Category Archive Home

NINI MAANA YA KUWA MKRISTO?

Jina la Bwana Yesu Kristo libarikiwe.

Je unajua ni kwanini Bwana Yesu aliwaagiza Mitume wake pamoja na sisi wote kwamba tuende ulimwenguni kote tukawafanye watu wote kuwa WANAFUNZI na si WAKRISTO? (Mathayo 28:19).

Je! Unajua neno Ukristo mara ya kwanza lilizaliwa wapi?

Tusome Matendo 11:26..

Matendo 11:26 “hata alipokwisha kumwona akamleta Antiokia. Ikawa kwa muda wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja na kanisa na kuwafundisha watu wengi. Na WANAFUNZI waliitwa WAKRISTO kwanza hapo Antiokia”.

Umeona hapo?..Maana yake kabla akina Petro, akina Yohana, na wengine wote waliomwamini Yesu kujulikana kama wakristo, walikuwa wanajulikana kama wanafunzi, hapo kabla.

Maana yake kuwa mkristo ni kuwa MWANAFUNZI WA YESU. Hili ni jambo la muhimu kujua sana.

Sasa swali tunakuwaje wanafunzi wa Bwana Yesu?..au watu wa kanisa la kwanza walikuwa wanafanyikaje kuwa wanafunzi?.

Bwana Yesu alitoa vigezo..Katika kitabu cha Luka..

Luka 14:27 “Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu”

Sasa tukirudi katika Matendo biblia inasema “Wanafunzi waliitwa wakisto kwa mara ya kwanza hapo Antiokia”..Maana yake mkristo yeyote ni mwanafunzi.

Kwa mantiki hiyo basi sentensi ya Bwana aliyoisema katika Luka 14:27 ni sahihi kabisa kuiweka hivi…

“Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa MKRISTO”.

Umeona hapo?..Hebu tosegee tena mbele kidogo..

Luka 14:26 “Makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia,

26 Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake;  naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu”.

Maana ya hiyo sentensi ni kwamba..

26 “Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, HAWEZI KUWA MKRISTO”.

Kuchukia wazazi kunakozungumziwa hapo kuwachukia kwa chuki, bali kuchukia mawazo yao au mipango yao inayokinzana na mapenzi ya Mungu, kwamfano mzazi au ndugu anakuambia inakupasa urithi mikoba ya uchawi, au urithi chuki zake kwa mtu fulani, hapo Bwana anasema hatuna budi kuyachukia hayo mawazo na kuyakataa na kutoshirikiana nao hata kama watakutenga..hapo ni sawa na umewachukia ndugu zako, Kristo anakokuzungumzia..na ndio vigezo vya kuwa mwanafunzi yaani MKRISTO.

Tusogee tena mbele kidogo..

Bwana anasema..

Luka 14:33 “Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu”.

Kufuatia Matendo 11:26 inayosema kuwa Wanafunzi ndio wakristo..basi ni sahihi kabisa kuyaweka haya maneno ya Bwana katika hii Luka 14:33 hivi…

“Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, HAWEZI KUWA MKRISTO”.

Hiyo ikifunua kuwa kumbe miongoni mwa lile kundi lote lililokuwa linamfuata Bwana, wakristo walikuwa ni wachache sana..yaani ni wale wanafunzi wake tu, wa kike na wakiume, ambao walijikana nafsi na kujitwika misalaba yao na kumfuata Bwana Wengine wote hawakuwa wakristo.

Na maandiko yanasema Yesu ni yeye yule, jana na leo na hata milele. (Waebrania 13:8).

Ikiwa na maana kuwa kama vigezo vyake vya mtu kuwa mwanafunzi (yaani mkristo) vilikuwa ni kujikana nafsi na kubeba msalaba…basi vitakuwa ndio hivuo hivyo hata leo, kwasababu yeye ni yule yule habadiliki..

Waebrania 13:8 “Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele”.

Je! Wewe ni MKRISTO?…Umejikana nafsi? Umeuchukia ulimwengu na kuuacha?..kama bado basi fahamu kuwa wewe si mkristo, haijalishi unasali katika dhehebu kubwa au umebatizwa, bado sio mkristo.

Kama bado unalewa, au unazini, au unavaa nguo za kubana na kuonyesha maungo yako, bado sio mkristo..

Amua leo kujikana nafsi na kuubeba msalaba wako, wacha dunia ikuone umechanganyikiwa lakini wewe unajua unayafanya mapenzi ya Baba yako aliye mbinguni..

Bwana Yesu alisema..“Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake? ( Marko 8:36 ).

Itakufaidia nini uonekane wa kisasa halafu huendi mbinguni??

Bwana atupe macho ya kuona.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp


Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

Print this post

Kibiriti ni kitu gani? kama kinavyozungumziwa kwenye maandiko?

Kibiriti tofauti na kinavyojulikana leo kwamba, ni kipande kidogo cha boksi kilichojaa chiti zinazotumika katika kuwashia moto. Lakini tafsiri halisi ya “kibiriti” au “kiberiti” sio hiyo. Kibiriti ni aina ya mawe, yanayopatikana duniani, yajulikanayo kwa jina hilo la  kibiriti au Salfa..Kwa lugha ya kiingereza ni “Sulfur”.

Mawe haya kwa mwonekano yana rangi ya “manjano iliyofifia”..Tabia ya mawe haya ni kwamba yanawaka “kiwepesi” kama vile mafuta ya taa yanavyowaka kiwepesi yanapokutana na moto.. kadhalika na mawe haya ni myepesi kuwaka yanapokutana na moto.

Katika hali yake ya asili yanapokutana na moto kidogo tu! Yanaanza kuyeyuka taratibu taratibu na mwisho kuwa Uji mzito mweusi, kama tope!..ambao ni wa moto sana, usiozimika kirahisi, mfano wa Magma ya volkano. Lakini pia jiwe hilo hilo, likipelekwa kiwandani linaweza kuchanganywa na malighafi nyingine kutengeneza bidhaa nyingine zinazowaka kirahisi kama “Njiti za kiberiti” au “Unga wa risasi”. Lakini katika hali yake ya asili jiwe hilo la Salfa(kiberiti) likichomwa bila kuchanganywa na kitu kingine chochote, linayeyuka na kuwa tope zito la moto.

Lakini tukirudi kwenye biblia tunana sehemu kadhaa jiwe hili la Salfa(kiberiti) likitajwa.

Sehemu  ya kwanza lilitajwa kipindi cha Sodoma na Gomora, wakati Bwana alipoiangamiza miji ile kwa moto.  Biblia inasema moto na kibiriti vilishuka kutoka mbinguni.

Luka 17:28 “Na kadhalika, kama ilivyokuwa katika siku za Lutu, walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakinunua na kuuza, wakipanda na kujenga;

29 lakini siku ile Lutu aliyotoka Sodoma KULINYESHA MOTO NA KIBIRITI kutoka mbinguni vikawaangamiza wote”.

Kiberiti kinachozungumziwa hapo ni hayo mawe ya Salfa yaliyochanganyikana na moto, ambayo yalishuka kutoka juu..Na yaliposhuka moja kwa moja yakaanza kuyeyuka na kuwa TOPE ZITO JEUSI kama la volcano na kuchoma kila kitu.

Mpaka hapo utakuwa umeshaanza kuelewa kwanini Jehanamu ya moto, sehemu nyingine inafahamika kama ZIWA LA MOTO. Kwasababu huwezi kutaja neno ziwa bila kumaanisha “kimiminika” hivyo ziwa la moto maana yake ni “ni moto mwingi ulio katika mfumo wa kimiminika” mfano wa huo moto wa KIBIRITI (Salfa).

Ufunuo 21:7 “Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu.

8 Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ZIWA LIWAKALO MOTO NA KIBERITI. Hii ndiyo mauti ya pili”.

Utasoma tena neno hilo katika..

Ufunuo 14:9 “Na mwingine, malaika wa tatu, akawafuata, akisema kwa sauti kuu, Mtu awaye yote akimsujudu huyo mnyama na sanamu yake, na kuipokea chapa katika kipaji cha uso wake, au katika mkono wake,

10 yeye naye atakunywa katika mvinyo ya ghadhabu ya Mungu iliyotengenezwa, pasipo kuchanganywa na maji, katika kikombe cha hasira yake; NAYE ATATESWA KWA MOTO NA KIBERITI mbele ya malaika watakatifu, na mbele za Mwana-Kondoo.

Na pia Ufunuo 19:30 inazungumzia jambo hilo hilo…

Ufunuo 19:20 “Yule mnyama akakamatwa, na yule nabii wa uongo pamoja naye, yeye aliyezifanya hizo ishara mbele yake, ambazo kwa hizo aliwadanganya watu wale walioipokea ile chapa ya huyo mnyama, nao walioisujudia sanamu yake; hao wawili wakatupwa wangali hai katika lile ZIWA LA MOTO LIWAKALO KWA KIBERITI;

Na mwisho neno hilo limetajwa katika

Ufunuo 20:10 “Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, AKATUPWA KATIKA ZIWA LA MOTO NA KIBERITI, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo. Nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele”.

Sasa kwanini biblia imesema shetani na malaika zake WATATESWA katika Moto na Kiberiti, na SI WATACHOMWA TU!!.

Ni kwasababu Moto wa kiberiti ni tofauti na moto wa kawaida, moto wa kawaida wenyewe unaunguza tu! Na kuteketeza, lakini moto ulio katika mfumo wa kimiminika, tena kama uji uji huo ni unatesa.. Ndio maana kuungua kwa moto wa kawaida ni heri kuliko kuungua kwa vimiminika kama maji au uji..

Wanaofanya kazi za kuyeyusha Salfa(kibiriti) wanakuwa katika uangalifu mkubwa sana kwasababu wanasema moto ule ni mbaya kuliko moto mwingine wowote kwasababu “ule uji wake unapogusa mwili unakuwa unagandamana na ngozi” kwahiyo ili kuuondoa ni lazima ngozi ichubuke, na unakuwa na maumivu makali sana yanayotesa. Ndicho kilichowatokea watu wa Sodoma na Gomora, (walikufa kwa mateso na si kwa kuchomeka tu basi!.)

Na ndicho kitakachowakuta watu wote watakaotupwa katika lile ziwa la Moto.. watateswa katika ziwa la moto.

Swali ni je!, umempokea Yesu?.. Maandiko yanasema.. “Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ZIWA LIWAKALO MOTO NA KIBERITI.”

Je na wewe ni miongoni mwa wachukizao?, ni miongoni mwa wachawi, ni miongoni mwa wazinzi na waabudu sanamu?. Kama ndio!, basi tubu leo kwasababu Neema ya Kristo bado ipo, Ziwa la moto kaandaliwa shetani na malaika zake lakini si sisi!, lakini endapo tukiasi kama shetani alivyoasi basi na sisi tutaadhibiwa vile vile kama wao katika ziwa la moto.

Huko ni sehemu ya Mateso, moto ule ni kwa lengo la kutesa, na sio kuchoma tu!.

Bwana atusaidie tusifike huko, bali tuishi maisha ya kumpendeza yeye na kuyaishi maagizo yake.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

(Moto na kiberiti, www.wingulamashahidi.org)

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Kwanini Mungu awachome watu kwenye ziwa la moto na hali yeye ndiye aliyewaumba?

Noeli ni nini, na je! Neno hili linapatikana katika biblia?

KUWA MAKINI NA MITANDAO, NI SHIMO REFU.

OLE WAKO KORAZINI NA BETHSAIDA.

YEYE ALIYEUWASHA HUO MOTO LAZIMA ATALIPA.

Rudi nyumbani

Print this post

JE! USIPOTIMIZA NADHIRI ZAKO ZOTE KWA BWANA. HAWEZI KUKUSAMEHE?

Hili ni swali ambalo linaulizwa na wengi,  hususani watu ambao walimwekea Mungu nadhiri huko nyuma lakini mwisho wa siku wamejikuta hawawezi kuzitoa.

Sasa kabla ya kwenda kuona kama msamaha upo au haupo, Jambo la kwanza unalopaswa kufahamu kuhusu nadhiri ni kwamba lile ni  tendo la hiyari ambalo mtu anamwekea Mungu mwenyewe, na hapo ndipo Mungu anataka umakini sana kwasababu hakumlazimisha kufanya hivyo.

Biblia inasema ni heri, usiweke kabisa nadhiri kuliko kuiweka, halafu ukashindwa kuitoa,

Mhubiri 5: 4 “Wewe ukimwekea Mungu nadhiri, usikawie kuiondoa; kwa kuwa yeye hawi radhi na wapumbavu; basi, uiondoe hiyo uliyoiweka nadhiri.

5 Ni afadhali usiweke nadhiri, Kuliko kuiweka usiiondoe”.

Unaona hapo? Mungu anasema yeye hawi radhi na wapumbavu. Ikiwa na maana kuwa nadhiri ambayo haitolewi kwa wakati, Ni haki ya Mungu kumwadhibu huyo mtu kwa jinsi atakavyo yeye.

Kwahiyo kabla hujatamka nadhiri yoyote kwa kinywa chako mbele za Mungu, hakikisha kwanza unaelewa unachokitamka, na una uwezo wa kukisimamia.Biblia inasema..

Mithali 20: 25 “Ni mtego, mtu aseme kwa haraka, Kitu hiki ni wakfu; Na baada ya kuweka nadhiri kuuliza-uliza habari”.

Sasa tukirudi kwenye kiini cha somo, Je! Kutotimiza nadhiri zako, Mungu hawezi kukusamehe?

Tukumbuke katika biblia ni dhambi moja tu isiyosameheka kwa Mungu, na dhambi yenyewe ni “Kumkufuru Roho Mtakatifu”  Lakini hiyo haimaanishi kuwa adhabu za dhambi nyingine hazipo hapana.. Kuna dhambi ambazo Mungu atakusamehe bila adhabu, lakini pia zipo dhambi ambapo Mungu atakusamehe pamoja na adhabu. Kwa urefu wa somo hilo fungua hii link>>>>>> https://wingulamashahidi.org/2018/07/17/dhambi-ya-mauti/

Sasa ikiwa mtu hajamtimizia Mungu nadhiri zake, anaweza akatubu na pengine Mungu akamsamehe kabisa na mbinguni akaenda, lakini adhabu ya kosa lake, bado akaitumikia hapa hapa duniani, adhabu inaweza ikawa pengine hata kifo,n.k.

Lakini bado tukirudi katika biblia tunaona wapo watu ambao walihalifu nadhiri zao, lakini hawakuadhibiwa na Mungu, mmojawapo ni Daudi wakati ule anataka kwenda kumuua Nabali, aliapa kwa Mungu kwamba kama hatamuua Nabali na nyumba yake yote, basi Mungu amfanyie yeye hivyo . Lakini tunaona hakumuua Nabali alipofika katika nyumba ile, na Mungu vilevile hakumuua Daudi na nyumba yake kwa kutotimiza nadhiri zake. Hizo ndizo zinazojulikana kama nadhiri wa wapumbavu.

1Samweli 25: 22 “Mungu naye awafanyie hivyo adui za Daudi, na kuzidi, nikimwachia katika wote walio wake hata mtoto mume mmoja, kutakapopambazuka asubuhi”.

Sehemu nyingine, utaona ni wakati Sauli anapigana na wafilisti naye pia aliweka nadhiri kuwa mtu yeyote asionje chochote mpaka atakapomaliza kupigana na wafilisti na kuwashinda, atakayeonja atauawa lakini mwanae Yonathani, hakusikia agizo hilo, yeye akala, na Sauli alipopata taarifa akataka kumwangamiza, lakini Israeli wakamzuia, kwasababu yeye ndiye aliyeleta wokovu katika taifa. Na baada ya hapo hatuoni kama Mungu alimwangamiza Sauli kwa kuhalifu agizo lile.(Soma 1Samweli 14)

Lakini tunaona pia kulikuwa na mwamuzi mwingine aliyeitwa Yeftha, yeye alimwekea Mungu nadhiri kuwa atakaporudi kutoka vitani na ushindi, basi chochote kitakachotokea cha kwanza mbele yake, atamtolea Mungu kama sadaka ya kuteketezwa. Hakufikiria kwamba anaweza kutokea mtu mbele yake..

Lakini kweli Mungu alipomfanikisha katika vita, kitu cha kwanza kutokea mbele yake, hakikuwa ng’ombe, au mbuzi, bali binti yake wa pekee. Hivyo ikambidi aende kumchinja mwanawe na kumtoa kafara kwa Mungu, japo ambalo ni kinyume kabisa na maagizo ya Mungu, na ni machukizo. Yeftha Alikuwa na uwezo wa kuizuia nadhiri yake ya kipumbavu, kama alivyofanya Daudi au Sauli, lakini alitimiza nadhiri isiyokuwa na maana yoyote mbele za Mungu.

Hivyo, Mungu anaweza akaadhibu au asiadhibu, yote yapo katika uwezo wake mwenyewe..

Lakini katika yote, Mungu tangu zamani kwa hekima yake alishaona kuwa wapo watu wake, ambao watakuja kutamka nadhiri zao bila hata ya kufikiria, na ili kuwaepusha na adhabu, akampa maagizo Musa, juu ya nadhiri za wapumbavu kama hizo akasema..

Walawi 5:4 “au, kama mtu akijiapisha, kwa kutamka haraka kwa midomo yake, kutenda uovu, au kutenda mema, neno lo lote mtu atakalolitamka kwa kiapo pasipo kufikiri, na neno hilo likamfichamania; hapo atakapolijua, ndipo atakapokuwa na hatia katika mambo hayo mojawapo;

5 kisha itakuwa, hapo atakapokuwa na hatia katika mambo hayo mojawapo, ndipo atakapoliungama jambo hilo alilolikosa;

6 naye atamletea Bwana sadaka yake ya hatia kwa ajili ya hiyo dhambi yake aliyoifanya, mwana-kondoo wa kike, au mbuzi mke, kutoka katika kundi lake, kuwa ni sadaka ya dhambi; kisha kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya hiyo dhambi yake”.

Umeona?, Mtu kama huyo ambaye alitamka tu maneno bila kufikiri hatma yake itakuwaje mbeleni, pengine mwingine alisema mimi sitaoa au kuolewa maisha yangu yote, bila kupiga gharama zake. Mungu alimwambia Musa, mtu huyo atubu, kisha sio kutubu tu, bali aambatanishe na sadaka yake ya makosa kama vile atakavyoelekezwa na kuhani.

Hii ikiwa na maana, hata sasa wapo watu waliotamka nadhiri zako mbele za Mungu, lakini sasa wameshindwa kuzitoa, jambo la kwanza wanalopaswa kulifanya  hapo ni kutubu kwa kumaanisha kabisa, sio kutubu kwa dakika mbili au tatu, hapana ni kulia kwa kumaanisha mbele za Mungu kwa kipindi fulani (ukikumbuka kuwa Mungu hawi radhi na wapumbavu, anaweza kukuondoa duniani kwa kosa hilo tu)..Kisha baadaye ukishamaliza maombi yako ya toba ya muda mrefu, andaa sehemu nono ya ulichonacho nacho (yaani sadaka), kisha kipeleke madhabahuni pa Mungu kwa ishara ya unyenyekevu kwa hofu nyingi.

Na baada ya hapo Mungu atakusamehe.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

Print this post

REKEBISHA YAFUATAYO ILI UCHUMI WAKO UKAE SAWA.

Jina la Bwana Yesu libarikiwe, karibu tujifunze biblia, Neno la Mungu wetu.
Leo tutajifunza, mambo Matatu ambayo, kama Mkristo ukiyarekebisha hayo basi uchumi wako utaimarika zaidi.

1. KUWA MWAMINIFU KWA MUNGU WAKO.

Dawa ya kwanza ya mafanikio yoyote yale, yawe ya kimwili au kiroho, ni kuwa MWAMINIFU KWA BWANA.

Mithali 3:7
“ Usiwe mwenye hekima machoni pako;
Mche BWANA, ukajiepushe na uovu.

8 Itakuwa afya mwilini pako,
Na mafuta mifupani mwako.

Kumcha Bwana ni kuishi maisha matakatifu na yanayompendeza yeye, ambayo Nuru yako inakuwa inaangaza kila mahali.
Jambo moja kubwa wakristo wengi wasilolijua ni kwamba, tumewekwa ulimwenguni ili tuhubiri injili, licha ya kwamba Mungu anataka sisi tupate faida katika mambo yetu kutoka kwake, lakini pia Mbingu inategemea kupata faida kutoka kwetu.. Na faida yenyewe ni sisi kuwavuta wengine waingie katika ufalme.

Kwahiyo maana yake ni kwamba kama wewe unafanya biashara, au kazi yoyote ya kuajiriwa au kujiajiri.. Mungu anategemea maisha yako yawe sababu ya kuwavuta wengine.

Hivyo Bwana akikuamini, atakuvutia watu wengi kwako, kama ni wateja au watu wa fursa wakujie, lengo si tu waje kununua bidhaa zako, au kukupa wewe fursa, bali Mungu anawasogeza kwako ili wapate kuiona nuru yako na wamgeukie Mungu na kutubu..Hivyo wewe unafanyika daraja la wao kumfikia Mungu zaidi.

Lakini kama wewe maisha yako hayana ushuhuda wowote,maana yake ni maisha ya uzinzi, ya wizi, ya ulevi, utukanaji, umbea, usengenyaji n.k.

maana yake Mungu akikuletea watu, ni sawa na kampelekea shetani kondoo..Hivyo ili awalinde watu wake wasizidi kupotea, anazuia wateja wasije kwako, kwasababu utawaharibu kwa tabia zako..na Mungu hapendi watu wake wapotee.

Atawazuia wasije kwako, na atawapeleka kwa watu wengine wenye staha zaidi..Huku nyuma wewe utabaki kufikiri umelogwa, kumbe ni wewe mwenyewe umejiharibu kwa kutokuwa mwaminifu kwa Mungu wako.

Mathayo 5:14
“Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima.

15 Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani.

16 Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni”.

Angaza Nuru yako ili milango ifunguke.

2. KUWA MWAMINIFU KATIKA KAZI UNAYOIFANYA.

Hili ni jambo la pili ambalo, ni muhimu kulijua.

Wengi wetu hatujui kuwa Mungu si Mungu wa kuwadhuru watu, bali wa kuwapatia watu mema.. Mteja yeyote Mungu anayemleta kwako, ni kwasababu Mungu anataka apate huduma bora ya viwango, ili aweze kumshukuru Mungu baada ya hapo, na Mungu apokee shukrani zake..

lakini hawezi kumleta kwako wewe unayeuza kitu kilichoisha muda wake wa matumizi (kime-expire). Hapo Mungu atakuwa muuaji na mkatili na si Mungu mwenye fadhili..

Alisema..

Mathayo 7:9
“9 Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe?

10 Au akiomba samaki, atampa nyoka?

11 Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?”

Hiyo ndio maana watu wateja hawawezi kuja kwako, kwasababu Mungu hawezi kuwaongoza watoto wake kwenda kula sumu, au vitu vilivyo chini ya ubora..vinginevyo atakuwa mwongo hapo aliposema.. “Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?”.

Hebu tengeneza picha wewe umeamka asubuhi, na kumwomba Baba akulinde na yule mwovu na pia akupe riziki njema..halafu unatoka hapo Mungu anakuongoza kwenda kununua Soda iliyo-expire! Kwenye duka la mtu fulani…huyoo Mungu si atakuwa mkatili sana?..

Hivyo ili Mungu kumpa mtoto wake kipawa chema sawasawa na Neno lake hilo, atamwepusha kuja kwenye duka lako, au kukupa wewe ajira..badala yake anampeleka kwenye duka lingine au kumpa mtu mwingine ajira ambaye atatoa huduma iliyo bora na kuleta faida katika ufalme wa mbinguni.

Hiyo ndio sababu wakristo wengi Mungu anaifunga milango ya riziki katika biashara zao, au katika mambo yao mengine na kuishia kudhani wamelogwa, na kuzunguka huku na huko kutafuta maombezi kumbe ni kwasababu wao wenyewe sio waaminifu katika kazi zao na hawatoi huduma iliyo bora!.

Na vile vile kuwa mwaminifu katika kumtolea Mungu, maandiko yanasema wote wasiomtolea Mungu zaka ni wezi, wanamwibia Mungu..hivyo Mungu hawezi kuwabariki wezi.

Malaki 3:8 “Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu.

9 Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote”

Mithali 3:9 “Mheshimu BWANA kwa mali yako,Na kwa malimbuko ya mazao yako yote.

10 Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi, Na mashinikizo yako yatafurika divai mpya”.

3. IMARISHA KAZI YAKO, AU UJUZI WAKO.

Hili ni jambo lingine pia la muhimu kujua.
Wengi wetu hatupendi kuziimarisha kazi zetu, au ni walegevu katika kuziimarisha, wakati mwingine tukidhani si mpango wa Mungu.

Lakini leo nataka nikuambie kuwa kuiimarisha kazi yako, ni jambo la muhimu sana na la kimaandiko.

Kila siku buni na tafuta mbinu mpya na ongeza ujuzi katika shughuli unayojishughulisha nayo au unayoifanya..hayo ni mapenzi ya Mungu pia!

Bwana Mungu baada ya kuimaliza kazi yake ya uumbaji pale Edeni, alipumzika, lakini baada ya kipindi fulani alinyanyuka tena na kusema..”Si vyema mtu huyu awe peke yake nitamfanyizia msaidizi wa kufanana naye”.Ndipo akamletea Hawa kama msaidizi.

Kadhalika na sisi hatuna budi kusema siku zote “si vyema kazi hii ikabaki yenyewe, basi niongeze nyingine kama hii, na nyingine na nyingine”.

Si vyema kazi hii iwe kama ilivyokuwepo mwaka jana, basi nitaiimarisha hivi na hivi..si vyema ujuzi huu nilionao nikaendelea nao, basi nitauongeza tena na tena..

Kwa kufanya hivyo, Bwana atakubariki kwasababu na yeye pia anafanya matengenez kila siku katika maisha yetu.
Haya ndiyo mambo makuu matatu yanayozuia uchumi wetu kusonga mbele.

Na yaliyo ya muhimu zadi ni hayo mawili ya kwanza.

Tofauti na wengi wanaofikiri kwamba matatizo mengi yanasababishwa na uchawi.

Uchawi wa kwanza shetani anaologa nao mtu sio kuifanya biashara yake isifanikiwe..anachokifanya cha kwanza, na tena anakifanya kwa bidii ni kumfanya MTU AWE MTENDA DHAMBI!.

Kwasababu anajua Dhambi ndio mzizi na chanzo chaatatizo yote na shida na dhiki.

Mtu aliyejitenga na dhambi kamwe shetani hamwezi, na wala hakuna uchawi mwingine wowote utakaoweza kufanya kazi juu yake.

Lakini kama mtu hajajitenga na dhambi, basi uchawi mwingine wowote utafanya kazi juu yake na kumletea madhara.

Swali ni je?

WEWE NI MWAMINIFU KWA MUNGU?…NA JE! NI MWAMINIFU KATIKA KAZI YAKO?..NA JE UMEJITENGA NA DHAMBI?

Kumbuka hakuna mtu yeyote kwa nguvu zake anaweza kuishinda dhambi, Bali tunaishinda dhambi kwa Kumwamini kwanza Bwana Yesu, kwamba yeye ni Bwana na Mwokozi na anaweza kutusamehe dhambi zetu na kutuosha..

Kwa kumwamini huko, na kubatizwa basi yeye mwenyewe anaingia ndani yetu, na kutupa huo UWEZO WA KIPEKEE WA KUSHINDA DHAMBI, ambao unatufanya kuwa Wana wa Mungu.

Yohana 1:12 “ Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake”.

Uwezo huo unatufanya tuwe watu wengine tofauti na tulivyokuwa hapo kwanza..Ndio hapo zile pombe tulizokuwa hatuwezi kuziacha ghafla tunajikuta tunaweza kuziacha, ule uasherati tuliokuwa tunaona ni mgumu kuuacha tunajikuta tunaushinda, yale matusi ambayo tulikuwa tunaona ni mepesi kuyatamka ulimini mwetu tunajikuta hatuyatoi tena vinywani mwetu n.k.

Bwana atubariki.

Maran atha!

Group la whatsapp Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Tafadhali washirikishe na wengine habari

hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp


Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

Print this post

Lumbwi ni nini katika biblia?

Lumbwi ni jina lingine la mnyama anayeitwa  KINYONGA.

Katika biblia utamsoma kwenye kifungu hiki..

Mambo ya Walawi 11:29-30
[29]Tena katika vitu vile vitambaavyo, vitambaavyo juu ya nchi, hivi ni najisi kwenu; kicheche, na panya, na mjombakaka, kwa aina zake,
[30]na guruguru na kenge, na mjusi na goromoe, na lumbwi.
[31]Wanyama hao ndio walio najisi kwenu katika hao watambaao; awaye yote atakayewagusa, wakiisha kufa, atakuwa ni najisi hata jioni.
Lumbwi /kinyonga ni mmoja wa wanyama ambao walikuwa najisi kuliwa au kuguswa mizoga yake.
Unaweza ukajiuliza ni kwanini Mungu amweke kama kundi la wanyama najisi ni kwasababu ya tabia yake ya kujibadilisha badilisha kutokana na mazingira.
Na hata leo hii wapo watu ambao Mungu anawaona ni vinyonga rohoni. Na hivyo sikuzote wanakuwa najisi mbele zake.
Utakuta leo anatembea na Mungu vizuri lakini akikutana tu na watu wa kidunia anakaa kama mtu wa kidunia..au leo anamsifu Mungu kweli katika Roho kesho yupo disco anamwimbia shetani na kumchezea kwa shangwe kabisa..ni mtu ambaye anabadilika kutokana na mazingira. Na hiyo ni hatari sana.
Bwana atufumbue macho yetu..tusiwe wakina lumbwi. Tumfuate Kristo kila mahali..tusibadilishwe na mazingira yoyote..viwango vyetu viwe vilevile bila kujali tunapitia nini sasa, moto au baridi. Tuwe walewale kwa Bwana.
Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

ZIKUMBUKE FADHILI ZA MUNGU

Biblia inamaanisha nini inaposema “Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake”?

Wibari ni nani?(Mithali 30:26)

POPOBAWA NI KWELI YUPO?

Rudi nyumbani

Print this post

Mizimu ni nini?

Ni kweli mizimu ipo?, Na tunawezaje kujihadhari nayo?.


Katika tafsiri inayojulikana na wengi ni kwamba Mzimu/Mizimu ni roho za watu waliokufa ambazo zinaweza kurudi na kuwatokea wengi.

Roho hizo zinaweza kurudi zenyewe au kurudishwa na mtu, kwa lengo fulani, aidha kutatua tatizo lililoshindikana katikati ya mtu au jamii ya watu, au kujilipiza kisasi kwa mambo aliyofanyiwa mtu huyo kabla ya kufa.

Lakini je! Kibiblia MIZIMU ni kweli ipo?

Jibu ni la! Hakuna roho yoyote ya mtu aliyekufa, inayoweza kurudi yenyewe au kurudishwa na mtu, na kisha kutatua jambo fulani la kimaisha.

Jambo hilo liliwezekana kwa sehemu katika agano la kale kabla ya Bwana Yesu kuja, shetani alikuwa na uwezo wa kuzipandisha juu za watu waliokufa. Utaona katika maandiko aliweza kumpandisha juu nabii Samweli (1Samweli 28:11-14).

Lakini katika agano jipya, baada ya Bwana Yesu kushuka kuzimu na kuzichukua zile funguo za mauti na kuzimu, ambazo mara ya kwanza zilikuwa mikononi mwa shetani, kukawa kuanzia huo wakati na kuendelea hakuna yeyote anayeweza kuzipandisha juu roho za watu waliokufa..

Hata shetani mwenyewe hawezi tena, kwasababu funguo za kuzimu na mauti anazo Kristo mwenyewe..yeye ndiye anayewamiliki wafu wote, wema na waovu.

 Warumi 14:9 “Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia”.

Sasa swali linakuja, kama wafu hawawezi kurudi kama mizimu, hivyo tunavyoviona, au tunavyovisikia vikiwatokea watu vikiwa na sura za wapendwa wao waliowahi kuishi ni vitu gani?

Jibu rahisi ni MAPEPO yaliyojigeuza na kuvaa sura za watu waliokufa.

Maandiko yanasema shetani anaweza kujigeuza akawa kama Malaika wa Nuru, atashindwaje kujigeuza na kuvaa sura ya mtu fulani aliyekufa?. Ni kitu kirahisi sana kwake.

2 Wakorintho 11:14
“Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru”.

Kwahiyo shetani na mapepo yake wanachokifanya ni kuvaa sura za watu waliokufa na sauti zao, na kuigiza kama ndio wale watu halisi, na watu wanapowaona au kuwasikia wanaamini ni wafu wao wamerudi (Mizimu).. lakini kiuhalisia kumbe sio, bali ni mapepo yaliyojigeuza.

Na kwasababu shetani ni yule yule, anapenda kukaa nyuma ya kitu na kutafuta kuabudiwa..anakaa nyuma ya wote wanaoabudu sanamu, wanaoabudu miti wakidhani ni Mungu, wanaoabudu mizimu, wanaoabudu jua n.k

Hivyo hatuna budi tuwe macho na tujihadhari na kumwabudu shetani bila kujua, kwa kukosa maarifa.

Kadhalika kama bado tupo nje ya wokovu, hakuna namna yoyote tunaweza kujiepusha na madhara ya roho hizo chafu, ambazo zinazunguka huku na huko, kuuharibu ulimwengu.

Bwana atubariki.

Maran atha!

Group la whatsapp Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Noeli ni nini, na je! Neno hili linapatikana katika biblia?

THAWABU ZA SIRI, ZA WATAKATIFU MBINGUNI.

WAKAMCHA BWANA, NA KUITUMIKIA MIUNGU YAO WENYEWE.

MAJINI WAZURI WAPO?

Rudi nyumbani

Print this post

Kwanini Eliya alijulikana kama “Eliya Mtishbi”?

Je! Mtishbi ni jina la Baba yake au?

Jibu: Tishbi sio jina la mtu bali la mji, kama vile ulivyo mji wa Samaria au Nazareti.

Kwahiyo kama vile mtu aliyetoka mji wa Nazareti anavyoitwa Mnazareti, au aliyetokea mji wa Samaria anavyoitwa Msamaria, kadhalika mtu yeyote aliyetokea mji huo wa Tishbi aliitwa Mtishbi.

Mji huo wa Tishbi, ulikuwepo katika nchi ya Gileadi, iliyopo ng’ambo ya pili ya mto Yordani. Kwasasa ni maeneo ya nchi ya Yordani (Jordan).

Na katika mji huo mdogo wa Tishbi ndiko Nabii Eliya alikokulia na kuishi sehemu kubwa ya maisha yake.

1 Wafalme 17:1
“Basi Eliya Mtishbi, wa wageni wa Gileadi, akamwambia Ahabu, Kama BWANA, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama mbele zake, hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu”

Maandiko hayajaeleza kwa undani maisha ya Nabii Eliya, ya utotoni, na ujanani, na vile vile hayajaeleza kama alikuwa na mke au watoto.

Lakini kikubwa tunachoweza kujifunza kwa Nabii huyu, ni roho ya kuomba kwa bidii..mbali na kwamba Mungu alimtumia kwa viwango vya juu sana, lakini pia alikuwa ni mtu wa kuomba kwa bidii sana, maandiko yanasema hivyo..

Yakobo 5:16
“Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii.

17 Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita.

18 Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake”.

Na sisi tunajifunza tuwe watu wa kuomba kwa bidii kwasababu Eliya alikuwa ni MTU tu! Kama sisi na si malaika, au mtu fulani aliyeumbwa kipekee tofauti na sisi..alichokuwa na cha ziada ni bidii ya kuomba.

Hivyo na sisi tunajifunza tuwe watu wa kuomba kwa bidii, na sio tu kuomba bali pia kuombeana. Kwasababu kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana kama akiomba kwa bidii.

Bwana atujalie tuwe na bidii kama za hawa mashujaa wa Imani.

Maran atha!

Group la whatsapp Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

MLANGO MWINGINE WA ADUI KUTULETEA MAJARIBU.

KUJIFUNUA KWA YESU KWA PILI.

Zeri ya Gileadi ni nini?

Sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji zilikuwaje?

Rudi nyumbani

Print this post

Baali alikuwa nani?

Baali alikuwa ni aina ya mungu aliyekuwa anaabudiwa na watu wa kaanani na nchi za Tiro na Sidoni, ambaye kulingana na historia za wakaanani, anatajwa kuwa mwana wa mungu aliyeulikana kwa jina la El na mkewe aliyejulikana kwa jina la Ashera..hawa ndio waliomzaa huyu Baali ambaye baadaye alikuja kuabudiwa kama mungu.

Tafsiri ya jina “Baali” ni “bwana” na aliaminika kama mungu wa rutuba na wa uzao.

Aliaminika kusaidia kuongeza rutuba ya nchi, pale ambapo chakula hakikupatikana kutokana na ardhi kutozaa..basi walimwomba huyu mungu baali, ili nchi iweze kuzaa mazao.

Kadhalika pale ambapo mtu au watu walipatwa na matatizo ya kutokupata watoto, walimwomba na kumtegemea mungu huyu kwaajili ya kupata uzao.

Mungu huyu aliabudiwa sana na watu wa kimataifa, lakini ulifika wakati hata wana wa Israeli wakaanza kumwabudu.
Wana wa Israeli walianza kumwabudu baali kwa mara ya kwanza katika kile kipindi cha Waamuzi.

Waamuzi 2:11 “Wana wa Israeli walifanya yaliyokuwa ni maovu mbele za macho ya BWANA, nao wakawatumikia Mabaali.

12 Wakamwacha BWANA, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine, baadhi ya miungu ya watu wale waliokaa karibu nao pande zote, wakajiinamisha mbele yao; wakamkasirisha BWANA, akaghadhibika.

13 Wakamwacha BWANA, wakamtumikia Baali na Maashtorethi”.

Waliendelea hivyo na ibada hizo za mabaali, lakini si kwa kiwango kikubwa..

Hali ilikuja kuwa mbaya zaidi ulipofika wakati wa Mfalme mmoja wa Israeli aliyeitwa Ahabu, ndipo kipindi hicho ibada hizo zilishika hatamu mpaka Bwana Mungu akamtuma Eliya Nabii.

Mfalme Ahabu aliabudu baali kwa kiwango ambacho hakuna mfalme yeyote alikifikia.

1 Wafalme 16:30“ Ahabu mwana wa Omri akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA kuliko wote waliomtangulia.

31 Ikawa, kama ingalikuwa neno dogo tu kuyaendea makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, akamwoa Yezebeli binti Ethbaali, mfalme wa Wasidoni, akaenda akamtumikia Baali, akamsujudia.

32 Akamjengea Baali madhabahu katika nyumba ya Baali, aliyoijenga huko Samaria.

33 Ahabu akaifanya Ashera; Ahabu akazidi kumghadhibisha BWANA, Mungu wa Israeli, kuliko wafalme wote wa Israeli waliomtangulia”.

Lakini je! Baali alikuwa ni mungu kweli?

Jibu ni la!.

Mungu ni mmoja tu, aliyeziumba mbingu na nchi, jina lake YEHOVA. Hao wengine sio miungu bali ni roho za mapepo..BAALI ni pepo!..

Ndio maana haikuweza kujibu chochote mbele za uwepo wa Bwana wa majeshi, wakati ule wa Eliya.

1 Wafalme 18:26
“ Wakamtwaa yule ng’ombe waliyepewa, wakamtengeza, wakaliitia jina la Baali tangu asubuhi hata adhuhuri, wakisema, Ee Baali, utusikie. Lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu. Nao wakaruka-ruka juu ya madhabahu waliyoifanya”.

Hiyo inatufundisha kuwa ibada zote za miungu na za sanamu ni chukizo kwa Bwana.

Na wote wanaoabudu sanamu, na miungu hawataurithi uzima wa milele, maandiko yanasema hivyo.

Bwana atubariki.

Group la whatsapp Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Je Mungu anaweza kumdanganya mtu?

Bwana aliposema kuwa yeye ni “Mungu wa miungu” alikuwa na maana gani?..je! yeye ni Mungu wa sanamu?

Maashera na Maashtorethi ni nini?

Mlima Gerizimu na Ebali ni ipi, na umuhimu wao rohoni ni upi?

Je Mungu anaweza kumdanganya mtu?

Rudi nyumbani

Print this post

NI YESU YUPI UMEMPOKEA?, NI ROHO IPI UMEIPOKEA? NA INJILI IPI UMEIPOKEA?

Jina la Bwana Yesu libarikiwe, karibu katika kuyatafakari maandiko..

2Wakorintho 11:4 “Maana yeye ajaye akihubiri YESU MWINGINE ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea ROHO NYINGINE msiyoipokea, au INJILI NYINGINE msiyoikubali, mnatenda vema kuvumiliana naye”!

Hapo katika  sentensi hiyo, Mtume Paulo aliposema “mnatenda vema kuvumiliana naye”..hakuwa anawasifu watu wa Korintho kwa wao kupokea roho nyingine, au kumkubali Yesu mwingine, bali kinyume chake! Alikuwa ANAWASHUTUMU!.

Sentensi hiyo ili ieleweke vizuri tunaweza kuiweka hivi ….“Mnachukuliana na mtu anayekuja kwenu na kuwahubiria yesu mwingine au injili nyingine msiyoikubali)” yaani “mnaona ni sawa na tena mnakubaliana naye”.

Hapo Mtume Paulo, alimaanisha kwamba, hawapaswi kuchukuliana na mtu yeyote anayekuja kwao na kuwaletea yesu Mwingine au roho nyingine au injili nyingine ambayo hawakuhubiriwa na mitume..kinyume chake wawakatae watu hao na wakatae injili yao na kuipuuzia…lakini hawa watu Wa Korintho walikuwa hawafanyi hivyo!.. walikuwa wanakaa na kuwasikiliza!..jambo ambalo ni hatari kwa roho zao.

Na hata sasa kuna yesu mwingine anayehubiriwa tofauti na Yule Yesu wa kwenye biblia, kadhalika kuna roho nyingine tofauti na Yule Roho Mtakatifu anayehubiriwa katika biblia, na vile vile kuna injili nyingine tofauti na injili halisi ya kwenye biblia..

yesu mwingine ni yupi?

Bwana Yesu halisi anasema wa kwenye biblia anasema.. “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi (Yohana 14:6)”…lakini yesu mwingine anasema “zipo njia nyingi za kufika kwa baba, ikiwemo kupitia mtakatifu Fulani au kupitia maombi ya mtakatifu Fulani aliyekufa, au kupitia kanisa Fulani au kupitia dini nyingine yeyote”

Kadhalika Bwana Yesu halisi wa kwenye biblia alisema… “mtu yeyote akitaka kunifuata ajikane mwenyewe ajitwike msalaba wake anifuate(Mathayo 16:24) na tena anasema “itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake? Ama mtu atoe nini badala ya nafsi yake?(Marko 8:36)”..lakini yesu mwingine anasema.. “sio lazima kujikana nafsi, sio lazima kuacha dhambi, sio lazima kubadilika kimwonekano, Mungu anatazama roho hatazami mwili” n.k

Huyo ndio mfano wa yesu Mwingine ambaye Paulo, aliwaonya watu wa Korintho kwamba wasimkubali,na wala wasichukuliana naye kwasababu ni shetani.

Kadhalika ipo roho Nyingine.

Roho Mtakatifu wa kweli wa kwenye biblia, akija juu ya mtu, jambo la kwanza analolifanya ni kumgeuza Yule mtu na kuwa mtakatifu, kama jina lake lilivyo.. “Roho Mtakatifu”..sifa yake ni utakatifu, na kazi ya pili ni kutuongoza na kututia katika kweli yote ya maandiko, na ya tatu ni kutukumbusha maandiko ..

lakini zipo roho ambazo mtu anapozipokea hazimfanyi kuwa mtakatifu, badala yake ndio zinampa kibali cha kutenda dhambi, kuvaa vibaya,(nusu uchi), kutukana, kuwa na kinyongo na visasi..kadhalika hazimwongozi mtu katika kusoma Neno na kulijua katika ukweli wote. Badala yake ndio zinamletea uvivu wa kuisoma biblia na kuijua..Hizo roho ni roho nyingine, ambazo sio Roho Mtakatifu, ni roho za adui, ambazo zinajigeuza na kujifananisha na Roho Mtakatifu.

Kadhalika kuna Injili nyingine.

Injili maana yake ni “habari njema za Yesu Kristo” ambazo zinaleta WOKOVU kwa mtu.(Warumi 1:16). Na wokovu ni kupata kuokoka kutoka katika hatari Fulani ijayo, au iliyopo.

Zipo injili ambazo hazimfanyi mtu aokoke kutoka katika hatari ya adhabu ya milele (katika Jehanamu ya moto), badala yake zinamfanya astahili kwenda Jehanamu.

Mfano wa injili hizo ni “injili za kutokusamehe, vinyongo na visasi”. Siku hizi hadi makanisani zinahubiriwa. Bwana Yesu alisema, msipowasamehe watu makosa yao, hata baba yenu wa mbinguni hatawasamehe (Mathayo 6:15)..Kwahiyo kutokusamehe tayari ni tiketi ya kwenda jehanamu moja kwa moja..Na injili yeyote inayohubiri kutokusamehe ni injili nyingine ya kuzimu.

Leo hii utakuta mkristo kajaa uchungu, na vinyongo..kwa mambo baadhi tu aliyofanyiwa mabaya..na anakwenda kanisani anakutana na injili ya kupiga adui zake, na kuipokea akidhani yupo salama..kumbe yupo hatarini?

Jiulize ndugu, Umempokea Yesu yupi? Wa kwenye biblia au Yule mwingine?..na umeipokea roho ipi?, Ni Roho Mtakatifu au ya adui?.. na ni Injili gani umeipokea?..ile iletayo wokovu, au ikupelekayo kuzimu?

Maandiko yanatuasa kuwa “tuzipime roho”, na sio roho tu!, bali pia tumpime Bwana yupo tumempokea Yesu Kristo au yesu kristo, na ni injili ipi tumeipokea.

Maran atha!

Group la whatsapp Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Je! Watu ambao hawajawahi kusikia injili kabisa siku ya mwisho watahukumiwa?

Ni kwa namna gani malaika wa mbinguni wanaweza kutuhubiria sisi injili?

Tofauti kati ya uchafu wa mwilini na rohoni ni  ipi?

Matoazi na Matari ni nini? (Kutoka 15:20)

Rudi nyumbani

Print this post

Ni nani aliyemshawishi Daudi akawahesabu Israeli? Ni Mungu au shetani?

Katika 2Samweli 24:1 tunaona maandiko yanasema ni Mungu ndiye aliyemtia Daudi nia, lakini tukirudi katika 1Nyakati 21:1, tunaona maandiko yanasema ni shetani.


Tuanze na 2Samweli 24:1..

2Samweli 24:1 “Tena hasira ya BWANA IKAWAKA JUU YA ISRAELI, AKAMTIA DAUDI NIA JUU YAO, AKISEMA, NENDA, UKAWAHESABU ISRAELI NA YUDA”.

Tusome pia…

1Nyakati 21:1 “TENA SHETANI AKASIMAMA JUU YA ISRAELI, AKAMSHAWISHI DAUDI KUWAHESABU ISRAELI.

2 Basi Daudi akamwambia Yoabu, na wakuu wa watu, Nendeni kawahesabu Israeli toka Beer-sheba mpaka Dani; mkanipashe habari, nipate kujua jumla yao”.

Hapo tukiangalia tunaona ni kweli sentensi mbili zinajichanganya..lakini je! Ni kweli zinajichanganya?

Jibu ni la! Hazijichanganyi..fahamu zetu ndizo zinazojichanganya..lakini biblia siku zote itabaki kuwa Neno la Mungu, lililohakikiwa na Roho Mtakatifu na lisiloweza kukosewa.

Ili tuelewe vizuri maana ya mistari hiyo, hebu tutafakari katika mfano wa kawaida wa kimaisha.

Watu wawili tofauti wameshuhudia ajali barabarani.. Mmoja akatoa ushuhuda akasema “Yule mtu alipokuwa anavuka gari lilimgonga na halikusimama”…Na mwingine akatoa ushuhuda akasema.. “Yule mtu alipokuwa anavuka, Yule dereva alimgonga na hakusimama..akakimbia ”. Je! Katika hao mashuhuda wawili kuna ambaye hayupo sahihi?.. Bila shaka wote wapo sahihi!!.. aliyesema “gari limemgonga” na aliyesema “dereva kamgonga”..wote wapo sahihi..

Kwasababu Yule aliyesema gari limemgonga, hajahusisha dereva aliyekuwa analiendesha lile gari, kadhalika Yule aliyesema ni dereva kamgonga hajahusisha kifaa kilichotumika kumgongea Yule mvuka barabara, ambacho ni gari.

Kadhalika katika mistari hiyo hapo juu..Tunaona mmoja kamtaja kuwa ni Bwana Mungu ndiye aliyemtia nia Daudi, bila kuhusisha chombo alichokitumia (yaani shetani)..kadhalika mwandishi mwingine wa kitabu cha Mambo ya Nyakati, kakitaja chombo tu (yaani shetani)na bila kumhusisha aliyekitumia hicho chombo (yaani Mungu).

Kwahiyo kwa ujumla aliyeleta hayo yote ni Mungu, na shetani katumika tu kama chombo!..na hiyo yote ni kwasababu ya makosa ya Israeli. Na pia ilikuwepo sababu kwanini iwe ni kosa Daudi kwenda kuwahesabu Israeli kama utapenda kujua zaidi juu ya hilo, unaweza kufungua hapa >>>> USIZITEGEMEE NGUVU ZAKO

Kwahiyo tunachoweza kujifunza ni kwamba, Mungu anaweza kutumia chombo chochote kile kutimiza kusudi lake.

Kwamfano utaona Mungu alipotaka kuwatoa Israeli kuwapeleka Babeli, hakushuka yeye mwenyewe na kuwaondoa, bali utaona alimtumia Nebukadneza kama chombo chake cha kufanya hiyo kazi.

Kadhalika Bwana Mungu anaweza kumtumia shetani kutimiza kusudi lake.

Kwamfano mtu anayemkataa Mungu kwa makusudi, anaweza kuruhusu shetani ayaharibu maisha yake, mpaka atakapofikia hatua ya kujitambua.. Na hata wakati mwingine kama mtu huyo kama bado anazidi kushupaza shingo, basi Mungu anaweza kumweka chini milki ya shetani moja kwa moja.

Hivyo hatuna budi kukaa katika neema ya Mungu, na kuishi maisha yampendezayo, ili tusimkasirishe Bwana Mungu wetu aliyetuumba. Kwasababu maandiko yanasema.. yeye mwenyewe hapendi kumtesa mwadamu wala kumhuzunisha.. (Maombolezo 3:34).

Hivyo kwa hitimisho ni kwamba kama bado hujampokea Yesu, fahamu kuwa hizi ni siku za mwisho. Na Kristo yupo mlangoni kurudi, unyakuo wa kanisa ni wakati wowote. Je akija leo na kukukuta katika hali hiyo ya dhambi, utakuwa mgeni wa nani?

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Ni miaka mingapi ya njaa Daudi aliyoambiwa achague? Ni miaka 7 au miaka 3?

Ni miaka mingapi ya njaa Daudi aliyoambiwa achague? Ni miaka 7 au miaka 3?

KUOTA UNAENDESHA GARI.

KUOTA NYOKA.

Rudi nyumbani

Print this post