Category Archive Uncategorized @sw-tz

TENDA AGIZO LA YESU, HILO NDIO LITAKALOKULINDA.

Shalom, nakusalimu katika jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo, karibu tuyatafakari maneno ya uzima pamoja.

Muda mfupi kabla ya Bwana Yesu kwenda kutukuzwa na maelfu ya watu kule Yerusalemu lipo agizo ambalo aliwapa wanafunzi wake wawili, na agizo lenyewe lilikuwa ni kwenda kumletea mwana punda aliyekuwa amefungwa mahali Fulani. Wengi wetu tunaweza kuona lile lilikuwa ni agizo jepesi, lakini kiuhalisia halikuwa jepesi kama tunavyodhani, kwani walipotumwa walioambiwa sio wakaombe wapewe, hapana bali wakachukue, kana kwamba  hao punda walikuwa ni wa kwao.

Embu tusome kidogo;

Luka 19:29 “Ikawa alipokaribia Bethfage na Bethania, kwenye mlima uitwao wa Mizeituni, alituma wawili katika wale wanafunzi,

30 akisema, Nendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mtakapoingia ndani mtaona mwana-punda, amefungwa, ambaye hajapandwa na mtu ye yote bado, mfungueni mkamlete hapa.

31 Na kama mtu akiwauliza, Mbona mnamfungua? Semeni hivi, Bwana anamhitaji.

32 Na wale waliotumwa wakaenda wakaona kama alivyowaambia.

33 Na walipokuwa wakimfungua mwana-punda, wenyewe waliwaambia, Mbona mnamfungua mwana-punda?

34 Wakasema, Bwana ana haja naye”.

Utajiuliza ni kwanini, Bwana atumie kauli hiyo, mfungue na sio waombeni mniletee? Unadhani hakujua kanuni za kuchukua mali za watu wengine? Alijua sana, lakini si kila wakati aliruhusu hilo, pengine wale wanafunzi walisema kwanini Bwana asituambie tukaanze na kuomba kwanza, si tutapewa tu, kuliko kwenda na kufungua wanyama ambao si wetu, si tutaitwa wezi?

Ni sawa na leo hii mtu akuambie, nenda pale mlimani city, utakuta gari limepakiwa, ingia kisha piga ufunguo, endesha uniletee, bila shaka utasema huyu mtu hanitakii mema bali mabaya.. anataka nikachomwe moto kama mwizi.

Lakini Kristo alikuwa na sababu kufanya vile, alijua mwisho wake utakuwaje..Vilevile alijua madhara ya kutanguliza kuomba omba vibali kwenye kazi yake, alijua milolongo ambayo wangekutana nayo, alijua vikwazo ambavyo shetani angevizusha mahali pale..pengine nyie ni wakina nani, mmesajiliwa wapi, shughuli yenu ni nini, hatuwatambui hapa mtaani, msimgolee yule punda, elimu yenu ni ipi, leta uthibitisho kwanza wa barua kutoka kwa huyo Bwana wenu, n.k. vinginevyo tutawashitaki..

Lakini wao hawakuongea chochote walipofika, badala yake walianza kufanya kama Yesu alivyowaagiza, kufungua punda na pengine katika hatua ya mwisho kabisa pale walipoanza kuondoka, ndipo wahusika walipowaona, na kuwauliza nyie mnafanya nini hapo? Mnawapeleka wapi hao punda?..Wakasema Bwana anawahitaji..

Sasa wale kuona tayari punda wao wameshafunguliwa na gharama imeshaingiwa, kuwarudisha itakuwa ni hatua ndefu sana wakaona ni bora wawache tu, pengine wawape masharti Fulani madogo ya kuwatumia, au walipie gharama Fulani kidogo tu. Hilo halijalishi maadamu punda wameshapatikana.

Vivyo hivyo na hata sasa, usitegemee kwanza ruhusu za watu kufanya jambo lolote la ki-Mungu, ni ngumu sana kusikilizwa au kusapotiwa, fanya kwanza kisha baadaye wakikuuliza kwanini ulifanya waambie ni kwababu Yesu aliniagiza..hata wakikasirika lakini tayari ulishafanya, lile agizo la Yesu litakulinda.

Vikwazo vya shetani ni vingi sana, unaweza ukajikuta haumfanyii Mungu lolote kisa, visheria Fulani vidogo vidogo, au viutaratibu Fulani vinakubana. Wewe fanya tu agizo lake litakulinda mbele ya safari. Unaweza hata usifanya huduma kisa hujakamilisha taratibu hii au ile, hayo tumeyaona sana sehemu nyingi, usingojee kukamilisha taratibu za wanadamu kwanza, endelea na taratibu za Mungu, kisha hizo za wanadamu zitafuata baadaye watakapokuuliza..kwasababu ukisema uanzie kwao, utavunjika moyo mapema mpendwa. Vikwanzo ni vingi kila kukicha.

Bwana Yesu alishatoa agizo, enendeni ulimwenguni kote, mkuhubiri injili kwa kila kiumbe. Hilo agizo halisemi, mkaombe kwanza kuhubiri, hapana, wewe kahubiri kwa jinsi Mungu alivyokujalia kisha wakikufuata, waeleze hilo ni agizo la Yesu. Kwa kufanya hivyo Yesu mwenyewe atafungua njia ya kukusaidia, atakuwekea wepesi, au kupewa kibali cha kuendelea na kazi ya Bwana.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

EPUKA KUUNDA MATARAJIO YAKO, KWENYE AHADI ZA MUNGU.

LISHIKILIE SANA LILE AGIZO LA KWANZA.

Baghala ni nini katika maandiko?(2Wafalme 5:16).

Mafundisho

Fitina maana yake nini kwenye biblia?

WAOMBEENI WANAOWAUDHI.

Rudi nyumbani

Print this post

Nini maana ya “Ulipo mzoga, ndipo watakapokutanika tai?

SWALI: Shalom naomba kufahamu maana ya huu mstari..

Luka 17:37 “Wakajibu, wakamwuliza, Wapi, Bwana? Akawaambia, Ulipo mzoga, ndipo watakapokutanika tai”.


JIBU: Kabla ya wanafunzi wa Yesu kumuuliza Bwana hilo swali “WAPI?”..Kuna maneno ambayo yalitangulia juu kidogo, ambayo tukiyasoma yatatusaidia kuelewa vizuri huo mstari ulimaanisha nini, embu tusome kidogo.

Luka 17:22 “Akawaambia wanafunzi, Siku zitakuja mtakapotamani kuona siku moja katika siku zake Mwana wa Adamu, msiione.

23 Tena watawaambia, Tazama, kule! Tazama, huku! Msiondoke mahali mlipo, wala msiwafuate”;

Ukisoma kwenye Mathayo imeeleza kwa undani zaidi, inasema..

Mathayo 24:23 “Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki.

24 Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule.

25 Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele.

26 Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki”.

Maneno hayo Yesu aliyatanguliza kama angalizo la nyakati za hatari zitakazotokea siku za mwisho, akiwaonya kwamba wengi watakuja wakiwavuta watu kwao wakiwaambia Kristo yupo huku au kule, kwa maneno yao ya ushawishi, wakijinadi, tuna hichi au kile, sisi tuna miujiza mikubwa, sisi tuna upako wa mafuta mabichi, sisi ni wataalumu wa tiba za kiroho, sisi tuna makanisa makubwa kuliko yote duniani n.k.

Hivyo Yesu kwa kulijua hilo kwamba litakuja kutokea akawapa tahadhari wanafunzi wake kwamba wasitoke kuwafuata, wasiwe wepesi kuwaendea, wabaki mahali walipo, wasiende popote, kwasababu watawapotosha..

Sasa katika mazingira hayo ya kutokwenda mahali popote ndipo wanafunzi wake mwishoni wakamuuliza swali, NI WAPI sasa patakuwa sahihi pa kwenda..au tutakwenda wapi?

Ndipo Yesu akawaambia palipo na mzoga ndipo watakaposanyika Tai.. Ikiwa na maana mahali palipo na chakula cha Tai ndipo watakapokuja hapo na kukusanyika..

Na kama tunavyojua ndege aina ya tai wanaouwezo wa kuona mbali sana, leo hii kama kuna mnyama kafa porini na angani hakuna ndege yoyote, ukikaa baada ya muda mfupi utawaona tai wengi wamekusanyika hapo.. utajiuliza wametokea wapi na wakati anga lilikuwa jeupe halina ndege hata mmoja? Ni kwasababu jicho la Tai huwa linaona chakula kutokea mbali sana. Tai anaona mahali ambapo wewe huwezi kumwona.

Ni kama tu vile, mahali Fulani pawe na kinyesi cha mnyama au mtu, dakika si nyingi utaona nzi wengi wamekusanyika, na utajiuliza wametoka wapi wadudu hao na mahali hapo ni porini..Jibu ni kwamba, Mungu kawaumbia uwezo mkubwa wa kunusa vitu vya asili yao, tokea mbali, na ndio maana utawaona hata kama eneo hilo limejificha namna gani, wataenda tu.

Vivyo hivyo na wana tai wa Mungu, Kristo kawawekea uwezo Fulani wa kujua chakula chao halisi kilipo haijalishi ni wapi walipo watakipata tu. Tai si kama kuku, ambaye anaona vya hapo chini tu, bali Tai anaona vya mbali sana. Vivyo hivyo na sisi kama ni wanatai, ni lazima tuwe wa kufuata kile chakula kilicho chetu tu..Si kila chakula cha kukikurupukia kisa kipo karibu na sisi, au kinavutia..

Bali tuwe na macho ya tai ya kujua chakula chetu kipo wapi..

Hizi siku za mwisho, usiwe wa kukurupukia kila aina ya mafundisho, au imani. Kristo ameshatuonya..

Tafuta chakula cha wakati wako unaoishi.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Mada Nyinginezo:

Rudi nyumbani

Print this post

WAOMBEENI WANAOWAUDHI.

Bwana Yesu alisema..

Mathayo 5:43 “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako;

44 lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,

45 ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki…..

48 Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu”.

Kumuombea anayekuudhi sio kitu kirahisi hata kidogo, huo ndio ukweli..afadhali ungeambiwa achana naye tu yapite, lakini unaagizwa  umuombee, si jambo jepesi, Lakini hivyo ndivyo vipimo vya ukamilifu wa mtu kwa Mungu. Hakuna njia ya mkato.

Pale unapoona jirani yako anakuzungumzia vibaya, mpaka anakuharibia  pengine siku yako, badala umchukie na kumwekea vinyongo, au umzungumze na wewe vibaya , unaambiwa na Yesu umuombee.. Ukishindwa kufanya hivyo, basi wewe bado hujawa na tabia kama za Mungu ndani yako, bado hujawa mkamilifu kulingana na maandiko.

Bwana Yesu alitoa, mfano hai akasema, hata Mungu mwenyewe, huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua yake waovu na wema..Kiasi kwamba mchawi anatoka kuwaloga watu usiku, na kuwasababishia matatizo, lakini asubuhi anaamka na mvua kwenye shamba lake, na linastawi vizuri sana , mpaka anavuna, na kuuza, na kupata chakula kwa ajili yake na watoto wake na cha akiba.

Jambazi, anatoka kuiba usiku na kuharibu, na akiamka asubuhi anakutana na jua kama wewe unavyoliona, sio kwamba Mungu anapendezwa na tabia zake, la, lakini anaonyesha rehema zake kwao pengine siku moja watatubu, na kuacha njia zao.

Na sisi pia kuna wakati tulishawahi kuwa waovu mbele za Mungu, kiasi kwamba ilikuwa ni haki ya Mungu atulipizie kisasi tuondoke chini ya jua, lakini mara nyingi tumeona hakufanya chochote, mpaka sasa tumetubu tumeokolewa, na tunamtumikia. Laiti kama asingekuwa mvumilivu kwetu, leo hii tungekuwa kwenye moto wa jehanumu.

Huo ndio ukamilifu wa Mungu, na yeye pia akatupa agizo hilo hilo kwamba tuwaombee wale wanaotuudhi, wale ambao tunawaona ni maadui zetu haswa haswa, tuwaombee, tusijifanye sisi ni washupavu sana, tunajua kupambana, tunajua kusimamia haki zetu, tukadhani kuwa mawazo ya Mungu ni kama ya kwetu, badala ya kuwaombea mema, tukaanza kuwaombea vifo, kuwaombea njaa, kuwaombea wasifanikiwe..n.k.

Mungu atahuzunishwa na sisi, na kutuona kama ni wachanga wa njia zake.

Kumbuka hatujaitwa kuwaiga wanadamu, bali tumeitwa kumuiga Mungu. Kama vile Yesu alivyosema,…

Yohana 5:19 “Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vile vile”.

Haijalishi wanadamu wote watasema, wapige maadui zako. Lakini maneno ya Yesu ni tuwaombee. Hata kama yataonekana ni maombi magumu kwetu, lakini kwa Mungu ni manukato. Tujizoeshe kuwa watu na namna hiyo kila siku. Ndipo tutakapoona Mungu akituzidishia na sisi rehema zake kila siku.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho mengine

Mada Nyinginezo:

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 9 (Kitabu cha Ayubu).

Rudi nyumbani

Print this post

ELIMA MCHAWI, ANAFANYA KAZI HADI SASA.

Sikuzote roho haiji hivi hivi tu, bila kuwa na chanzo Fulani, na chanzo hicho kinaweza kuwa mtu, au kitu au sehemu, Sasa pale yule mtu anapoondoka, huwa anaacha tabia yake Fulani inayoendelea na tabia hiyo ikishakita mizizi vizuri ndio inaitwa roho,..

Kwamfano kwenye biblia utamwona mwanamke anaitwa Yezebeli, huyu mwanamke alikuwa ni mchawi, na mzinzi, na tabia zake tunazijua vizuri kwenye biblia, jinsi alivyoiharibu Israeli na kuigeuzwa kuwa nchi ya kichawi. Lakini tunasoma mara baada ya kufa kwake, roho yake iliendelea kutembea duniani, na ndio maana miaka mingi baadaye utaona Bwana Yesu anamzungumzia tena habari zake kana kwamba bado yupo duniani, katika kitabu cha Ufunuo,

Ufunuo 2:19 “Nayajua matendo yako na upendo na imani na huduma na subira yako; tena kwamba matendo yako ya mwisho yamezidi yale ya kwanza.
20 Lakini nina neno juu yako, ya kwamba wamridhia yule mwanamke Yezebeli, yeye ajiitaye nabii na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ili wazini na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu”

Utamwona pia Eliya, pindi alipoondoka roho yake ilianza kutembea tena wakati baada ya wakati, Kumbuka hawi Eliya mwenyewe kama Eliya, Au Yezebeli kama Yezebeli, bali ile tabia  ya rohoni iliyokuwa juu ya Eliya, ndiyo inayotembea juu ya watu kadha wa kadha, Roho hiyo ilikuja juu ya Elisha, baadaye Yohana Mbatizaji n.k. na itaendelea kutembea hadi wakati wa nyakati za mwisho kabisa.(Malaki 4:5)

Halikadhali Na Bwana wetu Yesu Kristo, yeye alitembea hapa duniani, kwa miaka 33 na nusu, lakini alipoondoka, hakuondoka hivi hii ilikuwa ni sharti aichalie Roho yake katikati yetu, na ndio Roho Mtakatifu tuliye naye sasa. Kiasi kwamba mtu akiyaamini maneno yote ya Bwana Yesu moja kwa moja anampokea Roho wake ambaye atamsaidia aishi maisha kama ya Yesu.

Sasa tukishaweka msingi kama huo, tuende moja kwa moja katika somo letu la leo ambalo linamzungumzia yule Elima mchawi aliyekutana na Paulo na Barnaba  pindi walipokuwa wanahubiri injili huko Pafo, tusome.

Matendo 13:6 “Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake Bar-Yesu;
7 mtu huyu alikuwa pamoja na liwali Sergio Paulo, mtu mwenye akili. Yeye liwali akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno la Mungu.
8 Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani.
9 Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho,
10 akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka?
11 Basi, angalia, mkono wa Bwana u juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza, akazunguka-zunguka na kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza.
12 Ndipo yule liwali, alipoyaona yaliyotendeka, akaamini, akiyastaajabia mafundisho ya Bwana”`.

Huyu mtu alikuwa ni mchawi, na wakati huo huo ni nabii wa Uongo. Kazi yake na lengo lake, lilikuwa ni kuwafanya watu wasiiamini njia ya wokovu, pale tu wanapokutana na injili ya kweli ya msalaba. Ni mchawi aliyebobea kwenye kitendo cha kupinga tu, na kushawishi watu kuiacha imani, na ndio maana mtume Paulo alimwambia “Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka?”

Kwa kazi yake hii, mpaka akawa ameshawafikia kabisa na watu wakubwa na wenye akili kama huyu Sergio Paulo, ikiwa na maana kuwa  huku chini tayari alishaburuza.

Kama tunavyoona hapo, Paulo alipoanza kumuhubiria huyu liwali, yeye bila kupoteza muda alianza kuwabishia wakina Paulo, na kutoa hoja zake za uongo, na pengine kumwambia yule liwali hawa watu ni waongo, wapiga dili, hakuna kitu kuokoka hapa duniani, huyo Yesu aliibiwa hajafufuka, hawa ni wapotoshaji n.k.

Lakini Paulo kulijua hilo, akamkemea saa ile ile akawa kipofu kwa muda.

Sasa huyu mtu alishakufa lakini aliiacha roho yake hapa duniani, na roho hiyo inatembea kwa kasi sana, sasa hivi duniani imewavaa watu wengi, na wenyewe hawajijui kuwa wanafanyika kuwa wachawi, pasipo wao kujijua.

Kuna watu kazi yao ni kupinga tu kila habari ya Kristo, wakiona kila mtumishi wa Mungu anahubiri, au kushuhudia, wanasema ni nabii wa uongo, wanasema ni wazinzi, wakisikia injili ya kweli inahubiriwa wanasema anapotosha,

Sasa kibiblia watu kama hao ni wachawi, hawajijui tu kama wameshafikia hiyo hatua

Katika nyakati hizi za kumalizia ni kujiangalia sana, si kila wazo la kila mtu la kulisikiliza, au kulipokea haijalishi atakuwa ni ndugu yako, au rafiki yako, au mfanyakazi mwenzako. 

Bwana Yesu alisema, angalieni jinsi msikiavyo (Luka 8:18)

Kaa mbali nao, ikiwa unaona kila wakati tu wanakosoa habari za Mungu au watumishi wa Mungu, hakuna kipengele hata kimoja watakisifia, kaa mbali nao, wanakuwekea tu moyo mgumu wa kutokuamini.

Ukikutana na watu kama hao ujue unaongea na wachawi, jiupushe nao. Leo hii duniani utakutana nao wengi sana akina Elimu, Bar Yesu. Wewe jikite katika kumtafuta Muumba wako kwa bidii, mpende Mungu wako, sikiliza na soma Neno la Mungu, achana na hao wanaoipuuzia, au kukejeli kila kitu cha ki Mungu kinachokatiza mbele yao.

Jiepushe nao.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho mengine

Mada Nyinginezo:

JINSI PAULO ALIVYOPAMBANA NA UJINGA WA ROHONI.

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

Nini maana ya neno ‘Kuabiri’ kama linavyotumika katika  biblia?

ILI NIWE KIELELEZO KWA WALE WATAKAOMWAMINI BAADAYE.

KUMTUMIKIA MUNGU, KUNAWEZA KUWE KINYUME NA MATARIJIO YAKO.

Rudi nyumbani

Print this post

TANGAZO

Jumapili ya tarehe 24 tutakuwa na ibada yetu ya pili. Tunawakaribisha Wakazi wa Daresalaam Na wengineo.

Pamoja na ushirika tutakuwa na muda wa kuuliza maswali ya biblia, Ushauri na maombezi

Hivyo mnakaribishwa wote.

Mahali ni Tegeta Nyuki.

Muda ni saa 3:00 asubuhi mpaka saa 6:30.

Karibuni sana.

Mwl. Denis.
Wingu la Mashahidi.

Kwa mawasiliano: piga +255693036618 au +255789001312

Shalom.

Print this post

KWANINI MIMI?

Kuna wakati unaweza kupitia mahali ukajikuta upo katika hali ambayo hujui sababu ni nini, haujui kosa lako ni lipi mpaka upokee mapigo mazito kama hayo.  Unabakia kujiuliza maswali kwanini mimi?

Ayubu alipitia mazingira kama hayo, katika maisha yake yote alijitahidi sana kuwa mkamilifu na mwelekevu mbele za Mungu, hakuruhusu dhambi imtawale katika maisha yake yote, alikuwa ni mwombaji, na mkaribishaji mzuri wa wageni, hivyo Mungu akambariki sana.

Lakini ukafika wakati, akashangaa ghafla mambo yamebadilika, mifugo yake yote imeibiwa, mali zake zote zimepotea, kama hilo halitoshi akasikia watoto wake wote 10 wamekufa kwa ajali mbaya sana ndani ya siku moja.. Wakati yupo katikati ya msiba, ghafla tena anaanza kuugua kwa magonjwa ya ajabu, kiasi kwamba inambidi akae kwenye majivu muda wote, alikonda kiasi cha kuona mifupa tu.

Embu jiweke wewe katika hiyo nafasi, unadhani haitakuwa rahisi kumkufuru Mungu? Ni rahisi sana, na ndicho alichokifanya mke wa Ayubu. Lakini Ayubu hakumkufuru Mungu, yeye hakufikia hatua hiyo mbaya bali aliishia kusema KWANINI MIMI?

Kwanini mimi na si mtu mwingine,…Na hiyo kwanini mimi ilimpelekea mpaka kuanza kulaani, kila kitu kwenye maisha yake, akailaani mpaka siku ya kuzaliwa kwake, akaona kama vile yeye si mtu mwenye bahati, ni heri tu asingezaliwa duniani.

Ayubu 3:2 “Ayubu akajibu, na kusema;

3 Na ipotelee mbali ile siku niliyozaliwa mimi, Na ule usiku uliosema, Mtoto mume ametungishwa mimba.

4 Siku hiyo na iwe giza; Mungu asiiangalie toka juu, Wala mwanga usiiangazie.

5 Ishikwe na giza, giza tupu, kuwa yake; Wingu na likae juu yake; Chote kiifanyacho siku kuwa giza na kiitishe………

11 Mbona si kufa mimi tokea mimbani? Mbona nisitoe roho hapo nilipotoka tumboni?

12 Mbona hayo magoti kunipokea? Au hayo maziwa, hata nikanyonya?

13 Maana hapo ningelala na kutulia; Ningelala usingizi; na kupata kupumzika;”

Ayubu, kila kukicha alitamani afe.(Ayu 7:4)

Hiyo hali inawakumba watu wengi sasa hivi hususani pale wanapopitia matatizo fulani madogo au makubwa, aidha wanapofiwa na wazazi wao, au watoto wao, au wanapopoteza mali zao, au vitu vyao ya thamani, au wanapokumbana na magonjwa mazito yasiyotibika, kama vile kansa, kisukari, au ukimwi, wanajiuliza ni tatizo gani walilolifanya mpaka wayapate magonjwa hayo, mbona wanakula vizuri tu, mbona hawatendi dhambi, inakuwaje wakumbane na hizo shida kwenye miili yao.

Wengine, wanauliza kwanini mimi nizaliwe kipofu, nilimkosea nini Mungu, kwanini nizaliwe mfupi, kwanini niwe mlemavu, kwanini nina mapungufu haya n.k..

Sasa katika haya maswali , kwanini! kwanini! kwanini!.. Mungu naye alianza kumuuliza Ayubu maswali mengine ya ziada, ambayo alitaka na yeye ampe majibu yake. Ukisoma Ayubu 38 na kuendelea utaona maswali aliyoulizwa Ayubu ni yapi, ambayo tunajua yote alishindwa kuyatolea majibu yake..Kwamfano maswali haya aliulizwa;

Ayubu 38:28 “Je! Mvua ina baba? Au ni nani aliyeyazaa matone ya umande?

29 Barafu ilitoka katika tumbo la nani? Na sakitu ya mbinguni ni nani aliyeizaa?

30 Maji hugandamana kama jiwe, Na uso wa vilindi huganda kwa baridi.

31 Je! Waweza kuufunga mnyororo wa Kilimia, Au kuvilegeza vifungo vya Orioni?

32 Je! Waweza kuziongoza Sayari kwa wakati wake? Au waweza kuongoza Dubu na watoto wake?

33 Je! Unazijua amri zilizoamuriwa mbingu? Waweza kuyathibitisha mamlaka yake juu ya dunia?

34 Waweza kuiinua sauti yako mpaka mawinguni, ili wingi wa maji ukufunikize?

35 Waweza kuutuma umeme, nao ukaenda, Ukakuambia, Sisi tupo hapa?

36 Je! Ni nani aliyetia hekima moyoni? Au ni nani aliyetia ufahamu rohoni?”

Akagundua kuwa kumbe ni mambo mengi sana huku duniani, Mungu hajatupa majibu yake, , lakini tunaendelea tu kuishi nayo, wala hatuumizi vichwa vyetu kutaka kuyajua, na maisha yanaendelea kama kawaida. Sasa kwanini tutake kutolea majibu kila hali tunayopitia.

Ayubu baada ya kulijua hilo, alikaa kimya. Akamwambia Mungu hakika nilikosea kuzungumza maneno yasiyofaa. Na baada ya Mungu kugundua kuwa Ayubu kalijua hilo, akaugeuza uteka wake akampa mara dufu zaidi ya vile alivyovipoteza. Na sisi pia, tuliookoka, mambo yanapogeuka na kuwa ndivyo sivyo, sio wakati wa kuanza kulaumu, kwanini iwe mimi na sio Yule,..Kumbuka kila mtu anayo mapito yake, sio kila tatizo utalipatia jawabu lake sasa hivi,  pengine utakuja kujua mbeleni au usijue kabisa, kikubwa mshukuru Mungu, na usonge mbele. Wakati utafika jaribu hilo litaisha, usianze kuuliza maswali ambayo hujui majibu yake, utaishi kulaumu, Mtumaini Mungu.

Songa mbele kama mkristo uliyeokoka..Timiza wajibu wako wa kumwomba Mungu na kumshukuru, na kuishi maisha ya utakatifu, Upo wakati Mungu atakuondolea huo ugonjwa, au hilo tatizo, au hiyo shida.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho mengine:

Mada Nyinginezo:

HUDUMA YA (ELIFAZI, SOFARI, NA BILDADI).

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 9 (Kitabu cha Ayubu).

Maswali na Majibu

JINSI SHETANI ANAVYOZUIA MAJIBU YA MAOMBI YETU.

KWANINI KRISTO AFE?

Rudi nyumbani

Print this post

JINSI PAULO ALIVYOPAMBANA NA UJINGA WA ROHONI.


Contact

Paulo katika kazi yake ya utume, hakuwa tu na jukumu la kuwahubiriwa watu Kristo  ili wamwamini, kisha wapokee ondoleo la dhambi halafu basi..Hapana, bali pia ni mtu ambaye alikuwa anatia bidii nyingi sana katika kuwajuza watu juu ya ukweli wote wa Mungu na siri nyingine zilizojificha katika maandiko tangu zamani.

Na ndio maana utaona alisema..

Waefeso 5:17 “KWA SABABU HIYO MSIWE WAJINGA, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana”.

Paulo alipiga vita ujinga ambao watu wanao kuhusu Mungu, kwasababu alijua ni jinsi gani unavyoweza kumgharimu mkristo kwa sehemu kubwa. Ujinga ni ile hali ya mtu kukosa maarifa ambayo kama angeyapata basi yangemsaidia kuishi au kutenda mambo fulani kwa ufanisi mahali alipo.. Kwamfano, mtu ukikosa kufahamu kuwa duniani kuna kitu kinachoitwa teknolojia, na kwamba ukitaka kuwasiliana na mtu aliye mbali utatumia kifaa kinachoitwa simu,

Sasa wewe hataki kusikia habari za simu, badala yake unataka tu kukaa maporini , kuwinda swala, kuna wakati utafika utahitaji kuwasiliana na ndugu zako wa mbali, hapo ndipo itakugharimu utumie  miguu yako au punda kwenda kuwafuata na hiyo pengine itakuchukua mwezi mzima kwenda na kurudi, kiasi kwamba kama angepata maarifa ya simu, au vyombo vya moto basi kuwasiliana kwako au kusafiri kwako kungekuwa ni kurahisi sana na kwa haraka.

Vivyo hivyo na katika Ukristo, tunakosa maarifa mengi sana, na hiyo inapelekea pengine tunashindwa kuufurahia wokovu wetu , au kuona safari  hii ni ngumu sana, au kushindwa kabisa kustahimili mengi.  Siku zote Hatuwezi kumtumikia Mungu, juu ya kiwango cha ufunuo tulichonacho kuhusu yeye. Kiwango chako cha kumwelewa Mungu ndicho kitakachoeleza maisha ya wokovu unayoishi sasa.

Sasa Mtume Paulo ni mtu ambaye alikuwa anatamani kupata maarifa ya kutosha kuhusu ufalme wa mbinguni, na ndio maana siri nyingi zihusuzo kanisa, na Mungu tunazipata katika nyaraka zake.Na ndio maana sehemu nyingi utaona anasema Neno hili SITAKI MKOSE KUFAHAMU. Akiwa na maana hataki tuwe wajinga..

Embu tuangalie baadhi ya vitu ambavyo alitaka sisi tusikose kufahamu.

  1. Tumaini la ufufuo wa wafu:

Anasema..

1Wathesalonike 4:13 “Lakini, ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini”.

Ukiendelea kusoma pale utaona anaeleza jinsi siku ya unyakuo itakavyokuwa, kwamba utatangulia kwanza ufufuo wa wafu, hivyo wewe kama ni mkristo, ukiifahamu siri hiyo kwamba lipo tumaini la kufufuliwa na kuonana wa wapendwa wetu katika Imani waliotutoka, hatutakuwa na huzuni ya kupitiliza, kama watu wa kidunia walivyo, hatutakuwa wa kulalamika, na kulaumu laumu muda wote.

2) Kuhusu hukumu watakayokabidhiwa watakatifu.

1Wakorintho 6:2 “Au hamjui ya kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Na ikiwa ulimwengu utahukumiwa na ninyi, je! Hamstahili kukata hukumu zilizo ndogo?”

Watakatifu watakaoshinda hawatahukumu tu ulimwengu, bali mpaka na malaika, Je ulishawahi kulifikiria hilo wewe utawahukumuje malaika? Fikiria tena hilo, uone ni  mambo makubwa kiasi gani Mungu amewaandalia watu wake huko mbeleni.

3) Siri ya Yesu iliyojificha katika agano la Kale.

1Wakorintho 10:1 “Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari;

2 wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari;

3 wote wakala chakula kile kile cha roho;

4 wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo”.

Paulo anatufunulia siri nyingine kuwa hatupaswi kusoma agano la kale kama historia Fulani tu, tunapaswa tujue ndani ya historia zile Kristo amejificha, na Hivyo tunapaswa tusomapo tumwone Kristo, kwasababu vyote vile vilimfunua yeye. Hivyo Paulo anatuasa tusiwe wajinga pia katika hilo, tusome mawazo yetu tukiyaelekeza kwa Kristo.

4) Kuhubiri injili kuna dhiki.

2Wakorintho 1:8 “Maana ndugu, hatupendi, msijue habari ya dhiki ile iliyotupata katika Asia, ya kwamba tulilemewa mno kuliko nguvu zetu, hata tukakata tamaa ya kuishi”.

Wengi tunadhani katika kumtumikia Mungu ni mteremeko tu wakati wote, hapana, Bwana Yesu kiongozi wetu alipitia dhiki, mitume pia walipitia dhiki wakati mwingine, vivyo hivyo na wewe, unapaswa ulielewe hilo, ili kusudi kwamba litakapotokea, usije ukawa mjinga kwa kuacha kuifanya kazi ya Mungu, ukasema huyu ni shetani, kwani Mungu sikuzote haruhusu watu wake wapitie dhiki.

5) Miili yetu ni Hekalu la Roho Mtakatifu.

1Wakorintho 3:16 “Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?

17 Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi”.

Anataka tufahamu kuwa hii miili tuliyopewa na dhamana, ni mali ya mwingine sio yetu, hivyo tuithamini kwasababu tukiiharibu kwa uzinzi, au pombe, au michoro, au chochote kile, tutaharibiwa na sisi. Hilo tusiwe wajinga, wengi wameuliwa na Mungu kwa njia hiyo.

6) Utumishi wa Madhabahuni.

1Wakorintho 9:13 “Hamjui ya kuwa wale wazifanyao kazi za hekaluni hula katika vitu vya hekalu, na wale waihudumiao madhabahu huwa na fungu lao katika vitu vya madhabahu?”

Paulo hataki watu wawe  wajinga pia kufahamu, watumishi wa Mungu wana haki ya kula vya madhabahuni, kwasababu ndivyo Mungu alivyoagiza na wala sio mwanadamu. Hivyo sio jambo la kujadiliana nalo au kushangaa utakapokutana nalo.

7) Karama za Rohoni.

1 Wakorintho 12:1 “Basi, ndugu zangu, kwa habari ya karama za roho, sitaki mkose kufahamu”.

Hapa yapo makundi mawili ya wakristo, lipo kundi ambalo haliamini kabisa, au haliruhusu karama za Mungu kutenda kazi katika kanisa la Kristo, wakisikia kuna mtu anakarama ya kuona maono wanasema ni shetani, wakiona kuna mtu ananena kwa lugha wanasema huyo sio Roho. Hivyo utakuta kanisa limebakiwa kuongozwa na wenyeviti na makatibu, na maaskofu- jina, na makasisi, basi, hakuna chochote cha Zaidi ya litrujia kufuatwa.

Kundi lingine,  ni lile lisiloweza kumbanua karama za Roho, huduma za Roho, Utendaji kazi na Ujazo/Ubatizo  wa Roho Mtakatifu. Haya yote Mtume Paulo alitaka tusiwe wajinga, matokeo yake ni kuwa leo hii utakutana na watu wengi wenye karama huku wakiendelea na maisha yao ya kale wakidhani kuwa wana Roho Mtakatifu kumbe walishaachwa zamani, japokuwa karama zao zinaendelea kufanya kazi.

8) Mpango wa Mungu kwa mataifa.

Warumi 11:25 “Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili”.

Hii ni siri kubwa ambayo  tukiijua  hatutaishi maisha ya patapotea kwenye ukristo wetu, siku tukifahamu kuwa Utimilifu wa mataifa utawasili, na kwamba kuanzia huo wakati na kuendelea sisi hatutakuwa na neema tena ya kuupokea wokovu, bali itarudishwa tena Israeli kwa kipindi kifupi, ndipo tutakapoishi maisha ya umakini sana katika Ukristo wetu.

Wengi wetu tunadhani, tutaendelea tu hivi hivi mpaka Yesu atakaporudi, Ndugu, Wokovu utaishia kwa wayahudi sio sisi. Kwahiyo tukiwa wajinga tukidhani kuwa tutaendelea hivi hivi, tujue tupo katika hatari kubwa sana ya kuuokosa, Unyakuo. Bwana Yesu kuna wakati atasimama, na kuufunga mlango. Wakati huo utakuwa ni hapa hapa duniani, na sio mbinguni. Kwasababu Utimilifu wa mataifa utakuwa umewasili. Mungu atakuwa ameshamalizana na sisi, utakuwa ni wakati wa wayahudi tena.

Embu jiulize, Je, ikiwa neema hiyo inarudishwa kule Israeli, utampatia wapi tena Kristo, na wakati Roho Mtakatifu hayupo tena juu yako. Ikiwa leo hii, unamkataa unampinga, angali neema ipo, unadhani nafasi hiyo itakuwepo tena? Hivyo usiichezee hii neema ambayo ndio tunakaribia kumaliza nayo. Dalili zote zinaonyesha kuwa hatuna muda mrefu Unyakuo utapita. Wafu watafufuliwa, na sisi tutaungana nao kwenda kumlaki Bwana Yesu mawinguni.

Hivyo tubu dhambi zako mgeukie Mungu.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho mengine:

Mada Nyinginezo:

MPAKA UTIMILIFU WA MATAIFA UTAKAPOWASILI.

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita..

UTAWALA WA MIAKA 1000.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

Rudi nyumbani

Print this post

Tarishi au Matarishi ni akina nani  kwenye biblia?

Tarishi ni mtu aliyeajiriwa kwa kazi ya kusafirisha na kuwasilisha barua au nyaraka mahali pengine. Katika biblia watu ambao walikuwa wanatumwa kusambaza barua za wafalme kwa watu wa mji, au viongozi  waliitwa Matarishi.

Kwa mfano katika habari hii, utaona enzi zile za wafalme kulikuwa na  Mfalme aliyeitwa Hezekia ambaye alikusudia kurejesha tena sikukuu zilikuwa zimesahauliwa katika Israeli kwa miaka mingi, Hivyo ili adhma yake iweze kufanikiwa  ilimbidi awaandae hawa wajumbe (matarishi) ili wamsaidie kulipeleka hili agizo lake kwa watu wote waliokuwa Israeli wapande Yerusalemu kwenda kumfanyia Mungu sikukuu ya pasaka..

2Nyakati 30:5 “Basi wakafanya amri kupiga mbiu kati ya Israeli yote, toka Beer-sheba mpaka Dani, ya kwamba watu waje wamfanyie pasaka Bwana, Mungu wa Israeli, huko Yerusalemu; maana tangu siku nyingi hawakuifanya kama vile ilivyoandikwa.

6 Wakaenda MATARISHI wenye nyaraka za mfalme na wakuu wake, kati ya Israeli yote na Yuda, na kwa amri ya mfalme, kusema, Enyi wana wa Israeli, mrudieni Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na Isaka, na Israeli, apate kuwarudia waliosalia wenu waliookoka mikononi mwa wafalme wa Ashuru”.

Utaona tena, kipindi kile, cha Mfalme Ahasuero, Amri ilipotolewa na Mfalme kuwa wayahudi wote wanapaswa wauliwe ndani ya siku moja, utaona agizo hilo lilisambazwa katika miji yote kwa mikono ya  hawa matarishi.

Esta 3:13 “BARUA ZIKAPELEKWA KWA MIKONO YA MATARISHI mpaka majimbo yote ya mfalme kuwaangamiza Wayahudi wote, na kuwaua, na kuwafisha, vijana kwa wazee, watoto wachanga na wanawake pia, siku moja, yaani, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili ndio mwezi wa Adari; na kuyachukua mali yao kuwa nyara”.

Neno hilo utalisoma pia katika vifungu hivi..

Esta 8:10 “Akaandika kwa jina la mfalme Ahasuero, na kutia muhuri kwa pete ya mfalme, akazipeleka barua kwa MATARISHI, wamepanda farasi, wamepanda wanyama wepesi sana waliotumika kwa huduma ya mfalme, ndio waliozalishwa katika zizi la mfalme”.

Ayubu 9:25 “Basi siku zangu zina mbio kuliko TARISHI; Zakimbia, wala hazioni mema”.

Yeremia 51:31 “TARISHI mmoja atapiga mbio kumlaki mwingine, Na mjumbe mmoja atapiga mbio kumlaki mwenziwe, Ili kumpasha habari mfalme wa Babeli, Ya kuwa mji wake umetwaliwa kila upande”.

Soma pia 2Nyakati 30:10, Esta 8:14

Lakini swali la kujiuliza na sisi je  ni matarishi wa habari gani? Je Ni habari za Kristo, au habari za watu mitaani?. Sote tunawajibu wa kuwa matarishi wa Kristo, tuwe wepesi kwenda kuwahubiria wengine habari njema za msalaba, ili waokolewe, kuliko habari nyingine zozote. Bwana anatazamia, vinywa vyetu, mikono yetu, maisha yetu,  vyote vitumike katika kuutangaza ufalme.

Je, mimi na wewe tunafanya hivyo?. Majibu tunayo mioyoni mwetu,

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Pomboo ni nini katika biblia?(Kutoka 25:5, Ezekieli 16:10)

Mharabu ni nani katika biblia?

Matuoni ni nini katika biblia?

USIPIGE MATEKE MCHOKOO!

Rudi nyumbani

Print this post

Neno Buruji lina maana gani katika biblia?

Buruji ni aina ya mnara ambao ulijengwa  zamani mahususi kwa ajili ya kuvamia kambi za maadui zilizojengwa kwa kuta ndefu.

Kwa namna ya kawaida ilikuwa ni ngumu kuvamia ngome za namna hiyo..kwani askari walikaa juu ya kuta hizo ndefu wenye mishale ya moto na mawe mazito..kwahiyo kama nyinyi mtakwenda kushindana nao kwa njia za kawaida kwa pale chini. Kitakachokuwa kinaendelea ni kifo tu.

Hivyo iliwabidi wabuni njia nyingine za kuwashambulia maadui waliojizungushia boma juu ya kuta..ndipo hapo sasa yakagunduliwa  haya maburuji..ambayo kwa chini yalikuwa na matairi manne..na urefu wake ulilingana na zile kuta za maadui zao au zaidi kidogo..hivyo askari walikuwa wanapanda mpaka juu kabisa mwa maburuji hayo…mahali ambapo watakuwa usawa mmoja na wale maadui zao..kisha wanaanza kuwashambulia..huku wanazidi kuusogelea ukuta wa mji kidogo kidogo.

Na wakishafanikiwa kufika kwenye ukuta wanashusha ngazi zao..kisha wanashuka kutokea huko huko juu na kuingia katika mji na kuanza kuwashambulia. 

Tazama picha juu uone jinsi zilivyotengenezwa

Kwa kuwa buruji hizo zilikuwa zinajengwa kwa mbao..sasa ili kuzuia moto kutupwa kuziteketeza..walizizungushia chuma au ngozi za wanyama kiasi kwamba mishale ya moto hata ikitupwa haikuweza kuleta madhara.

Isaya 23:13

  • [13]Tazama, nchi ya Wakaldayo; watu hao hawako tena; Mwashuri ameiweka tayari kwa hayawani wa jangwani; WAMESIMAMISHA BURUJI ZAO ZA VITA, wameyaharibu majumba yake ya enzi, akaufanya kuwa uharibifu.

Pia kibiblia minara yote ya maficho iliyokuwa ndani ya ngome iliitwa kwa jina hili

Vifungu hivi vinaelezea neno hilo.

Waamuzi 9:46

[46]Kisha watu wote waliokaa katika ile buruji ya Shekemu waliposikia habari hiyo wakaingia ndani ya ngome ya nyumba ya El-berithi.

2 Mambo ya Nyakati 26:15

[15]Akafanya katika Yerusalemu mitambo ya vita, iliyobuniwa na watu wastadi, iwekwe juu ya 

na juu ya buruji, ili kutupa mishale na mawe makubwa. Jina lake likaenea mbali sana; kwa kuwa alisaidiwa mno ajabu, hata akapata nguvu.

Soma pia Waamuzi 9:47,49 Yeremia 31:38, Sefania3:6 Wimbo 8:9 Nehemia 3:8

Halikadhalika pia kiroho zipo kuta nzito adui yetu ibilisi ameziweka mbele yetu.. lakini Tukimtumainia Bwana yeye mwenyewe ndio atakuwa buruji letu. Hatuhitaji nguvu za mwilini kupambana naye..bali zile za Rohoni..Wana wa Israeli walimwamini Mungu na wakafuata maagizo yake kwa ukamilifu..na walipokutana na zile kuta za Yeriko, sote tunafahamu ni nini kilitokea..ni kwamba zilizama chini zote..pakawa tambarare kama vile hakujawahi kuwa na kuta au ngome..

Halikadhalika na sisi tunahitaji kumwamini Mungu na kuishi sawasawa na njia zake. Na hayo mengine ya vita vya ibilisi yeye atayashughulikia mwenyewe kirahisi kabisa.

Bwana akubariki.

Je! Umeokoka?Je umepata uhakika kama ukifa leo utakwenda wapi?..una habari kuwa hili ndio kanisa la mwisho lijulikanalo kama Laodikia? Na kwamba zile dalili zote za kuja kwa Yesu zimeshatimia tunachongojea sasa ni Unyakuo tu?

Unangojea nini? Tubu mrudie muumba wako katika hizi dakika za lala salama.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho mengine:

Mada Nyinginezo:

Ngome ni nini?  Kwanini Mungu anafananishwa na ngome?

Rudi nyumbani

Print this post

INJILI YA MANENO LAINI ITAKUGHARIMU.

Ukiona unahubiriwa juu ya hukumu ya Mungu, au juu ya habari ya siku za mwisho halafu unachukia au unakwazika, lakini wakati huo huo ukiambiwa habari za mafanikio na mema ndio unafurahia, basi fahamu kuwa upo karibu sana kupotea.

Kwasababu kitengo hicho ndicho kitengo-mama cha shetani kuwadanganyia watu, Embu fikiria pale Edeni Mungu hakuwaficha chochote bali aliwaeleza Adamu na hawa madhara ya dhambi, akawaambia mkila matunda la ujuzi wa mema na mabaya hakika MTAKUFA..

Lakini shetani akaibuka na mahubiri yake laini, kinyume na yale Mungu aliyowaangiza, na kuwaambia hakika HAMTAKUFA,…Unaona? Hawa aliposikia habari za mema zimekuja, habari za mafanikio, habari za uzima wakati wote, habari za kuwa juu tu, haijalishi kuwa utamkasirisha Mungu kiasi gani, haijalishi kuwa utazini kiasi gani, atatoa mimba nyingi namna gani,  maadamu ni ya kutakiwa mema, basi akayachukua tu na kuyadharau yale ya Mungu, akayashilia yale ya shetani akayaamini kwelikweli kuwa hatakufa, bali ataishi naye atayasimulia matendo ya Bwana.

Ndugu yangu hizi ni siku za mwisho, ambazo biblia ilizitabiri kuwa kutatokea wimbi kubwa la manabii wa uongo, ambao kimsingi kazi yao kubwa itakuwa ni hiyo..kuwahubiria watu maneno laini, haijalishi watakuwa hawajaokoka, au la, hilo haliwahusu, kazi yao ni kuwatabiria mafanikio tu na uzima, na mema, lakini madhara ya dhambi hawataambiwa.. Kama alivyofanya shetani kwa Hawa pale Edeni.

Isaya 30:9 “Kwa maana watu hawa ni watu waasi, watoto wasemao uongo, watoto wasiotaka kuisikia sheria ya Bwana;

10 wawaambiao waonaji, Msione; na manabii, Msitoe unabii wa mambo ya haki, TUAMBIENI MANENO LAINI, HUBIRINI MANENO YADANGANYAYO;

Kwa  hawa manabii, na waalimu wa uongo kamwe hutasikia Neno ‘ukizini hakika utakufa’, na kwenda jehanamu, huwezi kusikia maneno kama hayo, kwasababu shetani anataka wewe uendelee kubakia hivyo hivyo katika ujinga, ili ufe ghafla ujikute kuzimu uanze kujuta kwanini sikufahamu haya yote.

Angalia shida tunazozipitia duniani leo hii, ni kwasababu ya wazazi wetu kusikiliza injili laini za shetani,  Inasikitisha kuona pale mtu unapoambiwa kuhusu dhambi zako, unaona kama vile unahukumiwa. Mama yetu  Hawa aliona kama Mungu anamtamkia mabaya, akafanya makosa yale..Na sisi vivyo hivyo tukipuuzia injili ya kuambiwa ukweli, injili za kukemewa dhambi, injili za ziwa la moto. Tujue kuwa tunajiandaa kwa majuto ya milele.

Mara nyingi wana wa Israeli waliingia katika makosa kama haya mpaka wakapelekwa utumwani Babeli kwasababu ya kuwasikiliza manabii wa uongo waliokuwa wanawatabiria amani tu muda wote, bila kushughulika na dhambi zao, ambazo ndio kiini cha matatizo yao.

Soma vifungu hivi;

Ezekieli 13:16 “yaani, manabii wa Israeli, watabirio habari za Yerusalemu, na kuona maono ya amani katika habari zake; wala hapana amani, asema Bwana MUNGU”.

Yeremia 6:14 “Wameiponya jeraha ya watu wangu kwa juu juu tu, wakisema, Amani, Amani, wala hapana amani”.

Unaona yaliyokuwa yanaendelea kale ndiyo yanayoendelea sasa.

Leo swali linakuja kwako, Je unaufungaje mwaka wako?, mwaka huu wa 2020 ndio unapita, unakuja mwingine mpya wa 2021, kumbuka kwa jinsi miaka inavyosogea ndivyo tunavyoyakaribia mambo mawili makuu mbele yetu, la kwanza Ni Unyakuo. Na la pili ni Kifo chako. Maelfu ya watu kila sekunde wanakufa duniani, vilevile na wewe hujui siku yako itakuwa ni lini, pengine ni kesho, au mwanzoni mwa mwaka ujao, Jiulize ukifa leo ghafla huko utakapokwenda utakuwa ni upande gani?

Vilevile jiulize ikiwa unyakuo utapita leo usiku halafu ukaachwa, utakuwa kwenye hali ya namna gani..Kumbuka ni siku kama hizi  ndizo Bwana atakazorudi, watu watakuwa wakila na kunywa, wakipanda na kujenga, wakisherehekea, ndipo huo mwisho utakapokuja..Jiulize utakuwa wapi wakati huo ukikujia kwa ghafla.

Ukijifunza kuyatafakari hayo, hutaishi maisha ya ilimradi tu hapa duniani, bali utajiangalia sana mwenendo wako, ili siku ile isije ikakunasa kama mtego.

Hivyo, tubu dhambi zako mgeukie Muumba wako, usikubali uanze mwaka mpya na viporo vya dhambi vya mwaka huu, mgeukie Yesu Kristo leo hii, akusafishe dhambi zako.

Ikiwa upo tayari kutubu sasa, basi uamuzi huo utakuwa ni wa busara sana kwako. Mahali popote ulipo, tafuta sehemu ya utulivu, piga magoti, kisha kwa kumaanisha kabisa kutoka katika moyo wako sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU  MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE, NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Basi kwa sala hiyo fupi, Mungu ameshakusamehe, kilichobakia kwako ni kubatizwa, ikiwa hukubatizwa, na kudumu katika neema na utakatifu siku zote za maisha yako.

Ikiwa utahitaji msaada zaidi ya kiroho, basi tutafute kwa namba hizi +255693036618

Mungu akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

UNYAKUO.

JE! JICHO LAKO LINAONA NINI KATIKATI YA MAJARIBU?

KUMTUMIKIA MUNGU, KUNAWEZA KUWE KINYUME NA MATARIJIO YAKO.

BIBLIA INAITAJA NJIA KUU YA MFALME, NJIA HII NI IPI?

NJIA YA KUPATA WOKOVU.

Rudi nyumbani

Print this post