko mnakuja kufumaniwa..na picha zinapigwa na kuwekwa kwenye mitandao..mtumishi fulani au mpendwa fulani afumaniwa na mke wa mtu…utajisikiaje siku hiyo?..Wewe ulidhani ni moto mdogo tu umewasha kumbe hujui utakwenda kuwa mkubwa wa kushtusha mji mzima, na hivyo hivyo na dhambi nyingine zote, tunaweza kuziona zina madhara madogo hapa tu..lakini baada ya kuzitenda ndio tutaona ukubwa wake..

Kwahiyo tunapaswa kuzidi kuwa makini kwa kila kitu, Mfano wa Yuda ni somo tosha kwetu…Tujichunge yasijikute na sisi, shetani akatudangaya tukajikuta tunamsulubisha Kristo mara ya pili kwa aibu na mateso. Na mwisho wa siku tukashindwa hata kurudi kule tulipokuacha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAP


Mada Nyinginezo:

MADHARA YA DHAMBI YA UASHERATI.

Je Mtu anaweza kusema uongo, Na Mungu akambariki?

NAMI NINAZO FUNGUO ZA MAUTI, NA ZA KUZIMU.

JE NI DHAMBI KUWA NA MAHUSIANO KABLA YA NDOA?

Kwanini wanawake wengi huwa wanalipuka mapepo?

MAMBO 5 AMBAYO KILA MKRISTO ANAPASWA KUFAHAMU.

Rudi Nyumbani:

Print this post

JE! TUNAPASWA KUUAMINI UNABII WA SYLVIA BROWNE?

Hivi karibu mwanamke huyu amepata umaarufu mkubwa duniani japo alishafariki mwaka 2013, lakini kitabu chake kilichoitwa “End of days”, ambacho ndani yake kimeandika baadhi ya nabii zitakazotokea siku za mwisho, ndicho kilichomfanya ajulikane kwa haraka, na moja ya nabii hizo ni kuhusiana na mlipuko wa gonjwa ambalo kwasasa linajulikana kama Covid-19, kama wengi wanavyojua alitabiri kwa ufasaha kuwa kipindi cha mwaka wa 2020 kutazuka gonjwa linaloshambulia mapafu, ambalo litaathiri karibu dunia nzima, na akaongezea kusema kuwa hata hivyo gonjwa hilo litatoweka lenyewe kama lilivyokuja, na litarejea tena baada ya miaka 10 ndipo litakapotoweka moja kwa moja.

Lakini unabii mwingine alioutoa ambao ndio kiina cha ujumbe wa leo, ni ule aliosema, mwaka alioutaja kama “3020” Kutazuka viumbe wa ajabu duniani, ambao wataitwa “VAMPIRES” ni watu ambao watafufuka, na watakuwa wanaishi kwa kutegemea kunywa damu za watu, watakuwa hawapatani na mwanga, lakini baadaye watauliwa na hali itarejea kama kawaida. Hivyo watu wengi waliposikia hivyo mitazamo yao ikabadilika kuhusu mambo yajayo..

Lakini ulishawahi kujiuliza juu ya nabii nyingine alizowahi kuzitoa huyu mama? Siko kumkosoa lakini lipo japo nataka ujifunze mwisho wa makala hii ..baadhi ya hizo alisema..

Mwaka 2010 kutatokea Aliens (Viumbe kutoka sayari nyingine) duniani..Jambo ambalo halikutokea, mpaka sasa halipo.

Mwaka 2004, alitabiri Osama ameshakufa,.Lakini Osama alikuja kupatikana mwaka 2011 na kuuawa.

Ndani ya kitabu chake kimoja aliandika, chanjo ya ugonjwa wa HIV, itapatikana mwaka 2005. Lakini chanjo hiyo mpaka leo hii haijapatikana.

Na nyingine nyingi, ambazo hatuwezi kuzichambua moja moja kwasababu sio lengo la ujumbe huu kuwakosoa watu, lakini tufumbuke macho, tusipelekwe na kila aina ya mafunuo yanayokuja duniani siku hizi…

Sasa tukirudi kwenye lile la mwaka 3020 alilolisema kuwa kutatokea viumbe wajulikanao kama Vampires..Na hili limewafanya watu wengi waamini kwa asilimia kubwa kwamba watatokea, kwasababu tu lile la ugonjwa ufananao na nimonia (Corona) lilitokea kisahihi.. na wengine wamekuwa na mtazamo mwingine wa kuishi wakidhani kuwa hii dunia itaendelea kuwepo mpaka huo mwaka wa 3000 yeye alioutaja…

Ni vizuri ukafahamu biblia inatukumbusha kwamba hata kama unabii utatolewa na mtu fulani na ukawa sahihi kabisa, bila kuwa na kasoro kasoro lakini kama unakinzana na maagizo ya Mungu, hatupaswi kupokelewa hata kidogo kwani ni wa uongo, (Soma kumbukumbu 13)

Hivyo usikimbilie kuupokea kila unabii ukasema unatoka kwa Mungu, kisa tu umetokea! bila wewe kukaa chini na kuutathimini katika maandiko..

Hizi ni nyakati za mwisho, kuhusu janga hili la Corona wapo wengine wengi sana wametabiri kiufasaha kuhusu juu ya gonjwa hili kama ulikuwa hujui lakini hawakuwa wakristo fuatilia hata habari ya Novel ya the eyes of the darkness, utaona, wapo wengine wengi sana, watafute internet utawaona,.. Lakini Pia Mungu anaweza kumtuma mtu wake kabisa , atoe unabii na ukaja kutimia, na akatoa maagizo yanayokinzana na Neno lake, Kumbe Ni Mungu ndiye aliyemtuma ili akupime moyo wako kama kweli unalishika Neno lake au la!!.. Na kama ukifuata tu, ndio umekwenda na maji.. Hebu tusome kidogo andiko linalozungumzia mambo hayo…

Kumbukumbu 13: 1 “Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu,

2 IKATUKIA HIYO ISHARA AU HIYO AJABU ALIYOKUAMBIA akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo;

3 wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto, kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, yuawajaribu, apate kujua kwamba mwampenda Bwana, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote”.

Sasa tukirudi kwenye maandiko hakuna mahali popote panapotabiri kuhusu ujio wa “Vampires”..Au kutokea kwa viumbe vingine kutoka sayari za mbali (Aliens).. unabii huo ni batili..Hizo ni ndoto za wanasayansi ambazo zinakinzana na Neno la Mungu..

kama hayo yatakuja kutokea basi ungeshayaona kwenye maandiko tangu zamani, kwasababu hakuna jipya chini ya jua..Kwamfano tabiri za kutokea magonjwa ya mlipuko mfano wa tauni, yalitabiriwa hivyo mtu akitabiri kuhusu hilo sio jambo la kushangaza kwasababu biblia ilishaeleza, vile vile matetemeko, au njaa, au vita,manabii wa uongo, wapinga Kristo n.k. yote hayo yapo kwenye maandiko na yalishatabiriwa.. Lakini sio watu wanaofufuka na kunyonya damu za watu, watakaofufuka ni watakatifu tu, na sio kitu kingine chochote..Yesu pekee ndio UFUFUO NA UZIMA(Yohana 11:25), Na yeye peke yake ndiye mwenye funguo za kuzimu na mauti, shetani hana tena hizo funguo, hawezi kumfufua mtu wala kumleta mtu juu kama alishanyang’anywa hayo mamlaka kitambo sana…sasa jiulize atakayewafufua hao mavempire(mazombie) Wanyonye watu damu ni Bwana Yesu?..tafakari..unaona kabisa haingii akilini, ni kinyume na maandiko?…Ufufuo uliotabiriwa ni ufufuo wa wenye haki kwa ajili ya uzima na ufufuo wa waovu kwa ajili ya kuhukumiwa kwa maovu waliyoyafanya, na si kwaajili ya kunywa damu za watu!.

Yohana 5:28 “ Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake.

29 Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu”.

Hivyo jihadhari na udanganyifu wa ndoto za wanasayansi..

Kwa hiyo ndugu kwa maneno mafupi..Ni kwamba tunaishi katika siku za mwisho, na siku yoyote Kristo anarudi kulinyakua kanisa lake.. anayekupa matumaini kuwa kutakuwa na miaka mingine elfu moja ya kuishi mbeleni (1000), anakupoteza, ni agenda za shetani kuwaminisha watu kuwa muda bado sana, Kwamba Kristo bado sana arudi. Ilihali Dalili zote tulizoelezwa na Kristo zimeshatimia..Hivyo ni wakati wa kujiandaa sasa, acha kufuata mafunuo yasiyo dhahiri ya siku hizi za mwisho..Yapo mengi na yataendelea kuwa mengi, kwajinsi siku zinavyozidi kusogea..Ukiyafuata utayumbishwa sana, na kupotezewa mwelekeo wa imani yako kama huna msingi mzuri wa kimaandiko..Hizi ni nyakati za mwisho kweli kweli mpinga-Kristo ameshajiweka tayari kuanza kazi na sio VAMPIRE au ALIENS.

Hivyo Tubu dhambi zako leo, mpokee Kristo, kama hujamwamini, jiweke tayari kwa kurudi kwa pili kwa Kristo duniani.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

KUTAKUWA NA MATETEMEKO YA NCHI, NJAA NA TAUNI.

Kuna ufufuo wa aina ngapi?

BASI TUENDELEE KUMJUA MUNGU,NAYE ATATUJILIA KAMA MVUA YA VULI.

Je! Ni sahihi kuoa/kuolewa na mtu uliyemzidi umri?

MKUMBUKE MKE WA LUTU.

KUZIMU ni mahali pa namna gani, Je! huko wanaishi watu wakifa na kwenda kupata mateso au ni vinginevyo?

Rudi Nyumbani:

Print this post