Ni dhambi kuota unafanya kitu kiovu kama uzinzi, uuaji, wizi, uasherati, au ulevi?
JIBU: Ndoto huja pasipo hiari ya mtu..hakuna mtu anayeweza kupanga aote nini leo au kesho…Zinakuja tu zenyewe pasipo mtu kupanga….Lakini ndoto nyingi ni MATOKEO ya kitu Fulani ambacho kinaendelea katika maisha ya mtu.
Kwamfano umelala na njaa..usiku utajikuta unaota unakula!,(Isaya 29:8) umeshinda ukifanya shughuli Fulani siku nzima ukilala utajiona unaendelea kufanya vile vitu katika ndoto…kabla ya kulala ulikuwa unatazama kitu Fulani kwenye luninga au mtandaoni ambacho kimegusa hisia zako…utakapolala ni rahisi sana kukiota kile kitu
Vivyo hivyo..umekuwa karibu na mtu Fulani kwa muda mrefu katika maisha yako ghafla akaondoka au akafariki..Ni lazima utakuwa unamwota ota mara kwa mara. Kwahiyo ndoto nyingi ni matokeo ya kitu Fulani ambacho kinaendelea katika maisha ya mtu..Ndio maana biblia imeweka wazi jambo hilo katika..
Mhubiri 5:3 “Kwa maana ndoto huja kwa sababu ya shughuli nyingi; na sauti ya mpumbavu kwa njia ya wingi wa maneno”.
Kwahiyo ukiota unaiba na ndoto inajirudia rudia ni matokeo ya kitu ambacho kinaendelea katika maisha yako… “Hiyo ndoto uliyoiota sio dhambi”…lakini ni ujumbe kwamba katika maisha yako kuna uwezekano bado kuna vimelea vya wizi…hivyo zidi kuyachunguza kwa undani maisha yako na kuyatakasa…Ukiona unafanya uasherati, ni hivyo hivyo…chunguza mtindo wa maisha yako unayoishi, labda bado unatabia ndogo ndogo pengine unaridhia picha chafu au video chafu ambazo unapishana nazo kwenye mitandao, au bado unayaendekeza mawazo machafu ya zinaa yanapokujia kichwani mwako..kwahiyo ndio maana zinaendelea mpaka kwenye kichwa chako unapolala..
Na jambo muhimu la kufahamu ni kwamba kama ulikuwa umetoka kwenye dunia moja kwa moja ukaokoka…Bwana anakuwa amekusamehe maisha yako na dhambi zako, lakini madhara ya dhambi katika maisha yako hayataondoka siku ile ile unapookoka..yataondoka kidogo kidogo mpaka mwisho wake kuisha kabisa…yaani kama ulikuwa ni mzinzi wa kupindukia kabla ya kuokoka…
Siku ile unapookoka Roho Mtakatifu anaiondoa ile tabia ndani yako…lakini utaendelea kuvuna matokeo ya uzinzi wako kwa kipindi Fulani, ndio hapo hayo mandoto ya mambo uliokuwa unayafanya nyuma yanaweza kuendelea kwenye kichwa chako kwa kipindi kadhaa (Hayo ndio madhara ya dhambi)…
Lakini yajapo hayo baada ya kumwamini na kupokea Roho Mtakatifu usiogope!.. unapoota unafanya hayo mambo katika ndoto baada ya kumwamini Yesu, na ilihali hayo mambo katika maisha yako halisi umeshayaacha kitambo…unachotakiwa kufanya ni kuikataa hiyo hali…na kusema mimi sio huyo!!!..usiruhusu kuikubali hiyo hali kwamba ni wewe…Ikatae!, usikubali kukata tamaa wala kuwa mdhaifu…na itafika kipindi Fulani hayo mandoto yatakwisha kabisa….
Wengi wanapofikia hatua kama hii, wamemwamini Yesu, wamekwenda kubatizwa na wamepokea Roho Mtakatifu lakini wanapojikuta baada ya siku kadhaa wanaota wanafanya mambo ambayo wameshayatubia, wengi wanarudi nyuma na kuvunjika moyo na kuhisi hawakutubu vizuri…Na hapo shetani anachukua nafasi ya kuwarudisha tena katika mambo waliyokuwa wanayafanya, na mtu anasimama kurudia rudia kuokoka hata mara 100 katika maisha yako..
Na jambo lingine ambalo litakusaidia kuepukana kwa haraka na ndoto za namna hiyo, ni kuwa mwombaji na mtafakariji wa Neno, walau Sali kila siku lisaa limoja, kama Bwana Yesu alivyotuagiza, lakini kama utakuwa maisha yako ya kuomba, hali hizo zitaendelea kukurudia rudia bila kikomo..Maombi ni ngao ya majaribu ya shetani. Ukisema umeokoka halafu maombi yanakushinda, basi bado hujaokoka.
Hivyo kwa ujumla dhambi ni mbaya na ina madhara! Na inatesa hata baada ya kuiacha!…Ukiingia mkataba na shetani, hutatoka kirahisi. Ni sawa na gari lililokuwa kwenye mwendo likapiga breki ghafla..Matairi yatasimama, injini itasimama lakini gari litazidi kuendelea mbele kidogo…na dhambi ni hivyo hivyo..utaacha uasherati, ulevi, na kila kitu siku ile unaokoka lakini mambo hayo yataendelea katika ulimwengu wako wa ndoto, lakini ukizingatia hayo tuliyoyasema utaepukana na hizo hali kwa haraka sana.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp
Mada Nyinginezo:
KUOTA UNAFANYA TENDO LA NDOA.
Kuota unafanya Mtihani.
KUOTA UNAOLEWA/UNAOA.
KUOTA UNAKULA CHAKULA.
KUOTA UNANG’OKA MENO.
Rudi Nyumbani:
Print this post